UKWELI WA USHIA

 
NDOA YA MUTA'AA (Muda)NOUMAN:
Kwa nini nyinyi Mashia mnahalalisha-ndoa ya Muta'aa-au ndoa ya muda, wakati waislaam wote wamekubaliana ya kuwa ni haram?
RIDHA:
Ni kutokana na kauli ya Omar bin Khattab isemayo: Hakika Mtume (s.a.w) aliihalalisha na kuijuzisha!.
NOUMAN:
Ni ipi kauli hiyo?
RIDHA:
Bwana Jaahidh [1] na Qurtubiy [2] na Sarkhasiy Al-hanafiy [3], na Fakhrur-raziy [4]na wengine wengi kati ya wanazuoni wa kisunni wamepokea ya kuwa Omar alisema katika hotuba yake:
متعتان كانتا علي عهد رسول الله صلي الله عليه وآله وسلم وأنا أنهي عنهما, وأعاقب عليهما: متعة الحج, ومتعة النساء!
Muta'aa mbili zilikuwa ni halali katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu na mimi ninazizuia, na nitamuadhibu mwenye kuzitekeleza Muta'a hizo: Nazo ni Muta'atul-haji, na Muta'atun-nisaa (yaani haji tamatui na ndoa ya Muta'a) Na katika Historia ya Ibnu Khalakan [5] amepokea ya kuwa Omar alisema:
متعتا ن كانتا علي عهد رسول الله صلي الله عليه وآله وسلم وعلي عهد أبي بكر وأنا أنهي عنهما
(Muta'aa mbili zilikuwepo katika zama za Mtume (s.a.w) na katika zama za Abu Bakar na mimi ninazizuia na kuzikemea). Unasemaje ewe Nouman? Je Omar anasema kweli ya kuwa muta'aa mbili zilikuwa ni halali katika zama za Mtume (s.a.w) au anasema uongo?


NOUMAN:
Bila shaka anasema kweli.
RIDHA:
Ikiwa ni hivyo: je sisi tuna hoja yoyote lau kama tutaacha kauli ya Mtume (s.a.w) na kuchukua au kushikamana na kauli ya Omar?
NOUMAN:
Hoja ni katazo la Omar binil-khattab.
RIDHA:
Kama ni hivyo sasa kauli hii ya Mtume (s.a.w) inamaana gani isemayo kuwa:
حلا ل محمد حلا ل إلي يوم القيامة وحرامه حرام إلي يوم القيامة
(Kilicho halalishwa na Muhammad ni halali hadi siku ya kiama na kilicho haramishwa na Muhammad ni haram hadi siku ya Kiama) [6] hadithi iliyo (Muttafaq) maulamaa wote wa kiislaam wamekubaliana juu ya usahihi wake bila kumtoa yeyote? NOUMAN: Baada ya kufikiria kwa kina na kwa muda mrefu, uyasemayo ni sawa, lakini ilikuwaje Omar akazuia na kukataza kutekelezwa kwa Muta'aa hizo? Na katika kuharamisha kwake huko alijitegemeza kwenye kitu gani? Hili ndio suali linalo nitatiza.


RIDHA:
Hiyo ilikuwa ni ijtihadi yake binafsi Omar, na kila ijtihadi itakayo pingana na dalili ya kisheria basi ijtihadi hiyo haikubaliki.
NOUMAN:
Hata kama ijtihadi hiyo itatoka kwa mtu kama Omar bin Khattab?
RIDHA:
Hata kama itatoka kwa mtu mkubwa kuliko yeye, je unadhani kauli ya Mwenyezi Mungu mtukufu na kauli ya Mtume (s.a.w) ni yenye haki zaidi ya kufuatwa, au kauli ya Omar binil-khattab?

