SHAHADA YA SAYYIDAT FATIMA (A.S)

 

SEHEMU YA NNE:
FADHILA ZA SAYYIDAT FATIMA (A.S).
Sayyida Fatima (a.s) alikuwa ni miongoni mwa Watu wa Kisaa,na miongoni mwa watu wa Mubaahala ambao (tarehe ishirini na nane (28) mfungo tatu mwaka wa kumi (10) Hijria) waliongozwa na Mtume (s.a.w) kwenda kukutana na ujumbe wa kikristo kutoka Najran ili kujadiliana kuhusiana na Nabii Isa (a.s) ambapo maudhui ilikuwa ni kuhusu:

{Kuzaliwa kwa Nabii Isa bila Baba},Wakristo wao walikidai na kudhani kuwa Nabi Isa (a.s) Baba yake ni Mwenyeezi Mungu (s.w),siku hii ilikuwa ni siku maalum kwa ajili ya kuwarekebisha imani yao watu hao ambapo mtume (s.a.w) aliwasomea aya inayosema:

"Hakika mfano wa Isa mbele aya Mwennyeezi Mungu ni kama mfano wa Adam,aliumbwa kwa udongo kisha akamwambia kuwa naye akawa". Wakristo baada ya kug'ang'ania imani yao na itikadi yao hii batili ndipo Mwenyeezi Mungu (s.w) alipomwamrisha Mtume wake (s.a.w) katika aya ya 61 ya Suurat Aali Imraan,ambapo alimtaka afanye nao maombi kwa unyenyekevu,kisha waiweke laana ya Mwenyeezi Mungu (s.w) iwe ni yenye kuwashukia wenye kusema uongo.Ujumbe huo wa Wakristo uliokuja kukutana na Kundi la Mtume (s.a.w) ulikuwa ukiongozwa na Makasisi watatu:Ambao ni:

1-Ahtam
2-Al'aaqib
3-Sayyid.
Lakini wakristo baada ya kuona Nyuso alizokuja nazo Mtume (s.a.w) si Nyuso za kawaida wakaamua kuishia mitini!! Mmoja wa viongozi wa wakristo hao aliyekuwa akiitwa Sayyid, aliwashauri wakiristo hao wabishi kupindukia wenye itikadi dhaifu kwa kuwambia namna hii:

"Enyi Wakristo! Mimi naziona Nyuso hizi (yaani kundi hili la Mtume -s.a.w-) kama zitamuomba Mwenyeezi Mungu auondoe mlima mahala pake,wallah atauondoa.Msiapizane naye mtaagamia,na hatabaki mkristo hata mmoja hapa duniani mpaka siku ya kiyama" Askofu Ahtam naye baada ya kuziona Nyuso zile zikiwaka na kun'gara,hakuamini macho,akashindwa kuvumilia kwa mshangao ikabidi awambie wakristo na maaskofu wenzake:Niacheni nikamuulize Muhammad kuhusiana na hawa watu!! Alipomkaribia Mbora wa Mitume (s.a.w) akamuuliza:

"Ewe Abulqaasim! Unatoka na kina nani kwa ajili ya maapizano haya"? Mtume (s.a.w) akamjibu:Ninaapizana nanyi nikiwa na watu bora hapa duniani na watukufu mno mbele ya Mwenyeezi Mungu (s.w) nao ni:Mtume akaaza kuwataja kwa majina yao mmoja baada ya mwingine: 1-Ali
2-Fatima
3-Hasan {a.s}
4-Husein.


* * * Yule Askofu wa tatu Al-aaqib aliyekuwa ndiye mwenyekiti wa ujumbe huo,wakristo walimuuliza na akajibu namna hii:
"Enyi Wakristo wallah nyinyi mnajua kuwa Muhammad ni Nabii aliyeletwa na amekuja na ushahidi uliowazi kuhusiana na Nabii Isa (a.s),wallah hakuna watu walioapizana na Nabii wakasalimika,ikiwa mtaamua kuapizana naye basi mtaangamia."

