UKWELI WA USHIA

 
KUSUJUDU JUU YA UDONGOSAMI:
Ewe Ali kwa hakika nyinyi Mashia mnamshirikisha Mwenyezi Mungu, kwa kusujudu kwenu juu ya udongo, je udongo huo sio kiasi kidogo cha udongo ulio kauka mnao uabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu?
ALI:
Niruhusu nikuulize swali moja.
SAMI:
Bila wasi wasi wowote uliza.

ALI:
Je ni wajibu kusujudu juu ya kiwiliwili cha Mwenyezi Mungu mtukufu?
SAMI:
Hakika kauli yako hii ni kufru, kwa sababu Mwenyezi Mungu hana kiwiliwili, haonekani kwa macho, wala haguswi kwa kiwiliwili, na mwenye kuitakidi ya kuwa Mwenyezi Mungu ana kiwiliwili basi yeye ni kafiri. Hakika sijda ni wajibu ifanyike kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee, yaani lengo la kusujudu na kunyenyekea inabidi liwe ni Mwenyezi Mungu alie takasika, ama kusujudu juu ya Mwenyezi Mungu hiyo ni kufru (huo ni ukafiri).

ALI:
Kutokana na maneno yako haya imethibiti kuwa kusujudu kwetu juu ya udongo si shirki, kwa sababu sisi tunasujudu juu ya udongo, si kwamba tunausujudia udongo. Na tujaalie jambo lililo muhali ya kuwa, lau kama tunge kuwa tunaitakidi kwa mfano ya kuwa udongo ndio (Mwenyezi Mungu) basi ilikuwa ni lazima kuusujudia, si kusujudu juu yake, kwa sababu hakuna mtu yeyote anaesujudu juu ya Mola wake.

SAMI:
Hakika ni mara ya kwanza kwangu kusikia uchambuzi kama huu, na kwa hakika ni uchambuzi ulio sahihi, kwani lau kama nyinyi mnge kuwa mnauzingatia (Udongo) kuwa ni Mungu msinge sujudu juu yake, na kusujudu kwenu juu yake ni dalili ya kuwa ninyi hamuuzingatii udongo huo kuwa ni Mungu. SAMI: Basi niruhusu nikuulize swali.

ALI:
Uliza.
SAMI:
Basi ni sababu ipi iwafanyayo muendelee kusujudu juu ya udongo kwa wakati wote, na kwa nini hamsujudu juu ya vitu vingine, kama mnavyo sujudu juu ya udongo?
ALI:
Kuna hadithi tukufu iliyo pokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w) kwa makubaliano ya madhehebu zote za Waislaam ya kuwa Mtume (s.a.w) alisema:
(جعلت لي الأ رض مسجدا وطهورا )

(Kwa hakika ardhi imefanywa kwangu iwe ni mahala pa kusujudia na mahala pa kujitwahirishia) [1] Kwa hivyo basi udongo halisi ndio ambao inajuzu kusujudu juu yake kwa makubaliano ya makundi yote ya Waislaam, kwa sababu hiyo sisi wakati wote husujudu juu ya udongo ambao waislaam wote wamekubaliana juu ya kuwa inajuzu kusujudu juu yake.

SAMI:
Wamekubaliana vipi Waislaam wote juu ya jambo hilo?
ALI:
Mwanzo kabisa alipo kuja Mtume (s.a.w) katika mji wa madina, na kujenga msikiti katika mji huo, je msikiti huo ulikuwa umetandikwa kwa mazulia?
SAMI:
Hapana.. haukuwa umetandikwa kwa mazulia.
ALI:
Basi Mtume (s.a.w) na Waislaam walikuwa wakisujudi juu ya nini?

