MUONGOZO KWA WASOMAJI

 
WANAOTHIBITISHA KUWA IPO

________________________________________
a. Amepokea Ibnu Abbas kwamba: "Umar bnul Khattab, siku moja alipokuwa juu ya Mimbar alisema: "Sisi tulikuwa tukisoma katika Qur'an: AN LAA TARGHABU A'N ABAAIKUM FAINNAHU KFRUN BIKUM AN TARGHABU A'N ABAAIKUM"... Taz: Sahihi Bukhari J. 8 Uk. 26 Sahihi Muslim J. 5 Uk. 116 b. Umar bnul Khattab alileta Ayatur rajmi ili itiwe katika msahafu, lakini haikuandikwa, kwa sababu Umar alikuwa peke yake hakuwa na shahidi. Taz: Al' It'qan J. 1 Uk. 101 Aya yenyewe aliyoileta Umar inasomeka hivi: ASH'SHAYKHU WASH'SHAYKHATU IDHA ZANAYAA FARTUMUHUMAA ALBATTATA NAKAALAN MINALLAHI WALLAHU A'ZIZUN HAKIMUN". Taz: Tafsirul Qurtubi J. 14 Uk. 113 Al' It'qan J.2 Uk.32 c. Inasimuliwa kuwa: katika mbao za Mwana Aisha ilikuwako Qur'an ikisomeka hivi: "INNA LLAHA WAMALAIKA TAHU YUSWALLUNA A'LAN NABIYY YA AYYUHA LLADHINA AMANU SWALLU A'LAYHI WASALLIMU TASLIIMA WA A'LALLADHI NA YUSWALLUNA ASSUFUFAL AWWALA" Mwana Aisha (mkewe Mtume) alikuwa nayo Qur'an hiyo kabla Uthman bin Affan hajabadilisha misahafu!! Taz: Al' It'qan J. 2 Uk. 33 d. Anasema Mwana Aisha (mkewe Mtume) katika zama za Mtume (s.a.w.) Suratul Ahzabi ilikuwa inafikia Aya mia mbili, lakini, ulipoandikwa msahafu Aya zikawa hivi kama zilivyo sasa ambazo ni sabini na tatu tu!! Aya mia moja ishirini na saba zimepotea!!! Taz: Tafsirul Qurtubi J. 14 Uk. 113

WALIOSEMA KUWA HAIPO

________________________________________
Mizani ya kupima riwaya zilizo tajwa hapo juu kuonyesha kuwa kuna baadhi ya amma sura au aya zilizopotea, riwaya hizo na za mfano wa kama hizo ni batili, Mwenyeezi Mungu anasema:- (Qur'an) "Haitaifikia batili mbele yake wala nyuma yake" 41:42 "Hakika sisi tumeiteremsha Qur'an, na hakika sisi ndio wenye kuilinda" 15:9. Hii ndio itikadi ya Shia Ithna Ashar. Taz: Al'I'tigad J. 1 Uk. 16 Tafsir Aalair Rahman J. 1 Uk. 25 Albayan fit'tafsiril Qur'an Uk. 213 Tafsirul Qur'an, assayid shubbar Uk. 17

KUSOMA QUR'AN KWA AJILI YA MAITI

________________________________________ Wako baadhi ya Waislamu wanapinga kumsomea Qur'an maiti, wakisema kwamba kufanya hivyo ni bid'a na bid'a mahala pake ni motoni. Katika kupinga jambo hili wanatoa hoja zao kama ifuatavyo: a. Imethibiti kuwa: Mtume (s.a.w.) hakumsomea Qur'an maiti yeyote katika uhai wake, kama jambo hilo ni jema Mtume asingeliacha kufanya kheri hiyo. Kwa hiyo, yeyote leo anae soma Qur'an kwa ajili ya mait, akaamini kuwa itamnufaisha, bila shaka mtu huyo anadai kuwa Mtume amefanya khiyana katika umma huu. Na hilo ni kosa kubwa kuamini kuwa Mtume hakufikisha baadhi ya mambo katika umma wake. b. Mwenyeezi Mungu anasema: "Na ya kwamba mtu hatapata isipokuwa aliyoyafanyia juhudi" 53:39. Na kwa Aya hii Imam Shafi amesema kuwa: Kisomo (anachosomewa maiti) thawabu za kisomo hicho hazifiki kwa maiti. Kwa sababu hilo haliko katika matendo yake, na kwa sababu hii, Mtume hakuwawekea umma wake, wala hakuhimiza (wafanye) kwa mtu yeyote. Wala hakupendekeza, wala sahaba yeyote hakuna aliyepokea (jambo hili) Taz: Tafsir ibn Kathir J. 4 Uk. 276 c. Amesema Mtume (s.a.w.): "Anapokufa mwanadamu, matendo yake humalizika yote isipokuwa mambo matatu: sadaka ya kudumu, au elimu yenye kunufaisha, au mtoto mwema atakaemuombea baada yake". Kwa hiyo, wasomaji wa khitima hupoteza bure muda wao, kwa kufanya jambo haliko katika Uislamu.

