MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

 MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE


KIMEANDIKWA NA SAYYID MUJTABAA MUUSAWIY LARI


YALIOMO
Neno la mchapishaji.................................................................................ii
Utangulizi..................................................................................................iii
Somo la Kwanza: Ustawi wa Imani katika vipindi mbali mbali..............2
Somo la Pili: Maono ya kina ya Binadamu humhimiza kumtafuta
Mwenyezi Mungu.......................................................12
Somo la Tatu: Mwenyezi Mungu na mantiki ya jaribio (JARABA)..25
Somo la Nne: Kuamini ukweli wa kisichoonekana kunahusisha mengi
zaidi ya Mwenyezi Mungu.........................................35
Umuhimu na kanuni za uhai.........................................44
Somo la Tano: Kuonekana Mwenyezi Mungu katika maumbile.........48
Somo la Sita: Haja ya dunia kwa mtu asiye na haja..........................72
Chanzo cha viumbe vyote chenyewe hakihitajii kuwa na
asili.............................................................................. 77
Somo la Saba: Ukomo wa nyororo ya usababishaji.............................84
Somo la Nane: Fitina ya uongo wa Kisayansi.....................................94
Somo la Tisa: Qur'ani humdhihirisha vipi Mwenyezi Mungu?.........112
Somo la Kumi: Masharti kwa ajili ya kitu kikamilifu kwa
kuabudiwa.................................................................123
Ibada, njia bora ya binadamu ya kuonyesha shukrani.129
Somo la Kumi na Moja: Sifa za Mwenyezi Mungu zisizoweza kufananishwa.............................................................
136
Upweke wa Mwenyeezi Mungu (Tawhiid)...140
Somo la Kumi na Mbili: Uwezo wa Mwenyezi Mungu usiopingika....151
Somo la Kumi na Tatu: Ujuzi wa Mwenyezi Mungu usio na mpaka..159
Somo la Kumi na Nne: Maoni kuhusu haki ya Mwenyezi Mungu....167
Somo la Kumi na Tano: Uchunguzi wa bahati mbaya na dhiki............175
Somo la Kumi na Sita: Dhiki, sababu ya kuzinduka...........................183
Somo la Kumi na Saba: Baadhi ya vipengele visivyo na uwiano.........190
Somo la Kumi na Nane: Mtizamo wa jumla wa tatizo........................200
Somo la Kumi na Tisa: Hiari..............................................................216
Somo la Ishirini: Aina ya ridhaa na chaguo kama utashi wa
Mwenyezi Mungu..........................................234
Somo la Ishirini na Moja: Tafsiri isiyo sahihi ya majaliwa na uwezo wa
Mwenyezi Mungu wa kukadiria.................248
KUHUSU MWANDISHI
Sayyid Mujtaba Mussawi Lari ni mtoto wa marehemu Ayatullah Sayyid Ali Asghar Lari mmojawapo wa wanachuoni na watu mashuhuri katika jamii ya Iran. Babu yake alikuwa marehemu Ayatullah Hajj Sayyid Abd ul- Husayn Lari ambaye alipigania uhuru wakati wa mapinduzi ya kikatiba. Wakati wa kipindi kirefu cha mapambano yake dhidi ya serikali dhalimu ya wakati huo, alijaribu kuanzisha serikali ya Kiislamu na alifaulu kufany hivyo kwa kipindi kifupi huko Larestan.


Sayyid Mujtaba Musawi Lari alizaliwa mwaka 13/4/1935 kwenye jiji la Lar ambako alihitimu elimu yake ya Msingi na masomo ya mwanzo ya Kiislamu. Mnamo mwaka wa 1332/1953, aliondoka Lar na akaenda Qum kuendelea na masomo yake ya elimu ya Kiislamu, akiwa anafundishwa na maprofesa na waalimu wa taasisi ya Kidini, pamoja na wanazuoni wakuu katika maarifa ya sheria (maraji).


Mnamo mwaka wa 1341/ 1962, akawa mshiriki katika Maktabil-Islam, gazeti la kidini na kisayansi lililokuwa lianaandika mfululizo wa makala kuhusu maadili ya Kiislamu. Makala hizi baadaye zilikusanywa na kuchapishwa kitabu kilichoitwa Ethical and psychological Problems. Matoleo tisa katika kitabu hiki kwa lugha ya kiajemi (Fursi) yamechapishwa, na pia kimetafsiriwa katika lugha ya Kiarabu na hivi karibuni kwa Kifaransa.


