WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Na tukirejea kwenye maudhui ya Mtume (s.a.w.w.) kumpenda Aisha kwa kuwa eti alihifadhi kutoka kwa Mtume nusu ya dini, na yeye Mtume alikuwa akisema, "Chukuweni nusu ya dini yenu kutoka kwa kijanajike hiki chekundu". Hadithi hii haifai wala haina msingi wowote wa kusihi kwake, wala haiwezi kulingana na hadithi ambazo zimepokewa kutoka kwa yeye Aisha (akielezea) miongoni mwa hukumu zinazochekesha na kuhuzunisha, hadithi ambazo (ukweli ulivyo) Mtume wa Mwenyezi Mungu kamwe hakuzisema. Basi hebu na tutosheke na mfano mmoja juu ya hayo unaohusu suala la kumnyonyesha mtu mzima, hadithi ambayo Aisha alikuwa akiieleza kuwa imetoka kwa Mtume (s.a.w.w.) na ni hadithi ambayo Muslim ameithibitisha ndani ya Sahihi yake, na Maliki naye ndani ya Muwatta yake na ni hadithi ambayo tumetosheleza juu ya uchunguzi wetu kuhusiana nayo ndani ya kitabu chetu "Liakuna Maas-Sadiqin" basi atakaye ufafanuzi na uthibitisho wa uwazi wa mambo na akirejee kitabu hicho. Na itoshe tu kuhusu riwaya hii mbaya ya kwamba wakeze Mtume wote waliyapinga matumizi yake na wakaikanusha mno kiasi kwamba hata huyo aliyeipokea alibakia kwa mwaka zima anaogopa kuitaja kutokana na ubaya wake na kutokuwa na haya. Na tutakapoirejea Sahihi Bukhari katika mlango usemao, "Sala hupungnzwa mtu akitoka nyumbani mwake " amesema: Kutoka kwa Az-zuhri, naye kutoka kwa Ur-wah, amepokea toka kwa Aisha (r.a.) amesema: "Hapo mwanzo Sala ilifaradhishwa rakaa mbili, Sala ya safari ikabakishwa (kuwa rakaa mbili) na Sala isiyo ya safari ikakamilishwa (kuwa rakaa nne). Az-Zuhri akasema nikamwambia Ur-Wah, mbona Aisha anakamilisha (rakaa nne katika safari)? Akasema, Anabadilisha kama alivyobadilisha Uthman" Riwaya hii ameithibitisha Muslim ndani ya Sahihi yake katika mlango wa Sala ya wenye safari na kuipunguza.


Kwa maelezo yaliyowazi zaidi ni kama ilivyo ndani ya Bukhari amesema: "Imepokewa kutoka kwa Az-zuhri, naye kutoka kwa Ur-wah naye kutoka kwa Aisha kwamba, hapo mwanzo Sala ilifaradhishwa rakaa mbili, basi Sala ya safari ikabakishwa kuwa rakaa mbili na Sala isiyo ya safari ikakamilishwa (kwa rakaa nne) Az-zuhri akasema, nikamuuliza Ur-wah mbona Aisha anakamilisha (rakaa nne) katika safari? akasema: "Amebadilisha kama alivyobadilisha Uthman." Bila shaka ni kupingana kuliko dhahiri, yeye mwenyewe bibi Aisha ndiye aliyepokea kwamba Sala ya msafiri ilifaradhishwa rakaa mbili, lakini ni yeye huyo huyo anafanya kinyume cha vile alivyofaradhisha Mwenyezi Mungu na alivyofanya Mtume wake, na anabadilisha na kuzigeuza hukumu za Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili aimarishe sunna ya Uthman, na kwa sababu hizi basi tunakuta ndani ya Sihah za Ahlis-Sunnah wal-jamaa mna hukumu nyingi lakini hawazitumii kwa kuwa wao mara nyingi wanatumia (hukumu) zilizoanzishwa na Abubakr na zile zilizoanzishwa na Ummar, Uthman, Aisha na zile alizoanzisha Muawiyah ibn Abi Sufiyan na Masahaba wengineo. Sasa basi iwapo kijanajike hiki chekundu ambacho kwake inapatikana nusu ya dini kinafanya mabadiliko katika hukumu za Mwenyezi Mungu vile kinavyopenda, mimi siamini kwamba mumewe ambaye ni Mtume wa mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) anakiridhia, na katika hali hiyo awaamuru watu wakifuate. Wakati huo huo kumekuja riwaya ndani ya Sahihi Bukhari na Sihah nyigine za Masunni zikiashiria kwamba, kukifuata (kijanajike chekundu hicho) ndani yake kuna maasi dhidi ya Mwenyezi Mungu, na tutakutosheleza kwa hilo utapofika wakati wake apendapo Mwenyezi Mungu.


