FADHILA ZA SAYYIDNA ALI (A.S)

 

HADITHI A KUMI NA NANE
"Ali ni bora kuliko Masahaba wote"
Amehadithia Umar bin Khattab kwamba siku moja tulikuwa tumekaa katika duara na alipita Salman al-Farsi akienda kumwangalia mtu fulani. Kati yetu mmoja akasema, "Laiti mngependa nikujulisheni nani aliye bora wa umma huu baada ya Mtume wake, na aliye bora kuliko hawa watu wawili Abu Bakr na Umar?" Salman aliposimama kutaka kuondoka, akaulizwa: "Ewe Aba Abdallah unasemaje? Naye akasema, "Niliingia kwa Mtume (S.A.W.W.) wakati yumo katika sakaratil mauti na nikamwuliza, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, umeshausiya?" "Akasema, huwajui waliousiwa?" (ewe Salman). Nikasema "Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajua" Akasema, "Hakika Adam alimwusia (wasii wake) Shithi, hivyo alikuwa bora kuliko watoto wake wote baada yake. Nuhu alimuusia (wasii wake) Saam ambaye alikuwa bora baada yake. Musa akamusia Yusha, ambaye alikuwa bora baada yake. Suleiman akamwusia (wasii wake) Aasif Bin Barkhiya naye alikuwa bora baada yake. Isa akamwusiya Sha'muni As-Safaa ambaye alikuwa bora baada yake, na mimi nimemwusia (wasii wangu) Ali, ambaye ni mtu bora kuliko wote nitakayemwacha baada yangu".

Hadithi nyingi zenye maudhui haya zimepokewa katika vitabu vya ki-Sunni kutoka kwa Umar bin Khattab na Ibnu Umar. Katika Yanabi-ul-Mawddah (Uk. 253) hadithi iliyonakiliwa kutoka kitabu cha "Mawad-datulQurba" cha Sayyid Ali Hamdani as-Shafii, imeelezwa kuwa "Imepokewa adithi kutoka kwa mwana wa Umar (R.A.) kwamba alipita Salman Al-Farsi akienda kumuangalia mtu, na sisi tulikaa kikundi kwa duara. Kati yetu mmoja alisema: 'Laiti ningalikuambieni aliye bora katika umma huu baada ya Mtume wake, na bora kuliko hawa watu wawili Abu Bakr na Umar'. Akaulizwa Salman nani aliye bora? Akasema, "Bila shaka naapa kwa Mwenyezi Mungu, ningependa niwaambieni aliye bora katika umma huu baada ya Mtume wake, na bora kuliko hawa watu wawili, Abu Bakr na Umar." Kisha Salman akawa anaondoka, akaulizwa, "Ewe Aba Abdillahi umesema nini?" Akasema: "Niliingia nyumbani kwa Mtume (S.A.W.W.) wakati yuko katika sakaratil mauti; nikasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je umeusiya? Akasema: "Ewe Salman unajua nani waliousiwa?" Nikasema, "Mungu na Mtume wake wanajua." Akasema, "Hakika Nabii Adam, alimwusia Shithi, ambaye alikuwa bora baada yake, Nuhu alimwusia Saam, ambaye alikuwa bora baada yake, Musa alimwusia Yusha, naye alikuwa bora baada yake, Isa alimwusia Sham-uni As-Safaa aliyekuwa bora baada yake. Na mimi nimemwusia Ali, ambaye ni bora kuliko wote baada yangu.

Hadithi hii inatueleza kwamba kila Mtume katika Mitume waliopita alikuwa na wasii wake, hakufa bila ya kumtaja wasii wake. Kadhalika, Mtume wetu (S.A.W.W.) alimjulisha Salman na watu wengi kuwa kwa hakika kuainisha na kumtaja Mwusiwa wa Mitume ni jambo la lazima; kwa hivyo, Mitume wameainisha wausiwa wao kwa amri ya Mwenyezi Mungu, sio amri yao binafsi. Basi kuchagua Mtume, wasii wa Mtume, Khalifa, na Imam iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, si kwa mtu mwingine. Mwenyezi Mungu amesema katika Kurani:

WA-RA-BUKA YAKH-LUKU MAA YA-SHAA-U WAYAKH-TAARU, MAA-KAANA LAHUMUL KHIYA-RATU, (28:68) (Na Mola wako huumba atakavyo na huchagua atakavyo; Hawana viumbe hiari).

