MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

 MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMUKimeandikwa na:

Jopo la Maulamaa (Misri)

Kimetarjumiwa na:

Ustadh Abdallah Mohamed

©Haki ya kunakili imehifadhiwa na:

AL-ITRAH FOUNDATION

ISBN: 978 - 9987 - 512 - 16 - 4

Kimeandikwa na:

Jopo la maulamaa (Misri)

Kimetarjumiwa na:

Ustadh Abdallah Mohamed

Kimehaririwa na:

Hemedi Lubumba Selemani

Kimepangwa katika Kompyuta na:

Ukhti Pili Rajab

Toleo la kwanza: Mei, 2008

Nakala: 1000

Kimetolewa na kuchapishwa na:

Alitrah Foundation

S.L.P. 19701 Dar es Salaam, Tanzania

Simu: +255 22 2110640

Simu/Nukushi: +255 22 2127555

Barua Pepe: alitrah@raha.com

Tovuti: www.alitrah.org

Katika mtandao: www.alitrah.info

YALIYOMO

Mwanzo.............................................................................................2
Sehemu ya Kwanza:
Hali na haki za mtoto katika Uislam.....................................5
Mapenzi ya Mtume kwa mtoto..............................................7
Umuhimu wa mtoto katika Uislamu kabla ya kuzaliwa........8
Familia katika Uislamu..........................................................9
Pendo la wazazi...................................................................10
Usawa baina ya mtoto katika Uislamu na maoni yake juu ya
watoto wa kike.....................................................................12
Sehemu ya Pili:
Maisha na makazi ya mtoto.................................................14
Kuishi kwa mtoto.................................................................16
Jukumu la wazazi huko akhera, na mtunzo ya mtoto ........18
Jukumu la wazazi na makazi ya mtoto.............................. 20
Kuwalinda watoto ni huruma na huruma ni kinga............. 28
Uislamu na uzazi wa mpango............................................. 24
Uislamu na karantini za afya...............................................25
Sehemu ya Tatu:
Chakula bora na manufaa yake katika afya ya kimwili kiakili..........................................................................................
27
Umuhimu wa kinyonyesha kwa matiti katika Uislamu.......30
Lishe kwa akina mama waja wazito wanaonyonyesha.......33
Mchango wa chakula bora katika kukuza akili timamu..... 34
Sehemu ya Nne:
Maoni ya Uislamu juu ya malezi ya mtoto..........................38
Mtoto baina ya silika na athari na mazoea ya mazingira, na
jukumu la wazazi.................................................................39
Mwalimu aliye mfano bora, na kufundisha mtoto nidhamu..................................................................................
41
Uislamu na malezi ya kujitegemea kwa mtoto................... 42
Uislamu na kumuelimisha mtoto........................................ 44
Umuhimu wa vidude vya kuchezea watoto (toys) katika
Uislamu............................................................................... 46
Sehemu ya Tano:
Elimu ya afya, kimwili na kimazingira...............................47
Usafi wa swala.................................................................... 48
Usafi wa mikono................................................................. 49
Usafi wa kichwa..................................................................50
Usafi wa macho...................................................................50
Usafi wa Pua........................................................................50
Usafi wa mdomo (kinywa)..................................................51
Usafi wa nguo......................................................................51
Usafi wa nyumba.................................................................52
Kufanya Iktisadi katika matumizi ya maji...........................52
Usafi wa chakula na maji.....................................................53
Makatazo ya kwenda haja ndogo kwenye maji yaliyotulia.........................................................................................
53
Makatazo ya kukojoa majabalini na maweni.......................53
Mambo matatu yaliyolaaniwa........................................ .....54
Usafi wa barabara............................................................... 54NENO LA MCHAPISHAJI
Kitabu ulichonacho mikononi mwako asili yake kimeandikwa kwa Kiingereza na jopo la maulamaa wa Misri kwa jina la Child Care in Islam. Sisi tumekiita, Malezi ya Watoto katika Uislamu. Kama inavyofahamika kwamba Uislamu ni dini na ni mfumo wa maisha, basi mafundisho yake hayakuacha kitu kinachohusiana na maisha ya mwanadamu - kuanzia tumboni mwa mama yake, kuzaliwa kwake, kunyonya na kulikizwa kwake, kufunzwa mambo ya kimsingi na mama yake, mpaka kufikia kimo cha kwenda shuleni. Haya yameelezwa kwa utaratibu mzuri sana kutoka kwenye vyanzo viwili vikubwa vya sheria ya Kiislamu - Qur'ani na Sunna.


