DALILI ZA KIAMA

 
Kutotekeleza amri ya kutenda mema na kuepuka mabaya

Miongoni mwa dalili za kukaribia kiama ni kuwa watu wanaojua kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha kutenda mema na kuepuka uovu hawatatekeleza jambo hilo: Siku ya mwisho haitasimama mpaka watakapobakia watu ambao hawatajali mema na kamwe hawatozuia maovu (Ahmad).

Karibu na kusimama kwa kiama mambo mema yatapungua (Bukhari) Katika hadithi nyingine inabainishwa dalili ya kiama kuwa Waislamu walioamini watadhoofishwa kwa msukumo wa watenda dhambi:
Saa itafika pale sauti zitakapopazwa misikitini (Tirmidh) Saa itafika pale viongozi watakapokuwa madhalimu (Al Haithami, Kitab al Fitan)

Mtume (s.a.w) kasema, katika zama za mwisho, kutakuwa na watu wachache sana wanaoweza kuitwa waumini: Utafika wakati kwa watu wangu ambapo misikiti itajaa watu lakini watakuwa hawana muongozo sahihi (Ibn Babuya, Thawab ul A'mal Hadith moja inasema kuwa waislamu wa kweli watalazimika kuficha imani zao na kufanya ibada kwa siri:

Wakati utafika ambapo wanafiki wataishi kwa siri miongoni mwenu na wenye imani watajaribu kuhuisha dini yao kwa watu wengine Katika Hadith ifuatayo inabainishwa ishara ya zama za mwisho kuwa Misikiti itafanywa sehemu za mikusanyiko ya kijamii tu. Utafika wakati ambapo watu watatumia misikiti kama vijiwe tu vya kukutania. Katika zama mwisho, watatokea watu watakaosoma Qur'an kwa ajili tu ya kujinufaisha badala ya kupata radhi za Allah:

Na aombe thawabu kwa Allah yule asomaye Qur'an. Kwa sababu katika zama za mwisho kutakuwa na watu wengi watakaosoma Qur'an na kutafuta malipo kwa watu wengine. (Tirmidhi). Dalili nyingine ni kuwa Qur'an itasomwa kwa ajili ya kujifurahisha (kujiburudisha) tu kama vile wimbo:

Wakati Qur'an itakaposomwa mithili ya uimbaji wa nyimbo na wakati mtu atakapoheshimika (atakaposifika) kwa kuimba namna hiyo hata kama hana ilimu ( Al-Tabarani, Al-Kabir) Baadhi ya watu watakaotambuliwa kama Waislamu watakuwa na uelewa potofu juu ya kadari, wakati ambapo wengine wataamini nyota kuwa zinaweza kuwapatia ujuzi wa kujua maisha yao ya baadae. Hii ni dalili ya zama za mwisho:

Saa itafika wakati watu watakapoamini nyota na kukanusha Qadari (Al-Haythami, Kitab al Fitan) Licha ya ukweli kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha riba hivi leo riba ndio mtindo wa maisha. Katika Hadith ifuatayo hii inaelezewa kama dalili mojawapo ya ya kiama:

Bila shaka kitakuja kipindi ambacho hakuna hata mtu mmoja atakayesalimika na riba. Endapo mtu ataepuka riba kwa njia ya moja kwa moja basi hatoweza kuukwepa moshi (athari) utakaotokana nayo. Kwa kiasi fulani athari zake zitamfika tu. (Imesimuliwa na Abu Huraira)

Hapa labda tutoe ufafanuzi kidogo. Katika ulimwengu wetu wa leo riba imejikita katika mifumo ya fedha na uchumi wa kitaifa na kimataifa. Aidha sekta za kiserikali na binafsi zinashiriki katika uchumi wa riba. Mabenki na makampuni binafsi ya kitaifa na kimataifa hasa yale yanayoendesha shughuli za ukopeshaji wa fedha au bidhaa yanatoza riba kwa viwango mbalimbali. Karibu Asasi zote za utoaji wa mikopo ya fedha zinatoza riba.

Kwa hali hiyo hakuna mtu ambaye anaweza kudai kuwa yeye amesalimika na riba. Maadam mfumo wa uchumi wa Taifa haukusalimika na riba basi sote tunahusika na jambo hili. Hivyo hadithi ya Mtume (s.a.w) inawafikiana kabisa na mazingira yetu.

