FADHILA ZA SAYYIDNA ALI (A.S)

 

HADITHI YA KUMI NA MOJA
"Imani ya Ali ni kubwa zaidi kuliko kitanga cha wakaazi wa mbingu na "
Imenakiliwa katika Dhakhairul-Uqba (Uk. 100) hadithi kuwa Umar bin Khattab amesema: 'Nashuhudilia kwa Mtume (S.A.W.W.) kuwa bila shaka nimemsikia akisema: "Lau mbingu saba na ardhi saba zingewekwa katika kitanga kimoja (mizani) na ikawekwa imani ya Ali katika kitanga (mizani) cha pili, ingezidi (uzito) imani ya Ali". Hadithi hiyo imenakiliwa na Ibnu Saman katika Al-Muwafaka, Al-Hafidh As-Salafi katika Al-Mashikhatul baghadadiyah, na Al-Muhibbu Attabari As-Shafii katika kitabu chake "Ar-Riyaadhun Nadhra (J. 2, Uk. 226) na maneno ya hadithi hiyo katika vitabu hivyo viwili hayatafautiani.


Hadithi hii imenakiliwa na kundi la wanazuoni wa ki-Sunni, Shafii, Hanafi na wengine, kati yao ni Sheikh Suleman Al-Kunduzi katika "Yanabiul Mawadah" (Uk. 254) ambaye amesema, "Imepokewa hadithi kutoka kwa Ubaidullah Juwayshfa bin Murra Al-Iry kutoka kwa babu yake kuwa watu wawili walimwendea Umar bin Khattab na kumwuliza kuhusu Talaka ya mjakazi (ngapi?). Alikwenda nao katika mahala watu wamekaa duwara, katika duara hiyo alikuwa mtu mmoja kipara, Umar akasema, ewe mwenye upara unaonaje katika Talaka za mjakazi? Basi akaashiria (yule kipara) kwa kidole cha chanda na cha kati. Ibnul Khattabi akasema Talaka ni mbili. Kisha akawaambia: 'Huyu ni Ali bin Abi Talib".


Nimeshuhudia kuwa kwa hakika mimi nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akisema "Lau imani ya wakaazi wa mbingu saba na ardhi saba ikiwekwa katika kitanga kimoja cha mizani) na ikawekwa imani ya Ali katika kitanga (mizani) cha pili ingezidi (uzito) imani ya Ali Ibnu Abi Talib".

Hadithi hiyo imenakiliwa na Sayed Ali Hamadany Ash-Shafii katika Al-Mawaddah. Katika Mawaddah ya saba. Miongoni mwa walionakili hadithi hii pia ni Al-Khateeb Al-Muwaffak bin Ahmad Al-Khowarazmi Al-Hanafi katika "Al-Manaqib" (Uk. 78). Amesema kuwa hadithi hii imetoka kwa Sabrah kutoka kwa baba yake ambaye ameipata kutoka kwa babu yake nayo ni kuwa "watu wawili walimwendea Umar wakamuuliza nini hukumu ya Talaka ya mjakazi? Akaenda nao kwa kikundi cha watu waliokaa duara, ndani mwao, alikuwepo mtu mwenye kipara. Umar akamuuliza unasemaje katika hukumu ya Talaka ya mjakazi (ngapi?) Akajibu kwa ishara ya vidole vyake kuwa ni mbili. Hapo Umar akageuka na kuwaambia Talaka ni mbili. Mmoja ya wale wawili akasema, sisi tumekuja kwako na wewe ndio Khalifa tukauliza. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba (Ali) hakukusemeza (ila kwa ishara tu). Umar akamwambia, ole wako! Unamjua huyu ni nani? Huyu ni Ali bin Abi Talib. Mimi kwa hakika nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akisema, "Lau mbingu saba na ardhi saba zingaliwekwa katika kitanga cha mizani na ikapimwa imani ya Ali, uzito wa Imani ya Ali ungezidi uzito wa imani ya mbingu na ardhi."


Hadithi hii pia imeelezwa kutoka kwa Muskala Al-Abdi kutoka kwa baba yake ambaye ameipata kwa baba yake kuwa Umar bin Khattab amesema; "Ninathibitisha jina la Mtume (S.A.W.W.) kuwa nimemsikia akisema: "Lau zingewekwa mbingu sababu na ardhi saba katika kitanga (kimoja) cha mizani, na ikawekwa imani ya Ali bin Abi Talib katika kitanga cha (pili) cha mizani, ingezidi imani ya Ali." Kwa ufupi ninataja majina ya wapokezi wa hadithi hiyo na vitabu vyao: (a) Ali Al-Muttaki katika "Kanzul Ummali" (J. 6, Uk. 156) ambaye amenakili kutoka "Firdausul Akhbar" cha Daylami kutoka kwa Ibnu Umar si Umar. (b) Al-Kanji katika "Kifaytul Talib" (Uk. 129). (c) Al-Jawhari katika "Fadhailu Ali" (d) Muhaddithi wa Shaam katika Tareekh yake katika mlango kuhusu wasifu wa Ali (A.S.).

