DALILI ZA KIAMA

 
Kukanusha dini sahihi na maadili ya Qur'an

Hadithi zinazozungumzia dalili za siku ya mwisho zinatupa maelezo ya kina juu ya wakati ambao dalili hizi zitadhihirika. Twaweza kufahamikiwa kutokana na hadithi za Mtume (s.a.w) kuwa awamu ya kwanza ya zama za mwisho ni kipindi ambacho kitaonekana kuwa cha kidinidini, lakini kumbe ni kipindi ambacho kitaikataa kabisa dini ya Allah na maadili ya Qur'an.

Ni kipindi ambacho yale mambo yaliyobainishwa katika aya za Qur'an yatafumbiwa macho, dini itatumbukia katika mifarakano, migogoro, hamasa na ushabiki. Ibada zitafanywa kwa ria na dini itatumika kama biashara ya kujipatia faida na maslahi ya kidunia. Ni katika kipindi hiki ambapo Imani haitategemea elimu na utafiti bali itakuwa mwigo wa kufuata mkumbo tu na hamasa ya mtu. Katika kipindi hiki watu wanaoitwa Waislamu watakuwa wengi mno wakati ambapo wanazuoni wa kweli na Waislamu wenye Ikhlasi watakuwa wachache mno.

Zifuatazo ni dalili zilizotajwa na Mtume (s.a.w) Karne 14 zilizopita, dalili ambazo zinathibitika wazi wazi katika wakati tulionao: Kwa mujibu wa Qur'an, Mtume (s.a.w) anasema kuwa watu wake wameitelekeza Qur'an:

Na Mtume alikuwa akisema, Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya Qur'an hii kuwa kitu kilichoachwa. (25:30). Inabainishwa katika hadithi kuwa katika zama za mwisho muongozo wa Qur'an utatupiliwa mbali na watu watajitenga nao:

Karibia ya kusimama kwa saa kutakuwa na zama ambazo elimu ya (Qur'an) itatoweka na giza totoro litagubika… (Bukhari). Utakuja wakati wa uma wangu ambapo hakutabaki chochote kilichobaki katika Qur'an isipokuwa sura yake ya nje tu na hakutabaki chochote cha Uislamu isipokuwa jina lake tu na wao watajiita kwa jina hili ingawaje ni watu waliombali kabisa na Uislamu. (Ibn Babuya, Thawab ul-A'amal). Mfano umetolewa katika suratil Jumaa aya 5:

Mfano wa wale waliopewa Taurat, kisha hawakuichukua kwa ktuitumia ni kama Punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa…Hapana shaka kuwa aya hii inatoa onyo kwa Waislamu, ikiwakumbusha kuwa wajihadhari wasije wakatumbukia katika dhambi ileile nzito. Qur'an imeshushwa kama kitabu cha muongozo ambao watu waufuate.

Mtume (s.a.w) kasema kuwa licha ya ukweli kuwa Qur'an itasomwa lakini elimu na hekima iliyomo ndani yake hatazingatiwa. Hii di dalili nyingine ya ule wakati wa zama za mwisho:

Utakuja wakati juu ya umma ambapo watu watasoma Qur'an lakini haitakwenda kokote isipokuwa itaishia kwenye makoo yao (haitaingia nyoyoni.) (Bukhari). Mtume wa Allah alisema jambo fulani kisha akasema utatokea wakati ambapo elimu haitakuwepo tena. Aliuliza Ziyadi: Ewe Mtume wa Allah itatowekaje elimu licha ya ukweli kuwa tutakuwa tukiisoma Qur'an na kuwafundisha watoto wetu kuisoma na watoto wetu nao watawafundisha watoto wao kuisoma hadi siku ya kufufuliwa? Hapo Mtume akasema je Mayahudi na Wakristo hawasomi Taurati na Biblia na kutotenda kwa mujibu wa yale yaliyomo humo? (Ahmad, ibn Majah, Tirmidhi).

