WAULIZE WANAOFAHAMU

 
MLANGO WA SITA, YANAYOHUSU UKHALIFA.
Ukhalifa: Ukhalifa ni kitu gani? Ukhalifa ni kile kitu ambacho Mwenyezi Mungu amekifanya kiwe ni mtihani kwa umma, nacho ndicho kile walichokigawa na kukipupia wenye tamaa, na ni kitu ambacho katika kukigombea damu zisizo na makosa zilimwagika, si hivyo tu bali kwa sababu ya huo ukhalifa baadhi ya Waislamu walikufuru, (matokeo yake) wakahadaiwa na wakatengana wao na njia iliyonyooka na kuwaingiza ndani ya moto wa Jahiim. Hatuna budi kuleta somo kwa ufupi kuhusiana na Ukhalifa, somo ambalo pamoja na ufupi wake litazingirwa na mambo yaliyojificha na utata ambao Ukhalifa ulikuwa ndio uwanja wa utata huo muda kidogo kabla na baada ya kutawafu Mtume (s.a.w.). Kitu cha kwanza ambacho kinakuja haraka katika akili ni kwamba, suala la uongozi kwa Waarabu lilikuwa miongoni mwa mambo ya lazima katika kila zama. Utawaona wao wakimtanguliza kiongozi wa kabila au kiongozi wa familia juu ya nafsi zao (awaongoze). Basi huwa hawaamui jambo lolote wala hawatumii maoni yoyote mpaka kwanza wamshauri kiongozi wao, na wala hawamtangulii kwa kauli yoyote ile.


Basi kiongozi huyu wa ukoo mara nyingi huwa ni mkubwa kwa umri na mjuzi wao katika mambo na ni mtukufu wao kwa nasaba. Na inadhihiri kwamba, kiongozi huyu hujitokeza kufuatia matukio ndani ya ukoo wake, na miongoni mwa mambo ambayo hujitokeza kwake ni kama vile kuwa na akili tambuzi, ushujaa, ufahamu wa mambo, ukarimu kwa wageni na mengineyo miongoni mwa mambo matukufu, lakini mara nyingi (uongozi huu) hupatikana kwa njia ya kurithi na siyo kuchaguliwa. Baada ya hapo tunakuta kwamba, makabila na koo mbalimbali pamoja na kujitegemea kwake (kiuongozi), huwa yanautii uongozi wa kabila moja ambalo huenda likawa na idadi ya watu wengi, mali nyingi na linao mashujaa wanaojitosa katika vita na kuzilinda kabila nyingine. Mfano wa hilo ni Maquraishi ambao walikuwa wakiyaongoza makabila mengine ya kiarabu yaliyokuwa yakiwatii kuwa ni viongozi na mabwana ambao uongozi wao ulilazimika kutokana na wao kuwa ndiyo walinzi wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu.


Na ulipokuja Uislamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) aliuthibitisha mfumo huu kwa kiwango fulani katika mahusiano, kwani alikuwa akimtawalisha juu ya makabila yaliyokuwa yakimfikia na kuukubali Uislamu, kiongozi wao na mbora wao ili awe ni msimamizi atakayewasalisha na kukusanya zaka zao na huwa yeye ndiye kiungo baina yao na Mtume. Hatimaye Mtume Muhammad (s.a.w.w.), kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu alianzisha dola ya Kiislamu ambayo maamuzi yake na mafunzo yake yatatii wahyi unaomshukia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ukiwa ndio muongozo wa jamii na ni muongozo kwa mtu binafsi, muongozo huo ukiwa unahusu kufunga ndoa na talaka au kuuza na kununua, kupokea na kutoa, mirathi na zaka na yote yanayomhusu mtu binafsi na jamii katika wakati wa vita na wakati wa amani. Hii ikiwa na maana kwamba mahusiano na ibada zote zitii hukumu za Mwenyezi Mungu, na jukumu la Mtume (s.a.w.w.) ni kufikisha na kuwa macho katika kutekeleza hukumu hizo.


