HIKAYA ZA B A H L U L MWENYE BUSARA

 

HIKAYA ZA B A H L U L MWENYE BUSARA
Kimekusanywa na kutarjumiwa na:
AMIRALY M. H. DATOO
BUKOBA - TANZANIA

Y A L I Y O M O
MANENO MAWILI ......... 3
KATIKA KUMTAARUFISHA BAHLUL 4
(1). BAHLUL NA CHAKULA CHA KHALIFA 6
(2). BAHLUL KUKALIA KITI CHA KHALIFA 6
(3). BAHLUL NA MFANYA BIASHARA 7
(4). BAHLUL AMSHAURI HARUN: 8
(5). BAHLUL NA FAQIHI 9
(6). BAHLUL NA MTUMWA ALIYEOGOPA MAJI 11
(7). SWALI KUTOKA HARUN. 12
(8). BAHLUL AUZA PEPO 12
(9). HARUN RASHID AMKASIRIKIA BAHLUL 13
(10). BAHLUL NA HARUN KWENDA KUOGA PAMOJA 14
(11). MABISHANO PAMOJA NA ABU HANIFA 15
(12). BAHLUL NA WAZIRI 16
(13). BAHLUL AMSIHI ABDULLA MUBARAK 16
(14). BAHLUL AMSIHI HARUN. 20
(15). BAHLUL AMSIHI FADHIL IBN RABI'I 21
(16). KISA CHA KUJENGA MSIKITI 23
(17). BAHLUL NA MWIZI WA VIATU. 23
(18). BAHLUL NA RAFIKI YAKE. 24
(19). BAHLUL NA MGANGA WA HARUN. 24
(20). BAHLUL AULIZWA SWALI 25
(21). SADAKA YA KHALIFA 26
(22). NEEMA BORA YA ALLAH S.W.T. 26
(23). BAHLUL NA MWIZI 27
(24). BAHLUL NA AMIR WA KUFA 28
(25). BAHLUL KUPWEWA ZAWADI 28
(26). KUATHIRI KWA DUA 29
(27). UBORA NA SIFA ZA IMAM ALI A.S. 29
(28). UTETEZI WA BAHLUL MAHAKAMANI 31
(29). MBINU ZA BAHLUL. 32
(30). HARUN RASHID NA TAPELI 33
(31). HARUN RASHID NA MVUVI. 35
(32). SWALI JUU YA AMIN NA MA'AMUN. 37
(33). BAHLUL AMJIBU KHALIFA. 39
(34). BAHLUL NA SHEIKH JUNAID 39
(35). BAHLUL NA QADHI 42
(36.). SWALI KUHUSU MTUME LUT A.S. 43
(37). SWALI KUHUSU SHEITAN 44
(38). BAHLUL NA MHUDUMU 44
(39). BAHLUL NA HARUN WAWINDA 44
(40). BAHLUL NA MWENYE NYUMBA 45
(41). KHALIFA NA ULEVI 45
(42). BAHLUL NA MNAJIMU 46
(43). BAHLUL NA KITABU CHA FALSAFIA 47
(44). KUMWELIMISHA PUNDA? 47
(45). BAHLUL NA TAPELI 48
(46). UJANJA WA BAHLUL 49
(47). UAMUZI WA BAHLUL 49
(48). BAHLUL AZURU MAKABURI 50
(49). BAHLUL NA MGENI 51
(50). BAHLUL AENDA BAFUNI 52
(51). BAHLUL NA MZOZO WA KUKU 53
(52). HARUN AJENGA JUMBA LA KIFALME 55
(53). ULIPAJI WA DENI. 55
(54). BAHLUL NA MAFUVU YA KALE 56
55. BAHLUL KUFIKISHA SALAAM 56
MANENO MAWILI ...
Katika kuona haja ya kupata nasiha na mawaidha nimeonelea vyema kutumia mbinu hii ya kuchapa nasiha na mawaidha katika sura ya hekaya za Bahlul. Kwani maisha yake yanatuchekesha na kutu furahisha papo hapo tunapata mafundisho ndani mwake. Vile vile nimekikusanya na kukitarjumu kitabu kimoja chenye masimulizi na hadithi zilizopo katika Qur'an Tukufu. Hivyo ni matumaini yangu kuwa vitabu hivi na vingine vitatusaidia sisi sote katika kulenga maisha yetu vile ipasavypo.
Amiraly M.H.Datoo 28 Safar 1423
P.O.Box 838, 11.5.2002
BUKOBA
Tanzania.