Utakuta maulamaa na watunzi wa vitabu hivi wametaja kisa hiki kama inavyotakiwa na kama kilivyokuwa,ambapo wametaja kuwa wakristo hao waliogopa kufanya maapizano,wakaamua kuomba sulhu kwa kutoa Dirhamu Elfu Arobaini. Tukio hili linadhihirisha ukubwa wa Mwenyeezi Mungu,Mwenye nguvu na Hekima.

Pia tukio hili linadhihirisha ubora wa Sayyidat Fatima (a.s) ambaye alichukua nafasi ya wanawake wote wa uliwmenguni siku hiyo ya Mubaahala kwani mpangilio wa kikosi cha Mtukufu Mtume (s.a.w) ulikuwa katika mfumo alioutaka na alioukusudia Mwenyeezi Mungu (s.w) katika aya hiyo ya 61 ya suurat Aali Imraan.aya, aya hiyo inasema hivi: * "Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu" Mtume (s.a.w) akamuita Hasan na Husein (a.s).
* "Na wanawake wetu na wanawake wenu" Mtume (s.a.w) akamuita Fatima (a.s).
* "Na nafsi zetu na nafsi zenu" Mtume (s.a.w) akamuita Ali (a.s).

Sayyidat Fatima (a.s) pia alikuwa ni miongoni mwa wale ambao A'yatut-tat-hiir imeshuka kwao ikisema: "…Hakika Mwenyeezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume), na anataka kukutakaseni sana sana".{33:33) Ambapo Jibraiyl (a.s) alijifakharisha baada ya kuona kwamba naye miongo mwao (au yuko pamoja nao) chini ya Kisaa (Shuka). Sayyidat Fatima (a.s) pia ni Mama wa Maimam kumi na Wawili (a.s),wote hao asili yao ni Sayyidat Fatuma (a.s) na wote hao ni wajukuu wa Mtume (s.a.w).Pia Sayyidat Fatima (a.s) ni Mbora wa wanawake wote wa ulimwengu mzima tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka mwisho wake.

Na alikuwa (a.s) ndiye anayemfanana sana Mtume (s.a.w) katika mazungumzo kuliko watu wote,desturi yake,mwenendo wake na tabia yake vilikuwa vinahadithia na kusimulia desturi,mwenendo na tabia ya mtume (s.a.w).Matembezi yake (a.s) {alipokuwa akitembea} ndiyo yale yale ya Mtume (s.a.w), na alikuwa kila anapoingia kwa Mtume (s.a.w),basi Mtume (s.a.w) alikuwa akimkaribisha na kubusu mikono yake na kumkarisha sehemu yake ile aliyokuwa amekaa kabla ya Fatima (a.s) kuingia.Na Mtume alipokuwa akiingia kwa Fatima (a.s),basi Fatima (a.s) alikuwa anasimama na kumkaribisha na kumbusubu mikono yake (s.a.w).

Mtume (s.a.w) alikuwa mara nyingi {zisizohesabika} akimbusu Fatima (a.s), na alipokuwa akihitajia na kuitamani harufu nzuri ya peponi, basi alikuwa akinusa harufu yake na alikuwa (s.a.w) akisema: "Fatima ni sehemu ya Nyama yangu, atakaye mfurahisha atakuwa kanifurahisha mimi na atakayemfanyia ubaya atakuwa kanifanyia ubaya mimi, Fatima ni mbora wa watu kwangu"

Na kuna mengine mengi sana ambayo yanadhihirisha mahaba kibao ya Mtume (s.a.w) kwa mwanae Fatima (a.s), kama vile kumuita Fatima (a.s) kwa jina hili: {Ya Habiybat Abiyha}-yaa ni:
{Ewe Habibi (Kipenzi)wa Baba yake}.