MAJIBU YETU

________________________________________
Kabla ya kuingia katika majadiliano hayo ni vyema kuzingatia jambo mmoja, nalo ni "NINI QUR'AN"? Taarif ya Qur'an ni: "Maneno ya Mwenyeezi Mungu aliyoyateremsha kwa Mtume wake Muhammad (s.a.w.) hali yakuwa ni muujiza wake" sasa, Ikisemwa kuwa: Mtume (s.a.w.) hakuwasomea Qur'an maiti wake, huwa inakusudiwa Qur'an gani?? Kwa sababu, katika salatiil maiti mna Suratul Fatiha, na Mtume (s.a.w.) aliwasalia mauti wake. Isipokuwa, ikithibitishwa kwa dalili kuwa: Suratul Fatiha si Qur'an.[1] Kuhusu Aya iambiwayo kuwa inazuia thawabu za Qur'an kumfikia maiti 53:39 tuangalie matni yake: "WA AN LAYSA LIL'INSANI ILLA MASAA", yaani, "Na yakwamba mtu hatapata isipokuwa aliyo yafanyia juhudi." Hivi ndivyo ananyosema Mwenyeezi Mungu na wala hasemi: "LA YANTAFIU'UL INSANU ILLA MASAA", yaani, "Hanufaiki mwanadamu isipokuwa kwa yale aliyoyafanyia juhudi". Hapa pana tofauti kubwa kati ya ibara ya kwanza na hii ya pili. Ibara ya kwanza inafidisha kuwa: "Mwanadamu atalipwa thawabu kwa mujibu wa matendo yake". Na ibara ya pili inafidisha kuwa: "Mwanadamu hanufaiki kwa chochote isipokuwa kwa matendo aliyoyatenda mwenyewe." Kwa ibara hizi ni sawa na kusema kuwa: "Athumani ana kibanda kidogo cha makuti, na humo ndimo anamoishi. Kwa hiyo, Athumani hana nyumba nyingine yoyote atakayoishi isipokuwa katika kipanda hicho. Lakini hali hii haizuii yeyote mkarimu kumjengea Athumani nyumba kubwa na bora. Mkarimu kama atajenga nyumba iliyo bora na kubwa, kisha akampa Athumani, haiwezi kusemwa: Athumani hawezi kukaa katika nyumba hiyo eti kwa sababu hakuijenga yeye. Amma Hadithi iamiwayo kuwa iazuia thawabu ya Qur'an kumfikia maiti isemayo: "IDHA MATA IBNU ADAMA IN'QATAA A'MALUHU ILLA MIN THALATHA..." yaani, "Anapokufa Mwanadamu matendo yake yote hukatika isipokuwa mambo matatu...." wala Hadithi haisemi: "IDHA MATA IBNU ADAMA IN'QATAA INTIFAU'HU" yaani, "Anapo kufa Mwanadamu humalizika kunufaika kwake". Ibara ya kwanza inafidisha kuwa: "Kinachomalizika ni matendo yake". Na ibara ya pili inafidisha kuwa: "Kinachomalizika ni kunufaika". Kwa mizani ya somo hili, natija inaonyesha kuwa Qur'an ikisomwa kwa ajili ya maiti, lazima thawabu ya kisomo hicho zitamfikia maiti, na hapa tutaonyesha hali tatu zilizo hai: a. Mtume (s.a.w.) amesema:- "MAN MATA WA A'LAYHI SIYAM SAMA A'NHU WALIYYUHU". yaani, atakae kufa na juu yake kuna saumu atafunga kwa niaba yake walii wake". Hadithi hii imekubaliwa na Waislamu wote na hata Imam Shafi naye ameikubali. Je! Kama mlango wa kunufaika umefungwa, thawabu ya funga anayofanyiwa maiti na walio hai ingemfikiaje? b. Mtume (s.a.w.) alimwambia mwanamke mmoja: "Mhijie mama yako". Na akamwambia mwanamume: "Mhijie baba yako". Hadithi hii pia imekubaliwa na Waislamu wote, Je! Thawabu za hija anayohijiwa na walio hai zinamfikiaje maiti, kumbe mlango wa kunufaika umefungwa?? c. Mwenyeezi Mungu anasema: "Zinamtukuza mbingu saba na ardhi (saba) na vilivyomo ndani yake, na hakuna chochote isipokuwa kinamsabihi kwa sifa zake njema lakini nyinyi hamfahamu kutukuza kwao" 17:44. Iliposemwa: "Na hakuna chochote isipokuwa kinamsabihi kwa sifa zake njema". Hii inafidisha kuwa: Vitu vyote vinamsabihi Mwenyeezi Mungu, na kwa kuelewa zaidi hili tumsikilize Mtume (s.a.w.). Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume (s.a.w.) alipita kwenye makaburi mawili akasema: Hawa waliomo katika makaburi haya wanaadhibiwa... Mara akaagiza kuti la mtende, akalipasua vipande viwili kisha akachimbiaa kimoja katika kaburi hili na kingine akachimbia katika kaburi lile, halafu akasema: Bila shaka vitawapunguzia (adhabu) madam havijakauka". Hiposemwa: "Madam havijakauka" inafidisha kuwa: Wakati wote vitakapokuwa vibichi (vipande vya kuti Ia mtende) vitakuwa vinamsabihi Mwenyezi Mungu. Hapa Mtume (s.a.w.) ana thibitisha kuwa: Tasbihi za kuti zina mpunguzia adhabu maiti, kupunguziwa adhabu ni hatua ya kuingia mtu katika neema (pepo). Mpenzi msomaji! Tasbihi za kuti la mtende zitampa nafuu maiti, lakini Mwislamu akisoma Qur'an kwa ajili ya kumuombea maiti itakosa kumfikia?? Taz: Tafsirul Qurtubi J. 10 Uk. 267 Notes: [1] Tarehe 18-8-1984 katika mkoa wa Mwanza Tarafa ya Nyakato Kijiji cha Buzuruga, kulitokea tatizo kubwa lililosababishwa najeshi la jadi Ia sungusungu. Jeshi la jadi la sungusungu kwa makusudi kabisa, ililiivamia nyumba ya MwisIamu, likaingia ndani na kuchanachana vitabu vitano vitakatifu vya Kiislamu. YASIN NDOGO (b) MAJMUUL MUBARAK (c) IRSHADUL MUSLIMINA (d) HADITHI ZA MTUME (e) AHLUL BADR. Kisha Sheikh Mkuu wa Tanzania alitoa fat'wa kwa kupitia Redio Tanzania kuwa: "Qur'an haikuchanwa" ingawa kwa maelezo yao - kama yalivyo kwenye kitabu: "Taarifa ya ujumbe wa Sheikh Mkuu" ukurasa 14 inasema: "Irshadul Muslimina kilichanwa kwa dharau" mwisho wa kunukuu. Kwa hiyo, Irshadul Muslimina iliyochanwa kwa dharau, ukikifunua kitabu hicho ukurasa wapili katika mlango wa kwanza utaiona Aya ya kumi na nane na ya kumi na tisa nusu yake, za Suratul Jathia. Bakwata inasema: Qur'an haikuchanwa lakini aya mbili katika Suratul Jathia zimechanwa kwa dharau!!! Sijui kwa Bakwata Qur'an inathubutu kwa vipi! Kwa kukamilika Sura ngapi au Aya ngapi hata isemwe ni QUR'AN? Kwa nini washutumiwe na kulaniwa watu wanaopendekeza kuwa: Sharia ya Mirathi na ya ndoa zifanyiwe marekebisho?? Katika Mirathi wanachoomba iondolewe ni Aya isemayo "LIDH'DHAKARI MITHLU H'ADH'DHIL UNTHAYAYNI" 4:11 katika Ndoa wanaomba iondolewe Aya: "MATHNA WATHULATHA WARUBAA" 4:4 sasa, unaweza kuhesabu silabi za Aya hizi, kisha uhesabu silabi za Aya zilizomo katika vitabu vilivyochanwa. Ndipo utamjua nani mwenye kosa wakufaa kushutumiwa na kulaaniwa! Kwakuwa sheria ni msumeno, hapa napenda kukumbusha baadhi ya matukio kama haya yalioyofanywa na wakubwa. Baada ya kufariki Mtume (s.a.w.) sheria isemayo kuwa "Katika mafungu manane ya sadaka, fungu moja kati ya haya ni la wale wanaoingia Uislamu. Fungu hili lilifutwa!! Na Aya inasomeka hivi: "WAL'MUALLAFATI QULUBUHUM" Taz: Tafasirut Tabari J. 10 Uk. 113 Hukumu ya Aya hii imefutwa, kwa hiyo, maasi ya kunyanyasa sheria ya Mwenyeezi Mungu hayakuanza juzi katika Tarafa ya Nyakato, bali yameanza mbali huko baada ya kufariki tu Mtume (s.a.w.).