HADITHI YA KUMI NA TISA
"Ubora wa pekee wa Imam Ali (A.S.)
Umar bin Khattab (A) amesema kwamba, Mtume Mtukufu (S.A.W.W.) alisema: "Hakupata kuchuma mtu yeyote chumo la ubora kama ubora wa Ali, unamwongoza mwenyewe utukufu huo katika uongozi, na humwepusha na ubaya na upotovu. Ilivyokuwa hakuchuma yeyote chumo alilochuma Ameerul-Mumineen Ali (A.S.) hajatokea Sahaba mwema yeyote mwenye utukufu kama wa Ali (A.S.). Wanazuoni wa ki-Sunni wamedhihirisha kuwa kati ya Masahaba watukufu hakuna mwenye utukufu kama wa Ameerul-Mumineen Ali bin Abi Talib (A.S.).

Jalalud-Dini Assuyuti Ash-Shafii ameeleza wazi maudhui haya katika kitabu chake "Tarikhul-Khulafaa" (J. 1, Uk. 65) ambamo amesema kuwa Ahmad bin Hambali amesema: "Haukupokewa wala haukuja ubora kwa yeyote katika Masahaba wa Mtume (S.A.W.W.) kama ule uliopokewa kuhusu Ali (R.A.)."

Ibun Abdil Bir amesema katika 'Al-Istiab (J.2, Uk. 479), kilichopigwa chapa Haydarabad (India) mwaka 1319 A.H., kuwa wamesema Ahmad bin Hambal na Ismail bin Ishak Al-Kadhi kuwa "Haikuwahi kupokewa utukufu na yoyote katika Masahaba kama utukufu wa Ali bin Talib (R.A.)" Ath-Thalabi ameitoa kauli hiyo katika tafsiri yake ya aya hii tukufu:

"INNAMA WALIYYUKU MULLAHU WA RASULUHU WALAD-HINA AMANULLADHINA YUQI-MUNASSALAATA WA YUTUNAZ-ZAKATA WA HUM RAKIUUN" (Hakika Bwana wetu hasa (mwenye mamlaka juu yenu) ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walioamini ambao husimamisha swala na hutoa zaka katika hali ya rukuu. (Qur'an: 5:56)


HADITHI YA ISHIRINI
"Malaika mwenye sura ya Ali mbinguni"
Al-Muwaffaq bin Ahmad Al-Khowarazmi Al-Hanafi ameeleza hadithi katika kitabu chake Al-Manaaqib (Uk. 230) kutokana na Hamaad bin Thabit Al-Banani, ambaye ameipata kutoka Ubaid bin Umar Al-Laythi kutoka kwa Uthman bin Affani kutoka kwa Umar bin Khattabi kwamba Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala amewaumba Malaika kutokana na nuru ya uso wa Ali bin Abi Talib.

Wamepokea hadithi hii wanazuoni wa ki-Sunni katika vitabu vyao vingi vya hadithi. Miongoni mwao ni Al-Kanji As-Shafii katika kitabu chake "Kifaayatul-Taalib (Uk. 51) na hadithi yenyewe ni hii: "Anas amesema kuwa Mtume (S.A.W.W.) alisema, "Nilipokwenda Miraji usiku mbinguni nikamwona malaika mmoja amekaa juu ya mimbari ya nuru na malaika wengine wameizunguka ile mimbari. Nikamuuliza Jibreeli, huyu ni malaika gani? Akajibu, msogelee na mwamkie, nikamsogelea nipate kumwamkia, nikaona huyu ni ndugu yangu na Binamu wangu Ali Abi Talib!! Nikasema ewe Jibreeli, amenitangulia Ali kuja mbingu ya nne?"