Dalili nyingine ya zama za mwisho ni kuwa Hija itafanywa kwa ajili ya kusafiri tu, kufanya biashara, kujionesha tu na kuombaomba. Wakati huo utafika pale matajiri watakapokwenda Hija kwa malengo ya kusafiri kwa minajili ya kujifurahisha, biashara, kujifaharisha na kujionesha, na masikini kwenda kuomba. Imesimuliwa na Anas (r.a )

Tatizo kubwa ambalo Wanaadamu wanakabiliana nalo hivi leo ni kusambaratika kwa jamii. Kuporomoka huku kwaonekana katika vipengele mbali mbali vya maisha. Kuvunjika kwa familia, ongezeko la talaka na uzazi haramu ndio mambo ambayo yanapelekea kusambaratika kwa taasisi ya familia. Maisha hivi leo yamekuwa ya misukosuko, mashaka, huzuni, wasiwasi na vurugu tupu. Watu waliokosa maadili ya kiroho wanaona kuwa ili kuondokana na adha ya dunia basi bora wajitumbukize katika ulevi wa pombe na dawa za kulevya. Wengine wanaona kuwa hakuna ufumbuzi wa hali ngumu inayowakabili basi njia wanayoona itawatowa matatizoni ni kujinyonga. Moja ya Ishara kubwa za kuanguka kwa jamii ni kule kuongezeka kwa mambo ya haramu.

Kiwango cha uhalifu kimeongezeka kwa kiasi kinachowashangaza mabingwa wa maswala ya jamii. Ripoti ya uhalifu na haki ulimwenguni, "Universal Crime and Justice," Iliyotayarishwa na kituo cha udhibiti wa jinai cha umoja wa mataifa, United Nations' International Crime' imetoa tathmini ya jumla ya uhalifu ulimwenguni. Ripoti hiyo inasema:

Kimsingi, kama ilivyokuwa katika miaka ya themanini, kiwango cha uhalifu pia kiliendelea kuongezeka katika miaka ya tisini. Kila mahali ulimwenguni, katika kila kipindi cha miaka mitano, theluthi moja ya watu wanaoishi mijini wamekumbwa na mikasa ya uhalifu. Kote ulimwenguni vitendo vya wizi, ujambazi, utapeli, uasherati vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku. Matukio haya, pamoja na sababu nyinginezo, yamekuwa yakihusishwa na athari mbaya za kiuchumi.

Kiwango cha utumiaji wa dawa mbali mbali za kulevya nacho kimeongezeka katika miaka ya karibuni. Watu hasa vijana wamekuwa wakibwia unga na kujidunga sindano zenye dawa za kulevya. Kwa kweli tatizo hili limeleta madhara ya kiafya, athari mbaya za kifamilia na kijamii.

Kwa hakika sababu za matatizo yote haya zimeelezwa katika Qur'an pale inaporejea historia ya jamii zilizopita. Kuporomoka kwa jamii na matatizo mbali mbali ni matokeo ya wanadamu kumsahau Mwenyezi Mungu na lengo halisi la maisha na hivyo kuyatupa maadili ya kiroho.

Matukio yote ya kuporomoka kwa jamii tunayoyashudia hivi leo tayari yalikwishabashiriwa na Mtume (s.a.w) karne 14 zilizopita. Mtume (s.a.w) amesema kuwa miongoni mwa dalili za zama za mwisho ni pale watu watakapokabiliana na vita na mabadiliko ya kijamii (Ahmad Diya"al diin al Kamush Khanawi, Ramuzi al ahadith). Zifuatazo ni hadith zinazohusiana na awamu ya kwanza ya zama za mwisho:

Kutakuwa na miaka ya udanganyifu ambapo mtu mkweli hatoaminiwa na muongo ataaminiwa (Ibn Kathir). Kutakuwa na miaka ya vurugu. Watu watamuamini muongo na kutomuamini yule anayesema ukweli. Watu hawatamuamini mtu mkweli na watamuamini yule ambaye ni fisiki. (Ahmad). Siku ya kiama haitakuja mpaka watu duni kabisa wawe watu wenye furaha kabisa (Tirmidh).