Ama wale wasemao kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alikuwa akimpenda bibi Aisha kwa sababu Jibril alimjia Mtume akiwa na picha ya bibi Aisha kabla hata hajamuoa, na kwamba Jibril alikuwa haingii kwa Mtume ila awapo nyumbani kwa bibi Aisha, riwaya hizi zinawachekesha hata wenda wazimu, kwa sababu mimi binafsi sifahamu iwapo picha hiyo aliyokuja nayo Jibril ilikuwa ni ya Photograph au ya kuchora, wakati ambapo Ahlus-sunna wanazo riwaya kwamba, Abubakr ndiye alimtuma Aisha aende kwa Mtume akiwa na chombo kilichotiwa tende ili tu Mtume amuangalie Aisha, na Abubakr yeye ndiye aliyemtaka Mtume (s.a.w.w.) amuoe Binti yake huyo, basi je, kulikuwa na haja gani kwa Jibril kushuka na picha yake wakati Mwanaisha anaishi umbali wa mita chache tu kutoka nyumbani kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.)? Mimi naamini kwamba bibi Mariyah Al-qibtiyyah aliyekuwa akiishi Misri akiwa mbali na Mtume (s.a.w.w.) na hapana yeyote aliyekuwa akitazamia kuja kwake, yeye ndiye aliyestahiki kuwa Jibril ashuke na picha yake na ambashirie Mtume (s.a.w.w.) kwamba Mwenyezi Mungu atamruzuku kutokana naye Ibrahim.Lakini riwaya hizi ni miongoni mwa uzushi wa Aisha ambaye alikuwa hapati kitu cha kujifaharisha kwa wake wenzi isipokuwa visa ambavyo mawazo yake huvizusha, au riwaya hizo ni katika uzushi wa Banu Umayyah kwa kupitia ulimi wa bibi Aisha ili wapate kuyatukuza mambo yake mbele ya watu wenye akili finyu. Ama kusema kwamba Jibril alikuwa haingii nyumbani kwa Mtume akiwa kalala isipokuwa nyumbani kwa Aisha riwaya hii ni mbaya kuliko ile ya kwanza, kwani kinachofahamika katika Qur'an ni kuwa, Mwenyezi Mungu alimkemea bibi Aisha pale alipokula njama dhidi ya Mtume wake, akamkemea kwa kumjulisha kwamba, ''Jibril na Waumini wema na Malaika baada ya msaada wake (Mwenyezi Mungu) watamsaidia (Mjumbe wa Mwenyezi Mungu). Basi kauli za Masheikhe wetu si chochote isipokuwa ni dhana na mawazo yao tu, na kwa hakika dhana haitoshelezi cho chote mbele ya haki, basi waambie je mnayo elimu yoyote ile muitoe kwetu sisi, (hamna) bali hakuna mnachokifuata isipokuwa ni dhana na hamna chochote ila mnazua tu. Aisha baada ya kufariki Mtume (s.a.w.w) Ama tunapoyasoma maisha ya Ummul-Muminina Aisha binti Abubakr baada ya mumewe kufariki (roho yangu iwe fidia yake) na baada ya mambo kumkalia vizuri na baba yake kuwa ndiyo Khalifa na kiongozi juu ya umma wa Kiislamu, hapo ndipo bibi Aisha akawa yeye ndiye mwanamke bora katika dola ya Kiislamu kwa kuwa mumewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na baba yake ni Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.Kwa kuwa yeye anaamini au anadhani kuwa ndiye mbora miongoni mwa wakeze Mtume (s.a.w.), si kwa chochote bali kwa kuwa Mtume alimuoa akiwa bikra, na Mtume hakupata kuoa mwanamke bikra ila yeye, kisha Mtume (s.a.w.) alifishwa na yeye bibi Aisha akiwa katika umri wa ujana, kwani umri wake ulikuwa miaka kumi na minane siku Mtume alipofishwa kwa mujibu wa makadirio ya juu na riwaya zilizo mashuhuri. Na wala hakuishi pamoja na Mtume isipokuwa miaka sita au minane kwa tofauti za riwaya, kwani miaka ile ya mwanzo aliimaliza akicheza michezo ya kitoto hali yakuwa ni mke wa Mtume (s.a.w.) na katika hali hiyo kama alivyomueleza Burairah mjakazi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliposema kuhusu Aisha: "Hakika yeye ni msichana mdogo akilala na kuuacha unga uliokandwa na matokeo yake huja mnyama miongoni mwa wanyama wafugwao na kula ule unga uliokandwa."