FADHILA ZA SAYYIDNA ALI (A.S)

 

DIBAJI
BISMILLAHIR RAHMANIR RAHIM
Hii ni tafsiri ya kitabu kiitwacho
kilichoandikwa na Najumuddeen Sharif Al-Askari, wa Najaf, Iraq. Katika kitabu hicho mno hadithi 77 za Mtukufu Mtume Muhammad (S.A.W.W.) ambazo zimepangwa katika mada 50 kuhusu fadhila, ustahili na sifa za Sayyidina Ali bin Abi Talib (A.S.). Mabwana Ahmad bin Hanbal, Ismail bin Ishaq Al-Kadhi, Ahmad bin ali bin Shuaib-An-Nasai, na Abu Ali An-Neshapuri wanatamka kuwa haukupokewa utukufu na ubora wa Sahaba yeyote kwa hadithi sahihi na sanadi madhubuti, kama ulivyopokelewa utukufu na ubora wa Ali bin Abi Talib (A.S.).


Hadithi zote zilizotajwa katika kitabu hiki zimepokewa na Masahaba mashuhuri kama Bw. Abu Bakr, Bw. Umar bin Khattab, bw. Uthman bin Affan, na Bw. Jabir bin Abdullah, Bibi Aisha, na Bw. Abdullah bin Umar (R.A.). Mtungaji ameyataja majina ya vitabu pamoja na Juzu na ukurasa zilimopatikana hadithi hizo. Wal-hamdu Lillahi Awwalan Wa Akhiran wa Swallal-llahu Ala Muhammadin wa Alihit-Taahireen. Al-Ahkar S. Muhammad Mahdi Al-Muusawy.

HADITHI YA KWANZA
"Hakuna atakayepita Sirati ila tu yule mwenye kuidhiniwa na Ali kupita." Ibn Hajar Al-Haitami Ash-Shafiiy katika kitabu chake cha As-Sawaaiqul-Muhriqa (uk. 78/97) ameeleza hadithi kutoka kwa Ibnu-Saman kuwa Abi Bakr amesema, "Nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akisema, 'Hakuna atakayepita Sirati (njia ya kuendea Peponi) ila tu yule aliyeidhiniwa na Ali kupita'".

Vile vile katika kitabu cha Sunan Addarqutni imeelezwa hadithi inayosema hivi: Ali aliwauziza wale watu sita waliowekwa na Umar kushauriana mambo ya Ukhalifa kama kuna anayeweza kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kama kuna yeyote miongoni mwao aliyeambiwa na Mtume (S.A.W.W.) maneno haya, "Ewe Ali, wewe ndiye mgawaji wa Pepo na Moto siku ya Qiyama". Kama si mimi basi ni nani?' Wakasema, "Bila shaka ni wewe tu". Maneno hayo yanatokana na hadithi iliyoelezwa na Antara ambaye aliipokea kutoka kwa Ali al-Ridha ambaye amepokea kutoka kwa baba zake kwamba Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Ewe Ali hakika wewe ni mgawaji wa Pepo na Moto. Siku ya Qiyama, utauambia moto: 'Huyu wangu na huyu wako'".

Na katika kitabu cha Manaqib cha Khowarazmi imetajwa hadithi ya Antara kuwa Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Ewe Ali hakika wewe ni mgawaji wa Pepo na Moto na wewe ndiye utakayengoja mlango wa Pepo na kuingia ndani bila ya hisabu". 1 Katika kitabu cha Dhakhairul Uqba cha Tabari Assh-afii imeelezwa hadithi ya kumsifu Ali (A.S.) kuwa kwa hakika hapiti yeyote katika sirati ila yule aliyeidhiniwa na Ali kupita.2

