WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Mama Aisha aliacha huru watumwa arobaini kwa ajili ya kutoa kafara ya kuvunja kiapo chake
Je, ikoje daraja ya Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa mkewe Aisha ambaye alitoa kafara ya kutengua kiapo pale alipowapa uhuru watumwa arobaini. Hivi yeye bibi Aisha ni mcha Mungu mno kuliko Mtume wa Mwenyezi Mungu? Bukhari ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul-adab, Babul-hijrah waqaulu Rasulillahi (s.a.w.w.) La yahillu lirajulin an yahjura akha-hu fauqa thalathi. Kwamba Aisha alisimuliwa ya kuwa Abdallah ibn Zubair alisema kuhusu kitu fulani alichonunua au alichopewa na Aisha: "Wallahi Aisha akome au sivyo nitamdhiki." Basi Aisha akasema "Je, ni yeye (Abdallah ibn Zubair) ndiye aliyesema hivi?'' Watu wakasema: "Ndiyo" Aisha akasema: "Basi naweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu sitamsemesha kamwe mwana wa Zubair."

Ibn Zubair akawaomba (watu) waingilie kati kuwapatanisha yeye na bibi Aisha baada ya muda mrefu wa kususiana. Aisha akasema: "Wallahi sipatani naye kamwe, na wala sivunji nadhiri yangu." Basi hali hiyo ilipochukua muda mrefu kwa Ibn Zubair. aliwazungumza Mis-war ibn Makrimah na Abdur-rahman ibn Al-as-wad ibn Abdi Yaghuth, hawa ni miongoni mwa bani Zuhrah akawaambia,"Nakuapieni Mwenyezi Mungu, nawaombeni kwa haki ya Mwenyezi Mungu muniingize nyumbani mwa bibi Aisha, kwani si halali kwake kuweka nadhiri ya kuninunia." Ms-war na Abdur-rahman wakaenda naye hali ya kuwa wamejifunika shuka wakapiga hodi kwa bibi Aisha wakasema, "Amani iwe juu yako na rehma za Mwenyezi Mungu na baraka zake, je, tuingie?" Bibi Aisha akasema, "Ingieni." Wakasema: "Sote?" Akasema, "Ndiyo ingieni nyote." Lakini alikuwa hajui kwamba Ibn Zubair yuko pamoja nao.


Walipoingia Ibn Zubair naye akaingia na akapita kvvenye pazia na akamkumbatia Aisha, akawa anamnasihi bibi Aisha na huku analia naye Mis-war na Abdur-rahman wakawa wanarnnasihi bibi Aisha mpaka amkubalie na kumsemesha Ibn Zubair, na wakasema, "Hakika Mtume (s.a.w.w.) amekataza kususiana jambo ambalo unalifahamu, kwani haifai kwa Muislamu kumsusia nduguye zaidi ya siku tatu." Basi walipomkazania bibi Aisha kumkumbusha na kumuonya, akawa naye huwakumbusha huku akilia akasema, "Hakika mimi niliweka nadhiri, na nadhiri ni jambo zito, basi nao hawakumuachia mpaka akamsemesha Ibn Zubair, na kutokana na nadhiri yake aliachia huru watumwa arobaini, na aliendelea kuikumbuka nadhiri yake baada ya hapo, basi hulia mpaka machozi yake yanalowesha ushungi wake."


Pamoja na kwamba kiapo cha bibi Aisha hakijuzu kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) ameharamisha kwa Muislamu kumsusia nduguye zaidi ya siku tatu, lakini yeye bibi Aisha hakukubali ila atoe kafara ya kiapo chake kwa kuwaachia huru watumwa arobaini. Jambo hili pia linatujulisha dalili nyingine kwamba bibi Aisha peke yake alikuwa ni dola tosha kabisa, vinginevyo vipi bibi Aisha aweze kumiliki watumwa arobaini au thamani yake? Jambo hilo siyo jepesi, na wala historia haikusajili kwamba Mtume (s.a.w.w.) alipata kuacha huru watuniwa kwa idadi kubwa kama hii katika uhai wake wote. Kwa hakika jamaa hawa hawakuacha ovu au kasoro yoyote ile isipokuwa walimpachika nayo Mtume, na yote hayo ni kwa kutaka kuyahalalisha matendo ya viongozi wao. Mwenyezi Mungu awalaani, ni wapi wanakoelekezwa? Na katika kuhalalisha kupuuza kwao hukumu za kisheria tazama maelezo yafuatayo:-

(Eti) Mtume anaziacha hukmu za Mwenyezi Mungu wakati wowote akipenda Suala hili ni kama alivyoliandika Bukhari ndani ya sahih yake katika Kitabul-aiman wan-nudhur, mlango wa kutenda dhambi kwa kusahau. Imepokewa kutoka kwa A'taa, kutoka kwa ibn Abbas (r.a.) amesema: "Mtu mmoja alimwambia Mtume (s.a.w.w.) nimezuru kabla ya kupiga." (Yaani nimetufu nyumba tawafu ya ziyarah) Mtume akasema: "Si vibaya." "Nimenyoa kabla ya kuchinja." Mtume akasema: "Hapana ubaya." Mwingine naye akasema: ."Nimechinja kabla ya kupiga." Mtume akasema "Hakuna ubaya."