Tumeikuta hadithi hiyo katika kitabu cha Tareekh cha Ibnu Asakir (Uk. 88) katika juzu ambayo ni mahsusi kuhusu Ameerul Mumineen Ali bin Abi Talib (A.S.) na nakala yake ipo katika Maktaba ya Al-Imam Ameerul Muumineen katika mji wa An-Najaful Ash-raf, (e) As-Safuri Ash-Shafii aliyofariki mwaka 658 A.H. katika kitabu chake kiitwacho "Nuzhatul Majalis" (J.2, Uk. 240) kilipigwa chapa Misri mwaka 1320 A.H.


HADITHI YA KUMI NA MBILI
"Sifa pekee tatu za Ali"
Katika "Manaaqib" cha Al-Khateeb Al-Muwwafak bin Ahmed Al-Khowarazmi Al-Hanafii (Uk. 232) imenakiliwa hadithi kutokana na Umar bin Khattab kuwa amesema: "Hakika amepewa Ali bin Abi Talib mambo matatu ambayo kwayo natamani walau ningalikuwa nalo mojawapo ingekuwa bora kwangu kuliko kupewa ngamia wekundu. Akaulizwa ni yepi hayo? Akasema, "Kuozwa mtoto wa Mtume (S.A.W.W.) (Mwana Fatma); kukaa msikitini pamoja na Mtume (S.A.W.W.) kuwa na ruhusa kuwapo kwake msikitini kama ilivyo halalishiwa Mtume (S.A.W.W.), yaani, kuweko msikitini katika hali ya (janaba); na kupewa bendera siku ya (vita) ya Khaibar."


Hadithi hii imenakiliwa na kikundi kikubwa cha wanazuoni wa ki-Sunni, Hanafi, Shafii na wengine. Miongoni mwao ni Ubaidullah Amritsari Al-Hanafi katika kitabu chake Arjahu Mataalib. Jalalud-Deen Syooti, Ash-Shafii, katika kitabu chake Tareekhul Khulafaa (J. 1., Uk. 66) amesema hivi: 'Abu Huraira amesema kuwa Umar bin Khattabi ametamka ya kuwa; "Hakika amepewa Ali mambo matatu. Natamani ningalikuwa nalo moja tu katika hayo, ingekuwa bora kwangu kuliko kupewa ngamia wekundu." Aliulizwa ni yepi? Akasema: Kuozwa Fatma mtoto wa Mtume Muhammad (S.A.W.W.); kukaa msikitini pamoja na Mtume (S.A.W.W.) na kuhalalishiwa yeye (humo) alichohalalishiwa Mtume (S.A.W.W.); na kupewa kwake bendera siku ya Khaybar." Na miongoni mwao ni Al-Hakim Ash-Shafii katika Mustadrak-us-Sahiehain (J.3, Uk. 125) kutokana na Abu-Hurayra.

Maneno ya hadithi aliyopokea yeye na aliyoipokea Suyooti ni sawa, na ameongezea kusema kuwa "Hadithi hii ni yenye sanadi sahihi, lakini Bukhari na Muslim hawakuitaja." Vile vile hadithi hii imetajwa na Ibunu Hajar Al-Haytami Ash-Shafii katika As-Sawaiq (Uk. 78) na maneno yake na ya Suyooti ni sawa. Kadhalika, Ahmad bin Hambal kwa sanadi iliyo sahihi kutokana na Ibnu Umar na Ibnu Katheer Ad-Damashki katika kitabu chake Al-Bidaya-wannihaya (J. 6, Uk. 341) inayotokana na Umar wameinakili hiyo hadithi. Ali Al-Muttaki Al-Hanafi katika Kanzul-Ummal (J.6, Uk. 393) katika hadithi nambari 6013 iliyotokana na Musnad Ibnu Abi-Shaiba, ambayo maneno yake yanafanana na ya Khowarazmi. Na pia katika hadithi nambari 6014 na 6015. Mfano uliotolewa na Umar wa ngamia wekundu una maana ya kuwa zamani hizo ngamia kama hao walihisabika kuwa ni mali bora kabisa kwa Waarabu.