[63] Naam miaka kumi na minane kwa msichana aliyefikia umri wa kuvunja ungo kama isemwavyo hivi leo, na aliyetumia nusu ya umri wake akiwa pamoja na Mtume na akiwa miongoni mwa wakewenza wanaofikia kumi au tisa, na (siyo wakeze Mtume tu alioishi nao bibi Aisha nyumbani kwa Mtume) bali kuna mwanamke mwingine ambaye tumeghafilika kumtaja aliyekuwepo katika zama za maisha ya bibi Aisha. Mwanamke huyo alikuwa ni tishio kwa Aisha kuliko mkemwenziwe yeyote, kwani upendo wa Mtume (s.a.w.w.) kwake ulikuwa hauna mfano naye si mwingine bali ni Fatmah ambaye ni binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) aliyemzaa kwa bibi Khadija, na Khadija huyu Mkuu ni nani? Huyo ni Khadija ambaye Jibril alimtolea salam na kumbashiria nyumba peponi isiyokuwa na fujo wala makelele [64] Khadija ambaye ilikuwa haiwezekani kupita tukio lolote isipokuwa Mtume (s.a.w.w.) humtaja Khadija, na hapo ndipo Aisha maini humkata na moyo kumuwaka kwa wivu, kwa hasira zake hufura na kupoteza muruwa wake, akawa hutukana kwa lile aonalo linafaa na bila kujali heshima na uhusiano uliopo kati yake na mumewe.Hebu na tumsikilize yeye mwenyewe bibi Aisha anasimulia juu ya Khadija kama alivyopokea Bukhari, Ahmad, Tirmidhi na Ibn Majah: Amesema bibi Aisha, "Sikumuonea wivu mke yeyote wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kama nilivyomuonea wivu Khadija na hii ni kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akimtaja mara nyingi na kumsifu, basi nilimwambia (Mtume) ni kwa jambo gani unamtaja ajuza huyu miongoni mwa maajuza wa Kiquraish mwenye kona za midomo myekundu, na amekwisha kufa zamani, hapana Mwenyezi Mungu amekubadilishia mbora kuliko yeye." Bibi Aisha anasema, (ghafla) uso wa Mtume ulibadilika sana na nilikuwa siuoni kubadilika hivyo ila unaposhuka Wahyi na akasema (Mtume): "Wallahi Mwenyezi Mungu hajanibadilishia mke bora kuliko yeye (Khadija), kwa hakika aliniamini wakati watu waliponipinga na alinisadiki wakati watu waliponikatalia na aliniruhusu nitumie mali yake wakati watu waliponinyima na Mwenyezi Mungu aliniruzuku watoto kwake wakati alininyima watoto kwa wanawake wengine." Hapana shaka kwamba jibu la Mtume (s.a.w.w.) kwa Aisha linabatilisha madai ya wale wasemao kwamba Aisha alikuwa bora mno na akipendwa mno miongoni mwa wake wa Mtume (s.a.w.w.). Na ubaya zaidi ni kwamba, Aisha aliongeza wivu na chuki kwa Khadija pale Mtume wa Mwenyezi Mungu alipomkemea kwa kemeo hili na akamjulisha kwamba Mola wake hajambadilisha mke bora kuliko Khadija. Ni kwa mara nyingine tena Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) anatufahamisha kwamba yeye hafuati matamanio na wala hapendi (kwa sababu ya) uzuri na bikra, kwani Khadija (a.s.) kabla ya Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kisha olewa mara mbili na alikuwa mkubwa zaidi ya Mtume kwa miaka kumi na mitano, lakini pamoja na hayo Mtume alimpenda mno wala hakuacha kumtaja, na kwa hali hii naapa kuwa hii ndiyo tabia ya Mtume (s.a.w.w.) ambaye hupenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na huchukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.