Na imepokewa kutoka kwa Abdallah ibn Amr ibn Al-'as kwamba, Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akihutubu siku ya kumi ya mfunguo tatu, kuna mtu fulani alisimama akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi nilikuwa nikidhania kadhaa wa kadhaa kabla kadhaa wa kadhaa (yaani nilikuwa nikidhania namna fulani kabla ya kufanya namna fulani), kisha mtu mwingine akasimama akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi nilikuwa nikidhania kadhaa wa kadhaa juu ya mambo haya matatu (kunyoa, kuchinja na kupiga)." Mtume akasema, "Fanya tu hapana ubaya kwa yote hayo kwenye kipindi hicho." Basi Mtume hakuulizwa chochote siku hizo ila alisema, "Fanya, fanya tu wala hakuna ubaya." Cha kushangaza utaposoma riwaya hizi hali ya kuwa unazipinga utaona baadhi ya wanaopinga ukweli wanakukabili kwa kusema kuwa, "Dini ya Mwenyezi Mungu ni nyepesi wala haina uzito na kwamba Mtume (s.a.w.w.) amesema, "Fanyeni wepesi msifanye uzito (katika dini)."


Bila shaka maneno haya ni sahihi lakini lengo lake ni siyo sahihi, kwani hapana shaka yoyote kuwa, Mwenyezi Mungu anatutakia wepesi wala hatutakii uzito na wala hakufanya juu yetu uzito wowote ndani ya dini, lakini siyo kwa yale aliyokwisha kuyapitisha na kutuwekea kuwa miongoni mwa hukumu na mipaka kupitia Qur'an Tukufu na Sunna Tukufu ya Mtume, si hivyo tu bali ametupatia ruhusa ya lazima kila hali inapobidi (yaani tukikosa uwezo wa kuyatenda). Miongoni mwa mambo hayo ni kama vile kutayammam pindi maji yanapokosekana au kuchelea ubaridi wa maji, na kama vile kusali kwa kukaa inapobidi na kula mchana wa Ramadhani, kupunguza sala safarini, yote haya ni sahihi. Lakini siyo kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, kwa mfano kuufanya utaratibu wa udhu au kutayammam kama tunavyotaka tukakosha mikono miwili kabla ya kukosha uso, au tukapaka miguu miwili kabla ya kupaka kichwa, namna hii haifai.


Lakini wazushi walitaka kumdharaulisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa kila kitu, ili tu wapate njia (ya kufanya wapendavyo) kama wasemavyo watu wengi leo hii (ikiwa utawahoji) watasema, "Hiyo siyo juu yako bwana, la muhimu ni kusali tu, wewe sali upendavyo." Na cha kushangaza (zaidi) ni kwamba, Bukhari mwenyewe anathibitisha katika ukurasa huo huo ambao iko hiyo (isemwayo kuwa ni) kauli ya Mtume, (Fanya, fanya tu na wala hakuna ubaya)!! Yeye anathibitisha tukio ambalo ndani yake inadhihirika kuwa Mtume (s.a.w.w.) ni mwenye kutilia mkazo sana mipaka (ya Mwenyezi Mungu). Amesema: Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah ya kwamba, mtu mmoja aliingia msikitini kuswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akiwa upande fulani ndani ya msikiti, akaja yule mtu akamsalimia Mtume, Mtume akamwambia rudi kaswali tena kwani wewe hujasali, yule mtu akarudi akasali kisha akamsalimia Mtume, naye akamjibu, Mtume akamwambia rudi ukasali kwani bado hujasali. Basi yule mtu akairejea ile sala mara tatu na kila mara Mtume humwambia, "Rudi kasali kwani hujasali." Basi yule mtu akamwambia Mtume, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nifundishe." Mtume akamfundisha kutulizana katika rukuu na kutulizana katika sijda. Mtume akasema, "Kisha urukuu mpaka utulie hali ya kuwa umerukuu, halafu nyanyua kichwa chako mpaka usimame wima sawa sawa, kisha usujudu mpaka utulie hali ya kuwa umesujudu, kisha nyanyuka na utulie sawasawa hali ya kuwa umekaa, halafu sujudu mpaka utulizane hali ya kuwa umesujudu kisha nyanyuka mpaka usimame sawa sawa kisha fanya hivyo katika sala yako yote."Kama ambavyo Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, kaika Kitabut-tauhid Babu Qaulillah A 'zza wa Jalla Faqrauu ma-tayassara minal-Qur'an. Imepokewa kutoka kwa Umar ibn Khatab anasema: "Nilimsikia Hisham bin Hakim anasoma Suratul-fur-qan katika zama za uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), basi nikamsikiliza kisomo chake, mara ghafla akawa anasoma herufi nyingi ambazo Mtume hakunisomesha, basi karibu nimshambulie ndani ya sala, nikavumilia mpaka akatoa salamu nikamvuta nguo yake nikasema, nani aliyekusomesha sura hii niliyokusikia unaisoma? Akasema: Amenisomesha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), nikasema, muongo wewe, mimi amenisomesha kinyume cha ulivyosoma wewe.