Na katika hali ambayo ni ya kimaumbile ni kwamba, bila shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akifikiri juu ya mtu atakayemrithi katika jambo hili muhimu na tukufu, na hilo si jingine bali ni uongozi kwa umma. Ni katika hali ile ile ya kimaumbile kwa kila kiongozi wa dola yoyote ile lazima aone umuhimu (iwapo analithamini Taifa lake) wa kuwepo mtu atakayemchagua awe naibu wake kwa kila majukumu ambayo yeye atapokuwa hayupo huyo mtu ayasimamie, na atakuwa ni waziri wake wa mwanzo na aliye karibu naye. Na ni kawaida ya maumbile vile vile, naibu wake huyu awe anatambulikana kwa mawaziri wote kadhalika mbele ya taifa. Haiwezekani kabisa, wala akili haiwezi kuamini kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) aliyapuuza yote haya na wala hakuyathamini, na hapana shaka kwamba yeye Mtume ilikuwa ndilo jambo limsumbualo. Hapana shaka kwamba hadithi zinazolihusu jambo hili ziligandamizwa kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Makhalifa ambao walikuwa wakiongoza kwa nadharia ya Shura, na ndiyo wao waliofanya kila juhudi kuyapinga maandiko na matamko yaliyombainisha na kumtambulisha Khalifa. Na katika juhudi hizo pia kulifanyika (namna ya) kuutia kombo utukufu wa Mtume (s.a.w.w.) na kumtuhumu kuwa anaweweseka.


Hatimaye akatiwa dosari yeye Mtume na Kiongozi aliyemtawalisha kushika uongozi wa jeshi kwa madai kwamba hafai uamiri na uongozi kwa sababu ya umri wake mdogo, kisha kuwatia shaka (watu) juu ya kufariki kwa Mtume (s.a.w.w.) ili mambo yavurugike na watu wasije kuwahi kwenda kumpa baia Khalifa aliyebainishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu tangu hapo kabla. Na kwa njama hizo waliweza kufanya mkutano uliojitokeza ghafla huko kwenye Saqifa, wakati Imam Ali na wafuasi wake wakishughulika kuandaa mazishi ya Mtume (s.a.w.w.), wao wakamchagua yule wanayemtaka na nafsi zao zikaridhika na kuimarisha mategemeo yao kwa huyo waliyemchagua. Kilichofuatia ilikuwa ni kuwalazimisha watu wote kula kiapo cha utii huku wakionywa na kutishwa na kuahidiwa (chochote kitu kwa wenye kukubali) na kuonywa (kuadhibiwa kwa watakaopinga), na kisha kuupiga marufuku upinzani wa aina yoyote katika uwanja na siasa.


Hatimaye ikafuatia kusimama imara bila samahani dhidi ya kila yule ambaye nafsi yake inamshawishi kuvunja kiapo cha utii au atakayetia mashaka kuhusu uhalali wa Ukhalifa mpya hata kama atakuwa ni Fatmah binti ya Mtume. Ilifuatia kuweka vikwazo na kuzizuwia moja kwa moja hadithi tukufu za Mtume zote, ili zisije zikasambaa miongoni mwa watu na mambo yakavurugika, hata kama jambo hilo litalazimu maisha ya mtu au mauaji ya kikundi fulani ili kuzimisha upinzani kwa madai ya kuondosha fitna kwa upande mmoja na kuritaddi kwa upande mwingine. Yote hayo tumeyatambua kwa kupitia yale waliyoyaandika wanahistoria, japo baadhi yao wanajaribu kuuficha ukweli kwa kuweka riwaya zinazogongana au kuweka tafsiri na nyudhuru ambazo utafiti na matukio vimekwisha kuuweka wazi.


Huenda baadhi yao wakasameheka, kwani kuna aliyechukua elimu yake kutoka ndani ya rejea ambazo ziliandikwa chini ya athari za kisiasa na kijamii, athari ambazo ziliachwa na ile fitina kubwa, na ikafuatiwa na matukio mbali mbali wakati Banu Umayyah walipoutawala Ukhalifa na wakawapa mali na vyeo baadhi ya Masahaba na tabiina waliofuatia ambao walikuwa wameajiriwa (kutengeneza riwaya za uongo). Kuna baadhi ya wanahistoria ambao waliochukua habari kutoka kwa watu hawa kwa dhana zao nzuri tu juu ya watu hawa, hali ya kuwa hawafahamu hiyana yao na yaliyojificha ndani ya nyoyo zao, basi ndipo zilipochanganyika riwaya sahihi na zile za uongo, na ni vigumu kwa mchunguzi kuufikia ukweli. Ili kumsogeza karibu msomaji anayetafiti kutaka kupata ukweli, hapana budi kuyaleta maswali haya ili ibainike kwa kupitia maswali hayo au majibu yake angalau sehemu ya ukweli au sehemu ya maelekezo ambayo yatamfikisha kwenye ukweli. Maswali na majibu ambayo anayetafuta ukweli haifai kuyaacha.