Kwa hiyo basi kuna tofauti kubwa kati ya riwaya hii ya kweli na zile riwaya zilizoundwa ambazo zinadai kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akimpenda mno Aisha mpaka wakeze wanamtumia ujumbe kumtaka awe muadilifu kuhusu Binti ya Abu Quhafah. Na hebu tumuulize Ummul-Muminina Aisha ambaye hakupata kumuona Bibi Khadija japo mara moja katika uhai wake wala hakukutana naye, ni vipi anamsema kuwa ni kikongwe mwenye kona za midomo myekundu? Na je, hii ndiyo tabia ya mwanamke Muumini wa kawaida ambaye inaharamishwa kwake kumteta mwenzake awapo hai, basi vipi itakuwa hali kwa yule aliyekwisha kufa na kufika mbele ya Mola wake? Basi hali itakuwaje ikiwa mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ndiye atetwaye, mke ambaye Jibril alikuwa akishuka nyumbani mwake na kumbashiria kupata nyumba yenye utulivu peponi? Na kwa kutilia mkazo ni kwamba, chuki na wivu uliokuwa ukifukuta ndani ya moyo wa Aisha kwa sababu ya Khadija ilikuwa ni lazima ufure na upate mahali pa kupumulia, vinginevyo bibi Aisha angepasuka!! Kwa hiyo basi Aisha hakupata (mahali pa kushushia pumzi zake) isipokuwa hapo mbele yake alikuweko Fatmah binti ya Khadija ambaye ni mtoto wa kambo wa bibi Aisha na ambaye alikuwa katika umri unaolingana naye au anamzidi kidogo kwa (mujibu wa) tofauti ya riwaya. Bila shaka vile vile kwamba lile pendo la kweli la Mtume (s.a.w.w.) kwa Khadija lilitengenezeka na kuimarika kwa binti yake wa pekee Fatmah, kwani ndiye yeye peke yake aliyeishi pamoja na baba yake akiwa amebeba sifa njema kutoka kwa Khadija ambazo Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akizipenda, Mtume akawa humwita (Fatmah) mama wa baba yake.Bibi Aisha alizidi wivu kumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu anamtukuza na kumwita kuwa yeye ni mwanamke bora kuliko wanawake wote ulimwenguni na ni mwanamke bora kati ya wanawake wa peponi. Kisha Mwenyezi Mungu akamruzuku Mtume kutokana na Binti yake huyu mabwana wa vijana wa peponi Hasan na Husein, na ndiyo maana Aisha akawa humuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) anakwenda kwa Fatmah na kukesha huko kwa ajili ya kuwalea wajukuu zake na anasema: "Wanangu hawa wawili ni viliwazo vyangu katika umma huu." Ikawa huwabeba mabegani kwake, na yote hayo humuongezea Aisha wivu kwa kuwa yeye ni mgumba. Kisha Aisha alizidi wivu mpaka akamuingiza katika wivu huo mume wa Fatmah baba wa Hasan na Husein, si kwa lolote bali ni kwa sababu ya Mtume akimpenda mno mume wa Fatmah na kumtanguliza mbele kuliko baba yake Aisha kwa kila hali, basi hapana shaka kwamba, bibi Aisha alikuwa akiishi katika mazingira haya. Hatimaye anamuona mwana wa Abu-Talib (Ali) anafuzu kila mara dhidi ya baba yake (Aisha) na anakuwa mbele kwa kupendwa na Mtume (s.a.w.w.) na kumtanguliza juu ya wengine.


Aisha hakika alikuwa akifahamu kwamba baba yake alirudi akiwa ameshindwa katika vita ya Khaibar yeye pamoja na aliokuwa nao katika jeshi, na kwamba Mtume (s.a.w.w.) alihuzunishwa na jambo hilo na akasema: "Kesho nitampa bendera mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda mtu huyo, ni shujaa wala si mwoga." Na mtu huyo alikuwa ni Ali ibn Abu Talib mume wa Fatmah, kisha Ali alirudi baada ya kushinda vita ya Khaibar akiwa na Safiyyah binti Huyayi ambaye Mtume (s.a.w.w.) alimuoa na kwa hilo moyo wa Aisha ukawa kama umepigwa na radi. Kadhalika Aisha alifahamu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alimtuma baba yake akiwa na Suratul-Baraah ili akaifikishe (awasomee) Mahujaji, lakini baadaye Mtume alimtuma Ali ibn Abi Talib amfuate na akaichukue kutoka kwa Abubakr, na huyo baba yake Aisha akarudi huku analia na kumuuliza Mtume sababu (ya kumrudisha). Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akamjibu, "Hakika Mwenyezi Mungu ameniamuru asifikishe Surah hiyo isipokuwa mimi au mmoja katika watu wa nyumba yangu."