Basi nikamburura hali ya kuwa nimemtanguliza mpaka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), nikasema, Bila shaka nimemsikia huyu anasoma Suratul-furqan kwa herufi ambazo mimi hukunisomesha. Mtume akasema, "Mwachilie (kwanza), ewe Hisham hebu soma.'' Basi akasoma kisomo nilichomsikia akikisoma. Mtume akasema: "Hivyo ndiyo ilivyoteremshwa." Kisha Mtume akasema, Ewe Umar (hebu nawe) soma, Nikamsomea kisomo alichonisomesha, Mtume akasema: "Hivyo ndivyo ilivyoteremshwa, hakika hii Qur'an imeshushwa kwa aina ya visomo saba, nanyi someni kilicho chepesi." Basi hivi baada ya riwaya hii kunabakia shaka yoyote kwamba wazushi hao walivuka mpaka katika kuchafua heshima ya Mtume (s.a.w.w.) hadi upande wa Qur'an Tukufu na eti Mtume aliwafundisha Masahaba visomo vinavyohitilafiana na anawaambia kila mmoja wao kuwa hivyo ndivyo ilivyoshuka? Na lau kisomo kile kingekuwa na hitilafu isiyo kubwa, basi Umar asingekurubia kuikata sala ya Hishamu na kumkemea.


Jambo hili linanikumbusha wanachuoni wa Kisunni ambao wanang'ang'ania kisomo maalum, hawakubali kwa mtu yoyote kusoma kinyume cha vile wanavyofahamu wao. Siku moja nilikuwa nasoma: Udhkuru ni'imatii al-latii an-a'mtu alaikum. Basi mmoja wao alinikemea kwa nguvu na akapiga kelele akisema, "Usiiponde Qur'an kama hujuwi kusoma." Nikasema: "Nimeiponda vipi?" Akasema: "Udhkuruu ni 'imatiya, sio Udhkuruu ni 'imati'!! Kama ambavyo Bukhari amethibitisha ndani ya sahih yake, Kitabul-istiqradh wa Adaid-dain, Babul khusumat, juzuu ya tatu ukurasa wa 88. Imepokewa kutoka kwa Abdil-malik ibn Maisarah amenieleza amesema, Nilimsikia An-nizzal, nilimsikia Abdallah anasema: "'Nilimsikia akisoma aya fulani ambayo mimi niliisikia kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) kinyume cha hivyo, basi nikamshika mkono nikampeleka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mtume akasema: Kila mmoja wenu anasoma vizuri"


Shu'ubah amesema, "Mimi namdhania alisema: Msihitilafiane, kwani waliokuwa kabla yenu walihitilafiana na hatimaye wakaangamia." Utakasifu na sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu!! Ni vipi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) atazikubali hitilafu zao kwa kusema kila mmoja wenu anasoma vizuri na wala asiwarejeshe kwenye kisomo kimoja kitakachoondoa hitilafu iliyopita kati yao? Kisha baada ya hapo awaambie kuwa: "Msihitilafiane mtaangamia." Je, huku siyo kupingana? Enyi waja wa Mwenyezi Mungu hebu tutatulieni na Mwenyezi Mungu atakurehemuni. Na je, hivi kuhitilafiana kwao (kama ilivyo riwaya hiyo) si kulikubaliwa na Mtume mwenyewe na akatoa baraka zake na kuwahimiza wahitilafiane?. Haiwezekani kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (kukubali) kupingana huku na kuhitilafiana ambako akili haikubaliani nako. Basi Je, hawaizingatiii Qur'ani ambayo inasema: "Lau ingekuwa (hii Qur'an) imetoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu basi wangekuta hitilafu nyingi ndani yake.' Qur'an 4:82 Je, kuna hitilafu kubwa yenye hatari mno juu ya umma wa Kiislamu kuliko (hitilafu ya) visomo vingi ambavyo vimebadilisha maana za Qur'an vikapelekea tafsiri nyingi na maoni tofauti, mpaka ikawa ile aya ya udhu ambayo tunahitilafiana ndani yake wakati iko wazi? Mtume kufanya mambo kama mtoto mdogo!! na kumuadhibu asiyestahiki adhabu. Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabul-maghazi, Babu maradhin-nabi (s.a.w.w.) wawafatih. Naye Muslim ndani ya sahih yake katika Kitabus-salam Babu karahiyyatit-tadawi Bil-ladud.


