ASHURA

 
MWISHO WA "WATU WA NYUMBA" (UTAJI)
Akijikuta peke yake pasi kuwa na mtu aliyeko ndani wala nje ya kambi yake, Husayn aliita kwa sauti je... yuko yeyote wa kutusaidia?, yuko yeyote wa kutuitikia na kututimizia haja yetu?, mwito huu haukuitikiwa na yeyote ila mtoto mchanga Ali Asghar ibne Husayn aliyekuwa wa mwisho katika watoto wake, ambae alikuwa na umri wa miezi sita tu, aliangua kilio kana kwamba kuitikia mwito wa babaake. Husayn alimbeba mtoto huyu mchanga akipapatika mikononi mwake kwa kiu ya maji, mtoto huyo hakuweza kustahimili dhiki, Husayn alitoka nae nje lakini ah... maadui walimjibu kwa kumfuma mtoto huyo kwa mshale wa vyembe vitatu na mtoto akafa mikononi mwa babaake.


Husayn alirudi katika hema lake na mwili wa mtoto mikononi mwake. Mamaake alipomuona aliliya na kuomboleza akisema: je watoto wa umri wenu pia huuliwa namna hii? Husayn hatimae alimchimbia kaburi ndogo kwa upanga wake na kumzika mtoto huyo. Baada ya mazishi ya mtoto Ali Asghar yasiyo kuwa na sherehe yoyote, Husayn aliingia tena kambini, akamwita kila mwanamke mmoja mmoja aliyekuwako na watoto akawaaga kwaheri ya mwisho, akamuaga dadake Zainabu pamoja na binti yake Sakina aliyekuwa kipenzi cha moyo wake, ambae alikuwa na umri wa miaka min'ne tu. Alimnasihi kuvumilia na kuwa na subira juu ya dhuluma yote yatakayo kuja, kwa sababu ya matakwa ya Mwenyezi Mungu, kupitia kwa Mtume wake mtukufu, ni muhimu kuliko kumhusu yeye mwenyewe. Katika dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake mtukufu hayana budi khususa kumuhusu yeye mwenyewe.Hatimaye akiandamana na Zainab, Husayn akamwendea mtoto wake mkubwa, aliyekuwa akiugua siku nyingi Ali Zainul Abideen, ambae ni mtoto mkubwa katika watoto wake na khalifa wakuelekea. Ali ibne Husayn, alivyokuwa katika hali ya maradhi kwa muda wa siku nyingi, hakuwa na khabari yoyote juu ya matukio ya siku na vifo vya watu wote wa babaake, alishutushwa na majeraha yaliyompamba babaake Husayn. Husayn alimtuliza na kumuaga kwaheri. Alipanda farasi wake mara ya mwisho akisaidiwa na dadake Zainab. Sasa Zainab ndiye mwangalizi mkuu wa usalama na jeshi katika kikundi chake kilichokuwa hakina yeyote, ila Zainul-Abedeen, Ali ibne Husayn na wanawake waliopotelewa na waume zao, watoto na ndugu zao kwa kushahidiwa vitani na baadhi ya watoto wachache. Husayn alisimama kati kati ya maadui na kuwaita akiwaambia wamuachilie na kusalimisha maisha yake ili apate kwenda zake baada ya kumuulia watu wake wote, marafiki zake, ndugu zake na wajomba zake na watoto wake ndani ya siku moja.Jawabu lake alijibiwa kwa umoja wa maadui, kwamba hawatamuachilia hadi atakapomtambua Yazid licha ya alivyodokezewa na Mtume. Husayn hapo alisema na kujitambulisha nafsi yake mbele ya majeshi ya Yazid kwamba yeye ni mjukuu wa Mtume, mtoto wa Ali na Fatimah binti ya Mtume na ndugu yake Hassan na kuimwaga damu yake hakutawafalia chochote katika ulimwengu wao sasa na wa baadaye pia. Alijaribu pia kuamsha fikira zao akiwambia iwapo hamuamini katika dini yoyote basi fikirini kama watu walio huru (kwamba yatendwayo si haki).Husayn mwenye umri wa miaka 57, bado alikuwa mkakamavu na mvumilivu juu ya kupoteza watu wake 72, katika kambi yake ambamo walikuwako miongoni mwao watu 18 wa jamii yake, ukoo wa Abutalib. Naam, Husayn sasa alipigana kishujaa na maadui zake hata kufikia wakati wa sala ya Al-asiri, Umar bin Sa'ad aliamuru vikosi vyote vya majeshi yake wamzingire kwa umoja na kupigana naye. Katika kipindi hicho ardhi yote ilitingishika, na jua lilipatwa na kutanda kiza cheusi kwa kutangazwa Husayn ameuawa katika Karbala, Husayn amekutuliwa katika Karbala, miongoni mwa sauti za maadui ilisikika na kuleta takbira ya "Allahuakbar", Mungu ni mkubwa, kwamba jamaa wa mwisho, mtakatifu wa nyumba ya Mtume (utaji) ameangushwa na kukatwa kichwa akiwa na njaa na kiu na Shamir ibne Joshan kwa tamaa ya kidunia aliyoahidiwa na Yazid. Dhuluma yao haikukomelea hapo kwa kumkutuli Imam Husayn bali mwili wake pamoja na miili ya wenzie wote ilikanyagwa kanyagwa na kuvurugwa na kwato za farasi wa maadui kiasi cha kuangamizwa kabisa. Historiya inajidhihirisha yenyewe.