Imepokewa hadithi kutoka kwa Qais bin Hatim ya kwamba walikutana mabwana Abu Bakr na Ali bin Abi Talib (A.S.). Abu Bakr akafurahi kumwona Ali (A.S.) na Ali akamwuliza amefurahia nini? Abu Bakr akamjibu, "Nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akisema: Hapiti yeyote katika sirati ila yule aliyedhiniwa na Ali kupita". Pia amesema kuwa amenakili hadithi Ibnu Saman katika kitabu Al-Muwafaqh na katika Manaqib cha Khowarazmi. 3 Na vile vile katika kitabu chake maarufu kiitwacho Maqtalul Husein 4 hadithi hiyo ilipokewa kutoka kwa Hasan Al-Basary ambaye alipokea kutoka kwa Abdallah, kuwa amesema Mtume (S.A.W.W.): "Siku ya Qiyama Ali bin Talib atakaa juu ya Firdausi (mlima ulio juu ya Pepo), na juu yake kuna Arshi ya Mola wa viumbe, na pembezoni mwa jabali yateremka mito ya Peponi na yatawanyika katika Pepo mbali mbali na yeye (Ali) amekaa katika kiti cha nuru, na mito yapita mbele yake iitwayo At-Tasneem, basi hapiti yeyote katika sirati ila awe nayo hati ya utii kwake na Ahli-Baiti zake. Ataangalia Ali, atamtia ampendaye Peponi, na amchukiaye Motoni."

Ibrahim Bin Muhammad Al-Hamwini Ash-Shafii katika Faraidus-Simtain 5 na Muhib At-Tabari katika Riyadhun-Nudhra 6 pia wameeleza hadithi hiyo. Kadhalika Hakim katika Al-Arbaeen pia amepokea hadithi hiyo. Ibn Abi Adsa katika historia amepokea hadithi hii hivi: Abu Bakr alimwambia Ali, "Nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akisema kuwa yeyote hapiti katika sirati ila tu yule aliyeruhusiwa na Ali kupita". Sulaiman Al-Hanifi katika kitabu chake cha Yana bee-ul-Mawad-dah 7, Ibnul Maghazili Shafii katika Manaa-qib na Ghaaya-tul Maraam na katika Tareekh cha Al-Katibul Baghdadiy 8, hadithi hiyo imesimuliwa kutokana na Ibnu Abbas. Vile vile Qadhi Ayadh ameeleza katika kitabu chake cha Shifaa, Allama Sayed Abu Bakr Shahabud-Deen Shafii katika kitabu chake cha Rash-fatus-Saa-di Min Buhuur, Fadhaail Bani Al-Hadi 9, Qarashi katika Shamsul Akbaar 10, Sheikh Abdallah Shabrawi Shafii katika Al-Ithnaaf Bihub-bil-Ashraaf 11 na katika Is-Afur-Raghibeen . 12 Basi hadithi hiyo wamehadithia kikundi kikubwa cha Masahaba licha ya Abu Bakr, Ibn Abbas. Ibn Masood na Anas bin Malik.

HADITHI YA PILI
"Kuangalia Uso wa Ali ni Ibada"
Ibnu Hajar, katika kitabu chake kiitwacho Ass-Sawaiq, (uk. 108) ameeleza kwamba, "Abu Bakr (R.A.) alikuwa akimwangalia sana usoni Ali. Aisha akamwuliza sababu yake, naye akajibu, "Nimesikia Mtukufu Mtume (S.A.W.W.) akisema kuwa kuangalia uso wa Ali ni Ibada".

Hadithi hii imeelezwa na Muhib-buddeen Attabari Ash-Shafii katika kitabu chake Ar-Riyaadhun-Nadhra (J. 2, uk. 244), na Ibn Katheer katika "Al-Bidaya Wan-Nihaya (J. 7, uk. 357) kutokana na Mabwana Abu Bakr, Umari, Uthman bin Affani, Abdalla bin Masoodi, Maadhi bin Jabal, Imraan bin Haseen, Anas, Thubani, Aisha, Abidhar na Jabir. (Tena akaendelea kusema) na katika hadithi aliopokea Aisha inasema hivi: "Kumdhukuru Ali ni Ibada". Muhib-buddeen Attabari amesema katika kitabu chake Dhakhairul Uqba (Uk. 95) kuwa hadithi hii ameipata kutoka kwa kikundi cha Masahaba na kutoka kwa Ibnu Mas'udi, na Amru bin Asi, na Jabir, na Abu Hurayrah, na Aisha. Hadithi alioipokea Aisha imo katika kitabu cha Al-Muwaafaqa cha Ibnu Samran aliyoipokea Ibnu Mas'udi imeelezwa na Abul Hasan Al-Hirbi, aliyoipokea Amrul Asi imenakiliwa na Al-Ab-hari na aliyoipokea Jabir na Imran bin Haseeni, na Maadhi, na Abu-Hurayrah ameeleza Ibnu Abil-Furati.