Akanijibu "La sivyo, lakini malaika walimwomba Mwenyezi Mungu na kuonesha mapenzi yao kwa Ali; basi Mwenyezi Mungu akamwuumba malaika huyu kwa nuru yake katika sura ya Ali, basi malaika wanamzuru kila usiku wa kuamkia Ijumaa na siku ya Ijumaa kila mara malaika sabini elfu wanafika hapa na wanamtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu na thawabu ya tasbihi hizo, wanawatunzia wenye kumpenda Ali". Mtume akasema hadithi hii ni hasan na nzuri.


HADITHI YA ISHIRINI NA MOJA
"Ali ni mjuzi bora wa hukumu za Sharia"
Katika kitabu cha Ibnu Hajar Ash-Shafiiy 22 katika mlango ambamo ametaja sifa za Masahaba amemsifu Ali (A.S.) kwa kusema kuwa Ibnu Saadi ameeleza hadithi katika "Tabakati" aliyoipokea kutoka kwa Abi Hurairah akasema kuwa "Umar Bin Khattab amesema kuwa Ali ni mwenye kujua hukumu na maamrisho ya sheria kuliko sote. Mahala pengine Umar Bin Khattab (R.A.) amesema, "Ali Bin Abi Talib ndiye mwenye ujuzi zaidi wa hukumu na maamrisho ya Mwenyezi Mungu kuliko sote" 23

Jalalalud Deen As-Suyuti Shafii katika kitabu chake 24 katika mlango ambamo ametaja utukufu na sifa za Ali (A.S.) amesema Ibnu Saad amenakili hadithi kutoka kwa Ali. Hadithi hiyo ni kuwa aliulizwa Ali (A.S.) "Vipi wewe umepokea Hadithi nyingi sana za Mtukufu Mtume (S.A.W.W.) kuliko Masahaba wengine wa Mtume (S.A.W.W.)? Akasema, "Hakika mimi nilikuwa nikimwuliza naye akaniambia na nikinyamaza hunifunulia". Kadhalika Suyuti amenakili maneno haya kutoka kwa Abi Hurairah ambaye amesema kuwa Umar Bin Khattab amesema, "Ali ni mjuzi zaidi wa kila kitu katika hukumu za sheria kuliko sote". Hakim amenukulu maneno kutoka kwa Ibnu Masudi ambaye amesema: "Tulikuwa tunasema kuwa hakika mwenye maarifa ya hukumu zote za sheria kuliko watu wote wa Madina ni Ali". Suyuti ameendelea kusema, "Imepokewa kauli kutoka kwa Said Ibn Musayib kuwa amesema kuwa Umar bin Khattab alikuwa akiomba kwa Mwenyezi Mungu yasimfikie matatanishi yoyote wakati baba wa Hasan (Ali) hayupo."

Bila shaka kuomba kwa Umar (R.A.) asifikwe na matatizo wakati (Ali) baba wa Hasan asipokuwapo yametajwa na wanazuoni wengi wa Kisunni, Shafii na Hanafi; miongoni mwao ni Ibnu Abdil-Brr 25 ambaye alipokea maneno haya kutoka kwa Said Bin Musayyib kwamba "Umar alikuwa akiomba kwa Mwenyezi Mungu yasimpate matatizo mahali asipokuwapo Abul-Hasan." Vile vile Muhib-buddini Tabary Shafii katika kitabu chake 26 baada ya kueleza kisa cha mwanamke ambaye alizaa mtoto katika muda wa miezi sita na kupelekwa kwa Umar kutoa hukumu juu yake. Ameeleza maneno ya Said Bin Musayyib kwamba "Umar alikuwa akijilinda na matatizo wakati Abul-Hasan hayupo, (hadithi hii wamepokea Ahmad Bin Hambal na Abu Omar).