Kwa mujibu wa Uislamu kipindi cha mafunzo ya watoto huanza wakati mwanaume na mwanamke wanapoingia katika ushirika wa ndoa, kama wazazi wa baadaye, ni lazima wajihisi kwamba wana wajibu wa kuwalea watoto wao. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za kurithi (tabia), mwenendo wote wa tabia nzuri na mbaya wa wazazi hurithiwa na watoto wa wazazi hao. Hivyo, mzazi akiwa na tabia nzuri atawarithisha watoto wake tabia hiyo, na ni kwa sababu hii mafunzo ya watoto huanzia punde tu wakati mume na mke wanapoingia katika ndoa. Ili kufanikisha somo la kitabu hiki, jopo hilo la maulamaa limerejea sana kwenye vyanzo hivyo viwili - Qur'ani na Sunna. Watoto ni taifa la kesho, na ili kuwa na taifa zuri lenye maadili mema, lazima kuwalea watoto katika mazingira mazuri ya kimaadili; na ni mafunzo ya Kiislamu tu, kama yatafundishwa vizuri na kuzingatiwa basi Umma utaondokana na matatizo mengi ya kijamii kama inavyoonekana hivi sasa.


Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan katika wakati huu ambapo jamii inazidi kudidimia katika maovu kutokana na kumomonyoka kwa maadili mema. Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili. Tunamshukuru ndugu yetu A. Mohamed kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha uchapishaji kitabu hiki.


Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.
Malezi ya Watoto katika Uislamu
Mwanzo
Qur’ani tukufu na Hadith, ndivyo vitu viwili vya kimsingi ambavyo vinaunda Sheria za Kiislamu na kuzihakikisha, na ni kutokana na vitu viwili hivyo ndipo misingi yote ya dini inaporejea. Hata hivyo, ni Qur’ani tukufu tu ndiyo marejeo makubwa ambayo Hadith zinategemea. Kwa ajili hiyo, Hadith hazitofautiani au kupingana na Qur’ani ambayo inaaminiwa kuwa ndiyo asili ya ukweli wote. Miongoni mwa maudhui yenye maana sana ya Qur’ani tukufu, ni kuwa inaeleza kanuni na Sheria zote za mwanzo kusaidia watu ili waweze kupanga vizuri maisha yao, na hivyo kuweza kubadilisha desturi zilizokuwa zikifuatwa.Kwa maana hiyo Qur’ani imehifadhi haki za kila mmoja, na za jamii, imefanya kuenea kwa uadilifu, imewapa watu moyo wa kuishi pamoja kwa ushirikiano na ihsani, na imeweka kipimo cha kumcha Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo tofauti pekee baina ya watu. Hadith ni chochote kile ambacho Mtume (s.a.w.w.) amekitenda na ambacho si Qur’ani; au mambo ambayo yamemfikia kupitia kwa ufahamu wake au maono, na kuthibitishwa na Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo (Sunnah) inakusanya vitendo na maneno yanayohusika na ufafanuzi wa itikadi, Swala au ibada nyinginezo, pia kulingana na uhusiano mwema baina ya ndugu, kumfundisha mwenendo mzuri, na kuamrisha mambo mema na kukataza maovu.


Kwa hivyo chochote kilichotendwa na Mtume (s.a.w.) katika hali kama hiyo, huchukuliwa kama sunnah, na watu wanatakiwa kukifuata. Chochote kile ambacho hakihusiani na hayo yaliyotajwa hapo awali, kama vile kula, kunywa, au kuvaa nguo, hakichukuliwi kuwa ni sunnah, na watu hawalazimiki kukifuata.


