FADHILA ZA SAYYIDNA ALI (A.S)

 

HADITHI YA ISHIRINI NA NNE
"Hadithi ya Ghadeer-El-khum"
Katika Riyaadhan-Nazarah Juzu 2, uk. 244, imeelezwa hivi: Omar alimwambia Ali (a.s.) "As-Bahtal-Maw-Laa Kul-li Muminin wa Muminah" (Umekuwa bwana-mwenye mamlaka wa kila mwenye kuamini mwanamume na mwanamke). Maelezo kamili ya usemi wa Omar (r.a.) aliyomwambia Ali (a.s.) utapata kujua ukitazama katika vitabu walivyovitunga wanavyuoni wa Kisunni na wengineo juu ya kisa cha Ghadir. Na hapa tunataja alivyoandika Ibnu Kathir Al-Hanbaly katika kitabu chake Al-Bidaya Wan-Nihaya, Juzu 8, uk. 349. Anataja majina ya kikundi cha Masahaba kilichopokea hadithi ya Ghadir, na akasema kuwa: Omar Ibnu Khattab ni mmojawapo kati yao.


Hadithi yenyewe iliyotokana na El-Baraau imesema hivi: Tulitoka pamoja na Mtume (S.A.W.W.) mpaka tulipoteremka (mahali paitwapo) Ghadir Khum; akamtuma mpiga mbiu (mtangazaji) kuita watu, basi tulipokusanyika alisema Mtume (S.A.W.W.), "Je, mimi si bora zaidi na mwenye amri juu ya nafsi zenu?" Tukasema, "Ndiyo, vivyo hivyo unao mamlaka juu yetu." Mtume (S.A.W.W.) akasema (tena), Je, mimi si bora zaidi kuliko mama zenu? Tukasema, "Ndio bila shaka wewe ni broa zaidi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume akasema, "Je, mimi si bora mno kuliko baba zenu?" Tukasema, "Ndio bila shaka wewe ni bora zaidi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume (S.A.W.W.) akasisitiza kusema kuwa, "Je sikuwa mimi bora mno kwa jambo lolote kwenu?" Tukasema, "Ndiyo hivyo hivyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume (S.A.W.W.) ndipo aliposema, "Mtu yeyote ambaye mimi ni bora mno kwake, basi na Ali Bin Abi Talib ni bora mno kwake katika kila jambo; Ewe Mola wangu mpende ampendaye Ali na mfanye adui amfanyiaye Ali uadui."


Basi Omar (r.a.) alisema, "Nakupongeza na kukupa mkono wa furaha ewe mtoto wa Abi Talib, leo umekuwa ndiyo bora mno wa kila mwenye kuamini." Na vile vile amepokea hadithi hii Ibnu Majah El-Qazwini katika 'Sunan' yake, kutokana na hadithi ya Hammadi bin Salma aliyoipokea kwa Ali bin Zaydi na Aba Haroon El-Abdi kutoka kwa Adi bin Thabit, naye amepokea kwa El-Barau na yeye ameipokea hadithi hii kwa Sa'ad El-Waq'qaas, na Talha bin Ubaydullah na Jabir bin Abdil-Laahi na kwa Abi Saeed El-Khudriyu na Habashi bin Junaadah na Jareer bin Abdil-Laah na vile vile Omar Bin Khattab na Abi Huray-rah.


Wapokeaji wa hadithi ya El-Ghadiir ni wengi sana, wala haiwezekani kuwaorodhesha wote katika kitabu kidogo kama hiki. Mtungaji mmoja maalum aliandika kitabu kuhusu wapokeaji wa hadithi ya El-Ghadiir; na mtungaji mwingine maalum aliadika kitabu kuhusu maelezo ya matamshi na maneno ya hadithi ya El-Ghadiir.

Na vitabu hivyo vimepigwa chapa India (bara hindi) na Iran (Uajemi). Na Ibnu Sabbaghu El-Maliki ameeleza katika kitabu chake 'Al-Fusuulul Muhimma' kauli ya Omar bin Khattab aliyemwambia Ali (a.s.) siku ya El-Ghadiir. Baada ya kumaliza Mtume (S.A.W.W.) hotuba yake, Omar bin El-Khattab alikutana na Ali Bin Abi Talib na akamwambia hivi: "Nakupa pongezi na mkono wa furaha ewe mtoto wa Abi Talib, wewe umekuwa ndiye bwana wa kila mwenye kuamini mwanamume na mwanamke." Na yeyote atakaye anaweza kuyapata na kuona yote hayo katika kitabu cha El-Ghadiir cha mwanachuoni mkubwa Al-Allama Sheikh Abdulhusein El-Aminii Mwenyezi Mungu amrehemu na kumridhia (Amin). Bila shaka atajua mambo ambayo yaliyopokewa katika hadithi ya El-Ghadiir kwa njia zote walizopokea.


HADITHI YA ISHIRINI NA TANO
"Haki iko na Ali na Ali yuko na haki"
Katika kitabu cha 'Riyaadhun Nadhra', Juzu 2, uk. 244 imesemwa kuwa katika jumla ya hadithi alizozipokea Omar (r.a.) kuhusu habari ya Ali (a.s.) ni ile hadithi aliyoisema Mtume (S.A.W.W.) kumwambia Ali: "Wewe kwangu ni katika daraja ya Harun kwa Mtume Musa."