ISRAA NA MIIRAJI

________________________________________
Israa ni: Mwendo wa usiku, kama ilivyokuja katika Qur'an: "Utukufu ni wa yeye ambaye alimpeleka Mja wake usiku, kutoka Msikiti mtukufu (wa Makka) mpaka Msikiti wa mbali (Falastin) ambao tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake, ili tumuonyeshe baadhi ya ishaara zetu" 17:1 Miiraji ni: Msafara ulioanzia katika Msikiti wa Falastin kwenda juu. Tukio la Israa limepokewa na waandishi wa Tarikh kwa njia tofauti, kuna wanaosema kuwa Israa ilitokea mwaka wa kumi na mbili baada ya kupewa Utume, Wengine wanasema ilikuwa mwaka wa kumi na moja, wengine mwaka wa kumi, wengine mwaka wa tano, wengine mwaka wa tatu na wengine mwaka wa pili. Taz: Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 108 Tarikhul Khamisi J. 1 Uk. 307 Assahihu Minsiiratin Nabi J. 1 Uk. 269 Kauli ya sawa katika mjadala huu ni: Israa imetokea katika mwaka wa tatu kwa sababu zifuatazo" a. Mtume (s.a.w.) alikuwa akipendelea sana kumbusu binti yake Mwana Fatima (a.s) mpaka Mwana Aisha (mkewe Mtume) likamuudhi sana hilo, akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyeezi Mungu! Una nini? Kila mara ninakuona sana unambusu Mwana Fatima kama unayekula asali!! Mtume (s.a.w.) akamjibu: "Ni kweli, ewe Aisha! Mimi nilipopelekwa juu (Miiraji) Malaika Jibril (a.s.) aliniingiza Peponi humo nilikula Tunda fulani, likabaki mgongoni, niliposhuka nilimwingillia Khadija (mkewe) mara akapata ujauzito wa Mwana Fatima kutokana na hilo tunda. Na yeye ndiye Tunda bora, kila ninapokumbuka Peponi, humbusu Fatima". Taz: Tarikh Bughdad J. 5 Uk. 87 Mizanul'itidal J. 2 Uk. 297 Mustadrakul Hakim J. 3 Uk. 156 Majmauz Zawaid J. 9 Uk. 202 Kanzul Ummal J. 14 Uk. 97 Dhakhaairul U'qbaa Uk. 36 Katika hadithi hii tunajifunza kuwa: Mwana Fatima (a.s.) amezaliwa mwaka wa tano baada ya Biitha (kupewa Utume) kwa hiyo, Israa na Miiraji ilikuwa kabla ya kuzaliwa Mwana Fatima, kwa sababu Mwana Fatima ni Tunda la peponi alilokula Mtume siku aliyopelekwa Miiraji. Tunda lililobaki mgongoni kwake hata baada ya miaka miwili akazaliwa Fatima, Bibi bora kabisa katika mabibi wa Peponi - Hadithi. b. Mtume (s.a.w.) alipopelekwa juu (Miiraji) Malaika walikuwa wakiuliza kila mahala Je! Muhammad amekwisha pewa Utume? Hili linaonyesha kuwa Tukio la Israa na Miiraji lilitokea katika miaka ya awali ya Utume, wala siyo baada ya miaka kumi na mbili. Kwa sababu ingekuwa hivyo bila shaka suala la Utume lingekwisha eleweka zamani pasingekuwepo haja ya kuliuliza. Israa na Miiraji ilitokea kabla ya kusilimu Abubakr bin Abi Quhafa, kwa sababu, Abubakr amesilimu baada ya miaka mitano ya biitha. Taz: Assahihu Minsiiratin Nabii J. 1 Uk. 274 Usudul Ghaba J. 4 Uk. 18 Ikiwa Israa na Miiraji imetokea kabla ya kusilimu Abubakr, basi madai ya Laqabu isemwayo kuwa alipata Abubakri ya "SIDDIQ" yanatupwa: Kwa sababu ikiwa laqabu hiyo (kama inavyodaiwa) alupata baada ya kusadikisha msafara wa Mtume (s.a.w.) aliopelekwa katika Israa na Miiraji. Litawezekanaje hilo, ilihali wakati wa tukio la Israa na Miiraji Abubakri alikuwa kafiri! Hapo tasdiq itapatikana?!

