TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

 


Yunus 79-86
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran. Hii ni darsa ya 321, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus tunaianza darsa yetu kwa aya za 79 na 80 ambazo zinasema:
"Na akasema Firauni: Nileteeni kila mchawi mjuzi." "Basi walipokuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni mnavyotaka kuvitupa." Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa as alitakiwa na Mola wake aianze kazi yake ya kulingania La ilaha illa llah kwa kumwendea Firauni na kumtaka aikubali tauhidi yaani kumuabudu Mungu mmoja wa haki na pia kuwakomboa Bani Israil na madhila ya Mafirauni. Aya tulizosoma zinasema Firauni, ambaye hakuwa na uwezo wa kukabiliana na huja na burhani alizopewa na Musa as alianza kuutuhumu muujiza alioonyeshwa na Nabii huyo kuwa ni uchawi na hivyo kutoa amri ya kuitwa wachawi wake wote ili kukabiliana na muujiza huo wa Mtume wa Allah Musa as.


Lakini Nabii Musa ambaye hakuwa na chembe ya shaka kuwa haki iko upande wake aliwataka wachawi wa Firauni wafanye kila walichonacho cha uchawi na mazingaombwe yao ili watu wajionee wenyewe na kuamua. Hivyo miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa mataghuti wa kila zama huamua kuwatumia vibaya wataalamu na taaluma zao ili kuweza kufikia malengo yao maovu. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa Mitume walikuwa na yakini na risala waliyokuwa wakiilingania, na juu ya kupata nusra na msaada wa Allah sw. Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya za 81 na 82 ambazo zinasema: "Walipotupa, Musa alisema: Mliyoleta ni uchawi; Mwenyezi Mungu sasa hivi ataubatilisha. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu."


"Na Mwenyezi Mungu ataithubutisha haki kwa maneno yake, ingawa watachukia hao wabaya." Kama ilivyoelezwa pia katika suratu Shuaraa, wachawi wa Firauni walitupa kamba zao na vifimbo vyao, na kutamka kuwa kwa utukufu wa Firauni tunaapa kuwa sisi ndio washindi. Hakika ni kuwa wachawi wa Firauni hawakufanya chochote kubadilisha kamba na vifimbo vyao, bali walifanya kiini macho tu na hivyo watu wakahisi kana kwamba vifimbo na kamba hizo zilikuwa zinaonyesha harakati za kutambaa. Na ndiyo maana Nabii Musa aliwatangazia kinagaubaga kuwa Mwenyezi Mungu atauanika hadharani ubatili wa uchawi wao huo na kuithibitisha haki mbele ya macho ya watu. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa hata kama batili itarembwa na kupambwa kwa kila namna ya urembo mwishowe itabainika na kutoweka tu. Nukta nyingine ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa nia na njama ya mustakbirina ya kutaka kuizima nuru ya haki haiwezi kufaulu na kusimama mbele ya irada ya Allah SW ambaye ameahidi kuwa nusra na msaada wake hautoacha kuwafikia wale waliosimama upande wa haki.


Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 83 ambayo inasema: "Hawakumuamini Musa isipokuwa baadhi ya vijana wa kaumu yake kwa kumuogopa Firauni na wakuu wao, wasiwatese. Kwani hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi. Na kwa yakini alikuwa miongoni mwa (maasi) waliopita mpaka."


Katika awamu ya kwanza ya kazi yake ya kulingania laa ilaha illa llah, Nabii Musa AS alimwendea Firauni na wasaidizi wake kisha katika awamu ya pili akakabiliana na wachawi na kuwashinda . Ama katika hatua ya tatu aliwafuata watu wa Bani Israil ambapo mwanzo wake ni vijana wa kaumu hiyo ndio waliomuamini. Tabaan vijana hao nao waliamini pamoja na kwamba walikuwa wakikabiliwa na mateso na madhila ya Firauni. Miongoni mwa yale tunayojifunza na kutokana na aya hii ni kuwa tabaka la kwanza kumwamini Musa katika Bani Israil lilikuwa ni tabaka la vijana, na hii ni kwa sababu nyoyo ya za vijana huwa safi na bongo zao huwa pia hazijakomazwa na fikra za kitaasubi. Halikadhalika aya hii inatuonyesha kuwa hata katika mifumo inayotawaliwa na mafirauni, mtu anaweza kujivua na upotofu wa mfumo huo na kushikamana na njia ya haki ya akina Musa AS.