datooam@hotmail.com


KATIKA KUMTAARUFISHA BAHLUL
BAHLUL ni kumaanisha kwa ujumla wa kucheka,uwema na pendeza. Majibu haya yanaweza kuwa mafunzo kwa watu wa kila aina hadi katika zama zetu na mbeleni. Watu wengi waliweza kutokezea kwa jina hilo, lakini mashuhuri ni lile la Bahlul aliyekuwapo katika zama za Harun al-Rashid. Bahlul alikuwa ni mmoja wa wanafunzi bora wa Imam Jaafer as-Sadiq a.s. na vile vile alikuwa mpenzi wa Ahli-Bayt a.s. ya Mtume s.a.w.w. Vile vile inasemekana kuwa Bahlul alikuwa na undugu wa Harun Rashid kwa upande wa mama yake na riwaya nyingine imesemwa kuwa alikuwa jamaa wa karibu wa Harun. Qadhi Nurallah Shushtary anasema katika kitabu chake Majalis al-Muuminin Bahlul alikuwa ni mtu mwenye akili mno ambaye kwa sababu fulani fulani alijegeuza mwendawazimu. Bahlul alizaliwa Kufa na jina lake la asili lilikuwa Wahab bin Umru. Kwa mujibu wa riwaya moja, Harun Rashid alimwona Imam Musa bin Jaafer a.s. kama tishio kubwa kwa kubakia utawala wake. Hivyo alijishughulisha katika mbinu za kutaka kumwua. Na aliweza kutafuta hila moja ya kumwua. Hivyo alimzulia dai la kuasi na hivyo aliwataka hukumu wacha Mungu ya kumwua Imam, ambamo Bahlul pia alikuwamo. Wote walitoa fatwa ya kuuawa kwa Imam a.s. lakini Bahlul aliipinga. Bahlul alimwendea Imam a.s. na kumjulisha yale yaliyokuwa yakitokea, na alimwambia Imam a.s. ampatie ushauri na njia za kuyakabili hayo. Imam a.s. alimwambia kuwa ajigeuze na awe mwenda wazimu.


Hii ndiyo sababu ya yeye kuwa mwenda wazimu kwa matakwa ya Imam a.s. na hivyo aliweza kuepukana na adhabu na maangamizi ya Harun Rashid, aliyekuwa Khalifa wakati huo. Na hivyo bila ya woga wowote akijifanya mwenda wazimu, aliweza kukabili, kumsuta hata Khalifa na mawaziri wake na papo hapo aliwatetea wanyonge na wale wote waliokuwa wamedhulumiwa. Pamoja na hali yake hiyo, watu walimpenda kwa mioyo yao, hadi leo hekaya zake zinasimuliwa katika vikao na kujifunza mengi kutokana hayo. Kwa mujibu wa riwaya ya pili - ambayo inasadikiwa zaidi. Masahaba na wapenzi wa Imam a.s. walikuwa wametingwa na udhalimu wa Khalifa na watawala wake. Hivyo wote walimwomba Imam a.s. uongozi kuhusu swala hilo. Imam a.s. aliwajibu kila mmoja kwa herufi moja tu. "Jim" kwa hivyo walielewa kuwa hapakuwapo na haja ya kuulizia ziada. Kila mmoja alielewa hilo herufi tofauti tofauti. Mmoja alielewa "Jila Watan" yaani kutoka nyumbani, mwingine alielewa 'Jabl yaani 'Mlimani' na Bahlul alielewa kuwa ikimaanisha 'Junuun' Yaani "Uenda wazimu" na hivyo alijigeuza hivyo na kwa hayo, wote waliweza kunusurika na janga hilo la kuteketezwa na udhalimu wa Khalifa.