Baadaye majeshi ya Yazid, yaliwavamia watu wa nyumba ya Mtume na kuzitia moto hema zao, waliwapokonya wanawake mavazi yao ya mitandio na hijab za vichwani, wakawapokonya kila kitu chao kichache walichokuwa nacho, waliwapokonya hata na bembeya ya mtoto Ali Asghar, jamii ya Mtume ilitendewa kinyama ikidhalilishwa na kuchukuliwa mateka. Zainab bint Ali, "Fatimah" wa pili na mshirika wa Husayn alijitolea kishujaa nakusimama imara, akijipa nguvu na kupiga moyo konde alivuta subira, baada ya kupotelewa na waume wote alishika jukumu la kuwakinga na kuwasaidia wanawake wote na watoto pamoja na Zainul-abedeen aliyekuwa mgonjwa akiu-gua ndani ya hema lililoshika moto na kuziponya nafsi zao. Alikuwa ndiye mwangalizi wao, mkuu wa usalama alisamehe usingizi na kujitolea kukesha usiku kucha akitekeleza jukumu lake kuihudumia jamii yake iliyo athiriwa. Iwapo hamuamini katika dini yoyote basi tafakurini japo kama watu walio huru. Imam Husayn ibne Ali (a.s.)


WATU WA NYUMBA YA MTUME WAKIWA KIZUIZINI
Ilikuwa siku ya kumi na moja ya mwezi wa Muharram mwaka mpya wa kiislamu Ali ibne Husayn, ambae daraja yake na heshima yake tukufu imeambatana na fakhari ya swalihina Zainul Abedeen na kiongozi wa wenye kusujudu Sayyidu Sajideen, alichukuliwa akafungwa kwa mnyororo mzito pasi kuhurumiwa juu ya hali yake ya ugonjwa. Wanawake na watoto wa nyumba wote walichukuliwa na kufungwa kwa kamba pamoja, walipandishwa juu ya migongo ya ngamia pasi kuwa na matandiko ya kukalia, na maiti za wale waliokutuliwa (mashahidi) ziliachwa vile vile pasi kuzikwa.


