WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Kauli ya Ahlul-dhikri kuhusu baadhi yaMasahaba.
Imam Ali (a.s.) amesema akiwazungumzia Masahaba hawa wanaohesabiwa kuwa ni miongoni mwa (watu) wa mbele: "Niliposimamia Ukhalifa, kuna kundi lililotengua (kiapo chake) na kundi jingine lilitoka, na wengine wakafanya ujeuri, kama kwamba wao hawakuyasikia maneno ya Mwenyezi Mungu aliposema, Hayo ni makazi ya akhera tunawapa wale wasiotaka ukubwa katika nchi wala uovu, na marejeo (mema) ni kwa ajili ya wamchao Mwenyezi Mungu. Bila shaka Wallahi Wallahi, waliyasikia maneno hayo na wakayafahamu, lakini dunia imewapendeza machoni mwao na mapambo yake yamewafurahisha." (Nahjul-Balagha uk.90). Na amesema tena (Imam Ali a.s.) kuwahusu hao Masahaba: "Wamemfanya shetani kuwa ndiyo msimamizi wa mambo yao, naye amewafanya wao kuwa ni washirika (wake) basi ametaga (mayai) na kuyaangua ndani ya nyoyo zao na anatambaa ndani ya akili zao, basi (shetani) anaona kwa kutumia macho yao na anazungumza kwa kupitia ndimi zao, akawapoteza na kuwapambia maovu yakawa ndiyo matendo ya yeyote aliyeshirikishwa na shetani ndani ya utawala wake na akazungumza batili kwa ulimi wake." (Nahjul-Balagha uk.96).Na amesema tena Imam (a.s.) juu ya Sahaba mashuhuri Amri ibn Al-'as: "Anashangaza mwana wa Nnabighah, hakika amesema (mambo) batili na ametamka uovu, ama (na ifahamike kwamba) kauli mabaya ni kusema uongo, hakika yeye akizungumza husema uongo, na akiahidi huenda kinyume na ahadi, na akiomba (kitu) hulazimisha (apewe) na anapoombwa ni bakhili, ana hiyana kwenye ahadi na anakata udugu." (Nahjul-Balagha uk.200). Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema (s.a.w.): "Alama za mnafiki ni tatu: Akizungumza husema uongo, na akiahidi huenda kinyume na ahadi na akiaminiwa hufanya khiyana." (Ewe msomaji fahamu kwamba machafu yote haya na zaidi kuliko haya yanapatikana kwa Amru ibn Al-'as. Na amesema Imam Ali (a.s.) akimsifu Abudharri Al-Ghifari na wakati huo huo akamshutumu Uthman ibn Affan pamoja na washirika wake ambao walimfukuza Abudharri na kumpeleka mahala paitwapo Ar-rabdhah kisha kutomruhusu kurudi Madina mpaka akafa huko akiwa peke yake. "Ewe Abudharri, hakika wewe umechukizwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi mtarajie huyo ambaye kwa ajili yake umechukizwa, bila shaka jamaa hawa walikuogopa juu ya dunia yao, nawe uliwachelea kwa ajili ya dini yako, kwa hiyo viache mikonini mwao vitu ambavyo kwavyo walikuogopa na uwakimbie ukiwa na kile ambacho wewe uliwachelea wao kwa ajili yake, hakika wanakitaka mno hicho ulichowazuwia, nawe umetosheka mno na hicho waliochokuzuwilia, na hivi karibuni utajua ni nani atakayepata faida kisha (ni nani) mwingi wa husuda, na lau mbingu na ardhi zingekuwa zimeshikana juu ya mja kisha (mja huyu) akamcha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu angemjalia mja huyo njia katika mbingu na ardhi. Usiwe na kiliwazo kingine isipokuwa haki, na kisikufanye mpweke chochote isipokuwa batili, basi lau ungeikubali dunia yao wangekupenda na lau ungekata sehemu (katika dunia) wangekupa amani." (Nahjul-Balagha u. 299).
