WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Kama uonavyo ewe msomaji kwamba, madai yote hayana ushahidi wowote na wala akili na ukweli ulivyo havikubaliani. Sisi tutaleta ushahidi ili kuyatengua (madai hayo). Kama Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akimpenda kwa kuwa yeye ni mzuri na kuwa yeye ni bikra pekee aliyepata kumuoa, basi ni jambo gani lililomzuwia Mtume kuowa wanawake bikra na wazuri ambao walikuwa bora kwa wema na uzuri na walikuwa wakipigiwa mfano (kwa uzuri) katika makabila ya Kiarabu wakati yeye Mtume alikuwa akiwafahamu' Na juu ya hayo wanahistoria wanautaja wivu wa Aisha kwa Zainab binti Jah-shi na Safiyyah binti Huyayi na Mariyah Al-Qibtiyyah kwa sababu wao walikuwa wazuri zaidi kuliko yeye. Ibn Saad ndani ya Tabaqat yake Juzuu ya 8 uk.148 na Ibn Kathir katika tarekh yake wameleta riwaya kwamba, Mtume (s.a.w.w.) alimuoa Mulaikah binti Ka'b, na bibi huyu alikuwa akifahamika kwa ubora na uzuri, basi Aisha akamwendea bibi huyu (nyumbani kwake) kisha akamwambia: "Hivi huoni haya kuolewa na mtu ambaye amemuua baba yako?" (Kutokana na ushawishi huu) bibi yule akamwambia Mtume: "Najilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana nawe." (Neno hilo likamchukiza) Mtume (s.a.w.w.) akamtaliki bibi huyo, kisha jamaa zake wakaja kwa Mtume (s.a.w.w.) wakamwambia "Huyu ni mtoto mdogo naye hana hiyari, kwa hakika amehadaiwa mrejee" Mtume (s.a.w.w.) akakataa, na baba wa binti huyu aliuawa siku ya Fat-hi Maka, aliuawa na Khalid ibn Walid mahala paitwapo Khindimah.


Riwaya hii inatujulisha wazi kwamba makusudio ya Mtume wa Mwenyezi Mungu haikuwa kuoa mabinti wadogo tena wazuri, vinginevyo (kama malengo yake yangekuwa ni kuoa watoto wadogo tena wazuri) asingeachika Mulaikah binti Ka'b hali yakuwa ni msichana mdogo na bora tena mzuri kama ambavyo riwaya hii na nyinginezo zinavyotuonesha njia alizozitumia Aisha kuwahadaa wanawake waumini wasio na kosa lolote na (kusababisha) wasiolewe na Mtume wa Mwenyezi Mungu? Na (huyu bi Mulaikah) alitanguliwa na kuachika kwa As-ma binti Nuuman pale Aisha alipomuonea wivu akamwambia kuwa: "Mtume humfurahia sana mwanamke pindi akiingia kwake akamwambia, najilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana nawe." (Bibi Aisha pia) anamchochea huyu bi Mulaikah hisia za mauaji ya baba yake na kwamba aliyemua ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na anamwambia, "Huoni haya kuolewa na mtu aliyemuua Baba yako?" Maskini binti huyu hakuwa na jawabu lolote isipokuwa ni kumchukia Mtume wa Mwenyezi Mungu, unadhani angejibu nini binti huyo wakati ambapo watu walikuwa bado wapo kwenye zama za ujinga na wakichukua kisasi na kumcheka asiyechukua kisasi kwa ajili ya baba yake? Kilichobaki tujiulize na tunayo haki ya kujiuliza, Ni kwa nini Mtume (s.a.w.w.) aliwaacha wanawake hawa wawili bila kosa lolote na ambao walikuwa muhanga wa vitimbi na hadaa za Aisha?


Kabla ya kufanya kitu cho chote, hatuna budi tufahamu katika akili zetu kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) ni Maasum (hafanyi dhambi) na wala hamdhulumu yeyote wala hafanyi ila ni haki, basi (kama ni hivyo) hapana budi kwa kuwataliki (kina mama hao) kuna hekima ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndiyo wanaoifahamu kama ambavyo Mtume hakumtaliki Aisha pamoja na matendo yake, vile vile kuna hekima yake. Pengine huenda tunaweza kuwa na msimamo wa jambo fulani katika hekima hiyo katika uchambuzi ufuatao. Ama kwa upande wa yule mwanamke wa kwanza ambaye ni Asma binti Nuuman, bila shaka kutotumia kwake busara kunadhihirika pale hila za Aisha zilipomchemsha, basi neno lake la kwanza alilomkabili nalo Mtume wa Mwenyezi Mungu wakati alipomnyooshea mkono wake likawa "Ninajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana nawe". Pamoja na uzuri wake na ubora wake Mtume hakumbakisha kutokana na ujinga wake (wa kutofikiri). Ibn Saad na wengineo anasema ndani ya Tabaqat yake Juz.8 uk.145. Imepokewa kutoka kwa ibn Abbas amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alimuoa Asma binti Nu'uman na (bibi huyu) alikuwa mzuri mno miongoni mwa wanawake wa zama zake na alikuwa ametimia." Basi huenda Mtume (s.a.w.w.) alitaka kutufundisha kwamba akili pevu ni bora kuliko uzuri, kwani ni mara ngapi mwanamke mzuri ujinga wake umempelekea kufanya uchafu?