Wafungwa hawa walichukuliwa kutoka Karbala na kupelekwa Sham (Damascus), Jiji kuu la utawala wa Yazid, kupitia Kufa, ambako ni umbali wa mwendo upatao maili elfu moja, kukiwa na jua na joto kali lenye kuchoma katika jangwa. Njiani walimopitia, katika kila kijiji, "watu wa nyumba" walitembezwa na kutambulishwa kwa wana kijiji wa pale katika hali ya kufedheheshwa mno. Wanawake ilibidi wafunike nyuso zao kwa nywele zao za kichwani, kwa sababu ya kupokonywa hijabu zao au vitambaa vya kufunga vichwani, majeshi hayo ya Yazid aliyejiona khalifa hayakuwa na heshima wala majuto japo tembe juu ya watu hawa watakatifu wa nyumba ya Mtume, licha ya adabu mbele za wana wake hata kuwatendea haki mayatima kama yalivyo mafunzo ya Mtume na pia kuelezwa katika kitabu kitakatifu cha Qur'an.Wafungwa hawa, kisha walipelekwa katika baraza ya ibn Ziad, huko Kufa. Ibne Ziad alikuwa mtoto wa haramu wa Abu Sufian, hivyo ni ndugu wa Muawiya. Tabia zake za hila na ubaya na ukatili usiokuwa na huruma zilijulikana kote katika ulimwengu wa waarabu. Aliwapokea wafungwa hawa watakatifu wa nyumba ya Mtume kwa shangwe kuu. Aliamrisha kila pembe ya mji wa Kufa barabara zake zipambwe kwa mapambo mazuri mazuri na kushangilia ushindi wa Banu Umayya juu ya 'Ufalme' wa Hashim na watu wa nyumba ya Mtume Muhammad, watembezwe mbele za umati walio kusanyika. Katika msafara mmoja kama huo Ibne Ziad alipomchocha bibi mtakatifu Zainab aliyeheshimiwa sana akashangazwa mno kumwona bibi huyu (simba mke) alivyomjibu kishujaa katika barabara ya mji kwa sauti ya juu pasi kumjali hata watu wakadhania kwamba ni sauti ya Ali ibne Abu Talib alipohutubu pasi na uoga: "Kama wewe ni mtoto mmoja wa watumwa aliyenunuliwa na kukombolewa..." Hapo akamweleza mababu na babu zao wa ukoo wa Umayya waliokombolewa na kuachiliwa huru na Mtume Muhammad wakati wa ushindi wa kutekwa Makka.Ama hotuba ya Zainab katika Kufa ilishitua na kuzindua watu wa Kufa hata Ibne Ziad akawa hawezi tena kuwazuilia, kwa hivyo aliamua kuwahamisha mara moja. Labda alisahau kwamba wanawake hawa si kitambo kirefu, (miaka ishirini tu) iliyopita walikuwa ni mabanati watakatifu katika utawala wa Kufa wakati wa ukhalifa wa Imam Ali aliyekuwa na jiji lake kuu hapa hapa. Wale watu wa nyumba ya Mtume, walipelekwa Sham (Damascus) pamoja na vichwa vilivyo anguliwa vya hao mashahidi kama alama ya kuonyesha ushindi wa Banu Umayya katika kasri kuu ya makao ya Yazid. Mateka hao waliwekwa kizuizini kwa muda wa mwaka mzima.


Katika tukio moja la baraza la Yazid, alimdhihiki Ali ibne Husayn, akimuuliza je, N'nani mshindi mkuu na shujaa aliyetambulika katika vita hivi? Ali ibne Husayn, Zainul-abedeen, alimjibu: "Ushindi mkubwa na ushujaa uko upande ule ule wenye lengo lililobakia la dini, madamu mwito wa Muhammad Rasulullah (Muhammad ni Mtume wa Allah) kutajwa baada ya Allahu Akbar (Allah ni mkubwa) kutaendelea kudumu, basi Husayn ni mshindi mkuu.


Yazid, alitumia njia zote za hila na udhalimu na unyama wake juu ya kuwatesa na kuwaadhibu watu wa nyumba ya Mtume wakiwa kizuizini katika gereza la Damascus mpaka siku moja Sakina binti Husayn alikufa akiwa kizuizini. Ama tukio la kifo cha mtoto huyu Sakina, lilishutua watu, walianza kukusanyikana na kuungana dhidi ya majeshi na kumkera Yazid wakitaka watu wa nyumba ya Mtume waachiliwe mara moja. Yazid alitambua sasa tisho lao juu ya utawala wake ambao wazee wake walipanga kwa hila na kumrithisha, alilazimika kukubali ombi lao na kuwaachilia watu wa nyumba ya Mtume katika mwaka wa 62 B.H. (862 A.D.) Hakuwaachilia na kuwapa heshima zao tu, bali aliwakubalia matakwa yao ya kuadhimisha siku za maombolezo wakiwa Sham (Damascus) kabla ya marejeo yao Madina.Ali ibne Husayn, aliwasili Madina na baada ya kupitia ziara ya babake aliyeshahidiwa pamoja na wenziwe wote katika Karbala, lakini alikuwa ni yeye mmoja tu, mwanamume kutoka jamii yake aliyerejea. Bashir ibne Jaslam ndie aliyeongoza msafara huu uliovunjikwa na moyo. Walipokurubia kuta za Madina, Binti mdogo wa Ali ibne Abi Talib aliangua kilio na kuomboleza, O jiji la babu yetu (Mtume mtukufu) usitukubalie sisi... kwa heshima tuliondoka hapa, tumeteseka na kutendewa kinyama, tumerejea pasi na mashujaa wetu na watoto wetu. Msafara ulisimama kando nje ya jiji la Madina, Bashir aliteremka na kuingia mjini akitongoa khabari zenye kuliza na kumiminikwa na machozi.Enyi watu wa Madina mjukuu wa Mtume alishahidiwa katika Karbala na jamaa zake wamerejea. Kwa kusikia tangazo hili lenye kushutua na kuhuzunisha mno, watu wote wa Madina walikusanyika katika msikiti mtukufu wa Mtume, ambapo kila mmoja mke kwa mume aliomboleza. Tahadhari na uepukane na Ushirika wa mtu dhalimu maana yeye hukuuza kwa kupata tonge moja (ya chakula) ama kiasi kidogo zaidi ya hicho.