Aidha, Abul-Mudhaffar Yusuf Bin Kazaghli Hanafi katika kitabu chake 27 alisema kuwa, "Omar alisema kuwa katika hukumu yake kumbusu mwanamke aliyezaa katika (muda wa) miezi sita, aliamrisha apigwe mawe, lakini Ali Bin Abi Talib aliwazuia kufanya hivyo baada ya kuwabainishia sababu yake." Hapo Omar akasema, "Ewe Mola wangu usinibakishe katika matatizo wakati mtoto wa Abi Talib (A.S.) hayupo." Hayo yametolewa na Ali Al-Muttaqi Hanafiy katika kitabu chake kwa maneno yasemayo hivi: "Amesema Omar, "Ewe Mola wangu, usiniteremshie shida yoyote asipokuwepo Abul-Hasan (Ali) ubavuni mwangu." Muhib-buddin Tabary katika kitabu chake ameeleza maneno kutokana na Yahya Bin Aqeel kwamba Omar akimwambia Ali wakati anapomwuliza maswala yake: "Mwenyezi mungu asinibakishe duniani baada yako" (kwani hakuna awezaye kuondoa mashaka yangu). Mtungaji ameeleza hadithi hii kutokana na Abi Saidi Al-Khudriy kuwa yeye alimsikia Umar akimwambia Ali baada ya kumwuliza swali na kujibiwa, kuwa "Naomba kwa Mwenyezi Mungu nisiishi hata siku moja asipokuwepo huyo Abul Hasan."

Hakika Omar anayo maneno mengi na maelezo mbali mbali juu ya jambo hili aliyokuwa akiyasema wakati Ali (A.S.) alipokuwa akijibu swali lake. Baadhi ya maneno hayo tumeyakusanya katika kitabu chetu kiitwacho "Ali Wal-Khulafaa" 28 Angalia kitabu hicho ili upate kufahamu kuwa Ali (A.S.) alikuwa na daraja mbele ya watu wa zama zake, miongoni mwao wakiwa Makhalifa na wengine ijapokuwa alikuwa hukaa nyumbani tu. Ali ndiye aliyekuwa tegemeo la watu katika kuyatatua maswali na matatizo ya Waislamu. Na tumetaja katika hicho kitabu chetu "Ali Wal-Khulafaa" visa 140 vya matatizo na shida watu walizoleta kwa Ameerul Muumineen Ali (A.S.) na akawatatulia hata wakatosheka na kuridhika. Katika jumla ya wanazuoni wa Kishafii ambao waliotaja usemi huu wa Omar kuhusu Ali (A.S.) "Kuwa Ali ndio mjuzi wa sheria kuliko sote" ni Al-Kanjy Ash-Shafii katika kitabu chake 29 ambamo ameeleza hadithi aliyopokea Said Bin Jubayri kwa Ibnu Abbas kutoka kwa Omar (R.A.) kuwa yeye (Omar) alisema: "Ali ndiye mwenye ujuzi zaidi wa sheria kuliko sote." Tena akaendelea Umar kusema, "Nimeyachukua maneno haya juu ya Ali kwa Mtume (S.A.W.W.) wala sitaacha kamwe kuyasema."

Usemi huu wa Omar (R.A.) kuwa nimeyachukua hayo kwa Mtume (S.A.W.W.) ni dalili ya kwamba Mtume (S.A.W.W.) alisema: "Ali ndiye hakimu bora kuliko wote nyie." Kwa hivyo, Ali kuwa ndiye hakimu bora kuliko sisi sote inatokana na usemi wa Mtume (S.A.W.W.). Vile vile hadithi hiyo imeelezwa na Ibnu Sabbagh Al-Maliki katika kitabu chake 30 na Al-Kanji Ash-Shafii katika kitabu chake 31 baada ya kusema kuwa Ali alikuwa ndiye mjuzi zaidi kuliko Masahaba wote, na kuwa kuna njia na sababu nyingi zinazoonyesha kuwa Ali (A.S.) alikuwa mjuzi zaidi kuliko Masahaba wote. Neno lake Mtume (S.A.W.W.) lilikuwa "Ali ndiye hakimu kuliko nyote". Kwani hakimu (kadhi) anahitaji kujua kila namna ya elimu. Kwa vile akamchagua Ali juu ya wote kuwa hakimu (Kadhi), basi nidhahiri kuwa alizidi kuliko wote katika elimu zote.

