ASHURA

 

ASHURA

Shahada ya Imam Husayn
Mtazamo wa Kihistoria


Kimetolewa na:
Bilal Muslim Mission of Kenya
P.O. Box 82508
Mombasa - Kenya
E.Mail: tableegh@kenbilal.org


YALIYOMO
Kisa cha siku ya Ashura... ii
Utangulizi... iii
Yazid ni nani?. 1
Roho ya Karbala 3
Utume wa Muhammad (s.a.w.w.) 5
Hijra na Ahlul Bayt.. 9
Khalifa wa Mtume. 14
Utiifu wake.... 16
Udhalili na ugandamizi. 19
Husayn kuhama kutoka Madina.. 23
Husayn kuwasili Karbala.. 27
Mauwaji ya kikatili ya watu wa nyumba ya Mtume 31
Mwisho wa watu wa nyumba... 35
Watu wa nyumba ya Mtume wakiwa kizuizini. 39
Bayana wazi 43
Utenzi:- Mauwa ya Peponi... 47
Daraja ya Ahlul Bayt (Kiarabu)Imam Shafi 49
Daraja ya Ahlul Bayt (Kiswahili)..Imam Shafi 50
Msamiati. 51


KISA CHA SIKU YA ASHURA NA KUULIWA KWA IMAM HUSAYN
Hii ni kumbukumbu ya kujitolea mhanga na kuuliwa kwa Imam Husayn na takriban jamii yote ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kuinusuru dini na kuitetea haki dhidi ya hao walowezi na wapinzani wa dini, na kuregesha mwito ule ule wa "hakuna Mungu apasae kuabudiwa ila Allah". Imam Husayn (a.s) ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliuwawa kwa ajili ya kuutetea Uislamu. Sababu kuu ya kuuwawa Imam Husayn ni kwamba yeye alikataa dhulma na uwongo. Alikataa kula kiapo cha utii (baiyat) kwa Yazid. Imam Husayn alitaka kuisimamisha haki na ukweli kama aliokuwanao babu yake Mtume Muhammad (s.a.w.w).


UTANGULIZI
Sifa njema zote ni zake Mwenyezi Mungu Bwana wa viumbe vyote aliyeniwezesha kufasiri mfululizo wa 'tukio la Siku ya Ashura na kuuwawa (Shahidi) kwa Imam Husayn' (a.s) kama ulivyochapishwa kwa lugha ya kiingereza katika gazeti la 'Daily Nation' tarehe 19th hadi 28th Mei 1996 kwa hisani ya 'Tawhid Distribution Service'. Inapata zaidi ya miaka 1360 tangu kuuwawa (shahidi) kwa Imam Husayn (a.s) na wafuasi wake katika uwanja wa karbala na majeshi katili ya Yazid ibne Muawiya ibne Abu Sufiyan. Tukio hili halikuwa la kawaida kwani alishalibashiri mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliposema:


''Kwa hakika kifo (shahada) cha (Imam) Husayn kitaamsha mori katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele' (mustadrak juz. II uk. 217). Hakuna shahidi aliyeheshimika na kukumbukwa kila mara, na kwa wakati mrefu zaidi kama Imam Husayn (a.s.) kujitoa kwake muhanga kupigania haki na kumuamini Mwenyezi Mungu hata katika majaribio mengi ni hakikisho wazi la ukweli wa Uislamu. Mfululizo huu una azma ya kutilia nguvu Aya inayosema:
. 3:169
''Usiwadhanie wamekufa wale waliokufa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bali wa hai na Mwenyezi Mungu anawaruzuku''. (Qur'an 3:169) nakukumbusha hekima na mafundisho ya Imam Husayn. Ni tumaini letu kwamba mawazo ya Imam Husayn yatakuwezesha kuwa na mtazamo usio wa anasa za dunia, bali wa kutafuta malengo makuu zaidi unaporudi kwa muumba wako.