Zilinifikia barua nyingi kutoka miji mbali mbali, barua ambazo ndani yake kulikuwa na maswali muhimu yanayoonesha hamu kubwa ya wasomaji watukufu kutaka kuchunguza zaidi na kuufuatilia ukweli. Nami nilizijibu baadhi ya barua hizo na nyingine niliziacha siyo kwa sababu ya kuzidharau lakini ni kwa kuwa majibu yake yamo ndani ya kitabu changu kiitwacho; Thummah-tadaitu na kile kingine kiitwacho; Liakuna Maas-sadiqin. Na ili kuongeza faida basi nina yaaridhi maswali hayo ndani ya mlango huu pamoja na majibu yake na ninaambatisha pia ufafanuzi, kwani huenda msomaji akakuta baadhi ya hadithi na matukio yamerudiwa ndani ya kitabu kimoja au ndani ya vitabu vitatu kwa namna mbali mbali.


Swali la 1: Ikiwa Mtume alikuwa anafahamu matokeo yatakayoufika umma wake miongoni mwa migogoro na hitilafu kwa sababu ya Ukhalifa, ni kwa nini basi hakumbainisha Khalifa wake? Nimefanya hivyo makusudi nikifuata mwongozo wa Kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu ambacho hukariri kueleza tukio katika sura kadhaa ili liimarike ndani ya akili ya muumini na liwe katika hali ya uwezekano wa kufahamika na wote. Jawabu: Bila shaka Mtume (s.a.w.w.) alimbainisha Khalifa wake baada ya Hijja yake ya mwisho. Khalifa huyo ni Ali ibn Abi Talib, na aliwashuhudisha-Masahaba wake ambao walihiji pamoja naye na alikuwa akitambua kwamba umma utamfanyia hiyana na utarudi kinyume nyume kwa visigino vyake.


Swali la 2: Ni vipi hakuna Sahaba yeyote miongoni mwa Masahaba wa Mtume aliyemuuliza Mtume kuhusu jambo hili wakati ambapo walikuwa wakimuuliza kila kitu? Jawabu: Bila shaka walimuuliza na alitoa jawabu: Mwenyezi Mungu anasema: "Wanasema, je sisi tunayo amri juu ya jambo hili, waambie amri yote ni ya Mwenyezi Mungu" (Qur'an, 3:154). Na walimuuliza naye akasema: "Hakika Walii wenu (msimamizi) ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini ambao hutoa zaka hali yakuwa wamerukuu" (Qur'an, 5:55) Na walimuuliza tena akasema: "Hakika huyu ni ndugu yangu na ni Wasii wangu na ni Khalifa wangu baada yangu."[162] Swali la 3: Ni kwa nini baadhi ya Masahaba walimpinga Mtume wa Mwenyezi Mungu pale alipotaka kuwaandikia maandiko ambayo yatawalinda wasipotee baada yake na wakasema kuwa anaweweseka?

Jawabu: Ni kweli kabisa kwamba Masahaba walimpinga Mtume (s.a.w.w.) pale alipotaka kuwaandikia maandiko ambayo yatawalinda wasipotee na wakamtuhumu kuwa anaweweseka. Hali ilitokea baada ya wao kufahamu kuwa yeye anataka kumbainisha Ali ibn Abi Talib katika maandiko hayo, kwani hapo kabla alikwisha kuwaambia wakati wa hija ya mwisho ya kuwa washikamane na kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi chake na hawatopotea kamwe, hivyo basi walifahamu kabisa kwamba madhumuni ya maandiko hayo yatakuwa ndiyo maneno yale, kwa kuwa Ali ndiye kiongozi wa kizazi cha Mtume. Kwa hiyo walimtuhumu kuwa anaweweseka ili matokeo yake aache kuandika hasa kutokana na vurugu na hitilafu zilizotokea kuhusu maandiko hayo kabla hajayaandika, na ikiwa Mtume anaweweseka (kwa mujibu wa itikadi yao) basi bila shaka maandiko yake yatakuwa ni upuuzi, kwa namna ilivyo hapa hekima inapelekea kutokuandika.