Imepokewa kutoka kwa bibi Aisha amesema: "Tulimpanua mdomo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipokuwa mgonjwa akawa anatuashiria tusimpanue mdomo, basi siye tukasema, hiyo ni chuki ya mgonjwa dhidi ya dawa, alipozindukana akasema, Je, sikukukatazeni kunipanua mdomo? Tukasema hiyo ni chuki ya mgonjwa dhidi ya dawa, Mtume akasema: Basi hatobakia mtu hapa ndani ila apanuliwe mdomo hali nami ninaangalia, isipokuwa Abbas kwani yeye hakukushuhudieni." Yanashangaza mambo aliyozushiwa Mtume huyu ambaye wazushi hawa wamemfanya kama mtoto mdogo ambaye hunyweshwa dawa chungu asiyoikubali kwa kupanuliwa mdomo na kubanwa pua, (eti Mtume huyu) anaashiria wasimpanue mdomo lakini wao wanamlazimisha tu pamoja na kutotaka kwake. Na anapozinduka anawaambia: "Je, sikuwakatazeni kunipanua mdomo?" Wao wanajitetea kwamba, walidhania kwamba katazo hilo ilikuwa ni la mgonjwa kuichukia dawa, basi Mtume anawahukumu wote kuwa wapanuliwe midomo yao hali ya kuwa naye anaangalia ili atulize hasira zake na hatobakia miongoni mwao isipokuwa ammi yake Abbasi kwani yeye hakuwepo wakati wakimpanua mdomo.

Bibi Aisha hakukikamilisha kisa hiki, Je, Mtume alitekeleza hukumu yake kwao au hapana? Je, alimtumia Hani kutekeleza, na kilitimia vipi kitendo cha kupanuliwa midomo baina ya wanawake na wanaume waliokuwepo hapo? Mtume (eti) anaondosha baadhi ya aya za Qur'ani! Bukhari ameandika ndani ya sahih yake, Kitabu fadhailil-Qur 'an, Babu Nis-yanil-Qur'an na pia Babu man-laa yaraa ba-asan an-yaqula Suratu kadhaa wa kadhaa. Naye Muslim ameandika ndani ya sahih yake, Kitabu Salatil-musafiriina waqasriha, Babul-amri Bitaa 'hudil-Qur'an wakarahiyatu Qauli nasitu ayata kadhaa. Ametusimulia Abu Usamah kutoka kwa Hisham bin Urwah naye kutoka kwa Baba yake naye kutoka kwa Aisha amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alimsikia mtu fulani usiku msikitini akisoma sura fulani, Mtume akasema, Mwenyezi Mungu amrehemu, kwa hakika amenikumbusha aya kadhaa wa kadhaa (yaani aya fulani) nilikuwa nimesahaulishwa katika Sura kadhaa wa kadhaa."


Vile vile Bukhari ameandika riwaya nyingine kutoka kwa Ali ibn Mushir, kutoka kwa Hisham naye kutoka kwa baba yake ambaye kapokea toka kwa Aisha (r.a.) amesema, "Mtume alimsikia msomaji fulani akisoma usiku msikitini akasema, Mwenyezi Mungu amrehemu, hakika amenikumbusha kadhaa wa kadhaa hiyo ni aya fulani niliiondosha kutoka Sura kadhaa wa kadhaa." (Eti) huyu ndiye Mtume ambaye Mwenyezi Mungu alimtuma alete Qur'an ambayo ni muujiza wa kudumu, na ndiye Mtume ambaye alikuwa akiihifadhi Qur'an tangu siku ya kushuka kwake kwa jumla kabla ya kushuka kwake bayana na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Usiutikise ulimi wako kwa (kuufanyia haraka) ufunuo." Na amesema tena: "Na bila shaka hii Qur'an ni uteremsho wa Mola kwa walimwengu wote, ameteremka nao roho muaminifu (Jibril) juu ya moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji, kwa lugha ya Kiarabu iliyo fasaha, na haya (yaliyomo katika Qur'an) yamo katika vitabu vya kale (walivyoteremshiwa Mitume waliopita."


Lakini waovu, wazushi na wapinzani wanapinga (ukweli huu) wanachotaka wao ni kumzulia uongo Mtume, na kumzushia mambo yasiyo na maana, mambo ambayo haiyakubaliani na akili. Ni wajibu kwa Waislamu wanaotafiti na kuchunguza wamtakase Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kutokana na riwaya kama hizi, ambazo zimejaa katika vitabu vya hadithi na hasa vile vinavyoonekana kuwa ni eti ni sahihi. Sisi hatukuziandika riwaya hizi isipokuwa tumezitoa ndani ya kitabu cha Bukhari na Muslim ambavyo kwa Masunni ndivyo vitabu sahihi mno baada ya kitabu cha Mwenyezi Mungu. Sasa basi iwapo hali ndiyo hii kwa upande wa hivyo vitabu vinavyosemwa kuwa ni sahihi, (na tumeona ni jinsi gani vilivyoivunja heshima ya Mtume (s.a.w.w.) na isma yake, basi hapo tena usiulize kitu kuhusu hivyo vitabu vingine vilivyobakia (yamo makubwa zaidi). Yote haya ni miongoni mwa uzushi wa maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui wa Mtume wake (s.a.w.w.), maadui ambao walikuwa wakijipendekeza kwa watawala wa Kibanu Umayyah katika zama za Muawiyah na baada yake mpaka wakavijaza vitabu kwa hadithi za uongo.