HADITHI YA KUMI NA TATU
"Kumpenda Ali ni kumpenda Mtume"
Imesimuliwa hadithi kutoka kwa Ibnu Abbas kuwa Umar bina Khattab alikuwa akisema, "Jizuieni na kumtaja (kwa ubaya) Ali bin Abi Talib; hakika mambo mengi nimeyaona kwake kutoka kwa Mtume natamani ningalikuwa nalo moja tu katika ukoo wa Al-Khattab ingekuwa bora kwangu kuliko kuvipata vitu vyote vinavyopata mwangaza wa jua. Nilikuwa mimi na Abu Bakr na Abu Ubaida pamoja na baadhi ya masahaba wa Mtume, tukaenda mpaka mlangoni kwa Ummu Salama, Ali alikuwa amesimama mlangoni, tukamwambia tunamtaka Mtume (S.A.W.W.). Akasema anakuja. Akatoka Mtume (S.A.W.W.) tukaenda kwake.


Mtume akamwegemea Ali bin Abi Talib, kisha akampiga begani (Ali) na kusema, "Wewe ni wa kwanza kuamini miongoni mwa walioamini, mwenye maarifa ya Neema za Mwenyezi Mungu, mwenye kutekeleza ahadi za Mungu, mwadilifu katika ugawaji, mpole mno kwa raia, mbora wao mno katika kuvumilia taabu, msaidizi wangu, utakayeniosha, utakayenizika, utakayetangulia katika mambo yote ya shida (magumu) na machungu, hutarudia ukafiri baada yangu, wewe utakuwa mbele yangu na umeshika mikononi 'Liwaul-Hamad', utawafukuza watu (wasiokupenda) kwenye hodhi (Kauthar) yangu". Kisha Ibnu Abbas akasema, "Hakika Ali amefuzu kwa kuwa ni mkwe wa Mtume (S.A.W.W.) na kuwa mbora katika jamaa (Ahli-Baiti) na mkarimu wa kusaidia katika jambo lolote la kheri, mjuzi wa Tanzeel (Qurani), mjuzi wa Taaweel (Mafafanuzi) ya Qurani, mwenye kuwapita na kuwashinda mashiyaa".

Zimepokewa hadithi nyingi zenye kueleza maudhui ya hadithi hii, zilizo pamoja na zilizo mbalimbali. Hadithi hiyo hiyo ameinakili Ali Al-Muttaqi Alhanafi katika kitabu cha "Kanzul-Ummal". 18 Yamo maongezeko katika maneno ambayo hayajanakiliwa mahala pengine isipokuwa hapa.

Katika Musnad ya Umar bin Khattab kutoka kwa Ibnu Abbas imeelezwa kuwa Umar bin Khattab amesema, "Jizuieni kumtaja Ali (kwa ubaya) kwani mimi nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akieleza sifa tatu za Ali; na mimi natamani zaidi kuwa na walau moja katika hayo kuliko kuvipata vitu vyote vinavyopata mwangaza wa jua. Mimi nalikuwa na Ab u bakr, Abu Ubaida na kundi la Masahaba wa Mtume (S.A.W.W.) na Mtume alimuegemea Ali bin Abi Talib, mpaka akampiga bega la Ali kwa mkono wake na kisha kusema: 'Ali wewe ni wa kwanza kuamini katika walioamini na ni wa kwanza katika kusilimu, wewe daraja yako kwangu kama daraja ya Harun kwa Musa. Mwenye kudai kuwa ananipenda miye na huku anakuchukia wewe ni mrongo."


HADITHI YA KUMI NA NNE
"Ubora wa Ali hauwezi kupimika"
Imepokewa hadithi kutoka kwa Umar Bin Khattab ambaye amesema kuwa Mtume (S.A.W.W.) amesema: "Lau bahari ingekuwa wino, miti kalamu, binadamu waandishi na majini wahasibu, wasingeweza kuuhesabu ubora wako, ewe Abal Hasan" 19 (yaani Ali).

HADITHI YA KUMI NA TANO
"Ali ni kiongozi wa kila aliyemkubali Mtume kuwa ni Kiongozi wake." Imepokewa hadithi hii kutoka kwa Umar bin Khatttab kwamba Mtume (S.A.W.W.) alimfanya Ali kuwa kiongozi na akasema; "Yeyote mimi nikiwa kiongozi wake basi Ali pia ni kiongozi wake. Ewe Mola! Mpende anayempenda Ali, umfanyie uadui anayemfanyia uadui Ali, mwache anayemwacha (kumsaidia) Ali, mnusuru anayemnusuru Ali. Ewe Mola! Wewe ndiye shahidi juu yao. Umar Bin Khattab akasema, "Ewe Mola! Wewe ndiye shahidi juu yao.