SAMI:
Walikuwa wakisujudu juu ya ardhi yenye udongo au mchanga.
ALI:
Kwa hivyo sala zote za Mtume (s.a.w) zilikuwa zikifanyika juu ya ardhi, na alikuwa akisujudu juu ya udongo, vile vile Waislaam katika zama zake na baada yake walikuwa wakisujudu juu ya udongo. Kwa hivyo kusujudu juu ya udongo bila shaka yoyote ni jambo lililo sahihi, na kwa maana hiyo sisi tunasujudu juu ya udongo kwa kufuata sira na sunna ya Mtume na kwa kufuata nyendo za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w), na kwa maana hiyo sala zetu bila shaka ni sahihi


SAMI:
Basi nyinyi Mashia kwa nini hamsujudu juu ya kitu kingine tofauti na udongo muuchukuao na kuubeba pamoja nanyi kutoka katika ardhi nyingine, au kwa nini hamsujudu kwenye udongo mwingine?

ALI:
Kwanza kabisa: Mashia wanasema kuwa inajuzu kusujudu juu ya kila ardhi sawa iwe ni ile iliyo shikamana na kuwa kama jiwe au mchanga. Pili: Nisharti sehemu ya kusujudia iwe twahara, yaani isiwe na najisi, kwa hivyo basi haijuzu kusujudu juu ya ardhi iliyo najisika, au mchanga usio twahara, kwa maana hiyo ndio maana tunabeba kipande cha udongo mkavu ulio twahara, na kwa kufanya hivyo tunaepukana na hali ya kusujudu juu ya udongo ambao hatujui ya kuwa ni twahara au laa. Na kwa kuongezea ni kuwa, sisi tunasema kuwa inajuzu kusujudu juu ya udongo wa ardhi au ardhi ambayo hatujui kuwa ni najsi au laa.


SAMI:
Ikiwa kwa kufanya hivyo mnataka kusujudu juu ya udongo halisi ulio twahara.. kwa nini hambebi mchanga ili muweze kusujudu juu yake?
ALI:
Kwa sababu kubeba mchanga husababisha kuchafuka kwa nguo, kwani mahala popote utakapo wekwa katika nguo nilazima nguo hiyo itachafuka, kwa sababu hiyo sisi huuchanganya na kiasi fulani cha maji kisha tunauacha ukauke, ili tunapo ubeba usisababishe kuchafuka kwa nguo.

Kisha kusujudu juu ya kipande cha udongo ulio kauka kuna dalili zaidi juu ya unyenyekevu na khushui kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtukufu. Hakika sijda ndio mwisho wa unyenyekevu, kwa sababu hiyo haijuzu kukisujudia kitu kingine tofauti na Mwenyezi Mungu alie takasika. Kwa hivyo basi ikiwa lengo la kusujudu ni kwa ajili ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, kila sijda ambayo itakuwa ni yenye kuonyesha na kudhihirisha unyenyekevu zaidi, hakuna shaka yoyote kuwa itakuwa ni nzuri sana.

Kwa ajili hiyo imekuwa ni sunna sehemu ya kusujudia iwe chini zaidi kuliko sehemu ya mikono na miguu, kwani kufanya hivyo ni dalili zaidi juu ya unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu mtukufu. Na vilevile ni sunna kuipakaza pua kwa udongo wakati wa sijda. Kwa sababu kufanya hivyo kuna dalili zaidi juu ya unyenyekevu na khushuu'i kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.


Kwa maana hiyo kusujudu juu ya ardhi, au juu ya kipande cha udongo ulio mkavu ni vizuri zaidi kuliko kusujudu juu ya vitu vingine tofauti na vitu viwili hivyo kati ya vitu ambavyo inajuzu kusujudu juu yake, kwani kufanya hivyo ni kuweka sehemu ya mwili iliyo tukufu zaidi- ambayo ni paji la uso- juu ya ardhi- kwa ajili ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu mtukufu na kudhalilika mbele ya utukufu wake Mwenyezi Mungu.

