UKWELI WA USHIA

 
KUBUSU MADHARIHI (MAKABURI)MAALIK:
Ewe Swaadiq ni sababu gani iwafanyayo kubusu Dharihi ya kaburi la Mtume na maimam na kutoacha kitendo hicho?
SWAADIQ:
Je kuna tatizo (ishkali) lolote kufanya hivyo?
MAALIK:
Inasemekana kuwa kufanya hivyo ni miongoni mwa matendo ya shirki.
SWADIQ:
Nani asemae kuwa kufanya hivyo ni shirki?
MAALIK:
Waislaam ndio wasemao hivyo.
SWADIQ:
Ajabu! Basi ni watu gani ambao wanabusu madharihi?
MAALIK:
Inasemekana kuwa ni kikundi kidogo cha Mashia.
SWADIQ:
Je umewahi kwenda hija?
MAALIK:
Ninamshukuru Mwenyezi Mungu.. ndio nimefanikiwa kwenda hija.
SWADIQ:
Je umelitembelea kaburi la Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) katika mji wa Madinah?
MAALIK:
Ninamshukuru Mwenyezi Mungu nimefanikiwa kulitembelea.
SWAADIQ:
Je hukuwaona maelfu ya waislaam wa madhehebu ya sunni wakikusudia na kutaka kulibusu dharihi la kaburi la Mtume wa Mwenyezi Mungu na huku wakipigwa na walinzi wa kikundi cha (Hay'atu amri bil-maarufi)?!!
MAALIK:
Ndio..
SWAADIQ:
Kwa maana hiyo si sisi Mashia pekee tunao busu madharihi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu, bali waislaam wote huyabusu.
MAALIK:
Sasa kwanini baadhi wanasema kuwa kufanya hivyo ni haram, na kwamba kufanya hivyo ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu mtukufu?
SWAADIQ:
Hawa ni watu wachache wa kikundi fulani kati ya makundi ya waislaam, wajionao kuwa wao ndio wenye haki, na kwamba wao ndio waislam wa kweli na wanawaona waislaam wengine kuwa ni makafiri na washirikina wanamuabudu asie kuwa Mwenyezi Mungu, na hawawaoni watu wengine kuwa ni waislaam walio kosea, kwa hivyo ndio maana huwaona wakiyakufurisha madhehebu (makundi) mengine yote ya kiislaam. Je hukuona ile kamati ya (Al-amri bil-maarufi)!! katika nchi ya Hijazi wakimpiga anaekusudia na kutaka kubusu dharihi la kaburi la Mtume (s.a.w) na kumwambia: Ewe kafiri! Ewe mshirikina! Ewe zindiki! Ewe nguruwe! Ewe mbwa! Na mengineyo kati ya aina mbali mbali za matusi na tuhuma zilizo mbaya kabisa.Na matusi hayo humuelekea kila mtu: Sawa awe Shia, Hanafiy, Maalikiy, Shafiiy, Hanbaliy, Zaydiah, na waislaam wengine..[1]
MAALIK:
Ndio.. yote hayo nimeyaona, na yaliyo mabaya zaidi kuliko hayo: Kwa hakika mimi niliwaona wakimpiga kichwani mtu mmoja alie ng'ang'ania kufanya hivyo kwa fimbo kiasi kwamba huenda pigo hilo lilipelekea kumpasua na kutoka damu, na wakati mwingine huwapiga kwa mikono yao-kwa nguvu- na wakiwapiga vifuani waislaam walio kuja kufanya ziara mapigo ambayo huwaumiza na kuwadhuru vifua vyao na kuwasababishia maumuvu na maradhi miili yao! Na ni kwa kiwango gani niliumia kwa kuyao mambo hayo na vitendo hivyo!!.


Hija ambayo Mwenyezi Mungu ameifanya kuwa ni kongamano la waislaam wote ulimwenguni ili waweze kuzungumza katika kongamano hilo kuhusu mambo yao mbali mbali, hivi leo imekuwa ni mahala pa kutia tofauti kati ya waislaam kutokana na matendo ya kikundi hicho kidogo kinacho jiita kuwa ni (hay'atul-amri bil-maaruf wannahyi anil-munkar)!!!.
SWAADIQ:
Ala ayyi hal, ewe Maalik.. je wewe unambusu mwanao?
MAALIK:
Ndio!
SWADIQ:
Je unamshirikisha Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kumbusu mwanao?
MAALIK:
Hapana, hapana.. kamwe simshirikishi Mwenyezi Mungu.
SWADIQ:
Vipi usimshirikishe Mwenyezi Mungu kwa kumbusu mwanao?
MAALIK:
Kwa hakika mimi ninambusu mwanangu kwa ajili ya mapenzi yangu kwake, na hilo si shirki.