NOUMAN:
Je katika Qur'ani tukufu kuna aya izungumziayo uhalali wa ndoa ya Muta'aa?
RIDHA:
Ndio, nayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu alie takasika isemayo:
فما استمتعتم به منهن فآتوهن أجورهن فريضة
(Ambao mmestarehe nao katika wao, basi wapeni mahari yao yaliyolazima) [7] Na Allamah Aminiy katika kitabul-ghadiir ametoa vyanzo na vitabu vingi kati ya vitabu vya Ahli sunna kama vile Musnad Ahmad bin Hanbal Imam wa madhehbu ya Hanbali, na wengineo ya kuwa aya hii ilitelemka kuhusiana na ndoa ya Muta'aa…na kwamba aya hii ndio dalili ya kwanza juu ya uhalali wa ndoa hiyo [8]


NOUMAN:
Sikuwa nikilifahamu hilo hapo kabla.
RIDHA:
Rejea kitabu (Al-ghadiir) utayakuta niliyo kueleza, na zaidi ya hayo niliyo kueleza. Je inajuzu kuacha jambo lililo halalishwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kushikamana na makatazo ya Omar, na kuharamisha kwake ndoa hiyo? Kisha mimi ni katika umma wa nani? Umma wa Mtume (s.a.w) au katika umma wa Omar?


NOUMAN:
Bila shaka ni katika umma wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na fadhila ya Omari inapatikana kutokana na ukweli kuwa yeye ni katika Umam wa Mtume (s.a.w).
RIDHA:
Kama ni hivyo ni kipi kikufanyacho usite kuchukua kauli ya Mtume (s.a.w)?
NOUMAN:
Kinizuiacho ni makubaliano ya waislaam wote juu ya uharamu wa Muta'aa na hilo ndio linitialo utata kuhusu ndoa hii.
RIDHA:
Hakuna makubaliano ya waislaam wote juu yahilo kamwe.
NOUMAN:
Vipi kusiwe na makubaliano?
RIDHA:
Wewe mwenyewe unakiri ya kuwa Mashia wanahalalisha ndoa ya Muta'aa, na Mashia takriban wanafikia nusu nzima ya Waislaam, sasa makubaliano gani hayo ambayo kiasi cha waislaam milioni mia moja wametoka kwenye makubaliano hayo [9] nao ni Mashia? Kisha ni kwamba Maimamu walio maasumini rehma na amani ziwe juu yao- ambao ni Ahlul baiti wa Mtume (s.a.w) ambao Mtume (s.a.w) aliwafananisha na jahazi la Nuhu, ambalo mwenye kulipanda jahazi hilo ataokoka, na mwenye kukengeuka na kuto panda jahazi hilo ataangamia na kupotoka, [10] na akasema (s.a.w) kuwahusu wao:
إني تارك فيكم الثقلين كتاب الله وعترتي أهل بيتي, وإنهما لن يفترقا حتي يردا علي الحوض

(Hakika mimi nimeacha kwenu vitu vizito viwili kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, na hakika vitu viwili hivyo havitatengana mpaka vije kwangu kwenye Hodhi) [11].


Hawa ambao waliwafuata na kufuata nyendo zao walikuwa ni miongoni mwa watu walio faulu na kuokoka na ndio walio shikamana na haki, na wenye kuwafuata wengineo na kuwaweka nyuma ya migongo yao walikuwa ni miongoni mwa watu walio potea na wenye kutanga tanga.. hawa walikuwa wakijuzisha kufanya ndoa ya Muta'aa, na wanaona kuwa haikufutwa, hadi wakafahamika kwa jambo hilo, na Mashia wakalichukua hilo kutoka kwao.

Na Imepokelewa hadithi sahihi kutoka kwa Amiril-muuminiin ya kuwa amesema:
لولا أن عمر نهي عن المتعة ما زني إلا شقي

(Lau kama Omar asinge kataza ndoa ya Muta'aa asinge fanya zina isipokuwa mtu muovu sana) [12] Kwa maana kuwa: Kuzuia na kukataza kwa Omar ndoa hiyo ya Muta'aa ilikuwa ni sababu iliyo wazuia watu wasiifahamu ndoa ya Muta'aa na ndoa hiyo ya muda, kwani si kila mmoja anauwezo wa kuoa ndoa ya daima, kwa maana hiyo watu wanaelekea kwenye zina ikiwa ni matokeo ya Omari kuharamisha ndoa ya Muta'aa.