Muhib-bud-Dini Tabary ameashiria katika maneno yake kuhusu hadithi ya Man-zilah: Hii ni hadithi maarufu sana na imepokelewa na kundi kubwa sana la Masahaba watukufu kutoka kwa Mtume (S.A.W.W.) kuhusu Ameerul Mumeneen Ali Bin Abi Talib (a.s.); na Omar Bin Al-Khattab ni miongoni mwao na ametiwa katika wapokeaji hadithi hii na kama inavyoonekana wazi wazi katika maneno ya Ibnu Kathiri katika kitabu chake Al-Bidaaya Wannihaya, Juzu 7, uk. 310 ambamo amesema: Katika Musnad ya Ibnu Hanbal imeelezwa hadithi iliyopokelewa na Aisha binti Saad kwa baba yake ni kuwa hakika Ali alitoka pamoja na Mtume (S.A.W.W.) hata walipofika mahali pa kuagana, Ali akawa analia huku akisema: Unanifanya kuwa ni Khalifa wako juu ya wanawake, watoto na wasioweza kwenda ….. Mtume (S.A.W.W.) akasema: "Je, huridhii kuwa wewe kwangu ni katika daraja ya Harun kwa Musa ila tu utume unaishia kwangu?"


(Yaani, katika maneno ya hadithi hii ifahamike wazi wazi kuwa Ali (a.s.) hakupata utume isipokuwa yeye alipata daraja ya ukhalifa alioachiwa na Mtume (S.A.W.W.) hapo Madina wakati ambapo Mtume (S.A.W.W.) alipokuwa anakwenda katika vita vya Tabuuk, na daraja hii aliyopata Ali (a.s.) ya ukhalifa ni sawa na ile daraja aliyopata Nabii Harun (a.s.) kwa Nabii Musa (a.s.) isipokuwa Harun alikuwa Mtume ambapo Ali (a.s.) hakuwa Mtume kwani hapana tena utume baada ya Mtume Muhammad (S.A.W.W.) ambaye ni Mtume wa mwisho.


Na Ibnu Kathiri ameendelea kusema kuwa uhusiano wa Hadithi hii ni wa hakika na thabiti sana, na watu wengi walioipokea hadithi hii kwa Aisha binti Saad kutokana na baba yake. Na El-Hafidh bin Asaakar amesema: "Hadithi hii imepokelewa kutoka kwa Mtume (S.A.W.W.) na kundi kubwa la Masahaba na miongoni mwao akiwamo Omar bin Khattab, Ali, Ibnu Abbasi, Abdullah bin Jaffer, Muawiyah, Jaabir bin Sumra, Abu Said, El-Barau bin Aazib, Zayd bin Arqam, Zayd bin Abi Awfi, Thubayt bin Shareet, Habash bin Junaadah, Maalik bin El-Huwyrith, Anas bin Maalik, Abdul-Fadhl, Ummu Salmah, Asmaa binti Umaysi na Faatimah binti Hamza. (Na Ibn Kathir) amesema kuwa Al-Haafidh bin Asaakir amezipekua sana hadithi hizi kuhusu Ali (a.s.) katika kitabu chake cha Tarekh na hakika amefanya kazi nzuri na ya faida na amejitokeza na kujulikana kwa wenye kutazama na wenye shaka na kwa wapinzani.


Ibnu Kathiri ameinakili hadithi hii ya 'Manzilah' katika kitabu chake 'Al-Bidaaya Wannihaya' kutokana na Saad bin Abi Waq-qaas na amesema kuwa uhusiano na maelezo ya hadithi hii yote ni ya hakika na thabiti.

Idadi ya wale walioipokea hadithi hii ya 'Manzilah' inafikia (watu) ishirini, na mwanzo wao ni Omar bin Khattab (r.a.) na mwisho wao ni Saad bin Abi Waq-qaas, yaani ndiye baba wa yule Omar bin Saad ambaye aliyemwua Al-Imam Husein (a.s.) (mjukuu wa Mtume (S.A.W.W.)) El-Kunji Ash-Shafiy amesema katika kitabu chake Kifaa-yatu-taalib, uk. 151, kuwa wapokeaji wa hadithi ya 'Manzilah' ni kundi kubwa la Masahaba na miongoni mwao akiwemo Omar bin Khattab, Saad, Abu-Huray-rah, pamoja na kundi lile jingine ambalo lililokwishatajwa majina yao hapo mwanzo. Na wala haifichikani kabisa kwa yule mwenye kujua au kupekuwa kwa kutafuta hakika ya hadithi hii ya 'Manzilah' kuwa ni katika hadithi zilizo sahihi kwa wanavyuoni wa Kisunni na wa Kishi (Mwenyezi Mungu awarehemu).


Na Bukhari ameinakili hadithi hii ya 'Mazilah' katika kitabu chake Saheeh Bukhari, Juzu 14, uk. 385 kilichopigwa chapa India mwaka 1272 A.H. Juzu 17, uk. 475, na Muslim katika Saheeh Muslim J. 2, uk. 323 kilichopigwa chapa Misri mwaka 1322, na El-Haakim An-Nisaapuri Ash-Shafii katika Mustadrak, J. 3 Uk. 109 na 132, vile vile, Tirmidhiy katika kitabu chake Jami Tirmizee, Juzu 2, uk. 460, kilichopigwa chapa 1310 A.H., amepokea kwa njia nyingi hadithi hii. Na Ibnu Maajah El-Qazwini katika Sunani yake Juzu 1, uk. 28 kilichopigwa chapa mwaka 1313 A.H. ametaja hadithi hii ya 'Manzilah', Nasaaee katika kitabu chake El-Khasaais, uk. 7, uk. 8, uk. 23 na uk. 32, Adh-Dhahabi katika Tal-Khees Mustadrak As-Sahee-hain, Juzu 3, uk. 134, kilichopigwa chapa Haydarabad mwaka 1341 A.H., na El-Baghawi katika Masaa-Beeh As-Sunna, Juzu 2, uk. 201, chapa ya Misri 1318 A.H., na Abu Daudi Tayaalasi katika Musnad yake Juzu 1, uk. 29, kilichopigwa chapa Hydrabad, hadithi ya 209. Kadhalika, Ahmad bin Hambal ameitaja hadithi hii katika 'Musnad' yake kilichopigwa chapa Misri 1313 A.H., Juzu 1, uk. 170 na 173 na 175 na 177 na 182 na 184 na 331; na katika Juzu 3, uk. 32, na 338 na 369 na mahali mwingine zaidi katika hiyo hiyo Musnada.