Wasomaji wanaulizwa kutuandikia maoni yao na maswali kuhusu tukio hili au jambo lolote kuhusu Uislamu. Tunawatunukia kitabu hiki mashujaa shahidi wa Karbala akiwemo kiongozi thabiti Sayyidu Shuhada Aba Abdillah Husayn bin Ali bin Abi Talib na mashujaa wote waliojitolea mhanga kuitetea dini tukufu ya Uislamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu S.W.T. atukubalie juhudi zetu za kuchapisha kitabu hiki.
Bilal Muslim Mission of Kenya
P. O. Box 82508, Mombasa - Kenya.

Dhul Qa'ad 1421
February 2001YAZID NI NANI ?
"Sisi tuwatumwa wa Yazid na ni kwake yeye kutuweka huru au kutuuza kwenye soko." Watu wa Madina walilazimishwa kuyasema maneno haya kama ishara ya kumkubali Yazid bin Muawiya ambaye alitawala dola ya Kiislamu toka mwaka wa 680 mpaka 683 miladi. Fikra hii ya kuwatawala raia kama watumwa wa mtawala ilikuwa kinyume kabisa na mafundisho ya Kiislamu. Maneno tuliyoyataja hapo juu ambayo yalikuwa ni kiapo kilicholazimishwa watu wa Madina katika mwaka wa 683 ni thibitisho tosha la kuonyesha fikra za Yazid pamoja na viongozi wengine wa utawala wake.


Uislamu ulileta mizani ya kubainisha haki za mtawala na raia. Qur'an tukufu yaeleza haya: "Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrishieni kurudisha amana kwa mwenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu, hukumuni kwa uadilifu. (Qur'an 4:58) Ikiwa mtawala hatekelezi majukumu yake kama inavyotakikana (Utawala wa Uadilifu) basi hupoteza hadhi ya kuwa kiongozi. Imam Ali bin Abi Talib anasema: "Kwa kuniwekea majukumu yenu, Mungu ameifanya haki yangu kwenu nyinyi na vile vile nyinyi mnayo haki juu yangu". Kwa ufahamu huu, ni kitu cha kusikitisha kuona historia baada ya miaka 50 tu tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w.w), mtu kama Yazid bin Muawiya kuwa kiongozi wa Waislamu! Kwake Yazid, raia walikuwa ni kama vitu alivyo virithi kutoka kwa babake.


Kwa ujumla, karibu Waislamu wote wa wakati huo walikuwa wamelazimishwa aidha kwa vitisho au kwa kuhongwa, kumkubali Yazid kuwa mtawala baada ya Muawiya, babake. Mipango hii ilifanywa mwishoni mwa utawala wa babake. Wakati Yazid aliingia kwenye utawala, mtu wa pekee aliyekuwa na sifa na tabia nzuri na ambaye pia alikuwa tisho kwake ni Imam Husayn bin Ali, mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Husayn bin Ali ndiye tumaini la mwisho kwa Umma wa Kiislamu kupambana na Yazid. Na kweli Husayn hakuuvunja moyo Umma wa babu yake.


ROHO YA KARBALA MATENGENEZO YA UMMAH LEO
Ili tuweze kuielewa roho ya Karbala hatuna budi kuielewa Karbala yenyewe ni nini, na duri yake katika historia. Karbala ni jina la mahali katika Iraq. Mahali hapo palitokea mapambano makali sana baina ya makundi mawili ya Waislamu. Kundi moja liliongozwa na Husayn bin Alii, na la pili liliongozwa na wafuasi wa Yazid bin Muawiya. Katika mapambano hayo, wale wa jeshi la Husayn - waliopata watu 75 hivi, waume na wake - waliuwawa kikatili karibu wote, pamoja na Husayn "wao", isipokuwa wachache tu wakiwemo wanawake. Hivyo "ushindi" ukawa ni wa jeshi la Yazid lililokuwa na watu wasiopungua 6000.