Kama inavyosomeka katika hadithi hizo kutakuwa na ongezeko la watu waovu ambapo wale wanaoonekana wakweli kumbe ni waongo na wale wanaoonekana waongo kumbe ndio wakweli. Hizi ni dalili za zama za mwisho. Hadithi moja inabainisha kuwa kutakuwa na watu wachache sana wakweli na kiasi kidogo sana cha pesa kitakachopatikana kwa kuzingatia kanuni na sheria za dini yetu:

Katika zama za mwisho watu watakuwa wakifanya biashara lakini hakutakuwa na mtu yeyote mkweli (Bukhari na Muslim). Ushahidi wa kweli utatupiliwa mbali na ushahidi wa uongo na kusingiziana ndivyo vitakavyoshamiri. Hii ni dalili nyingine ya zama za mwisho. Kwa hakika katika saa ya mwisho kutakuwa na ushahidi wa uongo na ufichaji wa ushahidi (Ahmed na Hakim). Kutakuwa na shutuma za uongo za mambo machafu na masingiziano. (Tirmidh)

Kigezo pekee ambacho kwacho watu watapimwa ubora wao ni mali, hashima itategemea mtu ni tajiri kiasi gani:
Kabla ya saa ya mwisho kufika, kutakuwa na salamu maalumu kwa watu wa tabaka fulani. (Ahamad) Hakutakuwa na hukumu mpaka pale salamu zitakapotolewa sio kwa watu bali kwa watu mahususi. (Mukhtasari Tazkira Khutub). Inasemwa katika hadithi kuwa dalili nyingine ni kuvurugika kwa uhusiano wa kijamii baina ya watu:

Ni wale watu ambao mtu anawajuwa tu ndio watakaopewa salamu (Ahmad Diyal al diya'al Din al Kamushi Khanawi, Ramuzi al ahadithi) Katika hadithi ifuatayo inaelezwa kuwa nafasi za kazi zitatolewa kwa watu wasio na sifa: Pale madaraka na mamlaka yatakapokwenda mikononi mwa watu wasio na sifa, basi hapo muisubiri ile saa (kiama). (Bukhari). Dalili nyingine ya zama hizo itakuwa ni kuvunjika kwa uhusiano wa wanafamilia, marafiki, majirani na kuvurugika kwa jamii na maadili:

Mtu kutokuwa na mapenzi na Mama yake na kumfurusha Baba yake (Tirmidh). Kwanza kutakuwa na sokomoko kwa mtu kuhusiana na familia yake, mali yake, nafsi yake, watoto wake, jirani zake (Bukhari na Muslimu).
Dalili nyingine ya zama za mwisho ni kuwa vijana watakuwa waasi na mapenzi na heshima kati ya vijana na wazee vitapungua: Wakati wazee watakapokosa huruma kwa vijana, na wakati vijana watakapokosa heshima kwa wazee… Watoto watakapokuwa na jazba… Basi hapo hukumu ipo jirani.
(Imeripotiwa na Umar (r.a)). Hadithi nyingine zinaonyesha dalili nyingine ya zama za mwisho kuwa talaka na idadi ya watoto wa nje ya ndoa vitaongezeka: Talaka itakuwa ni jambo la kila siku (Allamah Safarini, Ahwal Yaum al Kiyama). Kutakuwa na wingi wa watoto wa haramu (Al Muttaqi Al Hindi, Muntakhab Kanzul Ummaal).

Kwa kutenzwa na itikadi ya Ulahidi na mtazamo wa kidunia, watu wataikumbatia dunia kupindukia na wataghafilika na maisha ya akhera. Hii ni dalili nyingine ya zama za mwisho: Uchoyo na Uroho utaongezeka. (Muslim, ibn Majah). Wakati huo, watu wataiuza dini yao kwa kiasi kidogo cha maslahi ya dunia (Ahmad). Hadithi nyingine inasema kuwa watu watalaaniana na kuapizana: Katika siku za mwisho kutakuwa na watu ambao pale wakutanapo hulaaniana na kutukanana badala ya kusabahiana (kwa salamu) (Allama) (Jalaludiin) Suyuti, Durre Mansouri). Dalili nyingine ya zama hizo ni utesi na dharau kwa watu wengine:

Kutakuwa na wingi wa wasutaji, vizabizabina, Wambea, wagombanishaji, waamsha fitina na watu wenye dharau katika jamii. (Al Mutaqi Al Hindi, Muntakhab Kanzul Ummaal) Dalili nyingine ya Kiama ni rushwa:

Udanganyifu na ulaghai yatakuwa mambo ya kawaida (Allama Safarini Ahwal Yaum al Qiyama) Rushwa itaitwa zawadi na itaonekana kama halali tu: (Ammal Al diin al Qazwini, Mufid al ulumi wa Mubid al Humum). Mtume (s.a.w) kasema, mauaji yataongezeka sana katika zama za mwisho: Kiama hakitasimama hadi pale mauaji yatakapozidi. (Bukhari).