Ibnu-Atheer El-Juzary Ash-Shafii ambaye alikufa mwaka 630 A.H. ameinakilia hadithi hii katika kitabu chake kiitwacho Taaree-khul-kaamil, Juzu 2, uk. 106 chapa ya Misri 1303 A.H., Ibu Asakir katika kitabu chake Mukhatasar Tareeh, Juzu 4, uk. 196, chapa ya Misri 1333 A.H., Ali El-Muttaqi Hanafii katika Kanzul-Ummal, J. 6, uk. 153 na mahali pengine, na Muhibbud-Deen Tabary katika kitabu chake Dhakhaa-Irul-Uqba, uk. 58 na 63, na katika kitabu chake kingine Riyaadhun-Nadhra J. 2, uk. 157, na Muwaffaq Bin Ahmad El-Khwarazmi Hanafi katika Munaaqib, uk. 32. Na Ibnu Hajar El-Haytami katika kitabu chake: As-Sawaa-iqul-Muhriqa, uk. 30 na 74. Aidha, Ibnu Khillikaan ameinakili katika kitabu chake Wafayaatul Aayaan J. 2, uk. 104, na Ibnu Hajar El-Asqalaani katika kitabu chake Al-Isabah, J.2, uk. 507. Shab-lanji Shafii katika Noorul-Ab-saar, uk. 68, Jalaalud-Deen Suyutee ameitoa hadithi hii ya Mazilah katika Taareekhul-Khulfaa, J. 1, uk. 65, Ibnu Abdi Rabbih katika Taareekhul-Khulafaa, J. 1 uk. 65, Ibnu Abdi Rabbih katika kitabu chake Al-Iqdul Fareed Juzu 2, uk. 194, kilichochapwa Boolaaq mwaka 1302 A.H. Abdul-Bir El-Qartaby katika kitabu chake 'Al-Isti-Aab' kilichopigwa chapa Haydarabad mwaka 1318 A.H. Al-Kanji Ash-Shafii ameeleza katika kitabu chake Kifaa-yatu-Taalib katika hadithi ndefu. Hapa tunaitaja kwa ufupi bila ya kuwataja wapokeaji wa hadithi hii; nayo ni kama hivi: Amehadithia Al-Harith bin Malika kwamba, "Nilikwenda Makka basi nikakutana na Saad bin Waqqaas, na nikamwambia, Je umepata kusikia daraja (sifa) ya Ali? (Saad bin Abii Waqqas) akasema: Bila shaka nimemshuhudia yeye (kuwa) anazo daraja nne! Na bila shaka ninapendelea sana kuwa na walau daraja mojawapo katika hizo nne na kwangu daraja hiyo ni bora mno kuliko ulimwengu na kuishi ndani yake… wa umri wa Nuhu (A.S.).


"Hakika Mtume (S.A.W.W.) alimpendelea Abubakar kwenda Makka kuwasomea washirikina wa Kikureshi baadhi ya aya za mwanzo wa sura ya Baraa'a. Basi Abubakar akaenda nazo kwa muda wa mchana na usiku tu (siku moja). Baadaye Mtume (S.A.W.W.) akamwambia Ali: "Mfuate Abu-Bakar na uichukue hiyo Sura ya Baraa'a na uifikishe (wewe)," Basi Ali (A.S.) akamrudisha Abbakar (R.A.) na alirejea (Abu-Bakar) huku akilia na akasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, limeteremka juu yangu jambo lolote?" Mtume (S.A.W.W.) akasema: La, hakuna ila heri tu, bali kwa hakika hawezi kufikisha ujumbe wangu isipokuwa mimi mwenyewe au mwanaume aliye katika mimi; (au hapa badala ya kusema: mwanamume aliye katika mimi, Mtume (S.A.W.W.) alisema: Ahali Baytii).


Na Saad bin Abi Waq-qaasi ameendelea kusoma kuwa: "Tulikuwa msikitini siku moja pamoja na Mtume (S.A.W.W.) wakati alipotangaza wakati wa usiku kuwa watoke nje wote humo msikitini isipokuwa dhuria ya Mtume (S.A.W.W.) na dhuria ya Ali (A.S.). Basi tukatoka huku tukivivuta viatu vyetu. Ilipofika asubuhi, Abbas Ammi yake akamjia Mtume (S.A.W.W.) na akasema; Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ammi zako na Masahaba wako umewatoa, na ukamweka mtoto huyu (Ali Bin Abi Talib), Mtume (S.A.W.W.) akasema: Mimi siye niliyeamrisha kuwatoeni wala kumweka mtoto huyu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ndiye aliyeamrisha hayo. (Na daraja ya tatu), Saad amesema: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.W.) alimpeleka Omar (R.A.) pamoja na Saad kwenda kuiteka "Khaybar". Saad akajeruhiwa, na Omar (R.A.) akarejea bila ya kushinda. Hapo Mtume (S.A.W.W.) akasema "Nitampa kesho bendera mwanaume yule ambaye anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, yeye anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na akataja sifa zake nyingi zingine. Kisha akamwita Ali (A.S.). Masahaba wakasema: "Yeye ni mgonjwa wa macho. Ali akaletwa huku akishikwa mkono na Mtume (S.A.W.W.) akamwambia, "Yafungue macho yako." Ali akajibu "Siwezi." (Saad) amesema: Mtume akamtia mate machoni mwake na akayasugua kwa kidole chake cha gumba na akampa bendera.