Swali la 4: Kwa nini Mtume hakusisitiza (kuendelea) kuandika maandiko hayo hasa kwa kuwa yatauhifadhi umma wa Kiislamu usipotee? Jawabu: Haikuwa katika wasaa wa Mtume kuendelea kutaka kuandika maandiko hayo, kwa sababu kuhifadhika kutokana na upotofu kulikwishapingwa pale Masahaba wengi walipokubaliana kuwa yeye Mtume anaweweseka. Basi ndipo hayo maandiko yalipokuwa msingi wa kupotea badala ya kuwa yawe ni mlinzi dhidi ya upotofu, na lau Mtume (s.a.w.w.) angelazimisha kuyaandika, basi yangetokea madai batili baada yake ambayo yangeleta mashaka hata kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu na maandiko ya Qur'ani. Swali la 5: Kabla ya kufa Mtume (s.a.w.w.) aliusia mambo matatu kwa kuyatamka, basi ni vipi sisi yametufikia mambo mawili na la tatu likapotea? Jawabu: Mambo yako wazi kwamba ule usia wa mwanzo ndiyo uliopotea kwa kuwa unahusu Ukhalifa wa Ali, na kwa kuwa Ukhalifa uliosimama ulizuwia jambo hilo lisizungumzwe, vinginevyo mtu mwenye akili ataaminije kuwa Mtume aliusia kisha usia wake ukasahaulika kama alivyoeleza Bukhari? Swali la 6: Je, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akifahamu muda wa kifo chake?


Jawabu: Bila shaka alikuwa akifahamu tangu hapo mwanzo muda wa kufa kwake kwa wakati uliopangwa na alilifahamu hilo kabla ya kutoka kwenda hija yake ya mwisho na kwa ajili hiyo aliita Hija ya kuaga, na kwa ajili hiyo wengi wa Masahaba walitambua kukaribia kwa mauti yake. Swali la 7: Ni kwa nini Mtume (s.a.w.w.) alitayarisha jeshi na akawajumuisha ndani ya jeshi hilo wakuu wa Muhajirina na Ansari miongoni mwa Masahaba wakubwa, na akawaamuru waende Mu'utah huko Palestina kabla ya kufa kwake kwa siku mbili? Jawabu:Mtume(s.a.w.w.) alipozitambua njama walizokuwa wamezipanga Maquraish na kwamba wameafikiana kupuuza usia wake baada yake na kumuondosha Ali kwenye Ukhalifa, alikusudia kuwatayarisha jamaa hawa ili wawe mbali na Madina wakati wa kufa kwake, basi hawatakuwa wamerudi ila baada ya kuwa jambo la Ukhalifa litakuwa limemkalia'vizuri Khalifa wake, na hawataweza baada yake kupitisha sera zao, hakuna tafsiri nyingine inayokubalika kuhusu jeshi la Usmah isipokuwa hii.


Swali la 8: Kwa nini Mtume (s.a.w.w.) hakumchagua Ali kuwemo ndani ya jeshi la Usamah? Jawabu: Hiyo ni kwa sababu Mtume hawezi kuondoka ila aache Khalifa atakayeendesha mambo baada yake, na kwa kuwa Mtume (s.a.w.) hakumchagua Ali kuwemo ndani ya jeshi ambalo ndani yake walikuwemo wakuu wa Kimuhajirina na Ansari ikwa ni pamoja na Abubakr, Umar, Uthman na Abdurrahman ibn A'uf, basi maamuzi haya yenye hekima yanatujulisha kuwa Ali ndiye Khalifa wa Mtume moja kwa moja, na kwamba wale wote ambao Mtume hakuwachagua kuwemo ndani ya jeshi hilo, hakuna mtu miongoni mwao aliyekuwa na tamaa ya Ukhalifa wala mwenye kumbughudhi Ali na kutaka kumfanyia hiyana. Swali la 9: Kwa nini Mtume aliwawekea Kiongozi ambaye ni kijana mdogo asiyekomaa?


