WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Abubakr anampa ukhalifa jamaa yake Umar, na anakhalifu maandikoyaliyo wazi kuhusu jambo hilo.
Amesema Imam Ali kuhusiana na suala la Ukhlifa: "Ama Wallahi ameuvaa (Ukhalifa) mtoto wa Abu Quhafa hali ya kwa anajua kabisa kwamba nafasi yangu katika huo Ukhalifa ni kama nafasi ya mpini ulioko kwenye jiwe la kusagia nafaka." Akielezea kwa njia ya kinaya Imamu (a.s.) anasema: "Hububujika kutoka kwangu fadhila kwa vile Mungu alinienzi kwa kuniweka karibu na materemkio ya wahyi, hivyo basi nilijizuia nikakaa mbali nao, nikawa nafikiri kati ya kuingia vitani hali nikiwa mikono mitupu, au nivute subira katika giza lililoshona hakika mtu mzima huzeeka, na mtoto huwa kijana. Muumini atataabika kwa juhudi kubwa kubakia na imani safi katika hali hiyo mpaka akutane na Mola wake." Anaendelea kusema, "Niliona kusubiri ni bora na ni hekima, basi nikasubiri hali katika macho kuna tongo tongo na shingoni kuna mwiba umenasa, naouna urithi wangu nimenyang'anywa. Wa kwanza akaenda kisha akampasia mtoto wa Khatab baada yake, ajabu ilioje kwamba yeye (Abubakr) alitaka kujitoa katika ukhalifa alipokuwa hai na ampasie mwenzake ashike baada ya kifo chake ili kudhibiti walichokigawa nusu mbili, kila mmoja akawa mgumu hagusiki na anajikwaakwaa akitaka udhuru."[145]


Kila mwenye kuhakiki na kutafiti atafahamu kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliutangaza ukhalifa na kumbainisha Ali ibn Abi Talib kabla ya kufa kwake kama ambavyo. wengi wa Masahaba wanalifahamu hilo na wakitanguliwa na Abubakr na Umar.[146] Na ndiyo maana Imam Ali alikuwa akisema. "Hakika yeye anajua kabisa kwamba, nafasi yangu katika huo ukhalifa ni kama nafasi ya mpini ulioko kwenye jiwe la kusagia." Na huenda hilo ndilo lililowafanya Abubakr na Umar wazuwie kusimuliwa hadithi za Mtume (s.a.w.w.) kama tulivyotangulia kueleza katika mlango uliopita, na wakashikamana na Qur'an kwa kuwa Qur'an japokuwa ndani yake (imo) aya ya Wilayah lakini jina la Ali halikutajwa wazi wazi kama ilivyo ndani ya hadithi za Mtume kwa mfano Mtume (s.a.w.w.) aliposema "'Yeyote ambaye mimi nilikuwa mtawala wake, basi huyu Ali ni mtawala wake." Na alisema Mtume: "Ali anatokana nami, nami natokana naye, naye ni mtawala wa kila muumini baada yangu."[147]

Na kwa ajili hiyo tunafahamu kiwango cha mafanikio ya sera aliyoiandaa Abubakr na Umar katika kuzuwia na kuchoma moto hadithi za Mtume (s.a.w.w.), na wakaweka vizibo juu ya vinywa ili Masahaba wasizizungumze hadithi hizo kama tulivyotangulia kueleza ndani ya riwaya ya Qurdhah ibn Ka'ab. Vizuizi hivyo viliendelea kwa robo karne ambao ni muda wa utawala wa Makhalifa watatu hadi pale alipokuja Imam Ali kwenye Ukhalifah akawashuhudisha Masahaba ile hadithi ya Ghadir.


Masahaba thelathini walishuhudia, kumi na saba miongoni mwao ni katika wale waliopigana vita ya Badri.[148] Hii dalili wazi inayoonesha kwamba, Masahaba hawa thelathini wasingeweza kuzungumza hivyo lau kama Amirul-Muuminina Ali asingewataka kufanya hivyo, na lau Ali asingekuwa Khalifa na ameshika nguvu za utawala, basi woga ungewafanya wakakaa chini kimya wasishuhudie hilo kama yalivyotokea hayo kwa vitendo kutoka miongoni mwa baadhi ya Masahaba ambao hofu na husuda iliwakalisha chini wasishuhudie. Mfano wa hao ni Anas ibn Malik, Bar-raa ibn Azib, Zaid ibn Ar-qam na Jarir ibn Abdillah Al-bajali.[149] Kwa tendo lao hilo la kunyamaza waliwapatwa na madhara makubwa kutokana na dua ya Imam Ali ibn Abi Talib. [150] Na wala Abu Turab (Imam Ali a.s.) hakuneemeka na Ukhalifa huo kwani siku zake zote zilikuwa ni mitihani, fitina, njama na vita dhidi yake vilivyoelekezwa kwake kutoka kila pande. Zilijitokeza zile chuki na mafundo ya zama za Badri, Hunain na Khaibar, mpaka alipouawa kishahidi nahizo Sunna za Mtume hazikupata sikio lenye kuzisikiliza mbele ya hao waliotengua na kuvunja viapo vyao, bali walitoka katika dini na ni waongo (waliotumia dini kwa maslahi yao) ambao walikwisha zowea kutenda maovu, rushwa na kuipenda dunia katika zama za Ukhalifa wa Uthman. Kwa ajili hiyo mwana wa Abu Talib hakuweza kurekebisha maovu yaliyotendwa kwa robo karne katika muda wa miaka mitatu na minne ila kwa kuiangamiza nafsi yake, na haiwezekani yeye kuiangamiza nafsi yake kwani yeye anasema:


"Wallahi mimi nafahamu mno ni kitu gani kitakachowafanyeni muwe wema, lakini siwezi kukurekebisheni kwa kuiangamiza nafsi yangu." Na haukupita muda mrefu isipokuwa Muawiyah ibn Abi Sufiyan aliukalia ukhalifa, akaziendeleza sera zile kama tulivyotangulia kusema, akazuwia hadithi isipokuwa zile zilizokuwepo zama za Umar. Yeye alikwenda mbele zaidi kuliko hivyo, akateua kikundi miongoni mwa Masahaba na Tabiina ili waweke hadithi (za uzushi) na hapo ndipo Sunna ya Mtume (s.a.w.w.) ikapotea ndani ya bahari hiyo kubwa ya hadithi za uzushi ziliundwa, na ngano zinazohusu fadhila za Masahaba. Baada ya hapo Waislamu wakaendelea hivyo kwa karne nzima wakiwa ndani ya sunna za Muawiyah na zikawa ndizo zinazofuatwa na Waislamu wote. Tunaposema sunna za Muawiyah, maana yake ni sunna aliyoiridhia Muawiyah miongoni mwa matendo ya Makhalifa watatu, Abubakr, Umar na Uthman na yale aliyoyaongeza yeye na wafuasi wake miongoni mwa uzushi na uongo, ikwemo kumlaani na kumtukana Imam Ali na watu wa nyumba yake na wafuasi wake miongoni mwa Masahaba wema.


Kwa sababu hiyo basi, ninarudia kukariri kwamba,"Abubakr na Omar walifanikiwa katika sera hii ya kufuta sunna ya Mtume kwa madai ya kuirejea Qur'an." Bila shaka utaona leo hii baada ya kupita karne kumi na nne, pale utakapotoa hoja kwa sunna madhubuti ya Mtume kuthibitisha kwamba, Mtume (s.a.w.w.) alimbainisha Ali kuwa ndiyo khalifa wake, hapo hapo utaambiwa, "Achana na sunna ya Mtume ambayo ndani yake kunahitilafu nyingi, kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu na kitabu cha Mwenyezi Mungu hakikutaja kwamba Ali ndiyo khalifa wa Mtume bali kimesema kuwa, mambo ya Waislamu yanakwenda kwa kushauriana."