Al-Kanji Ash-Shafii aliyefariki dunia mwaka 658 A.H., katika kitabu chake 'Kifaa-yatut-taalib (Uk. 67) amesema hivi, 'Abudhar anasimulia kwamba Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Mfano wa Ali miongoni mwenu au amesema miongoni mwa Umma huu ni mithili ya Kaaba ilivyovikwa, kuiangalia ni Ibada na kuiendea kuhiji ni fardhi". Ameongezea kuwa Hadithi hii inayotokana na Abudhar na kupokewa kutoka kwa Abu Alman Al-Khitabi. Jalaa-lud-deen Assuyooti Ash-Shafii (aliyezaliwa katika mwaka 849 A.H., na kufariki dunia mwaka 911 (A.H.) katika kitabu chake "Taareekhul-Khulafaa (J.1, Uk. 9) pia ameitaja.


Vile vile hadithi hii ameitaja Ibnu Asaa-Kir kutokana na Abu Bakr, Uthmani bin Affani, Maadhi bin Jabali, Anas, Thobani, Jabir bin Abdillah na Aisha Al-Khowarazmi Al-Hanafi katika kitabu chake Al-Manaa-quib (Uk. 251) amesema aliipokea hadithi hii kutoka kwa Imraan bin Haseen nayo inaeleza hivi: "Kumwangalia Ali ni Ibada". Na Ibnu Asakir amepokea hadithi hiyo kwa njia ishirini na moja, baadhi yake zinahitilafiana maneno, baadhi ya maelezo yanasema hivi: Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Kuangalia uso wa Ali ni Ibada". Na zingine zaeleza hivi: Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Kumwangalia Ali ni Ibada", na zingine zaeleza hivi: Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Kuangalia uso wa Ali ni Ibada". Na zingine zaeleza hivi: Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Kumdhukuru Ali ni Ibada". Hii ya mwisho imepokewa na Bi Aisha kutoka kwa Mtukufu Mtume (S.A.W.W.).


Al-Muwaf-faq bin Ahmad Al-Hanafii, katika kitabu chake Al-Manaa-qulb (Uk. 251), ametaja hadithi kutokana na Imran bin Haseen kuwa "Nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akisema: "Kumuangalia Ali ni Ibada". Sheikh Kanduzi Al-Hanafii ametaja hadithi moja katika kitabu chake "Yanaa-bee-ul Mawad-dah (Uk. 254) kwa kunakili kutoka kitabu cha Mawad-datul Qurba cha Sayed Al Alo-Hamdani Ash-Shafii, kuwa Abdudhari amesema, Mtume (S.A.W.W.) alisema, "Ali ni mlango wa elimu yangu na mfafanuzi wa umma wangu baada yangu kwa yale niliyojia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, basi kumpenda yeye (Ali) ni Imani, na kumbughudhi ni unafiki". Vile vile akaendelea kusema kuwa hadithi hii ameeleza Abu Naeem na ameinakili katika Uk. 235 kama ilivyopokelewa na Abi Dar-da ambaye amesema kuwa Mtume (S.A.W.W.) alitamka, "Ali ni mlango wa elimu yangu na mfafanuzi wa umma wagu baada yangu kwa yale niliyojia kutoka kwa Mola, basi kumpenda Ali ni Imani na kumbughudhi ni unafiki, na kumwangalia ni rehema na kumpenda ni Ibada."