Jawabu: Ilivyokuwa mahasidi na wenye hiyana dhidi ya Ali wanalalamika juu ya umri wake mdogo na kuwa wakuu wa Kiquraishi ambao wamekwisha fikia miaka sitini hawataki kuongozwa na Ali mwenye umri ambao haujavuka miaka thelathini isipokuwa kidogo, basi Mtume (s.a.w.w.) aliwawekea kiongozi ambaye ni Usama mwenye umri wa miaka kumi na saba wala hajakomaa na yeye alikuwa miongoni mwa watumwa waliopewa uhuru hiyo yote ilikuwa ni kuwalazimisha ili awabainishie kwanza wao wenyewe na pili Waislamu ya kwamba muumini wa kweli ndani ya Imani yake anawajibika kusikia na kutii japo atakuta ndani ya nafsi yake kuna uzito kwa yale aliyoyamua Mtume na anatakiwa atekeleze mara moja. Je, Usamaha ibn Zaid ibn Harithi anayo daraja kiasi gani mbele ya Ali ibn Abi Talib ambaye amiri jeshi wa waumini na Bwana wa Mawasii naye ndiye mlango wa Elimu ya Mtume (s.a.w.w.) na ni simba wa Mwenyezi Mungu aliye mshindi, Haruna wa Muhammad (s.a.w.w.). Na kwa ajili hiyo basi walifahamu umuhimu wa Mtume kumpa Usamah uongozi juu yao ndipo walipoupinga uongozi wake na wakakataa kutoka wakamgomea, na wala hatusahau kwamba miongoni mwao walikuwemo wenye vitimbi ambao Qur'an imezungumza kuwahusu wao kama ifuatavyo:

"Na bila shaka walifanya hila zao (vitimbi vyao) na hila zao ziko kwa Mwenyezi Mungu (amezidhibiti) na hata kama vitimbi vyao hivyo vingeweza kuiondoa milima." (Qur'an 14:46) Swali la 10: Kwa nini Mtume (s.a.w.w.) aliwakasirikia mno wale waliogomea (jeshi la Usamah) mpaka akawalaanini?" Jawabu: Bila shaka ghadhabu ya Mtume (s.a.w.w.) ilizidi mno, pale alipofahamu kwamba wao wanamlaumu katika uteuzi wake wa amirijeshi. Lawama zilielekezwa kwa Mtume na wala siyo kwa Usamah, na hilo lilithibitika kwa Mtume pale walipokosa imani na ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w.) na kwamba wao wameazimia kutekeleza sera zao kwa gharama yoyote ile itakayo wagharimu. Hali hiyo ndiyo ilyomfanya Mtume atoe laana yake ya mwisho kwa wale waliogomea ili awafahamishe wao na wafuasi wao na Waislamu wote kuwa sasa mambo yamefikia kikomo chake na aangamie mwenye kuangamia hali ya kuwa anajua.Swali la 11: Je, inafaa kumlaani Muislamu hasa pale laana hiyo inapotoka kwa Mtume (s.a.w.w.)? Jawabu: Ikiwa Uislamu ni kutamka shahada mbili nazo ni mtu kusema kuwa: "Nakubali kwa moyo na ninatamka kwa ulimi kwamba, hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na ninakubali kwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kisha mtu huyo asifuate maamrisho yao wala hamsikilizi wala kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w.), inafaa kumlaani mtu huyo, na ndani ya Qur'an tukufu zimo aya nyingi juu ya hilo, tunataja baadhi yake kama mfano: Mwenyezi Mungu anasema: "Bila shaka wale wanaoyaficha yale tuliyoyateremsha miongoni mwa mawaidha na uongofu baada ya kuwa tumeubainisha kwa watu, basi hao Mwenyezi Mungu anawalaani na wanalaaniwa na kila chenye kulaani." (Qur'an, 2:159) Ikiwa Mwenyezi Mungu anamlaani mtu anayeuficha ukweli, basi unafikiria vipi kuhusu mtu anayeipinga haki na kufanya kila njia kuiharibu? Swali la 12: Je, hivi Mtume (s.a.w.w.) alimchagua Abubakar asalishe watu?