Na hii ndiyo hoja yao, kwani sijazungumza na yeyote miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni isipokuwa, Shuraa ndicho kitambulisho chao na ndiyo mila yao. Pamoja na kwamba ukhalifa wa Abubakr ulitimia bila kutegemewa, na eti Mwenyezi Mungu aliwakinga Waislamu kutokana na shari, lakini cha ajabu ni kwamba haukupatikana kwa kushauriana kama wanavyodai baadhi yao, bali ulipatikana kwa ghafla na tena kwa nguvu, shinikizo na vitisho, na wengi miongoni mwa Masahaba bora waliupinga wakiongozwa na Imam Ali ibn Abi Talib, Sa'ad ibn Ubbadah, Ammar ibn Yasir, Salman, Miqadad, Zubair, Abbas na wasiokuwa hawa kama walivyoeleza wanahistoria wengi waliozungumzia tukio hili.


Hebu tulipuuze tukio hili na tuone Abubakr alivyomtawaza Umar baada yake na tuwaulize Masunni ambao wanategemea msingi wa mashauriano. Je, ni kwa nini Abubakr alimbainisha Umar kuwa khalifa wake na akawalazimisha Waislamu wakubali bila ya kuwaachia washauriane kati yao kama mnavyodai? Ili ikubainikie zaidi, na kama ilivyo kawaida yetu kwamba hatutoi ushahidi isipokuwa kwa kutumia vitabu vya Masunni, sasa namletea msomaji namna Abubakr alivyomtawalisha jamaa yake. Ibn Qutaibah ameandika ndani ya kitabu chake; Tarikhul-khulafai katika mlango unaohusu maradhi ya Abubakr na kumtawaza kwake Umar (r.a.) amesema: ...Kisha akamuita Uthman ibn Affan akamwambia: "Andika usia wangu." Akamtamki na Uthman akaandika; "Bismillahir-Rahmanir-Rahiim, huu ndiyo usia aliousia Abubakr ibn Abi Quhafah mwishoni mwa uhai wake duniani hali yakuwa anaondoka, na ni mwanzoni mwa uhai wake wa akhera akiwa ndiyo anaingia ndani yake. Hakika mimi nimemtawalisha juu yenu Umar ibn Khatab, iwapo mtamuona kuwa ni muadilifu miongoni mwenu basi hiyo ndiyo dhana yangu kwake na ndiyo matarajio yangu ndani yake, na iwapo atabadili na kugeuza mimi nilichokikusudia ni kheri na sijui ghaibu na hivi karibuni watajuwa wale waliodhulumu ni mgeuko gani watakaogeuka." Kisha akaufunga waraka huo na akampa.


Muhajirina na Ansari wakaingia kwake waliposikia kwamba yeye Abubakr amemtawalisha Umar wakasema: "Tunakuona umemtawalisha Umar juu yetu na bila shaka wewe unamfahamu na unaujua ukali wake kwetu sisi hali yakuwa wewe uko nasi basi itakuwaje utakapotoweka nawe utakutana na Mwenyezi Mungu na atakuuliza, sasa utasemaje?" Abubakr akasema: "Ikiwa Mola wangu ataniuliza bila shaka. nitasema kuwa, nimemtawalisha juu yao mtu ambaye ni mbora wao katika nafsi yangu.[151] Kuna baadhi ya wanahistoria kama vile Tabari na Ibnul-athir wanaeleza kwamba, Abubakr alipomuita Uthman ili aandike usia wake, alizimia wakati akimtamkia, basi Uthman akaliandika jina la Umar ibn Khatab.


Alipozindukana akasema soma uliyoyaandika, akasoma na akataja jina la Umar, basi Abubakr akasema: "llikuwaje ukafanya hivi?" Uthmani akasema, "Hukuwa ni mwenye kumvuka Umar." Abubakr akasema, "Umepatia." Alipomaliza kuandika watu fulani miongoni mwa Masahaba waliingia kwa Abubakr, akiwemo Tal-ha na akamwambia Abubakr, "Utasema nini kwa Mola wako kesho nawe umekwisha mtawalisha juu yetu mtu mkali na msusuavu, nafsi za watu zitatawanyika na nyoyo zitamkimbia." Abubakr akasema: "Niegemesheni." alikuwa kalala, wakamuegemesha, akamwambia Tal-ha, "Hivi unanikhofisha Mwenyezi Mungu atakaponiuliza jambo hilo kesho? Nitamwambia kuwa, nilimtawalisha juu yao mbora wa watu wako.[152]


. Na ikiwa wanahistoria wanaafikiana juu ya Abubakr kumtawalisha Umar bila ya kuwashauri Masahaba, basi tunaweza kabisa kusema kwamba, "Yeye alimtawalisha Umar bila ridhaa ya Masahaba na hali ya kuwa wamekasirika." Na ni sawa sawa Ibn Qutaibah aliposema kuwa, Muhajirina na Ansari waliingia kwa Abubakar wakambwambia: "Bila shaka wewe unafahamu ukali wake kwetu sisi." Au kama alivyosema Tabari kwamba, "Waliingia kwa Abubakar watu fulani miongoni mwa Masahaba akiwemo Tal-ha na akamwambia Abubakr, "Utasema nini kwa Mola wako kesho wakati wewe umemtawalisha juu yetu mtu mkali na msusuavu, nafsi za watu zitatawanyika na nyoyo zitamkimbia." Basi matokeo yake ni ya aina moja nayo ni kwamba mambo ya Masahaba hayakuwa ya mashauriano na hawakuwa wameridhia kutawalishwa Umar, jambo hilo alililazimisha Abubakr bila ya kuwashauri.


Kilichotokeo kile kile ambacho Imam Ali (a.s.) alikizungumza wakati alipolazimishwa na Umar ibn Khatab kumbai Abubakr ambapo Imam Ali alisema, "Mnufaishe leo hii naye kesho atakurudishia." Hali hii moja kwa moja ndiyo ile aliyoisema mmoja wa Masahaba kumwambia Umar ibn Khatab pale alipotoka na ile barua ambayo ndani yake umo usia wa ukhalifa, yule Sahaba akamwambia, "Ewe Baba Hafsi kuna nini humo ndani ya barua hiyo?" Umar akasema: "Sifahamu, lakini mimi nitakuwa wa kwanza kusikiliza na kuitii." Basi yule mtu akasema: "Lakini mimi Wallahi najua kilichomo, wewe ulimtawalisha kipindi kilichopita basi na yeye amekutawalisha mwaka huu."[153] Hii inatubainikia wazi kwamba, hapana shaka ndani yake kuwa, ule msingi wa Shuraa (mashauriano) ambao Masunni wanaupigia ngoma, hauna maana kwa Abubakr na Umar au kwa maelezo mengine ni kwamba Abubakr ndiyo wa kwanza kuubomoa msingi huu na kuupuuza na kufungua mlango kwa watawala wa Kibanu Umayyah waurudishe kuwa ni Ufalme wa Kaisari.


Watoto wanarithiana na baba zao, na vile vile ndiyo walivyofanya Banu Abbas baada ya Banu Umayyah, na hiyo nadharia ya Shuraa ikabaki kuwa ni ndoto inayowadanganya Masunni, haikuthibitika hapo zamani na wala haitathibitika. Jambo hili linanikumbusha mazungumzo yaliyofanyika kati yangu na mwanachuoni fulani miongoni mwa wanachuoni wa Kiwahabi kutoka Saudia ndani ya Msikiti mmoja mjini Nairobi Kenya. Mazungumzo yetu yalihusu utata wa ukhalifa, nami nilikuwa nikitetea maandiko yanayohusu ukhalifa na kwamba jukumu lote (la kuteua khalifa) ni la Mwenyezi Mungu na huliweka mahala atakapo na watu hawana hiyari na hawawezi kuliingilia jambo hilo.