Ama kwa upande wa yule mwanamke wa pili ambaye ni Mulaikah bint Ka'ab aliyebeuliwa na Aisha kwa kuambiwa kuwa mumewe ndiye aliyemuua baba yake, Mtume hakutaka mwanamke huyu maskini (ambaye alikuwa na umri mdogo asiye na uamuzi kama walivyoshuhudia hayo jamaa zake aishi pamoja na) Aisha mwenye vitisho na mawazo yaliyo komaa mambo ambayo huenda yangesababisha matatizo makubwa hasa hasa kutokana na Aisha ambaye asingempa nafasi ya kufurahi na Mtume (s.a.w.w.). Na hapana shaka kwamba zipo sababu nyingine ambazo Mtume wa Mwenyezi Mungu anazijuwa na kwetu zimefichikana. Jambo la muhimu ni kufahamu kwamba, Mtume (s.a.w.) alikuwa havutiki kwa uzuri na matamanio ya mwili na kijinsiya kama walivyodhania baadhi ya watu wajinga na baadhi ya Mustashrikina[58] ambao wanasema eti lengo la Muhammad lilikuwa ni kujipatia wanawake wazuri. Kwa hakika tumeona jinsi gani Mtume wa Mwenyezi Mungu alivyowataliki wanawake hawa wawili bila kujali udogo wao na uzuri wao, kwani walikuwa wazuri mno katika zama zao kama ilivyoandikwa katika vitabu vya historia na vitabu vya hadithi. Kwa hiyo kauli ya anayedai kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akimpenda Aisha kwa umri wake mdogo na uzuri wake inapingwa na haikubaliki. Ama wale wasemao kwamba Mtume alimpenda Aisha kwa sababu ni binti ya Abubakr, jambo hili siyo sahihi, lakini tunaweza tu kusema kwamba Mtume alimuoa Aisha kwa sababu ya Abubakr, kwa kuwa Mtume aliwaoa wanawake kutoka katika makabila mbali mbali kwa sababu za kisiasa ili kuziunganisha nyoyo (za watu hao) na kuyaelekeza mapenzi na huruma kwa makabila hayo badala ya (kueneza) ugomvi na chuki. Hapana shaka kwamba Mtume alimuoa dada yake Muawiyah, Ummu Habibah binti Abi Sufiyan, wakati ambapo huyu Abu Sufiyan alikuwa ni adui namba moja wa Mtume (s.a.w.w.) na alifanya hivyo kwa kuwa yeye (Mtume) siyo mtu mwenye chuki pia yeye ndiye rehma kwa walimwengu. Huruma na upole wa (Mtume s.a.w.) vilivuka kutoka kwenye makabila ya Kiarabu mpaka akafikia hadi ya kuwaolea Mayahudi na Wakristo na hata Waqibt (wa Misri) ili awaunganishe watu wa dini wao kwa wao.


