HIKAYA ZA B A H L U L MWENYE BUSARA

 
HIKAYA ZA B A H L U L MWENYE BUSARA
(42).
BAHLUL NA MNAJIMU
Alikuja mtu mmoja kwa Harun Rashid na akadai kuwa na ilimu ya unajimu. Ikatokea Bahlul kuwapo hapo, na yule Mnajibu akaketi karibu na Bahlul. Bahlul alimwuliza: "Je waweza kuniambia mtu aliyeketi karibu nawe?" Mnajibu akasema: "La! simjui, Bahlul alimwambia: "Si maajabu hayo! Wewe huwezi kumjua mtu aliye karibu nawe, sasa itawezekanaje ukatuambia ukweli kuhusu habari za nyota zilizo mbinguni?" Mnajimu huyo akanyamaa kwa maneno ya Bahlul na akaondoka kutoka baraza lile.

(43).
BAHLUL NA KITABU CHA FALSAFIA
Ilikuwa ni siku ya Idd, Bahlul alikwenda msikitini alikuta watu wengi mno wameshajazana na hivyo hapakuwa na nafasi na viatu vya kila aina vilikuwa vimezagaa kila mahala. Kwa kuwa alikwisha ibiwa viatu vyake hapo awali, hivyo alihofu kuibiwa safari hii pia, ndivyo maana akatoa leso yake akaviviringishia na alipoingia Msikitini aliketi katika kona moja akiuangalia mno ule mzigo alionao. Ubavuni mwake alikuwapo mtu mmoja ambaye alimwuliza: "Mimi ninadhani kuwa wewe umekichukua kitabu muhimu mno, je kinahusu somo lipi?" Bahlul alimjibu: "Kitabu cha Falsafia!" Yule aliuliza: "Je umenunua kutoka duka lipi?" Bahlul alimjibu: "Nimenunua kutoka duka la mshona viatu!"


(44).
KUMWELIMISHA PUNDA?
Mtawala wa Kufa aliletewa Punda mmoja mzuri sana kama zawadi. Watu waliokuwapo katika Baraza walianza kumsifu huyo punda, mara mmoja miongoni mwa waliokuwepo, alisema: "Ehee! Mimi nitamuelimisha Punda huyu, hivyo nipo tayari kuwa mwalimu wake." Mtawala alipoyasikia hayo, alisema kwa furaha: "Maneno hayo aliyoyasema lazima uyatimize na hivyo ukifanikiwa nitakuzawadia utajiri mkubwa na lau utashindwa, basi nitatoa amri ya kuuawa." Huyo mtu alijutia mzaha wake . Pasi na lingine la kusema au kufanya, aliomba apatiwe kipindi fulani ili aweze kutekeleza hayo. Mtawala alimpa siku kumi tu. Mtu huyo alimchukua yule Punda akamleta nyumbani mwake. Kwa kweli alikuwa amezongwa na mawazo na kutaabika mno kwani alikuwa haelewi ni lipi la kufanya. Hatimaye alimwacha Punda nyumbani na yeye akaondoka kwenda sokoni. Hapo njiani alikutana na Bahlul na kwa kuwa alikuwa akimjua Bahlul busara zake, hivyo hakusita kumuomba msaada wake katika swala mushkeli kama hilo.