MTUME ALIKWENDA MWENYEWE AU NI NJOZI?

________________________________________
Tukio la Israa, wako baadhi ya Waislamu wanao ona kuwa Mtume (s.a.w.) alioteshwa na wala hakwenda mwenyewe akiwa macho. Na mategemeo yao ni ile habari aliyoisimulia Mwana Aisha kuwa: "Siku hiyo hakukikosa kiwiliwili cha Mtume". Taz: Tarikhul Khamisi J. 1 Uk. 308 Al' mawahibul laduniyya J. 2 Uk.2

MAJIBU YETU

________________________________________
a. Mwana Aisha wakati wa tukio hilo alikuwa hajaolewa na Mtume, bali yaelekea hata kuzaliwa alikuwa bado!! b. Mwenyeezi Mungu anasema: "Utukufu ni wa yeye ambaye alimpeleka Mja wake usiku, kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa mbali" 17:1. lliposemwa: "ASRAA BIA'BDIHI" tamko la "A'BD" hutumiwa kwa roho na kiwiliwili pamoja. Kwa hiyo, Mtume (s.a.w.) alikkwenda mwenyewe akiwa macho. c. Kama Israa ingelikuwa kwa njozi, basi kusingekuwako na upinzani mkubwa hivyo, na watu wasingeritarddi. Taz: Tafsir ibn Kathir J. 3 Uk. 24 Tarikhul Khamisi J. 3 Uk. 308 Almuswannaf J. 5 Uk. 327 d. Kama Israa ingelikuwa kwa njozi, basi Abu Talib na Bani Hashim wasingetoka kumtafuta, kwa sababu Bani Hashim walitoka kumtafuta siku hiyo. Taz: Assahihu Minsiiratin Nabii J. 1 Uk. 276

MUSA NA SALA TANO

________________________________________
Imepokewa katika riwaya kuwa: Sala tano zimefaradhiwa wakati Mtume (s.a.w.) alipopelekwa katika msafara wa Miiraji huko juu Inasemwa kuwa, zilifaradhiwa sala hamsini kwa kila siku, na Mtume (s.a.w.) alipokuwa akirudi na agizo hilo, alipofika mbingu ya sita akakutana na Nabii Musa (a.s.) akamshauri Mtume Muhammad (s.a.w.) arudi kwa Mola wake amuombe ampunguzie Sala hizo. Mtume alirudi kwa Mola wake na akapunguziwa Sala kumi, aliposhuka katika mbingu ya sita akakutana na Nabii Musa akiwa na sala arobaini. Nabii Musa akamrudisha kwa Mola wake apunguziwe Sala hizo, Mtume akafanya hivyo, Mwenyeezi Muungu akapunguza Sala kumi. Mtume alipofika kwa Nabii Musa, akamrudisha kwa Mola wake akaombe takhfif; Mtume alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza sala kumi Mtume akashuka alipofika kwa Nabii Musa akiwa na sala ishirini, Nabii Musa akamtaka arudi kwa Mola wake akampunguzie, kwa sababu umma wake hawawezi hilo. Mtume (s.a.w.) alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza Sala kumi, Mtume akashuka akiwa na sala kumi, alipokutana na Nabii Musa akamrudisha kwa Mola wake ili apunguziwe, Mtume alifanya hivyo, Mwenyeezi Mungu akapunguza Sala tano, Mtume (s.a.w.) aliposhuka kwa Nabii Musa (a.s.) akiwa na sala tano, alipotaka kumrudisha kwa Mola wake, Mtume (s.a.w.) alisema:- "Kwa hakika, nimerudi kwa Mola wangu mara tano, kuomba takhfif mpaka sasa naona aibu kubwa". Ndipo aliposhuka Mtume (s.a.w.) akiwa sala tano, ambazo wanapaswa Waislamu kuzisali kwa kila siku.

UCHUNGUZI

________________________________________
Tunaamini kuwa: "Mwenyeezi Mungu haweki sheria yoyote isipokuwa ina maslahi ndani yake. Kwa mantiq hii, Mtume (s.a.w.) asingehitaji kurudi mara zote hizo kwa ajili ya kupunguziwa. Kwa sababu kufanya hivyo ni kutaka sheria isiyo na maslahi, kama ambavyo sababu zilizompelekea Nabii Musa kutaka zipunguzwe Sala hamsini ni kushindwa kuzitekeleza sala hizo. Kama kwamba Nabii Musa anaamini kuwa Sheria hii (ya Sala hamsim) inakwenda kunyume na maslahi, na hilo ni muhali (haliwezekani) kwa Mwenyeezi Mungu. Aidha, vipi Mwenyeezi Mungu hakujua kuwa: Umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.) hauwezi hilo, bali Musa yeye alijue hilo?? Au tuseme, ni takhfif kwa jambo lisilowezekana, vipi, Mwenyeezi Mungu anatwambia wakati wote: "Mwenyeezi Mungu huwatakieni yaliyo mepesi wala hawatakieni yaliyo mazito". 2: 185. "Wala hakuweka juu yenu dhiki katika dini" 22:78. Na vipi Nabii Ibrahim hakushitushwa na misafara ya nenda rudi ya Mtume Muhammad, asimuulize kuna nini! Maana kwa mujibu wa riwaya zinzosimulia tukio hili zinasema kuwa, Nabii Ibrahim (a.s.) alikuwa katika mbingu ya saba na Nabii Musa (a.s.) mbingu ya sita. Aidha, kwanini Mwenyeezi Mungu asimpe moja kwa moja Mtume wake Sala tano, kuliko usumbufu huu alioupata Mtume wa nenda rudi mpaka akaingiwa na aibu kubwa akashuka kwa shingo upande na sala zake tano!!?

