TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

 


Surat Yunus 11-14
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hapa tunaianza kwa aya ya 11 ambayo inasema:
"Na lau kama Mwenyezi Mungu angeliwafanyia watu haraka kuwaletea shari, kama wanavyojihimizia kuletewa kheri, bila shaka wangelisha timiziwa ajali yao. Lakini tunawaacha wale wasiotumainia kukutana nasi, wakihangaika katika upotovu wao." Moja ya utaratibu ambao Allah sw ameuweka kuhusiana na waja wake ni kutoa muhula na fursa kwao, ili kila mmoja aamue na kuchagua kwa hiyari yake njia gani anayotaka kufuata, ikiwa ni ya kuiamini haki au kuikufuru. Kwa bahati mbaya akthari ya watu huwa hawaitumii kwa njia sahihi fursa hiyo adhimu wanayotunukiwa na Mola wao, na badala yake huogelea kwenye dimbwi la maasi na maovu. Pamoja na hayo Mola aliye mrehemevu huendelea kuamiliana kwa upole na ukarimu na waja wake kwa kuwapa fursa nyingine ya kutubia kwa madhambi waliyoyafanya ili wapate maghufira na msamaha wake.


Ama ikiwa hata baada ya kupata fursa hiyo mja ataamua kuselelea katika kutenda maovu na kumwasi Mola Muumba, mja wa aina hiyo huachwa kama alivyo aendelee kufuata njia hiyo ya upotofu hadi kipindi cha uhai wake kinapomalizika, ambapo hapo huelekea ulimwengu mwingine wa akhera na huko hupata jaza na malipo ya maovu na maasi aliyoyafanya hapa duniani. Aya hii pamoja na mambo mengine inatufunza kuwa kutoangamizwa kwa makafiri na madhalimu hapa duniani hakumaanishi kuwa yale wayafanyao ni ya sawa au kwamba Mwenyezi Mungu sw anashindwa kuwateremshia adhabu. Bali hiyo inatokana na ile fursa na muhula ambao Allah ameamua kuwapa waja wake hao.


Ifuatayo sasa ni aya ya 12 ambayo inasema: "Na mtu akiguswa na shida hutuomba, naye kaegesha ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama kwamba hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyompata. Namna hivi wamepambiwa warukao mipaka yale waliyokuwa wakiyatenda."

Raha na neema za kidunia wapenzi wasikilizaji humfanya mtu aghafilike na Mola wake na kuikumbatia dunia. Ama shida, masaibu na matatizo mara nyingi humfumbua macho mtu huyo na kumfanya aelewe kuwa binadamu ni kiumbe dhaifu kiasi kwamba pale anapotingwa na matatizo hutambua jinsi ya kumwomba na kumlingana Mwenyezi Mungu kutaka msaada, awe kitandani anaugua maradhi akiomba aponywe, au baharini na angani pale mauti yanapomkabili akawa hana njia nyingine yoyote ya kujiokoa, na hivyo kutaka nusra ya Mwenyezi Mungu sw. Ya laiti baada ya mja kuitikiwa kilio chake hicho angeweza walau kumshukuru tu Mola wake na kuendelea kumkumbuka japo kwa siku chache. Lakini wapi! Akthari ya watu humsahau haraka Mwenyezi Mungu kana kwamba hawakuwa wametingwa na masaibu na ni yeye Mola aliyetukuka ndiye aliyewaondolea masaibu hayo. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa imani ya kuwepo na Mungu mmoja imekita ndani ya nafsi ya kila mwanadamu, na kwa kweli maafa, shida na misukosuko huwa ndiyo chachu ya kuiamsha fitra na maumbile hayo yaliyolala ya kukiri kuweo kwa yule aliye na uwezo mutlaki wa kila kitu.


Aya za 13 na 14 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema: "Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza uma nyingi kabla yenu walipodhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa hoja zilizowazi; lakini hawakuwa wenye kuamini. Namna hivi tunawalipa watu wanaofanya waovu.""Kisha tukakufanyeni nyinyi ndio wenye kushika mahala pao baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyotenda." Ijapokuwa kama tulivyotangulia kunena katika aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu huwapa muhula wale wanaomwasi na kufanya madhambi na kutowaangamiza papa hapa duniani, lakini hili huwa ni tofauti linapohusu umma au kaumu nzima ya watu, pale watu hao wanapokithirisha dhulma na madhambi, kwani hatima ya kaumu za aina hiyo ni kuangamizwa. Kisha baada ya kuangamizwa kaumu hizo huletwa mahala pao kaumu ya watu wengine ambao wanatakiwa kuyachukulia yale yaliyowasibu waliowatangulia kuwa ni ibra na funzo kwao, vinginevyo na wao pia watapatwa na majaaliwa kama yao.Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa dhulma na uonevu ni mambo yanayoandaa mazingira ya kuangamizwa watu, tabaan wale watu ambao hakuna matumaini tena kwa wao kuamini na kuifuata haki. Halikadhalika aya zinatuelimisha kuwa hatima na majaaliwa ya watu yako mikononi mwao wenyewe, na kwa kweli ni matendo yao mabaya na maovu ndiyo yanayoainisha wawe na hatima gani. Na pia aya zinatufunza kwamba endapo mtu atajiona amepata madaraka au mamlaka ya utawala, ajue kuwa huo ni mtihani ambao Mwenyezi Mungu amempa kumjaribu. Tunamwomba Allah atuwafikishe kufuzu mitihani yake na atuzindue kila pale tunapoghafilika na kumkumbuka yeye. Amin.
Surat Yunus 15-18
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 309 tunayoianza kwa aya ya 15 ambayo inasema: "Na wanaposomewa aya zetu zilizo wazi, wale wasiotaraji kukutana nasi husema: Lete quran isiyokuwa hii au ibadilishe. Sema: Siwezi kuibadilisha kwa hiyari ya nafsi yangu. Mimi sifuati ila ninayofunuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa nikumuasi Mola wangu adhabu ya siku iliyo kuu."