Bila shaka miongoni mwa masahaba wengine kila mmoja wao alimshinda mwenziwe katika elimu fulani; kama alivyosema Mtume (S.A.W.W.) "Mjuzi kati yenu zaidi wa elimu ya mirathi ni Zaydi, na msomaji wenu zaidi ni Ubbay." Al-Kanjy akaendelea kusema kuwa Mtume (S.A.W.W.) alitaja daraja ya kila mmoja, na akataka azikusanye daraja hizo kwa binamu yake Ali Bin Abi Talib (A.S.) kwa tamko moja tu. Hivyo Mtume (S.A.W.W.) aliwaambia masahaba, "Hakimu (Kadhi) wenu (mwenye ujuzi kuliko wote) ni Ali". Na katika kitabu Riyaadhun nadhra 32 imepokewa hadithi ya Anas kutoka kwa Mtume (S.A.W.W.) kuwa amesema, "Hakimu (Kadhi) kuliko wote wa umati wangu ni Ali. Hadithi hii imeadikwa katika kitab cha El-Masaabeeh.


HADITHI YA ISHIRINI NA MBILI
"Ali ni Bwana wa kila mwenye kumsifu"
Akielezea cheo cha Ali (A.S.) kauli ya Omar (R.A.) ilikuwa "Ali ni bwana wangu na vile vile amenitatulia shida na kutoa hukumu ya haki mara nyingi sana." Yote haya utapata ukitazama kitabu cha Riyaa-Dhun-Nadhra, Juzu 2, Uk. 244.

Maelezo mafupi ya maneno ya Omar (R.A.) na kutaja kwake kuwa 'Ali ni bwana wangu' kumeelezwa na Muhib-Buddeen Attabary Ash-Shafiiyu katika kitabu chake Dha-Khaa-irul Uqba, Uk. 68, ambamo amenakili Omar (R.A.) kuwa: "Walikuja mabedui wawili wakigombana na kesi yao mbele yake. Omar akamwambia Ali (A.S.) "Hukumu kati yao ewe Abdul-Hassa!" Basi Ali (A.S.) akahukumu kati yao; Mmoja wao akasema, "Huyu ndiye ahukumu kati yetu!" Basi Omar (R.A.) aliruka na akamshika shingo ya (kanzu yake) na akasema: "Masikini wee! Unamjua huyu ni nai? Huyu ni bwana wangu na bwana wa kila mwenye kuamini, na yeyote asiyetaka kuwa Ali bwana wake basi si mwenye kuamini." Hadithi hii imeelezwa na Ibn as-Samani katika kitabu chake kiitwacho 'El-Muwaafaqah'. Muwaffaq Bin Ahmad El-Hanafiy pia ameitoa hadithi hii katika 'El-Munaaqib' na hadithi nyingine ya aina hiyo katika tukio jingine na Mwenyezi Mungu akipenda utaiona baadaye.


Omar (R.A.) katika kisa tulichokwishakieleza hapo awali maneno aliyomwambia yule mtu aliyetoa usafihi juu ya Ameerul-Mumeneen (Ali) (A.S.) kuhusu maneno ya Mtume (S.A.W.W.) juu ya cheo cha Ali, ni hadithi alioieleza El-Muhib Attabary katika kitabu chake tulichokitaja na kusema kuwa Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Baada yangu Ali ni bwana wa kila mwenye kuamini." Hadithi aliyopokea Imran Bin Hussein ni kwamba Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Hakika Ali ni katika mimi, na mimi ni katika yeye, na yeye baada yangu ni bwana wa kila mwenye kuamini." Hadithi hii imeelezwa na Tirmizi katika kitabu chake Saheeh Tirmizi; Juzuu 2, Uk. 46 (kimepigwa chapa Bara Hindi mwaka 1310 A.H.). Muhib-Buddeen Tabary Shafii amenukulu hadithi nyingine kwa jina la "Hadithi ya Omar (R.A.)" ambayo ni kama ifuatavyo:-