Kisa na sababu ya vita hivyo ni nini? Alivyosema Husayn, ambaye ndiye aliyetoka kwenda kupigana, ni kwamba hakutoka kwa sababu yoyote nyengine isipokuwa ni kwa kutaka "kuutengeneza" umma wa Mtume Muhammad s.a.w.w., na "kutaka kuamrisha mema na kukataza maovu", na "kufuata sera" ya Mtume Muhammad s.a.w.w. Lakini ni nani Husayn, na ni nani Yazid? Husayn ni mtoto wa Alii bin Abii Twalib kuzaa na Mw. Fatima binti ya Mtume Muhammad s.a.w.w. Na Yazid ni mtoto wa Muawiya bin Abii Sufyan. Na kila mmoja katika hao ameelezwa kwa sifa zake katika vitabu vya Kiislamu vya historia.


Kukielewa vizuri chanzo cha vita hivyo, bila ya kwenda nyuma sana katika historia, ni sharti tuelewe khalfia ya mkataba uliofanywa baina ya Muawiya bin Abii Sufyan, babake Yazid, na Hasan bin Alii bin Abii Twalib, ndugu yake Husayn, na jinsi ulivyovunjwa. Pia ni muhimu kuelewa tabia na khulka za wahusika wawili hao: Yazid na Husayn, na jinsi jamii ya Kiislamu wakati huo ilivyokuwa imezorota katika nyanja mbali mbali za maisha yao. Katika hali kama hiyo, ile roho ya kiislamu ya kupambana na maovu ilipotea. Kitu kilikuwa na thamani zaidi kuliko utu! Dini haikuwa na uzito tena. Nyoyo zilijaa khofu; tamaa ikawa mbele. Waislamu waligawanyika kikabila na kitabaka. Rushwa ikawa ndiyo sera rasmi. Vitisho vikawa ni jambo la kawaida. Ukatili waliofanyiana Waislamu, wenyewe kwa wenyewe, hausemeki; na mengi mengineyo.


Ugonjwa ueneapo namna hiyo, na wale wa kuuganga wawapo hawana moyo wa kuuganga kwa khofu au ghafla zilizowashika, pafanyweje? Ni lazima papigwe mshindo mkubwa sana ili "waliokufa wafufuke." Na mshindo huo, zama hizo, ulikuwa ni shahada ya Imam Husayn a.s. huko Karbala. Asingejitolea yeye muhanga, na watu wake, Uislamu usingekuwako hadi hii leo. Hiyo ndiyo roho ya Karbala. Ilihitajika siku hizo. Inahitajika leo, na itaendelea kuhitajika popote penye dhulma. Kama isemwavyo: "Kila siku ni Ashura, na kila ardhi ni Karbala. Hiyo ni khotuba iliyotolewa na Sheikh Abdillahi Nassir kwenye semina ya Imam Husayn. (Tarehe 28/5/2000)


UTUME WA MUHAMMAD (S.A.W.W.)
Kama ilivyoahidiwa katika Torah, (Taurat) kitabu kitakatifu cha Musa na Injili (Biblia) ya Issa, Muhammad, muokozi wa Binaadamu, alizaliwa katika Al-Hijaz ambayo kwa sasa inajulikana kama Saudi Arabia miaka 53 kabla ya hijra (570 AD). Na kulingana na ahadi hii ya vitabu vya kale, Qur"an tukufu yasema:
. (61:6)
"Na (wakumbushe) aliposema (Nabii) Isa bin Mariam (kuwaambia Mayahudi): "Enyi wana wa Israil, mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kutoa habari njema ya Mtume atakayejia nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad. (Muhammad)." (Qur'ani 61:6)


Na kutokana na Abraham na mtoto wake Ismail, Muhammad pia hutajwa kama Ahmad. Mtume alizaliwa akiwa yatima, maana babake Abdullah ibne Abdulmuttalib, alifariki kabla ya Mtume kuzaliwa. Alilelewa na Babu yake Abdulmuttalib, hata alipofikisha umri wa miaka 6, mamake mzazi Amina binti Wahab, alifariki pia, vile vile baada ya kifo cha babu yake Abdulmutalib, alilelewa na Ammi yake Abu Talib, ambae alimtunza kwa mapenzi kama mzazi wake na juu ya hayo alijitolea kumridhisha na kumtekelezea kila alilohitaji.