Amesema Imam Ali (a.s.) kuhusu Mughirah ibn Al-akhnas ambaye naye ni miongoni mwa Masahaba wakubwa:"Ewe mwana wa aliyelaaniwa aliyekatikiwa, na (ewe mwana wa) mti ambao hauna mizizi wala matawi, Wallahi Mwenyezi Mungu hajamtukuza yule ambaye wewe unamtetea, na wala hatosimama yule ambaye wewe unamnyanyua, hebu tuondokee, Mwenyezi Mungu ayaangamize makazi yako, kisha azidishe mashaka yako, kamwe Mwenyezi Mungu asikubakishie muda wa kubakia kwako." (Nahjul-Balagha uk. 306). Na amesema Imam (a.s.) kuwahusu Tal-ha na Zubair, ambao ni Masahaba mashuhuri waliompiga vita Imam Ali baada ya kuwa wamempa baia na hatimaye wakatengua baia yao:-"Wallahi hawakunikuta na aibu ya aina yoyote ile, na wala hawakufanya uadilifu kati yangu na wao, na kwa hakika wao wanaitetea damu ambayo wao ndiyo walioimwaga...Hapana shaka hilo ndilo kundi lililoasi, ndani yake yumo jamaa (wa karibu yangu (yaani Zubair) na yumo nyoka, madai yao si kweli bali kuna jambo walitakalo, hapana shaka mambo yako wazi na hakika uovu umeondoka toka mahala pake na ulimi wake umekatika kutoka mahala pake pa uchochezi Ni nyie mlionijia mbio mbio kama mwanamke mwenye watoto anavyowakimbilia wanawe na huku mnasema, "Baia Baia" lakini mimi nikakikunja kiganja changu ninyi mkakinyoosha, nikautoa mkono wangu nanyi mkauvuta, Ewe Mwenyezi Mungu hakika wawili hawa wameniasi na wamenidhulumu, wametengua kiapo chao kwangu, wamewavuruga watu dhidi yangu, nakuomba uyafungue waliyoyafunga na wala usiwakubalie waliyoyaamua na uwaoneshe ubaya wa waliyoyategemea na kuyafanya. Niliwataka wajirekebishe kabla ya mapambano, na hapo vitani niliwataka wawe mbali wakanipinga na kuukataa msamaha wangu.Na amesema Imam Ali (a.s.) ndani ya barua aliyowaandikia Zubair na Tal-ha: "Enyi Masheikh wawili badilisheni maoni yenu (mujisahihishe) kwani sasa hivi jambo kubwa litakalowafika ni aibu kabla ya fedheha na moto havijakutana... Was-salaam." Nahjul-Balagha uk. 626). Na amesema kuhusu Marwan ibn Al-hakam wakati alipomteka katika vita ya Jamal kisha akamwachia huru, na huyu Marwan ni miongoni mwa watu waliombai Imam Ali kisha akatengua baia yake: Anasema Imam Ali, "Sina haja na baia yake, hakika kiganja chake ni kiganja cha Kiyahudi, lau atanibai kwa kiganja chake hatimaye atatengua kimya kimya, ama huyu (Marwan) atamiliki uongozi kama mbwa arambavyo pua yake (muda mchache) naye ni baba wa watawala wanne, na kutokana naye na wanawe hao umma (wa Kiislamu) utakumbana na siku nyekundu. matatizo na umwagaji damu Na amesema Imam (a.s.) kuhusu Masahaba ambao walitoka pamoja na bibi Aisha kwenda Basrah katika vita ya Jamal na katika hao walikuwemo Talha na Zubair: "Wakatoka hali ya kuwa wanaikokota heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kama akokotwavyo mjakazi anaponunuliwa wakaielekeza Basra, wao wakawazuwia wake zao majumbani mwao, na wakamtoa nyumbani kwa ajili yao na wasiokuwa wao mtu ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimzuwia asitoke, wakiwa ndani ya jeshi ambalo hapana mwanaume yeyote aliyekuwa ndani ya jeshi hilo isipokuwa (hapo kabla) alikuwa amenitii na kunipa kiapo cha utii kwa hiyari yake mwenyewe bila kulazimishwa.Wakamshambulia muwakilishi wangu na muweka hazina wa nyumba ya mali ya Waislamu hapo Basra na wengineo miongoni mwa wakazi wa mji huo, wakauwa watu kadhaa hali yakuwa wamefungwa. na wengine wakawauwa baada ya kuwahadaa. Basi Wallahi lau wasingemuuwa miongoni mwa Waislamu isipokuwa mtu mmoja ambaye kumuuwa kwake iwe kuwa ametenda kosa lolote, hakika ingenihalalikia mimi kulipiga jeshi hilo lote, kwani walipomfikia hawakupinga (kuuawa kwake) wala hawakumtetea kwa ulimi wala kwa mkono, achilia mbali ile hali ambayo wao wamewauwa Waislamu kwa kiasi cha idadi ambayo waliyoingia nayo dhidi yao. (Nahjid-Balagha uk.370). Na amesema Imam (a.s.) kuhusu bibi Aisha na wafuasi wake miongoni mwa Masahaba katika vita ya Jamal: "Ninyi mmekuwa askari wa mwanamke na wafuasi wa mnyama, akipiga kelele ninyi mnaitikia na akijeruhiwa mnakimbia, tabia yenu ni mbaya, ahadi yenu ni yenye kuvunjika na dini yenu ni unafiki." (Nahjul-Balagha uk.98)."Ama fulani umemtangulia mtazamo wa wanawake wenziwe, anayo chuki inayotokota kifuani mwake mfano wa chungu kinachotokota, lau angeitwa ili atende kwa mwingine kama haya yaliyomleta