Amma Mwanachuoni huyo yeye alikuwa akitetea shuraa kwa nguvu zote na pembeni yake lilikuwepo kundi la wanafunzi ambao wanachukua elimu kwake na wakimuunga mkono katika kila alisemalo kwa madai kwamba hoja zake ni kutoka ndani ya Qur'an Tukufu, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake (s.a.w.): "Washauri katika jambo." Na anasema tena: "Na jambo lao ni kushauriana kati yao." Niligundua ya kwamba mimi ninashinikizwa na jamaa kwa kuwa wao wamejifunza kutoka kwa waalimu zao fikra zote za Kiwahabi, kama nilifahamu pia kwamba, wao hawawezi kukubali kusikiliza hadithi sahihi na wanang'ang'ania baadhi ya hadithi walizozihifadhi na nyingi ya hizo ni hadithi zilizozushwa (na kusingiziwa kuwa Mtume alisema hivyo) basi hapo nilikubaliana na msingi wa Shuraa nikawaambia wanafunzi hao na waalimu wao kama ifuatavyo: "Je, hivi ninyi mnaweza kuitosheleza serikali ya Mtukufu Mfalme (wa Saudia) juu ya msingi wa Shuraa ulioko kwenu mpaka (Mfalme), ajiondoe kwenye utawala wake na afuate viongozi wenu bora waliopita na awaachie Waislamu hilo bara Arabu likiwa na uhuru wa kuchagua kiongozi wao? Mimi sidhani kama (Mfalme huyo) atafanya hivyo, kwani baba zake na babu zake hawakumiliki ukhalifa peke yake bali bara Arabu nzima pia imekuwa ni milki yao mpaka ardhi yote ya Hijazi wakaipa jina la Mamlaka ya Saudia.


Basi hapo ndipo aliposema mwanachuoni wao mkuu kuwa: "Sisi hatujishughulishi na mambo ya kisiasa, sisi tumo ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo ameamuru litajwe jina lake na paswaliwe ndani yake. Mimi nikasema: "Je, hali hiyo hata kwa msomi mwenye maarifa?" akasema: "Ndiyo, sisi hapa tunawafunza namna hiyo vijana. Mimi nikasema: "Sisi tulikuwa katika uchambuzi wa kielimu." Akasema: "Bila shaka wewe ndiwe uliyeuharibu (uchambuzi huo) kwa kuingiza mambo ya siasa" Basi nilitoka hapo pamoja na niliokuwa nimefuatana nao hali ya kuwa ninawasikitikia vijana wa Kiislamu ambao uwahabi umetawala fikra zao kwa kila namna mpaka wakawa ni maadui wa wazazi wao. Wazazi wao wote ni watu wanaofuata madhehebu ya Shafii, madhehebu ambayo yako karibu mno na madhehebu ya watu wa nyumba ya Mtume kama ninavyoamini mimi, (kwani hapo kabla) Masheikh walikuwa na heshima na utulivu mbele ya wasomi na wasiokuwa wasomi hasa kwa kuzingatia kwamba wengi wa Masheikh hao ni Masharifu wanatokana na kizazi kitukufu, basi hatimaye wakaja Mawahabi wakawashinikiza vijana kutokana na ufakiri wao na wakawahadaa kwa mali na nyenzo za maisha. Wakaugeuza mtazamo wao (kwa kuwaambia) kuwa wayatendayo ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu Masharifu ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu kwani (heshima hiyo waifanyayo) ni kumtukuza kiumbe. Basi hapo ndipo watoto hawa wakawa ni kero na balaa kwa baba zao, na hali kama hii kwa bahati mbaya ndiyo inayotokea katika miji mingi ya Kiislamu katika Afrika.


Hebu na turejee kwenye kifo cha Abubakr, kwani tunamkuta kabla ya kufa kwake anajuta kwa yale aliyoyatenda. Ibn Qutaibah ameandika ndani ya kitabu chake kiitwacho, Tarikhul-khulafai kauli ya Abubakr anasema: "Naam yamenifika, Wallahi sijuti isipokuwa kwa sababu ya mambo matatu niliyoyafanya, lau ningeyaacha mambo hayo nisiyafanye, Laiti mimi ningeiacha nyumba ya Ali, mapokezi mengine yanasema, Laiti nisingeifedhehesha nyumba ya Fatimah kwa jambo lolote lile japokuwa walikuwa wametangaza vita dhidi yangu, na laiti mimi ile siku ya Saqifah ya Bani Saidah ningeweka (mkono wangu) ndani ya mkono wa mmoja wao kati ya watu wawili, Abu Ubaidah au Umar akawa yeye ndiyo amir nami nikawa waziri, na laiti mimi pale o nilipoletewa Dhil-fujaat as-Sulami hali ya kuwa yu mateka, basi bora ningemuuwa kwa kumchinja au ningemuachia huru na nisinge mchoma moto.[154]


Nasi tunaongezea hapo tunasema, "Laiti ewe Abubakr usingemdhulumu' bibi Fatmah na wala usingemuudhi na usingemkasirisha, na laiti wewe ungejutia kabla ya kufa kwake na umridhishe, hayo yanaihusu nyumba ya Ali uliyoifedhehesha na ukaruhusu ichomwe moto." Ama kuhusu ukhalifa, basi laiti wewe ungewaacha jamaa zako ambao ndiyo nguzo zako (yaani) Abu-ubaidah na Umar na ukaweka mkono wako ndani ya mkono wa muhusika wake kisheria ambaye alitawalishwa na Mtume akawa yeye ndiye Amir!! Kwa kufanya hivyo ulimwengu huu tunao ushuhudia leo hii usingekuwa hivi, na dini ya Mwenyezi Mungu ingekuwa ndiyo inayoongoza ulimwengu kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu na ahadi ya Mwenyezi ni ya kweli. Ama kumuhusu Al-fujat as-Sulami uliyemchoma moto sisi tunakwambia, "Basi laiti wewe usingezichoma moto Sunna za Mtume ambazo ulizikusanya, hapana shaka ungejifunza mengi kutokana nazo kuhusu hukumu za sheria zilizosahihi na wala usingetegemea jitihada ya maoni yako.


Na mwisho, tunakwambia ukiwa juu ya kitanda cha mauti "Laiti wewe ulipofikiria juu ya kuacha ukhalifa, ungelirejesha haki (hiyo) mahala pake kwa yule ambaye mahali pake katika ukhalifa ni sawa na mahali pa mpini wa jiwe la kusagia nafaka." Na wewe unafahamu mno kuliko watu wengine juu ya ubora wake, ucha Mungu wake, elimu yake na kwamba yeye alikuwa kama nafsi ya Mtume (s.a.w.w.) na hasa kwamba yeye alikuachia jambo hilo na hakukupinga (yote hayo akikusudia) usalama wa Uislamu. Basi kwako kulikuwa na uhuru wa kuupa nasaha umma wa Muhammad (s.a.w.w.) na uuchagulie mtu ambaye atautengenezea mambo yake na kuuweka pamoja na akaufikisha kwenye kilele cha mafanikio. Na tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akusamehe madhambi yako na amridhishe bibi Fatmah, baba yake, mumewe na wanawe, kwani wewe ulimkasirisha (binti ya Mtume) aliye sehemu ya mwili wa Mtume na Mwenyezi Mungu hukasirika kwa ajili ya kukasirika kwake na huwa radhi kwa kuwa radhi kwake, kama ambavyo mwenye kumuudhi Fatmah basi hakika huwa kamuudhi Baba yake kwa mujibu wa hadithi ya Mtume (s.a.w.), na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: ''Wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, watapata adhabu kali."


