MASHAIRI

 
YAPASA TUYALILIE MAUTI YAKE HUSSEIN

Na: Masoud Abdallali Muh'd,
Mombasa - Kenya

IMAM SHAFII ASEMA:
1. Hussein! aliuliwa shidi pasi na makosa yoyote na kanzu yake ikatapakazwa wekundu.
2. Ikiwa dhambi zangu ni kuwapenda watoto wa Mtume Mohammad (s.a.w.) basi ni dhambi ambazo sitatubiya.
3. Kwa sababu ya Ahlil-Beit wa Mtume (s.a.w.) Ulimwengu mzima ulitetema na majabali na milima ilikaribia kuyeyuka.
4. Ni nani atakayemfikishia Hussein ujumbe wangu na hata kama nyoyo zatukia?

SIFA ZA IMAM HASSAN NA IMAM HUSAIN (A.S.)
________________________________________
Nawapa na taarifa Japo kuwa walikufa
Walikuwa wana sifa Njema ilotimilia

Walikuwa watukufu Tena ni waaminifu
Walo na njema sharafu Alowajazi Jalia

Walikuwa Maimamu Kuongoza Isilamu
Mashujaa walotimu Dini kuipigania

Walikuwa watu wema Vijana wenye heshima
Akiwapenda Hashima Wajukuu wa Nabiya

Walikuwa wenye dini Maovu hawathamini
Na nyingi mno imani Nyoyoni ilowangia

Walikuwa na huruma Isilamu wenye hima
Toka kwa watu wazima Na vijana wote pia

Walikuwa wasifika Duniani kutukuka
Tena waliyoumbia Kwa uzuri na tabia

Walikuwa makarimu Huwezi kuwalaumu
Kisha ni wenye ilimu Ya dini na ya dunia

Walikuwa wafalume Wajukuu wa Mtume
Mashujaa wenye tume Vitani kushambulia

Sifa zao ni kathiri Tena zote ni nzuri
Wala hazina akhiri Wallahi zimezidiaMtoto wake Husseini
________________________________________
Jambo jengine ni hili La majonzi ikhiwani
Hiki si kisa cha pili Ambacho ni cha huzuni
Ni cha kijana rijali Mtoto wake Husseini

Kadhulumiwa Husseini Na wake mwana mchanga

Naye kafa madhulumu Kijana wa mikononi
Muovu huyo Khasimu Adui aso imani
Bure kaimwaga damu Ya kijana maskini

Kadhulumiwa Husseini Na wake mwana mchanga

Kifo chake ni dhuluma Kijana huyu yakini
Adui aso huruma Aso Imani moyoni
Kwa mshale kamfuma Ukamwingia mwilini

Kadhulumiwa Husseini Na wake mwana mchanga

Mshale ulimdunga Mtoto wake Husseini
Ikawa hapana kinga Ya kuiyepuka zani
Akafa mwana mchanga Kiumbe cha Rahamani

Kadhulumiwa Husseini Na wake mwana mchanga

Ovu liso wezekana Kupata chake kifani
Kiumbe chake rabana Kilo safi cha peponi
Walimu-uwa kijana Bila kosa asilani

Kadhulumiwa Husseini Na wake mwana mchanga

Huyo ni wake uwele Alo mughuri shetani
Alomdunga mshale Kipenzi chake amini
Naye piya vile vile Ataingia motoni

Kadhulumiwa Husseini Na wake mwana mchanga

Kwa kumuuwa kijana Malaika kwa yakini
Hata akatubu sana Haipati samahani
Adhabu yake ragana Kwake haiwezekani

Kadhulumiwa Husseini Na wake mwana mchanga

IMAM HUSAIN (A.S.) ASEMA:

"Kufa kwa heshima ni bora kuliko kuishi kwa aibu".

YA SAYYIDNA HUSEINI :
________________________________________
Kukuomba sina budi Ya razaku ya wadudi
Ili utimu mradi Yote nalo kusudia