Darsa ya 231 inahitimishwa na aya za 84, 85 na 86 ambazo zinasema: "Na Musa akasema: "Enyi kaumu yangu Ikiwa nyinyi mumemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye kama nyinyi ni Waislamu kweli." "Wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Ee Mola wetu. Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na hao watu madhalimu." "Na utuokoe kwa rehama yako na hao watu makafiri."


Katika kukabiliana na mateso makali na maudhi na madhila ya akina Firauni, Nabii Musa AS aliwataka watu wa kaumu yake watawakal kwa Mwenyezi Mungu na kuwaonyesha kuwa kutawakkal na kumtegemea Allah tu na kusalimisha muislamu mambo yake yote kwa Mola wa haki ni sharti la imani ya kweli. Nao wale waliokuwa wamemuamini kikweli kweli Musa as waliyasikiliza mawaidha hayo waliyopewa na Mtume wao na kusema, sisi hatuna kimbilio wala egemeo jengine ghairi ya Allah sw na hivyo tunamuelekea yeye na kumwomba atulinde na shari ya madhalimu na makafiri.Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa wakati wa masaibu na misukosuko Mola Mwenyezi huwa ndiye tegemeo pekee la mja muumini, na kwa kweli kwa kumtegemea yeye Mola aliye Muweza wa kila kitu na kujisalimisha kwake kwa kushikamana na maamrisho yake na kujiepusha makatazo yake, mja huweza kufaulu katika kukabiliana na misukosuko yoyote inayomkuta. Aidha kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa dua na kushtakia hali yake mja kwa Mola, ni miongoni mwa njia za kumnasua mja na mazonge. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu ya juma hili na kumwomba Mola aijaze subra ndani ya nyoyo zetu, athibitshe imani zetu na atunusuru na kila fitna inayoweza kutuweka mbali na dini yetu. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.


Yunus 87-92
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran. Hii ni darsa ya 322, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 87 ambayo inasema:
"Na tukampelekea Musa na ndugu yake wahyi ya kwamba: Watengenezeeni majumba watu wenu katika Misri na zifanyeni nyumba zenu zielekeane, na mshike Sala na wabashirie Waumini."

Ili kuijenga tena jamii ya Bani Israil, baada ya kuikomboa na madhila ya Firaun, Nabii Musa as aliamriwa na Mola wake kuwakusanya watu wa kaumu yake mahali pamoja na kwa msaada wao kujenga nyumba kwa ajili ya makaazi yao. Nyumba hizo zilitakiwa ziweko mahali pamoja zikiwa zimeelekeana na si kutawanyika huku na huko ili iwe rahisi kwao kujumuika pamoja kwa ajili ya kupanga na kuchukua maamuzi mbali mbali ya kijamii, na pia endapo Firauni atataka kuwaangamiza waweze kusimama pamoja na kukabiliana naye.Baadhi ya wafasiri wa quran wanasema, kutokana na kutolewa amri ya sala katika aya hii, muradi uliokusudiwa hapa juu ya neno qibla ni kuzijenga nyumba zao hizo kwa namna ambayo zitakuwa zimeelekea upande wa kibla ili wakiwa ndani ya nyumba zao waweze kutekeleza ibada zao. Pamoja na hayo maana hiyo ni ya kiistilahi, na kimsingi makusudio ya neno qibla kilugha ni maana hiyo hiyo ya kuelekeana. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa mojawapo ya sifa za Mitume ilikuwa ni kuwafikiria watu na hivyo kila wakati wakichukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kuwasaidia watu wa kaumu zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kushughulika na masuala ya kimaada na kimaisha kusitughafilishe na utekelezaji wa sala na kumwabudu Mola wetu. Kutekeleza kwa pamoja yote hayo ndiko kutakakotufanya tupate rehma na baraka za Mola Karima.


Zifuatazo sasa ni aya za 88 na 89 ambazo zinasema: "Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na watu wake wakubwa mapambo na mali katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanapoteza watu na Njia yako. Mola wetu! Ziangamize mali zao na zifunge nyoyo zao, wasiamini mpaka waione adhabu chungu." "Mwenyezi Mungu akasema: Maombi yenu yamekubaliwa. Basi simameni sawasawa, wala msifuate njia za wale wasiojua."