Ama mwanadamu-katika hali ya sijda- kuweka paji lake la uso juu ya zulia lenye thamani ya juu na lililo tengenezwa na kupambwa kwa madini kama Fedha, Akiki, Dhahabu na mengineyo, au juu ya nguo yenye thamani kubwa…. jambo hilo ni kati ya mambo yanayopunguza hali ya unyenyekevu na khushuu'i, na huenda kufanya hivyo kukapelekea kuto dhalilika mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu.

Kutokana na hayo je inawezekana kusujudu juu ya kitu kinacho mzidishia mtu unyenyekevu mbele ya Mola wake kikazingatiwa kuwa ni shirki na kufru? Na kusujudu juu ya kitu kinacho ondoa unyenyekevu kwa ajili Mwenyezi Mungu mtukufu kikazingatiwa kuwa ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu? Hakika hiyo si jambo lingine bali ni kauli ya uzushi na uongo.

SAMI:
Basi ni maneno gani haya yalipo juu ya udongo ambao mnasujudu juu yake?
ALI:
Kwanza kabisa: si kweli kuwa sehemu zote za udongo huo zimeandikwa juu yake, kwa hakika kuna udongo mwingi ambao haukuandikwa hata herufi moja. Pili: Udongo ulio andikwa katika upande fulani ni udongo ulio chukuliwa katika ardhi tukufu ya Karbalaa. [2] je katika hilo kuna shirki? Na je hilo linautoa udongo huo katika hukumu ya kujuzu kusujudu juu yake? Hapana kamwe.

SAMI:
Je udongo wa ardhi ya (Karbalaa) unakhususiya gani kwani tunawaona Mashia wengi wanajifunga tu na kusujudu juu ya udongo huo vyovyote itakavyo kuwa?
ALI:
Sababu ya kufanya hivyo ni kuwa imepokelewa katika Hadithi tukufu:

السجود علي تربة الحسين (عليه السلا م) يخرق الحجب السبع

(Kusujudu juu ya udongo wa kaburi la Husein kunavuka vizuizi saba) [3] Yaani kusujudu juu ya udongo huo kunapelekea kukubaliwa kwa sala, na sala hiyo kupanda kwa Mwenyezi Mungu mtukufu juu ya mbingu saba. Na haikuwa hivyo isipokuwa ni kwa kufahamu ubora wa udongo huo, ubora ambao haupatikani katika udongo mwingine tofauti na udongo mtukufu wa Karbalaa.


SAMI:
Je kusujudu juu ya udongo wa kaburi la Husein kunaifanya sala iwe ni yenye kukubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu hata kama sala hiyo itakuwa batili?
ALI:
Mashia wanasema kuwa sala ambayo haikutimiza masharti ya kusihi kwake ni batili, haikubaliwi. Lakini sala iliyo timiza masharti yote ya kusihi kwake ni yenye kukubalika mbele ya Mwenyezi Mungu, na huenda isikubaliwe, kwa maana kuwa hapewi thawabu mtu kwa sala hiyo, kwa hivyo sala iliyo saliwa juu ya udongo wa kaburi la Imam Husein ikiwa ni sahihi, hukubaliwa na kupewa thawabu juu ya sala hiyo, kwa hivyo basi kusihi ni kitu, na kukubaliwa kwa sala ni kitu kingine.


SAMI:
Je ardhi (tukufu ya Karbalaa) ni tukufu zaidi kuliko ardhi yote hata ardhi ya Makka na Madina, hadi kusujudu juu yake kuwe bora?
ALI:
Kuna kizuizi gani katika hilo?
SAMI:
Hakika udongo wa (Makka tukufu) ambao tangu kutelemka kwa Adam (a.s) bado ni ardhi ya Kaaba, na ardhi ya (Madinatu- lmunawwarah) ardhi ambayo ndani yake kunakiwiliwili cha Mtume mtukufu (s.a.w) zinakuwa na daraja la chini zaidi kuliko daraja la ardhi ya Karbalaa? Hili ni jambo la ajabu! Na je Husein bin Ali ni bora kuliko babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu?