Saad bin Abi Waqqaas anaendelea kunena: "Daraja ya nne ni: Siku ya Ghadiri Khum, Mtume (S.A.W.W.) alisema: Enyi watu! Je, sikuwa mimi ndiye bora mno kwa wenye kuamini kuliko nafsi zao? Wakasema: hapana shaka wewe ni bora mno kwetu; na Mtume (S.A.W.W.) alisema hivyo mara tatu na wao wakaitika vivyo hivyo mara hizo pia; kasha akamwambia Ali "Nisogelee". Hapo basi Mtume (S.A.W.W.) akaunyanyua mkono wa Ali (A.S.) kwa mkono wake juu hadi kwapa lake nikaliona na Mtume (S.A.W.W.) akasema: Mtu yeyote ambaye mimi nimekuwa bora kwake na mwenye mamlaka juu yake, basi na Ali ni bora kwake na mwenye mamlaka juu yake. Na alisema mara tatu. Saad bin Abi Waqqaas amesema: (Daraja la tano) ni kuwa Mtume (S.A.W.W.) alikwishapanda ngamia wake mwekundu (kwenda katika vita ya Tabuuk) na alimwacha Ali kuwa ni Khalifa wake (hapo Madina).


Basi Makurayshi wakamwonea husuda na wakawa wanasema: Mtume amemwachia Ali kwa vile amemchukia (ndipo hakumchukua pamoja). Ali yakamfikia maneno hayo na hapohapo akamwendea Mtume (S.A.W.W.) akikamata kikuku cha kupandia ngamia wa Mtume huku akilia na kusema "Makurayishi wamedai kusema kwamba: umeniacha hapa kwa sababu umechukia kuwa pamoja na mimi. (Saad amesema). Hapo Mtume (S.A.W.W.) akawaita watu wote na walipokusanyika akasema, "Enyi watu, je miongoni mwenu yeyote (yule) huwa hakosi kuwa na husuda? Je, Huridhiki ewe mtoto wa Abi Talib kuwa kwangu miye wewe ni katika daraja ya Haruna kwa Musa, isipokuwa hapana Mtume yeyote baada yangu? Basi, Ali akasema: "Nimeridhika kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Kisha El-Ganji amesema, "Hadithi hii kweli na pande zake zote ndio sahihi na upande wake wa kwanza, ni ule aliopokea Imam wa watu wa hadithi - Ahmad Bin Hambali nao ni kule kupelekwa Abu Bakar na Sura ya Bara'-ah. Tabraani pia kuandika hayo.


Hadithi ya kuzuiliwa Abu Bakar katika kufikisha aya za Surat Bara'ah ni hadithi mashuhuri ambayo imepokelewa na wanazuoni wa Kisunni, Shafii na Hanafi, na mengineo katika vitabu vyao vinavyozingatiwa sana vya Tafsir na Tarekh. Na miongoni mwao ni Abul Fida Ismail bin Omar Ad-Dimishki aliyekufa mwaka 774 A.H. katika kitabu chake Al-Bidaaya Wan-Nihaya. Ibn Hajar El-Haytami Ash-Shafii katika kitabu chake "As-Swaaiqul", "Muhriqah", na Ibun Hajar Al-Asqlaani Ash-Shafii katika kitabu chake "Al-Isaaba." Vilevile imehadithiwa na El-Haakim An-Nisapuri Ash-Shafii katika kitabu chake Al-Mustadrak (ya) Saheehein, Tirmidhy Abu Isa Muhammad bin Isa katika Saheeh yake, Al-Mutaqy Hanafi katika Kanzul-Ummal. Imam Ahmad bin Hambal katika Musnad, Muhib-bud-Deen Tabary Ash-Shafii katika Saheehein yake, Al-Mutaqy Hanafi katika Kanzul-Ummal, Imam Ahmad bin Hambal katika Dhakhairul Uqba. Na wanazuoni wengi wengine wa Kishafii na Hanafii na wengineo ambao wameitaja na kueleza hadithi hii.


Na hadithi ya kufungwa milango aliyokuwa ikipitiwa kwenda katika Masjidin Nabawi (Msikiti wa Mtume) nayo ni milango ya vyumba walimokuwa wakiishi Muhaajirin (R.A.) wameipokea wanazuoni wa Kisunni, Shafii, na wegineo. Miongoni mwao ni Tirmidhi katika Saheeh yake, Ahmad bin Hambal katika Musnad yake, Al-Muhibbud-Deen Tabary katika Dhakhairul Uqba, Al-Mawaffaq bin Ahmad El-Khwarazmi katika Al-Manaaqib, El-Maghaaziliy Shafii katika kitabu chake kiitwacho El-Manaaqib, Sheikh Sulayman El-Kauduzi Hanafi katika kitabu chake Yanabii-ul-Mawaddah, Jalaaud-Deen Suyuti Shafii katika kitabu cha Adarurrul-Manthur kilichopigwa chapa Misri mwaka 1314 A.H. Al-Ganji Shafii amesema: "Ama ule upande wa tatu wa hadithi ya kutekwa kwa 'Khaybar' umeelezwa na Muslim katika saheeh yake."