Jambo muhimu linalotupasa sisi kulifahamu kupitia maarifa tuyasomayo ndani ya vitabu vya Sira ni kwamba Abubakr ndiye aliyemtaka Mtume (s.a.w.w.) amuoe binti yake Aisha, kama ambavyo Umar naye alimtaka Mtume (s.a.w.) amuowe binti yake Hafsah, Mtume (s.a.w.) alikubali kwani moyo wake uko wazi kuwaenea walimwengu wote. Mwenyezi Mungu anasema: "Na lau ungekuwa (wewe Muhammad) ni mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka wangekukimbia." (Qur'an, 3:159). Tukizirejea riwaya ambazo amezitaja Aisha na akasema katika riwaya hizo kwamba, "Mtume (s.a.w.) hakukaa muda mrefu ila alidhani kuwa nimepitiwa na usingizi, akachukua nguo yake taratibu na akafungua mlango akatoka kisha akaufunga." Basi tunafahamu uongo wa madai ya kwamba Mtume alikuwa hawezi kuvumilia kwa kumkosa Aisha.[59] Matokeo ya utafiti huu siyo natija ya kubahatisha iliyoundwa kimawazo tu (bila ushahidi) sivyo kabisa, bali inao ushahidi ndani ya vitabu vya Kisunni. Muslim ameandika riwaya ndani ya Sahih yake, na wengineo ndani ya Sihah zao za Kisunni kwamba, Umar ibn Khatab amesema, "Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu alipojitenga mbali na wakeze, niliingia msikitini nikawakuta watu wakiwa wanawaza na wanasema, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) amewataliki wakeze, na tukio hili lilitokea kabla hawajaamriwa kuwa na hijab, basi Umar akasema, hapana budi nilitambue jambo hilo leo. Akasema, nikaingia kwa Aisha nikamwambia, Ewe binti Abubakr hivi hadhi yako imefikia kiasi cha kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.)"?


Aisha akasema, "Ewe Mwana wa Khatab kuna uhusiano gani kati yangu na wewe kamuulize binti yako" Omar akasema: "Nikaingia nyumbani kwa Hafsah binti Umar nikamwambia, Ewe Hafsah hivi hadhi yako imefikia kiasi cha kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, Wallahi bila shaka wewe unajua kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu hakupendi na lau siyo mimi Mtume wa Mwenyezi Mungu angekwisha kukuacha, Hafsah akalia sana"[60] Bila shaka riwaya hii inatujulisha wazi kwamba hapana shaka kuwa Mtume (s.a.w.w.) alimuoa Hafsah binti Umar si kwa sababu ya kumpenda, lakini ni kwa maslahi ya kisiasa ambayo hali halisi ilipelekea iwe hivyo. Miongoni mwa mambo yanayotuongezea uhakika wa kukubalika kwa mtazamo tulionao katika kuyapata matokeo mazuri ya uchambuzi huu ni kwamba, Umar ibn Khatab anamuapa Mwenyezi Mungu kuwa Mtume (s.a.w.) hampendi Hafsah, na Umar anatuongezea uhakika tena kwamba binti yake Hafsah yeye pia anafahamu ukweli huu wenye uchungu, pale alipomwambia, "Wallahi hakika wewe unafahamu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu hakupendi." Basi baada ya hayo hakuna shaka yoyote inayobakia kwetu sisi kwamba kuolewa kwa Hafsah kulikuwa ni kwa ajili ya maslahi ya kisiasa (hasa) pale Umar aliposema: "Lau si mimi Mtume wa Mwenyezi Mungu angekwisha kukuacha."


Kwa hiyo riwaya hii inatufanya tuifikirie vile vile sababu iliyomfanya Mtume kumuoa Aisha binti Abubakr na kuonesha kwamba Mtume alisubiri na akavumilia maudhi yote ya Aisha kwa ajili ya Abubakr, vinginevyo kwa Hafsah itakuwa ni afadhali zaidi Mtume ampende yeye kwani hapakuwa na mambo mengi yaliyotokana naye aliyoyafanya kumuudhi Mtume, tena kwa kiwango kikubwa kuliko mambo aliyoyatenda Aisha binti Abubakr. Na tukiuchunguza ukweli halisi na tukazipuuza riwaya zilizozushwa ambazo Banu Umayyah wamezitengeneza kuhusu ubora wa Aisha, bila shaka tutakuta kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu mara nyingi alikuwa akikerwa na Aisha na mara nyingi alikuwa akimgombeza. Hapa tunanakili riwaya moja aliyoiandika Bukhari na wanachuoni wengi wa hadithi wa Kisunni inayoeleza kiwango cha kero ambayo alikuwa akiionesha Ummul-Muuminina Aisha mbele ya mumewe (ambaye ni) Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.). Bukhari amethibitisha ndani ya Sahih yake katika juzuu ya saba katika mlango wa "Kauli ya mgonjwa, hakika ninaumwa, au Eeh kichwa changu. " Amesema: Nilimsikia Qasim ibn Muhammad amesema: "Aisha alisema, Eeh, kichwa changu!" Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema, "Lau hali hiyo ingekupata nami nikawa ni hai basi ningekutakia msamaha na kukuombea dua" Aisha akasema,"Ole wangu, Wallahi hakika nikuonavyo wewe (naona) unapenda nife, na lau nitakufa bila shaka jioni (usingejali bali) ungeendelea kufurahi na baadhi ya wake zako." [61] Je, riwaya hii inakujulisha juu ya Mtume kumpenda Aisha?


