WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Uthman ibn A'ffaan anafuata sunna ya jamaa zake katika kuyapinga maandikoya Qur'an na Sunna ya Mtume
Huenda Uthman ibn Affaan alipomuahidi Abdur-rahman ibn A'uf mwanzoni tu mwa baia yake ya Ukhalifa kwamba atawahukumu kwa mujibu wa sunna ya Makhalifa wawili Abubakr na Umar, alikuwa akikusudia kwamba naye atajitahidi kama walivyojitahidi wao kina Umar kugeuza maandiko ya Qur'an na matamko ya Sunna ya Mtume kama walivyokuwa wakifanya kina Umar. Yeyote atakayefuatilia sera yake (Uthman) zama za Ukhalifa wake, atamkuta yeye kuwa alikwenda mbele zaidi katika ijtihadi mpaka akawasahaulisha watu ijtihadi za jamaa zake kina Abubakr na Umar.

Mimi sitaki kurefusha maudhui hii ambayo imejaa ndani ya vitabu vingi vya historia vya hapo zamani na sasa hivi, yakiwemo yale aliyoyazua Uthman miongoni mwa mambo ya kutisha yaliyosababisha mapinduzi dhidi yake na yakaangamiza maisha yake. Lakini nitafupisha kwa kutoa mifano michache ili imdhihirikie msomaji na kila anayetafiti yale waliyoyazusha vvenye kutetea ijtihadi ndani ya dini ya Muhammad (s.a.w.w.). A. Muslim amethibitisha ndani ya sahih yake katika kitabu Salatil-musafir kutoka kwa Aisha amesema: "Mwenyezi Mungu alifaradhisha rakaa mbili wakati (wa mwanzo) alipoifaradhisha (sala) kisha akaikamilisha (kwa rakaa zingine mbili) ikiwa ni nyumbani, na ikathibitishwa sala ya safari kwa ile faradhi ya mwanzoni."

Kama ambavyo Muslim ameandika katika mlango huo huo uliotajwa hapo juu kutoka kwa Ya'ala ibn Umayyah amesema: "Nilimwambia Umar ibn Khatab, Si vibaya kwenu ninyi kupunguza sala ikiwa mtachelea kukushambulieni wale waliokufuru, lakini sasa watu wako katika amani." Umar akasema: "Nilishangazwa na yaliyokushangaza wewe, ndipo nilipomuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kuhusu jambo hilo akasema: Hiyo ni zawadi Mwenyezi Mungu amekuzawadieni, basi ikubalini zawadi yake."


Kama ambavyo Muslim ameandika ndani ya sahihi yake ndani ya Kitabul-musafirina waqas-riha kutoka kwa ibn Abbas amesema: "Mwenyezi Mungu amefaradhisha sala kwa ulimi wa Mtume wenu kuwa ni rakaa nne nyumbani, na safarini rakaa mbili na katika khofu rakaa moja." Vile vile Muslim ndani ya sahih yake amethibitisha kutoka kwa Anas ibn Malik amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akitoka mwendo wa maili tatu au Far-sakh tatu, husali rakaa mbili." Na kutoka kwake tena amesema: "Tulitoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu mjini Madina mpaka Maka, basi Mtume akasali rakaa mbili mpaka aliporudi, nikasema: Alikaa siku ngapi Maka? Akasema siku kumi." Kwa kupitia hadithi hizi ambazo amezithibitisha Muslim ndani ya sahih yake inatubainikia kwamba, aya tukufu iliyoshuka kuhusu kupunguza sala katika safari, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliifahamu na kisha akaifasiri kwa kauli na matendo ya kwamba ni ruhusa aliyoizawadia Mwenyezi Mungu kwa Waislamu na wanalazimika kuikubali."


Na kutokana na hali hii yanatenguka madai ya Ad-dawaalibi na walio kama yeye katika kumtakia udhuru Umar na kuyapitisha makosa yake kwamba yeye aliangalia sababu asilia ya hukumu na hakuangalia dhahiri yake, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alimfundisha Umar lengo la kushuka aya ya kupunguza sala pale Umar aliposhangaa kwamba maandiko yaliyothibiti haisimami juu ya sababu yake ya asili, kwa hiyo sala itapunguzwa hata kama watu wako katika amani na hawachelei kushambuliwa na wale waliokufuru.