Nasi tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na ghadhabu za Mwenyezi Mungu, na tunamuomba aturidhie sisi na Waislamu wote wa kiume na wa kike na waumini wote wa kiume na wa kike. Umar ibn Khattab anakipinga Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa kutumia ij tihadi yake Bila shaka khalifa wa pili anayo historia iliyojaa jitihada yake dhidi ya aya za Qur'ani tukufu zilizo wazi na Sunna tukufu ya Mtume. Masunni wanakifanya kitendo hicho (cha Umar) kuwa ni miongoni mwa sifa zake ambazo kwazo humsifia na miongoni mwao hujaribu kumtakia udhuru na kuleta taawili za kimya kimya ambazo hazikubaliki kiakili wala mantiki.

Vinginevyo basi ni vipi atakuwa yule mtu anayekipinga kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake kuwa yeye ni miongoni mwa Muj-tahidina, na hali Mwenyezi Mungu anasema: "Haiwi kwa muumini mwanaume au muumini mwanamke, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri wawe na hiyari katika shauri lao, na yeyote mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakika amepotea upotofu ulio wazi kabisa." (Qur'an, 33:36) Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wasiyohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndiyo makafiri, na wasiyohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndiyo madhalimu, na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio mafasiq (waovu)..." (Qur'an, 5:44, 45, na 47) Bukhari ameandika ndani ya sahihi yake, Kitabul-i'tisami bil-kitab was-sunnah, mlango wa kushutumu maoni binafsi na kujitwika mzigo wa kiasi, usifuate, usiseme usiyoyajua kwamba, Mtume (s.a.w.w.) amesema: "Kamwe Mwenyezi Mungu haiondoi elimu baada ya kuwapa, lakini huiondoa kutoka kwao kwa kuwafisha wanachuoni pamoja na elimu yao, basi watabakia watu wajinga watakapoulizwa nao watajibu kwa mujibu wa maoni yao, hivyo watawapoteza wengine nao watapotea."[155]


Kama alivyoandika tena Bukhari ndani ya sahihi yake katika kitabu kile kile ndani ya mlango unaofuatia: Mtume (s.a.w.w.) alikuwa haulizwi yale ambayo hajateremshiwa wahyi kuhusiana nayo isipokuwa husema kuwa sijuwi. Alikuwa hatoi jawabu mpaka ateremshiwe wahyi, na wala hakusema kwa maoni (yake) wala kwa kukisia, na hiyo ni kwa sababu ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo: "Kwa yale aliyokufunulia Mwenyezi Mungu (ndiyo uyaseme)." Na wamekwisha sema wanachuoni wa hapo kale na wa sasa hivi kwamba: "Yeyote atakayesema (lolote) kuhusu kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa kutumia maoni yake basi bila shaka atakuwa amekufuru." Na hii bila shaka ni kuhusu aya ambazo ni muhkam na ni kuhusu kauli na matendo ya Mtume (s.a.w.). Basi ni vipi kanuni hii husahauliwa pale jambo linapohusishwa na Umar ibn Khattab au mmoja wa Masahaba au mmoja wa Maimamu wa Madhehebu manne? Inakuwaje kauli (itolewayo na hao) kwa maoni yao ikipingana na hukumu za Mwenyezi Mungu iitwe Ijtihadi ambayo mtu hupata thawabu moja kwa kufanya ijitihadi hiyo endapo atakosea, na akipatia atapata thawabu mbili? Huenda msemaji fulani akasema kuwa: "Jambo hili (la kufanya ijtihadi) umma wote wa Kiislamu Masunni na Mashia umekubaliana kutokana na hadithi ya Mtume Mtukufu ipatikanayo kwao."


Mimi nasema: "Jambo hili ni sawa, lakini wametofautiana ni mahali gani panapofaa kufanya hiyo ijtihadi, kwani Mashia wanawajibisha ijtihadi katika mambo ambayo haikuja hukumu ya wazi toka kwa Mwenyezi Mungu wala kwa Mtume wake (s.a.w.) kuyahusu mambo hayo. Ama Masunni wao hawajilazimishi katika ijtihadi kwa namna hii. na kwa kuwafuata Makhalifa na viongozi wao, hawaoni ubaya kujitahidi dhidi ya maandiko (ya Qur'an wala hadithi sahihi), na bila shaka mwanachuoni mkubwa Sayyid Sharafud-din Al-musawi ameandika ndani ya kitabu chake kiitwacho, An-nassu wal-ij-tihad zaidi ya maeneo mia moja ambayo Masahaba wakiongozwa na Makhalifa watatu wa mwanzo walikwenda kinyume cha maandiko ya Qur'an na Surma zilizo wazi, basi ni juu ya wachunguzi kukisoma kitabu hicho (ili kupata ukweli huo), Na maadamu tunaichambua maudhui hii kikweli kweli, basi hatuna budi kuleta baadhi ya maandiko aliyoyakhalifu Umar ibn Khattab, na hilo imma alilifanya kwa kutoyajua maagizo hayo, na ni jambo la ajabu kwani mjinga hawezi kuhukumu akahalalisha na kuharamisha yeye mwenyewe. Mwenyezi Mungu anasema: "Na wala msiseme kwa sababu ya uongo usemwao na ndimi zenu (kwamba) hii ni halali na hii ni haramu, msije mkamzulia Mwenyezi Mungu uwongo, hakika wale wamzuliao Mwenyezi Mungu uongo hawatafaulu." (Qur'ani 16:116)


Wala mjinga hawezi kusimama kwenye cheo cha Ukhalifa kwa ajili ya kuongoza umma kikamilifu. Mwenyezi Mungu anasema: "Basi je, aongozaye katika haki siye anayestahiki zaidi kufuatwa au (anastahiki) yule asiyeongoka (yeye mwenyewe) isipokuwa aongozwe? Basi mukoje ninyi, ni vipi mnavyohukumu?" (Qur'an, 10:35) Na imma Umar siyo kwamba hayajui maandiko bali anayajua, lakini alifanya ij-tihadi kwa makusudi kwa maslahi fulani na hali fulani iliyolazimika kwa mujibu wa maoni yake binafsi. Jambo hili Masunni hawalichukulii kuwa ni kufru na ni kutoka katika dini, kama itakuwa hapana budi (yeye Umar) alikuwa hakutambua kuwepo kwa watu wanaozifahamu vyema hukumu miongoni mwa watu aliokuwa nao katika zama zake, na hii siyo kweli kwa sababu ya kutambua kwake Umar kwamba, Ali (a.s.) alikuwa akikijua vyema Kitabu (cha Mwenyezi Mungu) na Sunna. Na kama si hivyo basi asingemuuliza maswali mengi magumu mpaka akafikia kusema juu ya Ali, "Lau kama siyo Ali, Umar angeangamia." Sasa basi ni kwa nini hakumuuliza juu ya mas-ala aliyojitahidi ndani yake kwa kutumia maoni yake ambayo anatambua kwamba yeye hayafahamu?


Mimi naamini kwamba, Waislamu waliohuru watakubaliana na hili, kwani aina ya ijtihadi kama hii ndiyo iliyoharibu itikadi ya Kiislamu, na ikaharibu hukumu, ikazipoteza na kusababisha wanachuoni wa umma huu wahitilafiane na kuwagawa makundi na madhehebu mengi. Kwa ajili hiyo kukawa na ugomvi na uhasama, na ndipo kulipotokea kushindwa kwa Waislamu na nguvu zao zikatoweka, wakabakia nyuma kiroho na kimazingira. Tunayo haki ya kuangalia hata kule kuwako kwa Abubakr na Umar juu ya kiti cha Ukhalifa na kumuondoa kwao muhusika wake kisheria. Sisi tunafikiria lau Abubakr na Umar wangezikusanya Sunna za Mtume na wakazihifadhi ndani ya kitabu makhususi, basi wangejichumia kheri nyingi mno wenyewe binafsi na juu ya umma na wala kusingeingia ndani ya Sunna ya Mtume yasiyokuwemo, na Uislamu kwa Kitabu chake (Qur'an) na Sunna yake, ungekuwa kitu kimoja, mila moja na umma mmoja wenye itikadi moja, na leo hii mazungumzo yetu yasingekuwa haya. Ama ilivyokuwa kwamba Sunna zilikusanywa kisha zikachomwa moto, zikazuwiwa kuandikwa na kunakiliwa japo kwa mdomo, basi huu ndiyo msiba mkubwa na hili ndilo balaa kubwa lililotupata. Lahaula wala quwwata Ilia billahil-aliyyil-adhim.