Mwisho tunafupisha (kwa kusema) kwamba, hakika Banu Umayyah wakiongozwa na Muawiya ibn Abi Sufiyan wanamchukia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), na tangu pale Ukhalifa ulipowazungukia walifanya (kila njia) kuubadilisha ukweli kinyumenyume, wakawapandisha (kwa ubora) watu fulani fulani mpaka wakawafikisha kwenye daraja la kusifiwa na kutukuzwa, wakati ambapo (watu hao) katika zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w.) walikuwa ni watu wa kawaida tu wala hawakuwa na lolote la maana. Na wakati huo huo Banu Umayyah waliwanyanyasa watu wengine ambao walikuwa katika daraja tukufu na yenye heshima katika siku za uhai wa Mtume (s.a.w.w.). Mimi naamini kwamba, kipimo chao pekee katika kuwapandisha daraja baadhi ya watu na kuwanyanyasa wengine hakuna isipokuwa ni ule uadui wao mkali na chuki yao isiyo na kipimo dhidi ya Mtume Muhammad na watu wa nyumba yake (ambao ni) Ali, Fatmah, Hasan na Husein (a.s). Na kwa hali hiyo kila mtu ambaye alikuwa mpinzani wa Mtume (s.a.w.w.) na watu wa nyumba yake ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa sana sana, Banu Umayyah walimpandisha daraja na kumtengenezea riwaya na ubora kemkem, walimkumbatia na kumpa vyeo na zawadi nyingi na hatimaye akawa mwenye hadhi kwa kutukuzwa na watu na kuheshimiwa.


Ama kila yule aliyekuwa akimpenda Mtume (s.a.w.w.) na akimtetea, wao walifanya kila juhudi kumuangusha na kumzushia maovu ya uongo na kumtengnezea riwaya ambazo zinakanusha heshima yake na ubora wake. Kwa hakika hali kama hii ndiyo iliyomfanya Umar ibn Khatab akawa ndiyo kiongozi mkuu wa Uislamu katika zama za utawala wa Banu Umayyah, Umar ambaye alikuwa akimpinga Mtume (s.a.w.w.) katika kila maamrisho yake mpaka akamtuhumu Mtume (s.a.w.w.) kwamba anaweweseka wakati wa mwisho wa uhai wake Mtume (s.a.w.w.). Ama Ali ibn Abi Talib ambaye kwa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na cheo kama kile cha Nabii Harun kwa Nabii Musa, na ambaye alikuwa akimpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wakimpenda (Ali) ambaye ni mtawala wa kila muumini, zilipofika zama za utawala wa Banu Umayyah akawa analaaniwa kwenye Minbar za Waislamu kwa muda wa miaka themanini. Hali kama hii (katika dola ya Banu Umayyah) Aisha ambaye alimsonga koo Mtume (s.a.w.) na akaasi amri zake nyingi kama ambavyo (kwa kumuasi Mtume) alimuasi Mola wake na akampiga vita wasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na kwa fitina yake hiyo kubwa ambayo Waislamu waliifahamu, alisababisha mauaji ya maelfu ya Waislamu. basi mwanamke huyu akawa ndiyo mwanamke mashuhuri katika Uislamu na eti watu wajifunze kwake hukumu za dini. Ama bibi Fatmah Zahra mwanamke bora ulimwenguni, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu hukasirika pindi Fatmah anapokasirika na huwa radhi Mwenyezi Mungu pindi Fatmah anapokuwa radhi, huyu akawa ni mtu aliyesahauliwa kabisa, kiasi kwamba alipofariki alizikwa usiku tena kwa siri. Na kabla ya hapo alitishiwa kuchomwa moto, na walimkamua tumbo lake kwa kumbana na mlango mpaka ujauzito ukampromoka, na kutokana na mazingira haya hakuna hata Muislamu mmoja katika Masunni anayefahamu japo riwaya moja aliyoipokea Fatmah kutoka kwa baba yake.Hali ni hiyo hiyo (kwa shinikizo la Banu Umayyah) Yazid ibn Muawiyah na Ziyad mwana wa baba yake na mwana wa Mar-wan na Haj-Jaj na mwana Al'as na wengineo miongoni mwa waovu waliolaaniwa kwa mujibu wa Qur'an kupitia ulimi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, wote hawa wakawa ndiyo viongozi wa waumini na watawala wa mambo yao. Ama Hassan na Husein ambao ni mabwana wa vijana wa peponi na ni kiliwazo cha Mtume katika umma huu na ambao ni Maimamu wanaotokana na kizazi cha Mtume (s.a.w.w.) ambao ndiyo ngome ya umma huu, wao wakawa ni wenye kufukuzwa, kutiwa magerezani na kuuawa kwa kutiliwa sumu. Mazingira ni yale yale, yule mnafiki Abu Sufiyan ambaye hapana vita yoyote iliyotokea dhidi ya Mtume isipokuwa yeye alikuwa ni kiongozi wa vita hiyo, huyu akawa mwenye kusifiwa na kushukuriwa mpaka ikasemwa eti Mtume kasema: "Yeyote atakayeingia ndani ya nyumba ya Abu Sufiyan atakuwa katika amani."