Umar Bin Khattab akasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (wakati ule ulipokuwa ukituhutubia) kulikuwa mtu mmoja ubavuni kwangu kijana mwenye uso mzuri ananukia vizuri, akaniambia Ewe Umar hakika Mtume (S.A.W.W.) ametoa ahadi ambayo hatavunja ila aliye mnafiki, basi jihadhari na kuivunja hiyo ahadi. Hapo Mtume akaukamata mkono wangu na akaniambia; Ewe Umar kwa hakika kijana huyo si binadamu, bali alikuwa Jibril; ametaka kutilia mkazo kwenu maneno niliyoyasema kuhusu Ali" 20

Hadithi hii wameipokea wanazuoni wengi wa ki-Sunni katika Hanafy na Shafiy. Ni dhahiri kuwa tukio hili lilitokea siku ya Ghadiri. Sayyid Meer Hamid Husein Al-Hindi ametunga kitabu kikubwa juu ya hadithi ya Ghadeer ambacho ni juzuu moja katika Abaqaatul-Anvaar. Vile vile Al-Aminy ameeleza hivyo katika kitabu kiitwacho Al-Ghadeer.

HADITHI YA KUMI NA SITA
"Ali atakuwa na Mtume Peponi"
Amesimulia Umar bin Khattab kwamba alimsikia Mtume (S.A.W.W.) akimwambia Ali (A.S.), "Ewe Ali mkono wako uko katika mkono wangu, utaingia pamoja nami siku ya Kiyama popote nitakapoingia." Vile vile Anas bin Malik amesema kuwa Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Siku ya Kiyama ataletwa ngamia wa peponi, Ewe Ali utampanda; goti langu na lako, paa lako na langu yatakuwa pamoja mpaka kuingia peponi."

Zimepokewa hadithi nyingi 21 kutoka kwa wanazuoni wa Kisunni kuwa hakika Ali (a.s.) atakuwa pamoja na Mtume (S.A.W.W.) Peponi. Miongoni mwao ni hadithi zilizopokewa na sahaba Zaidi Bin Arqam kuwa hakika Mtume (S.A.W.W.) alimwambia Ali: "Wewe utakuwa pamoja nami katika jumba langu Peponi pamoja na mtoto wangu Fatma. Kisha Mtume (S.A.W.W.) akasoma aya hii "Ikhwaanan alaa sururin mutqaabeleen (15:47), yaani "Ndugu wenye kupendana na waliokaa juu ya viti vya kifalme wameelekeana" (wanazungumza kwa furaha kubwa). (15:47).

Ameeleza Abdallah bin Mas'ud kwamba Mtume (S.A.W.W.) alimwambia Ali, "Huridhiki kuwa wewe utakuwa pamoja na mimi Peponi na Hasan, Husein na watoto wenu watakuwa nyuma yetu na wake zetu watakuwa nyuma ya watoto wetu, na Shia (wafuasi wetu watakuwepo kulia na kushoto kwetu?"

HADITHI YA KUMI NA SABA
"Udugu kati ya Mtume na Ali"
Imepokewa hadithi kuwa Umar bin Khattab amesema kuwa Mtume (S.A.W.W.) alipofunga udugu kati ya masahaba zake, akasema huyu Ali ni ndugu yangu katika dunia na akhera na Khalifa wangu kwa watoto wangu (Ahl) na Wasii wangu kwa umati wangu, na mrithi wa elimu yangu na ndiye mlipaji wa deni langu, mali yake ni yangu, na mali yangu ni yake, nafuu yake ni nafuu yangu, madhara yake ni madhara yangu; atakayempenda Ali hakika amenipenda mimi, na atakayembughudhi Ali hakika amenibughudhi mimi."

Kwa hakika Umar mwenyewe amekiri kwamba Ali ni wasii wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.W.) katika umma wake, na mrithi wake kwa watu wa nyumba yake (Ahli). Kwa hakika zimepokewa Hadithi zaidi ya 200 kutoka kwa Mtume (S.A.W.W.) zenye madhumuni ya hadithi hii. Hadithi nyingi katika hizo tumezikusaya katika kitabu chetu kiitwacho 'Ali wal Wasiya' kilichopigwa chapa Najaf, Iraq.