Malezi ya Watoto katika Uislamu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Hakika mimi ni mwanaadamu, pindi nitakapowaamrisha jambo linalohusiana na dini yenu, lifuateni, na nitakapowaamrisha jambo kutokana na maoni yangu, basi kumbukeni kuwa mimi ni mwanaadamu.” Ushahidi wa jambo hili ni ushauri ambao Mtume (s.a.w.) alizoea kuutoa kuhusiana na kutafuta tiba ya baadhi ya maradhi. Ushauri ambao hakuletewa wahyi ila ni kutokana na uzoefu alioupata kutokana na kuishi katika mazingira ya kibinaadamu.


Ametaja Abu Daud katika Isnadi yake, kutoka kwa Usama kwamba: “Nilikwenda kwa Mtume (s.a.w.) naye alikuwa ameketi na maswahaba zake, nao walikuwa (wametulia) kama kwamba kuna ndege juu ya vichwa vyao, nikawatolea salaam, kisha nikaketi. Wakaja mabedui kutoka huku na huko wakasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je tunaweza kujitibu?” Mtume (s.a.w.) akasema: “Mnaweza kujitibu, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuumba ugonjwa pekee ila ameumba na dawa yake, isipokuwa ugonjwa wa aina moja tu, kifo.” Hadith nyingine iliyopokewa kutoka kwa Umar Bin Dinar imetaja jambo hilo (pia).


Siku moja Mtume (s.a.w.) alimtembelea mgonjwa, akawaambia nduguze, “Mwiteni daktari,” mmoja wao akasema, “hata nawe pia wasema hivyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?!” Mtume akasema: “Ndiyo, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuumba maradhi ila ameumba na dawa yake.” Kitendo cha Mtume (s.a.w.) cha kuwataka ndugu za wagonjwa kumwita daktari kinaonyesha kwamba utabibu wa madawa si miongoni mwa


mambo aliyofunuliwa (wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na ni kwa sababu hii ndipo akawashauri watu kufuata ushauri wa daktari pale unapohitajika. Pia hali hiyo inahusiana na jinsi alivyokuwa akivaa na kula, ilivyokuwa ikilingana na tabia za wakati wake na mahali alipoishi. Na lau kama angeishi katika mazingira na wakati tofauti, basi pengine angestawisha desturi zingine.


Kwa hivyo basi, Sunnah (Hadith) inafafanua Qur’ani, inachambua hukmu zake, inaikamilisha, inaelezea na kuamua kuhusu mipaka ambayo inatawala kanuni zake kamili, na inafafanua sehemu zenye kutatanisha. Na endapo itaongezea chochote, ziada hiyo haiwezi kupingana na misingi ya kanuni za Qur’ani. Kwa hivyo uhusiano wa Sunnah na Qur’ani ulivyo ni kama hali ya kiongozi na mfuasi. Kwa ajili hiyo, Hadith inafuata kile kilichokuja katika Qur’ani na inaambatana nayo moja kwa moja. Inadhihirika wazi sasa, kwa nini Qur’ani inatangulia Sunnah, na kuchukuliwa kuwa ni msingi wa Uislamu, wakati ambapo Sunnah inaikamilisha Qur’ani kwa kanuni.


Mkusanyiko huu (wa kitabu hiki kinachohusu malezi ya mtoto) umetokana na yale yaliyotajwa katika Qur’ani yahusuyo malezi ya mtoto, na katika Sunnah kuhusiana na mambo haya. Ili kutoa mwanga, habari zaidi na ufafanuzi uliyomo katika Qur’ani, baadhi ya methali na dondoo maarufu zimeongezwa ili ziwe ni mifano mizuri na yenye nguvu zaidi.

SEHEMU YAKWANZA
Hali na haki za mtoto katika Uislamu Hawa ni watoto wetu kwetu sisi wenye hadhi Ni kama maini yetu yaendayo kwenye ardhi Na tulivyo kati yetu hatuwezi kuwa radhi Tuwaonapo wanetu wanaugua maradhi (Tafsiri ya shairi la kale la kiarabu) Umoja wa mataifa umeanza kuonyesha kuvutiwa na suala la watoto kwa kufanya maadhimisho ya ‘Siku ya Watoto’ katika mwezi wa Novemba kila mwaka, ambayo inalingana na maadhimisho ya kutangazwa kwa haki za mtoto.


