WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Swali la 19: Ni kwa nini walitishia kuichoma moto nyumba ya bibi Fatimah?
Jawabu: Idadi kubwa ya Masahaba ambao hawakumpa baia Abubakr walibakia ndani ya nyumba ya Ali ibn Abi Talib, na lau Umar asingefanya haraka kuizunguka nyumba hiyo na kutishia kuichoma moto, basi jambo hilo lingepata nguvu na umma ungegawika makundi mawili moja la Ali na lingine la Abubakar. Lakini Umar kwa ajili ya kupasisha jambo lililokwisha tokea alitazama mtazamo wa mbali pale aliposema, "Lazima mtatoka kwenda kutoa baia la sivyo nitaichoma moto nyumba hii na waliomo, akikusudia Ali na Fatmah binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.)." Na kwa kauli hii basi hakuweza kubakia katika watu yeyote ambaye nafsi yake inamtuma kuuvunja utiifu na akose kuingia katika baia. Basi je, ni utukufu gani mkubwa (uliokuwepo zama hizo) kuliko utukufu wa mwanamke bora ulimwenguni (Fatmah) na mumewe ambaye ni Bwana wa mawasii? Swali la 20: Ni kwa nini Abu Sufiyan alinyamaza (asiseme kitu) pale Umar alipowatishia na kuwaonya?


Jawabu: Wakati Abu Sufiyan aliporejea Madina baada ya Mtume (s.a.w.w.) kufariki, kwani Mtume alikuwa amempeleka Abu Sufiyan kwenda kukusanya zaka alishitukizwa na Ukhalifa wa Abubakr, na haraka alikwenda nyumbani kwa Ali ibn Abi Talib akamchochea afanye mapinduzi na awapige vita jamaa hao hali ya kuwa akimuahidi (kumsaidia) mali na watu. Lakini Ali (a.s.) alimfukuza kwa kutambua nia yake, naye Abubakr na Umar walipofahamu jambo hilo walimwendea Abu Sufiyan wakamlainisha na kumuahidi kumpa kila kitu alichokikusanya katika sadaka hizo na kumshirikisha katika Ukhalifa kwa kumchagua mwanawe kuwa Gavana wa Sham. Basi Abu Sufiyan aliridhika na hayo na akawanyamazia, ndipo wakamchagua Yazid ibn Abi Sufiyan kuwa Gavana wa Sham, na alipokufa wakamteua nduguye Muawiyah ibn Abi Sufiyan achukue mahali pake na wakamuwezesha huyu Muawiyah kuufikia Ukhalifa. Swali la 21: Je, Imam Ali aliridhia jambo hilo na akawapa baia jamaa hao?


Jawabu: Hapana kamwe Imam Ali hakuridhia jambo hilo na hakunyamaza bali alitoa hoja dhidi yao kwa kila kitu na hakukubali kuwapa baia licha ya vitisho vyao na maonyo. Ibn Qutaibah ameeleza ndani ya kitabu chake cha historia kwamba Imam Ali aliwaambia: "Wallahi sikupeni baia, ninyi ndio wenye haki kunipa baia mimi." Bali alimchukua mkewe bibi Fatmah akapita naye kwenye vikao vya Maansari, nao wakawa wanatoa sababu (kwa kusema) kwamba Abubakar amewawahi. Bukhari ameeleza kuwa Imam Ali hakutoa baia muda wote wa uhai wa bibi Fatimah, alipofariki bibi Fatmah na watu wakampuuza Imam Ali alilazimika kufanya sulhu na Abubakr, na Bibi Fatimah aliishi kwa muda wa miezi sita baada ya kifo cha Baba yake, Sasa je, bibi Fatmah alifariki akiwa hana baia wakati ambapo baba yake ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Yeyote atakayekufa na hali ya kuwa hana baia basi atakufa mauti ya kijahiliya."