Hebu yaangalie baadhi ya maandiko yaliyo wazi ambayo Umar alifanyia ijtihadi dhidi ya Qur'an. A. Qur'an inasema: "Na mkiwa na janaba basi ogeni, na mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu ametoka chooni au mmeingiliana na wanawake na hamkupata maji, basi kusudieni (mtayammamu) udongo ulio safi." (Qur'an, 5:6) Na inavyoeleweka katika Sunna ya Mtume (s.a.w.w.) ni kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) amewafundisha Masahaba namna ya kutayamamu na Umar mwenyewe akiwepo.


Bukhari amethibitisha hilo ndani ya sahih yake, Kitabut-tayammum, mlango wa udongo safi ni udhu wa Muislamu unamtosheleza maji, amesema: Imepokewa kutoka kwa Imran amesema: "Tulikuwa safarini pamoja na Mtume (s.a.w.w.) nasi tulikwenda na tulipokuwa tuko mwishoni mwa usiku (alfajiri) tukalala usingizi, na hapana usingizi mzuri kwa msafiri kuliko huo, basi hakikutuamsha kitu isipokuwa joto la jua na wa kwanza kuamka alikuwa fulani kisha fulani, Abu Rajai akawataja majina A'uf alisahau, kisha Umar ibn Khattab (alikuwa) wa nne. Mtume alikuwa akilala haamshwi mpaka aamke mwenyewe kwani sisi hatujui kinachomtokea usingizini mwake. Basi Umar alipoamka na akaona yaliyowapata watu naye Umar alikuwa mtu msusuavu, akasema Allahu Akbar, na akapaza sauti yake kwa Takbira basi aliendelea kusema Allahu Akbar na kupaza sauti yake kwa Takbira mpaka Mtume akaamka kutokana na Takbira yake. Alipoamka, watu wakamshitakia yaliyowapata, akasema hapana kheri wala haidhuru, ondokeni, basi akaondoka Mtume akaenda siyo mbali kisha akatua na akaagiza maji ya kutawadha na pakanadiwa kwa ajili ya Sala, akawasalisha watu. Alipomaliza sala yake, mara alimuona mtu kajitenga hakusali pamoja na watu wengine, Mtume akasema: Ni jambo gani lililokuzuwia kusali pamoja na watu wengine ewe fulani? Akasema, nimepatwa na janaba na hapana maji, Mtume akasema, udongo unakutosha."[156]


Lakini Umar anasema hali akipingana na Kitabu cha Mweyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake kwamba, "Yeyote asipopata maji basi asisali" Na haya ndiyo madhehebu yake ambayo wameyasajili wanachuoni wengi wa hadithi. Muslim ameandika ndani ya sahih yake Kitabut-taharah mlango wa kutayammam, kwamba kuna mtu alimjia Umar akamwambia; "Mimi nina janaba na sikupata maji." Umar anasema: "Usisali." Ammar akasema: "Ewe Amirul-muuminina hukumbuki tulipokuwa mimi na wewe katika kikosi cha jeshi tukapata janaba na hatukuwa na maji, ama wewe hukuswali na mimi nikajigaragaza kwenye udongo na nikaswali, Mtume akasema: Ilikuwa inakutosha kupiga mikono yako juu ya ardhi kisha ukapuliza halafu ukapaka kwa mikono hiyo uso na vitanga vyako.' Umar akasema: "Muogope Mungu ewe Ammar." Ammar akasema; "Ukipenda sitaisimulia habari hiyo."


Sub-Hanallah!! Umar hakutosheka na kuyapinga maandiko yaliyowazi katika Kitabu (cha Mwenyezi Mungu) na Sunna, mpaka anajaribu kumzuwia Sahaba kwa kumpinga kufuatia maoni yake, Ammar ibn Yasir naye analazimika kumtaka radhi khalifa huyo kwa kusema: "Ukipenda sitaisimulia habari hiyo." Basi itakuwaje mimi nishangae nanyi msishangazwe na ijtihadi hii na upinzani huu, pia kung'ang'ania huku juu ya maoni ya Umar pamoja na kuwepo ushahidi wa Sahaba (kuishuhudia Qur'an) kwani Umar hakutosheka (hakukubali) mpaka kufa kwake na hali kang'ang'ania itikadi hii, na haya Madhehebu yake yaliwaathiri Masahaba wengi ambao walikuwa wakikubaliana na maoni yake, bali huenda walikuwa wakiyatanguliza dhidi ya maoni ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Muslim ametoa ndani ya sahihi yake katika Kitabut-taharah, mlango wa kutayammam katika juzuu ya kwanza ukurasa wa 192 amesema: "Imepokewa kutoka kwa Shaqiq: Nilikuwa nimekaa na Abdallah na Abu Musa, Abu Musa akasema, Ewe baba Abdur-rahman waonaje lau mtu atapata janaba na hakupata maji kwa muda wa mwezi mmoja atafanyaje kuhusu sala?"


Abdallah akasema: "Hawezi kutayammam hata kama hatopata maji kwa kipindi cha mwezi mzima." Abu Musa akasema: "Itakuwaje basi kuhusu aya hii katika sura ya Maidah inayosema, Mkiwa hamkupata maji tayammamuni udongo safi." Abdallah akasema: "Lau wataruhusiwa kutumia aya hii nina shaka maji yakiwa baridi watatayammamu kwa udongo." Abu Musa akamwambia Abdallah, "Je, hukusikia kauli ya Ammar aliposema, Mtume alinituma shughuli fulani, basi huko nikapatwa na janaba nikajigaragaza kwenye udongo kama vile mnyama anavyojigaragaza, kisha nikaja kwa Mtume (s.a.w.) nikamweleza jambo hilo, akasema: Bila shaka ilikuwa inakutosha ukusudie kwa mikono yako hivi, kisha akapiga mikono ardhini kwa pigo moja, halafu akapaka mkono wa kulia kwa kutumia mkono wa kushoto nje ya viganja na uso wake."

Abdallah akasema: "Je, huoni kwamba Umar hakutosheka kwa kauli ya Ammar."[157] Nasi tukiizingatia riwaya hii ambayo ameithibitisha Bukhari na Muslim na wengineo miongoni mwa vitabu vya hadithi; tunafahamu kwa kupitia riwaya hiyo kiwango cha athari ya mwenendo wa Umar jinsi alivyowaathiri Masahaba wengi wakubwa, na kwa ajili hiyo tunafahamu pia kiwango cha kupingana kwa hukumu na kusongamana kwa riwaya na kupingana kwake, na bila shaka huenda mambo hayo ndiyo ambayo yanafasiri sababu ya watawala wa Kibanu Umayyah na Kibanu Abbasi kuzidharau hukumu za Kiislamu na kutozipa uzito, na ndipo wakaruhusu kuwepo madhehebu mengi yanayopingana katika hukumu ya jambo moja.


Hali halisi yamazingira haya inaonekana kama kwamba inawaambia kina Abu Hanifah, Malik, Ahmad na Shafii ya kwamba: "Semeni muyatakayo kwa maoni yenu, kwani ikiwa bwana wenu na Imam wenu Umar anasema ayatakayo kwa maoni yake atakavyo [158] dhidi ya Qur'an na Sunna basi ninyi hamna lawama, kwani ninyi si cho chote ila ni wafuasi, na ni wafuasi wa wafuasi, ninyi hamna jambo jipya." Kinachoshangaza kuliko hilo ni kauli ya Abdallah ibn Mas-ud kumwambia Abu Musa: "Hawezi mtu kutayammam japo hatoyapata maji kwa muda wa mwezi mzima." Na huyu Abdallah ibn Mas-ud ni miongoni mwa Masahaba wakubwa, yeye anaona kwamba mwenye janaba iwapo hatopata maji aache kusali kwa mwezi mzima wala asitayammam, na inaonesha kwamba Abu Musa alijaribu kumkinaisha kwa aya tukufu iliyoshuka maalum kuhusu maudhui hii katika sura ya Maidah, lakini Abdallah anajibu kwamba: "Lau wataruhusiwa kutumia aya hii nina shaka maji yakiwa baridi watatayammamu kwa udongo."


