DALILI ZA KIAMA

 DALILI ZA KIAMA

Kimiandikwa na:
HARUN YAHYA


Kimefasiriwa na: Shuaybu Husein Kifea
Dalili za Kiyama
Katika kipindi chote cha historia ya ulimwengu Wanaadamu wameuelewa ukubwa wa milima na upana wake, na ukubwa wa mbingu kutokana na njia zao mbali mbali za uchunguzi ijapokuwa wamekuwa na fikra potofu kuwa maumbile haya yatadumu milele. Imani hii ndio iliyozaa falsafa za kishirikina na za kilahidi za Ugiriki na dini za Sumeria za Misri ya kale. Qur'an inatuambia kuwa wale wanaoamini hivi wapo katika hatia kubwa. Miongoni mwa vitu ambavyo Mwenyezi Mungu amevibainisha katika Qur'an ni kuwa Ulimwengu umeumbwa na kwamba utakuwa na mwisho wake. Ulimwengu, kama walivyo binadamu na viumbe vingine hai, utatoweka.Dunia hii iliyopangiliwa vizuri ambayo imefanya kazi bila kasoro kwa mabilioni ya miaka, ni kazi yake Mola ambaye ameumba kila kitu, siku moja kwa amri yake itakoma kufanya kazi. Wakati huo tayari Mwenyezi Mungu amekwisha upanga. Wakati huo ambapo ulimwengu na kila kiumbe tokea vile visivyoonekana kwa macho hadi binadamu pamoja na Nyota na Magalaksi yatasita kufanya kazi, unaitwa "Saa" katika Qur'an. "Saa" hii haina maana kuwa muda wowote bali ni neno mahususi lililotumika katika Qur'an kuelezea wakati ambao dunia itakuwa imefika mwisho wake.Pamoja na maelezo ya mwisho wa dunia, Qur'an ina maelezo ya kina ya namna tukio zima litakavyotokea; "Mbingu zitakapopasuka," "Bahari zitakapowashwa moto," "Milima itakapoendeshwa (angani kama vumbi)" "Jua litakapo kunjwa kunjwa". Kihoro na khofu ambayo watu watakuwa nayo katika tukio hili la kutisha imeelezwa kwa kina katika Qur'an. Aya zinasisitiza kuwa hakutakuwa na pa kukimbilia wala pa kujificha. Tunachoweza kukisema hapa ni kuwa Ulimwengu utakuwa katika janga kubwa ambalo halijawahi kutokea hapo kabla.


Aya nyingi za Qur'an zinabainisha kuwa suala la mwisho wa dunia limegusa hisia za watu wengi katika kila kipindi cha historia. Katika aya kadhaa inaelezwa kuwa watu walimuuliza Mtume (s.a.w) juu ya lini utakuwa mwisho wa dunia;
Wanakuuliza juu ya Saa hiyo (yaani Kiama) kutokea kwake kutakuwa lini? (7:187),
Wanakuuliza Kiama kutokea kwake kutakuwa lini? (79:42)
Mwenyezi Mungu akamuamrisha Mtume kulijibu swali hilo hivi; Ilimu yake iko kwa Mola wangu tu. Hakuna wa kuhidhirisha wakati wake ila yeye tu (7:187). Hii maana yake ni kuwa Allah pekee ndiye aijuaye tarehe ya siku hiyo. Kutokana na aya hii tunaelewa kuwa elimu juu ya lini utafika wakati huo imefichwa kwa wanadamu. Lazima kuna sababu maalumu kwanini Mwenyezi Mungu ameifanya siku hii kuwa siri. La muhimu ni watu kujihadhari nayo; Ambao wanamuogopa Mola wao hata wanapokuwa Faraghani, na pia hukiogopa kiama (21:49). Kwahiyo watu wachunge mamlaka ya Mwenyezi Mungu na wautafakari ukubwa wake. Kabla ya siku hiyo ya machungu na majonzi haijawatokea kwa ghafla, watu waelewe kuwa mbali na Mwenyezi Mungu hakuna mahala pa kukimbilia. Kama siku ya mwisho ingejulikana watu walioishi huko nyuma pengine wasingelazimika kuufikiria kwa makini mwisho wa dunia, wasingejali matukio ya mwisho yaliyotajwa katika Qur'an.


Ispokuwa lazima ieleweke kuwa kuna aya nyingi zinazoelezea Saa hiyo na pale tunapozisoma tunakutana na ukweli madhubuti. Qur'an haitaji muda maalumu wa tukio hilo, bali inaelezea matukio ambayo yatatokea kabla yake. Aya hii inaelezea dalili kadhaa za saa hiyo; Kwani wanangoja jingine ila Kiama kiwajie kwa ghafla? Basi alama zake (hicho Kiama) zimekwisha kuja. Kutawafaa nini kukumbuka wakati kitakapowajia? (47:18) Kutokana na aya hii tunajifunza kuwa Qur'an inaelezea dalili zinazoonesha kufika kwa siku ya mwisho. Ili kuzielewa dalili hizi lazima tuzitafakari aya hizi. Vinginevyo kama aya inavyosema tafakuri yetu haitakuwa na maana pale Kiama kitakapotekea kwa ghafla. Baadhi ya hadithi za Mtume (s.a.w) ambazo zimetufikia zinazungumzia dalili za Kiama. Katika hadithi hizi za Mtume (s.a.w), kuna dalili za Kiama na maelezo ya kina kuhusu kipindi kinachokaribia kuhusu muda wa kukaribia Kiama, kipindi hiki ambacho dalili za Kiama zitatokea kinaitwa "Siku za Mwisho"


Suala la siku za mwisho na dalili za kiama, limevuta hisia za wengi katika kipindi chote cha historia ya Uislamu. Ndio maudhui makuu ya vitabu vingi vya wanazuoni na watafiti wa Kiislamu. Tunapoyakusanya pamoja maelezo yote haya, ndipo tutakapofikia hitimisho muhimu. Aya za Qur'an na hadithi za Mtume (s.a.w) zinaoneshakuwa kipindi cha siku za mwisho kimegawanyika katika awamu mbili.


Awamu ya kwanza ni pale ambapo mitihani ya kiroho na mali itausibu Ulimwengu. Awamu ya pili inaitwa zama bora, ni wakati ambapo mafundisho ya kimaadili ya Qur'an yatatawala na kuleta ustawi bora wa mwanadamu. Zama hizi zitakapofika mwisho wake na dunia itakapoingia katika kipindi ambacho jamii zitaporomoka, Kiama kitakuwa kimefika. Shabaha ya mfululizo huu wa mafundisho ya Qur'n ni kuzitazama dalili za Kiama kupitia aya za Qur'an na hadithi za Mtume (s.a.w) na kubainisha kuwa dalili hizi zimekwishaanza kujitokeza katika wakati huu tulionao. Ule ukweli kwamba kujitokeza kwa dalili hizi kulikwisha elezwa karne 14 zilizopita umzidishie Muumini Imani kwa Allah na unyenyekevu kwake. Kitabu hiki kimetayarishwa kwa kuzingatia ahadi ya Mola wetu;


Sema sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, karibuni hivi atakuonesheni ishara zake na mtazifahamu (27:93) Nukta yenye umuhimu makhsusi ambayo kwayo tunataka kumkumbusha msomaji ni kuwa Allah ndiye ajuaye ukweli juu ya kila kitu. Kama ilivyo katika mambo mengine yote, tunachokijua sisi kuhusu mwisho wa dunia ni kile tu ambacho Allah amekibainisha kwetu.