WAULIZE WANAOFAHAMU

 
Ummul-mu'minina Aisha anaishuhudia nafsi yake.
Hebu na tumsikie bibi Aisha mwenyewe analeta riwaya (inayomuhusu) na ni namna gani (tutaona) wivu ulivyo mkosesha lengo lake na kisha ni jinsi gani alionesha tabia mbaya mbele ya Mtume (s.a.w.). Anasema bibi Aisha: "Safiyah mkewe Mtume alimletea Mtume (s.a.w.) chakula alichomtengenezea wakati Mtume akiwa nyumbani mwangu, nilipomuona mjakazi (analeta chakula hicho) nilianza kutetemeka na nikashindwa kujizuwia, kisha nikaipiga sahani (ya chakula) na nikaitupa (chini). Mtume wa Mwenyezi Mungu akaniangalia na nilifahamu hasira (iliyojitokeza) usoni mwake, basi nikasema, Najilinda kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu asije nilaani leo hii." Mtume akasema: "Badilisha." Nikasema, kafara yake ni kitu gani ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Mtume akasema, "Ni chakula kama chakula chake (kilichokuwa humu) na chombo kama chombo chake".[48] Na kuna mara nyingine ameleta riwaya inayomuhusu yeye mwenyewe amesema:"Nilimwambia Mtume, anakutosha Safiyyah (kwa jambo) kadha wa kadha," Mtume akaniambia, "Kwa hakika umesema jambo (ambalo) lau litachanganywa na maji ya bahari lingeyaharibu."[49] Subhanallah!!!. Ana hali gani Ummul-Muminina, yuko mbali mno na tabia njema na haki ambazo Uislamu umezifaradhisha katika kuharamisha kuteta na uzushi? Na hapana shaka kwamba kauli yake aliposema, "Anakutosha Safiyyah (kwa jambo) kadha wa kadha, na kauli ya Mtume aliposema kuwa neno hilo lau litachanganywa na maji ya bahari lingeyaharibu," jambo hilo alilolisema Aisha kuhusu mke mwenziwe Bibi Safiyyah inaonesha lilikuwa ni jambo la kutisha na lilikuwa jambo la hatari. Mimi naamini kwamba wapokezi wa hadithi waliliona kuwa ni baya na la kutisha basi wakalibadilisha kwa ibara ya "kadha wa kadha" kama ilivyo kawaida yao kwa mambo kama haya.


Huyu hapa tena Aisha Ummul-Muminina anaeleza kwa mara nyingine wivu wake kwa wakeze Mtume anasema: "Sikumuonea wivu mwanamke yeyote isipokuwa wivu huo utakuwa chini ya wivu niliomuonea "Mariyah" na hiyo ni kwa sababu alikuwa mzuri mno na Mtume wa Mwenyezi Mungu alimpenda, mwanzoni alipokuja naye alimfikishia kwenye nyumba ya Harithah ibn Nuuman, na tulitishika kutokana naye lakini mimi nilishindwa kuvumilia, ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipomuhamishia Aliyah, kisha akawa huenda huko. Jambo hilo lilikuwa zito mno kwetu sisi na Mwenyezi Mungu akamruzuku (Mtume) kutokana na Mariyah mtoto wa kiume nasi akatunyima".[50] Kama ambavyo wivu wa bibi Aisha ulivuka mipaka kutoka kwa mke mweziwe bibi Mariyah hadi kwa mtoto mdogo Ibrahim. Aisha amesema: "Ibrahim alipozaliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuja naye kwangu akasema, Hebu muangalie namna alivyofanana nami, basi mimi nikasema, Sioni kufanana kokote, Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Hivi huoni weupe wake na mwili wake? Nikamwambia, Yeyote aliyenyweshwa mazima ya kondoo huwa mweupe na hunenepa".[51] Wivu wa Mwanaisha ulivuka mipaka yote na hauelezeki hasa pale ulipomfikisha kumdhania vibaya na kumtilia wasi wasi na mashaka Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), kwani mara nyingi alikuwa akijifanya kalala wakati Mtume anapolala nyumbani kwa Aisha, lakini kumbe humchunga mumewe na kumchunguza mahali alipo katika giza na kumfuatilia popote anapokwenda. Hebu ione riwaya hii inayotoka ulimini mwa Mama Aisha riwaya ambayo ameiandika Muslim ndani ya sahihi yake na Imam Ahmad ndani ya Musnad yake na wengineo.