Hadithi hii pia imo katika kitabu cha Firdausul-Akhbaar, cha Al-Daylami na al-Hamwini Ash-Shafii Ibrahim bin Muhammad aliyefariki dunia mwaka 772 (A.H.) ameinakili katika "Faraidu-Simtain", Al-Qanduzi Al-Hanafii katika Uk. 90 "Yanaabee-ul-Mawad-dah" amesema kwamba Ibnu Maghazili Ash-Shafii amenakili hadithi hiyo katika "Al-Manaa-quib" kutokana na Imrani bin Haseen na Waathila bin Al-Askari na Abu-Hurayrah. Maelezo ni kuwa "Mtume (S.A.W.W.) amesema, "Kumwangalia uso wa Ali ni Ibada", Hadithi hii Ibrahim bin Muhammad al Hamwini Ash-Shafii pia ameeleza katika kitabu chake Faraidus-Simtain, kutokana na sahaba Abu Saeed Al-Khudri na Al-Muwaffaq bin Ahmad Alhanafii katika "Manaaquib" Uk. 8 Al-Kanji As-Shafii katika Kifaayatut-Taalib Uk.

124 ameeleza hadithi ndefu ndani yake akieleza sifa nyingi za Ali. Miongoni mwao ni hadithi hiyo. Basi sasa tunataja maneno ya hadithi aliyonakili Al-Kanji kutoka kwa Jaffer bin Muhammad As-Saadiq (A.S.) ambaye amepokea kutoka kwa babu yake Ali bin Hussein naye ameipata kutoka kwa baba yake, Husain bin Ali, kutokana na baba yake Ameerul-Mumineen Ali (A.S.) kwamba Mtume (S.A.W.W.) amesema. "Hakika Mwenyezi Mungu amemjalia ndugu yangu Ali bin Abi Talib sifa nyingi ambazo hazidhibitiki kwa wingi wake. Atakayetaja sifa moja tu katika sifa zake anuwai na kuikiri Mwenyezi Mungu atamsamehe madhambi aliyoyatanguliza na yatakayokuja, na atakayeandika sifa yake moja katika sifa zake nyingi hawataacha malaika kumwombea maghfira muda wote maandishi hayo yatadumu na atakayesikiliza sifa moja katika sifa zake hizo Mwenyezi Mungu atamfutia dhambi zake kwa baraka ya kusikiliza, na atakayeangalia kitabu (kilichoandikwa) sifa zake Mwenyezi Mungu atamfutia madhambi yake kwa kuangalia hicho kitabu. Kisha Mtume akasema, "Kumwangalia ndugu yangu Ali ni ibada na kumtaja ni ibada. Mwenyezi Mungu haikubali imani ya mja, ila tu ya yule aliye chini ya uongozi wake (Ali) na ambaye ametengana na maadui zake."


Kwa vile katika vitabu vya hadithi inadhihirika kuwa waliosimulia na kupokea hadithi hiyo ni Masahaba wakubwa kumi na nane ambao wametajwa majina yao katika hadithi iliyotangulia, basi fikiri vema ili upate faida yake.

HADITHI YA TATU
"Ali kwangu mie kama vile ilivyo daraja yangu kwa Mola wangu". Ibn Abbas amehadithia kuwa siku ya sita baada ya kutawafu kwa Mtume Muhammad (S.A.W.W.), Ali na Abu Bakr walikwenda kuzuru kaburi la Mtume. Ali akamwambia Abu Bakr atangulie kuingia katika chumba alimozikwa Mtume (S.A.W.W.). Abu Bakr akasema kuwa asingeweza kumtangulia yule ambaye amesikia Mtume akimsifia kuwa ni mtu ambaye "Daraja ya Ali kwangu miye ni sawa a mimi nilivyo kwa Mola wangu". 13 Kadhalika kuna hadithi nyingi zilizopokewa na Abu Bakr zinazokariri utukufu wa Ali na kuonesha hadhi ya Ali. 14