Bahlul alikuwa akiishi maisha ya starehe na bora kabisa lakini baada ya ishara hiyo ya Imam a.s. aligeuzia uso dunia na kuziacha starehe zote hivyo akaishi maisha ya utawa na akawa na mavazi yaliyokuwa yamechakaa. Yeye alipendelea kuishi uwanjani kuliko majumba ya Wafalme, vile vile aliishi kwa kipande kikavu cha mkate kuliko kutegemea misaada ya hisani ya Khalifa kwani alikuwa akijiona yu bora kuliko Khalifa Harun Rashid, mawaziri wake na Baraza lake zima. Bahlul kwa hakika, alikuwa mcha Mungu na mpenzi wake, mwenye akili sawa na Aslim kamili. Yeye alikuwa ni mtu mwenye akili sana na fahamu zaidi na mwenye kutoa majibu ya papo hapo na mtatuzi wa masuala katika zama zake. Jina lake halikuwa mashuhuri tu miongoni mwa watu wenye akili tu bali kwa amri ya Imam a.s. alijifanya mwenda wazimu na hivyo aliweza Din na Sharia na kuelezea uhakika na ukweli wa Ahli Bayt a.s. Katika zama hizo hapakuwapo na njia nyyingine ila yeye kujifanya mwenda wazimu amasivyo Harun Rashid angalimwua. Kama vile Harun Rashid alisikiliza uthibitisho wa Uimam Musa ibn Jaafer a.s. kutoka mwanafunzi mmoja wa Imam Jaafer as-Sadiq a.s. Hisham bin Hikam, na akamwambia Waziri wake Yahya ibn Khalid Barki: "Ewe Yahya! Maneno ya mtu huyu, Hisham, kwangu mimi ni sawa na tishio la mapanga laki moja, lakini jambo la kushangaza ni kule kubainika kwake hai wakati mimi natawala!" Harun alibuni kila aina ya mbinu za kutaka kumwua Hisham. Na alipopata habari hizo, alitorokea Kufa ambako aliishi nyumbani (mafichoni) mwa rafiki yake, na katika kipindi kifupi alifariki.


(1).
BAHLUL NA CHAKULA CHA KHALIFA
Siku moja Harun al-Rashid alimpelekea Bahlul sinia iliyojaa kwa vyakula mbalimbali. Mfanyakazi alipomwakilishia Bahlul vyakula hivyo, alimwambia: "Hivi ni vyakula makhususi vya Khalifa na amekutumia wewe uvile." Bahlul alimtupia mbwa aliyekuwa ameketi karibu, vyakula vyote alivyoletewa. Alipoyaona hayo, mfanyakazi wa Harun al-Rashid alighadhabika mno na kusema kuwa hiyo ilikuwa ni kumvunjia heshima Khalifa na angalimjulisha hivyo. Hapo Bahlul alimjibu: "Ewe kaa kimya! Iwapo na mbwa atafahamu kuwa vyakula hivyo vinatoka kwa Khalifa, naye pia ataacha kuvila! Fundisho: Inatupasa kukatalia zawadi kutoka kwa waonevu na wadhalimu ili visituathiri sisi kutotimiza wajibu wetu wa ukweli na haki.


(2).
BAHLUL KUKALIA KITI CHA KHALIFA
Siku moja Bahlul aliingia katika Qasri ya Khalifa na kukuta kiti chake tupu aliona hakuna mtu wa kumzuia, hivyo alikwenda moja kwa moja akaketi juu ya kiti cha Khalifa. Walipotokezea maaskari wa Khalifa, walijaribu kumwondoa Bahlul, lakini alikataa, hivyo waliweza kumwondoa kwa kumpiga. Hapo Bahlul alianza kulia kwa sauti, na alipotokea Harun Rashid alimwona Bahlul akilia kwa sauti na aliwauliza maaskari wake sababu. Wao walimwelezea yote yaliyotokea. Hapo Khalifa aliwakemea maaskari hao na kumpa pole Bahlul. Kwa hayo, Bahlul alisema: "Mimi sikililii kile kilichonipata, bali ninakulilia wewe Khalifa, kwani mimi nimeteswa kwa kuketi punde tu, je wewe utateswaje kwa kukikalia kiti hiki kwa miaka yote hiyo kwani kiti hiki cha Ukhalifa ni kwa ajili ya watu wengine na wewe umewadhulumu hao, na kukikalia kwa mabavu!"