ALI:
Hapana. hakika utukufu wa Husein ni chembe ndogo ya utukufu wa Mtume (s.a.w), na utukufu wa Husein ni sehemu ndogo ya utukufu wa Mtume (s.a.w), na nafasi ya Husein mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu si kwa ajili ya jambo lingine bali ni kwa sababu ya kuwa yeye ni Imam alie fuata dini ya babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu hadi kufa shahidi katika hilo. Hapana, daraja ya Husein si chochote isipokuwa ni sehemu ndogo tu ukilinganisha na daraja ya Mtume (s.a.w). Lakini.. kutokana na ukweli kuwa Husein aliuliwa yeye na Ahli-bayti wake, na answari wake katika njia ya kuusimamisha Uislaam, na kuimarisha kanuni zake, na kuulinda usichezewe na watu wenye kufuata matamanio ya nafsi zao, Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kufa kwake shahidi alimpa badala yake mambo matatu:1-Kujibiwa kwa maombi chini ya kuba la kaburi lake.
2-Maimamu kutokana na kizazi chake.
3- Udongo wa kaburi lake kuwa ni dawa na tiba ya maradhi mbali mbali.[4]
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu akautukuza udongo wa kaburi lake kwa sababu yeye aliuwawa katika njia yake kwa mauaji yaliyo mabaya sana na ya kikatili, na wanawake wake wakachukuliwa mateka,, Maswahaba wake kuuwawa, na mabalaa mengi tofauti na hayo yaliyomfika kwa ajili ya dini..je katika hilo kuna kizuizi chochote? Na je kuufadhilisha udongo wa Kaarbalaa juu ya udongo wa sehemu nyingi ya ardhi hata juu ya ardhi ya Madina maana yake ni kuwa Husein (a.s) ni bora kuliko Mtume (s.a.w)? bali suala ni kinyume chake. Kwani kuutukuza udongo wa kaburi la Husein ni kumtukuza Husein, na kumtukuza Husein (a.s) ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w).


SAMI:
Haya ni kweli, na mimi nilikuwa nikidhania ya kuwa mnamfadhilisha Husein (a.s) hata kuliko Mtume (s.a.w), na hivi sasa nimefahamu ukweli kuhusu suala hili, na ninakushukuru kwa maneno yako haya mazuri ambayo umenifahamisha na kunizindua kwayo, na wakati wote nitachukua na kubeba kipande cha ardhi tukufu ya Karbalaa ili nikitumie kusujudu juu yake popote nitakapo kwenda kusali.. kama ambavyo nitaacha kusujudu juu ya kitu chochote mfano wa zulia na madini.

ALI:
Kwa hakika mimi nilitaka kukubainishia ya kuwa tuhuma hizi zielekezwazo kwetu sisi Mashia, hazina ukweli wowote, bali ni uongo mtupu ulio pangwa na kuelekezwa kwetu na watu waovu kati ya maadui wa Waislaam, wanao jiita kuwa ni waislaam, huenda ukajipamba na ukweli wakati wote, na wala usijali na kujishughulisha na utakayo yasikia dhidi ya Mashia bila kufanya utafiti kuhusu ukweli wa madai hayo na ukweli wake.