Sikutaka kusimama Mengi mno kuyasema
Ni mambo kunisukuma Ni lazima kuelezea

Natokeza hadharani Kwa ufupi nibaini
Yalomfika Husseini Ya Rabbi niafikia

Yale ni mambo adhimu Yalomfika Imamu
Sina shaka mwafahamu Nami tawahadithia

Ule mwaka wa sitini Wahijira sikiani
Kaondoka duniani Muawiya kajifiya

Yazidi alitangaza Nchi zote kaeneza
Dini ataiongoza Ili watu kumbaiya

Barua aliandika Madina kaipeleka
Kwa walioikafika Nae akimwelezea

Kwa makini isomeni Mfahamu yalo ndani
Kahitaji kura zenu Isilamu wote pia

Nazidi kuyabaini Yalio mwangu moyoni
Ni kura yake Husseini Ufike kumwelezea

Husseini kastakimu Akasema yakatimu
Huyo ni mtu dhwalimu Kidini hakutimiya

Kama mimi ni haramu Kukubali ya dhwalimu
Sitaki wake msemu Mwambiye sitoridhia

Kwanza yeye nakiburi Ni mlevi hana siri
Kajaa kila fujuri Nyote mnamtambua

Sitokuwa chini yake Hapa na pale afike
Taji hilo silo lake Hata yeye yamwelea

Mtume alibaini Kwa Hassani na Husseini
Ni Maimamu yakini Kila mtu kasikia

Alifu kumi na mbili Barua ziliwasili
Kwa mjukue Rasuli Iraq Zilitokea

Barua Zilimtaka Husseini huko kufika
Ukhalifa kuushika Dini kuisimamia

Yazidi si mtu mwema Sisi sote twafahamia
Na haya tunayosema Wewe twakushtakia

Husseini hakutwawili Katuma lbn Akili
Ili kujua ukweli Wa mambo yalomfikiya

Alipokewa vizuri Wadogo hatakibari
Walimfanya safiri Wa Husseini Msifiwa

Kisha mambo ligeuka Balozi walimwepuka
Mapanga wakayashika Muslimu kumuwa

Mwezi nane kutimia Mfungo tatu sikia
Husseini kashika njia Iraqi kaelekea

Naswaha zilimfika Twakuomba kutotoka
Iraqi usije fika Watu wakakukimbia

Husseini aliwambiya Hayo yote nasikia
Nitakwenda nadhuria Mtume kani uswiya

Wakiniuwa sijali Aliniambiya Rasuli
Kua hayo majangili Dhulima watatumia

Alipofika njiani Ilimaka yakini
Ni hayuko duniani Muslim kauwawa

Iraq waligeuka Unafiki wakashika
Hivi waja kukushika Husseini aliambiwa

Ule msiba adhimu Ulomfika Imamu
Yeye na wake kaumu Nakizaziche pamoja

Hapa ni pahali gani Niambiyeni jamani
Ni Karbala jangwani Huseini aliambiwa

Ibn Saad Omari Najeshile waliswiri
Maudhi na ujeuri Imamu wamfanyia

Unyama walifanyiwa Na kiu iliwauwa
Na maji kuzuiliwa Hayo yote watendewa

Kauwawa Akbari Pia hata Asghari
Na hao watu mashari Mungu yuwashuhudia

Asghari ni kijana Ni mdogo tena sana
Na kiu ilimbana Kwa chembe walimuua

Husseini aliuuiiza Fikirini mukiwaza
Kosa gani tulifanza Kutendewa kama haya

Himambo yenye huzuni Alotendewa Husseini
Nashindwa kuyabaini Ukumbuni ngatokea

Yangu haki mumetwaa Ya ukhalifa sisawa
Na leo mwanisumbua Nilipi mwafikiria

Au hamkusikia Usemi wahashimia
Hapo akiwauswia Kuhusu wake dhuria

Mama yangu ni Batuli Binti yake Rasuli
Na baba yangu ni Ali Waswii wake Nabia

Ya Husseini walimwaga Damu yake bila woga
Walijifanya wajinga Ufasiki mewashika

Kijukuu cha Rasuli Ni Husseini bin Ali
Achinjwa kama ghazali Wallahi twakulilia

Alipewa kila dhuli Mwanao ewe Batuli
Ateswa na majangili Waso dini sikiya

Walisahau ahadi Ya Mtume Muhammadi
Na wote ni mashahidi Mtume akiwauswia

Alimchinja Husseini Bila khofu na huzuni
Na Mungu si Athumani Nae atamlipia

Ni kifo chenye kutisha Tena kina babaisha
Wallahi chahuzunisha Kila kinapo tolewa

Na Mungu si Athmani Twalipa duniani
Wa kesho wenda motoni Adhabu yawangojea

Hapo ndipo nitafika Kalamu chini naweka
Kwa huzuni lonishika Siwezi kuendelea

Mola atupe Imani Yakumpenda Husseini
Tuwe nae na peponi Dua zetu zipokea

Kisha Swala na Salamu Zende hadi kwa Hashimu
Na alize Mainwnu Hasidi angachukia


Mashairi ya Masaibu ya Kerbala

Kimetolewa na
Ahlul Bayt [a.s.] Assembly of Tanzania
P O Box 75215
Dar es Salaam - Tanzania

Kimechapwa na
Bilal Muslim Mission of Tanzania
S.L.P. 20033
Dar es Salaam - Tanzania
________________________________________
Kimetolewa wavuni na timu ya
Ahlul Bayt Digital Islamic Library Project