SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

 

SEHEMU YA TANO:
KATIKA WINGI WA IBADA ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S):
Hakuna katika Umma huu aliyekuwa ni mwenye kumuabudu sana Mwenyeezi Mungu (s.w) kuliko Fatima (a.s),alikuwa anasimama katika (swala zake) mpaka miguu yake inatuna na kuvimba. Mtume (s.a.w) alimuuliza Fatima (a.s):

Ni kitu gani ambacho ni kheri (kuliko vitu vyote) kwa Mwanamke? Fatima akasema, ni: ((Mwanamke asimuone Mwanaume na Mwanaume asimuone Mwanamke)). Mtume (s.a.w) akamkumbatia kisha akasema:
"Kizazi wao kwa wao" Na Imam Hasan bin Ali (a.s) amesimulia akisema:

Nilimuona Mama yangu Fatima (a.s) akiwa amesimama katika Mihrab (yaani sehemu yake ya kusalia) yake usiku wa Ijumaa,alibaki akiwa ni mwenye kurukuu na kusujudu mpaka asubuhi,na nilimsikia akiwaombea Waumini wa kiume na Waumini wa kike na akizidisha kuwaombea dua,na hajiombei yeye binafsi kitu chochote,nikamuuliza mama yangu: Ewe Mama yangu!: "Kwanini Hujiombei wewe mwenyewe nafsi yako kama unavyomuombea asiyekuwa wewe"? Akasema mama yangu: Ewe Mwanangu: "Jirani kisha Nyumbani"