Mnamo mwaka 1342/1963. Alisafiri kwenda Ujerumani kutibiwa, na alirudi Iran baada ya miezi kadhaa, aliandika kitabu kiitwacho 'The face of Western Civilization'. Kitabu hiki kinajumuisha mazungumzo ya kulinganisha ustaarabu wa Kimagharibi na Kiisilamu, ndani ya kitabu hiki, mwandishi anataka kuthibitisha, kwa njia ya utambuzi, kifikira na ulinganisho kamili, ubora wa utambuzi na mambo mengi ya ustaarabu wa Uislamu kwa ule wa Magharibi. Kitabu hiki hivi karibuni tu kimechapishwa tena kwa mara ya saba. Mnamo 1349/1970, kitabu hiki kilitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na mtaalam wa mambo ya nchi za Mashariki, F.G. Goulding, na kilichochea hisia za watu huko Ulaya. Makala kuhusu kitabu hiki zilionekana kwenye magazeti kadhaa ya kimagharibi na BBC ilifanya mpango wa mahojiano na mtarjumi huyo ambapo sababu za kutafsiri na jinsi kilivyopelekwa hapo Uingereza zilizungumziwa. Tafsiri ya Kiingereza ya kitabu hiki hadi sasa imechapishwa mara tatu huko Uingereza, mara tano Iran na mara mbili Marekani.Mnamo takriban miaka mitatu baada ya kuchapishwa tafsiri ya Kiingereza, Rudolf Singler, profesa wa chuo Kikuu wa Kijerumani alikitafsiri katika lugha ya Kijerumani, na tafsiri hiyo ilithibitisha kuwa yenye kuvutia huko Ujerumani. Mmojawapo wa viongozi wa chama cha Social Democratic Party alimtaarifu Mtarjumi katika barua kwamba kitabu hicho kimeacha mvuto wa kina juu yake yeye, na kusababisha yeye kubadilisha maoni yake kuhusu Uislamu, na kwamba angelipendekeza Kitabu hicho kisomwe na marafiki zake. Tarjuma ya lugha ya Kijerumani imerudiwa kuchapishwa mara tatu hadi sasa.


Tafsiri za Kiingereza na Kijerumani za kitabu hiki zilichapishwa na Wizara ya Mwongozo wa Kiislamu kwa ajili kuisambaza zaidi nje ya Iran kupitia Wizara ya mambo ya Nje na taasisi ya mafunzo ya Kiislamic nchi za nje. Wakati huo huo ilipochapishwa tafsiri ya kwanza ya lugha ya Kijerumani, mwanachuo Muislamu wa asili ya kihindi aitwaye Maulana Raushan Ali alikitarjumi kitabu hiki katika lugha ya Urdu kwa lengo la kukisambaza India na Pakistani. Tarjumi hii ya Urdu imechapishwa mara tano hadi sasa. Sayyid Mujtaba Musawi Lari pia ameandika kijarida kuhusu Tawhid (upweke wa Mwenyezi Mungu), ambacho kilitafsiriwa Uingereza na kuchapishwa mara kadhaa Marekani.


Mnamo mwaka 1343/1964, aliasisi taasisi ya kutoa msaada huko Lar kwa madhumuni ya kueneza Uislamu, kutoa mafunzo ya Kiislamu kwa vijana walioko vijijini, na kuwasaidia wasiojiweza. Taasisi hii iliendelea kufanya kazi hadi 1346/1967. Taasisi hii ilitekeleza mambo makuu kama kuwapeleka wanafunzi wa sayansi za Kidini vijijini kufundisha Uislamu kwa watoto na vijana, kuwagawia maelfu ya watoto wa shule nguo, vitabu, vifaa vya kuandikia, kujenga idadi ya misikiti, mashule, zahanati mijini na vijijini, na huduma nyingine nyingi.


Sayyid Mujtaba Musawi Lari aliyaandama matakwa yake katika maadili ya Kiislamu, akiandika makala mpya kuhusu somo hilo. Mnamo mwaka wa 1353/1974, mkusanyiko wa makala hizi, zilizopitiwa upya na kuongezewa maneno, zilitoka katika muundo wa kitabu kilichoitwa 'The Function of Ethics in Human Development.' Kitabu hiki kimechapishwa mara sita hadi sasa.


Mnamo mwaka 1357/1978, alisafiri hadi Marekani kwa mwaliko wa Taasisi ya Kiislamu nchini humo. Halafu akaenda Uingereza, Ufaransa na baada ya kurudi Iran alianza kuandika mfululizo wa makala kuhusu itikadi za Uislamu kwa ajili ya gazeti la Sorouch. Makala hizi baadaye zilikusanywa na kutengenezwa kitabu chenye juzuu nne kuhusu imani za misingi za Uislamu (tauhid, uadilifu wa Mwenyezi Mungu, utume, uimamui, na ufufuo) kwa jina la 'The Foundations of Islamic Doctrine.' Kitabu hiki chenye juzuu nne kimetafsiriwa katika lugha ya Kiarabu, sehemu zake zingine zikiwa tayari zimekwisha chapishwa mara tatu. Tafsiri ya Kiingereza ya juzuu ya kwanza ya kazi hii ndio imetengeneza kitabu hiki cha sasa; juzuu zilizosalia pia zitatafsiriwa na kuchapishwa. Tafsiri za Urdu, Hindi na Kifaransa pia zimo katika mpango wa kutayarishwa; juzuu mbili za lugha ya Kifaransa zimekwishatokea.