Kwa hakika hadithi ya kutekwa kwa Khaybar kwa mikono ya Ameerul-Mumineen Ali (A.S.) imehadithiwa na kundi kubwa la wanazuoni wa Kisunni na Shia (Al-Imaaniyah). Mwenyezi Mungu awarehemu. Na miongoni mwao ni El-Haakim An-Nissapuri Ash-Shafiy katika 'Mustaadrak (ya) Saheehein. Al-Bukhaari katika Saheeh yake, Juzu 12, Juzu 14 na Juzu 15, Abul-Fida katika Al-Bidaaya Wan-Nihaya, Abu-Neem El-Isfahani katika Hilyatul Awliyaa, El-Baghawiy katika kitabu chake Massabeehus-Sunna Juzu 2, Tirmidhiy katika Saheeh yake, Juzu 2, Ibnu Maajah El-Qazwini katika Sunan yake ambacho ni kimojawapo katika Saheeh Sittah Ibnul Atheer Al-Jazari katika kitabu Usdul-Ghaba Juzu 4, katika maelezo ya maisha ya Ameerul Mumeneen Ali (A.S.)

Na upande wake wa nne umepokelewa na Ibnu Maajah na Tirmidhiy kutoka kwa Muhammad bin Bishaar, kutoka kwa Muhammad bin Jaffar. El-Ganji amesema:- Daraja na sifa ya tano ya Ali (A.S.) ni hadithi ya 'Manzilah! Hadithi hiyo imepokewa na kundi kubwa la wanazuoni wa Kisunni na wa Kishia (R.A.) na hadithi ya 'Manzilah' ni hadithi mashuhuri sana. Katika vitabu mahususi vya Kisunni na Shia na katika jumla ya vitabu hivyo ni Abakaatul An-Waari ndani ya Juzuu ambayo imehusika na habari za hadithi ya 'Manzilah' tu, nacho ni kitabu kikubwa sana kimepigwa chapa India. Basi katika kitabu kikubwa hicho mna uthibitisho wa kutosha kwa mwenye kutaka kujua ukweli na kumjua mwenye haki na kujua haki iko naye na yeye yu pamoja na haki.


HADITHI YA ISHIRINI NA SITA
"Laiti kama watu wote wangempenda Ali (A.S.) Mungu asingeumba Jahannamu.
Katika Yanaabee-ul-Mawaddah imeelezwa hadithi iliyopokewa na Sayyid Ali El-Hamdani kutoka kwa Omar Bin Khattaab kuwa amesema Mtume (S.A.W.W.) kwamba laiti kama watu wote wangekuwa wanampenda Ali, Mwenyezi Mungu asingeumba Moto." Wanazuoni wengi wa Kisunni, Shafii na Hanafy wamenakili hadithi hii kutoka kwa Omar Bin Khataab na kwa masahaba wengine watukufu. Na miongoni mwa (wanazuoni) hao ni Al-Muwaffaq Bin Ahmad El-Khwarazmi Hanafi katika Kitabu chake Taarekh Maqtalil Husein (A.S.) Juzu 1: ambaye ameinakili hadithi hii kutokana na Ibnu Abbas kuwa amesema kwamba Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Laiti kama watu wote wangekuwa wanampenda Ali Bin Abi Talib Mungu asingeumba Moto".

Na miongoni mwa walioeleza hadithi hii ni: Allamah Sayyid Muhammad Saleh El-Hanafii, ambaye ameieleza hadithi hii katika kitabu chake Al-Kaw Kabud-Durry uk. 122, kilichopigwa chapa Pakistan, ikitokana na Omar Bin Khattab kuwa amesema kuwa Mtume (S.A.W.W.) amesema "Laiti kama watu wangekuwa wanampenda Ali Bin Abi Talib (A.S.) Mwenyezi Mungu asingeumba Moto."

HADITHI YA ISHIRINI NA SABA
"Kumpenda Ali ni kumpenda Mtume (S.A.W.W) na Mwenyezi Mungu (S.W.T.).
Katika "El-Kaw Kabud-Durri" kilichopigwa chapa Pakistan, na kilichotungwa na Sayyide Muhammad Salehe Al-Hanafi imesema kuwa Omar Bin Khattab amesema kwamba "Mtume (S.A.W.W) amesema, "Yeyote atakayekupenda ewe Ali, atakuwa pamoja na Mitume katika madaraka yao siku ya Kiyama; na yeyote atakayekufa hali anakuchukia basi hatajali (angalia) hali amekufa Myahudi au Mkristo."


Zimepokewa kutoka kwa Mtume (S.A.W.W) hadithi nyingi sana ambazo zaonesha faida za kumpenda Al-Imam Ali Bin Abi Talib (A.S.), na madhara ya kumchukia. Katika kitabu Arjahul-Mataalib uk. 319, kilichotungwa na Ubaydullah Al-Hanafy, imesemwa kuwa Ibnu Mas'ud amepokea hadithi kutoka kwa Mtume (S.A.W.W) akisema, "Kuwapenda dhuria ya Muhammad (yaani Mtume wetu (S.A.W.W) siku moja tu, ni bora kuliko ibada ya mwaka, na yeyote atakayekufa katika hali hiyo ataingia Peponi."