Na Je, Ali alikuwa anafahamu kwamba yeye ataishi mpaka baada ya Abubakr, basi akachelewa kumbai kwa muda huo wa miezi sita? Ifahamike kwamba, Ali hakunyamaza muda wote wa uhai wake, kwani kila alipopata fursa hukumbusha dhulma aliyofanyiwa na kuporwa haki yake, na hiyo inatosha kuwa ni dalili ya yale aliyoyasema kwenye hotuba yake inayojulikana kama hotuba ya Shaqshaqiyyah. Swali la 22: Ni kwa nini walimchukiza na kumkasirisha bibi Fatmah wakati haja yao ilikuwa ni kuleta sulhu?


Jawabu: Bila shaka walikusudia kumchukiza bibi Fatmah kwa kumnyang'anya ardhi yake na milki zake na wakamnyima mirathi ya baba yake na wakayakanusha madai yake yote kiasi cha kumuondolea heshima yake na utukufu wake miongoni mwa watu kiasi wasimuamini endapo atachokoza kwa kuleta madai kuthibitisha matamko yanayohusu Ukhalifa. Na ndio maana Maansari walimtolea udhuru kwamba baia yao ameiwahi Abubakr, na lau mumewe (Ali) angewahi wasingempinga. Kwa ajili hiyo bibi Fatmah alimkasirikia mno Abubakr na Umar mpaka akawa huwaapiza katika kila sala anayoisali, na alimuusia mumewe kwamba asihudhurie jeneza lake yeyote miongoni mwao na amuepushe kabisa na watawala hao ambao yeye bibi Fatmah anawachukia. Na kwa hakika walikusudia kumuudhi ili wamuonyeshe Ali kuwa yeye ni dhaifu juu yao kuliko binti ya Mtume ambaye ndiye mwanamke bora ulimwenguni na ambaye Mwenyezi Mungu hukasirika kutokana na kukasirika kwake na huridhia kutokana na kuridhia kwake (Fatmah), kwa hiyo (Ali) hakuwa na la kufanya isipokuwa kunyamaza.


Swali la 23: Ni kwa nini wakuu wa Kiquraish waligomea jeshi la Usamah? Jawabu: Pindi mambo yalipokuwa yamemkalia vizuri Abubakr na akawa ndiye Khalifa wa Waislamu kutokana na juhudi za Umar licha ya kutoridhika kwa wapinzani, Abubakr alimtaka Usamah asimchukue Umar ibn Khatab ili abakie akimsaidia kwenye mambo ya utawala, kwani yeye peke yake hawezi kuyakamilisha na hapana budi awe na watendaji ambao ni wenye nguvu na ususuavu ambao walimpinga Mtume (s.a.w.w.) na wala hawakujali ghadhabu za Mwenyezi Mungu wala laana ya Mtume (s.a.w.w.) kwa yule atakayegomea jeshi la Usamah miongoni mwa wale aliowateua yeye mwenyewe Mtume. Hapana shaka kwamba waliopanga kufanikisha suala hili (la Ukhalifa) ndiyo waliogomea jeshi la Usamah ili wapate kufanikisha jambo lao na kusaidiana kuimarisha misingi yao.