Kwa hali yoyote ile, ipo haja ya kutaja hapa kwamba, mazingatio ya Uislamu kwa watoto yameanza zamani na yanarejea nyuma zaidi ya miaka elfu moja na mia nne. Uislamu kwa mfululizo unaadhimisha na kuonyesha huruma yake kwa mtoto, si baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla ya kuzaliwa, na umeelezewa kwa makini haki zake. Wakati wa utoto katika Uislamu umepewa picha ya ulimwengu mzuri wa furaha, uzuri, ndoto, mapenzi na ruya njema. Na aya za Qur’ani zinaonyesha mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa watoto, na ndipo akaapa Mwenyezi Mungu: “Naapa kwa mji huu, (wa Makkah). Na wewe utahalalishwa katika mji huu. Na (kwa) mzazi na alichokizaa.” (90:1-3).


Watoto wameelezwa katika Qur’ani kuwa ni bishara njema. Amesema Mwenyezi Mungu: “Ewe Zakaria tunakupa habari njema ya (kupata) mtoto jina lake ni Yahya….” (19:7). Pia watoto ni kiburudisho cha macho yetu. Amesema Mwenyezi Mungu: “Ewe Mola wetu, tupe katika wake zetu na watoto wetu watakaoyaburudisha macho yetu….”(25:74). Na watoto ni pambo la maisha katika ulimwengu huu. “Mali na watoto ni pambo la maisha ya duniani….” (18:16). Mtume (s.a.w.) anatudhihirishia ya kuwa ulimwengu wa utoto ni kama pepo, pale aliposema: “Watoto ni vipepeo vya Peponi.”


Kuwatunza watoto ni jambo la lazima, na kuwapenda humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Lau kama si watoto wanyonyeshwao, na wazee wanaorukuu (kwa kuswali) na wanyama walishwao mashambani, basi mngelipatwa na adhabu kali.” Inaonyesha wazi kwamba huruma na uangalifu wa Mwenyezi Mungu kwa watoto ndiyo uliofanya Mwenyezi Mungu kuzuia adhabu juu ya watu wake.


Mapenzi ya Mtume kwa watoto Mapenzi ya Mtume (s.a.w.) kwa watoto yalijaa ndani ya moyo wake mwema, imeelezwa katika Hadith: “Siku moja Mtume (s.a.w.) alipanda juu ya mimbari akiwahutubia watu, (mara) akawaona Hasan na Husein (a.s.) wanakimbia na huku wakijikwaa, akakatiza hotuba yake, akashuka kutoka juu ya mimbari kwenda kuwapokea watoto hao wawili. Akawabeba mikononi mwake, kisha akapanda tena juu ya mimbari akasema: “Enyi watu, hakika mali zenu na watoto wenu ni fitina, Wallahi nimewaona wajukuu zangu wawili wakikimbia na kujikwaa, basi sikuweza kujizuia mpaka nimeshuka nikawabeba.” Siku moja Mtume (s.a.w.) alikuwa anaswali, mara Hasan na Husein (a.s.) wakaingia ndani na kumpanda mgongoni kwake wakati alipokuwa amesujudu, Mtume (s.a.w.) akaendelea kusujudu tu. Alichukia kuwaharakisha washuke, mpaka waliposhuka wao wenyewe. Kisha alipotoa salaam na kumaliza Swala, akaulizwa na maswahaba zake sababu zilizomfanya asujudu kwa kitambo kirefu hivyo; akawajibu: “Wajukuu zangu wawili walikuwa wamepanda juu ya mgongo wangu nami nilichukia kuwahimiza washuke kwa haraka.”