HADITHI YA NNE
"Kwa hakika Ali ni mwingi wa huruma na upole"
Shaabi anaeleza kuwa safari moja Abu Bakr alimwona Ali akija mbele yake. Abu Bakr akatamka kuwa yeyote apendaye kufurahi kumwona mtu aliye karibu sana na Mtume (S.A.W.W.) aliye na daraja kubwa, aliyetaabika sana kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu na aliye bora mbele ya Mtume kuliko yeyote mwingine, basi anapaswa kumwangalia Ali ibn Abi Talib." Akaendelea kusema kuwa amemsikia Mtume (S.A.W.W.) akisema: "Kwa hakika Ali ni mwingi wa huruma na upole".


HADITHI YA TANO
"Ewe Abu Bakr! Gao langu na gao la Ali ni sawa".
Habashi Bin Junaadah anasimulia kuwa siku moja alikuwa amekaa mbele ya Abu Bakr. Basi akamsikia Abu Bakr akisema "yeyote yule aliyeahidiwa chochote na Mtume (S.A.W.W.) asimame." Mtu mmoja akasimama na kusema "Mtume (S.A.W.W.) aliniahidi kunipa magao matatu ya tende. Naomba nipimiwe." Abu Bakr akamwitisha Ali na kumweleza madai ya mtu yule. Ali akampimia tende na kisha akaamrisha tende zihisabiwe. Ikaonekana kuwa katika kila gao mlikuwa tende sitini bila kuzidi au kupungua. Hapo Abu Bakr akatamka "Mwenyezi Mungu na Mitume wake wamesema kweli. Usiku ule wa Hijra tulipokuwa tunatoka pangoni na kuelekea Madina Mtume akaniambia "Ewe Abu Bakr, gao langu na gao la Ali ni sawa katika hesabu".


HADITHI YA SITA
"Ewe Abu Huraira! Hujui kuwa mkono wangu na mkono wa Ali ni sawa katika Uadilifu?" Omar Ibn Al-Khattab amesema kuwa yeye alielezwa na Abu Bakr kwamba Abu Hureira alikwenda kwa Mtume (S.A.W.W.) na akakuta gao la tende mbele yake. Akamtolea salamu Mtume (S.A.W.W.) ambaye akamjibu na kumpa gao moja la tende. Alipohisabu akakuta tende 43. Baadaye akaenda kwa Ali Ibn Abi Talib ambaye pia akampa tende na alipozihisabu aliona kuwa idadi ilikuwa ile ile.

Jambo hilo likamshangaza sana. Akarejea kwa Mtume (S.A.W.W.) na kumweleza yale yaliyotokea. Mtume (S.A.W.W.) akatabasamu na kusema kuwa, "Ewe Abu Hureira hujui kuwa mkono wangu na mkono wa Ali ni sawa katika uadilifu?" 15


HADITHI YA SABA
"Mtume na Ahlul Kisaa"
Zaidi Ibn Yathee amekariri kuwa amemsikia Abu Bakr akisema kuwa alimwona Mtume (S.A.W.W.) amekaa katika hema akiegemea upinde wa Kiarabu. Pamoja naye walikuwa Seyyidna Ali (A.S.), Seyyidati Fatima (A.S.) Seyyidna Hassan na Seyyidna Hussein (A.S.). Mtume (S.A.W.W.) akatamka, "Enyi Waislamu, mimi nina amani na wale wanaokaa na amani na watu walio katika hema hili na ninapigana na wale wanaopigana nao. Pia ninawapenda wale wanaowapenda na nina uadui na wale wenye uadui nao. (Kadhalika) ni mtu yule tu aliye mwema na mwenye hadhi na aliyezaliwa kwa wema ndiye atakayewapenda hao na ni yule tu mwenye kizazi kibaya ndiye atakayewabughudhi hao."