Imam Ali ibne Husayn (a.s.)

BAYANA WAZI
Yazid baada ya yote hayo, alihisi na kujiona kashindwa, kwa hivyo alikusanya majeshi ya watu wapatao elfu kumi na kuwapeleka Madina ili kwenda kuharibu haribu na kuhasiri watu wa huko, katika mwaka wa 62 B.H. (681 A.D.) mara baada ya rejeo la Ali ibne Husayn. Majeshi hayo dhalimu hayakutosheka na kuhasiri watu wa Madina na kubomoa nyumba zao bali walihakikisha walimkosea adabu hata Mtume mtukufu kwa kuwafungia farasi zao na ngamia juu ya kaburi lake. Ziyada ya uharibifu na unyama wao, waliwashika na kuwanajisi wanawake wa kiislamu na kuwaulia waume zao. Hatimaye mwaka wa 63 B.H. (682 A.D.) Yazid alitoweka ghafla pasi kujulikana alikotokomea. Uhusiano wa ushirika na tangamano la jamii na watu watendao dhuluma na ukatili, husababisha lawama na kutoaminiwa.Imam Husayn ibne Ali (a.s.)
Mtoto wake Muawiya wa pili, alikamata ufalme na kutawala baada ya kutoweka Yazid. Mara tu Muawiya wa pili aliposhika ufalme aliwashambulia na kuwalaumu wazee wake wote waliotangulia kwa sababu ya kuifuja haki ya watu wa nyumba ya Mtume, na kuwaendea kinyume cha sharia. Naye hakuendelea kutawala mara alijiuzulu kutoka kiti cha ufalme. Utawala dhalimu wa Banu Umayya, haukuishilia hapo kwa sababu ya vikundi vyao vya njama walihakikisha kuendeleza utawala wao hadi mwishoni mwa mwaka wa 132 B.H. (749 A.D.) ndipo walipofikilia ukomo wao. Ali ibne Husayn, fakhari ya wenye kuabudu katika muda wa miaka arubaini (40) baada ya tukio la kuhuzunisha Karbala, aliendelea kuwafundisha na kuwaelimisha wanainchi juu ya dhuluma zilizo fanywa na Banu Umayya, naye mwishowe alitiliwa sumu na Hisham ibne Abdul Malik, akafa katika mwaka wa 98 B.H. (716 A.D.).Mwaka wa 102 B.H. (720 A.D.) kundi la ukoo wa Banu Abbasiya walianza kupigana na Banu Umayya ambao mwisho wao walishindwa na nguvu za Banu Abbasiya. Katika muda wote huu wa vita baina ya Banu Umayya na Banu Abbasiya, wakishughulika na kupigana, kung'ang'ania ufalme wa Hijaz, Muhammad ibne Ali (Al-Baqir) na Jaffer ibne Muhammad (As-sadiq) wote wakiwa ni dhuria wa Mtume mtukufu waliotokana na nasaba ya Husayn bin Ali walijitolea kueneza na kufunza watu mafunzo tofauti kwa umma.Mafunzo haya yalifikia kilele wakati wa Jaffer ibne Muhammad (As-sadiq) ambapo takribani wanafunzi wapatao elfu nne walielimishwa taaluma tofauti chini ya uangalizi wake. Wataalamu wakubwa kama Abu Hanifa na Avicenna (Ibne Sina) ambaye alikuwa mashuhuri katika mafunzo ya hesabu na elimu ya utambuzi ni katika baadhi ya wanafunzi waliosifika wa Jaffer ibne Muhammad (As-Sadiq). Ama tukidhukuru na kuichunguza hali ya historia na tukio lake, itaeleweka wazi kwamba mauwaji ya kikatili yaliyotokea Karbala katu hayakuwa ni ajali bali nitukio lililopangwa na hakikisho dhidi ya Mtume na watu wa nyumba yake kabla ya mauaji ya Ashura. Vilevile imedhihiri pasi na shaka yoyote kwamba ni mashambulizi dhidi ya islamu dini tukufu ya Mwenyezi Mungu na watu walioabudu masanamu, wasiokuwa waumini, waliojibandikiza majina ya kiislamu, lakini hawakupendezewa na dini tukufu ya Mwenyezi Mungu .Shukrani kuu, kwa jitihada ya mashujaa wa Karbala, waliojitolea na kukabiliana na mapambano na kushahidiwa katika njia za haki wakipigania uislamu. Leo jina la mtukufu Mtume Muhammad likifuatana na jina la Mwenyezi Mungu linasikilika mara tano kwa siku katika wito wake wa ibada kutoka kila pembe ya dunia. Mafunzo ya Mtume ya kuwa na tabia njema na mavazi rasmi ya sitaha kwa wanawake, (Hijab, mitandio na vitambaa vya kichwani) vinaendelea kutumiwa kote. Na uislamu ungali hai. kwa hivyo ushindi ni wa Husayn.