Mtume (s.a.w.) alizoea kuharakisha Swala yake pindi asikiapo mtoto analia, na husema: “Mimi huchukia kumchosha mama yake.” Siku moja alikuwa anapita nyumbani kwa Fatima (a.s.) (binti yake), akamsikia mjukuu wake Husein (a.s.) akilia, aliingia ndani na baada ya kumkemea Fatima akasema: “Je hujui kwamba nimsikiapo Husein akilia huwa nakereka?” Siku moja Mtume (s.a.w.) alitembelewa na Al-Akraa Ibn Habis, ambaye alimwona Mtume (s.a.w.) akiwabusu wajukuu zake, Al-Akraa akasema: “Unawabusu watoto wa binti yako? Naapa kwa Mungu nina watoto kumi,

Malezi ya Watoto katika Uislamu na sijawahi kumbusu hata mmoja.” Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Je ni kosa langu kama Mwenyezi Mungu ameing’oa rehma kutoka moyoni mwako.” 2. Umuhimu wa mtoto katika Uislamu kabla ya kuzaliwa Kutilia maanani kwa Uislamu kuhusu malezi ya mtoto hakuanzi baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla hajaanza kupata umbo (tumboni) kwani Uislamu unamuamuru mtu kuoa mke mcha Mungu na mtulivu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Jitahidi umpate mwenye kushikamana na dini, basi furaha zote ni zako.” Uzuri, na utajiri si sifa pekee za kutosha kuchagua mke, sambamba na sifa hizo, pia mke ni lazima awe na sifa zingine, kwa mfano kumpata aliye na dini, na awe ametoka kwenye nyumba yenye mema. Kwa sababu watoto wake atakaowazaa mke huyo watarithi tabia, adabu na mwenendo wake. Mwenyezi Mungu amekataza kuoa mwanamke mzuri tu asiye na tabia nzuri na nidhamu. Mtume (s.a.w.) amekataza: “Jihadharini na wanawake wazuri wenye sifa mbaya.”


Mtume (s.a.w.) ameweka mwongozo kwa mwanamke ambaye yu tayari kuolewa: atafute mume mcha Mungu, mwenye tabia za kidini, atakayeangalia jamii yake kwa ukamilifu, kutekeleza haki za mke, na kusimamia malezi ya watoto. Mtume (s.a.w.) amesema: “Atakapowajia mtu mtakayeridhishwa na jinsi alivyoshika dini, na tabia yake, basi muozeni, ama msipofanya hivyo, mtaleta fitina na ufisadi mkubwa duniani.” Mtume (s.a.w.) ameonya pia kuhusu kuoana na ndugu wa karibu, ili watoto wasizaliwe wadhaifu, akasema: “Oeni walio nje ya jamii yenu, msiwadhoofishe watoto wenu.”


Qur’ani imetaja ya kwamba, mwanadamu ameumbwa kutokana na tone la manii lililochanganyika: “Hakika tumemuumba mwanadamu kutokana na tone la manii lililochanganyika…” (76:2). Hii inaonyesha kwamba, mtoto azaliwaye na wazazi ambao si ndugu wa karibu atakuwa na uwerevu, utambuzi na mwenye nguvu za kimwili kuliko mtoto aliyezaliwa na wazazi wenye uhusiano wa karibu. Hii inaweza kuonekana kwamba Uislamu umezitangulia (kwa uvumbuzi) kanuni za kisayansi na elimu ya ‘tabia zinazorithishwa’ (Heredity) kwa kuonyesha umuhimu ulioko katika sehemu ya urithi wa tabia, na namna gani uteuzi mzuri wa watu wawili wanaooana utakavyopelekea kupata watoto ambao ni tuzo la Mwenyezi Mungu na furaha ya maisha.


Kwa kuwa mtoto atachukua mwenendo wa wajomba na shangazi zake, asili ya undani ya baba yake na mama yake, na akajifunza kupitia kwa urathi ambao umepitia kutokana kwa muungano wa baba yake na mama yake, na ndipo Uislamu ukazitengeneza asili hizi kwa njia hiyo ili kumhifadhi mtoto awe ni kiumbe mwenye heshima na nidhamu, na hivyo kuepukana na upungufu wowote. Mara tu mtu anapoanza kufikiria kuoa na kutunza familia, Uislamu unamuongoza kupitia katika njia hizo.


