TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

 


Yunus 93-97
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo huu wa 323 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 93 ambayo inasema:
"Na hakika tuliwaweka Wana wa Israili makazi mazuri, na tukawaruzuku vitu vizuri. Nao hawakukhitalifiana mpaka ilipowafikia ilimu. Hakika Mola wako atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitalifiana."

Katika aya hii Mwenyezi Mungu sw ameashiria neema kadha wa kadha alizowapa Bani Israil na kusema kuwa baada ya miaka na miaka ya kutangatanga na kutokuwa na pa kukaa tuliwapa Bani Israil eneo lenye hali nzuri kabisa ya hewa, na lenye rutuba na ustawi huko Sham na kuwaruzuku riziki zilizo bora kabisa.


Lakini badala ya kushukuru kwa hayo na kuwa watiifu wa kushikamana na maamrisho tuliyowateremshia wakaanza kufarikiana na kutengana na kila mmoja akaamua kufuata njia yake. Hivyo kila mmoja atatakiwa kuja kuutolea maelezo mwenendo huo muovu aliokuwa nao atakaposimamishwa mbele ya mahakama ya uadilifu siku ya Kiyama. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa katika mafundisho ya Mitume, mbali na kuzingatiwa suala la kuwalea na kuwajenga watu kiroho na kimaanawi, yanazingatiwa vile vile mahitaji yao ya kimaada kwa kuwapa uhuru, fursa na suhula za kimaisha za kupatia riziki safi na za halali. Aidha aya hii inatuonyesha kuwa hitilafu na mifarakano hutokana na kujiweka mbali watu na mafundisho ya mbinguni na hilo huwa sababu ya kuondokewa na neema za Mola wao.


Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 94 na 95 ambazo zinasema:
"Na kama unayo shaka juu ya hayo tuliyokuteremshia, basi waulize wasomao kitabu kabla yako. Kwa yakini imekwisha kujia haki kutoka kwa Mola wako. Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka." "Na kabisa usiwe miongoni mwa wale wanaozikanusha ishara za Mwenyezi Mungu usije ukawa miongoni mwa wenye khasara." Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinawahutubu wale waliokuwa na shaka kama yale aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad saw ni maneno ya haki au la na kuwaambia kwamba ikiwa mtavirejea vitabu vya mbinguni vilivyotangulia mtaona humo bishara na alama za Mtume Muhammad SAW. Mbali na hayo mtashuhudia pia kuwa zimezungumzwa na vitabu hivyo hatima za kaumu nyingi zilizotangulia zilizotajwa pia ndani ya Quran kama vile bani Israil, na hivyo kukubainikieni kwamba hii Quran pia ni kitabu cha haki kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu sw.


Ni wazi kuwa kama shaka yenu itaondolewa baada ya kubaini hayo na kutambua kuwa Quran ni kitabu cha haki, kukadhibisha kwenu kitabu hicho baada ya kubainikiwa na hayo kutakuwa ni kwa madhara yenu yenyewe kutokana na kujinyima fursa ya kuufikia uongofu hapa duniani. Ijapokuwa kidhahiri matamshi ya aya hizi wapenzi wasikilizaji yanaonekana kumhutubu Bwana Mtume, lakini ni wazi kwamba si yeye anayesemezwa hapa, kwa sababu ni jambo lililo muhali na lisiloingia akilini kwamba Bwana Mtume awe na shaka na wahyi alioteremshiwa na Mola wake.


Hivyo anaowahutubu Allah katika aya hii ni mushirikina na Ahlul Kitab, lakini kama ilivyo katika aya nyingi za Quran lugha iliyotumika inaonyesha kuwa mhutubiwa ni bwana Mtume wakati kumbe mlengwa hasa ni watu wengine wa kawaida. Pamoja na mambo mengine aya hizi zinatuelimisha kuwa shaka na hati hati ni vitu vya kawaida vinavyoweza kumtokea kila mtu. La muhimu ni kujivua na hali ya shaka kwa kurejea kwa maulamaa na wanazuoni wa kidini na kufikia kwenye daraja ya utambuzi kamili na yakini. Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa endapo mtu ataendelea kubakia katika hali ya shaka na kutochukua hatua ya kuiondoa shaka aliyonayo si hasha akajikuta anaishia kwenye kukadhibisha na kuikataa moja kwa moja haki.


Aya za 96 na 97 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hizo zinasema: "Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwisha thibitika juu yao hawataamini." "Ijapokuwa itawajia kila ishara mpaka waione adhabu inayoumiza."