Lakini Umar, yeye anayo maoni mengine (ayajuwayo) siyo yale anayoyaona Ad-dawalibi na wanachuoni wa Kisunni kwa mujibu wa dhana zao nzuri. Na hebu tumuangalie Uthman ibn A'ffan, hapana shaka naye ni mwingine anayejitahidi dhidi ya maandiko ya Quran na Sunna, mpaka naye anaunga msafara wa Makhalifa kwani mambo yalipomkalia vizuri (kwenye Ukhalifa) akaikamilisba sala katika safari na akaigeuza kuwa rakaa nne badala ya mbili. Kwa hakika nimekuwa nikijiuliza sababu za kuzibadilisha faradhi hizi na kuongeza ndani yake, kwani ni jambo gani lililopelekea hila hii, na sikuona isipokuwa alikusudia kuwavuruga watu na hasa Banu Umayyah (wamwone) kuwa yeye ni mwema na ni mchamungu kuliko Muhammad, Abubakr na Umar. Muslim ameandika katika sahih yake ndani ya mlango wa sala ya msafiri na kupunguza sala huko Mina amesema: "Imepokewa kutoka kwa Salim ibn Abdallah, kutoka kwa Baba yake, naye kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwamba yeye Mtume alisali Mina na sehemu nyingine rakaa mbili nao Abubakr na Umar hivyo hivyo, na Uthman (alisali) rakaa mbili hapo mwanzoni mwa Ukhalifa wake kisha baadaye alikamilisha (rakaa) nne." Kama iliyokuja katika sahih Muslim vile vile kwamba, Az-zuhri amesema; "Nilimwambia U'r-wah ana nini Aisha mbona anakamilisha katika safari?" Akasema: "Bila shaka yeye amebadilisha kama alivyobadilisha Uthman."


*Basi hivi ndivyo ilvyofanywa dini ya Mwenyezi Mungu katika hukumu zake na maandiko yake (inafanywa kuwa) ni yenye kufuata mabadiliko ya wabadilishaji na tafsiri za wenye kufasiri. B. Kama ambavyo Uthman alivyojitahidi kwa maoni yake kuyaunga mkono yale aliyoyafanya Umar, miongoni mwa hayo ni kuharamisha Mut'atul-hajji na ni kama alivyoiharamisha ndoa ya Mut 'a Bukhari ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul hajji mlango wa Tamattu'i na Iqran, kutoka kwa Mar-wan ibn Al-hakam amesema: "Niliwashuhudia Uthman na Ali (r.a.). na Uthman (alikuwa) akikataza Tamatu'i na kuzikusanya baina yao, basi Ali alipoona hayo alihirimia zote Umra na Hijja na akasema siwezi kuacha Sunna ya Mtume (s.a.w.w.) kutokana na kauli ya mtu fulani." Naye Muslim ameandika ndani ya sahih yake katika Kitabul-hajji Babu Jawazit-tamattu'i kutoka kwa Said ibn Al-musayyab amesema: "Ali na Uthman (r.a.) walikutana huko Us-fan, basi Uthman akawa anakataza Tamattu'i au Umrah, Ali akasema; unataka kulifanya nini jambo alilolitenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (unataka) kulikataza? Uthman akasema: "Achana nasi." Ali akasema, "Hakika siwezi kukuacha." Basi Ali alipoyaona hayo yeye akazihirimia zote pamoja."


Naam, huyu ndiye Ali mwana wa Abu Talib. amani ya Mwezi Mungu imshukie, hakuwa mwenye kuiacha Sunna ya Mtume (s.a.w.) kwa ajili ya kauli ya mtu fulani miongoni mwa watu, na ile riwaya ya tatu inatufidisha kwamba, mzozo uliopita baina ya Ali na Uthman na kauli ya Uthman aliposema Achana nasi, yapo mambo ambayo miongoni mwake ni kwenda kwake kinyume (yeye Uthman) katika kila kitu na kutokufuata yale ambayo Ibn Ammi yake (Mtume s.a.w.) kama ambavyo riwaya hiyo imekatwa kwani inasema: "Ali akasema hakika mimi siwezi kukuacha." Lakini basi alipoyaona hayo!! Je, ni mambo gani aliyoyaona Ali? Hapana shaka kwamba huyo (Uthman) pamoja na Ali kumkumbusha Sunna ya Mtume yeye aling'ang'ania kwenye maoni yake kuipinga Sunna ya Mtume na akawazuwia watu wasifanye Tamattu'i na hapo ndipo Imam Ali alipompinga Uthman na akahirimia zote pamoja yaani Hijja na Umrah. C.Kama ambavyo Uthman alijitahidi vile vile kuhusu vifungu vya sala, basi alikuwa hasomi Takbira wakati akisujudu wala wakati anyanyukapo kutoka kwenye sijida.