Sasa yakowapi makubaliano ya waislaam wakati maimamu hawa wa waislaam wanasisitiza juu ya uhalali wa ndoa ya Muta'aa na kujuzu kwake? Pamoja na ukweli kuwa masahaba wengi na Taabiina pia waislaam walilikataaa katazo la Omar na kupinga kuzuia kwake ndoa ya Muta'aa, wakishikamana na dalili ya Qur'an tukufu na ruhusa ya Mtume (s.a.w). Na wafuatao ni baadhi yao na baadhi ya kauli zao:
1- Omar bin Haswiin amesema:
نزلت آية المتعة في كتاب الله تعالي, لم تنزل آية بعد ها بنسخها, فأمرنا بها رسول الله صلي الله عليه وآله وسلم. تمتعنا مع رسول الله صلي الله عليه وآله وسلم ومات ولم ينهنا عنها, ثم قال رجل بعد برأيه ما شاء

(Aya ya Muta'aa ilishuka ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu mtukufu, hakuna aya nyingine iliyo telemka baada yake kuifuta, na Mtume (s.a.w) akatuamrisha kufanya hivyo. Tulifanya ndoa ya Muta'aa pamoja na Mtume (s.a.w) na akafariki dunia na hakuikataza ndoa hiyo, kisha mtu fulani akasema rai yake aliyo yataka baada yake.[13]


2- Jaabir bin Abdillahil-answariy, na Abu Said Al-khudriy, wamesema: Tulifanya ndoa ya Muta'aa hadi katika nusu ya utawa wa khalifa Omar, hadi Omar alipo wazuia na kuwakataza watu kufanya ndoa hiyo kutokana na suala la Omar bin Huraith. 3- Abdallah bin Masoud, Ibnu hazmi katika kitabu chake (Al-muhallaa) na Az-zarqaniy katika kitabu (Sharhul-muwatta'a) amesema kuwa ni miongoni mwa watu wanao thibitisha uhalali wa ndoa ya Muta'aa.


Na Bwana Al-huffadh ametoa kutoka kwake ya kuwa amesema: (Tulikuwa tukipigana vita pamoja na Mtume (s.a.w) hatukuwa na wanawake (wake zetu) tukamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je tupige punyeto? Mtume akatukaza na kutuzuia kufanya hivyo na akaturuhusu tuoe kwa kutoa nguo kwa muda maalum, kisha akasema:
( لا تحرموا طيبات ما أحل الله لكم)

(Msiharamishe vitu vizuri alivyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu) [14]
4- Abdallah bin Omar: Imepokelewa na Ahmad bin Hanbal-Imam wa madhehebu ya Hanbali- kwa kuitegemeza kutoka kwa Abdur-rahman bin Niam [15] Al-aarajiy amesema: Mtu mmoja alimuuliza mtoto wa Omar kuhusiana na ndoa ya Muta'aa- nami nikiwa kwake-yaani ndoa ya muda? Akasema: Nina apa kwa jina la Mwenyezi Mungu katika zama za Mtume (s.a.w) hatukuwa ni wenye kufanya zina wala hatukua ni wenye kufanya uovu) [16]
5- Abu Said Al-khudriy.
6- Salamah bin Umayyah bin Halaf.
Ibnu Hazmi amepokea kutoka kwao katika kitabu (Al-muhallaa) na Az-zarqaniy katika kitabu (Sharhul-muwatta'a) ya kuwa wao wawili walikuwa wakihalalisha ndoa ya Muta'aa, au ndo ya Muda [17].
7-Muabad bin Umayyah bin khalaf. Ibnu Hazmi katika kitabu chake (Al-muhallaa) amesema ya kuwa alikuwa akihalalisha ndoa ya Muta'aa. [18]
8-Zubair bin Awwam.