SWADIQ:
Je wewe unaibusu Qur'ani?
MAALIK:
Ndio.
SWADIQ:
Je kwa kufanya kwako hivyo humshirikishi Mwenyezi Mungu?
MAALIK:
Hapana.
SWADIQ:
Je jalada la Qur'ani unalo libusu si ngozi ya mnyama?
MAALIK:
Ndio.
SWADIQ:
Kwa hivyo wewe unamshirikisha Mwenyezi Mungu, na unaifanya ngozi ya mnyama kuwa ni mshirika wa Mwenyezi Mungu.. ametakasika Mwenyezi Mungu na hilo.

MAALIK:
Si hivyo. Kwa hakika mimi ninaibusu Qur'ani kwa sababu imekusanya maneno ya Mwenyezi Mungu, kutokana na mapenzi ya maneno ya Mwenyezi Mungu ndio maana ninalibusu jalada lililo ifunika Qur'ani hiyo, na hii ni kutokana na mapenzi mengi, na wingi wa shauku yangu kwa Qur'ani, ni tofauti iliyoje kati ya kitendo hiki na kumshirikisha Mwenyezi Mungu?


Kisha ninapo ibusu Qur'ani ninapata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya hivyo, kwa sababu kuibusu Qur'ani ni kuitukuza na kuienzi na kuiinua daraja yake, na kuitukuza Qur'ani kuna thawabu na malipo mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa hivyo ni tofauti iliyoje iliyopo kati ya tendo hili na kumshirikisha Mwenyezi Mungu?

SWADIQ:
Kwa nini maneno kama hayo usiyasema katika kubusu dharihi la Mtume (s.a.w) na madharihi ya maimam (a.s) [2] au unadai ya kuwa wale ambao wanabusu madharihi huvifanya vyuma hivyo kuwa ni washiriki wa Mwenyezi Mungu mtukufu?! Ikiwa ni hivyo kwanini hawabusu vyuma mbali mbali vilivyoko huku na kule katika ardhi? Lakini..kutokana na ukweli kuwa dharihi hilo limefunika kaburi la Mtume (s.a.w) au kaburi la mmoja wapo kati ya maimamu (a.s), kutokana na mapenzi ya Mtume (s.a.w) na maimamu na kutokana na shauku yao kwao ndio maana wanalibusu dharihi la kaburi lake kwa sababu wao hawawezi kumfikia Mtume na imamu mwenyewe (a.s).


Pamoja na kufanya kwao hivyo hakika wao hupata malipo kwa Mwenyezi Mungu mtukufu, na hupawa thawabu kwa kufanya hivyo, kwani kulibusu dharihi la mtu fulani ni kumtukuza mtu yule. Na kumtukuza Mtume (s.a.w) au mmoja wapo kati ya maimamu (a.s), ni kuutukuza Uislaam ambao huyu alikuwa ni Mtume wake (s.a.w) au alikuwa ni imamu wake alie kuwa akilingania watu kwenye Uislaam huo.

Na jambo lolote litakapo kuwa na sura ya kuutukuza Uislaam basi jambo hilo ni katika shiari za Mwenyezi Mungu ambazo amezizungumzia kwa kusema:
(ومن يعظم شعا ئرالله فإنها من تقوي القلوب )
suratul-haji aya 32.
MAALIK:
Ikiwa ukweli ni huo basi kwanini baadhi ya watu wanasema kuwa nyinyi ni wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu?
SWAADIQ:
Imepokelewa katika Hadithi tukufu kama ifuatavyo:
(إنما الأعمال بالنيات )
(Kwa hakika matendo hufanyika kutokana na Nia) [3] ikiwa mtu yeyote anabusu dharihi na katika kubusu kwake huko anakusudia kumshirikisha Mwenyezi Mungu bila shaka mtu huyo ni mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu (mshirikina). Na ikiwa kubusu huku kunatokana na mapenzi mengi, na kwa ajili ya kupata thawabu kwa ajili ya kuadhimisha na kutukuza shiari za Mwenyezi Mungu kwa kufanya hivyo, basi hupewa thawabu yule mwenye kuyatekeleza matendo hayo. Na wewe waulize wote wale ambao wanayabusu madharihi kati ya Mashia na Masunni kama ifuatavyo: Kwa nini mnabusu madharihi?


