UKWELI WA USHIA

 
SISI SI KATIKA MASHIA WA ALI (A.S) IKIWA HATUKUZIHESABIA NAFSI ZETU KILA SIKU [1]MIONGONI MWA MANENO YA MHESHIMIWA AYATULLAHIL-UDHMAA SAYYID SWADIQ SHIRAZIY
(Mwenyezi Mungu amzidishie umri)
Hakika Amirul-muuminiin Imam Ali bin Abi Twalib (rehma za Allah ziwe juu yake) alikuwa na orodha ya majina ya watu fulani wanaume kwa wanawake na orodha hiyo ikiwa imeandikwa juu yake (Si katika sisi), na kwa hakika Amirul-muuminiin aliwasifia na kuwaelezea watu hao ya kuwa watu hao ni miongoni mwa watu ambao hawakuzihesabia nafsi zao na wala hawakuya angalia matendo yao).


Kwa hivyo basi muumini yeyote akitaka asiwe katika hawa ni juu yake kila usiku unapo ingia aweke angalau dakika tano maalum, na katika dakika hizo ayarejee matendo yake yote aliyo yatenda katika siku ile, je yalikuwa ni matendo mazuri ? na akiyakuta matendo yake aliyo yatenda ni mazuri basi amshukuru Mwenyezi Mungu alie takasika juu ya hilo, na ikiwa matendo yake ni mabaya, basi amuombe Mwenyezi Mungu alie takasika msamaha na aazimie ya kuwa hatorudia tena kufanya matendo hayo.Kwani Imam Kaadhim (a.s) anasema:

(Si katika sisi mtu ambae haihesabii nafsi yake katika kila siku, akifanya mema humuomba Mwenyezi Mungu amuwafikishe kutenda mema zaidi, na akifanya maovu humuomba Mwenyezi Mungu msamaha kutokana na maovu hayo na kurejea kwake). [2]

Hakika kila mtu anatabia maalum na ana matakwa maalum, kwa hivyo maisha yanapo mzonga na matatizo ya kimaisha kumtatiza, basi tabia yake hubadilika na kuwa mbaya, kwa hivyo Qur'ani tukufu na Ahlul-bayti (a.s) wamesisitiza na kusema ya kuwa mtu mwenye tabia njema ataingia peponi ama mtu mwenye tabia mbaya kwa hakika mtu huyo ataingia motoni.


Imepokelewa katika riwaya ya kwamba mwanamke mmoja katika zama za Mtume (s.a.w) tangu asubuhi hadi jioni alikuwa akijishughulisha na ibada bila kupumzika, na katika masiku mengi ya mwaka alikuwa akifunga, lakini mwanamke huyo alikuwa na kasoro moja, nayo ni kuwa tabia yake ilikuwa ni mbaya na alikuwa akimuudhi jirani yake kwa ulimi wake mbaya, Mtume (s.a.w) akasema kuhusina na mwanamke huyo: (Hakuna kheri yoyote kwa mwanamke huyo, yeye ni mtu wa motoni) [3] Kwa hivyo ni juu ya kila mtu kufanya juhudi kwa ajili ya kujipamba na tabia njema kati ya jamaa zake, watu wake wa karibu, majirani zake na watu walioko pembezoni mwake. Hakika Mwenyezi Mungu anampenda mtu mwenye kutoa huduma na ambae anawasaidia watu na kutatua matatizo yao.


Ninawausia wanaume kwa wanawake usia mbili: Usia wa kwanza, Mkumbukeni Imam Husein (a.s) wakati wote, kuomboleza kifo cha Imam Husein ni tawfiki ya Mwenyezi Mungu ambayo huipata Muumini, na maombolezo hayo huwa ni wasila na nyenzo ya kutatua matatizo yote ya kidunia, kwa hivyo basi ni wajibu kuwe na vikao vya kila wiki kwa ajli ya kukumbuka mauaji ya Imam Husein (a.s) katika majumba yenu.

Na ninakumbuka ya kuwa kulikuwa na mtu mmoja alikuwa akija kumtembelea marehemu kaka yangu, na kaka yangu kama ada yake anapokutana na waumini alikuwa daima akimhimiza na kumsisitizia kuweka vikao na kufanya majlisi za kumkumbuka za Imam Husein katika nyumba yake, na bwana yule alikuwa akitoa udhuru ya kuwa nyumba yake ni ndogo na haitoshi kuweza kufanya hivyo kwa sababu nyumba yake ina chumba kimoja chenye ukubwa wa mita kumi na mbili tu, Marehemu Imam akamwambia:

Fanya majlisi katika chumba hicho kila wiki kwa muda wa saa moja. Yule bwana akaitikia wito na kufanya vile na kutokana na baraka za vikao vya kila wiki alivyo kuwa akivifanya katika chumba kile kidogo, na akisomea kwenye chumba hicho maombolezo ya msiba wa Imam Husein (a.s), baadae bwana yule akawa ni katika wafanya biashara wakubwa kabisa kiasi kwamba akawa ni mwenye kumiliki majumba na akawa ni mwenye kumiliki vitu vingi visivyo kuwa na hesabau ( yaani akawa tajiri mkubwa).