Bahlul alimwambia: "Ndiyo, naam! Mimi ninayo mbinu humo. Utafanikiwa iwapo utatekeleza vile nikuambiavyo." Bahlul alimwambia: "Usimpe chakula chochote kwa siku nzima. Chukua kitabu kimoja uweke ndani mwake uwele kidogo, na hivyo ndivyo umlishe huyo Punda, kwani atakuwa akila kutoka kitabuni. Na hivyo utekeleze kwa siku zote. Na ikifika siku ya kumi, usimpe chochote, abakie na njaa kali. Hapo ndipo umlete mbele ya mtawala na mbele ya watu wote ukiweke kitabu hicho mbele ya punda bila chalula chochote ndani yake." Huyo mtu alifanya hivyo hivyo kama alivyoelekezwa na Bahlul. Ilipowadia siku ya kumi, alimwendea Mtawala pamoja na kitabu na Punda na mbele ya wote akamuachia mbele yake Punda kile kitabu. Kwa kuwa punda alikuwa na njaa kali mno, hivyo alianza kufunua kila ukurasa wa kitabu hicho katika kutafuta chakula kama vile alivyokuwa amezoea. Huyo punda alipofikia ukurasa wa mwisho, akaelewa kuwa chakula chake hakikuwapo, na hivyo alianza kulia kwa sauti kubwa akitaka kuwaelezea wote kuwa alichokuwa akitaka ni chakula kwani alikuwa na njaa kali mno, lakini waliokuwapo hapo walidhani kuwa punda analilia kitabu kingine kwani amekimaliza hicho. Kwa kuyaona hayo, Mtawala huyo alijua kuwa kwa kwel i punda amesomeshwa na hivyo anajua kusoma kitabu. Mtawala alitimiza ahadi yake kwa kumpatia zawadi nono yule mtu hivyo Bahlul alimsaidia asiadhibiwe kwa kuuawa.


(45).
BAHLUL NA TAPELI
Siku moja Bahlul alikuwa na sarafu ya dhahabu mkononi mwake. Mtu mmoja alipoina, kwa kuwa alijua kuwa yu mwenda wazimu, alimwambia "Nipe, hiyo moja, nami nitakupa sarafu kumi za rangi hiyo." Bahlul alipoziona sarafu zake, alitambua kuwa zilikuwa ni za shaba ambazo hazikuwa na thamani yoyote ile. Hapo Bahlul alimwambia: "Nitakukubalia iwapo wewe utalia mlio wa punda mara tatu." Huyo Tapeli alikubali na akatoa mlio kama punda. Hapo ndipo Bahlul alipomwambia: "Nawe ni punda wa ajabu sana, pamoja na kuwa na upunda huu umetambua kuwa sarafu yangu ni ya dhahabu na zile ulizonazo nawe ni za shaba zisizo na thamani yoyote. Kwa kuyasikia hayo, Tapeli akaondoka zake moja kwa moja.


(46).
UJANJA WA BAHLUL
Siku moja mjini Baghdad, mtu mmoja alikuwa akidai kuwa yeye hadi leo hajawahi kudanganyika. Na katika kikundi hicho, Bahlul pia alikuwepo. Bahlul alimwambia huyo mtu: "Ni kazi ndogo sana lakini kwa wakati huu ninayo shughuli maalum ambapo sina fursa." Huyo mtu alisema: "Kwa kuwa unajua kuwa wewe hautaweza, hivyo unasingizia shughuli maalum. Hata hivyo, nenda ukimalize shughuli zako na uwahi haraka kwani mimi ninakusubiri papa hapa." Bahlul alimwambia: "Ndiyo, nisubiri hapa hapa kwani mimi nitafika sasa hivi." Kwa hiyo, Bahlul akaondoka zake, na wala hakurudi tena. Hapo nyuma yule mtu alisubiri kwa masaa mawili bila ya dalili zozote za Bahlul kurudi. Alisema akiwa amekasirika: "Kwa hakika Bahlul ni mtu wa kwanza kuniweka sawa kwani amenikalisha masaa yote bila sababu yoyote."(47).
UAMUZI WA BAHLUL
Mwarabu mmoja masikini alifika Baghdad. Alipokuwa akipita mitaani alikuta duka la kuuza vyakula vya kila aina na alinusa harufu nzuri nzuri za vyakula hivyo, lakini hakuwa na fedha za kununua kwa hiyo aliutoa mkate mkavu aliokuwa nao na akaanza kuupasha moto kwa mvuke wa vyakula vilivyokuwemo ndani ya sufuria. Mwenye duka akaangalia kwa punde, na mkate ulipokwisha, masikini alitaka kuondoka zake. Hapo mwenye duka alimzuia na kudai malipo, hapo ndipo palipoanza zogo baina yao wakati wakiendelea na zogo hilo, Bahlul alipita hapo, Mwarabu yule alitaka asaidiwe usuluhisho. Bahlul alimwambia mwenye duka: "Je huyu mtu amekula chakula chako au hakula? Mwenye duka alijibu: "Chakula hakijaliwa bali bila shaka amefaidika kwa mvuke wake." Bahlul alimwambia mwenye duka: "Ama hayo ni kweli kabisa, sikiliza!" Huku akitoa sarafu kutoka mfukoni mwake, alizihesabu moja baada ya nyingine na vile vile alikuwa akizidondosha chini zikitoa sauti. Hapo akamwambia mwenye duka: "Chukua sauti hizi za sarafu." Mwenye duka kwa ajabu alimwambia: "Je huu ni utaratibu gani wa kulipa fedha?" Bahlul alimwambia: "Kwa mujibu wa uadilifu na uamuzi wangu, mtu ambaye anauza harufu na mvuke bnasi malipo yake ni zile sauti za sarufu."


