ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 
KIMEANDIKWA NA: TIJANI SAMAWI
KIMETARJUMIWA NA: MUSABAHA SHABAN
UTANGULIZI
Na: Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi
Kwa Jina la Mwenyezi Muijgu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu Kitabu kilichopo mikononi mwako ni tafsiri ya kitabu cha Kiarabu kiitwacho Liakuuna Ma'as-Sadiqin kilichoandikwa na Shaikh Muhammad Tijani Samawi wa Tunisia. Ndani ya Kitabu hiki ameelezea mkusanyiko wa itikadi za Kiislamu kwa namna zilivyo ndani ya Qur'an na Sunna Tukufu ya Mtume (s.a.w.w.).

Kitabu hiki ni kama kile cha mwanzo, nacho kimepata umaarufu hasa kutokana na jinsi mwandishi alivyozichambua itikadi hizo kwa mujibu wa mtazamo wa Sunni na Shia, kisha akayabainisha maeneo wanayohitilafiana. Kwa mara nyingine tena mimi binafsi sikusita kumuomba Shaikh Musabah Shaban Mapinda kukitafsiri kitabu hiki katika lugha ya Kiswahili kutoka kwenye asili yake ya lugha ya Kiarabu.

Sababu iliyoifanya Mission yetu isimamie kazi hii ni kama ile ya kwanza, ambayo inatokana na maombi ya Maulamaa wengi katika Afrika Mashariki kututaka tukifasiri kitabu hiki kiingie kwenye lugha ya Kiswahili.

Namshukuru Shaikh Musabah kwa kukubali ombi langu na kuifanya kazi hii kwa moyo mmoja. Nimeiangalia pamoja naye tafsiri hii kwa makini kuhakikisha kuwa maudhui yake ya asili hayakupotoshwa katika lugha ya Kiswahili.

Shaikh Tijani Samawi ameandika vitabu zaidi ya hivi, na. Sheikh wetu Musabah Shaban Mapinda ametafsiri kitabu kingine cha mwandishi huyu kiitwacho Fa'salu Ahlad-Dhikri (Waulizeni wanaofahamu) ambacho tayari kimeshapangwa katika kompyuta. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tena kwani kitabu chetu cha "Hatimaye Nimeongoka" kimependwa mno na wasomaji na hivyo kutupa ari ya kuchapisha hiki ulichonacho mkononi na kitakachofuatia Insha-Allah.

Ushahidi wa kupendwa kwa kitabu hicho ni shukurani na pongezi tunazozipokea toka kwa wasomaji kwa namna mbalimbali ikiwemo kutuandikia barua n.k. Mission inatoa shukurani zake za dhati kwa mfasiri na kwa wale wote waliosaidia kwa njia moja au nyingine katika uchapishaji wa kitabu hiki.

Wa Ma Tawfeeq Ilia Billah
Sayyid Saeed Akhtar Rizvi
Dar -es- Salaam
17th Rabbi-Ul-Awwal, 1422 l(fh June, 2001

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
ENYI MLIOAMINI! MCHENI MWENYEZI MUNGU NA MUWE PAMOJA NA WAKWELI (TAUBAH: 119)
Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu, Mola ambaye ametuboresha kwa kutupa uongofu, usimamizi na akatupa uwezo. Na ndiye Mola mwenye kuwaneemesha waja kwa kila ya kheri na mafanikio ili wapate kuwa waja wema. Yeyote mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu, atamtosheleza na kumlinda kutokana na vitimbi vya mashetani, na yeyote mwenye kuiacha njia yake, basi huyo atakuwa miongoni mwa wenye kufedheheka. Kisha Sala na Salamu zimshukie Mtume aliyetumwa kuwa ni Rehma kwa walimwengu, yeye ndiye mkombozi wa wanyonge na wenye kudhulumiwa, na ni kipenzi cha masikini ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu kwa kutamania kuyapata yale aliyoyaandaa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake wenye utakaso wa moyo.