Katika Kanzul-Umaal, Juzuu ya 6, Al-Muttaqi Hanafi amedondoa hadithi kutoka Al-Muujamil Kabiir ya Tabaraani na katika Taareekh-ul-Kabiir ya Ibnu Asaaki ikitokana na Abi Ubaydah Bin Ammar bin Yaasir, ambaye ameipokea kutoka kwa baba yake na babu yake kuwa Mtume (S.A.W.W) amesema, "Ninamwusia kila aliyeamini kukubali kuwa Ali bin Abi Talib anayo mamlaka na amri juu yake; na yeyote anayekubali hayo kuhusiana na Ali (A.S.) basi amenikubali mimi, pia na mwenye kunikubali mimi amemkubali Mwenyezi Mungu kuwa anayo mamlaka na amri juu yake; na yeyote atakayempenda Ali (A.S.) ndiye mwenye kunipenda mimi; na yeyote mwenye kunipenda mimi basi hakika ndiye mwenye kumpenda Mwenyezi Mungu; na yeyote atakayemchukia Ali (A.S.) basi hakika ndiye mwenye kunichukia mimi; na yeyote atakayenichukia mimi, ndiye mwenye kumchukia Mwenyezi Mungu (Azza Wajallah).


HADITHI YA ISHIRINI NA NANE
"Ampendaye Ali (a.s.) anampenda Mungu na Mtume wake" Katika Taareekh ya Ibnu Asaakir imenakiliwa hadithi iliyotokana na Ibnu Abbas ambayo inasema, "Mimi nilikuwa pamoja na Omar bin Khattab katika baadhi ya njia za Madina huku tumeshikana mikono, mara Omar akasema: "Ewe Ibnu Abbas mimi sina shaka sahibu yako (yaani binamu yako Ameerul-Muuminiin Ali (a.s.) amedhulumiwa." Nikasema: Basi mrudishie (haki) yake aliyedhulumiwa, ewe Amiirul-Muuminiin! Akauvuta mkono wake na kuondoka kwa hasira. Kisha akasimama na kusema; Ewe Ibnu Abbas, watu hao walitaka kumdharau tu sahibu yako."


Nikasema, "Wallahi Mtume (S.A.W.W) hakumdharau wakati alipomtuma na kumwamrisha aichukue Suurat Baraa-ah kwa Abu Bakar na awasomee watu." Hakika tukio hili limeelezwa na kundi kubwa la wanazuoni wa Kisunni kwa maneno tofauti au kuongezwa maneno, na katika jumla ya wanazuoni walioieleza hadithi hii ni: Ali Al-Muttaqi katika 'Kanzul-Ummal', Juzu 6, kutoka kwa Ibnu Abbas ambaye amesema, "Nilikwenda na Omar bin Khattab katika vichochoro vya mji wa Madina. Omar bin Khattab akasema, "Ewe Ibnu Abbas (watu) wamemdharau rafiki yenu (Ali bin Abi Talib a.s.) kwa vile hawakumtawalisha katika mambo yenu. Nikasema "Wallahi hakika Mtume (S.A.W.W) hakumdharau wakati alipomchagua kuwasomea Surat Baraa-ah watu wa Makka." Omar akaniambia: "Unasema kweli, naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa bila shaka nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwambia Ali Bin Abi Talib, 'Yeyote atakayekupenda wewe ndiye amenipenda mimi; na yeyote atakayenipenda mimi amempenda Mwenyezi Mungu, na yeyote atakayempenda Mwenyezi Mungu ataingia Peponi."

Maudhui ya hadithi ya Omar (r.a.) inatoka kwa Mtume (S.A.W.W) na kundi la Masahaba walieleza kwa matamko mbali mbali. Katika Kanzul Ummal (juzu 6, 391) kutoka kwa Ibnu Abbas imeelezwa kuwa siku moja Mtume (S.A.W.W) alitoka hali ameukamata mkono wa Ali, na kusema, "Fahamuni! Yeyote atakayemchukia huyu (Ali), basi hakika amemchukia Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na yeyote atakayempenda huyu, basi hakika amempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Na katika Kanzul Ummal. Vile vile Juzu ya 6, yamenakiliwa maneno haya kutoka Mustadrak Sahiihain ya Hakim ambayo, kwa hakika ni hadithi kutoka kwa Salman ambaye amesema kuwa: Mtume (S.A.W.W) amesema "Yeyote ataayempenda Ali, basi hakika ndiyo amenipenda mimi, na yeyote atakayemchukia Ali, basi hakika amenichukia mimi."


HADITHI YA ISHIRINI NA TISA
"Omar Ibn Khattab akiri ubora wa Ali"
Omar bin Khattab (r.a.) amesema: "Najua kuwa Ali (a.s.) anayo mambo matatu, ambayo ningekuwa na mojawapo tu mimi, kati ya mambo hayo ningeona fakhari zaidi kuliko kupata ngamia wekundu. Jambo la kwanza ni kuwa Mtume (S.A.W.W) amemwoza Binti yake, na amemzalia mabwana wawili wa vijana wa watu wa Peponi: Hassan na Husain (A.S.) Na jambo la pili ni kufungwa milango yote isipokuwa mlango wake (yaani, Mtume (S.A.W.W) aliifunga milango yote iliyokuwa ikipitiwa na Masahaba kama vile Abu Bakar, Omar bin Khattab na wengineo kutoka majumbani mwao kuingia Masjidun-Nabawy. Na jambo la tatu ni kuwa Mtume (S.A.W.W) alimpa bendera siku ya vita ya Khaybar.


Hakika hili neno la Omar (R.A.) wamelitaja wanazuoni wengi wa Kisunni ima kwa ufupi au kwa maelezo marefu. Ambaye aliyelitoa kwa ufupi ni Muhibad-Deen Tabary katika Riyaadhun Nadhra Juzu 2, ambae amesema: "Na katika hadithi alizozipokea Omar (R.A.) kuhusu Ali ni ile hadithi ya mambo matatu, nayo ni kama hivi: Ali anayo mambo matatu; kuwa na mojawapo kwangu kati ya mambo hayo ni bora zaidi kuliko kupata ngamia wekundi. Na ambaye aliyeeleza kwa urefu ni Ali Al-Muttaqi Hanafi katika Kanzul Ummal, Juzu 6, ambaye amesema kuwa katika Musnad ya Abi Shayba hadithi iliyotokana na Abdalla bin Omar imesema kuwa: "Wallahi Ali anayo mambo matatu ambayo kwayo kuwa na mojawapo tu kati ya mambo hayo ni bora mno kwangu kuliko kupewa ngamia wekundu.