Swali la 24: Je, ni kwa nini Imam Ali (a.s.) alitengwa katika kila jambo na wala hawakumshirikisha kwa lolote lile? Jawabu:Halihalisini kwamba jamaa hao waliwakumbatia watu wengi miongoni mwa wale walioachwa huru (siku ya Fat-hi Makkah) na wakawapa vyeo ndani ya serikali yao kwa kuwashirikisha kwenye Ukhalifa na wakawateua miongoni mwao wawe maamiri na watawala katika bara Arabu yote na katika kila miji ya Kiislamu. Miongoni mwa hao walioteuliwa ni Al-walid ibn Uqbah, Marwan ibn Al-hakam, Muawiyah na Yazid watoto wa Abu Sufiyan, Amri ibn Al-a's, Mughirah ibn Shu'ubah, Abu-hurairah na wengi wengineo ambao walikuwa wakimkera Mtume wa Mwenyezi Mungu. Lakini Ali walimtenga na kumpuuza wakamuacha kajifungia nyumbani kwake, wala hawakumshirikisha kwa lolote katika utawala wao kwa muda wote wa robo karne ili wamdhoofishe na kumdharaulisha na wawafanye watu wasimthamini, kwani watu ni watumwa wa dunia wanamfuata aliye na (nguvu za) utawala na cheo na mali. Na maadam Ali alikuwa hapati chakula chake cha siku moja isipokuwa kwa pato litokanalo na mkono wake na jasho lake, basi kwa vyovyote vile watu watamkimbia na wala hawatamfuata. Na ndivyo ilivyokuwa, hakika Ali alibakia katika hali hiyo kwa muda wote wa Ukhalifa wa Abubakr, Umar na Uthman akiwa ndani, na wote hawa wakifanya kila namna kumdhalilisha na kuizima nuru yake na kuzificha fadhila zake na cheo chake. hali ya kuwa Imam Ali hana chochote cha kidunia kitakacho wafanya watu wampende.


Swali la 25: Ni kwa nini waliwapiga vita waliozuwia zaka pamoja na kuwa Mtume alikataza jambo hilo? Jawabu: Hiyo ni kwa sababu baadhi ya Masahaba walihudhuria baia ya (kula kiapo cha utii kwa) Imam Ali huko Ghadir Khum wakati walipokuwa wakirudi kutoka kwenye Hija ya kuaga hali ya kuwa wamefuatana na Mtume (s.a.w.w.)- Kwa ajili hiyo walijizuwia kutoa zaka hiyo kwa Abubakr kwa sababu wao hawakuwepo katika kifo cha Mtume wala hawakuwepo kwenye matukio yaliyofuatia kifo cha Mtume hasa juu ya kubadilika Ukhalifa kutoka kwa Ali kwenda kwa Abubakr. Hali hii ilisababishwa na wengi wao kutokuwa wakazi wa Madina, na hapana shaka kuwa baadhi ya habari ziliwafikia ya kwamba bibi Fatmah (a.s.) amekosana nao na amewakasirikia, na pia kwamba Ali (a.s.) amekataa kuwapa baia, na kwa yote hayo basi walikataa kutoa zaka kwa Abubakr mpaka mambo yawabainikie.


Hapo ndipo Abubakr na Umar na watumishi wa utawala wao walipoafikiana wawapelekee jeshi chini ya uongozi wa Khalid ibn Walid ambaye alikuwa ndiyo upanga wao, akaenda akazima upinzani wao na kunyamazisha fikra zao. Si hivyo tu bali aliwaua wanaume zao na kuwateka wanawake zao na watoto wao ili iwe ni onyo kwa yeyote ambaye nafsi yake itamshawishi kutotii au kuitia dosari heshima ya dola. Swali la 26: Ni kwa nini walizuwia hadithi za Mtume zisiandikwe? Jawabu: Tangu siku za mwanzo walifanya kila njia kuzuwia hadithi za Mtume, siyo tu kwa sababu hadithi hizo zinahusiana na suala la Ukhalifa na ubora wa Imam Ali, bali ni kwa kuwa nyingi katika hadithi hizo zinapingana na maneno yao na vitendo vyao ambavyo walikuwa wakivitumia kuendeshea mambo ya maisha na kuimarisha utambulisho wa dola mpya waliyoizusha juu ya misingi yake kwa mujibu wa ij-tihadi zao.