(48).
BAHLUL AZURU MAKABURI
Bahlul alikuwa akipendelea zaidi kukaa makaburini. Siku moja alipokuwa makaburini, Harun Rashid alifika hapo akienda mawindoni. Alipomfikia Bahlul alimwuliza: "Je Bahlul, wafanya kitu gani hapa?" Bahlul alimjibu: "Mimi nimekuja kuwaona wale watu ambao hawawasengenyi watu na wasiotarajia chochote na ambao hawawezi kunidhuru chochote." Harun alisema: "Je wewe waweza kuniambia kuhusu Qiyama, Sirati na maswali yatakayoulizwa kuhusu hii Dunia?" Bahlul alimwambia: "Waambie wahudumu wako wawashe moto na kuweka kikaangio cha mkate juu ili ipate moto." Ilipopata moto, Bahlul alisema: "Ewe Harun! Mimi nitasimama juu ya kikaangio hiki nitajitayarisha na nitakutajia kile nilichokula na kile nilichovaa."


Harun alikubali hayo. Bahlul alisimama juu ya kikaangio kilichopata moto na kwa upesi upesi akaanza kusema: "Bahlul, kilalio, mkate wa mtama na siki!" na alipomaliza, aliteremka chini huku miguu yake haikuungua hata kidogo. Ilipofika zamu ya Harun Rashid, alianza kujitaarufisha kwa mujibu wa matakwa yake, na kabla haja maliza kujitaarufisha, miguu yake ikaaungua na kumfanya aanguke chini. Alikuwa akijitaarufisha tu na wala hakuanza kuongelea yale aliyokula au kuvaa. Hapo ndipo Bahlul aliposema: "Ewe Harun! Maswali ya Qiyama yatakuwa hivi hivi. Wale wote watakaokuwa waja wema wa Mwenyezi Mungu, wenye kukinai na wasio na tamaa ya dunia ndio watu watakao pata raha kwa kupita haraka maswali na majibu ama wale wenye kupenda dunia na starehe zake, basi wao watabakia juu ya mtihani huo kwa muda mrefu pamoja na udhia wote."