Hadithi ambazo lengo lake ni kumtia doa Mtume (s.a.w.w.), kwani jamaa hao hawakumuamini kwa yote aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake. Na hii ni kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili walilenga kuyahalalisha matendo maovu na mabaya ya mabwana zao, matendo ambayo historia ya Kiislamu imeyanukuu. Kwa bahati nzuri Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwabainisha watu hawa kutoka mwanzoni mwa Utume wake na alitoa tahadhari dhidi yao na wapo aliowafukuza kutoka mjini Madina na akawalaani kutokana na uovu wao. Tabari ameandika ndani ya kitabu chake cha historia amesema: "Mtume (s.a.w.w.) alimuona Abu Sufiyan anakuja akiwa juu ya punda na Muawiyah anamuongoza, na Yazid mwanawe anamuendesha akasema: Mwenyezi Mungu na amlaani aliyepanda, anayeongoza na anayeendesha."[171] Naye Imam Ahmad ndani ya Musnad yake kupitia kwa Ibn Abbas amesema: "Tulikuwa safarini pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), akawasikia watu wawili wanaimba mmoja anamwitikia mwenzie, Mtume (s.a.w.w.) akasema hebu angalieni ni kina nani hao? Watu wakasema ni Muawiyah na Amr bin Al-a's. Mtume akanyanyua mikono yake akasema: Ewe Mwenyezi wadhalilishe mno na uwashinikize motoni."[172]


Na imepokewa kutoka kwa Abu Dharri Al-ghifari kuwa alimwambia Muawiyah kwamba, "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu baada ya wewe (Muawiyah) kupita (mbele Mwenyezi Mungu mlaani huyu na wala usimshibishe ila kwa udongo."[173] Naye Imam Ali (a.s.) alisema ndani ya barua aliyowaandikia watu wa Iraq kama ifuatavyo. "Wallahi lau ningepambana nao peke yangu nao wakawa wamejaa Dunia nzima, nisingejali wala kuona upweke, na bila shaka kutokana na upotofu waliomo wao na uongofu tulionao sisi, ni jambo la wazi na uhakika na linaonekana wazi. Bila shaka mimi natamani kukutana na Mola wangu na ni mwenye kusubiri thawabu zake njema, lakini masikitiko na huzuni inayonipata ni kuhusu uongozi wa umma huu kukaliwa na watu wapumbavu na waovu ambao wataigawana mali ya Mwenyezi Mungu na kuwamiliki waja wa Mwenyezi Mungu, watawapiga vita watu wema na watakuwa katika kundi la waovu."[174]


Na kwa kuwa Mtume alikwisha walaani kama ulivyokiwsha ona, na walishindwa kuzichafua hadithi hizo kwa sababu Masahaba wengi walikuwa wakizifahamu, basi ndipo walipoweka hadithi nyingine kuzikabili hadithi za Mtume ambazo zitaigeuza haki kuwa ni batili na zitakazomfanya Mtume (s.a.w.w.) kuwa mtu wa kawaida ambaye hupandwa na hasira za kijahiliyah, na ghadhabu humfanya avuke mipaka na hatimaye akatukana na kumlaani asiyestahiki kulaaniwa. Na kwa kuwatetea mabwana zao walio laaniwa (jamaa hao) walizusha hadithi hii ifuatayo: Bukhari ndani ya sahih yake ameandika katika Kitabud-da'awaat, Babu Qalin-Nabyyi (s.a.w.w.) Man Aadhaituhn faj-al-lahu zakaatan warahmah. Naye Muslim akaandika katika sahih yake Kitabul-birri was-silah wal-aadabi Babu man La'anahun-Nabiyyu (s.a.w.w.) an Sabbahu an Da'a alaihi walaisa hnwa ahlan Ilidhalika kaana lahu zakaatan wa-ajran warahmah.