Watu kuitumia dini kwa malengo ya kidunia na kujivika ngozi ya kondoo waonekane wema. Kufuata maadili ya Wayahudi na Wakristo Ni dalili moja wapo ya kiama kuwa baadhi ya Waislamu watafuata nyendo za Wayahudi na Wakristo tena watawaiga kimasonge. Mtume (s.a.w) kasema:

"Kwa hakika mtafuata nyendo za watu waliokuwepo kabla yenu shubiri kwa shubiri na dhiraa kwa dhiraa (Inchi hadi Inchi) kiasi ambacho hata wakitumbukia kwenye shimo la Kenge nanyi pia mtawafuata humo" tukauliza, ewe Mtume wa Allaha, una maana kuwa ni Wayahudi na Wakristo? Akajibu, kama si wao ni nani tena? (Bukhari) kutokana na hadithi hiyo tunaona kuwa kabla ya zama za mwisho kutakuwa na mielekeo mibovu ya kifikra na kimaadili na kwamba tawala zitakazokuwepo zitajitenga mbali na ukweli na haki jambo litakalosababisha mfarakano mkubwa na kuwatoa watu katika mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa maadili ya Wayahudi na Wakristo ndio maadili ya magharibi au ya Wazungu, na mifumo ya maisha iliyojitenga na Qur'an ndio mifumo ya Magharibi inayotawala dunia hivi leo.

Muumini na Kafiri
Mtume wa Mwenyezi Mungu kasema:
Kabla ya saa ya mwisho kutakuwa na vurugu vurugu tupu ambapo mtu atakuwa Muumini asubuhi na Kafiri jioni yake au atakuwa Muumini jioni na Kafiri asubuhi yake. (Abuu Daudi) Kuna vielezeo vingi vinavyoonesha hali hiyo hivi leo. Mtu anaweza kuswali swala tano lakini akawa muasherati, anaweza kushinda kutwa nzima anaswali lakini usiku anazini, anaweza kushinda na swaumu kutwa nzima lakini usiku yuko na hawara au kimada, mwingine anaweza kuwa sala tano lakini muongo, mwizi, tapeli, mla rushwa, mla riba na kadhalika. Mseto huu wa Uumini na Ukafiri unaonekana kwa watu wengi hivi leo japo kwa sura tofauti.

Kutozingatia halali na haramu
Dalili nyingine ya kiama ni kuwa watu hawatazingatia yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu katika Qur'an. Mtume (s.a.w) kasema: Utafika wakati ambapo mtu hatojali kama vitu avipatavyo ni vya halali au ni vya haramu (Bukhari).

Wanazuoni wenye nyuso mbili
Mtume (s.a.w) kasema: Katika zama za mwisho baadhi ya watu wanaokubalika kama wanazuoni watakuwa wanafiki kweli kweli wenye nyuso mbili; Mbwa Mwitu watasoma katika zama za mwisho. Wale watakaoziona zama hizo waombe nusra kwa Mwenyezi Mungu kutokana na uovu wa wanazuoni hao. Kutakuwa na mafisadi kweli kweli. Unafiki ndio utakaoshitadi. (Tirmidhi, Nawadil al Usul.)

Kutatokea watu katika zama za mwisho ambao watajinufaisha kwa kutumia dini (Tirmidhi) Kutumia dini kwa malengo ya kidunia Mtume wa Allah kasema;

Katika zama za mwisho watu wataitumia dini kitapeli kwa malengo yao ya kidunia na kujivika ngozi za kondoo hadharani kuonesha unyenyekevu. Ndimi zao zitakuwa tamu kama sukari lakini nyoyo zao zitakuwa nyoyo za Mbwa mwitu. (Tirmidh).

Watu hawatoheshimu mipaka ya sheria za Kiislamu. Hawatochelea kuutumia Uislamu kwa ajili ya kujipatia maslahi yao. Watu watajali zaidi kuonekana wanatenda mambo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wakiwa hawana chembe ya wema, huruma na usaidizi kwa wanaowahubiria. Watakuwa wakiwakamua wafuasi wao kutoa kwa kutumia aya na mahubiri ya kukhofisha na kutumainisha hali yakuwa wao wenyewe hawana ukweli katika nafsi zao.

Katika zama za mwisho za umma wa walioamini, watu watapamba Misikiti lakini wataziacha nafsi zao katika maangamizi, watu ambao watashindwa kuitunza dini ya Mwenyezi Mungu kama wanavyozitunza nguo zao, watatelekeza majukumu ya dini yao kwa sababu ya shughuli zao, watu hawa watakuwa wengi.