(1) (Mtume (s.a.w.w.) amemwoza binti wake ambaye alimzalia viongozi wa Peponi.
(2) Kufunga (kuziba) milango yote, isipokuwa mlango wake (wa Ali A.S.)
(3) Na Mtume (s.a.w.w.) alimpa Ali bendera siku ya Khaybar.


HADITHI YA THELATHINI
uAli kupewa Beramu siku ya Khybar"
Omar (R.A.) amesema kuwa Mtume (s.a.w.w.) amesema: Bila shaka, kesho nitampa bendera mwanaume anayempenda sana Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Mwenyezi Mungu ataifungua (Khaybar) kwa kumshindisha mwanaume huyo." Omar (R.A.) amesema: ""Sikutamani Uamiri ila siku hiyo Basi ilipofika asubuhi mimi nikajitokeza kwa ajili ya Uamiri. Mtume (s.a.w.w.) akasema: uCEwe Ali! Nyanyuka uende (Khaybar) na ukapigane wala usigeuke (yaani, usiache mapigano mpaka Mwenyezi Mungu akupe ushindi katika mkono wako (hadi ushinde na kuuteka)".


Basi Ali akafuata amri hiyo na akaona karaha kugeuka kwa vile Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha asigeuke mpaka ashinde. Alipokuwa anakwenda alisema: Mpaka lini nipigane nao? Mtume (s.a.w.w.) akasema "Mpaka watakapokiri na kusema Laa-Ilaaha Ila Laah! Basi watakaposema hivyo itakuwa haramu kuwaua na kuzichukua mali zao ila kwa haki." Kwa hakika kisa cha kutekwa kwa Khaybar kwa mikono ya Amirul Mumineen Ali (A.S.) ni jambo lenye maana sana na wapokeaji wa hadithi hii ni kundi kubwa la Masahaba na Tabieen. Ama kauli hii ya Omar na mapokezi yake imeelezwa na kundi la wanazuoni wa Kisunni kwa ufupi na kwa urefu.


Na katika hao wanazuoni walioitaja hadithi hii kwa ufupi ni Muhibbud-Deen Tabary ambaye katika (hadithi) alizozipokea Omar (R.A.) kuhusu Ali (A.S.) ni kauli yake isemayo: "Sikupenda Uamiri ila siku hiyo (Mtume (s.a.w.w.) alipomwambia Ali: nitampeleka (mahali) fulani (Khaybar). Ama katika wanazuoni walioieleza hadithi hiyo kinaga ubaga ni Ahmad bin Hambari: hakika yeye ameieleza hadithi hii katika Musnad yake kutokana na Musnad ya Abi Hurayrah, kuwa amesema Mtume (s.a.w.w.)siku ya Khaybar kuwa: "Nitampa bendera mwanaume anayempenda sana Mwenyezi Mungu na Mtume wake;" Omar (R.A.) amesema, "Nikatamani uamiri siku hiyo, basi nikajitokeza na nikafanya bidii ya kutumaini kuwa atanipa mimi, basi ilipofika asubuhi (Mtume (s.a.w.w.) akamwita Ali, na akampa (hiyo bendera) na kumwambia: "Upigane wala usirejee mpaka (Mwenyezi Mungu) akujalie uiteke Khaybar kwa mkono wako Basi Ali akaenda kidogo kisha akasema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nipigane hadi lini?" Mtume (s.a.w.w.) akasema: "Mpaka watoe shahada kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja tu na hakika Muhammad (s.a.w.w.) ni Mtume wake. Watakapofanya hivyo, hakika wamejikinga damu zao na mali zao (isipokuwa haki ya dini); na hesabu yao ni kwa Mwenyezi Mungu."

Hakika Bukhari na Muslim wamenakili hadithi na kisa hiki katika Saheeh zao mbili (Juzu 2, na katika Juzu 4 na katika Juzu 16). Na Muslim ameeleza katika Saheeh yake (Juzu 2) na kwa mapokezi mengihe katika J. 2, uk. 325. Na Ali El-Muttaqi Hanafi ameieleza katika kitabu chake Kanzul-Ummaal (Juzu 6) na vile vile wameieleza hadithi hii wanazuoni wengi wa Kisunni na Shia (Mwenyezi Mungu awarehemu).

HADITHI YA THELATHINI NA MOJA
"Ali ni katika Mtume (s.a.w.w.) na Mtume ni katika Ali"
Omar (R.A.) amesema kuwa Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Ali: ""Wewe ni katika mimi, na mimi ni katika wewe."

Bukhari ameeleza hadithi hii ya Omar (R.A.) kuhusu Ameerul Mumineen Ali bin Abi Talib (A.S.) katika kitabu chake Saheeh, Juzu 14, katika mlango wa sifa za Ali (A.S.). Amesema kuwa Omar (R.A.) amesema: "Mtume (s.a.w.w.) amefariki dunia hali yeye yu radhi naye." (Yaani, Ali Bin Abi Talib) na amesema Mtume (s.a.w.w.) kumwambia Ali "Wewe ni katika mimi, na mimi ni katika wewe."