Kutoka kwa bibi Aisha amesema: "Watu wawili waliingia kwa Mtume (s.a.w.w.) wakamsemesha juu ya kitu fulani, mimi sikufahamu ni kitu gani walichomkasirisha, basi Mtume aliwalaani na kuwatukana, hatimaye walipotoka mimi nikasema; Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nani aliyepata chochote cha wema ambacho hawa jamaa wamekipata? Mtume akasema: Kwani ilikuwaje? Bibi Aisha akasema, nikamwabia, umewalaani na umewatukana. Mtume akasema: Wewe hujui sharti niliyo mwekea Mola wangu, nilimwambia: Ewe Mwenyezi Mungu mimi mtu, basi yeyote katika Waislamu nitakayemlaani au kumtukana basi mfanyie (laana hiyo na tusi hilo) iwe ni zaka kwake na thawabu." Na imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah kwamba Mtume (s.a.w.w.) amesema: "Ewe Mwenyezi Mungu nachukua ahadi kwako ambayo usinikengeushe kwayo, kwani hapana shaka mimi ni mtu, basi yeyote miongoni mwa waumini nitakayemuudhi, kumshutumu, kumlaani na au kumpiga, basi yafanye hayo kwake iwe ni sala na zaka, pia yawe ni mambo yatakayomsogeza karibu yako siku ya Qiyama." Kwa kupitia hadithi hizi za uzushi Mtume anaonekana ni mwenye kukasirika siyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na anamtukana na kumshutumu, bali anamlaani na kumpiga asiyestahiki hilo.Basi ni Mtume gani huyu ambaye anazukiwa na shetani mpaka anatoka nje ya ulingo wa mambo yanayokubalika kiakili? Hivi kweli mtu yeyote wa dini wa kawaida tu, atakubaliwa kufanya matendo kama hayo? Au je, haiwezi kuonekana kwake kuwa hayo ni matendo mabaya? Na kwa kupitia hadithi kama hizi watawala wa Kibanu Umayyah ambao Mtume (s.a.w.w.) aliwalaani na kuwapiga mjeledi baadhi yao kwa sababu ya kutenda kwao machafu na wakafedheheka mbele ya watu wote, eti mara ghafla wanageuka wanakuwa ndiyo waliodhulumiwa na kutakaswa na kurehemewa pia kusogezwa karibu na rehma za Mwenyezi Mungu. Hizi ni hadithi zilizozushwa, zenyewe zinawasuta na kuwafedhehesha hao walioziunda, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwa na sifa ya kutukana na kulaani, wala hakuwa na uovu wala uchafu wowote ule, kamwe Mtume hakuwa hivyo. Ni maneno mabaya yatokayo vinywani mwao (hao waundaji wa hadithi za uongo) basi hasira za Mwenyezi Mungu ziwashukie na Mwenyezi Mungu amewaandalia watu hao adhabu kali.

Inatutosha riwaya moja tu waliyoiandika Bukhari na Muslim kutoka kwa bibi Aisha kwenye (riwaya hiyo itatosha) kubomoa madai haya ya uongo (dhidi ya Mtume s.a.w.w.). Bukhari ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul-adabi, mlango usemao kuwa Mtume (s.a.w.w.) hakuwa muovu. Imepokewa kutoka kwa bibi Aisha amesema kwamba: "Wayahudi walimjia Mtume (s.a.w.w.) wakamwambia: As-saamu alaikum. (yaani mauti yakushukieni) Aisha akasema, mimi nikasema Alaikum, Walaanakumullah waghadhiba alaikum (yaani, Nanyi yakushukieni, Mwenyezi Mungu awalaani na awakasirikieni) Mtume akasema, tulia ewe Aisha kuwa mpole, ole wako usiwe mkali tena muovu. Mimi nikasema Je, wewe hukuwasikia walivyosema? Mtume akasema hukusikia nilivyosema? Nimewarudishia vivyo hivyo nami nitapokelewa nilichokisema wakati wao hawatopokelewa." Kama alivyoandika Muslim katika sahih yake ndani ya Kitabul-birri was-silat wal-aadaabi kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu amemkataza Muislamu kuwa mwenye kulaani, na amewakataza (Waislamu) hata kuwalaani wanyama na aliambiwa, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu omba maombi dhidi ya washirikina." Mtume akasema, "Mimi sikutumwa ili niwe mwenye kulaani, bali nimetumwa ili niwe ni rehma."