Imam Ahmad ibn Hanbali ameeleza ndani ya Musnad yake juzuu ya nne ukurasa 440 kutoka kwa Imran ibn Hasin amesema: "Niliswali nyuma ya Ali sala iliyonikumbusha sala niliyosali pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu na Makhalifa wawili, akasema: Basi nikaenda nikasali pamoja naye, akawa husoma Takbira kila anaposujudu na kunyanyua kichwa chake kutoka kwenye rukuu, nikasema, Ewe baba Najiid ni nani wa mwanzo kuiacha Takbira hiyo, akasema, Uthman (r.a.) wakati alipozeeka na sauti yake kuwa dhaifu aliicha.

Naam, hivi ndivyo ilivyopotezwa Sunna ya Mtume na ikageuzwa (toka mahala pake) ikawa ni sunna ya Makhalifa na sunna ya kifalme na ni sunna ya kisahaba na sunna ya Banu Umayyah na sunna ya Banu Abbas na zote hizo ni Bid'a zilizozushwa (na kutiwa) ndani ya Uislamu, basi (ifahamike kuwa) kila uzushi ni upotovu na kila upotovu (malipo yake) ni motoni kama alivyosema Mtume (s.a.w.w.) Kwa ajili hiyo utaona leo hii namna na aina nyingi za sala za Waislamu, utawadhania wako pamoja lakini nyoyo zao ziko mbali mbali, kwani wanajipanga katika mstari ili wasali katika safu moja, basi utamuona huyu amenyoosha mikono yake na yule naye kakunja na mwingine naye anastaili yake peke yake katika kukunja mikono, kwani yeye anaweka mikono yake juu ya kitovu na au moyo Na mwingine utamuona amegusanisha nyayo zake na mwingine ameziachanisha. Almuradi kila mmoja anaamini kuwa yeye ndiyo yuko kwenye haki, na ukiyazungumzia hayo utaambiwa: "Ewe Bwana hizo ni aina (za sala) ambazo hazina umuhimu, wewe sali upendavyo la muhimu ni kuwa unasali basi!!


Naam, hii ni sawa kwa kiasi fulani, kwani muhimu ni kusali lakini ni lazima sala hiyo ikubaliane na sala ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), bila shaka Mtume amesema "Salini kama munionavyo mimi ninasali." Basi tunalazimika kujitahidi kuitafuta sala ya Mtume (s.a.w.) kwani sala ni nguzo ya dini. D. Uthman aliyestahiwa na Malaika wa Mwenyezi Mungu. Amesema Al-Balaadhuri ndani ya Ansabid-ashraf juz. 5 uk. 54. Habari za kifo cha Abudharri kutoka huko Rubdhah zilipomfikia Uthman alisema: "Mwenyezi Mungu amemrehemu (Abudharri)." Ammar ibn Yasir akasema: "Naam, amrehemu Mwenyezi Mungu kuliko nafsi zetu wote." Uthman akamwambia Ammar: Ewe muuma kwa meno dhakari ya baba yake, unadhani nimejuta kwa kumfukuza kwangu Abudharri." Kisha Uthman akaamuru aangushwe chini na alazwe chali na akasema, Nenda kajiunge mahali pake." Alipokuwa akijiandaa kutoka wakaja Banu Makhzuum kwa Imam Ali wakamwomba akaseme na Uthman juu ya Ammar, basi Imam Ali akamwambia, "Ewe Uthman mche Mungu bila shaka ulimfukuza (kutoka hapa Madina) mtu mwema miongoni mwa Waislamu akafia huko ulikomfukuzia, kisha wewe sasa hivi unataka kumfukuza mtu mfano wake?"