Watu wamegawika makundi matatu katika suala la namna wanavyoamiliana na ukweli wa mafundisho ya dini. Kundi la kwanza ni la wale wasioitambua haki na wala hawajishughulishi kutaka kuijua. La pili ni la wale ambao haki hawaijui lakini wanaamua kufanya juhudi za kuitafuta hadi kuifikia. Ama kundi la tatu ni la wale ambao wameitambua haki lakini kwa kuwa inagongana na maslahi yao ya kimaada ya hapa duniani, hawako tayari kuifuata. Aya tulizosoma zinawalenga watu wa kundi hili la tatu ambao nyoyo zao zimepiga weusi na kufanya kutu kutokana na inadi na ukaidi wao na ambao hakuna tena matumaini ya nyoyo zao kubadilika na kuiamini haki. Watu wa aina hii huwa ni katika wale walioghadhibikiwa na Mwenyezi Mungu; kwani hawawi tayari kuamini na kujisalimisha kwa Mola wao kama haijafikia hatua ya kuiona adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa macho yao.


Tatizo la watu hao si kutopewa hoja za kiakili wala kutoonyeshwa muujiza, ambao hata kama wataonyeshwa pia hawatouamini. Tatizo lao ni kwamba hawaa na matamanio yao ya nafsi hayawaruhusu kuungama kile ambacho wamepata utambuzi wake. Hivyo kama tutaona watu wengi hawaiamini haki, hilo lisitufanye tukautilia shaka ukweli wa maneno ya Mitume na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo. Bali tuelewe kwamba kuna watu ambao nafsi zao zimekubuhu kwa maovu na kuharibika kimaanawi kiasi kwamba hakuna chochote kile cha kuweza kuwaathiri wakabadilika.


Watu hao ni mithili ya mpira ambao kama utautupa baharini hakuna hata moja la maji litakalopenya na kuingia ndani yake. Hali ambayo ni matokeo ya kuziba kwa mpira tu vinginevyo bahari iko pale pale na maji yake yako kwa ajili ya kila mtu. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa tusiwe na matumaini kwamba watu wote wataiamini haki, bali tujue kwamba maovu na madhambi ni mambo yanayofanya utandu juu ya moyo wa mtu unaomfanya asiwe tayari kuikubali haki. Nukta nyingine ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa iko siku hata wale waliotopea katika kukadhibisha haki watabaini hakika hiyo lakini wakati huo watakuwa wamechelewa na kuikubali kwao haki wakati huo hakutowasaidia kitu. Darsa ya 323 imeifikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutuwafikisha kuifuata na atuonyeshe batili na kutupa taufiki ya kuiepuka. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh


Yunus 98-100
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran. Hii ni darsa ya 324, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 98 ambayo inasema:
"Kwa nini usiwepo mji mmoja ukaamini na imani yake ikawafaa isipokuwa kaumu Yunus? Waliamini na sisi tukawaondolea adhabu ya hizaya katika maisha ya dunia, na tukawasterehesha kwa muda."


Kama ambavyo tumewahi kuashiria katika darsa zetu za huko nyuma, ni kwamba utaratibu aliojiwekea Allah sw kuhusiana na waja wake ni kuwapa fursa na muhula wa kutubia madhambi yao na kutenda amali njema ili kufidia waliyoyatanguliza huko nyuma. Lakini pia kama tulivyowahi kueleza ni kwamba mlango wa toba uko wazi madamu mtu bado hajafikia lahadha ya kufikwa na mauti au kuteremkiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.


Kwani kutubia katika lahadha mbili hizo au kuiamini haki katika wakati huo hakuwi na faida yoyote kwa mtu, na sababu ni kwamba imani na toba ya lahadha hizo hutokana na khofu ya mauti na adhabu na si kwa hiyari yake mtu. Suala hilo la fursa na muhula wa kutubia na kuiamini haki hauishii kwa mtu binafsi tu, bali Allah ameuweka pia kwa kaumu na umma mzima wa watu. Kwa upande wa kaumu, ni ile ya Nabii Yunus tu (AS) ndiyo ambayo watu wake walipoiona adhabu waliiamini haki na kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, naye Mola Mrehemevu akaikubali imani yao na kuwapa fursa nyingine. Historia inasimulia kwamba baada ya miaka mingi ya kazi ya tablighi aliyoifanya Nabii Yunus as kuwalingania watu wake lailaha illa llah ni watu wawili tu ndiyo walioukubali wito wa uongofu.


