TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

 


Yunus 62-67
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 318 tunayoianza kwa aya za 62, 63 na 64 ambazo zinasema:
"-Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa na khofu (siku ya Kiyama) wala hawatahuzunika." "-Nao ni wale ambao waliamini na wakawa wanamcha Mungu." "-Wao bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa."


Katika darsa kadhaa zilizopita tulisoma aya zilizozungumzia hali ngumu ya adhabu watakayokabiliana nayo wale waliokufuru na kumshirikisha Allah sw. Aya tulizosoma hivi punde zinabainisha hali watakayokuwa nayo waumini wa kweli waliomcha Mwenyezi Mungu, ili kwa kulinganisha hali za makundi mawili hayo iweze kufahamika ni ipi njia ya saada na ipi yenye mwisho mbaya.


Utulivu wa roho na kutopatwa na ghamu wala hali yoyote ya huzuni ni miongoni mwa neema kubwa ambazo Allah atawatunuku waja wake wema. Waja ambao kutokana na kujiweka mbali na madhambi na maovu waliweza kujikurubisha kwenye chemchemu ya usafi, mema na mazuri yote yaani Allah sw na kwa taabiri ya quran tukufu kuingia kwenye kundi la mawalii yaani vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Ni wazi kuwa nafsi za watu kama hao siku zote humiminikiwa na rehma za bishara njema za Mola Karima na hivyo katu huwa hawapatwi na shaka, ugoigoi au hali ya ulegevu katika kutekeleza majukumu yao ya kidini. Bwana Mtume Muhammad saw amesema:" Kimya cha mawalii wa Mwenyezi Mungu ni dhikri, kutazama kwao ni ibra, maneno yao ni hikima na harakati zao katika jamii, ni sababu ya kupatikana baraka.


Naye Imam Ali as amesema: "Usije ukamdunisha mtu yoyote yule, kwani Mwenyezi Mungu ameficha mawalii wake miongoni mwa watu, hivyo si hasha yule umdunishaye akawa ni mmoja wao na wewe usijue". Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa yule ambaye moyo wake unamkhofu Mwenyezi Mungu tu hawezi kumkhofu yeyote mwengine. Aidha aya zinatuonyesha kuwa imani bila taqwa huwa haina athari; muumini wa kweli ni yule ambaye kila wakati anajichunga na kujiweka mbali na maovu na mambo machafu. Zifuatazo sasa ni aya za 65 na 66 za sura yetu ya Yunus ambazo zinasema:
"-Wala yasikuhuzunishe maneno yao. Hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.Yeye ndiye asikiaye na ajuaye." "-Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo mbinguni na ardhini. Na wala hawawafuati hao wanaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ni washirika wake. Wao hawafuati ila dhana tu na hawasemi ila uwongo."


Mushirikina wa Makka walikuwa wakimsingizia Bwana Mtume kila sifa mbovu kama vile kusema kwamba yeye ni mshairi, kuhani na mchawi bali hata mwendawazimu na wakisema: maneno haya ayasemayo Muhammad anafundishwa na watu wengine. Na wakati mwingine wakisema kuwa yeye ni mtu kama wao tu wala lolote la ubora zaidi yao.


Katika kuyajibu maneno hayo yasiyo na msingi ya Mushirikina Allah sw anamliwaza Mtume wake kwa kumwambia, irada ya Mola wako imeshakata na kuhukumu kuwa wewe na wafuasi wako muwe na izza na utukufu; nao hao mushirikina hawawezi kufanya lolote kukabiliana na irada hiyo. Na sababu ni kuwa ulimwengu na kila kilichomo ndani yake viko chini ya mamlaka yake Mola wako aliyetukuka, na kwa hivyo wale wanaowaendea waola ghairi ya Mwenyezi Mungu mtukufu si wao wenyewe wala hao waungu wao bandia walio na uwezo wa kufanya lolote. Aya hii pamoja na mambo mengine inatuelimisha kuwa mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na maadui wa Uislamu ni kuharibu haiba na shakhsiya ya viongozi wa dini hiyo tukufu.