Kutokana na maelezo haya, vile vile tunafahamu namna wanavyojitahidi dhidi ya maandiko ya Qur'an kwa mujibu wa maoni yao, na kile wakionacho wao kwa bahati mbaya ni ugumu na uzito (wanaouweka) kwa umma, wakati ambapo Mwenyezi Mungu anasema:"Mwenyezi Mungu anakutakieni wepesi wala hakutakieni uzito." (Qur'an, 2:185) Maskini huyu eti anasema:"Lau wataruhusiwa kuitumia aya hii nina shaka maji yakiwa baridi watatayammamu." Je, yeye alijiweka kuwa ndiyo mfikishaji wa ujumbe kwa niaba ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake? Na je, yeye ni 301 mwenye pupa (kuwaongoza) na ni mwenye huruma kwa waja kuliko Muumba wao na Mlezi wao? Na baada ya hayo Abu Musa anajaribu kumkinaisha kwa kutumia sunna ya Mtume ambayo aliisimulia Ammar na namna Mtume wa Mwenyezi Mungu alivyomfundisha kutayammam, lakini huyu Abdallah anaikataa Sunna mashuhuri ya Mtume kwa sababu Umar ibn Khattab hakutosheka na kauli ya Ammar.

Mpaka hapa tunafahamu kwamba kauli ya Umar ibn Khattab ndiyo hoja inayotosheleza kwa baadhi ya Masahaba na kwamba kutosheka kwa Umar juu ya hadithi au aya ndiyo kipimo pekee cha kusihi kwa hadithi au maana ya aya, japokuwa kutapingana na matendo na kauli za Mtume (s.a.w.w.). Kwa hiyo basi leo hii tunayakuta matendo ya watu wengi yanapingana na Qur'an na Sunna, sawa sawa katika kuhalalisha au kuharamisha, kwani ijtihadi ya Umar dhidi ya maandiko imekuwa ndiyo madhehebu yanayofuatwa, na ndiyo maana watu wanaojipendekeza kwa watawala, na wenye elimu walipoona hadithi ambazo zilizuwiwa katika zama za Makhalifa, baadaye zimeandikwa na wapokezi na wenye kuhifadhi wamezisajili hali ya kuwa zinapingana na madhehebu ya Umar ibn Khattab, hapo nao wakatengeneza riwaya nyingine za kwao wenyewe wakazinasibisha kwa Mtume (s.a.w.w.) ili kuyapa nguvu madhehebu ya baba Hafsa, (miongoni mwa hayo ni) kama masala ya ndoa ya Mut'a na sala ya tarawehe na nyinginezo.Basi riwaya zikaja zikipingana na imebakia mpaka leo kuwa ndiyo mahala pa ikhitilafu kati ya Waislamu na itabakia hivyo maadam wako wanaomtetea Umar kwa kuwa yeye ni Umar wala (mtu) hataki kuchunguza kwa ajili ya kutafuta haki na aseme kumwambia Umar Umekosea kwani sala haitenguki kwa kukosekana maji na kwamba kuna aya iliyotajwa ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu inayoruhusu kutayammam, na kuna hadithi ya kutayammam imetajwa ndani ya vitabu vyote vya Sunna. Basi kutokuzifahamu kwako wewe kunakunyima nafasi ya kukalia cheo cha Ukhalifa wala kuongoza umma, na kama ulizifahamu, hilo linakukufurisha iwapo utazipinga hukumu zake hiyo haikukufalia kitu (kuzipinga) ikiwa wewe ni muumini. Pindi Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapohukumu jambo eti wewe uwe na hiyari, ukahukumu utakavyo na kukipinga ukitakacho na hali ya kuwa unajuwa mno kuliko mimi kwamba yeyote mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake bila shaka amepotea upotevu ulio wazi.


B. Mwenyezi Mungu anasema: "Bila shaka sadaka hupewa mafakiri na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislamu) na katika kuwapa uungwana watumwa na wenye madeni (yaliyowazidi uzito) na katika njia ya Mwenyezi Mungu na wasafiri (walioharibikiwa) ni faradhi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi (na) mwenye hekima." (Qur'an, 9:60) Miongoni mwa sunna maarufu ya Mtume ni kwamba, yeye Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alikuwa akiwahusisha wanaotiwa nguvu nyoyo zao juu ya Uislamu kwa sehemu yao aliyowafaradhishia Mwenyezi Mungu kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Lakini Umar alikibatilisha kipato hiki kilichofaradhishwa na akajitahidi dhidi ya Qur'an katika zama za Ukhalifa wake na akawaambia "Hatuna haja nanyi Mwenyezi Mungu amekwisha uimarisha Uislamu na hana haja nanyi." Bali Umar aliipuuza hukumu hii katika zama za Ukhalifa wa Abubakr, pale walipomjia hao wanaotiwa nguvu nyoyo zao kama ilivyokuwa kawaida yao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.


Abubakr akawaandikia suala hilo wakaenda kwa Umar ili wakachukuwe sehemu yao, Umar akaichana barua hiyo na akawaambia: "Hatuna haja nanyi, Mwenyezi Mungu amekwisha uimarisha Uislamu na hana haja nanyi, basi kama mtasalim amri vinginevyo kati yetu na ninyi ni upanga tu." Walirudi kwa Abubakr wakamwambia, "Hivi wewe ndiwe Khalifa au yeye?" Akasema "Ni yeye apendapo Mwenyezi Mungu." Naye Abubakr alirudi nyuma kuyatekeleza yale aliyoyaandika akaafikiana na maoni ya jamaa yake Umar.[159] Na cha ajabu vile vile ni kwamba leo hii utawakuta wanaomtetea Umar katika suala hili na kulizingatia kuwa ndiyo miongoni mwa sifa zake na uhodari wake, na miongoni mwa hawa ni Sheikh Muhammad anayejulikana kama Ad-dawaalibi, anasema katika kitabu chake Usulul-Fiqhi uk. 239 kwamba, "Huenda ijtihadi ya Umar (r.a.) katika kukata kipato ambacho Qur'an imekiweka kwa ajili ya wanaoimarishwa nyoyo zao katika dini, ilikuwa katika utangulizi wa hukumu ambazo alizizungumzia Umar kufuatia mabadiliko ya maslahi kwa kubadilika zama pamoja na kwamba Qur'an kuhusiana na hilo bado imethibiti haikufutwa."


Kisha baada ya hapo (Sheikh huyu) akaanza kumtakia udhuru Umar kwamba yeye aliiangalia sababu ya kushuka kwa tamko hilo la Qur'an na siyo dhahiri yake ... mpaka mwisho wa maneno yake ambayo akili timamu haziwezi kuyafahamu. Sisi tunakubali ushahidi wake kwamba Umar alizigeuza hukumu za Qur'an kufuatia maoni yake kwamba, maslahi yanabadilika kwa mnasaba wa nyakati, na tunaipinga tafsiri yake kwamba Umar aliangalia sababu ya maandiko hayo na hakuangalia dhahiri yake na tunamwambia yeye na wengine kwamba matamko ya Qur'an na yale ya hadithi za Mtume hayabadiliki kwa kubadilika nyakati, kwani Qur'an inasema wazi kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu yeye mwenyewe hana haki kuibadilisha.