Hata kujibu yeyote kati yao isipokuwa kwa kusema tunafanya hivyo kutokana na mapenzi makubwa na shauku kubwa tuliyo nayo na kwa ajili ya kupata thawabu, na huwezi kumsikia yeyote kamwe-bila shaka yoyote- akisema ya kuwa anabusu dharihi kwa ajili ya jambo lingine tofauti na hili tulilo litaja.

MAALIK:
Ni kweli, maneno yako ni sahihi.
SWADIQ:
Na ikiwa kubusu peke yake bila kukusudia kumshirikisha Mwenyezi Mungu kunamfanya mtu kuwa mshirikina, bila shaka huwezi kumpata mwanadamu yeyote asie mshirikina, kwani waislaam imma wanabusu madharihi, au wanabusu Qur'ani.. kwa msingi wa hali mbili hizi wao-wote-ni washirikina. Sasa ikiwa hali ni kama hiyo Muislaam ni nani?

MAALIK:
Ninakushukuru sana, na kwa hakika mimi nitafanya mazungumzo na majadiliano na baba yangu alie kuwa akinilisha na kunifundisha mambo kama haya ya asabia yasiyo na maana yoyote, na sinto sikiliza maneno ya mtu yeyote wa madhehebu mengine, kwa hakika nimefahamu ya kuwa haki na ukweli uko pamoja nanyi-nyinyi Mashia- na wewe unahaki juu yangu milele, kwa sababu umenionyesha njia, si katika jambo hili tu bali katika mambo yote, ili nisifuate kila kinifikiacho masikioni mwangu, bila ya kufikiria kuhusu usahihi wake na ubatilifu wake.


________________________________________

[1] - Rejea: Tafswilul-milal wannihal wal-firaqil-islaamiyyah wa taarikhihaa: Na kati ya vitabu hivyo ni kitabu hiki: Kitabu Firaqush-shia cha Hasan bin Musa An-nubakhtiy ambae ni katika wanazuoni wakubwa wa karne ya tatu, na kitabu Al-faslu fil-milal wal-ahwaal wannihal cha Ali bin Ahmad Ali maarufu kwa jina la Ibnu Hazmi Ad-dhahiriy alie fariki mwaka 456 hijiria, na kitabu Al-milal wannihal cha Muhammad bin Abdul-kariim Shahristaniy alie fariki mwaka 548 hijiria, na kitabu Taarikhul-firaqil-islaamiyyah cha Muhammad Khaliil Zayni.

[2] - Maimamu (a.s) ni hawa wafuatao: Ali bin Abi Twalib (a.s) na wajukuu wawili wa Mtume (s.a.w) masayyid na mabwana wa vijana wa peponi Hasan na Husein (a.s) watoto wa Ali bin Abi Twalib (a.s), na maimamu tisa watokanao na kizazi cha Husein (a.s) walio zungumziwa na kukusudiwa katika Hadithi na riwaya mbali mbali zilizo mutawatir katika madhehebu mbali mbali za kiislaam ya kuwa maimamu watokanao na kabila la Kikuraishi ni kumi na mbili, nao ni Ali bin Husein bin Ali bin Abi Twalib (a.s), na mwanae Muhammad bin Ali, na mwanae Jaafar bin Muhammad, na mwanae Musa bin Jaafar, na mwanae Ali bin Musa, na mwanae Muhammad bin Ali, na mwanae Ali bin Muhammad, na mwanae Hasan bin Ali, na mwanae Muhammad bin Hasan (mwenye lakabu ya Sahibuz-zaman, na Mahdiy) na ambae zimepokelewa hadithi mutawaatir ya kuwa Masihi Issa (a.s) atasali nyuma yake katika Aakhiriz-zaman, kiasi kwamba ataujaza ulimwengu uadilifu na usawa kama ulivyo jawa na dhuluma na ujeuri, nae ndie atakae watia faraja Aalu Muhammad rehma na amani ziwe kwao wote.

[3]- Sahihi bukhari juzu ya 1\ 3 mlango wa 1\ kitabu Bad'il-wahyi ila rasuli llahi (s.a.w) katika kitabu bad'il-wahyi, Tafsirul-kabiir cha Fakhrur-raziy juzu ya 4\ 5 mas'ala ya nne katika tafsiri ya aya ya 112 ya suratul Baqarah, Tahdhibul-ahkaam juzu ya 1\ 83 -67 mlango wa 4 Swifatul-wudhuu katika kitabu twaharah, juzu ya 4\ 186\1