LENGO LA ISRAA NA MIRAJI

________________________________________
Tukitaka kujuwa shabaha na hekima na muujiza wa Israa na Miiraji, lazima kusoma nassi zake na vipengele vyake kwa undani na makini. Na hapa tutaonyesha mambo yafuatayo: a. Israa na Miiraji ni muujiza mkubwa wa kudumu, na leo katika karne hii ya ishirini tukio hili linakubaliwa na elimu ya sayansi na Teknolojia. Mwanadamu hashangai tena leo kusikia kuwa mtu amekwenda umbali wa maili nyingi zaidi katika upeo wa juu. b. Mwenyezi Mungu ametaja wazi lengo la msafara huo aliposema: "LINURIYAHU MIN AYAATINA", yaani, "Ili tumuonyeshe baadhi ya Aya (ishara) zetu" 17:1. Kwahiyo, lengo ni kumuonyesha Mtume (s.a.w.) baadhi ya ishara za utukufu wa Mwenyeezi Mungu. Na kwakupelekwa Mtume Israa na Miiraji, kumefunguwa moyo wake na akili yake zaidi kwa kupata taaluma kubwa katika ulimengu huu anaouongoza. c. (c) Mwanadamu (hasa Mwarabu) wakati huo aijishi katika ulimwengu finyu sana, na akili duni iliyofungwa katika tundu dogo. Kwa sabaha hii ikawa dharura kufunguliwa macho yake na moyo wake ili aujue ulimwengu anaoishi, ambao Mwenyeezi Mungu amemfanya awe khalifa wake.

KHADIJA ALIOLEWA NA YEYOTE KABLA YA MTUME?

________________________________________
Inasemekana kuwa: Mtume (s.a.w.) hakuoa mke yeyote aliye bikira isipokuwa Mwana Aisha tu. Wanasema kuwa: "Mwana Khadija kabla ya kuolewa na Mtume (s.a.w.) alikwisha olewa na waume wawili kabla ya Mtume Muhammad (s.a.w.) na amepata watoto wawili. Tutataja kidogo hapa baadhi ya hoja zinazosemwa juu ya Mwana Khadija kuhusu watoto aliopata kwa waume wengine kabla ya Mtume Muhammad (s.a.w.) ni kama ifuatavyo: i. Wanasema: Shahidi wa kwanza katika Uislamu ni mtoto wa Mwana Khadija aitwae Harithi bin Abi Hala, alipata shahada pale Mtume (s.a.w.) alipotangaza Uislamu hadharani. Taz: Al' Isaba J. 1 Uk. 293 Al'Awaail J. 1 Uk. 311-312 Lakini, hoja hii inaangushwa na riwaya ya Qatada inayosema kuwa: Shahidi wa kwanza katika Uislamu ni Sumayya, mama yake Ammar bin Yasir. Taz: Al' Isaba J. 4 Uk. 335 ii. Imepokewa kuwa: Mwana Khadija (a.s) alikuwa na nduguye akiitwa Hala, aliolewa na mtu mmoja katika Koo ya Al'Makhzumi, akazaa mtoto wa kike jina lake Hala, Kisha aliachika akaolewa na mtu mmoja katika Koo ya At'Tamim aitwaye Abu Hindi, akamzalia mtoto jina lake Hind. Huyu Abu Hindi, alikuwa na mke mwingine ambaye alimzalia watoto wawili: Zaynab na Ruqayya. Hatimae Abu Hindi na mkewe wa pili walikufa,akabakia Bi Hala ndugu ya Mwana Khadija, pamoja na watoto wawili: Zaynab na Ruqayya. Yule mtoto wake wa kuzaa: Hind, alikwenda kwa jamaa za mumewe. Ndipo Mwana Khadija alipowakusanya wote akawa nao, Bi Hala na watoto wawili walioachwa na mama yao: Zaynab na Ruqayya. Mwana Khadija alipoolewa na Mtume (s.a.w.) Bi Hala alifishwa, wakabaki Zaynab na Ruqayya wakilelewa na Mtume (s.a.w.). Katika mila za Kiarabu, walikuwa wakiamini kuwa mtoto wa kufikia ni mtoto wako halisi, kwa hiyo, watoto hawa wakapewa ubinti wa Mtume (s.a.w.) (Zaynab binti Muhammad na Ruqayya binti Muhammad).

Taz: As' Sahihu Minsiiratin Nabi J. I Uk. 123

MAJIBU YETU

________________________________________
a. Katika kitabu "Asha'shaafy" na "At Talkhis" inasema Mtume (s.a.w.) amemuoa Mwana Khadija akiwa bikira. b. Amesema Abulqasim Alkufy: Mtume (s.a.w.) alipomuoa Mwana Khadija (a.s.) wanawake wa kikuraishi walimkasirikia sana Mwana Khadija wakisema: Wamekuposa mabwana wa kikuraishi wenye heshima, umekataa kuolewa na yeyote kati yao, umekubali kuolewa na Muhammad, yatima wa Abu Talib Lofa hana mali!! Taz: Al' Istighatha J. 1 Uk. 70