Buraydah Aslami alikuwa akimchukia na kumbughudhi Ali (A.S.). Basi Mtume (S.A.W.W.) akamwambia, "Ati unambughudhi Ali? Akasema ndiyo Mtume (S.A.W.W.) akamwambia usimchukie kabisa na ukiwa unampenda, basi mzidishie mapenzi (yako)." Baada ya hapo Buraydah akasema, "Hapana mtu yeyote aliye mpenzi zaidi kwangu baada ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.W.) kuliko Ali, kwani yeye ni katika mimi na mimi ni katika yeye nay eye ndiye bwana wenu baada yangu." Hadithi mbili hizi zimenakiliwa na Ahmad bin Hambal na katika kitabu cha Ibnu Katheer kiitwacho "Al-Bidaaya Wan Nihaaya", Juzuu 7, Uk. 345. Vile vile katika Musnad Abi Daud Attayaalisi, Juzuu 11 Uk. 306 na kupigwa chapa Hayder Abad mwaka 1321 A.H. wawili hawa wamenakili hadithi nyingine zenye maana ya hadithi tuliyoitaja iliyomo ndani ya "Dhakhaa-irul-Uqba". Hadithi ya Imam Ahmad Bin Hambal imo katika kitabu cha Musnad Juzu 2, Uk. 460. Muwaffaq Bin Ahmad Al-Hanafii katika kitabu chake "Al-Manaaqib", Uk. 35 ameeleza hadithi nyingine iliyokuwa na sifa mbili kuhusu Ameerul-Muumeneen Ali Bin Abi Talib (A.S.) na hadithi hiyo imepokewa na Abi Hudhay-fa. Na siku ya kwanza ni Ali kuiteka Khaybar na ya pili ni kuwa "Hakika Mtume (S.A.W.W.) siku ya Ghadiri Khum alimsimamisha (Ali A.S.) na akawajulisha watu kuwa Ali ndiye bwana wa kila mwenye kuamini mwanamume na mwanamke". Hadithi yenyewe kama alivyoeleza Abi Hudhayfa kutokana na Abdurahman Bin Abii Laylaa ni kama hivi: Mtume (S.A.W.W.) siku ya (vita ya) Khaybar alitoa bendera kumpa Ali Bin Abi Talib, basi Mwenyezi Mungu akaifungua (akaiteka) Khaybar juu ya mkono wa Ali (A.S.) pia Mtume alimsimamisha Ali siku ya Ghadiir Khum na akawajulisha watu kuwa, "Hakika Ali ndiye Bwana wa kila mwenye kuamini mwanamume na mwanamke."

HADITHI YA ISHIRINI NA TATU
"Ali ni katika miye na mimi ni katika Ali".
Mtungaji wa kitabu cha "Riyadhun-Nadhra" Juzu 2 UK. 244, ameeleza hadithi inayotokana na Omar (R.A.) kuhusu Ali (A.S.) hadithi hiyo ni ya kupewa Bendera siku ya (vita ya) Khaybar, anahadithia ya kuwa Ali (A.S.) anazo sifa tatu, na ile hadithi ya mambo matatu aliyasema Mtume (S.A.W.W.) katika (habari) ya Ali (A.S.). (Na Omar) akatamani kuwa na mojawapo katika (mambo matatu) hayo, na hadithi aliyoisema Mtume (S.A.W.W.) kumwambia Ali (A.S.), "Wewe kwangu ni sawa na daraja ya Mtume Harun kwa Musa (A.S.)," na (ile) hadithi aliyosema Mtume (S.A.W.W.) Imani ya Ali ina uzito "Zaidi kuliko mbingu na ardhi saba; na hadithi ya kusema "Mtu yeyote ambaye mimi nimekuwa ndiye bwana wake basi na Ali ni bwana wake pia. Na neno lake (Omar) "Mimi sikupenda utawala ila siku Mtume (S.A.W.W.) alipomwambia Ali "(kuwa atampeleka kuiteka M.

Khaybar kadha." Na neno lake (Omar) kumwambia Ali, "Umekuwa bwana wa kila mwenye imani mwanamume na mwanamke" na neno lake, Ali ni bwana wa mtu ambaye Mtume (S.A.W.W.) ni bwana wake na neno lake Omar kwa Ali (A.S.) "Hakika Ali ni bwana wangu". Na kumtatulia matatizo yake. Na neno lake la kusema mjuzi na hakimu kuliko sote ni Ali; na mara nyingi kutaka msaada wake katika mambo mengi ya dini.