Jawabu: Kwa kupitia riwaya mbali mbali zinazopingana tunafahamu ya kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu hakumteua Abubakr awasalishe watu, isipokuwa kama tutayasadiki yale aliyoyasema Umar kuwa Mtume anaweweseka. Na yeyote mwenye kuyasadiki hayo basi bila shaka atakuwa kakufuru, vinginevyo ni kuwa ni vipi mtu mwenye akili atasadiki kuwa Mtume alimuamuru Abubakr awasalishe watu wakati ambapo alikuwa amemteua awemo ndani ya jeshi la Usamah na akamfanya huyu Usamah awe ndiyo Amiri na Imamu wake? Na itakuwaje ambainishe kuwa Imam kusalisha sala mjini Madina na hali yeye hakuwepo hapo, na wakati huo huo historia inashuhudia kwamba yeye Abubakr hakuwepo mjini Madina siku Mtume alipofariki? Habari iliyothibitika ni kama walivyoeleza baadhi ya wanahistoria ambao Ibn Abil-hadid amepokea kutoka kwao kwamba, Ali (a.s.) alimtuhumu bibi Aisha kuwa ndiye aliyemtumia ujumbe baba yake aje awasalishe watu, na Mtume alipolifahamu jambo hilo alikasirika na akasema: "Ninyi ndiyo wale wanawake waliomfanyia vitimbi Yusufu." Na ndipo Mtume alipotoka kwenda msikitini kisha akamuondosha Abubakr, kisha yeye mwenyewe akawasalisha watu sala ya mtu asiyejiweza ili asije akawaachia hoja baada ya hilo.


Swali la 13: Ni kwa nini Umar aliapa kuwa Mtume (s.a.w.w.) hajafariki na akatishia kumuua yeyote yule atakayesema kuwa Mtume amefariki, na hakutulizana ila baada ya kuwasili kwa Abubalcr? Jawabu: Umar alitishia kumuua yeyote yule atakayejaribu kusema kuwa Mtume (s.a.w.) amefariki ili awatie mashaka Waislamu na awaache wakihangaika (wamechanganyikiwa) kusudi baia ya Ali isitimie, na ili wapate kufika mjini Madina wale mashujaa wa upinzani ambao walikuwa wamekubaliana naye kuuchukua uongozi, kwani walikuwa bado hawajafika. Na kwa kuwa Umar alijikuta amewatangulia wenzake, aliitumia fursa hiyo kufanya mbinu ya kuwasahaulisha kisha akachomoa upanga wake akawatisha watu. Hapana shaka kwamba yeye aliwazuwia watu kuingia kwenye chumba cha Mtume ili wakajithibitishie hali ya mambo ilivyo, vinginevyo ni kwa nini basi hakuna hata mtu mmoja aliyethubutu kuingia isipokuwa Abubakr alipofika, yeye aliingia akaufunua uso wa Mtume kisha akatoka ili aje awaambie watu kwamba: "Yeyote aliyekuwa akimuabudu Muhammad basi Muhammad amekwisha kufa, na aliyekuwa akimuabudu Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu yu hai na hatokufa."


Hapa tunalazimika kufafanua kidogo kauli hii ya Abubakr. Je, hivi ni kweli kwamba Abubakr alikuwa akiamini kwamba miongoni mwa Waislamu yuko aliyekuwa akimuabudu Muhammad? Sivyo kabisa, isipokuwa hii ni sentensi ya majazi ambayo ilikusudiwa kuwashutumu na kuwadhalilisha Ali ibn Abi Talib kwa upande mmoja, na kwa ujumla Bani Hashim wote ambao walikuwa wakiona fahari mbele ya Waarabu wengine kwa kuwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu Muhammad (s.a.w.w.) anatokana nao na wao ni watu wake na ni jamaa zake na ndiyo wenye haki mno kwake kuliko watu wengine. Pia hiyo ni kauli inayotoa maelezo ya yale aliyoyatamka Umar ibn Khattab siku ile ya msiba wa siku ya al-hamisi pale Umar aliposema: "Kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu." Na ukweli halisi ulivyo ni kuwa, yeye Umar alikuwa na maana kwamba hatuna haja na Muhammad, kwani mambo yake yamefikia ukingoni na zama zake zimekwisha pita.