Swali la 27: Je, Abubakr alikuwa anaweza kumudu jukumu la Ukhalifa? Jawabu: Abubakr hakuwa na uwezo wa kumudu uzito wa Ukhalifa, na lau Umar ibn Khatab na baadhi ya wenye hila miongoni mwa wakuu wa Kibanu Umayyah mambo yangemshinda. Historia imeandika kwamba, Abubakar siku zote alikuwa akitii maamuzi na maoni ya Umar ibn Khatab aliyekuwa mtawala mtendaji. Dalili ya hilo ni kile kisa cha wale wanaoimarishwa nyoyo zao katika dini ambao walimjia Abubakr mwanzoni mwa Ukhalifa wake, akawaandikia barua na akawatuma waende kwa Umar ambaye mambo yanayohusu mali yalikuwa mkononi mwake. Basi Umar aliichana barua ile na akawafukuza, wakarudi kwa Abubakr wakamuuliza; "Hivi wewe ndiye Khalifa au yeye?" Akawajibu: "Ni yeye kwa mapenzi ya Mungu."


Kadhalika wakati Abubakr alipoigawa sehemu ya ardhi kumgawia Uyaynah ibn Hisn na Aqra'a ibn Habis, basi Umar akakataa alipoisoma barua ya Abubakr na akaitemea mate akaifuta. Watu wale wakarudi kwa Abubakr hali ya kuwa wanalalamika kutokana na aliyoyafanya Umar na wakamwambia: "Wallahi hatufahamu hivi wewe ndiye Khalifa au Umar." Akasema; "Bila shaka yeye ndiyo Khalifa." Umar alipofika hapo hali ya kuwa amekasirika na kumuhoji Abubakr kwa maneno makali juu ya kutoa kwake ardhi hiyo, Abubakr alimwambia Umar, "Hivi sikukuambia kwamba wewe una nguvu kuliko mimi juu ya jambo hili la Ukhalifa.? Hakika wewe umenizidi nguvu."[165]

Bukhari ameandika ndani ya sahihi yake kwamba, Umar alikuwa akiwahimiza watu wambai Abubakr na husema: "Bila shaka Abubakr ndiye Mwenzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na wa pili katika wawili (pangoni) na kwamba yeye ni mbora wa Waislamu kwa mambo yenu, basi simameni mumbai." Anas bin Malik anasema: "Nilimsikia Umar anamwambia Abubakr siku hizo, panda juu ya mimbari, hakuacha kumtaka apande mpaka akapanda juu ya mimbari na watu wote wakambai." Swali la 28: Kwa nini Abubakr aliusia Ukhalifa kwa Umar kabla ya kufa kwake? Jawabu: Hiyo ni kwa kuwa Umar ndiye aliyefanikisha kumtupa mbali Ali kutoka kwenye Ukhalifa, na ni kutokana na (yeye Umar) kuwa mpinzani mbaya wa Mtume (s.a.w.w.) hapo mwanzo pia kwa namna alivyowaburuta Maansari wambai Abubakr na kuwalazimisha watu kwa nguvu kutoa baia mpaka mambo yakafikia kutishia kuchoma moto nyumba ya bibi Fatmah. Pia ni kwa kuwa yeye alikuwa ndiye Khalifa mtendaji kama tulivyotangulia kusema, yeye ndiye aliyekuwa na kauli ya mwanzo na ya mwisho, na hapana shaka kwamba yeye alikuwa miongoni mwa Waarabu wenye mtazamo wa mbali, kwa hiyo alifahamu kwamba Waislamu na hasa Maansari hawatakubali kumpa baia kutokana na tabia yake ya ukali na ususuavu na hasira zake za haraka haraka. Kwa sababu hizo basi akamtangulizi Abubakr kwa kuwa tabia yake ilikuwa ya upole na huruma naye amewatangulia kusilimu. Isitoshe Aisha bint yake Abubakr alikuwa ni mwanamke shupavu anayeweza kuyakabili mambo mazito na kubadilisha mambo, katika hali hiyo Umar alikuwa akitambua vyema kwamba Abubakr ni mfuasi wake na atatii maelekezo yake kwa kila atakalolipendekeza kwake.Jambo hili halikuwa siri kwa Masahaba wengi juu ya yeye Abubakr kuusia Ukhalifa kwa Umar kutokana na maandiko yake, bila shaka Imam Ali alikwisha mwambia Umar tangu ile siku ya kwanza kuwa: "Leo hii mwandalie sehemu yake na umuimarishie, naye kesho atakurudishia." Kama alivyosema Sahaba mwingine kumwambia Umar wakati alipotoka na yale maandiko yaliyokuwa na usia wa Abubakr,(kisha Umar akajifanya kuwa hajui kilichomo, sahaba yule) akamwambia Umar, "Mimi nafahamu kilichomo, bila shaka wewe ulimtawalisha kipindi hicho cha kwanza naye amekutawalisha mwaka huu." Hivyo basi usia wa Abubakar kwa Umar ni jambo linaloeleweka kwa watu wote, na ikiwa Abubakr katika zama za uhai wake anakiri mbele ya watu wote kwamba Umar ana nguvu kuliko yeye, basi siyo ajabu kumpa utawala wakati wa kufa kwake.