Kinyume chake Bwana Abu Talib ambaye ni mlezi wa Mtume (s.a.w.w.) na alimlinda Mtume kwa uwezo wake wote, na yeye ndiye aliyetumia uhai wake akiwapinga jamaa zake na watu wake kwa ajili ya kufanikisha mwito wa mtoto wa nduguye kiasi kwamba aliishi miaka mitatu ndani vikwazo vya kiuchumi pamoja na Mtume kwenye viunga vya mji wa Maka, na aliificha imani yake kwa ajili ya maslahi ya Uislamu, ili tu zipatikane njia za yeye kuwa pamoja na Maquraish wasiwaudhi Waislamu kwa namna wanavyotaka, na hilo ni kama ilivyokuwa kwa yule Muumini wa jamaa ya Firaun aliyeficha imani yake, Abu Talib huyu malipo yake yakawa eti yumo ndani ya moto wenye joto hafifu na akiweka humo mguu wake mafuta yaliyoko katikati ya mifupa yake yatachemka. Kadhalika hali ni hiyo hiyo kwa Muawiya ibn Abi Sufiyan, ambaye ni muachwa huru mwana wa muachwa huru na ni mwenye kulaaniwa mwana wa aliyelaaniwa, mtu ambaye lizichezea hukumu za Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wala hakuzipa uzito unaostahiki, ambaye aliwauwa watu wema wasio na kosa lolote ili tu apate kuyatimiza malengo yake maovu, mtu ambaye alimtukana Mtume wa Mwenyezi Mungu mbele ya macho na masikio ya Waislamu,[62] mtu huyu akawa anaitwa ndiye mwandishi wa wahyi, na wanasema eti kwamba Mwenyezi Mungu amewaamini juu ya wahyi wake Jibril, Muhammad na Muawiyah, huyu akawa husifiwa kuwa yeye ni mwenye hekima, siasa na mnadhimu bora. Watu kama Abu Dharri Al-ghifari ambaye hapakuwepo mkweli kuliko yeye, huyu akaonekana kuwa ndiyo mwenye fitina. akapigwa na kufukuzwa na kuondolewa mjini Madina akapelekwa "Rabdhah."Nao Salmaan Al-Farisi, Miqdad, Ammar, Hudhaifah na Masahaba wote wema ambao walimtawalisha Ali na wakamfuata, kwa hakika walipambana na mateso na walitawanywa ovyo na kuuawa. Kutokana na mazingira haya basi, wafuasi wa Makhalifa, wafuasi wa Muawiyah na wafuasi wa madhehebu ambayo yaliundwa na tawala za kidhalimu, wao ndiyo waitwao "Ahl-lus-sunnah Wal-jamaa" ambao (kwa mtazamo wao)wanajiona kuwa ni wao pekee ndiyo wanaoutekeleza Uislamu ipasavyo na yeyote anayewapinga wanamuona kuwa yu miongoni mwa makafiri, hata kama atakuwa ni mfuasi wa Maimamu wema wa nyumba ya Mtume waliotakasika. Ama wafuasi wa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.), ambao wamemfuata (Ali) ambaye ni mlango wa elimu na mtu wa kwanza kusilimu, ambaye haki huzunguka pamoja naye popote alipo, na wakawafuata watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) ambao ni Maimamu Maasum, basi hawa wakawa ndiyo (huitwa) watu wa bid'a na upotofu, na yeyote mwenye kuwapinga na kuwapiga vita huyo ndiyo Mwislamu sawa sawa. "Lahaula wala quwwata illa billahil-aliyyil-adhim. " Amesema kweli Mwenyezi Mungu pale aliposema:"Na wanapoambiwa, msifanye uharibifu ulimwenguni wao husema, Sisi ni watenda mema, Hakika wao ni waharibifu lakini hawatambui. Na wanapoambiwa aminini kama walivyoamini watu, husema, Oh hivi sisi tuamini kama walivyoamini wapumbavu". Hakika wao ndiyo wapumbavu lakini hawatambui" (Qur'an 2:11-13).