POTE LENYE KUOKOKA

________________________________________
Amesema Mtukufu Mtume (s.a.w.) "Watafarakana umma wangu makundi sabini na tatu, kundi moja tu kati ya hayo litaokoka, na yaliyobaki yatatiwa motoni. Ali akauliza: "Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu! Kundi gani litakalookoka? Mtume (s.a.w.) akajibu: "Wewe na watu wako". Taz: Ithbatul Hudat J. 2 Uk. 260 Mfarakano kwa mara ya kwanza ulitokea kwa Waislamu pale tu alipofariki Mtume Muhammad (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) kabla ya kufariki dunia, aliweka sera kamili ya uongozi katika Uislamu. Iliposhuka Aya: "Hakika wale walioamini na wakatenda mema, basi hao ndio wema kushinda viumbe vyote" 98:7. Mtume (s.a.w.) akamwambia Ali: "Wewe Ali na kundi (pote) lako". Taz: Tafsirut Tabari J. 30 Uk. 171 Mtume (s.a.w.) amesema: "Ali yu pamoja na Qur'an, na Qur'an ipamoja na Mi, hawataachana mpaka wanifikie katika Haudh". Taz: Faidhul Qadir J. 4 Uk. 358 Musnad Ahmad J. 5 Uk. 31 Alfat'hul Kabir J. 2 Uk.21 Tarikhul Khulafai Uk. 174 Majmauz Zawaid J. 9 Uk. 134 Kifanyatut Talibi Uk. 399 Asnal matalibi Uk 136 Mtume (s.a.w) amesema: "Mimi ninakuachieni vizito viwili ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea baada yangu, Qur'an na Ahlul Bayt wangu, viwili hivi havitaachana mpaka vitakaponifikia katika Haudh". Taz: Tafsir ibn Kathir J. 4 Uk. 122 Tafsir ul Kazin J. 1 Uk. 4 Tarikhu Bughdad J. 8 Uk. 442 Sahihi Muslim J. 4 Uk. 1873 Jamiul Usul J. 1 Uk. 187 Albidayatu Wannihaya J. 7 Uk. 362 Majmauz Zawaid J. 9 Uk. 163 Musnad Ahmad J. 2 Uk. 17-26 Al Mustadrak J. 4 Uk. 109 Imam Ali (a.s.) mmoja katika Ahlul Bayt wa Mtume (s.a.w.) tazama pale iliposhuka Ayatut Tat'hir: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume) na (anataka) kukutakaseni sana sana" 33:33. Na mke wa Mtume (s.a.w.) (Ummu Salama) alipotaka kuingia katika nguo hiyo Mtume akamzuia!! Taz: Sahihi Muslim J. 4 Uk. 127 Sahihi Tirmidhi J. 4 Uk. 304 Alkhasais Uk. 4 Tarikh Bughdad J. 9 Uk. 126 Al' Isaba J. 1 Uk. 27 Usudul Ghaba J. 5 Uk. 521 Al Mustadrak J. 2 Uk. 416 Tafsirut Tabari J. 22 Uk. 5-7 Tafsirul Khazin J. 5 Uk. 259 Addurrul Manthur J. 5 Uk. 198