Amesema: "Ilipokuwa ni usiku wangu ambao Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kwangu, alirudi akaweka nguo zake, akavua viatu vyake akaviweka mbele ya miguu yake na akakunjua shuka yake juu ya kitanda chake kisha akalala, basi muda si mrefu alidhani mimi nimepitiwa na usingizi, alichukua nguo zake taratibu na akavaa viatu vyake taratibu halafu akafungua mlango akatoka kisha akaufunga mlango taratibu. Pale pale nami nikavaa nguo yangu na nikafunga shuka yangu nikatoka kumfuata nyuma yake mpaka akafika Baqii. Hapo akasimama kwa muda mrefu kisha akanyanyua mikono yake mara tatu, kisha akageuka nami nikageuka, akakaza mwendo nami nikakaza mwendo, akaongeza mwendo nami nikaongeza mwendo, alifika nami nimeshafika nikawa nimemtangulia nikaingia ndani, hakuna nilichofanya ila nililala, basi akaingia na akasema, Una nini ewe Aisha mbona unahema namna hii?. Nikamwambia, "Hapana lolote." Mtume akasema: "Lazima utaniambia vinginevyo Mwenyezi Mungu atanieleza." nikasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, namuapia baba yangu na mama yangu, basi nikamueleza hali ilivyokuwa. Akasema, "Wewe ndiyo ule weusi niliouona mbele yangu"? Nikasema, "'Ndiyo." Akanipiga kifuani pigo lililonipa maumivu, kisha akasema, "Hivi ulidhani Mwenyezi Mungu na Mtume wake watakudhulumu..."?[52] Na kuna mara nyingine bibi Aisha alisema, "Nilimkosa Mtume wa Mwenyezi Mungu basi nikadhani amekwenda kwa baadhi ya wajakazi wake, basi nikamtafuta, ghafla nikamuona amesujudu hali ya kuwa anasema, "Ewe Mola nisamehe"[53] Na mara nyingine amesema, "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu alitoka nyumbani mwangu usiku, basi nikaona wivu, aliporudi akayaona mambo ninayoyafanya, Mtume akasema, Una nini ewe Aisha je, umeona wivu? Nikasema, kwa nini mtu kama mimi nisione wivu kwa mtu kama wewe?!! Basi Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Hivi shetani wako kisha kuchukua?[54] Riwaya hii ya mwisho inajulisha wazi kwamba, bibi Aisha kila alipokuwa na wivu alikuwa anabadilika kutoka katika hali yake ya kawaida na kufanya mambo ya ajabu kama vile kuvunja vyombo au kuchanachana mavazi.Na ndiyo maana katika riwaya hii anasema, "Mtume alipokuja na akaona ninayoyafanya akasema, hivi shetani wako kisha kuchukua"? Hapana shaka kwamba shetani wa Aisha alikuwa akimchukua na kumzingira mara nyingi, na (shetani huyo) aliukuta moyo wa Aisha kuwa ni njia miongoni mwa njia za wivu. Imepokewa toka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema kwamba: "Wivu kwa mwanamume ni imani na kwa mwanamke ni kufru." Tafsiri yake ni kwamba, mwanamume anamuonea wivu mkewe kwa kuwa kisheria haifai awe na mshirika yeyote kwa mke huyo, ama mwanamke hana haki ya kuwa na wivu kwa mumewe kwa kuwa Mwenyezi Mungu amemruhusu mwanamume kuoa zaidi ya mke mmoja. Basi mwanamke mwema anayefuata hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu humpokea mke mwenziwe kwa moyo mkunjufu, kama isemwavyo leo hii hasa pale mumewe akiwa muadilifu mwenye msimamo na anamuogopa Mwenyezi Mungu. Je, nini fikra yako kuhusu uadilifu na msimamo wa Bwana aliyembora wa utu na kigezo cha ukamilifu, uadilifu na tabia njema? Sisi tunakuta kuna tofauti bayana kuhusu penzi la Mtume kwa Aisha na vile wasemavyo Ahlus-sunnah Wal-jamaa, eti kwamba Aisha alikuvva ni kipenzi mno kwa Mtume kuliko wakeze wengine, na kwamba alikuwa bora mno mbele yake mpaka kiasi wanaleta riwaya kwamba baadhi ya wake za Mtume walizitoa nauba zao (siku anazostahiki Mtume kuwa kwao) kwa Aisha walipofahamu kwamba Mtume (s.a.w.) anampenda mno bibi Aisha na havumilii kumkosa!!!. Je, hivi kweli inawezekana katika hali kama hii (tuliyoeleza juu ya Mama Aisha tukampata mtu kuutakasa na kuupa tafsiri (nyingine) wivu wa bibi Aisha usiokuwa na kipimo?