Bila shaka hiki ndicho alichokitilia mkazo Abubakr kwa kusema: "Yeyote aliyekuwa akimuabudu Muhammad basi yeye kisha kufa," ambapo makusudio yake yalikuwa na kwamba, Enyi mliokuwa mkijifaharisha juu yetu kwa Muhammad leo bakieni nyuma kwani mambo yake yamekwisha, sisi kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu kwani kiko hai hakitakufa. Na kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa, Ali na Bani Hashim wao ndiyo waliokuwa wakifahamu vyema kuliko watu wengine juu ya uhakika wa Mtume (s.a.w.w.) na walikuwa wakimheshimu mno na kumtukuza, na pia kutekeleza maamrisho yake na waliofuatia katika hili ni wale waliopewa uhuru (baada ya kuwa watumwa) miongoni mwa Masahaba na wale waliokuwa siyo miongoni mwa Maquraish, watu hao ilikuwa Mtume akitema mate huyakimbilia na kujipangusia usoni mwao, na hugombea mabaki ya maji ya udhu wake au nywele zake na wote hawa ni wale masikini na wanyonge ambao walikuwa ndiyo Mashia (wafuasi) wa Ali tangu zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w.) naye ndiye aliyewaita jina hili.[163]


Ama Umar ibn Khatab na baadhi ya Masahaba miongoni mwa vigogo wa Kiquraishi, mara nyingi walikuwa wakipinga maamuzi ya Mtume (s.a.w.w.) na wakimjadili na kumuasi, bali wakijiepusha na matendo yake [164] Na bila shaka Umar aliukata mti wa Baia'tur-ridh-wan kwa kuwa baadhi ya Masahaba walikuwa wakitabaruku kwenye mti huo, kama walivyofanya Mawahabi katika karne hii, kwani wao wameondosha kumbukumbu za Mtume (s.a.w.w.) hata ile nyumba ambayo alimozaliwa Mtume hawakuiacha, na sasa hivi wanajaribu kwa bidii zao na mali zao kuwazuwia Waislamu wasisherehekee kuzaliwa kwa Mtume, na wanazuwia kutabaruku kwa Mtume na kumsalia mpaka wameeneza fikra kwa watu wasiofahamu kuwa, kumsalia Mtume (s.a.w.w.) sala yake kamilifu ni ushirikina.


Swali la 14: Ni kwa nini Maansari walikusanyika kwa siri ndani ya Saqifatu Bani Saidah? Jawabu: Wakati Ansari walipozigundua njama zilizokuwa zimepangwa na Maquraishi za kumuondoa Ali kwenye Ukhalifa, Mtume alipofariki walikusanyika na wakataka kulipitisha suala la Ukhalifa kati yao, ili Khalifa atoke miongoni mwao. Na iwapo wakuu wa Kiquraishi ambao ndiyo muhajirina wako karibu ya Mtume na ni jamaa zake nao wanataka kutengua baia ya Ali, basi Ansari wana haki zaidi kuchukua Ukhalifa kuliko mwingine asiyekuwa wao kutokana na kuitakidi kwao kwamba Uislamu uliimarika kwa ukali wa panga zao, na kwamba Muhajirina wanawategemea wao kwani kama si wao Ansari kuuteka mji wao na makazi yao na kila walichokuwa wanakimiliki basi Muhajirina wasingeweza kuwa na ubora wala utajo wowote. Lau si kuwepo kutofautiana baina ya kabila la Ausi na Khaz-raji ambao walikuwa wakishindania uongozi ikawa kila mmoja wao anautaka Ukhalifa uende kwenye kabila lake, basi Abubakr na Umar wasingekuwa na fursa ya kuuchukua Ukhalifa kutoka kwa Maansari na wangelazimika kuwafuata Maansari. Swali la 15: Kwa nini Abubakr, Umar na Abu Ubaidah walikimbilia Saqifah na wakawavamia Maansari?


Jawabu: Ilivyokuwa Muhajirina, yaani wakuu wa Kiquraishi wanao watu wanaofuatilia nyendo za Maansari na kile kinachofanyika katika mipango yao, basi mmoja wao hao Maquraishi ambaye ni Salim aliyekuwa mtumwa wa Abu Hudhaifah alifanya haraka kuwajulisha kina Abubakr, Umar na Abu Ubaidah kuhusu mkutano huo wa siri. Basi ndipo walipokimbilia huko Saqifah ili wakawavuruge Maansari na mipango yao waliyokwisha kuipitisha na wawavamie na kuwa wao (Maquraishi) wanajua kila kitu kinachotokea wakati wao hawapo.