Bwana Raghib amesema: Abdallah bin Zubairi alikuwa akimtoa dosari Abdallah bin Abbas kwa kuhalalisha kwake Muta'aa akamwambia: Muulize mama yako ni vipi yalitokea mapenzi kati yake na kati ya baba yako (walipendana vipi)? Akamuuliza mama yake, akasema: Sikukuzaa isipokuwa ni kwa kupitia ndoa ya Mutaa'a (Ndoa ya muda). [19] Na hiyo ni dalili au ushahidi ulio thibiti juu ya kuwa Zubairi alikuwa akihalalisha ndoa ya muda.
9-Khalid bin Muhaajir bin Khalid Al-makhzumiy.


Amesema:Wakati akiwa amekaa kwa mtu mmoja alikuja mtu mmoja akamuuliza kuhusu fatwa ya Muta'aa nae akamuamuru kufanya muta'aa. Ibnu Abi Amratu Al-answariy akamwambia: Subiri usiwe na haraka. Akasema: Nina apa kwa jina la Mwenyezi Mungu hakuna jambo lingine isipokuwa ndio hivyo kwa hakika nilifanya hivyo katika zama za Imam wa wacha Mungu. [20]


10- Omar bin Huraith.
Bwana Haafidh Abdur-razzaq ametoa katika kitabu chake kutoka kwa Ibnu Juraih amesema: Nimepewa habari na Abu Zubair kutoka kwa Jaabir, amesema: Amru bin Huraith alikuja kwenye mji wa Al-kufah akafanya Mutaa'a na kijakazi kisha Amru akaja nae akiwa ni mja mzito, akamuuliza na yeye kukiri hivyo. Akasema: Na hilo lilifanyika wakati Omar alipo kataza na kuzuia kufanya Muta'aa [21] Na kuna masahaba wengine wengi walio dhihirisha kupinga kwao fatwa hii ya Omar, na ijtihadi yake aliyo ifanya katika mukabala wa Qur'an na Sunnah (wakati kuna kitabu na sunna) kwa mfano: Ubai bin Kaab. Rabiiah bin Umayyah. Sumair Au Sumrah- bin Jundub. Said bin Jubair. Twaus bin Al-yamaniy. Atwaa Abu Muhammad Al-madaniy.


As-sadiy. Mujaahid. Zufar bin Awsi Al-madaniy. Na wengineo.. kati ya masahaba wakubwa na taabiiina na maulamaa wakubwa wa kiisalaam. Ewe Nouman ninakuuliza swali moja: je baada ya ushahidi wote huu bado tu unasema ya kuwa kuna makubaliano ya waislaam wote juu ya uharam wa ndoa ya Muta'aa?

NOUMAN:
Samahani.. na naomba udhuru. Hakika hayo niliyo kwambia niliyasikia tu bila ya kuyafanyia uchunguzi juu ya usahihi wake na ubatilifu wake, na hivi sasa imenibainikia ya kuwa ni jambo la wajibu kwangu na ni lazima kwangu kuyafanyanyia utafiti mambo, ili kufahamu asili yake na ukweli wake, uchunguzi ulio mbali na asabia za kimadhehebu.