Mnamo mwaka wa 1359/1980, Sayyid Mujtaba Musawi Lari aliasisi Taasisi huko Qum iitwayo 'Office for The Diffusion of Islamic Culture Abroad.' Husambaza bure nakala za vitabu vyake vilivyotafsiriwa kwa watu wapendao kuzisoma duniani pote. Taasisi hii pia imechukua shughuli ya kuchapisha Qur'ani kwa lengo la kuisambaza kwa Waislamu binafsi, Taasisi na shule za Kidini hapa Afrika.


NENO LA MCHAPISHAJI
Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la: "God and His Attributes." Sisi tumekiita: "Mwenyezi Mungu na Sifa Zake." Kitabu hiki, "Mwenyezi Mungu na Sifa Zake" ni kazi ya kielimu iliyofanywa na Mwanachuoni mahiri, Sayyid Mujtaba Musawi Lari. Mwandishi wa kitabu hiki ameichambua itikadi ya Kiislamu na Umoja wa Mungu (tawhid) kwa kutumia uhojaji wa kifilosofia na maneno mepesi. Ili kukamilisha kazi yake hii ametegemea sana juu ya Sunna na nukuu nyingi kutoka kwenye Qur'an Tukufu.


Kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya 'Al-Itrah Foundation' imeona ikitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yale yale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili, ili kuongeza ujuzi wao katika masuala ya dini na ya kijamii.


Tunamshukuru ndugu yetu, Salman Shou kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.
Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.


UTANGULIZI
Ombwe la kielimu na kiitikadi linazidi kumsogeza mwanadamu mbali na utambuzi wa ukweli kuelekea kwenye dimbwi la upotovu. Leo tunashuhudia nguvu nyingi za ubunifu wa mwanadamu zikipotea bure pale anapofumbia macho ile bahari yenye utajiri na mawimbi ya utamaduni na fikra ambayo dini inaitengeneza na vile anavyoyaruhusu maisha yake ya kisomi kunyongwa na itikadi za dunia ya kisasa.


Leo, mawazo mbali mbali yanawasilishwa kwenye kizazi cha wakati wetu chenye kiu na ambacho kimechanganyikiwa, mawazo ambayo yanatokana na dhana potovu za juu juu za wanafalsafa na wanazuoni wenye peo finyu. Mawazo haya yanajifanya kujaribu kujibu mahitaji ya kizazi cha sasa, lakini hayapendekezi maana yoyote au lengo la maisha. Muundo wa mwelekeo mmoja wa fikira ambao ndio msingi wa mawazo haya sio malezi yanayofaa kwa ajili ya akili nyeti za zama zetu hizi, na wala haustahili hata kufikiriwa katika mazingira yoyote yale ambamo akili na busara bado vinakuwa na mshiko juu ya uhai.


Hapawezi kuwa na wasiwasi kwamba tofauti mbalimbali kubwa, ukatili, mateso na ghasia ambayo yanaweza kuonekana katika historia yote, yanatokana na ikhtilafu ambazo zinaitawala dunia yenyewe na maisha ya mwanadamu.


Tunaamini kwamba Uislamu na itikadi yake, iliyoegemea kwenye tawhiid, ikiwa na, kama ilivyo, mlolongo mpana wa chambuzi za kifalsafa na kisayansi za kina za dunia yenye madhumuni na uhalisia wa nje, na kumfahamisha mwanadamu juu ya mielekeo yote ya uhai wake, una uwezo wa kutatua kimsingi ikhtilafu zote na kutowiana kote na kummuongoza mwanadamu katika mwelekeo wa kitendo cha ubunifu kilichokubalika cha kumhakikishia mustakabali wake.


Kila mfumo wa imani, ingawa kanuni zake zinaweza kuwa zimeenea na misingi yake ikawa ya kudumu, inahitaji kuwasilishwa upya kwa kila kizazi kwa mujibu wa mazingira ya zama hizo. Wenye fikra na walezi wa kiroho, ambao wamezoena na ari ya wakati na wenye kuelewa haja ya utafiti zaidi katika shughuli za msingi ili kukabiliana na mageuzi yanayoletwa na falsafa na sayansi za kisasa, ni lazima kwa hiyo, watoe mazingatio ya uangalifu, makini na yenye upeo mpana juu ya maswali haya, wakichukua vyanzo vya Kiislamu. Ni lazima wawasilishe ukweli, kama mwelekeo mpana na endelevu wa Uislamu unavyotaka kwamba uwasilishwe, na kuizoesha dunia na kanuni za kimantiki za Uislamu.


Kitabu hiki cha sasa ni juhudi za kuwasilisha, kwa njia fupi na hai, uchunguzi wa misingi ya kiimani ya Uislamu, kwa kuchanganya mantiki ya kifalsafa kwa urahisi wa maneno. Kwa vile lengo letu limekuwa ni kuwasilisha kazi fupi kiasi, tumejizuia kutokana na kunukuu maoni ya wanafalsafa na wanasayansi mbalimbali kwa kirefu. Sehemu ya kwanza ya kazi yetu inashughulika na mada za tawhid na uadilifu. Tunategemea kwamba itakuwa ni mchango wa kufanya yajulikane maoni ya Uislamu juu ya maswali haya ya msingi. Sayyid Mujtaba Musavi Lari, Qum, Julai 15, 1981.