3. Familia katika Uislamu Familia katika Uislamu, ina utaratibu mzuri na wa hali ya juu sana, na ni utaratibu unaoheshimiwa sana hata ina mahali panapostahiwa. Ni kwa sababu hii na ndio maana Uislamu huipa nguvu (familia) kuanzia mwanzo wa nguvu yake. Ndoa ni sura mpya katika njia ya kuunda jamii, na uangalifu wa Uislamu katika nguzo hiyo muhimu, hatimaye unaongoza kuelekea katika maisha ya amani na furaha.


4. Pendo la wazazi Mtoto ni matokeo ya kimaumbile ya uhusiano imara wa wazazi, ubaba na umama ni matamko mawili ambayo Mwenyezi Mungu ameyazatiti kwa ihsani na mapenzi Yake, akayatajirisha na kuyapitia kwa maana ya kuungana watu wawili na kuendelea kuwa pamoja. Uhusiano wa karibu zaidi baina ya wazazi na watoto wao, ni miongoni mwa uhusiano ulio imara na wenye daraja ya juu zaidi kuliko uhusiano wowote ule wa kibinaadamu. Uhusiano huo umehifadhiwa na Mwenyezi Mungu, naye amehakikisha kuwa unaendelea na kustawi; kwa sababu kufanya hivyo ni kuendelea kwa jamii ya binaadamu na uhai. Upendo wa wazazi kwa watoto wao hauna nafasi yoyote ya kutia shaka, kwani ni alama ya Mwenyezi Mungu na ni neema Yake kubwa kwa walimwengu. Mwenyezi Mungu amesema: “Na katika alama zake, ni huku kuwaumbia wake zenu, kutoka miongoni mwenu ili mpate utulivu kwao, na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu.” (30:21). Baadhi ya wafasiri wameeleza ‘penzi’ na ‘huruma’ hapa, kwa maana ya mtoto ambaye ameupa nguvu uhusiano baina ya wazazi na ameupa amani na usalama.


Familia ndicho kitu cha kwanza ambacho Uislamu unakichukulia kuwa ni cha kwanza katika jamii ya watu. Familia huunda nyoyoni mwao penzi lisilo na kikomo kwa watoto wao, penzi hili ni nuru waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) aliwaambia maswahaba zake na huku akiwaonyesha mwanamke akasema: “Je Mnaweza kufikiria kwamba siku moja mwanamke huyu anaweza kumtupa mwanawe motoni?” Wao wakasema: “La”, akasema: “Basi Mwenyezi Mungu ni mwenye huruma zaidi kwa waja wake kuliko mama huyu alivyo na huruma kwa mtoto wake.” Basi haya ni maumbile, na ni aina ya pendo la kiasili ambalo hapana yeyote awezaye kulizuia au kushindana nalo, na kwa sababu hii ndipo Mwenyezi Mungu akawausia wazazi kuwaangalia watoto wao. Amesema: “Na tumemuusia mwanaadamu (kuwafanyia wema) wazazi wake, mama ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumnyonyesha na kumwachisha kunyonya katika miaka miwili, nishukuru Mimi na wazazi wako na kwangu ndio marejeo.”(31:14). Amesema tena:


“Na tumemuuusia mwanaadamu kuwatendea wema wazazi wake. Mama yake ameichukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu. Na kubeba mimba yake (mpaka) kumwachisha kunyonya ni miezi thelathini mpaka anapofikia kubaleghe kwake, na akafikia miaka arubaini. Akasema: ‘Ewe Mola wangu niwezeshe nizishukuru neema zako ambazo umenineemesha mimi na wazazi wangu. Na uniwezeshe nifanye amali njema uzipendazo, na unitengenezee watoto wangu. Kwa hakika natubu kwako, kwa hakika mimi ni miongoni mwa waislamu.’” (46:15). Mwenyezi Mungu amefanya kuwapenda watoto na kuwahurumia ni sehemu ya maumbile ya kiasili ya kibinaadamu yasioepukika. Pia ameziingiza hisia hizi thabiti ndani ya nyoyo za wazazi. Ni kwa ajili hii basi ndipo maelezo haya yote pamoja na wasia yameelekezwa moja kwa moja kwa watoto, kwa ajili ya kuwatendea wema na kuwapa heshima wazazi wao. Maelekezo haya amepewa mtoto ili kuzivutia hisia zake.