Akiwa katika siku za mwisho za uhai wake, na kutokana na kukata tamaa kwa watu wake kuiamini haki, Mtume huyo wa Allah aliwaapiza watu wa kaumu yake na kisha akaamua kuondoka na kwenda zake. Kama ilivyo kawaida ni kwamba dua za Mitume huwa hazirudi, na kwa hivyo ilipasa watu wa kaumu yake wateremkiwe na adhabu.


Hata hivyo mtu mmoja mtambuzi na mwenye hekima kati ya wale wawili waliomuamini Mtume huyo alipoona Nabii Yunus ameshatoa tamko la kuwaapiza watu wake waliokataa kuamini haki aliwaendea watu hao na kuwaambia:" Sasa subirini mshukiwe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, la kama mnataka mpate rehma zake Mola basi tokeni nje ya mji, na mutenganishe baina yenu na watoto wenu wadogo ili sauti za vilio vya watoto na za maombolezo ya mama zao waliotenganishwa nao ziweze kupanda na kusikika, na nyote pamoja mtubie kwa mliyoyafanya huko nyuma na kumwomba maghufira Allah sw.


Asaa kwa njia hiyo mkaweza kusamehewa. Hivyo watu hao wakaufuata wasia huo na hivyo adhabu haikuteremshwa tena, naye Nabii Yunus akarejea kwa watu wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na ayah ii ni kuwa miongoni mwa kaumu zilizopita, ni kaumu ya Yunus tu ndiyo iliyotubia kwa wakati na kabla ya kushuka adhabu na toba yao ikapokelewa na kuamini kwao kukakubaliwa. Funzo jengine tunalopata katika ayah ii ni kwamba hatima na majaaliwa ya watu yako mikononi mwao wenyewe, na hivyo kwa kuomba dua na kushtakia waja hali zao hiyo inaweza ikawa sababu ya kuzuia balaa lisiwashukie na rehma za Mola ziwamiminikie.


Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 99 ambayo inasema: "Angelitaka Mola wako wangeliamini wote waliomo katika ardhi. Je wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe waumini?" Moja ya kati ya mambo ambayo Mwenyezi Mungu sw amejifunga nayo mwenyewe ni kuwafikishia waja wake uongofu. Hata hivyo Mola Mwenye hikima hakutaka watu waiamini haki kwa nguvu na kulazimishwa. Bali ametaka waamue kwa hiyari yao waja, ima kuiamini au kuikufuru haki. Tabaan baada ya kuchagua kwa hiyari yake mtu ima kuamini au kukufuru ajiweke tayari pia kwa jaza na malipo atakayopata kutokana na chaguo lake.


Kwa kuzingatia kwamba sifa moja kubwa ya Bwana Mtume Muhammad saw kama ilivyoelezwa na quran ni kwamba alikuwa na hamu kubwa ya kuona watu wa umati wake wanaiamini haki na akiumia na kuungulika mno kwa kuwaona wamezama katika dimbwi la upotofu, lakini kwa kuwa Allah sw ametaka imani ya waja itokane na hiyari yao hivyo anamhutubu Mtume wake kwa kumwambia kwamba pamoja na hamu kubwa uliyonayo usifikirie kuwafanya watu waumini hata kwa kuwateza nguvu, kwani lau Mola wako angetaka iwe hivyo wanaadamu wote wangeiamini haki. Moja ya nukta za kuzingatiwa katika ayah ii ni kuwa imani huwa na thamani inapotokana na hiyari ya mtu, ama ikiwa itatokana na kulazimishwa haiwezi kuwa na faida kwa mtu.


Darsa ya 324 inahitimishwa na aya ya 100 ambayo inasema: "Na hawezi mtu kuamini ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye hujaalia adhabu iwafike wasiotumia akili zao." Kama tujuavyo, watu hawalazimishwi kuiamini haki, na kuamini kwa kulazimishwa hakuna thamani yoyote. Pamoja na hayo ni taufiki ya Mola ndiyo inayoufanya moyo wa mtu uikubali na kuiamini haki kwa hiyari na ukunjufu. Kwani ni yeye ndiye anayetukamilishia suhula zote kuanzia za kutufikia uongofu wenyewe kupitia kwa Mitume wake, pamoja na kutupa akili timamu ya kuchanganua na kupambanua zuri na baya, la kheri na la shari na lile la kimantiki na lisiloingia akilini.


Hivyo mtu asije akaingiwa na ghururi na kumpitikia kwamba ni uhodari wake ndio uliomfanya kuitambua haki na kuifuata. Na kwa hakika kila mtu anapojiona amepata taufiki ya kushikamana barabara na kamba ya uongofu, basi amshukuru sana Mola wake na kuomba taufiki ya kudumu katika kushikamana na mambo ya kheri. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.