Imam Shafi amesema: "Sala zetu hazikamiliki iwapo hatuwasalii enyi watu wa nyumba ya Mtume." Watawala kama Banu Umayya na Banu Abbasiya walikuja na wakaondoka, nguvu za utawala walizipata na kuzipoteza walitenda ukatili wao na udikiteta wao na kuwasumbua watu wa nyumba ya Mtume na kuzidisha sheria zao za kutawala kinguvu lakini Husayn anatawala nyoyo za walimwengu hata leo.


Siku zimebadilika katika majuma, miezi na miaka hadi karne, katika vizazi na vizazi hakuna akumbukwae kwa usawa ela Husayn, roho huliliwa na kuomboleza juu ya kifo chake, wengine japo kwa masaa machache na wengine kwa miezi lakini wakati husahaulisha yaliyopita ila Husayn, jinsi alivyotendewa kinyama na kukutuliwa pamoja na wenziwe wote katika uwanja wa Karbala, hakutasahaulika na ni kama moto unao waka ndani ya nyoyo za waumini, ambapo kila mwaka mashiko yao hukazanishwa na kurejelea upya wake. Na musiwadhanie wale waliouliwa katika njia za Allah kuwa maiti la-Hasha, wao wangali hai na wanaruzukiwa na Mola wao. Holy Qur'an (3:169)


Msimamo wa Husayn ungali hai na mhanga aliyojitolea haupuuzwi, yeye ni mfalme mkuu katika mashahidi na daima yumo ndani ya nyoyo za mmoja na wote. Waumini kote ulimwenguni, siyo kumtambua na kumuheshimu tu, bali kila mwaka ifikapo siku kama hii (Ashura) kumbukumbu za tukio la kushahidiwa kwake huadhimishwa. Ana heshimiwa baada ya Mtume Muhammad, babake Ali ibne Abu Talibu, mamake Fatimah binti Muhammad na ndugu yake Hasan ibne Ali. Amani ya Mwenyezi Mungu na iwe juu yao pamoja na kizazi chao. Hapa tuna furaha kuwaletea utenzi huu tulioupokea kutoka kwa malenga mashu-huri Al-ustadh Bahri D.P. wa Mombasa.
MAUWA YA PEPONI
1. Mauwa matakatifu, Ya-bustani nadhifu
Yaliyopamba sharafu Ya jamii Hashimiya
2. Mauwa yalo abadi Yapembeo "Mashahidi"
Toka jadi na jududi Ya jamii Hashimiya.
3. Mauwa yaliyoshani, Yalotukuka peponi
Ni Hassani na Husseni, Ya jamii Hashimiya.
4. Mtume ndo shina lao, La jivuli na uzao
Na Ali pamwe nao, Ya jamii Hashimiya.
5. Fatima mlezi wao, Binti asifiweo,
Peponi yao makao, Ya jamii Hashimiya.
6. Ashura ili yaumu, Iloogesha kaumu
Kwa mito yao ya-damu, Ya jamii Hashimiya.
7. Twarikhi iloandikwa, Milele itakumbukwa,
Hadi sikuye kufikwa, Ya jamii Hashimiya.
8. Pamwe na wote ambao, Waliyotoka makwao,
Kuf'wata sabili yao, Ya jamii Hashimiya.
9. Watakumbukwa dahari, Kwa laili wa nahari,
Mashahidi, wafakhari, Ya jamii Hashimiya.
10. Ya rabbi uwaliwaze, Mahali pema walaze,
Mashahidi watulize, Ya jamii Hashimiya.
11. Ya rabbi Mola wa haki, Twakuomba tubariki
Tusikose itifaki, Ya jamii Hashimiya.
12. Tamma nasi waumini, Utuuongoze manani,
Tuipate afueni, Ya jamii Hashimiya.
Al-Ustadh Bahri D.P.
Mombasa
1-5-1997Katika Musnad Ahmed imeandikwa kwamba Zayd b. Thabit amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alisema: Mimi ninawaachia nyinyi makhalifa wawili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wa Nyumba yangu; na kwamba viwili hivyo havitafarikiana mpaka vinirudie kwenye hodhi vyote. Juzuu ya Tano, Uk. 189