Kadhalika Sala na Salamu ziwashukie watu wa kizazi chake (Mtume), kizazi chema kilichotakasika (nao ni wale) ambao Mwenyezi Mungu ameinyanyua daraja yao juu ya viumbe wengine ili wapate kuwa kiigizo cha wenye kutambua, na wawe ni nuru ya uongofu na Safina ya uokovu, usia (kuipanda) atakuwa miongoni mwa wenye kuangamia. Kisha radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie Masahaba wa Mtume waliobarikiwa, ambao walimpa kiapo cha utii wakamsaidia na hawakuwa miongoni mwa waliotengua kiapo (hicho) na waliimarika juu ya usia wake baada yake na hawakubadilisha wala kugeuka na wakawa miongoni mwa wenye kushukuru... (Kadhalika radhi za Mwenyezi Mungu) ziwashukie wale waliowafuata hao kwa wema na wakaenda juu ya mwendo wa uongofu wao, (ziwashukie radhi hizo) wale wafuasi wa mwanzoni na waliokuja mwishoni mpaka siku ya hukumu.

Ewe Mola wangu! nikunjulie kifua changu na uniwepesishie mambo yangu na uufungue mfundo katika ulimi wangu ili maneno yangu yapate kufahamika. Ewe Mola wangu nakuomba uufungue moyo wa kila atakayesoma kitabu changu auone ukweli, na kwa kupitia ukweli huo wewe unawaongoa waja wako wenye utakaso wa moyo.

Amma baad, kwa hakika kitabu changu kiitwacho, "Thummah-Tadaitu" kimepata mapokezi mazuri mbele ya wasomaji watukufu ambao wametoa baadhi ya maoni muhimu kuhusu maudhui mbali mbali zilizomo ndani ya kitabu hicho, na wameomba waongezewe ufafanuzi zaidi kuhusu mambo ambayo Waislamu wengi Masunni na Mashia wametofautiana katika kuyafahamu. Ili kuondoa utatanishi wa jambo hilo kwa yule atakaye uthibitisho na kupata msimamo uliowazi, basi nimetunga kitabu hiki kwa mfumo ule ule nilioutumia katika kitabu kile, ili iwe rahisi kwa mtafiti aliye muadilifu kuufikia ukweli kwa njia zake zilizo bora.

Kwa kuwa mimi niliweza kuufikia ukweli kwa njia ya utafiti na kulinganisha (baina ya hoja za upande huu na upande mwingine), kitabu hiki nimekipa jina la "Maa'Sa'diqin" hali ya kuwa nataraji baraka za Mwenyezi Mungu. Nimefanya hivyo ili kufaidika na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Enyi mlioamini, mcheni Mwenyezi Mungu na muwe pamoja na wakweli." Je! ni Muislamu gani anayepinga au kutokuwa na haja ya kuwa pamoja na hao wakweli?

Mimi binafsi nimekinaika na ndilo jambo ambalo najaribu kulibainisha kwa wengine kwa kiasi nitakachoweza bila ya kulazimisha maoni yangu tu, bali ni pamoja na kuheshimu kwangu maoni ya wengine. Basi Mweyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kuongoa naye ndiye mwenye kuwasimamia watu wema. Kwa hakika wako baadhi ya watu wameipinga anuani ya jina la kitabu (changu) kilichotangulia, "Thummah-Tadaitu" (Hatimaye nimeongoka) kutokana na utata unaoweza kupelekea kufikiri na kujiuliza kwamba, Je, (Waislamu) wengine wako katika upotovu na ni kipi hicho kitakachojulisha juu ya upotovu huo ikiwa hii ndiyo maana iliyokusudiwa?