Na kwa hakika wameipokea hadithi hii kuhusu Ameerul Mumineen Ali bin Abi Tali (A.S.) kundi kubwa la wanazuoni wa Kisunni, Shafiiy na Hanafii kwa upokevu thabiti na sahihi ikitokana kwa masahaba na Tabieen watukufu wakubwa. Miongoni mwao ni Sibt Jawzi Hanafi katika kitabu chake Tadhkiratul Umma, kilichopigwa chapa Iran, Uk. 43. Yeye amesema: Mtume (s.a.w.w.) amesema, "Ali ni katika mimi na mimi ni katika yeye", siku ya vita ya Uhudi wakati kiongozi wa washirikina alipokusudia kumvamia Mtume (s.a.w.w.). Hapo Ali (A.S.) akajitolea kwa nafsi yake na akamhujumu yule kiongozi na akamwua. Papo hapo akateremka Jibreel (A.S.) na kusema: Ewe Muhammad, hakika huo ndio ukarimu na huku ndiko kusaidiana". Mtume (s.a.w.w.) akasema "Ali ni katika mimi na mimi ni katika yeye" Basi Jibreel akasema "Na mimi ni katika ninyi wawili." Na miongoni mwao ni Muhib bud-Deen Tabary Shafii katika kitabu chake Kifaa yatiit-Taalib, Uk. 142, AH El-Muttaqi Hanafi katika Kanzul Ummaal (Juzu 6, uk. 400). Angalia kitabu chetu All Wal Wasiy-Yah ambamo tumetaja wanazuoni wengine wengi wa Kisunni ambao wamenakili hadithi hiyo.


HADITHI YA THELATHINI NA MBILI
"Awapendaye Aali Muhammad ni mtu wa Peponi"
Omar bin Khattab (R.A.) amesema. "Fahamuni na mjuc kwamba utukufu hauwezi kukamilika ila kwa kumpenda Ali (A.S.) Kauli hii ya Omar (R.A.) Ibnu Hajar Ash-Shafii ameiandika katika kitabu chake, Assawaaiqul Muhriqa. Vile vile Ibnu Abdil Bir katika kitabu chake Istiab amenakili hadithi aliyopokea Ibnul-Musayyib ambaye amesema kuwa "Omar (R.A.) amesema "Wadhihirishieni mapenzi Masharifu na muwapende na mjilinde heshima na tabia zenu kutokana na watu wabaya na mfahamu kwamba haiwezi kukamilika heshima na sifa zenu zozote ila kwa kumpenda Ali.

Na Umar bin Khatab (r.a.) ameyachukua maneno haya kutoka kwenye hadithi ya Mtume (s.a.w.w.) iliyo mashuhuri sana iliyotolewa na wanavyuoni (Ulamaa) wengi wa Kisunni -Shafiiy na Hanafly, na wengineo. Na miongoni mwao ni Allama Ubaidullahi Ammrisari Al-Hanafiy, katika kitabu chake Ar-Jahul-Mataalib na kati yao ni al-Hamwini Shafiiy katika "Faraaidus Simtayin" Juzu ya pill. Na miongoni mwao ni Allama Zamakh-shari katika Tafsiri yake inayojulikana kwa jina la Al-Kash-shaf, jadala 2; na huyo Zamakh-shari ametoa hadithi hii kwa uthabiti na akasema Mtume (s.a.w.w.) amesema, "Yeyote atakayekufa katika (hali ya) kuwapenda (dhuria) wa Muhammad amekufa hali ya kuwa yu shahidi. Fahamuni si hivyo tu (bali) na yeyote atakayekufa katika (hali ya) kuwapenda Aali Muhammad, amekufa hali ya kuwa ni mwenye imani kamili.


Fahamuni (si hivyo tu (bali) yeyote atakayekufa katika (hali ya) kuwapenda Aali Muhammad amekufa hali ya kuwa ni mwenye imani kamili. Fahamuni (si hivyo tu; bali) ye yote atakayekufa katika (hali ya) kuwapenda Aali Muhammad (S.A.W.W) kwanza tu Malakul-Mawti atambashiria Pepo, kisha Munkar na Nakeer watambashiria Pepo. Fahamuni (si hivyo tu; bali) ye yote atakayekufa katika (hali ya) kuwapenda Aali Muhammad (A.S.) atafanyiwa shangwe kwenda peponi, kama vile anavyofanyiwa shangwe bibi arusi kwenda kwa mume wake, fahamuni (si hivyo tu; bali) na yeyote atakayekufa katika (hali ya) kuwapenda Aali Muhammad (A.S.) hufunguliwa yeye milango miwili ndani ya kaburi yake ya kwendea Peponi; fahamuni (si hivyo tu; bali) na yeyote atakayekufa katika (hali ya) kuwapenda Aali Muhammad (A.S.) Mwenyezi Mungu atafanya kaburi yake kuwa mahali pa kufanyia Ziara Malaika wa rehema kuja kuzuru."


Na hadithi hii ni ndefu sana; na tumetaja baadhi ya maneno yake tu. Je, unaweza kupatikana utukufu na usharifu wo wote utakaozidi sifa na utukufu wa mwenye kumpenda Muhammad na Aali Muhammad (s.a.w.w.) Je? Inaweza kukamilika heshima na utukufu wo wote bila ya (kupatikana )mapenzi ya Muhammad na Aali Muhammad (s.a.w.w.)?

Basi kauli ya Omar (R.A.) maafikiano na vile alivyotoa habari Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika alama za kuwapenda Aali Muhammad (s.a.w.w.) na Ali (A.S.) ndiye bora wao na ndiye mtukufu wao kwa maelezo ya hadithi nyingi za Mtume (s.a.w.w.).