Mtu mmoja akamwuliza Zaid, "Ewe Zaid, ulimsikia Abu Bakr akisema hivyo?" Akajibu kuwa "Naapa kwa jina la Mola wa Kaaba (kuwa nimesikia)". Hadithi hii ni mashuhuri kwa jina la HADITHUL-KISAA. Hadithi hiyo imepokewa kwa njia mbalimbali kutoka kwa wanazuoni wengi wa Kishaafy, Hanafy na wengineo.


HADITHI YA NANE
"Sifa pekee za Ali"
Imepokewa hadithi kutoka kwa Jabir bin Abdillah kuwa Umar amesema; "Masahaba wa Mtume wanazo sifa kumi na nane (18), ambazo kumi na tatu (13) katika hizo ni mahsusi kwa Ali, na tano tu ndizo tumeshirikiana naye kuwa nazo." 16

HADITHI YA TISA
Zimepokewa hadithi nyingi ambazo zinamhusu Ali kuwa daraja yake kwa Mtume (S.A.W.W.) ni kama daraja ya Haruni kwa Musa. Umar aliwahi kumsikia mtu mmoja akisema Ali. Basi Umar akamwambia mtu yule kuwa amekuwa miongoni mwa wanafiki kwa sababu alimsikia Mtume (S.A.W.W.) akimwambia Ali kuwa Ali kwake alikuwa mfano wa Harun kwa Musa ila tu utume ulimalizika baada yake.17

Mtungaji ameandika kuwa vitabu vingi vimetungwa juu ya hadithi hiyo (k.v.) Seyyid Meer Hamid Hussein Al-Hindy (R.A.) ametunga kitabu kikubwa cha hadithi zinazothibitisha wasia za Mtume kuhusu uongozi na ukhalifa baada yake.

HADITHI YA KUMI
Kumepokewa hadithi kutoka kwa Umar bin Khattab ambaye amesema "Nimemsikia Mtume (S.A.W.W.) akieleza sifa tatu za Ali ambazo miye ningetamani kuwa na walau moja kati ya hizo. Wakati wa kueleza hadithi hiyo tulikuwepo mimi, Abu Ubaida, Abu Bakari na kikundi cha Masahaba wa Mtume (S.A.W.W.). Mara Mtume (S.A.W.W.) akampiga Ali begani na akatamka: 'Ewe Ali, wewe ndiye wa kwanza katika walioamini na mwanzo katika waliosilimu na kwangu miye daraja yako mithili ya Harun kwa Musa."

Mtungaji amesema kwamba hadithi hiyo imetolewa na Kundi kubwa la wanazuoni wa Ki-Sunni, wa Ki-Hanafi na Shafii. Na katika 'Dhakaairul Uqba' cha Muhibudin Attabari Ashshafii (Uk. 58) chini ya maudhui ya "kuwa yeye (Ali A.S.) ndiye wa mwanzo miongoni mwa waliosilimu". Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Umar (R.A.) imesema, "Mimi nilikuwa na Abu Ubaida na Abu Bakar, na watu wengi, alipopiga Mtume (S.A.W.W.) bega ya Ali bin Abi Talib na akasema, "Ewe Ali, wewe ndiye wa mwanzo wa kuamini kati ya walioamini. Na ni wa mwanzo wa kusilimu kati ya waliosilimu, na wewe daraja yako kwangu ni kama daraja ya Harun kwa Musa."

Pia Hadithi hiyo imeandikwa na Al-Khateeb Al-Muwaffak Ahmad Al-Hanafii, katika 'Manaqib' (Uk. 32), na Ibnu Kha'llikan katika 'Wafayatul Aayan' (J. 2, Uk. 104). Ali Al-Muttaqui Al-Hanafi katika 'Kanzul-Ummal' (J. 6, uk. 395) amenakili hadithi hiyo kutoka vitabu vingi kama vile Tareekh Baghad cha Ibnu Najjar, Al-Kuna' cha Hakim, na kitabu cha Hasan bin Badri, ambacho kimekusanya hadithi zilizopokewa na Makhalifa.