Na hilo halikuishia katika zama za mwanzoni mwa kudhihiri kwa Uislamu bali linaendelea kushuhudiwa hata katika zama zetu hizi. Hata hivyo Allah sw ameshaahidi kuwa maadui hao katu hawatofanikiwa kwa kupitia njia hiyo kulifikia lengo lao hilo.

Tunaihitimisha darsa yetu ya 318 kwa aya ya 67 ambayo inasema:
"-Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyekujaalieni usiku mpate kutulia humo, na mchana wa kuonea. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaosikia."

Aya iliyopita imeashiria utawala mutlaki wa Allah SW katika ulimwengu na kila kilichomo ndani yake. Aya tuliyosoma ya 67 inagusia tadbiri yenye hikima kubwa ya Mola na kueleza kuwa mfumo wa mabadiliko ya usiku na mchana ni mojawapo ya madhihirisho ya uwezo wa Mola Mwenyezi katika uendeshaji wa ulimwengu.


Katika aya mbali mbali za quran usiku umetajwa kuwa kitoa utulivu cha mwanadamu. Ni wazi kwamba wakati ambapo utulivu wa kiwiliwili unayumkinika kwa kulala na kupumzika, utulivu wa roho hupatikana kwa dua, minong'ono na kushtakia mja hali yake kwa Mola na Muumba wake. Aya hii pamoja na mambo mengine inatuelimisha kuwa mfumo tuushuhudiao wa ulimwengu haukutokea kwa bahati tu bali ni kitu kilichoumbwa na kuendeshwa kwa lengo na irada maalumu. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu ya juma hili. Inshallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake washukurivu wa neema zake na wanaozingatia na kuyatafakari maumbile ya ulimwengu ili kuweza kuitambua ipasavyo adhama ya Mola wao... Amin. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.


Yunus 68-73
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo huu wa 319 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 68, 69 na 70 ambazo zinasema:
"Wamesema: Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto. Ameepukana na hayo. Yeye ni Mkwasi Mwenye kujitosheleza. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Nyinyi hamna uthibitisho wowote wa haya. Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyoyajua? Sema: Wale wanaomzulia Mwenyezi Mungu uwongo hawatafaulu."


"Hiyo ni starehe ya katika dunia tu, kisha kwetu ndiyo marejeo yao ni kwetu. Hapo tutawaonjesha adhabu kali kwa sababu ya kukufuru kwao." Moja kati ya itikadi porofu na ya uzushi ambayo walikuwa nayo watu wa kaumu na uma zilizopita na ambayo inashuhudiwa pia hata hii leo ni kumjaalia Mwenyezi Mungu kuwa na wana na kuwanasibisha na yeye Mola Mwenyezi. Katika historia ya Uyahudi, wafuasi wa dini hiyo walimfanya Uzair mwana wa Mungu, nao wakristo wakatenda hayo hayo kuhusiana na Nabii Issa mwana wa Maryam. Hali ya kuwa kwanza kabisa ni kwamba Mwenyezi Mungu hana mke hata awe na mtoto.


Pili ni kuwa Allah hahitaji kuwa na mwana, na tatu ni kwamba mtu ambaye ni kiumbe aliyeumbwa kamwe hawezi kuwa mwana wa Mungu kwa sababu jinsia ya mtoto hutokana na ile ya wazazi wake wawili yaani baba na mama, hali ya kuwa kama tulivyotangulia kusema Mwenyezi Mungu aliyetukuka ametakasika na sifa ya kuwa na mke. Kuhusiana na kauli zote hizo za batili na zisizo na mashiko quran tukufu inasema wale wanaotamka maneno hayo wajue kwamba lazima watawajibika kwayo, na siku ya kiyama watakuja kupata adhabu kali kwa sababu ya uzushi huo waliomnasbishia nao Mwenyezi Mungu sw.


Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa Mola mtukufu hatishwi na upweke hata ahitajie mwana kwa ajili ya kuuondoa upweke huo. Hahitajii msaada hata na awe na shida ya kuwa na msaidizi, na wala hachelei kuondoka hata iwepo haja ya mrithi wa baada yake. Subhanallah, ametakasika Mola aliyetukuka na kasoro zote hizo bali na nyinginezo. Aidha aya zinatuonyesha kuwa lau mja angelinganisha mapungufu yaliyonayo maisha ya kupita ya dunia na hilaki ya adhabu isiyoweza kukadirika ya akhera basi angechunga na kujiweka mbali na kutamka mengi na kutenda mengi yanayomghadhibisha Mola wake.


