MISINGI YA DINI NA MENGINEYO

 

AYATULLAHIL- UDHMAA SAYYID SWAADIQ AL-HUSAINIY SHIRAZIY


HUKUMU ZA KIISLAAM PAMOJA NA USUULUD-DIN- FURUUD-DIN- UBORA WA QUR'ANI TUKUFU- MFUMO WA UTAWALA KATIKA UISLAAM- MAMBO YA WAJIBU- HARAAM- MAADILI NA MAS'ALA MAPYA. KWA MUJIBU WA FAT'WA ZA AYATULLAHIL- UDHMAA SAYYID SWAADIQ AL-HUSAINIY SHIRAZIY (Mungu amzidishie uhai)
Ni wajibu kwa mukallaf kujifunza mas'ala ambayo anayahitajia sana katika maisha yake ya kila siku. (Mas'ala 12)
UTANGULIZI
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mwenye kurehemu. Sifa zote njema ni za Allah mola wa viumbe wote na sala na salam ziwe juu ya mbora wa viumbe wote, Mohammad Mustafa na kizazi chake kilicho twahara, na laana iwe juu ya maadui zao wote milele na milele. Amma baad: Inampasa kila muislaam asitosheke katika uislaam wake kwa kuwa na jina pekee la Uislaam (kwa kusema mimi ni Muislaam) na katika Qur'ani asitosheke kwa kusoma na kuwa na maandishi ya Qur'ani pekee, bali ni vema kwake kuufanyisha kazi Uislaam na kutekeleza hukumu za Qur'ani katika maisha yake yote na katika mambo yake yote, (yawe ni mambo yake binafsi, kimajii, kiuchumi, na kisiasa na mengineyo), ili awe Muislaam kwa maana halisi ya neno Uislaam, awe mtu mwema na mwenye kufaulu katika dunia na mwenye kufuzu na mwenye kuneemeka katika Akhera.


Na ni jambo lililo wazi kuwa saada ya Dunia na kufaulu katika Akhera, vitu hivi havipatikani kwa kushikamana na jina pekee na wala havipatikani kwa maombi pekee (Dua) bali jambo liyafanikishalo na kuyathibitisha kwa Muislaam ni kufanya matendo kwa mujibu wa mafunzo ya kiislaam na kutekeleza hukumu za Qur'ani za sawa na zenye kuleta maendeleo-baada ya kuwa na itikadi madhubuti ya Usulud-dini (misingi ya dini) ya kiislaam itikadi za kweli na za haki.


Kutokana na haya inamlazimu kila Muislaam anae taka kuishi maisha mema na yenye mafanikio katika Dunia na anataka mafanikio na awe ni mwenye kufaulu na mwenye neema katika Akhera- na sisi sote tunayataka ahayo-afanye juhudi za kujifunza itikadi zilizo sahihi na za haki za Uislazam na kuyatambua pia kuyaelewa mafunzo ya hali ya juu na mazuri ya Uislaam na kuzifahamu vema hukumu za Qur'ani zilizo madhubuti na za kiwango cha juu, kisha kuitakidi kimadhubuti kabisa itikadi ya kweli na kutekeleza matendo kwa wakati wote kwa mujibu wa mafunzo ya kiislaam na kutekeleza kiukamilifu hukumu za Qur'ani, hadi kufikia hatua ya kukusanya au kuoanisha kati ya jina na mwenye jina, na hivyo kuwa waislaam wenye kuridhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu na kwa Mtume wake (s.a.w) na tuwe ni wenye kuridhiwa kwa Ahlul bayti wake Mtume walio Maasuuminiin (a.s) na ili tuwe miongoni mwa watu wenye saada katika Dunia na wenye kufaulu katika Akhera.


Na ufuatao ni utangulizi ubainishao mambo ambayo ni wajibu kwa Muislaam kuyafahamu katika uwanja huu, na kwa muhtasari tunasema kama ifuatavyo: Hakika mafunzo matukufu na ya kiwango cha juu kabisa ya Uislaam na hukumu zenye kupea za Qur'ani yanagawanyika kwa muhtasari katika makundi matatu yafuatayo:
1-Usulud-din (Misingi ya dini)
2-Furuud-din (Matawi ya dini)
3-Maadili (Tabia Akhlaaq na adabu za kiislaam).
Kwa hivyo basi mwenye kuitakidi Usuulud-din na kufanya matendo yake kwa mujibu wa Furuud-din na kujipamba kwa maadili na adabu za kiislaam, atakuwa ni mtu mwenye saada katika nyumba mbili (Duniani na Akhera), na atapata faida katika sehemu mbili hizo na ataishi hali ya kuwa ni mwema na mwenye saada na kufa hali ya kuwa ni mwenye kusifiwa, na ufuatao hivi sasa ni ufafanuzi kwa ufupi wa kila moja kati ya makundi matatu haya tuliyo yataja.