________________________________________

[1] Sahihul-bukhariy juzu 2\ 128\ 328 Kitabut-tayammam.
Sahihi muslim juzu 2\ 9\ 5 Kitabul-masaajid wamawaadhius-salaat, na kuna hadithi Ifuatayo (Imefanywa kwangu Ardhi kuwa ni sehemu ya kusujudia na kujitwaharisha)
Sunanut-tirmidhiy juzu 2\ 131\ 317, Maa jaa'a annal-ardha kulluha masjidin illal-maqbarata wal-hammam.
Manlaa yahdhuruhul-faqiih cha Shekh Swaduuq juzu ya 1\ 155\ 1, mlamgo wa 38 sehemu ambazo inajuzu kusalia, na sehemu ambazo hazijuzu kusalia sehemu hizo.
Wasaailush-shia cha Al-hurrul-aamuliy juzu 2\ 969-970\ 2, mlango wa 7 Jawaazut-tayammum bit-turaabi wal-hajar wa jaamiu aj'zaail-ardhi dunal-maadini wa nahwihaa.
[2] Karbalaa:Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu: Mwanangu atazikwa katika ardhi iitwayo: Karbalaa. Nayo ni ardhi ambayo ilikuwa na kuba ya Uislaam, kuba ambayo Mwenyezi Mungu aliwaokoa waumini ambao walimuamini Nuhu katika tufani na kupanda juu ya kuba hiyo.Na Abu jaafar Imam Baaqir (a.s) amesema: Al-ghaadhiriyyah ni kipande cha ardhi ambacho Mwenyezi Mungu alizungumza na Musa (a.s) bin Imran katika sehemu hiyo na ni sehemu alipo muokolea Nabii Nuhu, na sehemu hiyo ni sehemu tukufu sana kati ya ardhi ya Mwenyezi Mungu, lau kama si hivyo basi Mwenyezi Mungu asinge ipa amana ya kuvihifadhi viwiliwili vya mawalii wake na watoto wa Mtume wake, (Hakika wamekufa katika ardhi ya Karbalaa manabii mia mbili na mawasii mia mbili) basi yazuruni makaburi yetu katika ardhi ya Ghaadhiriyyah. Na Mwenyezi Mungu ameifanya ardhi ya Karbalaa kuwa ni haram yenye amani na yenye baraka kabla Mwenyezi Mungu haja iumba ardhi ya kaaba na akaifanya kuwa ni haram (sehemu tukufu) kwa muda wa miaka ishirini na nne elfu, na ardhi ya Karbalaa na maji ya mto Furati ni ardhi ya kwanza na maji ya mwanzo kabisa yaliyo takaswa na Mwenyezi Mungu na yaliyo barikiwa)

Rejea ziara: Kaamiluz-ziyaarat cha Ibnu Qawlawaihi Jaafar bin Muhammad Al-qumiy (368 hijiria) ukurasa 444-445 mlango wa 88 kuhusu ubora wa Karbalaa. Na imepokelewa kutoka kwa Alaa bin Abi Aathah amesema: Nimehadithiwa na Ra'asi Jaaluut, kutoka kwa baba yake amesema: Sikupita Karbalaa isipokuwa nilikuwa nikimkimbiza mnyama wangu hadi ninapo ivuka sehemu hiyo, amesema: nikamuuliza kwa nini? Akasema: Tulikuwa tukizungumza ya kuwa mtoto wa nabii atauwawa katika sehemu hiyo. Akasema: Na nilikuwa nikiogopa nisije nikawa ni mimi, wakati alipo uliwa Husein tukasema: haya ndio tuliyo kuwa tukiyazungumza. Akasema: Na baada ya tukio hilo nilikuwa kila nipitapo sehemu hiyo nilikuwa nikipita kwa kutembea taratibu na sikuwa ni mwenye kukimbia)

Tariikhut-twabariy juzu ya 5\ 393. matukio ya mwaka 60 hijiria,
Al-kaamil fit-tarikh juzu ya 4\ 90. Matukio ya mwaka 61 hijiria.
[3] -Misbahul-mujtahid ukurasa 677 cha Shekh Tusiy (Mungu amrehemu) amesema: Muawia bin Ammar amepokea amesema:
(كان لأبي عبد الله خريطة ديباج صفراء فيها تربة أبي عبد الله عليه السلا م فكا ن إذا حضرته الصلاة صبه علي سجا دته وسجد عليه ثم قال عليه السلا م....)
Na imepokelewa kutoka kwenye kitabu Al-wassail \mlango wa Salah milango ielezayo vitu vinavyo juzu kusujudu juu yake\ mlango wa 16\ 3. [4] Rejea Kaamiluz-ziyaaraat\ ukurasa 274.