(49).
BAHLUL NA MGENI
Mgeni mmoja alifika Baghdad na alipofika katika Baraza la Harun Rashid, aliuliza maswali mengi mno ambayo mawaziri pamoja na wenye ilimu walishindwa kuyajibu ipasavyo. Kwa kuona hali hiyo, Khalifa alighadhabika mno (kwa kuwa alikuwa ni Khalifa wa Umma, ilimbidi ayajibu maswali yote, badala yake) akatishia kumpa mali ya wote hao, yule mgeni. Lakini wote walimwomba muda wa masaa ishirini na manne(24) , na Khalifa aliwapa muhula huo. Mmoja wao akasema, "Mimi nadhani tumtafute Bahlul ambaye ndiye pekee atakayeweza kutoa majibu sahihi ya mgeni huyo." Hivyo walimtafuta Bahlul na kumwelezea yote yaliyotokea. Bahlul alikubali kumjibu mgeni, naye atafika hapo. Alimwelekea mgeni akisema: "Maswali unayoyapenda, unaweza kuyauliza, mimi nipo tayari kukujibu." Mgeni huyo aliinua fimbo yake na akachora duara moja, kisha akamtazama Bahlul. Na Bahlul bila ya kusita akachora mstari katikati ikigawa katika sehemu mbili sawa. Mgeni akachora duara nyingine, na Bahlul akaigawa katika sehemu nne, na alimwambia mgeni kuwa: "Sehemu moja ni kavu wakati sehemu tatu zilizobakia ni maji."


Mgeni alitambua kuwa Bahlul alkwishamjibu ilivyo sahihi kabisa, hivyo alimsifu Bahlul mbele ya wote. Baada ya hapo, mgeni huyo akakiweka kiganja cha mkono wake kwa kugeuza juu ya ardhi huku akiinua vidole vyake kuelekea mbinguni. Bahlul alifanya kinyume na vile alivyofanya yaani vidole vikaelekea chini ardhini na mkono wake chini. Kwa hayo Mgeni alimsifu mno Bahlul mbele ya Khalifa, akisema: "Lazima uwe na fakhari kwa kuwa na mwenye ilimu kama Bahlul." Khalifa kauliza: "Mimi sikuelea maswali hayo wala majibu yake." Hapo mgeni alianza kumjibu: "Kuchora kwangu duara na Bahlul kugawa ni kuelezea kuwa dunia imegawanyika katika sehemu mbili- Kaskazini na kusini. Na mduara wa pili, ulielezea kuwa dunia ina sehemu nne ambayo Bahlul alimchorea mistari miwili. Sehemu moja ardhi kavu wakati sehemu tatu ni maji. Na niligeuza viganja vyangu na vidole juu kulimaanisha kuota mimea na majani. Na Bahlul alifanya kinyume na vile nilivyofanya mimi akimaanisha kuwa miti na mimea huhitaji mvua na miale ya jua. Kwa hakika kunatakiwa kufanya ufakhari kwa kuwa na mtu hodari kama Bahlul!" Watu wote walimshukuru Bahlul kwa kuwasaidia na kubakiza heshima yao na kuponea chupuchupu adhabu za Harun Rashid.


(50).
BAHLUL AENDA BAFUNI
Siku moja Bahlul alikwenda bafuni (bafu za kulipia fedha ) na huko wahudumu hawakumjali ipasavyo bali walimdharau tu. Lakini yeye alioga na alipotoka nje akaenda moja kwa moja kwa mwenye mali, akampa Dinar kumi. Wahudumu walipoona hayo, walijuta mno kwani wangalipatapo chochote kama bakhshishi yao. Juma lililofuatia, tena alikwenda bafuni kuoga. Safari hii wahudumu walimkaribisha vyema na kumpa kila aina ya huduma ipasavyo. Alipomaliza kuoga, aliwapa wahudumu Dinar moja tu. Hao walimwuliza kwa hasira: "Loh! Juma lililopita bila ya huduma zozote ulilipa Dinar kumi na leo vipi baada ya huduma zote hizo unatoa Dinar moja tu.?" Bahlul aliwajibu: "Malipo ya leo nilikuwa nimeshalipa wiki iliyopita, hivyo ninatoa Dinar moja tu ili mjue, muwe daima mukikwahudumia wateja wenu vile iwapasavyo bila ya kuweka tamaa mbele."