Muhammad alitambuliwa kitambo kwa tabia zake njema, utukufu na uaminifu aliokuwa nao hata kabla ya kutangazwa kwake utume. Alidhihirika wazi kama huyo ndiye Mtume wa mwisho kama ilivyoteremshwa aya:
( . (33:40)
"Muhammad, si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali yeye ni Mtume wa Mungu na wa mwisho wa mitume na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu." 33:40)
Mjumbe wa mwisho wa Allah alizaliwa katika enzi ambapo wanawake hawakuwa wakinyanyaswa tu, bali wakidhulumiwa na kuchukiwa. Watoto wakike walizikwa wakiwa hai. Hii ilikuwa ni desturi ya watu hao katika enzi hiyo. Na kuipinga na kuiondosha desturi hii isiyokuwa ya haki katika jamii, kukawa ndio mwanzo wa jukumu la utukufu wa kazi yake.


Mnamo mwaka 23, K.H. (599 A.D.) alizaliwa mtoto aliyeitwa Ali kwa Abu talib, ndani ya Al-Ka'aba nyumba takatifu ya Allah katika mji wa Makkah. Ali alikusudiwa kuwa mtetezi imara, na mfuasi mtiifu wa Mtume Muhammad. Katika umri wa miaka 25, Mtume alimuoa mjane aliyeitwa Bibi Khadija ambae alikuwa mwanamke mfanyibiashara mashuhuri katika nyakati zake. Khadija alivutiwa na kupendezwa na tabia za utukufu wa adabu na uaminifu wa Mtume, hata akaamua kufunga nae ndoa ambayo Mtume hakuikataa. Alikubali ingawa bibi Khadija alimpita kwa umri wake.


Kutokana na ndoa hiyo, Mtume alijaliwa mtoto mmoja tu, wakike ambae ni Fatimah aliyezaliwa katika Makkah mwaka wa 6 K.H (616 A.D) nae hakuwa ni kipenzi cha moyo wake tu bali alitokea kuwa mfano mwema na wakuigizwa katika mwendo wa wanawake ndani ya Uislamu. Mtume aliwatowa watu Gizani na kuwafunza utu kamili, aliwafunza jinsi mwanamke na cheo chake ipasavyo, kama ilivyotakiwa na Mwenyezi Mungu.
(4:19)
"Enyi, Mulioamini! si halali kwenu kurithi wanawake kwa jeuri. Wala msiwazuie (kuolewa na waume wengine kwa kuwa hamuwataki wala hamtaki kuwaacha ila kwa pesa) ili mpate kuwanyang'anya baadhi ya vile mlivyowapa. (Hapana ruhusa haya) isipokuwa wawe wamefanya uovu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na kama mkiwachukia basi (msiwaache) kwani huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake." (Qur'ani 4:19)Mtume alimuheshimu mno binti yake kama itakiwavyo katika utukufu wa shariya na kadhalika alisema, Fatimah ni pande la nyama yangu na yeyote anaemfurahisha yeye, atanifurahisha mimi na yeyote yule anaembughudhi huwa amenibughudhi mimi, na anaenibughudhi mimi anambughudhi Mwenyezi Mungu . Mtume alipofikisha umri wa miaka 40 mwaka 13, K.H. (610 AD) malaika mtakatifu Jibril alimwasilishia ujumbe wa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kuutangaza utume wake ambapo Muhammad aliwaita watu wote wa jamii katika dhifa na kutaka maoni na rai zao kuhusu ukweli na uaminifu wake nao walikubali kwa kauli moja.Ndipo alipowatangazia ujumbe wake: "Semeni hakuna mungu apasaye kuabudiwa ila Allah, nanyi mtapata kufanikiwa, kisha aliwajulisha habari za utume wake, ambapo baadhi ya jamaa zake waliokuwepo ma-ami zake na wengineo isipokuwa Sayyidna Ali walimpuuza na kumfanyia stizahi kwa kutoamini ndipo Mtume alipomtangaza hadharani Sayyidna Ali aliyekuwa na umuri wa miaka 11 kama msaidizi na khalifa wake pasikuwajali waliokuwepo."