Mwenyezi Mungu anasema: "Na wanaposomewa aya zetu zilizo wazi wale wasioamini kukutana nasi husema, leta Qur'an isiyokuwa hii au uibadilishe, waambie, Siwezi kuibadilisha kwa hiyari yangu, sifuati isipokuwa yanayofunuliwa kwangu, hakika mimi naiogopa nikimuasi Mola wangu adhabu ya siku iliyo kuu." (Qur'an, 10:15) Nayo Sunna tukufu ya Mtume inasema: "Halali (aliyoihalalisha) Muhammad ni halali mpaka siku ya Qiyama, na Haramu (aliyoiharamisha) ni haramu mpaka siku ya Qiyama."

Lakini kwa mujibu wa madai ya Ad-dawaalibi na wanaokubaliana na maoni yake miongoni mwa wanaotetea ijtihadi ni kuwa, hukumu zinabadilika kutokana na mabadiliko ya nyakati. Kama ni hivyo basi, hapana lawama kwa baadhi ya watawala ambao walizibadilisha hukumu za Mwenyezi Mungu, kwani miongoni mwao yuko aliyesema: "Kuleni ili mpate nguvu dhidi ya adui yenu hapana haja ya kufunga saumu katika zama hizi ambazo tunapambana na umasikini na ujinga na kubakia nyuma kimaendeleo, na saumu inatufanya tushindwe kuzalisha mali. Si hivyo tu bali alizuwia ndoa ya wake wengi kwani yeye anaona kuwa jambo hilo ni dhuluma, ni kuvunja haki za mwanamke." Akaendelea kusema kwamba: "Katika zama za Muhammad mwanamke alikuwa akizingatiwa kuwa ni nyenzo, ama sasa hivi tumemkomboa na kumpa haki zake zote.


Kiongozi huyu aliyaangalia maandiko kwa mujibu wa sababu asilia na wala hakuiangalia dhahiri yake kama Umar alivyoiangalia akasema: "Hakika mirathi leo hii ni lazima igawiwe kwa mwanamume na mwanamke kwa kiwango cha sawa kwa sawa, kwani Mwenyezi Mungu alimpa mwanamume sehemu mbili kwa kuzingatia kwamba yeye ndiye anayeilea familia wakati ambapo mwanamke alikuwa amepuuzwa, ama leo hii kutokana na juhudi za utawala wake sasa hivi mwanamke anajishugulisha na kuilea familia yake na aliwatolea mfano wananchi kwa mkewe ambaye alimsaidia nduguye mpaka akafikia ngazi ya waziri kutokana na ufadhili wake na uangalizi wake.'"

Kama ambavyo kiongozi huyo alihalalisha uzinifu na akaizingatia kuwa ni haki ya mtu binafsi aliyefikia umri wa utambuzi maadam haendi kinyume katika njia za kuendesha maisha, na akafungua majumba ya kulea watoto ambao wanazaliwa kutokana na zinaa akitetea hilo kuwa yeye ni mwenye huruma kwa watoto wa zinaa ambao walikuwa wakizikwa hali wakiwa hai kwa kuchelea fedheha, na zaidi ya hayo ni miongoni mwa ijtihadi zake zinazofahamika. Cha kushangaza ni kuwa kwa kiwango fulani rais huyu alikuwa ameathiriwa na hali ya Umar, kwani kuna kipindi alimtaja Umar kwa kumsifu, na kuna wakati akamtaja kwamba Umar hakuweza kuyabeba majukumu akiwa hai na baada ya kufa, wakati ambapo yeye atayamudu akiwa hai na baada ya kufa, na kuna wakati mwingine ni kama kwamba zilimfikia habari kuwa Waislamu wamezikosoa juhudi zake akasema: "Bila shaka Umar alikuwa mtu wa mwanzo tena mkubwa na mwenye kujitahidi katika zama zake, basi ni kwa nini mimi nisijitahidi katika zama zangu hizi mpya, kwani Umar alikuwa kiongozi wa dola na mimi pia ni kiongozi wa dola."


Kinachoshangaza zaidi ni kuwa kila anapomtaja Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) utaona katika maneno yake mna dharau na kejeli, kwani alisema katika hotuba yake kwamba, "Muhammad alikuwa hajui hata jiografia kwa kuwa alisema: Itafuteni elimu japokuwa itakuwa China, akidhani kwamba China ndiyo mwisho wa dunia, kwa hiyo Muhammad alikuwa hajui kuwa elimu itafikia kiwango hiki na kwamba tani nyingi za chuma (yaani ndege) zitaweza kuruka angani. unafikiri namna gani lau angetambua au kusimuliwa juu ya uranium na polasium na elimu za atom na nyukilia?" Kwa hiyo mimi simlaumu yeye maskini asiyefahamu chochote kuhusu kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake? Bali mtu huyu alijikuta tu amekwishaitawala dola kwa niaba ya Uislamu hali yakuwa anaukejeli Uislamu, anafuata utamaduni wa kimagharibi na anakusudia kuigeuza nchi yake na kuwa ni dola kama dola za Uiaya kwa kufuatia mtazamo auonao yeye.


Wako wengi miongoni mwa Marais na Wafalme waliofuata mwenendo wake, pale alipoungwa mkono na dola za Magharibi kiasi kwamba wakamsifu kuwa ni mpiganiaji haki mkubwa, kisha simlaumu kwani kila kitu kina chanzo chake na kila chombo hutoa kile kilichomo. Iwapo mimi nitakuwa muadilifu basi lawama nitazitupia kwa Abubakr, Umar na 'Uthman ambao ndio waliofungua mlango huu tangu siku aliyofariki Mtume (s.a.w.w.) na wakasababisha ijtihadi zote ambazo watawala wa Banu Umayyah na Banu Abbas waliziimarisha kwa kipindi cha karne saba, na karne zote hizo zilitumika kuharibu miongozo ya Uislamu katika maandiko yake ya asili na hukumu zake, na mambo yalizidi zaidi kuwa mabaya katika karne zilizofuatia hapo, mpaka ikafikia kwamba kiongozi (wa Kiislamu) analihutubia taifa lake la Waislamu hali ya kuwa anamkejeli Mtume wa Mwenvezi Mungu na hapana yeyote wa kumkemea, si ndani wala nje.


Haya ndiyo niliyoyasema na ninayasema kwa baadhi ya jamaa katika harakati za Kiislamu kwamba, ''Ikiwa ninyi leo hii mnampinga kiongozi kwa kutofuata Quran na Sunna ya Mtume, basi mnawajibika mumpinge aliyeleta uzushi huu wa kufanya ijtihadi dhidi ya Qur'an na Sunna, ikiwa kweli ninyi ni waadilifu na mnataka kuifuata haki kwa vitendo. Kwa bahati mbaya hawayakubali maneno haya na hunikosoa eti ni vipi nawalinganisha viongozi wa leo na Makhalifa waongofu? Nami huwajibu kwamba viongozi wa leo na wafalme wa leo ni matokeo kamili ya yale yaliyotokea ndani ya historia, na je ni lini Waislamu walikuwa huru baada ya kufariki Mtume na hata leo uhuru wao uko wapi?

