TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

 


Yunus 93-97
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Yunus 101-106 Monday, 21 April 2008 Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 325 tunayoianza kwa aya ya 101 ambayo inasema:
"Sema: Angalieni yaliyomo mbinguni na kwenye ardhi! Na ishara zote na maonyo hayawafai kitu watu wasioamini." Katika aya zilizotangulia tulisema kuwa kutotumia watu akili zao na kutotafakari juu ya alama na ishara za uwezo wa Allah ndiyo sababu ya watu kukufuru na kuikana haki.


Aya tuliyosoma inatilia mkazo suala la kutadabari na kubainisha kuwa, kutafakari na kuzingatia kwa kina madhihirisho ya uumbaji wa Allah ni utangulizi wa kumfikisha mtu kwenye imani thabiti na sahihi. Kwa upande mwingine kama tulivyosisitiza katika darsa iliyopita na nyingine kadhaa, imani lazima itokane na hiyari ya mtu na si kwa kulazimishwa na kutezwa nguvu, na ndiyo maana aya hii ya 101 inasisitiza juu ya kutafakari ili kwa kupitia njia hiyo ya uelewa na ufahamu mtu aiamini haki na kuweza kudumu na imani aliyonayo.


Bila shaka utafiti sahihi na wa kutafuta ukweli juu ya chungu ya maajabu yaliyomo katika mbingu na ardhi na ulimwengu mzima wa uumbaji humfanya mwanaadamu atambue adhama ya Mola wake na hivyo kunyenyekea na kujisalimisha kwa Muumba asiye na mshirika. Pamoja na hayo bado wanakuwepo watu ambao licha ya kushuhudia ishara za adhama ya Mola Muumba huamua kuikana na kuikataa haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa kutafakari na kutadabari juu ya uumbaji ni njia inayoweza kutumiwa na kila mtu kwa ajili ya kumjua Mwenyezi Mungu. Ifuatayo sasa ni aya ya 102 ambayo inasema:
"Basi je wanagojea jingine ila kama yaliyotokea siku za watu waliopita kabla yao? Sema: Basi ngojeni! Nami ni pamoja nanyi katika wanaongojea."

Katika aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu amewataka wapinzani wa haki kutafakari na kuzingatia kwa makini ishara za kuwepo Muumba wa ulimwengu katika mbingu na ardhini. Aya tuliyosoma hivi punde inasema wale ambao hawako tayari kutafakari juu ya hayo basi wajiweke tayari kukabili siku ngumu za mashaka na adhabu. Kwani utaratibu aliouweka Allah kuhusiana na uma au jamii za watu mbali mbali ni kwamba kama ilivyo kwa watu mmoja mmoja, majaaliwa na hatima ya jamii nzima ya watu hutegemea mwenendo wa akthari ya watu walioko katika jamii hiyo.


Kama wengi wao watakuwa ni watu wema basi jamii nzima huwa na muelekeo wa kutengenea hata kama watu wachache kati yao watakuwa mafasiki; la kama wengi wao watakuwa ni waovu basi jamii nzima itatumubukia kwenye ufisadi na kupatwa na mwisho mbaya hata kama ndani yake baadhi ya watu watakuwa ni waja wema. Historia ya kaumu zilizopita kama zile za Manabii Nuh, Lut na Hud as ni uthibitisho juu ya kutobadilika kwa utaratibu huo wa Allah sw. Hivyo bwana Mtume anatakiwa na Mola awaeleze Mushirikina wa Makka kwamba kama nao pai wataamua kusimama dhidi ya risala ya haki watafikwa na hatima sawa na iliyowapata watu wan kaumu hizo. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa ni historia ya waliotangulia ni funzo na ibra kwa wanaofuatia.


Ifuatayo sasa ni aya ya 103 ambayo inasema: "Kisha sisi huwaokoa Mitume wetu na walioamini. Ndio kama hivyo, inatustahiki kuwaokoa Waumini." Ikiendeleza yale yaliyokuja katika aya iliyotangulia kuhusiana na watu kupatwa na adhabu ya papa hapa duniani, aya ya 103 ya suratu Yunus inasema kwa kuwa hailaiki katika uadilifu wa Allah kuwachanganya wema na wabaya katika adhabu, hivyo kila kaumu inayofkia hatua ya kustahiki kufikwa na adhabu ni wale walio waovu na wale waliokuwa hawayajali maovu yanayotendeka katika jamii ndio wanakaopatwa na adhabu ya Allah, ama wale walio waumini Mwenyezi Mungu atawaokoa na adhabu hiyo. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa wale walio waumini wa kweli Mwenyezi Mungu huwalinda na adhabu hata ya hapa duniani, japokuwa watakuwa wakiishi katika jamii ya watu mafasiki.