Swali la 16: Kwa nini Umar ibn Khatab njia nzima alikuwa akiandaa kauli itakayowakinaisha Maansari? Jawabu: Hapana shaka kwamba Umar ibn Khatab alikuwa akichelea upinzani wa Maansari, kama ambavyo alikuwa akichelea pia kwamba Maansari hawatakubali kumuweka mbali Ali (kwenye Ukhalifa) jambo ambalo litasababisha kubomoka kwa yale waliyoyapanga na kuyaandaa, hivyo basi juhudi zao zitapotea bure baada ya kuwa walithubutu kukifanya mbele ya Mtume mwenyewe na wakaharibu mipango yake yote kuhusu Ukhalifa. Kwa ajili hiyo basi Umar katika njia yake kuelekea Saqifa alikuwa akitunga nini atakachokisema ili wamuunge mkono na waikubali sera aliyoiandaa yeye Umar na wenzake. Swali la 17: Kwa nini Muhajirina waliwashinda Maansari na wakampa Abubakr Ukhalifa?


Jawabu: Yako Mambo mengi yaliyotendeka katika kuwarudisha nyuma Maansari na kuwafanya Muhajirina wafaulu. Maansari walikuwa makabila mawili yanayogombea uongozi tangu zama za jahiliya (kabla ya Uislamu), na ugomvi wao ulitulizana kwa kuwepo Mtume (s.a.w.w.) miongoni mwao. Katika kipindi hiki Mtume alikuwa kesha kufa na ummati wake unataka kuupora Ukhalifa kutoka kwa muhusika wake kisheria, basi hapo ndipo Ausi waliponyanyuka wakimpendekeza kwa ajili ya Ukhalifa kiongozi wao Sa'ad ibn Ubbadah, lakini Bashir ibn Sa'ad ambaye aliyekuwa kiongozi wa Khaz-raj akamhusudu mwana wa ammi yake na akafanya kila njia kuhakikisha kuwa Sa'ad ibn Ubbadah hatoupata Ukhalifa. Aliyavunja mapatano ya Ansari na kujiunga kwa Muhajirina na akijifanya kuwa mwaminifu na mtoa nasaha njema.


Kama ambavyo Abubakr naye aliiamsha fitna ya zama za kijahiliya kati yao alipogonga kwenye nukta dhaifu pale aliposema: "Lau jambo hili tutawapa ukoo wa Ausi, ukoo wa Khaz-raji hawatoridhia na tutapowapa Khaz-raji basi Ausi nao hawatoridhia." Kisha akawapa tamaa ya kuwagawia sehemu ya serikali akasema: "Sisi ni maamiri nanyi muwe mawaziri na kamwe hatutayaacha maoni yenu."

Hatimaye kwa kutumia akili alifanya hila ya kuwa yeye ni mtoa nasaha mwaminifu kwa umma wakati yeye alipojitoa na kuonyesha kutokuwa na haja ya Ukhalifa na kwamba yeye hapendelei kuwa Khalifa akasema: "Mchagueni mumtakaye kati ya watu hawa wawili yaani Umar au Abu Ubaidah A'mir ibn Jarrah." (Wakati huo) mipango ilikuwa imeandaliwa vizuri na utaraibu (huo) ulifaulu, basi Umar na Abu Ubaidah wakasema: "Haiwezekani sisi kukutangulia wewe, wewe ni wa mwanzo kusilimu, nawe ndiwe mwenzi wa Mtume katika pango basi kunjua mkono wako tule kiapo cha utii kwako. Hapo hapo Abubakar akanyoosha mkono wake kutokana na maneno haya, na Bashir ibn Sa'ad kiongozi wa kabila la Khaz-raj alitangulia kumpa baia Abubakr na wengine waliobakia nao wakafuatia isipokuwa Sa'ad ibn Ubbadah.


Swali la 18: Ni kwa nini Sa'ad ibn Ubbadah alikataa kumbai Abubakr kisha Umar naye akamtishia kumuua Sa'ad? Jawabu: Maansari walipotoa baia na wakamkimbilia Abubakr kwa ajili ya kutaka kujipatia heshima na ujamaa kwa Khalifa huyo, Sa'ad alikataa kutoa baia na alijaribu kwa juhudi zake kuwazuwia watu wake wasitoe baia, lakini alishindwa kwa sababu alikuwa mgonjwa sana kalala kitandani na sauti yake haisikiki, hapo ndipo Umar aliposema: "Muuweni, hakika huyu ndiye mwenye fitna (muuweni) ili mzizi wa upinzani ung'olewe ili asije akapinga baia hii mtu mwingine, kwani huyu atavunja umoja wa Waislamu na atasababisha kugawanyika kwa umma na ataleta fitina."