(51).
BAHLUL NA MZOZO WA KUKU
Siku moja mfanyabiashara mmoja kutoka Bara Hindi alileta mali huko Baghdad na alipofika wakati wa njiani alibakia pamoja na msafara, na aliagiza chakula kwa mpishi mmoja, aliletewa kuku na mayai machache yaliyochemshwa. Baada ya kulala alipoamka alikuta msafara umeishaondoka na hivyo hakuweza kumlipa mpishi fedha za kuku na mayai. Baada ya mwaka mmoja kupita ikatokea kuwapo papo hapo, aliagiza chakula cha jioni. Mpishi alimletea vile vile yaani kuku na mayai machache yaliyochemshwa. Kulipokucha alimwita mpishi, na kumwambia: "Mimi unanidai deni la mwaka jana la kuku na mayai machache. Naomba unipatie hisabu hiyo na ya leo ili niweze kukulipa kwa pamoja." Mpishi, baada ya kupiga mahesabu yake kwa makini, alimwambia mfanyabiashara amlipe Dinar elf moja. Mfanyabiashara huyo aliposikia chakula cha jioni kugharimu Dinar elfu moja, alichukia na kusema: "Mimi nadhani kuwa wewe umewehuka kwa kudai Dinar elfu moja za kuku mawili na mayai machache." Mpishi alimjibu: "Loh! Unathubutu kuniambia mwehu huku mimi nimepiga mahesabu yangu kwa uangalifu ili nisije kukudai zaidi hata chembe kidogo?" Mfanyabiashara akasema: "Mimi nashukuru mno lakini umefikiaje kiasi hiki cha madai?" Mpishi akamjibu: "Tafadhali zingatia kwa makini kabisa nikuambiayo. Gharama hiyo ninayokudai imetokana na wewe kula kuku na mayai sita hapo mwaka jana.Iwapo kuku huyo angalikuwa hai basi mayai hayo angalilalia na hivyo angaliangua vifaranga. Na kila kifaranga angalitaga mayai kama hayo na vifaranga. Kwa hivyo, mimi ningalimiliki maelfu ya mayai na vifaranga, lakini yote hayo, nimekuachia wewe waniambia kuwa mimi ni mwendawazimu!" Wasafiri wote katika msafara walivutiwa na ugomvi huo, nao walifanya kila jitihada katika kuwanyamazisha na kuwasuluhisha lakini ilishindikana. Hatimaye ilifikiwa kuchukua hatua za kwenda mbele ili kupatia ufumbuzi wa maswala hayo. Mshauri alipoelezwa habari kwa ukamilifu, alitoa uamzi: "Ewe mfanyabiashara! Unatakiwa kumlipa mpishi huyu Dinar elfu moja." Kwa hayo, mfanyabiashara alihangaika na kubabaika kwani hakuelewa lipi la kufanya. Mmoja wa wasafiri, alikuwa ni rafiki yake Bahlul na alitambua kuwa ufumbuzi wa haki unaweza tu kutolewa na Bahlul. Basi aliwaambia: "Enyi wenzangu! Kutoka hapa hadi Baghdad si mbali na hivyo nitawaletea Qadhi wa Baghdad ili tupate hukumu yake katika swala hili. "Aliondoka mbio akimtafuta Bahlul, na alimkuta katika msikiti mmoja ambapo alimwelezea habari zote.


Alirudi pamoja na Bahlul hadi msafara huo. Walipoukaribia ule msafara, Bahlul alimwambia yule mtu "Wewe tangulia, nami ninakufuata kwa miguu na vile vile uwaambia kuwa mimi nitafika baada ya nusu saa hivyo wanisubiri. Qadhi ameahidi, atafika tu!" Huyo mtu aliwaambia hivyo hivyo,na watu wote walianza kupima kila dakika. Ilipofika nusu saa wakaona bado Qadhi hajafika, alifika baada ya saa moja na nusu na kila mmoja alisimama kutoa heshima zake. Aliketi na kuwaambia kuwa amekwisha pata habari za mgogoro wa mfanyabiashara na mpishi. Alisema: "Mimi naomba msamaha kwa kuchelewa kwani nilikuwa nikikoboa ngano, kwani ngano iliyokobolewa inaota vizuri zaidi na hivyo nilishughulishwa na hayo." Wote waliokuwapo walianza kusema: "Huyu Qadhi ni mtu wa ajabu kwani anakoboa ngano kabla ya kupanda shambani." Bahlul aliwajibu: "Kwani nini mumestaajaabishwa kwani kwenu hapa kuku aliyepikwa pia huweza kutaga mayai." Mshauri alisema: "Qadhi huyu amesema yaliyo sahihi kwani kuku aliyepikwa hatoi vifaranga!" Hatimaye, watu waliafikiana neno kwa kumpa fedha za kumridhisha yule mpishi. Nao wote wawili walikumbatiana kwa kufurahi.