kwangu asingefanya, na kwangu mimi anayo heshima yake ile ile ya mwanzo (kwa kuwa ni mke wa Mtume) na malipo (yake) yapo kwa Mwenyezi Mungu." (Nahjul-Balagha uk. 334). Pia Imam Ali (a.s.) alisema kuhusu Maquraishi wote, na hapana shaka alikuwa akiwakususudia Masahaba."Ama sisi kuwekwa kando kuhusiana na cheo hiki (cha Ukhalifa) wakati sisi ndio watukufu kwa nasaba na watu wa karibu mno na Mtume kimafungamano, yote hayo ni kwa sababu ya choyo na chuki katika nafsi za watu lakini hukumu ya yote hayo iko kwa Mwenyezi Mungu na marejeo ni kwake siku ya Kiyama Kwa hakika mambo ya dunia hii yananichekesha na kuniliza, hasa kuhusu huyu mwana wa Abu Sufiyan, hapana shaka ametenda mambo yanayoshangaza na kuzidisha mashaka. Jamaa hawa walitaka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kutoka kwenye taa yake na kuziba mbubujiko toka kwenye asili yake, na wakanichanganyia kinywaji kibaya, iwapo yataondoka matatizo kwetu na kwao nitawapasha ukweli halisi, vinginevyo basi usiwajutie kwani hakuna shaka Mwenyezi Mungu anayajua wayatendayo." (Nahjul-Balagha uk.348).Na alisema katika maana kama hii maneno yafuatayo alipokuwa akimzika bibi Fatma hali yakuwa akimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu. "Binti yako atakueleza namna Umma wako walivyosaidiana kuubomoa (Ukhalifa), basi muulize akueleze jinsi ya hali (ilivyokuwa) hali hii (imetokea) hata haujapita muda mrefu (toka kufariki kwako) na wala utajo wako haujatoweka..." (Nahjul-Balagha uk.460). Na amesema Imam Ali (a.s.) ndani ya barua aliyomuandikia Muawiya: "Wewe bila shaka neema zimekupa kiburi na shetani amechukua sehemu ya kwako wewe na amefikia malengo yake kupitia kwako, anazunguka (mwilini mwako) mzunguko wa roho na damu, tangu lini enyi kina Muawiyah, mmekuwa viongozi wa raia na watawala wa mambo ya Umma pasina kuwa kuna unyayo uliotangulia wala heshima tukufu? Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kushikilia mwenendo wa waovu waliotangulia, nakuonya kuwa wewe ni mwenye kuendelea kudanganyika kwa matamanio umekuwa tofauti kati ya nje yako na ndani yako, kwa hakika wewe Muawiyah umeitaka vita, basi hebu waache watu pembeni unitokee mimi, na yaache makundi haya mawili (langu na lako) yasipigane (utoke wewe na mimi) ili apate kutambulikana ni yupi kati yetu aliyemzoefu moyoni mwake na ambaye macho yake yamefumbwa. Basi (fahamu ya kwamba), mimi ndiye baba Hasan, ndiye niliyemuua babu yako, mjomba wako na nduguyo, nikawavunja vunja siku ile ya Badri, na ule upanga (niliowavunjia bado) ninao, na moyo ule ule (wa siku ile) nilipopambana na adui yangu (bado ni ule ule) kamwe sijabadili dini wala sijazusha Mtume mwingine (zaidi ya Muhammad) na ni bila shaka nipo kwenye dini ambayo mliikataa kwa hiyari yenu na mkaingia bila kupenda..." (Nahjul-Balagha uk. 526).Imam (a.s.) anaendelea kusema "Ama kauli yako (kusema) kwamba, sisi ni kizazi cha Abdu Manafi ni kweli, sisi ndio wao, lakini Umayyah halinganishwi na Hashim, na wala Harbu (babu yake Muawiyah) yeye si kama Abdul-Mutalib, na wala Abu-Sufiyan si (sawa kwa ubora) kama Abu Talib, wala Muhajir (aliyetoka Maka mwanzoni anajikusudia yeye mwenyewe Imam a.s.) si kama muachwa huru (anamkusudia Muawiyah) wala mwenye nasaba takatifu si kama mwenye nasaba ya kubandikizwa, wala atendaye haki si sawa na mpotoshaji, wala Muumini si sawa na muovu, kwa kweli badali mbaya ni ya yule anayefuata waliomtangulia ambao wameporomokea ndani ya moto wa Jahannam.


Mikononi mwetu (tumeshika) utukufu wa Utume ambao kwao tumemuinamisha mwenye nguvu na tukamnyanyua mnyonge, na pale Mwenyezi Mungu alipowaingiza Waarabu ndani ya dini yake kwa wingi, basi Umma huu ulijisalimisha kwa hiyari yake na wengine kwa kulazimika, hivyo ninyi mlikuwa miongoni mwa walioingia katika dini ima kwa matumaini fulani au kwa kuogopa, na (kwa kweli) wamefaulu wale waliotangulia kwa sababu ya kutangulia kwao na Muhajirina wa mwanzo wamejichukulia ubora wao." (Nahjul-Balagha uk.533).


"Kwa hakika umetuita kwenye usuluhishi wa Qur'ani na wewe si miongoni mwa watu wa Qur'ani, (fahamu kwamba) sisi hatukukuitikia wewe (matakwa yako) lakini tumeiitika Qur'ani katika hukumu yake Wassalaam...." (Nahjul-Balagha uk.595). "Waambie, ukweli umekwisha fika na bila shaka uongo ni wenye kuondoka." (Qur'ani, 17:81).