Yakapita baina yao mazungumzo mpaka Uthman akamwambia Ali, "Basi wewe unastahiki mno kufukuzwa kuliko yeye." Ali akasema, "Ukipenda nifukuze." Hapo wakakusanyika Muhajirina kwa Uthman wakamwambia, "Ikiwa kila mtu anapokusemesha, basi wewe humtoa na kumfukuza hapana, jambo hili haliwezekani" Hakumfukuza Ammar." Katika riwaya ya Ya'aqubi ndani ya tarikh yake juz. 2 uk.147 ameandika kwamba: Ammar ibn Yasir alimsalia Miqdad na akamzika wala hakumruhusu Uthman kufanya hilo kutokana na usia wa Miqdad, basi Uthman alimkasirikia sana Ammar na akasema, "Namuonya, Ole wangu juu ya mtoto wa mwanamke mweusi. nilikuwa namjuwa vilivyo."


Hivi kweli inawezekana kwa mtu mwenye heshima kama hiyo ambaye malaika walimstahi aseme maneno machafu na hasa kuwahusu waumini wema? Uthman hakutosheka kumtukana Ammar na kumwambia maneno machafu kama ule usemi wake usemao: "Ewe minima meno dhakari ya babake.'' Kiasi kwamba aliwaamrisha vijana wake wamkamate Ammar na wakamshika miguu na mikono yake kisha Uthman akampiga Ammar kwa miguu yake ambayo alikuwa amevaa buti (akampiga) mbeleni na akamjeruhi. Kipindi hicho Ammar alikuwa keshakuwa mtu mzima tena amedhoofika, na kutokana na kipigo hicho alizimia. Hiki ni kisa mashuhuri kwa wanahistoria,[160] matendo haya yalifanyika wakati kundi fulani la Masahaba walipoandika barua na kumuamuru Ammar aifikishe kwake (Uthman). Ni hivyo hivyo Uthman alivyomfanyia Abdallah ibn Mas-ud pale alipomuamuru mmoja wa askari wake aliyekuwa akiitwa Abdallah ibn Zum-a'h. Huyu Abdallah ibn Zum-a'h alimbeba Abdallah ibn Mas-u'ud mpaka akamfikisha kwenye mlango wa msikiti akamtupa chini akavunjika mbavu.[161] Hapakuwa na sababu yoyote ile isipokuwa tu ni kwamba, Abdallah ibn Mas-u'd alimpinga Uthman kwa tendo lake la kuwapa waovu wa kibanu Umayyah mali za Waislamu (kwa wingi) bila hesabu.


Hatimaye yalifanyika mapinduzi dhidi yake na yakatokea yaliyotokea, Uthman akauawa na watu wakazuwia asizikwe kwa muda wa siku tatu. Hatimaye walikuja watu wanne miongoni mwa Banu Ummayyah kutaka kumsalia, baadhi ya Masahaba wakawazuwia kumsalia, basi mmoja wao akasema: "Mzikeni hivyo hivyo, kwani Mwenyezi Mungu na Malaika wake wamekwisha kumsalia." Masahaba wakasema: "Wallahi kamwe hatozikwa kwenye makaburi ya Waislamu." Wakamzika mahali palipokuwa pakiitwa (Houshi Kaukah) ambako Mayahudi walikuwa wakizika maiti wao, na Banu Umayya walipotawala wakaiingiza sehemu hiyo (ya Houshi Kaukah) ndani ya Baqii.


Hii ni sehemu ndogo tu ya historia ya Makhalifa watatu (yaani) Abubakr, Umar na Uthman, nayo pamoja na kuwa ni ndogo, hiyo ni kwa sababu tumekusudia kufupisha na kutoa baadhi tu ya mifano, lakini inatosheleza kuondoa pazia kuhusu zile fadhila zinazodaiwa na sifa zilizozushwa ambazo wao hao Makhalifa watatu hawazitambui wala hawakupata kuziotea ndoto zama za uhai wao.


Swali linaloulizwa hapa ni hili lifuatalo: Masunni wanasemaje juu ya ukweli huu? Jawabu liko kwa wenye kumbukumbu nalo ni: Ikiwa ukweli huu munaujua na hamuupingi kwa sababu vitabu vyenu ndivyo vilivyothibitisha juu ya ukweli huu pamoja na kuunyamazia, basi mtakuwa mmeuporomosha huo uzushi uliozuliwa kuhusu Ukhalifa huo unaosemekana kuwa ni wenye uongofu. Na mkiwa mwakanusha ukweli huu na hamuamini kuwa ni ukweli, mtakuwa mmeviangusha vitabu vyenu ambavyo mnaamini kuwa ni vitabu sahihi, vitabu ambavyo vimeandika maelezo haya. Na kwa kufanya hivyo mtakuwa mmezitupa chini itikadi zenu zote.