Tabia hii ndiyo inayokubaliana na tabia tukufu na moyo wa huruma ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu anahusika nao, kwani hakuwa akimlaani na kutukana na kumpiga asiyestahiki bali alikuwa akikasirika basi hukasrika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na akilaani humlaani anayestahiki kulaaniwa, na akimpiga (mtu) humpiga ili kusimamisha hukumu za Mwenyezi Mungu, siyo kuwapiga wasiokuwa na makosa ambao hakuna ushahidi dhidi yao wala wale ambao hawakukiri kuwa wametenda kosa. Lakini jamaa hawa waliozusha mambo haya, hasira zao zilifura na mioyo yao kuungulia wakati riwaya zinazozungumzia kulaaniwa kwa Muawiyah na Banu Umayyah zilipoenea, wakawa hawana njia isipokuwa kutengeneza riwaya ili kuwapotosha watu na kumpandisha daraja Muawiyah ambaye ni mtu dhalili. Ndiyo maana utamkuta Muslim katika sahihi yake baada ya kuziandika riwaya hizi ambazo zinaifanya laana ya Mtume kwa Muawiyah kuwa ni zaka na ni rehma na ni vitu vya kumsogeza mbele ya Mwenyezi Mungu, Muslim akaandika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas kuwa amesema: "Nilikuwa nikicheza na watoto, Mtume wa Mwenyezi Mungu akaja, mimi nikajificha nyuma ya mlango, akaja akanipiga kwa kiganja chake na akasema, nenda kaniitie Muawiyah, Ibn 'Abbas anasema, nikaja nikamwambia Mtume, Muawiyah anakula, kisha Mtume akaniambia (tena) nenda kaniitie Muawiyah, nikarudi nikamwambia Mtume (bado) anakula, basi Mtume akasema: Mwenyezi Mungu asilishibishe tumbo lake."


Na ndani ya vitabu vya historia tunakuta kwamba, Imam Nasai baada ya kuandika kitabu cha Al-khasais ambacho ndani yake ameyaeleza mengi juu ya ubora wa Imam Ali ibn Abi Talib (a.s.), Imam Nasai alipoingia Shamu, watu wa Shamu walimpinga na kumuambia "Kwa nini hukutaja sifa za Muawiyah"? Yeye aliwaambia, "Siifahamu sifa yoyote (ya Muawiyah) isipokuwa ile kauli ya Mtume aliyoisema juu yake kwamba, "Mwenyezi Mungu asilishibishe tumbo lake." Basi walimpiga mbeleni (kwenye utupu) wakamuua kifo cha shahidi. Wanahistoria wanaeleza kuwa, dua ya Mtume ilikubaliwa kwani Muawiyah alikuwa akila mpaka anachoka kula lakini hashibi. Kwa kweli mimi nilikuwa sizijui hizi riwaya ambazo zinaigeuza laana kuwa ni rehema na kikurubisho kwa Mwenyezi Mungu mpaka pale aliponifahamisha mmoja wa Masheikh wa Tunis ambaye anasifika kwa elimu na maarifa, na tulikuwa tunajadiliana juu ya hadithi mbali mbali mpaka ikafikia kumtaja Muawiyah ibn Abi Sufiyan.


Sheikh huyu alikuwa akimzungumzia Muawiyah kwa kumsifia mno na kusema: "(Muawiyah) alikuwa mwenye akili mno tena ni mashuhuri kwa utambuzi na amazingatio mazuri." Sheikh aliendelea kusema: "Muawiyah alisifika kwa siasa yake na ushindi wake dhidi ya Sayyidna Ali (k.w.) katika vita." Mimi nilimvumilia kwa uchungu (Sheikh huyu) lakini hatimaye alivuka mpaka katika kumsifia Muawiyah mpaka nikashindwa tena kuvumilia na ndipo nikamwambia kwamba: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa hampendi Muawiyah na alimuombea dua mbaya na alimlaani." Basi jamaa waliokuwepo hapo walishangaa kuna wengine walikasirishwa na kauli yangu. Lakini yule Sheikh alinijibu kwa utulivu kunisadikisha (niyasemayo), jambo ambalo lilizidisha mshangao kwa jamaa waliohudhuria hapo na wakamwambia:"Sisi hatuelewi kinachofanyika hapa!! Wewe kwa upande fulani unamsifia Muawiyah na kumtakia radhi na kwa upande mwingine unakubaliana kuwa Mtume alimlaani, ni vipi yatawezekana mambo haya.?" Mimi na jamaa hao tukaulizana ni vipi jambo hilo litawezekana? Yule Sheikh akatujibu jawabu ambalo lilishangaza na ikawa vigumu kulikubali kwani alisema: "Hakika yule anayelaaniwa na Mtume wa Mweyezi Mungu au kutukanwa basi hiyo kwake ni zaka (utakaso) na ni rehema na kikurubisho mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu." Basi jamaa wote walijiuliza kwa mshangao, "Inawezekanaje hali hiyo?"


Yule Sheikh akasema: "Hiyo ni kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) amesema: Mimi ni mtu kama watu wengine, na nimekwisha kumuomba Mwenyezi Mungu aifanye dua yangu na laana yangu iwe ni rehma na zaka." Kisha akaongeza akasema: "Hata yule mtu aliyeuawa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) basi mtu huyo atatoka duniani na kuingia peponi moja kwa moja." Hatimaye nilikaa faragha na Sheikh huyu na nikamuuliza rejea ya hadithi aliyoitaja, naye akanielekeza kwenye Sahihi Bukhari na Sahih Muslim na nikazichunguza hadithi hizo, na hazikuniongezea isipokuwa uthibitisho wa njama walizozipanga Banu Umayyah ili kuufumba ukweli na kuficha aibu zao kwa upande mmoja na kuivuruga heshima ya Mtume (s.a.w.w.) kwa upande mwingine. Baada ya hapo nilikuta riwaya nyingi zinazolenga makusudio hayo hayo. Na ili wapate kutulia wenye njama hizi, bila shaka walitengeneza riwaya nyingi kuliko hizo kwa kutumia maneno ya Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu.