(52).
HARUN AJENGA JUMBA LA KIFALME
Harun alijijengea jumba la kifalme, na ilipokuwa tayari, siku moja alikuwa darini akiangalia mandhari yaliyomzunguka. Mara alimuona Bahlul akiangalia jengo hilo jipya. Harun alimwita kwa kusema: "Ewe Bahlul! Ninalo ombi, je unaweza kuniambia maneno mazuri mno kwa ajili ya Jumba hili langu la kifalme?" Bahlul alitafuta mkaa na aliandika kwa haraka juu ya ukuta wa Jumba hilo maneno yafuatayo: "Umeinua ardhi ambapo umeipotosha Din. Iwapo umeijenga kwa fedha za Umma, basi kwa hakika umedhulumu na kwa hakika Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu."


(53).
ULIPAJI WA DENI.
Mtu mmoja alinuia kumchokoza Bahlul katika imani yake kuhusu Imam al-Mahdi (a.f.) na kudhihiri kwake ili kueneza utawala wa haqi na uadilifu duniani kote. Katika kikao kimoja ambapo na Bahlul pia alikuwapo, alisema: "Ewe Bahlul! Je si wewe unaitakidi kuwa Imam wako wa 12 al-Mahdi (a.f.) atadhihiri katika zama za mwisho wa dunia na ataleta utawala wa haki na uadilifu? Iwapo wewe u-thabiti juu ya itikadi hii basi nikopeshe dinar mia tano ambazo nitakupa wakati Imam wako atakapodhihiri." Bahlul alimjibu: "Bila shaka hiyo ndiyo itikadi na Imani yangu na niko tayari kukukopesha hivyo lakini ni lazima unihakikishie kuwa wewe hautakuwa umegeuzwa kuwa mbwa au nguruwe! Iwapo utageuzwa, basi nani atakayelipa?" Kwa kusikia hayo wote waliokuwapo wakaangua kicheko na yule mchokozaji akabung'aa asiwe na la kusema. Bahlul alijiondokea.


(54).
BAHLUL NA MAFUVU YA KALE
Siku moja Bahlul alikuwa amekaa makaburini akiwa na fimbo ndefu, huku akichunguza mafuvu mengi ya vichwa vya zamani yaliyokuwa yametawanyika hapa na pale. Harun Rashid alipita hapo na kumwona Bahlul akichunguza mafuvu hayo, Alisema: "Ewe Bahlul! Wafanya nini?" Bahlul alimjibu: "Najaribu kutambua kama mafuvu haya ya vichwa ni ya wafalme au ni ya mafukara, kwani yote nayaona sawa!" "Na hiyo fimbo ni ya nini?" aliuliza Harun. "Naipimia ardhi." alijibu Bahlul. Alianza Harun kwa kudhihaki: "Je unapima ardhi, hoja gani?" Bahlul alimjibu: "Ewe Harun! Urefu wa mikono mitatu kwangu mimi ijapokuwa mimi ni masikini ni sawa na mikono mitatu kwangu kwako wewe ijapokuwa una fahari na mali!" (Yaani wote wanaingia katika kaburi la vipimo sawa hakuna ubaguzi wa tajiri kupewa pana au masikini kupewa finyo!)