سم الله الرّحمن الرّحيم الحمد لله رب العالمين والصلاة على النبى المرسل محمد المصطفى وعلى آله الطاهرين واصحابه النجباء نــــــــــــــوحـــــــــــة (للإمـام الشافعي رحمة الله عليه) مما نفى نومى وشيب لمّتي تاوب همى والفواد كئيب فزلزلت الدنيا لآل محمد فمن مبلغ عنى الحسين رسالة قتيل بلا جرم كان قميصه نصلى على المختار من آل هاشم لئن كان دنبي حب آل محمد هم شفعائي يوم حشرى وموقفى تصاريف ايام لهن خطوب وارق عينى والرقاد غريب وكادت لهم صم الجبال تذوب وان كرهتها انفس وقلوب صبيغ بماء لارجوان خضيب ونؤذى بنيه ان ذاك عجيب فذلك ذنب لست منه اتوب وبغـضهم للشافعى ذنــوب


DARAJA YA AHLUL BAYT KAMA ALIVYONUKULIWA IMAM SHAFII (R.A.)
1. Katika mambo yenye kunikesheza na kuzifanya nyeupe nyele zangu ni huzuni na misiba ya kilimwengu.
2. Huzuni yangu imenirudia na moyo wangu una huzuni. Jito langu halifumbi wala usingizi siujuwi.
3. Kwa sababu ya Ahlul-Bayt ya Mtume (s.a.w.w.), Ulimwengu mzima ulitetema na majabali na milima ilikaribia kuyayuka.
4. Ni nani atakaye mfikilizia Husayn ujumbe wangu na hata nyoyo zatukia?
5. Husayn! Aliuliwa shahidi pasi na makosa yoyote na kanzu yake ikapakazwa wekundu.
6. Twamuombea rehma Mtume katika ukoo wa Hashim na twawaudhi wanawe; hakika jambo hilo ni lenye kustaajabisha.
7. Ikiwa dhambi zangu ni kuwapenda watoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) basi ni dhambi ambazo sitotubiya.
8. Kuwa ni wao ndio watakao nishufaiya siku ya kufufuliwa na hisabu, na mwenye kuwabugudhi wao ni wenye dhambi kwa Shafii.MSAMIATI

Aali Jamaa
A.D. Auno Domini [Tangu kuzaliwa nabii Issa (a.s.)]
Akali Kiasi
Athiri tia doa, dosari
Ba'aya kiapo cha uaminifu.
B.H. Baada ya Hijra
Bugudhi sumbua, kera, udhi.
Dhidi pingana na, kinyume na.
Dhifa mwaliko / karamu
Kiwewe wasi wasi.
K.H. Kabla ya Hijra.
Kubeza kukejeli / kujivuna
Kumbukumbu ukumbusho.
Kutuliwa uawa kwa sababu ya Mwenyezi Mungu /dini
Madhila tabu, balaa.
Mbembefu mpenda anasa.
Mori hasira kubwa.
Nyanyasa hangaisha.
Nusuru okoa, ponesha.
Sairi bembeleza, rai.
Takwima kalenda.
Tangaa enea, sambaa.
Tarakanya vuruga, haribu.
Watesi maadui.
Warundifu wenye kuharibu, kuvunja.