Na kwa ajili hii inatubainikia kwa mara nyingine kwamba, yale wayasemayo Masunni kuwa Ukhalifa hauwezi kukubalika isipokuwa kwa njia ya mashauriano ni jambo ambalo halipo na wala halimo kabisa ndani ya mawazo ya Abubakr na Umar. Na ikiwa Mtume (s.a.w.w.) alifariki na akaliacha jambo hili liwe katika mashauriano kati ya watu kama wanavyodai Masunni, basi bila shaka Abubakr alikuwa ni mtu wa mwanzo kubomoa msingi huu aliipinga Sunna ya Mtume (s.a.w.w.) kwa kumuusia Umar baada yake.

Siku zote utawaona Masunni wanajinadi kwa fahari kubwa kwamba wao wanaamini mashauriano, na eti Ukhalifa haukubaliki isipokuwa kwa njia hiyo, na hukejeli kauli ya Mashia ambao wanaamini kuwa Ukhalifa haukubaliki isipokuwa utokane na maagizo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w.).

Masunni wengi utawasikia wanaikosoa itikadi hii na kwamba ni kitu kilichoingizwa ndani ya Uislamu kutoka kwa Waajemi/Wairani ambao wanasema kuwa uongozi wa mambo ya Mwenyezi Mungu ni suala la urithi (wa kizazi maalum). Ni mara nyingi Masunni wanatolea ushahidi aya isemayo: "Na mambo yao ni kwa mashauriano kati yao." Na wanadai kwamba aya hiyo ilishuka kuhusu Ukhalifa na kwa dalili hii sisi tunayo haki ya kusema kwamba Abubakr na Umar walikwenda kinyume na kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume na hawakuvithamini vitu hivyo viwili kuhusu suala la Ukhalifa. Swali la 29: Ni kwa nini Abdur-rahman ibn Auf alimuwekea sharti Imam Ali ibn Abi Talib kuwa ni lazima aongoze kwa mujibu wa Sunna ya Makhalifa hao wawili?


Jawabu: Miongoni mwa udhalili wa dunia mbele ya Mwenyezi Mungu, ni Abdur-Rahman ibn Auf kuwa mtu atakayeamua mustakabali wa umma wa Kiislam baada ya Umar, auchagulie umma mtu amtakaye yeye na amuondoshe asiyemtaka. Kamwe hilo haliwezekani, lakini yote hayo ilikuwa ni mipango ya Umar ambaye aliupatia kura ya turufu mkono wa Abdur-Rahman juu ya Masahaba wengine, na huyu Abdurrahman ibn A'uf yeye ni miongoni mwa Waarabu wenye vitimbi. Hapana shaka kwamba yeye ni miongoni mwa wajumbe wa kundi lililopanga mipango inayohusu Ukhalifa na namna ya kuuondosha kwa muhusika wake wa kisheria. Kwa kuwa Bukhari anakiri kwamba Abdur-rahman ibn Auf alikuwa akichelea jambo fulani kwa Ali,[166] basi moja kwa moja naye alifanya kila njia kumtenga Imam Ali mbali na Ukhalifa kwa namna yoyote atakayoiweza. Huyu Abdur-rahman ibn Auf anafahamu kama walivyokuwa wakifahamu Masahaba wengine kwamba Ali (a.s.) alikuwa hakubaliani na ij-tihadi za Abubakr na Umar na yale waliyoyabadilisha miongoni mwa hukumu za kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume (s.a.w.w.), na alikuwa akijaribu kwa uwezo wake kuwapinga na kuwakemea.