Tumezitaja baadhi ya hadithi nyingi alizozipokea Omar kuhusu ubora wa Amiril-Mumeneen Ali bin Abi Talib (A.S.) na baadhi yake zimesalia na tutazileta akipenda Mwenyezi Mungu, miongoni mwao ni uhakika wa kupewa kwake (Ali) bendera siku ya Khaybar na maelezo yake yametajwa katika vitabu vya hadithi na tarehe za wanavyuoni wa Kisunni na Shia.

Basi katika kitabu cha Kanzul-Ummal, Juzuu 6, Uk. 395 imeelezwa hadithi iliyopokewa kwa Ibnu Omar kuwa Omar Bin Khattab (R.A.) amesema kwamba Mtume (S.A.W.W.) amesema: "Bila shaka nitampa bendera mwanamume anayempenda (sana) Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni shujaa, si mwenye kukimbia (au kuogopa) na Mwenyezi Mungu atafungua (Khaybar) mikononi mwake, na huku Jibrili yu upande wake wa kulia, na Mikaili yu upande wake wa kushoto." Basi watu wakalala na shauku kubwa juu ya jambo hilo. Ilipofika asubuhi Mtume (S.A.W.W.) akasema, "Yuko wapi Ali?" Masahaba wakasema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Ali anaumwa macho Mtume (S.A.W.W.) akasema mleteni (Ali). Alipoletwa Mtume akamwambia, "Sogea karibu kwangu." Alipokaribia Mtume (S.A.W.W.) akapaka mate yake kwa mkono wake machoni mwa Ali. Basi Ali akasimama mbele ya Mtume kana kwamba hakuumwa macho kabisa. Na Dara Qutni ameinakili hadithi hii katika Sunani yake, na El-Khatibu Baghdaadiy katika Tarekhe yake, Maliki katika riwaya ya Maliki na Ibnu Assakir katika tarekhe yake.


Uhakika wa kisa cha Ushindi wa Khaybar kwa mkono wa Ali (A.S.) ni jambo linalojulikana na mashuhuri na kupokewa na wanavyuoni wengi sana kwa njia mbalimbali. Hapa tunawataja baadhi ya wanavyuoni wa Kisunni. Miongoni mwao ni Imamu Bukhari katika Sahihi yake, Juzu 13, Uk. 301, iliyopigwa chapa bara Hindi mwaka 1282 A.H., na Imam Muslim katika Sahihi yake, Juzu 2 uk. 102, na El-Baghawiy katika Misbaahas-Sunna, Juzu 1, uk. 201, na Tirmizi katika Jaa-Mi, Juzu 2, uk. 461, na Ahmad Bin Hambal katika Musnad yake, mahali pengi, Juzu 1, uk. 99 na 133; na Juzu 3 uk. 16; na Juzu 4, uk. 128; na Juzu 5 uk. 358.


Vile hadithi hii imetajwa na El-Hakimu An-Nisha-puuriy katika Mustadrak, Juzu 3, uk. 108, Abu Naim katika kitabu chake Hil Yatul-Awliya, Juzu 1, uk. 62, na Ibnu Katheer katika kitabu Al-Bidaya Wan-Nihaaya, Juzu 7, uk. 4336, na Ali El-Muttaqi katika kitabu Kanzul-Ummal kilichoandikwa pembezoni mwa Musnad ya Ahmad, Juzu 4, uk. 130. Alisema Marhab (aliyoyasema) na Ali (a.s.) akajibu hivi "Mimi ndiye ambaye mama yangu ameniita Haydar kama simba wa porini aliyekuwa na sura ya kutisha, nitakuuweni kwa upanga na kukumalizeni kama vile ninafyeka majani bila ya hofu yoyote." Hapo Ali (a.s.) akaking'oa kichwa cha Marhab kwa upanga na ndipo ushindi wa (Khyabar) ukapatikana kwa mkono wake.