Na kwa msingi wa upinzani huu, ninajibu kwa ufafanuzi: Kwanza: Ndani ya Qur'an tamko "Dhalalah" (yaani upotovu) limekuja kwa maana ya kusahau. Mwenyezi Mungu Anasema: (Qa'la Il-muha inda Rabbi fikitabin la Yadhillu Rabbi wala yansa). Maana yake: "Akasema elimu yake iko kwa Mola wangu ndani ya kitabu, Mola wangu hasahau wala haghafiliki". (Qur'an, 20:52)
Na amesema tena Mwenyezi Mungu: (Antadhilla ihdaahuma fatudhakkira Ihdaahumal-Ukhra), "Mmoja wao akisahau mwingine amkumbushe". (Qur'an 2:282)
Kama ambavyo pia limekuja ndani ya Qur'an Tukufu tamko la "Dhalalah" likielezea maana ya kutaka uhakika, kuchunguza na kutafiti. Mwenyezi Mungu amesema alipokuwa akimsemesha Mtume wake Mtukufu (s.a.w.) (Wawajadaka dhallan fahada) Qur'an, 93:7. Yaani, Alikukuta ukitafuta ukweli naye akakuongoa kwenye ukweli huo. Ni jambo maarufu katika sera yake Mtume (s.a.w.) kwamba, kabla ya kumshukia wahyi alikuwa akiwahama jamaa zake hapo Makkah ili apate kukaa faragha ndani ya pango la Hiraa kwa siku kadhaa akitafiti juu ya ukweli.

Na miongoni mwa maana kama hii kuna kauli ya Mtume (s.a.w.) isemayo: (Al-Hikmatu dhallatul-Muumin Ayna Mawajadaha akhadhaha): "Hekima ni kitu akitafutacho muumini, basi popote aikutapo na aichukue". Kwa hiyo ile anuani ya jina la kitabu changu cha mwanzo ni katika maana hii.

Pili: Kwa kukadiria (tuseme) kwamba anuani hiyo inayo maana ya upotevu ambao ni kinyume cha uongofu. Uongofu tunaoukusudia ni kwa kiwango cha kifikra kuweza kuipata njia ya Uislamu sahihi unaotuweka kwenye njia iliyonyooka, kama walivyofasiri hivyo baadhi ya wasomaji. Basi na iwe hivyo, nao ni ukweli ambao baadhi ya watu wanaogopa kuukabili kwa moyo thabiti wa kutenda unaokwenda sambamba katika akili na kauli ya Mtume (s.a.w.) aliposema: "Nimeacha miongoni mwenu vizito viwili, kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu, vitu ambavyo mkishikamana navyo hamutapotea kamwe baada yangu".

Basi hadithi iko wazi mno katika kuonyesha upotofu wa yeyote asiyeshikamana na viwili hivyo kwa pamoja (yaani kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi cha Mtume). Na kwa hali yoyote ile mimi nimekinaika kuwa nimeongoka kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani nimeshikamana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi cha Mtume (s.a.w.). Basi namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuongoa kwenye ukweli huu na kuwa tusingeongoka lau Mwenyezi Mungu asingetuongoa. Bila shaka wamekwisha kutufikia Mitume wa Mola wetu wakiwa na ukweli (tunaowajibika kuufuata).

Hivyo basi kitabu changu cha kwanza na cha pili vimebeba anuani zitokanazo ndani ya Qur'an, nayo Qur'an ndiyo maneno ya kweli mno na ni mazuri mno, na yote niliyoyakusanya ndani ya vitabu hivyo viwili - kama siyo haki tupu basi yako karibu mno nayo - kwani ni katika yale ambayo wameafikiana Waislamu wote Masunni na Mashia na ni katika yale yaliyothibiti kwa pande zote mbili kuwa ni sahihi, basi matokeo ya hayo yamekuwa ni kupatikana kwa vitabu hivi viwili "Thummah-Tadaytu na Liakuna Maas-Sadiqin " yote haya ni kwa utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Namuomba Mwenyezi Mungu auongoe umma wote wa Muhammad (s.a.w.) ili uwe ni umma bora na uongoze ulimwengu wote kwenye nuru na uongofu chini ya bendera ya Imam Mahdi anayengojewa, ambaye babu yake alituahidi - ili aje aujaze ulimwengu uadilifu na usawa baada ya kuwa umejazwa dhulma na ujeuri, na ili nuru ya Mwenyezi Mungu ipate kutimia japokuwa makafiri watachukia.