Bukhari ameandika katika sahihi yake ndani ya Kitabut-tawhiid mlango wa kauli ya Mungu isemayo: "Wanataka wayabadilishe maneno ya Mungu." Kutoka kwa Abu Huraira kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alisema: "Mtu mmoja alikuwa hajapata kutenda jambo la kheri hata kidogo alisema kuwa, Yeye akifa wamuunguze na wapeperushe nusu ya jivu nchi kavu na nusu yake baharini. Wallahi Mwenyezi Mungu akimtia mkononi mtu huyu atamuadhibu adhabu ambayo hatomuadhibu yeyote katika walimwengu. Basi Mwenyezi Mungu aliiamuru bahari ikakusanya (pvu) lililokuwa humo baharini, na aliiamuru nchi kavu ikakusanya jivu lililokuwa humo na kwa uwezo wake Mungu mtu yule aliyechomwa akawa mzima. Mwenyezi Mungu akamuuliza: Kwanini ulifanya hivi? Akajibu: Kwa ajili ya kukuogopa, kwani wewe ni mjuzi mno! Mwenyezi Mungu alimsamehe."


Kuna (habari) nyingine pia kutoka kwake (Abu Huraira) alisema: "Nilimsikia Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) akisema: Hakika mja alitenda dhambi na huenda alisema alifanya dhambi, akasema Ee! Mola nimetenda dhambi na huenda alisema nimefanya dhambi nisamehe, basi Mola wake atasema: Hivi mja wangu ametambua kuwa anaye Mola anaye samehe dhambi na atakayemuadhibu kwa ajili basi nimemsamehe mja wangu. Kisha atakaa kwa kipindi akitakacho Mwenyezi Mungu, halafu atatenda dhambi au atatenda kosa kisha akasema, Mola wangu nimetenda dhambi au nimekosa kosa jingine, lisamehe kosa hilo, atasema: Hivi mja wangu ametambua kwamba anaye Mola anayesamehe dhambi na kuadhibu, basi nimemsamehe mja wangu. Kisha atakaa kwa muda autakao Mwenyezi Mungu, hatimaye atafanya dhambi na huenda alisema ametenda kosa akasema, Mola wangu nimekosa au akasema nimetenda dhambi nyingine nisamehe. Mwenyezi Mungu atasema hivi mja wangu ametambua kuwa anaye Mola anayesamehe dhambi na kuadhibu basi nimemsamehe mja wangu mara tatu, sasa na afanye atakavyo."


Lo!! Ni Mola gani huyu enyi waja wa Mungu, pamoja na kwamba mja alitambua kutokana na khofu yake ile ya mwanzo kuwa anaye Mola anayesamehe dhambi, lakini Mola wake huyo anabakia kuwa hajui ukweli huu na kila mara akajiuliza, "Hivi mja wangu ametambua kuwa anaye Mola anayesamehe dhambi?" Ni Mola gani huyu ambaye kutokana na wingi wa madhambi yanayorudiwa mara kadhaa, na wingi wa msamaha unaorudiwa mara kadhaa, basi hatimaye amechoka na kubweteka na anamwambia mja wake fanya utakavyo.? "Hayo ni maneno mazito yatokayo vinywani mwao, hawasemi isipokuwa uongo, huenda ukajiangamiza nafsi yako kwa huzuni kutokana na matendo yao iwapo hawatayaamini mazungumzo haya."


Naam, bila shaka hapo kabla walikwishadai kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu alimuambia Uthmani kuwa,"Fanya upendavyo kamwe hakitakudhuru kitu baada ya leo." Maneno hayo yalisemwa wakati Uthman alipoandaa jeshi lililokuwa na zana duni za kivita (waliloliita jeshi la Usrah) kulingana na usemi wao. Hapana shaka kwamba (madai kama haya) ni mfano wa kitabu cha hundi ya msamaha inayompa mtu mamlaka ya kuingia peponi inayotolewa kwa majaala ya mtawa wa Kanisa, (hundi ambayo) inamruhusu mtu kuingia katika ufalme wa mbinguni. Kwa hiyo siyo ajabu kwa Uthman kufanya matendo maovu ambayo yalisababisha mapinduzi dhidi yake na kuuawa kwake kisha akazikwa kwenye makaburi yasiyokuwa ya Waislamu tena bila kukoshwa wala kuvishwa sanda. "Hayo ni matamanio yao (siyo hukumu ya Mtume s.a.w.w.) basi waambie leteni hoja zenu kama ninyi mnasema kweli."