Ukweli unavyoonekana, ni kinyume cha alivyokuwa akifanya bibi Aisha, kwani wake wengine wa Mtume wao ndiyo wangestahiki kumuonea wivu Aisha kwa kuwa Mtume kampenda mno na kuegemea kwake kama wanavyodai na kueleza katika riwaya. Sasa, ni kitu gani kinachohalalisha wivu wa bibi Aisha.? Historia haikusimulia isipokuwa hadithi zake na vitabu vya Sirah vimejaa sifa zake na kwamba yeye ndiye kipenzi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu, mwenye kujipendekeza ambaye Mtume alikuwa hawezi kutengana naye. Mimi naitakidi kwamba, yote hayo yametokana na Banu Umayyah ambao walimpenda bibi Aisha na wakamtukuza pale alipoyatumikia maslahi yao na akawatengenezea riwaya za yale wayapendayo, pia alimpiga vita adui yao Ali ibn Abi Talib (a.s.). Mimi naamini kwamba, Mtume (s.a.w. w.) hakuwa akimpenda Aisha kutokana na hayo aliyomtendea, kama tulivyotangulia kueleza!! Basi itakuwaje Mtume wa Mwenyezi Mungu ampende mtu ambaye ni muongo, anateta, kufitinisha na kumtilia mashaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuwadhania kuwa wanafanya dhulma? Itakuwaje basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) ampende mtu ambaye anampeleleza na anatoka nyumbani mwake bila ruhusa ya Mtume ili tu atake kufahamu Mtume anakwenda wapi?


Itakuwaje kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ampende mtu ambaye anawatukana wakeze mbele yake japokuwa wamekwisha kufa? Ni vipi Mtume atampenda mtu ambaye anamchukia mwanawe Ibrahim na kumsingizia mama wa Ibrahim bibi Mariyah kuwa katenda dhambi?"[55] Ni vipi Mtume wa Mwenyezi Mungu atampenda mtu anayejiingiza kati ya Mtume na wakeze kwa kuzua uongo na mara nyingine kueneza chuki na kusababisha Mtume kuwataliki wakeze? Itakuwaje basi Mtume wa Mwenyezi Mungu ampende mtu ambaye anamchukia binti yake Fatmah, na anamchukia nduguye Mtume na mtoto wa ami yake Ali ibn Abi Talib kiasi kwamba (bibi Aisha anashindwa kulitamka jina la Imam Ali, na wala tu nafsi yake haimfurahii Ali kwa wema.[56] Yote haya na zaidi ya haya yalifanyika katika zama za uhai wa Mtume (s.a.w.), ama baada ya kufa kwake, na ni haki yasimuliwe wala hapana ubaya. Matendo yote haya Mwenyezi Mungu na Mtume wake waliyachukia na wala hawakumpenda aliyeyatenda, kwani Mwenyezi Mungu yeye ndiye haki na Mtume wake alikuwa akiitekeleza haki hiyo, hivyo basi hawawezi kumpenda mtu asiyekuwa kwenye haki.Hapo baadaye kwa kupitia utafiti uliotangulia tutafahamu kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa hampendi Bibi Aisha, bali alipata kuutahadharisha ummati wake kutokana na fitina ya bibi Aisha.[57] Kuna wakati fulani niliwauliza baadhi ya Masheikh sababu za Mtume (s.a.w.) kumpenda kupita kiasi Bibi Aisha peke yake kuliko wake wengine, walinipa majibu mengi na yote hayo hayakuwa na maana yeyote. Mmoja wao alisema: "Kwa kuwa Aisha alikuwa mzuri kisha mdogo na ndiye bikra pekee ambaye Mtume alimuoa na nakushirikiana na mwingine kwa bibi Aisha ila yeye Mtume peke yake". Mwingine akasema, "Kwa kuwa alikuwa ni binti ya Abubakris -Sidiq ambaye alikuwa pamoja na Mtume pangoni". Wa tatu alisema: "Hiyo ni kwa sababu Mama Aisha alihifadhi nusu ya dini kutoka kwa Mtume, kwa hiyo ni mjuzi mwenye kufahamu". Na wanne alisema, "Ni kwa sababu Jibril alipata kuja akiwa katika sura yake (bibi Aisha) na Jibril alikuwa haji kwa Mtume ila Mtume awapo nyumbani kwa Aisha".