Bila shaka vile vile bibi Aisha alikuwa akifahamu kwamba Mtume (s.a.w.) alimtawaza mwana wa ammi yake Ali (a.s.) awe ni Khalifa kwa Waislamu baada yake, na akawaamuru Masahaba na wake zao wampongeze kwa kupata uongozi kwa waumini, na baba yake Aisha alikuja akiwa miongoni mwa watu wa mwanzo mwanzo huku akisema: "Pongezi pongezi ewe Mwana wa Abu Talib, leo umekuwa kiongozi wa kila Muumini mwanaume na Muumini wa kike." Bila shaka Bibi Aisha alikuwa akifahamu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimpa uamiri jeshi kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi na saba juu ya baba yake, na Mtume akamuamuru baba yake Aisha aende akiwa chini ya uongozi wa kijana na huyu na aswali nyuma yake. Hapana shaka kwamba Ummul-Muuminina Aisha alijihusisha kikamilifu katika matukio haya, kwani (yaonekana) alikuwa amekamia makusudio ya baba yake ya kugombea Ukhalifa na njama hizo zilikuwa zikipikwa na viongozi wa makabila katika Maquraish. Kwa hiyo basi alikuwa akizidisha chuki na ubaya dhidi ya Ali na Fatmah, na akijaribu kwa kila juhudi kuingilia kati ili kubadilisha msimamo kwa ajili ya maslahi ya baba yake kwa njia mbali mbali na kwa gharama yoyote ile.


Bila shaka tumekwisha muona ni jinsi gani alivyomwita baba yake eti kwa niyaba ya Mtume na akamuamuru aswalishe watu, baada ya yeye Bibi Aisha kugundua kwamba Mtume (s.a.w.w.) amemwita Ali ili amkabidhi jukumu hilo, na Mtume alipoifahamu njama hiyo alilazimika kutoka (kwenda msikitini) na hapo ndipo Abubakr alipompisha Mtume (s.a.w.w.) akawasalisha watu hali ya kuwa amekaa, na akamkemea kwa kumwambia. "Hakika ninyi ndiyo wale wanawake waliomfanyia vitimbi Yusuf' akiwa na maana kwamba, Vitimbi vya Aisha ni vikubwa. Na mtu yeyote mwenye kufanya uchambuzi ndani ya tukio hili ambalo bibi Aisha mwenyewe amelisimulia kwa njia ya riwaya zenye kutofautiana na kupingana, atakuta kuna mgongano ulio wazi kwani ilivyo ndivyo ni kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa kisha muandaa baba yake Aisha na kumuamuru atoke katika jeshi chini ya uongozi wa Usamah ibn Zaidi kabla ya kuswaliwa kwa Sala hiyo siku tatu kabla. Inavyofahamika moja kwa moja ni kwamba, kiongozi wa jeshi ndiye Imamu katika Sala, kwa hiyo Usamah alikuwa ni Imam wa Abubakr ndani ya msafara wa jeshi hilo.Bibi Aisha alipokwishafahamu jambo hilo aliona kuwa ni udhalili kwa baba yake na aliyajua makusudio ya Mtume (s.a.w.), na hasa alipogundua kwamba Mtume hakumchagua Ali ibn Abi Talib kuwemo ndani ya jeshi hilo ambalo alikuwa ameliandaa ili ndani ya jeshi hilo wawemo vigogo wa Muhajirina na Ansar ambao kwa Maquraish walikuwa ni watu watukufu na wenye daraja kubwa.

Isitoshe mama Aisha alikwisha fahamu kama ambavyo wengi wa masahaba walikwisha fahamu kuwa siku za kuishi Mtume (s.a.w.) zimebakia za kuhesabu, na huenda bibi Aisha aliungana na maoni ya Umar ibn Khattab kwamba sasa Mtume anaweweseka hajui alifanyalo. Kwa sababu hiyo wivu wake mkali ukamlazimisha kufanya vile aonavyo ili mradi tu akinyanyue cheo cha baba yake dhidi ya Ali Bin Abi Talib ambaye ni mgomvi wake.


Kutokana na yote haya ndiyo maana bibi Aisha alikanusha kuwa Mtume aliusia kuwa Ali ni Khalifa, na kwa sababu hiyo alitaka kuwakinaisha watu wenye mawazo finyu kwamba Mtume (s.a.w.) alikufa akiwa amempakata na ameegemea kifuani kwake, na pia ndiyo maana akasimulia kwa kusema kwamba, "Mtume alipokuwa mgonjwa alimwambia (bibi Aisha) niitie baba yako na nduguyo ili niwaandikie maandiko kwani huenda akadai mwenye kudai, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumini hawamkubali yeyote isipokuwa Abubakr." Basi Je, kuna mwenye kumuuliza bibi Aisha, "Ni jambo gani lililomzuwia asiwaite?"