(3).
BAHLUL NA MFANYA BIASHARA
Siku moja mfanya biashara wa Baghdad alimwendea Bahlul kwa kutaka ushauri wake. Alimwambia: "Ewe Sheikh Bahlul! Naomba ushauri wako katika ununuzi wa bidhaa ambazo zitanipatia faida nyingi." Bahlul alimjibu: "Chuma na Pamba" (mapokezi mengine yanataja tende na pamba)." Mfanyabiashara huyo aliyafuata mashauri hayo, na akapata faida kubwa sana katika kipindi kifupi. Ikatokea tena kukutana na Bahlul. Hapo alirudia ushauri wake kwa kusema: "Ewe Bahlul Mwehu! Je ninunue bidhaa zipi ili nipate faida nyingi?" Safari hii Bahlul alimjibu: "Vitunguu na matiki maji." Hapo mfanya biashara huyo alitumia fedha zake zote kwa kununulia bidhaa hizo akitarajia kupata faida zaidi. Baada ya kupita siku chache, bidhaa hizo zikaanza kuoza na hivyo kusababisha hasara kubwa mno. Hapo alitoka kumtafuta Bahlul na alipomwona alimwambia "Nilipokutaka ushauri mara ya kwanza ulinishauri kununua chuma na pamba (tende na pamba) kwa hiyo nilifaidika mno lakini mara ya pili, umenishauri kununua vitunguu na matiki maji, maboga yote yameoza kwa hivyo nimefilisika kabisa........." Bahlul alimkatiza na kumwambia "Mara ya kwanza wewe uliniita "Ewe Sheikh Bahlul!" na kwa kuwa uliniamini mimi ni mtu mwenye akili hivyo nilikupatia mashauri ya akili. Na kwa kuwa mara ya pili uliniita 'Ewe Bahlul mwehu' na kwa kuwa uliamini mimi ni mwehu, basi nilikujibu kiwehu.....!. Hapo mfanya biashara alibung'aa kwa majibu hayo na alielewa maana na kujiondokea kimya kimya. Fundisho: Islam inasisitiza ushauri kama alivyosema Mtume s.a.w.w.:- "Ushauri ni kinga dhidi ya tubu na usalama wa kutolaumiwa na watu...... na Atakaye ushauri husaidiwa......"


(4).
BAHLUL AMSHAURI HARUN:
Siku moja Bahlul alimtembelea Harun al-Rashid, na aliombwa atoe nasiha. Hapo Bahlul alianza: "Ewe Harun! Iwapo wewe utakuwapo porini ukashikwa na kiu ya maji ambayo hayapatikani, huku ukikaribia kufa. Je utalipa kiasi gani kwa kiasi cha kikombe kimoja cha maji?" "Sarafu za dhahabu (Dinar)!" alijibu Harun. "Iwapo mwenye maji asiporidhia sarafu hizo, je utampa nini badala yake?" aliendelea kusema Bahlul. "Nitampatia nusu ya dola yangu" alikatiza Harun kwa haraka. "Naam, baada ya kumalizia kiu chako, ukashindwa kupata mkojo (ukaziba) nawe usiweze kujitibu, je utampa nini yule atakaye kutibu huo ugonjwa?" Alisema Bahlul. "Nitampatia sehemu ya nusu ya dola yangu iliyobakia"Harun akanena katika hali ya bumbuwazi. Basi hapo kwa kupumua, Bahlul alisema: "Ewe Harun! Usijivunie Ukhalifa wako ambao unajua uthamini wake ni sawa na kikombe cha maji na uponyaji wa ugonwa wako. Hivyo, ni kheri yako iwapo utawatendea watu wako kwa upole na haki!"