Washirikina na waabudu masanamu ambao walikuwa walinganiwa wa wito wa tauhidi aliokuja nao Bwana Mtume Muhammad saw, badala ya kuachana na itikadi na ibada zao hizo potofu, ni wao ndio waliomtaka bwana Mtume akidhi matakwa yao kwa kuzifuta katika Quran zile aya zinazokataza na kukemea ibada ya masanamu, au hata ikiwezekana kuleta kitabu kingine kabisa kisicho na aya za aina hiyo, ili hapo ndipo wao wamwamini Mtume huyo wa Allah. Hali ya kuwa lengo la Mitume ni kuwaelekeza watu kwenye uongofu na si kutaka kujipatia wafuasi wengi zaidi. Kwa maana kwamba katu hawawezi kukubali matakwa yasiyo ya kimantiki ya watu kwa sababu tu ya kutaka kupata idadi kubwa zaidi ya wafuasi. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa hakuna mtu yeyote yule hata Mtume aliye na haki ya kuibadilisha hata aya moja ya vitabu vya mbinguni vilivyoteremshwa na Allah, bali manabii hao, wao wenyewe ni wenye kujisalimisha na kutii kikamilifu kila kilichokuja katika risala ya wahyi walioteremshiwa na Mola wao. Aidha aya inatuelimisha kuwa msingi wa mafundisho ya Uislamu ni kushikamana nayo kama yalivyo yale yaliyoletwa na Mwenyezi Mungu, na wala hakuna thamani yoyote kuifanya dini iwe na wafuasi wengi zaidi kwa gharama ya kubadilisha na kupotosha mafundisho yake ya asili.


Zifuatazo sasa ni aya za 16 na 17 ambazo zinasema: "Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nilikwisha kaa nanyi umri mzima kabla yake! Basi, je hamzingatii?" "Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uwongo Mwenyezi Mungu na akazikanusha aya zake? Hakika hawafaulu wale wafanyao maovu."


Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaendelea kutoa jibu kwa wale watu waliomtaka Bwana Mtume Muhammad saw aibadilishe quran na kuwaambia, Mtume huyu ameishi na nyinyi kwa miaka arubaini. Lau quran hii ingekuwa imetokana na fikra zake yeye mwenyewe bila shaka katika kipindi hicho chote mungeweza kushuhudia maneno mithili ya hayo katika fikra zake. Isitoshe ni kuwa yeye Muhammad hakuwahi kusoma popote wala kufunzwa na yeyote hata mseme labda hii quran itakuwa ni matunda ya elimu hiyo aliyokuwa amejifunza hapo kabla. Hivyo wale wanomtaka yeye aibadilishe quran hakika wanachofanya ni kuzikadhibisha aya za Mwenyezi Mungu na kumzulia uwongo yeye Mola Muumba, jambo ambalo ni sawa na kumfanyia dhulma kubwa kabisa yeye Mola, Mtume wake na kitabu chake cha quran. Baadhi ya tunayojifunza katika ya hizi ni kuwa vitabu vya mbinguni ni wahyi utokao moja kwa moja kwa Allah na wala si kitu kinachotokana na fikra za Mitume au mtu mwengine yoyote. Aidha zinatutaka tuelewe kuwa dhulma kubwa kabisa ni ile ya kupotosha na kuyabadilisha mafundisho asili ya dini.


Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 18 ambayo inasema: "Nao wanaabudu (waungu) wasiokuwa Mwenyezi Mungu wasioweza kuwadhuru wala kuwanufaisha. Na wanasema: "Hao ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu". Sema:"Je Mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi?".Ameepukana na upungufu (wa kutaka mshirika), na ametukuka na hao wanaowashirikisha naye."


Washirikina walikuwa wakiyaabudu masanamu ambayo si kwamba yalikuwa yana uwezo wa kuwadhuru hata kwa kukhofia hilo wahisi kuwa hawana budi ila kuwaabudu, na si kwamba pia kuna faida walikuwa wakipata kwa masanamu hayo hata tamaa ya kupata faida hiyo iwe sababu ya kuwafanya wawapigie magoti na kuwaomba. Ama hoja waliyokuwa wakiitoa washirikina hao ni kuwa masanamu hayo yalikuwa ni wasita na kiunganishi kati yao na Mwenyezi Mungu.


Hata hivyo hoja hii haikubaliki kwa sababu Mwenyezi Mungu hakuyafanya masanamu hayo ni wasita, kiunganishi na waombezi wa waja wake kwake yeye. Hii ni tofauti na wala haiwezi kulinganishwa na suala la tawasul wanayofanya watu kwa Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuomba wawatakie shufaa mbele ya Mola, kwani hao wako katika maisha maalumu ya barzakhi waliyojaaliwa na Allah na vile vile ni yeye Mola mwenyewe aliyewaelekeza watu watumie wasita wa waja wake hao walio wateule kwa ajili ya kumfikia yeye. Funzo moja muhimu tunalolipata kutokana na aya hii ni kuwa tujihadhari na kukifanya kitu au mtu yeyote yule kuwa mshirika wa Allah katika uungu, au kukifanya kitu au mtu kuwa na hadhi ya kuweza kutushufaia na kutuombea mbele ya yeye Mola, ghairi ya wale yeye Allah mwenyewe aliowapa daraja hiyo ya kuwa waombezi kwa waja wake. Darsa ya 309 imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki. Amin.