Ifuatayo sasa ni aya ya 104 ambayo inasema: "Sema: Enyi watu ikiwa nyinyi mnayo shaka katika dini yangu basi mimi siwaabudu mnaowaabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu. Lakini mimi ninamwabudu Mwenyezi Mungu anayekufisheni. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waumini." Baada ya aya ziliowahutubu washirikina na kuwabainishia ipi itakuwa hatima yao, aya hii inamtaka Bwana Mtume awaambie watu hao kuwa kama wanadhani kwamba wewe utayumba na kutia shaka katika kufuata njia yako ya haki na pengine kukushawishi ulegeze msimamo katika itikadi yako basi wape jibu zito na la wazi kwamba hutomwabudu mwingine yeyote ghairi ya Mola wako Allah sw na katu hutoyatukuza msanamu yao hayo wanayoyaabudu. Waambie kwamba mimi ninamwabudu Mungu ambaye mauti yangu na yenu yako mikononi mwake na hamuwezi nyinyi abadani kuyakwepa hayo wala hayo masanamu yenu pia hayana uwezo wa kukuepusheni na kifo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa shaka inayotiwa na wengine juu ya haki hata kama watakuwa wengi namna gani isituyumbishe katika kufuata njia ya uongofu. Aidha aya inatuonyesha kuwa aliye na ustahiki wa kuabudiwa ni yule ambaye uhai wetu na mauti yetu yako mikononi mwake.


Darsa ya 325 inahitimishwa na aya za 105 na 106 ambazo zinasema: "Na uelekeze uso wako kwenye dini ya kweli wala usiwe katika washirikina." "Na wala usiwaombe wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Ukifanya hivyo basi utakuwa miongoni mwa waliodhulumu."


Katika kuwatangazia watu na hasa washirikina yale aliyoamriwa na Mola wake, Bwana Mtume anabainisha katika aya hizi kuwa ni wajibu kuifuata na kushikamana nayo njia iliyonyooka na kuepuka kila aina ya upotofu. Ama kinyume chake, itikadi ya mushirkina imejaa upotofu na mambo ya uzushi chungu nzima na muhimu zaidi ni kuwa hivyo vinavyoabudiwa na washirikina hao yaani masanamu, havina uwezo wa kumdhuru wala kumnufaisha mtu kwa lolote. Hivyo anayevielekea na kuviabudu vitu hivyo huwa ameidhulumu nafsi yake na pia kuifanyia dhulma dini ya haki ya mbinguni.


Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa dini ya kufuata ni ile inayokubaliana na maumbile ya mwanadamu. Aidha aya zinatuonyesha kuwa kila mwenye akili na busara hufanya kitu ambacho ima kitamletea manufaa au kumuepusha na madhara. Lakini kama tujuavyo masanamu na miungu wengine wengine wote bandia hawana uwezo wa hayo. Kwa haya machache basi tunaifunga darsa yetu hii kwa kumwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki na kutuwafikisha kumwabudu yeye kwa ikhlasi. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.


Yunus 107-109
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 326 na ya mwisho inayozungumzia sura hiyo tunayoianza kwa aya ya 107 ambayo inasema:
"Na kama Mwenyezi Mungu akikugusisha dhara, basi hapana wa kukuondolea ila yeye. Na akikutakia kheri basi hapana awezaye kurudisha fadhila zake. Huzifikisha kwa amtakaye katika waja wake. Naye ni Mwingi wa Kusamehe na Mwingi wa Kurehemu."


Katika aya ya mwisho tuliyoisoma katika darsa iliyopita Allah sw alimtaka Bwana Mtume Muhammad saw asimame imara na kuwatangazia kinagaubaga washirikina kuwa njia yake yeye ni ya tauhidi, na wala hatolegeza msimamo kwa sababu ya kuwavutia ao washirikina waukubali Uislamu.


Aya tuliyosoma inaendeleza yale yaliyokuja katika aya iliyotangulia na kumwambia Bwana Mtume na Waislamu kwa jumla kwamba, elewa kuwa kheri yoyote utakayopata au dhara yoyote itakayofika iko mikononi mwa Mola wako Allah sw, na hakuna yeyote ghairi ya yeye aliye na uwezo wa kukupa kheri au kukupokonya neema yoyote uliyopewa na yeye Mola. Kama ambavyo bila ya ridhaa yake Mola, hakuna mtu yeyote awezaye kukudhuru, kama ambavyo endapo Mwenyezi Mungu sw atataka dhara yoyote ile impate mja hakuna yeyote aliye na uwezo wa kumkinga mja na dhara hiyo.


Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa mushirikina na makafiri waelewe kwamba kukataa kwao kuiamini haki hakutawawezesha kutoka nje ya irada ya Allah sw, na kwa hakika kile alichoandika Mola kiwafike ndicho kitakachotokea. Aidha aya inatuelimisha kuwa kheri na neema azipatazo mja zinatokana na ihsani na fadhila zake Mola na wala si kwa kustahiki mja. Ifuatayo sasa ni aya ya 108 ambayo inasema: "Sema: Enyi watu haki imekwisha kukujieni kutoka kwa Mola wenu. Basi anayeongoka, anaongoka kwa faida ya nafsi yake, na anayepotea, anapotea kwa khasara ya nafsi yake. Na mimi si mlinzi juu yenu."


Katika aya hii ambayo ni moja kabla ya aya ya mwisho ya suratu Yunus Bwana Mtume Muhammad saw anawahutubu watu wote kwa jumla kwamba mimi nina jukumu la kukufikishieni wito wa wahyi wa Mola wangu na kukulinganieni kuifuata njia yake tu; na wala sina haki ya kukulazimisheni muukubali wito huo. Kila mmoja kati yenu anaweza kuamua kwa hiyari yake kuukubali uongofu na kuongoka, au kuukana na kupotoka. Lakini jueni kwamba kuamini kwenu na kukufuru kwenu hakuna tofauti yoyote kwa Mwenyezi Mungu sw wala mimi Mtume wake, na kwa hakika kama ni kupata faida au madhara na hasara, hilo litakurudieni nyinyi wenyewe.


Kwani Mwenyezi Mungu yeye ni mkwasi wala hahitaji chohcote kwenu, nami pia nimetimiza wajibu wangu wa kukulinganieni na kukufikisheni risala ya uongofu kutoka kwa Mola wenu, na hivyo sina dhima yoyote juu ya kuamini au kutoamini kwenu. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu ameondoa dhima kwa waja wake kwa kuwaonyesha na kuwabainisha njia ya haki. Kufuata au kutofuata hilo liko katika hiyari ya waja wenyewe. Nukta nyengine ya kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa jukumu la maulamaa na wale wafanyao tablighi ya dini ni kuwaelimisha na kuwaonyesha njia watu na si kuwalazimisha waikubali na kuifuata.


Darsa ya 326 na sura yetu ya Yunus inahitimishwa na aya ya 109 ambayo inasema: "Na (nimeambiwa): Fuata yanayofunuliwa kwako kwa Wahyi. Na vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na yeye ndiye mbora wa mahakimu."


Aya hii ya mwisho ya sura hii inasisitiza kwa mara nyingine juu ya kushikamana barabara na njia ya haki ya risala ya wahyi utokao kwa Mola Muumba, kwanza kabisa ikimuelekea bwana Mtume mwenyewe na kisha waumini kwa jumla, kwa kuwataka waendelee kuwa na subra hadi ushindi wa haki dhidi ya batili. Kama inavyojulikana mataghuti na madhalimu hufanya kila vitimbi na njama ili kuwakwamisha waumini wa kweli wasiweze kushikamana na kamba ya lailaha illa llah kama inavyostahiki.


Na ndiyo maana aya inawataka waumini kusimama kidete dhidi ya njama hizo na kuvumilia tabu na mashaka yote yatakayowapata katika njia hiyo. Alaa kulli haal Mwenyezi Mungu sw anaona kila kinachofanywa na waja wake wote, na siku itafika ambapo atahukumu baina yao kwa uadilifu. Lakini hata hapa duniani pia, pale waumini wanaposimama kidete kukabiliana na madhalimu, mwishowe hupata nusra ya Allah na haki kuishinda batili. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa watu wana hiyari ama kuamini au kukufuru, hata hivyo kukufuru kwao kusitufanye sisi tukaingiwa na shaka katika kufuata njia ya uongofu ya kushikamana na maamrisho ya Mola wetu na kujiweka mbali na makatazo yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 326 imefikia tamati na kuhitmisha pia tarjumi na maelezo ya sura ya kumi ya Yunus. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atuwafikishe kuyatekeleza kivitendo yale yote tuliyojifunza ndani ya sura hii, Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.