Ama usia wa pili ni kutekeleza usia wa Imam Swadiq (a.s) kwa Mashia (wafuasi) wake ambao alisema katika usia huo:
(عليكم بالأ حدا ث )

Ni juu yenu enyi ndugu zangu waumini kuzitilia umuhimu itikadi za vijana na kufanya juhudi kubwa katika kuzirekebisha na kuziweka sawa zisiyumbe, na ziimarisheni dhidi ya watu wa batili na itikadi za batili na mbaya.

Fanyeni juhudi ya kufuatana nao na kuwa nao wakati wote mnapokwenda katika vikao vya Imam Husein (a.s), na wasikilizieni na muwafahamishe pia muangalie ni kitu gani wanacho fikiria na vipi wanafikiri, na wala msikabiliane nao kwa ukali na msiwafanyie ugumu, ikiwa mtaweza kujibu ishkali na maswali yao basi jambo hilo ni zuri sana, laa sivyo fuataneni nao kwa mtu anae weza kujibu mswali yao na kubatilisha ishkali zao, kwa mfano katika zama za Mtume mtukufu (s.a.w) na katika zama za maima watwaharifu (juu yao sala na sala zilizo bora kabisa) vijana wengi waliongoka katika itikadi zao na tabia zao, na Abu dharri alikuwa ni mmoja wa vijana hao, kwani Abu dharri alikuwa ni mshirikina lakini alisilimu na kuamini na akawa ni mtu mwenye kupigiwa mfano na akawa mfano mwema na wa aina ya pekee, na Bwana Othumani bin Affan alifanya kile kitendo cha kumfukuza na kumpekeleka kaskazini mwa nchi ya lebanoni ili asiufedhehi utawala wake na asieneze fadhila za Ahlul-bayti (a.s), lakini Aba Dharri kwa maneno yake na ushupavu wake na tabia yake aliweza kuwaongoa vijana wengi sana wa miji ile ambao baadae wakawa ni miongoni mwa watu wenye kuwatawalisha Ahlul-bayti (a.s) na wao wakaweza kuueneza Ushia katika miji ya Jabal Aamil na kaskazini mwa Lebanoni hadi hivi leo.


Na nyinyi mtokao katika mji wa Isfahani.. je mnafahamu ya kuwa Allamah Al-majlisiy alie zikwa katika mji wenu wa Isfahani babu yake wa juu kabisa hakuwa ni Shia?! Lakini kijana wa kawaida wa kishia aliweza kumkinaisha babu yake juu ya ukweli wa Ushia na itikadi ya Ahlul-bayti na Allamah Al-majlisiy akawa ni Shia mwenye Kuwatawalisha Ahlul-Bayti? Na sisi Mashia bado tunafaidika na Athari zake na elimu zake pia vitabu vyake mbali mbali, na huenda nyinyi nyote mmesikia kitabu chake cha riwaya kilicho kikubwa (Buharul-anwaar) ambacho alikusanya ndani yake maneno mazuri na maneno ya Maimam watwaharifu yenye nuru (rehma za mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote).


Kwa hivyo ni juu yetu, enyi ndugu waumini, tuwe kama kijana yule ambae aliongoka kupitia kwake babu yake Allamah Al-majlisiy, hadi tuweze kuwapata watu mfano wa Allamah Al-majlisy. Ni juu yetu kuwangoza viumbe na hasa vijana miongoni mwao ili Ushia ubakie ukiwa ni wenye nguvu na ukiwa imara na wafuasi wake wawe ni wenye kuongezeka siku hadi siku. Na mwisho ninakuombeeni tawfiq na kila la kheri na namuomba Mwenyezi Mungu ayakubali matendo yenu na msitusahau katika dua zenu.

________________________________________

[1] - Khutuba aliyo itoa mheshimiwa Swaadiq pindi alipo kutana na waumini kutoka katika mji wa Isfahani katika mwezi wa Rabii mwaka 1423 hijiria. [2] - Al-kafiy juzu 2\ Babu muhasabatul-amal \ ukurasa wa 453\ hadithi ya 2. [3] Mustadraku wasaailush-shia juzu ya 8\ mlango wa 72\ Wujub kaffil-adha anil-jari \ ukurasa 423.