RIDHA:
Je umeamini ya kuwa ndoa ya Muta'aa inajuzu na ni halali?
NOUMAN:
Hilo ni jambo nilililo liamini na kuwa na yakini nalo, na ninaitakidi ya kuwa wale ambao wanaharamisha ndoa hiyo hakika wameiharamisha kwa kufuata matamanio yao na matakwa yao. Kwani Qur'ani ni yenye kuhukumu kwamba ndoa ya Muta'aa inajuzu na kwamba ni halali na haikufutwa baada ya kuhalalishwa. Na si Omar wala alie mkubwa kuliko Omar mwenye uwezo wa kubadilisha na kugeuza hukumu za Mwenyezi Mungu na mshangao wangu hautakwisha kutokana na kitendo alicho kifanya Omar, ilikuwaje akatoa fatwa kama hii, kwani sioni dalili yoyote iliyo mfanya kutoa fatwa kama hii. Na nitakushukuru ikiwa utanitajia baadhi ya vitabu vilivyo yazungumzia maudhui haya kwa njia ya kielimu na bahthi iliyo safi, na kwa kufanya hivyo utakuwa umenisaidia usaidizi usio sahaulika.


RIDHA:
Ndio, nitakutajia vitabu hivyo, basi andika majina ya vitabu hivyo na kavichukue kutoka kwenye maktaba, na uvisome kwa mazingatio na kwa umakini, na usiiache asabia ikakushinda nguvu wakati ukisoma.
NOUMAN:
Ndio, nitafanya hivyo.
RIDHA:
Kitabul-ghadiir.. cha Allamah Al-aminiy (mwenyezi Mungu autakase utajo wake).
2-An-nassi wal-ijtihad.. cha Imam Sharafud-din.
3-Al-muta'aa.. cha ustadh Tawfiq Al-fakiikiy.
4- Al-fusuulul-muhimmah..cha Imam Sharafud-din.
5-hivi ni baadhi ya vitabu hivyo vilivyo zungumzia maudhui haya kwa njia ya kielimu.

NOUMAN:
Ninakushukuru sana, na ninakuombea kila la kheri kwa Mwenyezi Mungu.
RIDHA:
Na hapa kuna swali jingine liwaelekealo masunni walio chukua kauli ya Omar katika mas'ala ya ndoa ya Muta'aa.
NOUMAN:
Ni lipi hilo?
RIDHA:
Hakika Omar alikataza na kuzuia (ndoa ya Muta'aa) na (Muta'aatul-haji) ni sababu ipi iwafanyayo masunni wajuzishe (Muta'aatul-haji) na wasijuzishe (Ndoa ya muda) ? Ikiwa kauli ya Omar ni sahihi ..basi ilikuwa ni lazima Muta'aa zote mbili ziwe haram. Na ikiwa kauli ya Omar ni batili.. basi ilikuwa ni lazima Muta'aa zote mbili ziwe halali.

NOUMAN:
Je masunni wanasema ya kuwa (Muta'atul-haji) ni sahihi?
RIDHA:
Ndio wanasema hivyo, rejea vitabu vyao ili uweze kuelewa ukweli huo.
NOUMAN
Nina kushukuru sana . Utakasifu ni wako ewe Mola ulie tukuka na yale mabaya wakusifu nayo. Na amani iwe juu ya Mitume wote, Na tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote.
Surattis-swafaat 180\ 182. Subhana rabbika rabbil-izzati ammaa yaswifuun. Wasalaamun alal-mursaliin. Wal-hamdu lillahi rabbil-aalamiin.

SAYYID SWAADIQ HUSEINIY Al-SHIRAZIY.