55.
BAHLUL KUFIKISHA SALAAM
Bahlul alipokuwa katika hali ya ufukara, basi hakuna mtu aliyekuwa akimsalimia. Lakini baada ya kipindi kupita, alijipatia mali na hivyo akawa ni miongoni mwa matajiri. Hapo kila mtu akimwona anmtolea salaam: "Bwana Bahlul Salaam ……" Basi hapo Bahlul alikuwa akiwajibu: "Ndiyo bwana, salaam zako nitazifikisha …." Na hivyo alikuwa akijiondokea. Siku moja, mtu mmoja alijikaza na kumwuliza Bahlul tafsiri ya majibu atoayo wakati anaposalimiwa. Bahlul alimwelezea : "Mimi nilipokuwa fukara, hakuna aliyekuwa akinisalimia…. Na sasa kwa kuwa nimepata mali, basi nyote mwanijia mbio kunitolea salaam…… mimi ni yule yule Bahlul, kamwe sijabadilika vyovyote vile. Hivyo ninaamini kuwa ni mali yangu ndiyo itolewayo salaam… na ndiyo maana mimi ninaporudi nyumbani mwangu huenda katika hazina ya mali yangu na kuzifikisha salaam zenu mulizonitolea." Kwa kuyasikia hayo, bwana huyo alijiondokea kimya huku akikiri aliyoyatambua Bahlul.


VITABU VILIVYOKUSANYWA NA KUTARJUMIWA NA AMIRALY M. H. DATOO
P.O. Box 838 BUKOBA TANZANIA e-mail : datooam@hotmail.com
Na unaweza kuvipata katika Internet katika :
http://www.al-islam.org/kiswahili
1. UHARAMISHO WA KAMARI
2. UHARAMISHO WA RIBA
3. UHARAMISHO WA ULEVI
4. UHARAMISHO WA ULAWITI
5. UHARAMISHO WA ZINAA
6. UHARAMISHO WA UWONGO (juzuu ya kwanza )
7. UHARAMISHO WA UWONGO (juzuu ya pili )
8. USAMEHEVU KATIKA ISLAM
9. TAJWID ILIYORAHISISHWA
10. KITABU CHA TAJWID
11. KESI YA FADAK
12. TAWBA
13. BWANA ABU TALIB a.s. MADHULUMU WA HISTORIA
14. FADHAIL ZA IMAM ALI IBN ABI TALIB a.s.
15. TADHWIN AL-HADITH
16. TAFSIRI YA JUZUU' 'AMMA
17. HUKUMU ZILIZOTOLEWA NA IMAM ALI IBN ABI TALIB a.s.
18. MSAFARA WA AL-IMAM HUSSEIN IBN 'ALI IBN ABI TALIB A.S MADINA - KARBALA
19. DALILI ZA QIYAMA NA KUDHIHIRI KWA IMAM MAHDI a.s.
20. NDOA KATIKA ISLAM
21. MAKALA MCHANGANYIKO No. 1
22. MAKALA MCHANGANYIKO No. 2
23. UWAHHABI - ASILI NA KUENEA KWAKE
24. HEKAYA ZA BAHLUL
25. SHADA LA MAUA KUTOKA BUSTANI YA AHADITH
26. HIARI NA SHURUTISHO KATIKA ISLAM
27. WAANDISHI MASHIA KATIKA SAHIH NA SUNNAHN ZA AHL SUNNA
28. USINGIZI NA NDOTO
29. MAJINA KWA AJILI YA WATOTO WAISLAMU
30. QURBAA - MAPENZI YA WANANYUMBA YA MTUME S.A.W.W.
31. TUSIUPOTEZE WAKATI
32. DHAMBI KUU LA KUTOKULIPA ZAKA, KHUMS NA SADAQAH
33. JANNAT NA JAHANNAM
34. MASIMULIZI YA HADITH KUTOKA QUR'AN
35. SADAKA
36. MKUSANYIKO WA FAHRISTI YA AYAH ZA QUR'AN