Ifuatayo sasa ni aya ya 71 ambayo inasema:
"Wasomee khabari za Nuhu alipowaambia watu wake:"Enyi watu wangu! Ikiwa kukaa kwangu nanyi na kukumbusha kwangu Aya za Mwenyezi Mungu kunakuchukizeni, basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu. Nanyi tengenezeni mambo yenu na hao washirika wenu. Tena shauri lenu hilo lisifichikane kwenu. Kisha nihukumuni.Wala msinipe muhula." Nabii Nuh AS ni mmoja wa Mitume wateule wa Allah ambaye kwa miaka mingi sana alifanya kazi ya kuwalingania watu wa kaumu yake, lakini ni wachache tu miongoni mwao waliomuamini na akthari yao waliendelea kubaki kwenye shirki na ukafiri.


Aya hizi ambazo zilishuka huko Makka zinawaliwaza waislamu ambao walikuwa katika unyonge na hali ngumu ya maisha na kuwataka wawe na imani ya kupata msaada wa Mwenyezi Mungu na kuelewa kwamba Allah sw yuko pamoja na wao na hivyo wasimame imara kama alivyosimama Nabii Nuh as ambaye licha ya vitisho na kila aina ya njama za wapinzani wa haki alisimama peke yake na kubeza nguvu na vitisho vyao kwa kuwaambia jumuikeni pamoja nyote na amueni chochote mnachotaka kuamua juu yangu, lakini jueni kwamba mimi nimetawakal kwa Mwenyezi Mungu na kutegemea nguvu na uwezo wake yeye tu. Aya hii inatuelimisha kuwa historia ya waliotutangulia inabainisha wazi kwamba haki ni yenye kubaki na mwisho wa batili ni kutoweka na kwa hakika kuelewa yaliyojiri huko nyuma kunatoa mwanga wa kuonyesha njia ya huko tunakoelekea.Aya za 72 na 73 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hizo zinasema: "Lakini mkikengeuka (khiyari yenu). Mimi sikuombeni ujira. Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wanaojisalimisha kwake."

"Lakini walimkadhibisha. Basi tukamuokoa pamoja na waliokuwa naye katika jahazi. Na tukawafanya wao ndio waliobakia. Na tukawazamisha wale waliozikadhibisha Aya zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa wale walioonywa (wasisikie)." Katika harakati yao ya kuwalingania watu njia ya Mwenyezi Mungu Mitume sio tu walikuwa tayari kukabiliana na hatari yoyote hata inayotishia maisha yao lakini pia hawakutarajia kupata chumo au mali yoyote ile ya dunia kwa sababu ya kazi hiyo nzito waliyokuwa wakifanya. Kwa maneno mengine ni kuwa hawakuwa wakitarajia chochote kwa watu mkabala wa kheri waliyokuwa wakiwafikishia.Na ndiyo maana walikuwa wakiwaeleza bayana watu wao kwamba msidhani kuwa msipotuamini, kuna hasara tutakayopata kwani hatutarajii kupata ujira au malipo yoyote yale kutoka kwenu; sisi tunafanya yale tu tuliyoamrishwa na Mola wetu. Kisha aya zinaendelea kubainisha mwisho na hatima ya wapingaji haki na kueleza kuwa kwa kuteremka adhabu ya Mwenyezi Mungu na dhoruba kali, maji yalifunika kila kitu na ni wale waliokuwa wamepanda jahazi na Nabii Nuh ndio wao tu waliookoka na wakawa warithi wa ardhi, na kwamba hakuna mwisho mwingine unaowapata wale wanaoonywa wakapuuza zaidi ya huo uliowapata waliomkadhibisha Nauh as. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji ndiyo tumefikia tamati ya darsa hii ya 319 ya quran. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atulinde na kila aina ya shirki na kutuwafikisha kumwabudu kwa ikhlasi na kumtakasia dini yake. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.