Katika kuendelea na utekelezaji wa jukumu alilopewa na Mola wake la kupambana na Firaun, Nabii Musa AS alimwomba Allah SW auangamize utajiri uliopindukia mpaka aliokuwa nao Firaun na kutomruhusu aendelee kufanya ufisadi na uharibifu, pamoja na kutumia vibaya nguvu na mamlaka aliyokuwa nayo kutokana na utajiri na neema za kimaada alizoruzukiwa na yeye Mola Karima; mali na neema ambazo alikuwa akizitumia kwa ajili ya kupotosha watu na njia ya Mwenyezi Mungu. Nabii Musa aliomba dua hiyo kwa Mwenyezi Mungu pale ilipofika hadi akawa hana matumaini tena kwamba Firauni ataamini na kuikubali haki.


Allah sw aliitakabalia dua ya Mtume wake, na hivyo akamtaka Mussa as na watu wake wao wenyewe kwanza wasimame sawa sawa na kushikamana na njia ya Mola wao; kwani sharti mojawapo la kutakabaliwa dua ni waumini wenyewe kwanza kuwa wameshikamana barabara na njia ya uongofu. Na ndiyo maana kwa mujibu wa hadithi ni kwamba ilichukua muda wa miaka arubaini tokea Nabii Musa alipoomba dua ya kumwapiza Firauni hadi taghuti huyo alipoangamizwa kwa kugharikishwa baharini. Aya hizi pamoja na mambo mengine zinatufunza kwamba, kuwa na utajiri wa mali tu si kipimo cha kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu amemjali na kumpenda mja. Kwani katika dunia hii, hata makafiri nao wamepewa neema nyingi za kimaada. Halikadhalika aya zinatuonyesha kuwa pamoja na sisi kumwomba Mola awaangamize madhalimu, sisi wenyewe pia tujihimu na kutekeleza wajibu wetu ipasavyo.


Darsa ya 322 inahitimishwa na aya za 90, 91 na 92 ambazo zinasema: "Tukawavusha bahari wana wa Israili, na Firauni na askari wake wakawafuata kwa dhulma na uadui. Hata Firauni alipokuwa anataka kuzama akasema: "Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliyemuamini Wana wa Israili, na mimi ni miongoni mwa wanaonyenyekea." "Ala! Sasa (unaamini hayo)? Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa mafisadi!" "Leo basi tutakuokoa kwa kuuweka mwili wako, ili uwe ishara kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na ishara zetu."


Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinabainisha jinsi dua iliyoombwa na Nabii Musa as ilivyotakabaliwa, na kueleza kuwa pale jeshi la Firauni lilipoamua kukuandameni nyinyi kwa lengo la kukuangamizeni, sisi tulikufungulieni njia katika mto Nile na kukupitisheni salama usalimini. Ama Firauni na jeshi lake wao tuliwagharikisha kwenye mto huo na tukaamua kukiibua kutoka majini kiwiliwili cha Firauni tu peke yake, ili hilo liwe funzo na ibra kwa wengine. Nukta yenye kutoa mguso hapa ni kuwa ule utabiri wa Nabii Musa tuliouona katika aya iliyotangulia ulithibiti na kuwa kweli, kwani wakati Firauni alipoiona adhabu ya kugharikishwa imemkabili hapo alitamka kwa unyenyekevu kuwa amemwamini Mola wa haki waliyemuamini Bani Israil.


Lakini wapi! jibu alilopata ni kuwa, hivi sasa wakati mauti yamekukabili ndiyo unatubia na kuiamini haki. Hayo ni majuto matupu yaliyopitwa na wakati na majuto ni mjukuu. Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa katika kupambana na mataghuti, tutawakal na kumtegemea Mwenyezi Mungu tu, kwani yeye hatotuacha mkono bali atatufungulia njia ya faraja hata pale tutakapkuwa katika hali ngumu kabisa ya misukosuko.


Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa, kama sisi tutasimama imara na bila kutetereka katika njia ya laa ilaha illa llah mataghuti hawatokuwa na jengine la kufanya ghairi ya kupiga magoti na kusalimu amri, na kupata jaza ya maovu yao. Aidha aya zinatuonyesha kuwa kuna umuhimu wa kuzitunza na kuzihifadhi athari na turathi za watu waliotangulia zinazoonyesha uwezo wa Allah sw, ili ziwe funzo na mazingatio kwetu sisi na watakaokuja baada yetu. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii, kwa kumwomba Allah atuwafikishe kutubia makosa yetu mara tu tunapoteleza, na kupata maghufira na msamaha wake kabla ya kufikwa na mauti. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmallahi Wabarakaatuh.