AHLUL BAYT WALIO PAMOJA NA QUR'AN

________________________________________
1. Imam Ali bin Abi Talib (a.s.) amezaliwa ndani ya Al' Kaaba siku ya Ijumaa, tarehe kumi na tatu Rajab mwaka wa thalathini (mwaka wa ndovu). Wamekhitilafiana waandishi wa tarikh kujuwa tarehe aliyopigwa dharba Imam Ali, baadhi ya kauli hizo zasema: a. Alipigwa dharba tarehe 17 usiku wa kuamkia Ijumaa mwezi wa Ramadhan, akafishwa usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 19 Ramadhan. b. Alipigiwa dharba tarehe 19 usiku, akafishwa tarehe 21 Ramadhan mwaka 40. c. Alipigwa dharba kuamkia tarehe 21, akafishwa tarehe 23 Ramadhani. d. Alipigwa dharba kuamkia tarehe 23, akafishwa tarehe 25 Ramadhan. Taz: Kashful Ghumma J. 2 Uk. 63 Riwaya nyingine zinasema kuwa: a. Alipigwa dharba asubuhi ya tarehe 17 Ramadhan. b. Alipigwa dharba asubuhi ya tarehe 19 Ramadhan, mwaka 40 Hijra. Taz: Suratul Aimmatil Ithna Ashar J. 1 Uk 452 Abdur Rahman bin Muljam alikutana na msichana mmoja katika khawariji aitwaye Qatwam, ambaye baba yake na kaka yake waliuliwa na Imam Ali katika vita vya Nahrwan. Msichana huyo alikuwa mzuri kupita kiasi, Abdur Rahman alipomtaka Qatwam, alimjibu: "Kama utaweza kunipoza moyo wangu utanipata" Akamuuliza: "Ni lipi litakalo kupoza moyo wako?" Akajibu: "Unipe dirham alfu tatu, mtumishi mmoja, mjakazi, mwimbaji, na umuue Ali bin Abi Talib. Abdur Rahman bin Muljam akasema: "Hayo mengine yote ni mepesi sana, lakini hili la kumuua Ali, ni dalili ya kuwa umenikataa. Kwa sababu haiwezekani kumuua Ali nami nikasalimika, tukaweza kuoana". Ilipofika siku hiyo, kwa kauli zilivyo khitilafiana, kama ulivyoona hapo juu, Abdur Rahman bin Muljam akatimiza lengo lake. Imam Ali amezikwa Kufa katika nchi ya Iraq. Taz: Kashful Ghumma J. 2 Uk. 62 Tabaqatul Kubra J. 6 Uk. 12 Tadhkiratul Khawas Uk. 179 2. Imam Hasan bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina, tarehe kumi na tano Ramadhan mwaka wa tatu Hijra'. Mu'awiya alipotaka kumtawalisha mwanawe Yazid, alitumia mbinu, akamjenga Juuda bint Al'ash'a'th bin Qays. Huyu alikuwa mke wa Imam Hasan (a.s.). Muawiya akampa sumu ili amtilie Imam Hasan. Na endapo atamuua, basi atamfanyia mambo mawili, la kwanza atampa dirham laki moja na la pili atamuoza mwanawe, Yazidi. Imam Hasan akapewa sumu hiyo na baada ya hapo alibaki siku arobainni akafariki dunia! Amekufa mfungo tano mwaka 50 Hijra. Taz: Kashful Ghumma J. 2 Uk. 207 Tadhkiratul Khawas Uk. 211 Wengine wanasema: Amekufa mfungo sita mwaka 49 Hijra. Taz: Tadhkiratul Khawas Uk. 211 Baada ya kufa Imam Hasan Juu'da alipeleka ujumbe kwa Yazidi wa kutaka kuolewa naye kama walivyoahidiana na baba yake Mu'awiya, Yazidi aliruka na kusema: "Hukuweza kumhurumia Hasan utanihurumia mimi!!? Kama umeweza kumuua yeye mimi utanimaliza mara moja, Yazid akakataa kumuoa. 3. Imam Husein bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe tatu Shaaban mwaka wa nne Hijra. Imam Husein (a.s.) ameuliwa mwezi kumi Muharram siku ya Ijumaa (wengine wanasema Jumamosi) mwaka wa sitini na moja Hijra. Imepokewa kutoka kwa Anas kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: "Mwanangu Husein atauliwa katika nchi ya Iraq, yeyote miongoni mwenu atakaekuwapo, basi asimame kumnusuru. Taz: Dhakhairul Uq'baa Uk. 146. Imepokewa kwa mama Ummu Salama (mkewe Mtume) anasema: "Nilimuona Mtume (s.a.w.) akikipangusa kichwa cha Imam Husein na huku akilia. Nikamuuliza: "Unalilia nini!" Akasema: "Hivi sasa amenijulisha Malaika Jibril kuwa: Mtoto wangu huyu atauliwa katika ardhi litwayo "KARBALA" kisha akanipa gao la udongo na akaniambia: 'Huu udongo ndipo mahala atakapouliwa, utunze, siku yoyote utakapogeuka kuwa mwekundu basi jua yakwamba amekwisha uliwa". Taz: Dhakhairul' U'qbaa Uk. 147 Albidayatu J. 3 Uk. 174 Albidayatu Wannihaya J. 6 Uk. 230 Tarikhul Islam J. 3 Uk. 10 Almustadrak J. 3 Uk. 176 Kama ambavyo, siku aliyouliwa Imam Husein mbingu zilimlilia, na alama ya kuonyesha kuwa zinamlilia ni wekundu unao onekana kwenye mawingu. Kwa hiyo, Imam Husein (a.s.) analiliwa na mbingu mpaka leo hii. Taz: Tafsirul Qurtubi J. 16 Uk. 14 4. Imam Ali bin Husein (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe tano Shaaban mwaka thalathini na nane Hijra, kabla ya kufishwa babu yake (Imam Ali) kwa miaka miwili. Imam Ali bin Husein amefariki mwaka wa tisini na nne Hijra, akazikwa katikamji wa Madina katika kiwanja kitakatifu cha Baqii. 5. Imam Muhammad bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe tatu mfungo tano (wengine wanasema tarehe moja Rajab) mwaka hamsini na saba Hijra, kabla ya kuuliwa babu yake Imam Husein kwa miaka mitatu. Wamekhitilafiana mwaka aliofia kama hivi: a. Amefishwa mwaka 114 Hijra. b. Amefishwa mwaka 117 Hijra. c. Amefishwa mwaka 118 Hijra. 6. Imam Ja'far bin Muhammad (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe 16 mfungo sita (wengine wanasema tarehe moja Rajab) mwaka 80 Hijra. Imam amefishwa katika mji wa Madina mwaka 149 Hijra, amezikwa pamoja na baba yake na babu yake katika viwanja vitakatifu vya Baqii. Taz: Siiratul' Aimmatil Ithna Ashar J. 2 Uk. 225 7. Imam Musa bin Ja'far (a.s.) amezaliwa katika kijiji cha "AB'WAA" kilicho kati ya Makka na Madina, mahala ambapo kaburi la Mwana Amina bint Wahab mama yake Mtume (s.a.w.) lilipo. Amezaliwa mwaka 128 Hijra (wengine wanasema mwaka 129). Imam Musa amefariki mwaka 188 Hijra baada ya kutiwa jela na Haruna Rashid kwa miaka kumi moja. Taz: Tadhkiratul Khawas Uk. 350. 8. Imam Ali bin Musa (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina. Wamekhitilafiana kujuwa tarehe aliyozaliwa kama hivi: a. Amezaliwa mfungo pili mwaka 148. b. Amezaliwa mfungo tatu mwaka 148. c. Amezaliwa mfungo sita mwaka 148. d. Amezaliwa mwaka 153. Kifo cha Imam Ali bin Musa kimetokana na maji ya matunda yenye sumu aliyopewa na Maamun. Baada ya kunywa Imam alibaki siku mbili kisha akafariki dunia, mwaka 203 wengine wanasema mwaka 202 na wengine wanasema mwaka 206. Taz: Siiratul' Aimmatil' Ithna Ashar J. 2 Uk. 341 9. Imam Muhammad bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina, tarehe kumi na tisa Ramadhan mwaka 195 Hijra. Amefariki Imam Muhammad mwaka 220 wengine wanasema mwaka 225 Taz: Siiratul' Aimmatil' Ithna Ashar J.2 Uk. 448. 10. Imam Ali bin Muhammad (a.s.) amezaliwa Rajab mwaka 214 Hijra umbali wa maili tatu hivi kutoka katika mji wa Madina. Imam Ali bin Muhammad ameuliwa kwa sumu mwaka 254 Hijra. 11. Imam Hasan bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina mwaka 231 Hijra. Imam Hasan bin Ali amefariki siku ya Ijumaa tarehe nane mfungo sita mwaka 260 na akazikwa mahala alipozikwa Baba yake. 12. Imam Muhammad bin Hasan (a.s.) amezaliwa tarehe kumi na tano Shaaban mwaka 255 Hijra, wengine wanasema tarehe ishirini na tatu Ramadhan mwaka 258 Hijra. Imam Muhammad bin Hasan yuko hai mpaka sasa, alipofiwa Baba yake alikuwa na umri wa miaka mitano. Hawa ni Maimam kumi na wawili katika AhIul Bayt (a.s.) walio pamoja na Qur'an. Amesema Mtume (s.a.w.) "Dini itaendelea kuwa imara mpaka isimame kiama, na mtasimamiwa na viongozi kumi na wawili, wote katika Maquraishi". Taz: Sahihi Muslim J. 6 Uk. 3-4 Sahihi Bukhari J. 4 Uk. 165 Sunan Abi Daud J. 3 Uk. 106 Musnad Ahmad J. 5 Uk. 86-90 Kanzul Ummal J. 13 Uk. 26-27 Hilyatul Awliyaa J. 4 Uk. 333 Na ameonya Mtume (s.a.w.) kwa yeyote ambaye hatawatambua Maimam hawa: "Yeyote atakaekufa na asimjue Imam wa zama zake, atakufa kifo cha kipagani". Taz: Sharhul Maqasid J. 2 Uk. 275 Al'mirqat J. 2 Uk. 509 Al'ghaadir J. 10 Uk. 260