Ni maelekezo ya hali ya juu ambayo yanategemeza uhusiano wa karibu na hisia ya kibinaadamu ambazo ndio sababu kubwa ya kuwepo kwetu duniani.
5. Usawa baina ya watoto katika Uislamu na maoni yake juu ya watoto wa kike Kadri Uislamu unavyochukulia watoto kuwa ni kiburudisho cha macho yetu, ni lazima hii idhihiri kwa vitendo na kwa njia zake. Usawa baina ya watoto hauna budi kutekelezwa hata katika kuwabusu. Uislamu unataka usawa ufanywe kulingana na maagizo yake matukufu.


Siku moja Mtume (s.a.w.) alimwona baba ambaye alikuwa na watoto waw- ili, akambusu mmoja na kumwacha mwingine, kisha Mtume mtukufu akamuuliza: “Je huwezi kuwafanyia usawa?” Tukiangalia mvuto wa kumpendelea mtoto mmoja zaidi ya mwingine au jinsia moja (wa kike au wa kiume) zaidi ya nyingine, hii ni kinyume kabisa na maadili ya kiislamu, mila na fikra za usawa ambazo Uislamu umejengewa. Uislamu hautofautishi baina ya mwanamume na mwanamke, wala hautofautishi baina ya mvulana na msichana. Wote sawa, hapana yeyote ampitaye mwenzake ila kutokana na baadhi ya sifa alizonazo kitabia alizojipatia yeye mwenyewe, Mwenyezi Mungu amesema: “Mola akawakubalia (maombi yao), ya kwamba mimi sipotezi amali ya mwenye kutenda, awe ni mwanamume au mwanamke, baadhi yenu kwa baadhi nyingine….”(3:195).


Kwenda kinyume na misingi hii kunafuatia kwenda kinyume na fikra za usawa, maarifa, na haki. Kwa ajili hii, Uislamu unawaamuru Waislamu kuwafanyia usawa watoto wao ili kwamba kusiwe na yeyote yule atakayekuwa na kinyongo au kusononeka. Kwa njia kama hiyo, Uislamu unazuia kuzagaa kwa chuki badala ya mapenzi, na kusema maudhi badala ya amani. Mambo haya iwapo yataendelea, hatimaye yataleta matatizo ya kinafsi, majonzi, na utengano, na haya yote huvunja hisia za moyo. Mtume (s.a.w.) mara kwa mara alikataza kuwapendelea watoto wa kiume zaidi ya wa kike pasi na sababu yoyote, kwa maana hiyo, ndiyo akaipa daraja la juu heshima ya watoto wa kike na akaipa nguvu thamani na staha yao.


Amesema Mtume (s.a.w.): “Bora ya watoto wenu ni mabinti.” Mtume (s.a.w.) alipopewa habari ya kuzaliwa bintiye Fatima (a.s.), nyuso za maswahaba zilionekana kuparama, Mtume (s.a.w.) akawaambia: “Mna jambo gani linalowahuzunisha? (kumzaa Fatima) ni kama kupata ua la mrehani niunusao, na riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu.” Hapa Mtume (s.a.w.) kwa ubaba wake mtukufu alijaribu kubadilisha mawazo ya watu ya kuwapendelea watoto wa kiume zaidi ya watoto wa kike, tena hata aliwatanguliza watoto wa kike zaidi kwa kusema: “Mwenye kwenda sokoni, na kununua zawadi na kuwapelekea jamii yake, (familia yake) ni kama mtu aliyewapelekea sadaka wahitaji, basi aanze kuwapatia watoto wa kike kabla ya kiume.”Mtume (s.a.w.) amejaribu kwa kadri awezavyo kuvutia penzi la watoto wa kike kama vile lilivyo penzi la asili kwa watoto wa kiume. Amesema: “Mwenye kuwalisha (kuwalea) watoto watatu wa kike ataingia Peponi.” Akaulizwa: “Je wakiwa ni wawili?”, akajibu: “Hata kama wawili”, Akaulizwa: “Je mmoja”, akajibu: “Hata kama ni moja.”