UKWELI WA USHIA

 UKWELI WA USHIA

Kimeandikwa na mheshimiwa Ayatullahil udhmaa Sayyid Swaadiq Shirazy (Mwenyezi Mungu amrefushie umri. )


TAMKO LA MUASSASATUR-RASULIL-AKRAM (S.A.W)
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHMA MWENYE KUREHEMU
Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote na sala na salam (rehma na amani) ziwe juu ya muongozaji kwenye njia ya haki na mtoa bishara na taa yenye kuangaza Muhammad na Ahli zake walio watwaharifu. Ama baada, wapinzani na maadui wa madhehebu ya Shia bado wanaendelea kati ya kipindi na kipindi kingine na kazi yao ya kuamsha na kueneza shubha zao na kusambaza maneno yao ya uzushi na yasiyo na ukweli wowote dhidi ya madhehebu ya Ahlul-bayti (a.s) na kwa kufanya hivyo hutarajia ya kuwa huenda wakafanikiwa kuziyumbisha na kuzitia shaka itikadi za watu wenye mustawa mdogo wa kielimu na kuwatoa kwenye itikadi zao za asili.


Lakini ukweli ni kwamba usaidizi wa pekee wa Mwenyezi Mungu mtukufu autoao kwa madhehebu ya haki wakati wote na bila kukoma huwa ni kizingiti na kizuizi kikubwa cha kuyafikia malengo yao hayo.

Pamoja na shubha zote na uzushi wote utolewao na uenezwao dhidi ya Ushia, tunakuta kwamba ukweli na haki daima ni yenye kudhihiri na haifichiki kamwe, na imekuwa ni yenye kudhihiri kupitia mikononi mwa wateule kati ya wafuasi wema ambao wamejitolea nafsi zao kwa ajili ya kuyanusuru madhehebu ya haki ambayo aliyaanzisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) tangia kudhihiri na kuchomoza kwa Uislaam.

Na katika uwanja huu kuna vitabu vingi sana vilivyo andikwa na vilivyo madhubuti na vizuri, na kati ya vitabu hivyo ni kitabu kiitwacho (Haqaaiqu ani Shia) kilicho andikwa na mheshimiwa Ayatullahil-udhmaa Sayyid Swadiq Shirazy Mwenyezi (Mungu amrefushie umri) alicho kiandika katika masiku ya ujana wake, na kuthibitisha kwa dalili madhubuti haki na ukweli wa madhehebu ya Ahlul-bayti (a.s).

Na kitabu hiki kimetofautiana na vitabu vingine na kuvipituka kutokana na umadhubuti pia umakini wa dalili zake na mfumo wake ulio mzuri na madhubuti na mwepesi ambao humfikisha msomaji kwenye kina cha shubha zitolewazo na kubainisha ubatilifu wake kwa njia nyepesi na rahisi na kwa umakini wa hali ya juu kabisa.

Na kauli ya mwisho ni kuwa: Hakika kitabu hiki pamoja na kuwa hajmu yake ni ndogo na ibara zake kuwa nyepesi, ukweli ni kwamba wakati huo huo ni kijitabu chenye faida na chenye undani katika maana, kwa hivyo basi hapana budi na inawapasa waumini wakisome na kukipitia au kuzitwalii bahthi zake na kufaidika na maudhui yake yenye kina na madhubuti, tukimtaraji Mwenyezi Mungu awape tawfiq (awawafikishe) kwa yale ayapendayo na kuyaridhia yeye Muumba subhanah.