SERA ZA UTAWALA BAADA YA MTUME

________________________________________
Ukisoma Terikh, na kisha ukafuatilia sera za utawala wa makhalifa watatu, utajua wazi kwamba mabwana hao walizuia kuandikwa Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.) bali walikataza hata kuzizungumza mbele za watu. Kwa sababu walijua wazi kuwa sera za utawala wao haziendi sambamba na uongozi wa Mtume Muhammad (s.a.w.). Abubakr amekataza kuzungumza chochote juu ya Mtume (s.a.w.) na amesema: Yeyote atakaewauliza mseme: "Kati yetu sisi na nyinyi ni Qur'an, basi, halalisheni halali yake na haramisheni haramu yake". Taz: Tadh'kiratul hufaadh J. 1 Uk. 3 Kauli hii ya Abubakr imekuja baada ya muda mfupi wa tukio la karatasi, Umar bnul Khattab alipomjibu Mtume kuwa: "Mtume anaweweseka, ipo Qur'an inatutosha", Abubakr anasema: "Kati yetu sisi na nyinyi ni Qur'an"..... Qur'an iliyo kati yetu na Abubakr inasema kuhusu wanaozuia zaka: "Na miongoni mwao wako walio mwahidi Mwenyeezi Mungu, akitupa katika fadhili zake bila shaka tutatoa sadaka na lazima tutakuwa miongoni mwa watendao mema. Lakini alipowapa katika fadhili zake, wa kayafanyia ubakhili na wakageuka, nao ndio wakengeukao. Kwa hiyo akawalipa unafiki mioyoni mwao mpaka siku ya kukutana naye, kwa sababu ya kumkhalifu Mwenyezi Mungu ahadi waliyo mwahidi, na kwa sababu walikuwa wanasema uongo". 9:75-77. Aya hizi zimeshuka kwa ajili ya Thaalaba aliyezuia zaka wakati wa Mtume (s.a.w.). Lakini pamoja na yote hayo Mtume (s.a.w.) hakumpiga wala hakumnyang'anya mali yake, ingawa Mtume yote haya alikuwa na uwezo nayo. Ambapo suala la Malik bin Nawyira na wenzake waliodaiwa kuwa walizuia Zaka katika utawala wa Abubakr. Huo ni msimamo waliouonyesha dhidi ya utawala wa Abubakr aliyepora madaraka yasiyo kuwa yake. Kwa hiyo, kitendo cha kuzuia zaka kutoupa utawala wa Abubakr ni tafsiri halisi ya kupinga utawala huo na wala si kupinga hukumu ya faradhi ya zaka. Sasa, Abubakr yuko wapi na aya hizi aliyedai kuwa ndiyo sera yake?? Mbona amewaua watu waliozuia zaka kwa kigezo gani? Sera ya Abubakr inasema: "Kati yetu sisi na nyinyi ni Qur'an". Qur'an inasema: "Wanaume wana sehemu katika yale waliyoyaacha wazazi na jamaa walio wakaribia, Na wanawake wanayo sehemu katika yale waliyoyaacha wazazi na jamaa walio wakaribia" 4:7. Mwana Fatima bint Muhammad (s.a.w.) alipokwenda kwa Abubakr kutaka mirathi iliyoachwa na baba yake, Abubakr akakataa kumpa akidai kuwa amemsikia Mtume akisema: "Sisi Mitume haturithiwi". Hapa Qur'an hana haja nayo, ameshika lile asilokuwa na haja nalo tokea awali, hata hivyo, Abubakr kweli maneno ya Mtume anayakubali? MwanaAisha (Mwanawe) anasimulia tukio hili: Baba yangu alizikusanya Hadithi za Mtume (s.a.w.) ambazo zilikuwa mia tano, akakesha kucha akizigeuzageuza......kulipokucha akasema: Mwanangu! Niletee Hadithi ulizonazo, ni kampa, akazichoma moto!! Taz: Kanzul Ummal J. 5 Uk. 237 Tadh'kiratul hufaadh J. 1 uk, 5 Je! Ni kweli Abubakr anaitegemea Qur'an tu peke yake? Mwenyeezi Mungu anasema: "Sadaka ni kwa mafakiri tu na masikini na wanaozitumikia na waungiwao.......mioyo yao.....9:60. Iliposemwa: "Na waungiwao mioyo yao" ni wale waislamu wapya ambao ndio kwanza wanasilimu. Abubakr alipotawala, hukumu ya kifungu cha Aya hii akaifuta!!! Taz: Tafsirut Tabari J. 10 Uk. 113

Muongozo wa Wasomao

Kimeandikwa na
Omar Jumaa Mayunga

Kimechapishwa na
S.L.P. 70005
Dar es Salaam - Tanzania
________________________________________
Kimetolewa wavuni na timu ya
Ahlul Bayt Digital Islamic Library Project