Basi wao husema: "Ninyi Mashia kazi yenu ni kuwazulia Masahaba na kuwatukana, na lau siku moja tutashika madaraka tutakuchomeni moto." Basi mimi husema; "Mwenyezi Mungu asikupeni mafanikio hayo." C. Mwenyezi Mungu anasema: "Talaka ni mara mbili, kisha ni kumuweka kwa wema au kumuacha kwa wema. wala si halali kwenu kuchukua chochote mlichowapa (wake zenu) isipokuwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawawezi kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi mukiogopa kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. hapo itakuwa hapana dhambi kwao kupokea ajikomboleacho mwanamke, hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu basi musiiruke, na watakaoiruka mipaka ya Mwenyezi Mungu hao ndio madhalimu, na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwingine, na akimuacha basi hapo hapana dhambi kwao kurejeana wakiona kuwa watasimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu na hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu anayoibainisha kwa watu wanaojua." (Qur'an, 2:229-230)


Nayo Sunna Tukufu ya Mtume ilitoa tafsiri bila ya utata ya kwamba mwanamke hawi haramu kwa mumewe isipokuwa baada ya talaka tatu. hapo haitastahiki kwa mumewe kumrejea isipokuwa baada ya kuolewa na mume mwingine, na ikiwa atamuacha huyu mume mwingine hapo itawezekana kwa mume yule wa kwanza kumuoa upya kama wanaume wengine ambavyo wangewajibika kufanya, na ni juu yake mwanamke huyo kukubali au kukataa ni hiyari yake mwenyewe. Lakini Umar ibn Khattab kama ilivyokawaida yake, alivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu aliyoibainisha kwa watu wenye kufahamu, akaibadilisha hukumu hii kwa kuweka hukumu yake ambayo inasema: "Talaka moja kivitendo kwa tamko la talaka tatu linamharamishia mume mkewe." Umar akawa ameipinga Qur'an tukufu na Sunna ya Mtume(s.a.w.w.).

Imethibiti ndani ya sahihi Muslim Kitabut-talaq Babu Talaqit-thalath kutoka kwa ibn Abbas amesema: "Katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) na Abubakr, na miaka miwili ya Ukhalifa wa Umar, talaka ilikuwa ni talaka tatu (katika kikao kimoja) ni moja, basi Umar akasema: "Hakika watu wamelipupia jambo ambalo hapo kabla kulikuwa na utulivu kwa ajili yao kuhusiana nalo, lau tutalipitisha liwe ni hukumu juu yao, akalipitisha juu yao." Wallahi inashangaza, ni vipi Khalifa anathubutu kubadilisha hukumu za Mwenyezi Mungu mbele ya Masahaba na wanamkubalia kila anachosema na kukifanya na hakuna mwenye kukemea wala kupinga na wanatudanganya siye masikini kwamba eti Sahaba mmoja alimwambia Umar: "Wallahi lau tutaona unapotoka tutakurekebisha kwa hukumu ya upanga." Hii ni kauli ya uongo na ni uzushi ili watuoneshe kwamba Makhalifa walikuwa ni mfano bora katika kutoa uhuru na demokrasi, wakati historia inawapinga kwa ukweli wake kimatendo, na hapana mazingatio yoyote kwa maneno (kauli) ikiwa matendo yako ni kinyume chake.


Au huenda wao (Masahaba) walikuwa wanaona ndani ya Qur'an na Sunna mna upotofu na kwamba Umar ibn Khattab ndiyo alikuwa akilirekebisha na kuweka sawa. Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kauli za kuropoka. Na nilikuwa katika mji wa Qafsah, na mara nyingi nikiwajibu wanaume ambao wamejiharamishia wake zao kwa kuwa waliwaambia wake zao mara tatu; "Wewe ni haramu (kwangu)." Na walikuwa wakifurahi pindi ninapowafahamisha hukumu sahihi za Mwenyezi Mungu ambazo Makhalifa hawakuzivuruga kutokana na ijtihadi zao, lakini wale watu wanaojidai kuwa wao ni wenye elimu huwatisha kwa kuwaambia kwamba, "Mashia kila kitu kwao ni halali."


Namkumbuka mmoja wao kuna wakati fulani alinihoji kwa njia nzuri na akaniuliza: "Ikiwa Sayyidina Umar ibn Khattab (r.a.) aliibadilisha hukumu ya Mwenyezi Mungu kuhusu suala hili na nyinginezo halafu Masahaba wakamkubalia hilo, basi ni kwa nini Sayyidna Ali (a.s.) hakumpinga Sayyidna Umar? Mimi nilimjibu kwa jawabu alilolitoa Imam Ali (a.s.) wakati Maquraish waliposema kuwa, "Yeye ni mtu shujaa lakini hana ujuzi wa vita." Akasema (Imam Ali a.s.): "Naapa kwa Mwenyezi Mungu, je, kuna yeyote miongoni mwao amebobea mno shughuli za vita! ili nimpe daraja hiyo kutoka kwangu?


Nilisimama katika vita wakati sijafikia umri wa miaka ishirini, nami sasa nimekuwa zaidi ya miaka sitini, lakini ikimbukwe kuwa hana njia mtu ambaye watu wake hawamtii." (Hotuba ya 27 Nahjul-balagha). Basi je, Waislamu waliyasikiliza maoni ya Ali? (Hakuna) isipokuwa wafuasi wake waliouamini Uimamu wake, kwa hakika (imam Ali) alipinga kuharamishwa kwa mut'a na akapinga uzushi wa tarawehe na alizipinga hukumu zote zilizobadilishwa na Abubakr, Umar na Uthman, lakini. maoni yake yalibakia kwa wafuasi wake na vipenzi wake. Ama Waislamu wengine walimpiga vita wakamlaani na wakajaribu kila njia kumuua na kufuta utajo wake.


Hakuna kitakachoweza kujulisha kupinga kwake Imam Ali (kubadilishwa kwa hukumu za Mwenyezi Mungu) zaidi kuliko msimamo wake mtukufu wa kishujaa (aliouonesha) pale Abdur-rahman ibn A'uf waliyempendekeza achague khalifa baada ya kufa Umar akamwita (Imam Ali) na kumpa masharti kwamba atakapokuwa amemchagua awe khalifa, basi awahukumu kwa mujibu wa sunna ya Makhalifa wawili (yaani) Abubakr na Umar. Imam Ali (a.s.) akalikataa sharti hili na akasema: "Nitahukumu kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake." Na kwa ajili hii basi walimuacha na wakamchagua Uthman ibn Affan ambaye alikubali sharti la kuhukumu kwa mujibu wa sunna ya 'Makhalifa hao wawili.


Kwa hiyo basi, leo hii utaona kwamba mlango wa mji wa elimu (ambaye ni Imam Ali a.s.) alikuwa mjuzi mno kuliko watu wengine baada ya Mtume (s.a.w.w.), (na alikuwa) mfikishaji na mlinzi wa kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, lakini amepuuzwa kwa upande wa Masunni kiasi kwamba wao wanamfuata Maliki, Abu Hanifah, Shafii na Ibn Hanbal. Wanawafuata hawa katika kila jambo la dini miongoni mwa ibada na shughuli za uhusiano na wala hawamrejei Imam Ali katika jambo lolote.


Hivyo hivyo ndivyo walivyofanya Maimamu wao katika hadithi, kama vile Bukhari na Muslim, utawaona wanapokea hadithi kutoka kwa Abu Hurairah na Ibn Umar na au kutoka kwa mtu dhaifu na asiyejulikana, aliye karibu na aliye mbali (wanapokea tu). Wakati huo huo hawapokei kutoka kwa Ali isipokuwa hadithi chache alizozushiwa na ndani yake zinachafua heshima ya nyumba ya Mtume (s.a.w.w.), kisha wao hawatosheki na hilo bali anayemfuata Ali (a.s.) na wafuasi wema wa Imam Ali humkufurisha na kumpinga, pia (Masunni) huwatukana kwa kuwaita kuwa ni wapinzani na majina mengine mabaya, na ukweli wa mambo ni kwamba watu hawa (yaani Mashia) hawana kosa lolote isipokuwa ni kwa sababu ya kumfuata Ali ambaye alikuwa amepuuzwa na kutengwa katika zama za Makhalifa watatu, kisha baadaye akawa analaaniwa na kupigwa vita katika zama za Banu Umayah na Banu Abbas. Kila mwenye kufuatilia na akaifahamu historia, utaupata ukweli huu wazi wazi, na atafahamu yaliyopita na njama zilizopangwa dhidi yake (Imam Ali) na watu wa nyumba yake na wafuasi wake.