________________________________________


[1]- Albayaan wat-tibyaan cha Jaahidh juzu ya 2\ 223.
[2]- Tafsiiru Muhammad bin Ahmad Al-qurtubiy juzu ya 2\ 390-391\ 1042.
[3]- Al-mabsuut fii baabil-qiraan min kitabil-haji.
[4]-Tafsiirul-kabiir ya Fakhrur-raziy juzu ya 2\ 167 na juzu ya 3\ 201-202.
[5]- Taarikh Ibn Khalakan.
[6]-Rejea Sunan Ibnu Daud As-sijistaniy juzu ya 1\ 6\12 mlango wa 2 Taadhim hadithir-rasulillah (s.a.w) wattaghliidh alaa man aaradhahu, Al-kafiy juzu ya 1\ \5 \19, na rejea: Wasaailush-shia juzu ya 18\ 124\ 47b 12.
[7]- Suratun-nisaa aya 24.
[8]- Rejea kitabul-ghadiir juzu 6\ 229-236.
[9]- Hivi sasa idadi ya waislaam inafikia bilioni mbili…, na Mashia wanafikia nusu ya idadi hiyo. Na raisi wa Misri alie pita Anwar Sadaati alisema wazi wazi katika kongamano la waislaam lililo fanyika Kairo ya kuwa sensa imethibitisha ya kuwa nusu ya waislaam ni Mashia.
[10]- Rejea Buharul-anwaar juzu ya 10\ 111\ 1.
[11]- Musnad Ahmad bin Hanbal juzu ya 3\ 17,26, 59,na juzu ya 4\ 367.
[12]- Muhammad bin Muslim, kutoka kwa abi Jaafar (a.s) amesema: Jabir bin Abdillahi amesema kutoka kwa Mtume (s.a.w):
إنهم غزوا معه فأحل لهم المتعة ولم يحرمها وكان عليه السلا م يقول: لولا ما سبقني فيه ابن الخطاب يعني عمر ما زني إلا شقي)
(Hakika wao walipigana vita pamoja na Mtume (s.a.w) na kuwahalalishia Muta'aa na hakuiharamisha ndoa hiyo, na yeye (a.s) alikuwa akisema: Lau kama asinge nitangulia katika jambo hilo ibnu khattab yaani Omar, asinge zini isipokuwa muovu. ( Buharul-anwaar juzu ya 100\ 314\ 15b 10. Tafsiru twabariy juzu ya 5\ 9, kwa sanadi sahihi.
[13]- Tafsiru Muhammad bin Ahmad Al-answariy Al-qurtubiy juzu ya 2\ 385\ 1026, na katika tafsiri hiyo kuna maneno yafuatayo:
نزلت آية المتعة في كتاب الله- يعني متعة الحج- وأمرنا بها رسول الله صلي الله عليه وآله وسلم ثم لم تنزل آية تنسخ آية متعة الحج ولم ينه عنها رسول الله صلي الله عليه صلي الله عليه وآله وسلم حتي مات, قال رجل برأيه بعد ما شاء.
(Aya ya Muta'aa ilitelemka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu-yaani muta'atul-haji- na akatuamuru kufanya hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu kisha haikutelemka aya yoyote yenye kuifuta aya ya Muta'aatulhaji na hakuizuia wala kuikataza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) hadi kufariki kwake, akasema mtu fulani ayatakayo kwa rai yake baada yake.
[14]- Rejea Sahihi Bukhariy juzu ya 5\ 1935\ 4787, mlango wa 8 usemao (Yukrahut-tabattul wal-khiswaai, kukiwa na tofauti ndogo. Sahihi Muslim juzu ya 3\ 192-193, mlango wa Nikaahul-Muta'aa. Sunanul-kubraa juzu ya 7\ 200 baabush-shighaar, Ad-durrul-manthuur juzu ya 2\ 307, Tafsiri ya aya 87 ya suratul-maaidah, akinukuu kutoka kwa Maimamu tisa na mahufadhi, na vitabu vingine vingi tofauti.
[15]- kh l: Naiim
[16]- Musnad Ahmad juzu ya 2\ 95.
[17]- Rejea: Al-muhallaa cha Ibnu Hazmi na Sharhul-muwatta'I cha Zarqaniy.
[18]- Rejea: Al-muhallaa cha Ibnu Hazmi.
[19]- Al-muhadharaat juzu ya 2\ 94.
[20]- Sahihi Muslim juzu ya 3\ 197-198 mlango wa 3\ Nikahul-Muta'aa, Sunanul-kubraa cha Baihaqiy juzu ya 7\ 205 Baabun-nikaahil-Muta'aa.
[21]- Fat'hul-bariy juzu ya 9\141.