Kwa sababu hiyo basi, Abdur-rahman akamuwekea sharti Imam Ali kwamba aongoze kwa mujibu wa Sunna ya Abubakr na Umar hali ya kuwa anajua tangu mwanzo kuliko mtu mwingine kwamba Ali hajipendekezi wala hasemi uongo na wala sharti hilo kamwe hatalikubali, ni kama ambavyo pia Abdur-rahman alikuwa anajua ya kwamba Uthrnan ibn Affan ambaye mkwewe, Maquraishi na wajumbe wote wa mipango hiyo watamfurahikia akichukua Ukhalifa. Swali la 30: Je, hadithi ya Maimamu kumi na wawili inapatikana kwa Msunni?


Jawabu: Bukhari na Muslim wameithibitisha hadithi hiyo pia wanachuoni wote wa hadithi wa Kisunni wameithibitisha hadithi ya Mtume (s.a.w.w.) isemayo "Dini haitaacha kusimama hadi siku ya Qiyama mpaka wawepo Makhalifa kumi na wawili na wote ni Maquraishi.[167] Na hadithi hii imebakia kuwa ni mushkeli mkubwa ambao hauna jibu kwa Masunni, hapana yeyote miongoni mwa wanazuoni wao aliyethubutu kuwahesabu (Makhalifa hao) baada ya wale Khulafau-rashidina wanne, na watano ni Umar ibn Abdil-aziz, sasa wanabakia katika idadi hiyo (Makhalifa) saba ambao hawapo.

Masunni hawana njia vinginevyo nao waukubali Uimamu wa Ali na wanawe, Uimamu ambao Mashia wanaukubali na kwa kufanya hivyo wawe ni wafuasi wa watu wa nyumba ya Mtume, na au waipinge hadithi hii, jambo ambalo litavifanya vitabu vyao viwe tupu havina ukweli wowote isipokuwa uzushi mtupu. Zaidi ya hapo ni kwamba hadithi hii ambayo inahusisha Ukhalifa kwa Maquraish peke yao inapingana na ule msingi wa mashauriano ambao Masunni wanautetea, kwani uchaguzi na demokrasi inamkusanya kila mtu katika umma, na wala hailihusishi kabila maalum na kuyaacha makabila mengine bali inavuka kwenye makabila ya Kiarabu mpaka inafika kwenye makabila mengine miongoni mwa makabila ya Kiislamu yasiyokuwa ya Kiarabu.


Haya ndiyo majibu ya haraka kwa ufupi ili tumbainishie msomaji baadhi ya mas-ala ambayo huenda yakaichanganya akili yake, na hii ni kwa kuwa huenda akapata majibu kwa ufafanuzi ndani ya vitabu vya historia na vile vile ndani ya vitabu vyangu Thummah-tadaitu na Liakuuna Ma 'as-sadiqin. Basi ni juu ya mwenye kutafiti kuangalia rejea zinazo tegemewa, na ajitahidi kupata ukweli, azichambue riwaya na matukio ya kihistoria na kwa kupitia uchambuzi huo imbainikie haki ambayo imevishwa vazi la batili, alivue na aiangalie haki katika vazi lake la asili.