DALILI ZA KIAMA

 
Umasikini

Inafahamika kuwa umasikini ni ukosefu wa chakula, makazi, mavazi, huduma za afya na mahitaji mengine ya msingi kwa sababu ya kipato duni. Licha ya fursa zinazopatikana kutokana na maendeleo ya teknolojia, umasikini hivi leo ni moja kati ya matatizo makubwa kabisa yanayoukabili ulimwengu. Katika mabara ya Afrika, Asia, Amerika Kusini na Ulaya Mashariki watu wengi wanahangaika na njaa kila siku. Kwa sababu ya mgao mbaya wa rasilimali za ulimwengu umasikini umesababisha uwepo mgawanyiko kati ya nchi za kaskazini ya jangwa la sahara ambazo ni za ulimwengu wa kwanza na nchi za kusini maskini ambazo ni za ulimwengu wa tatu.


Ubeberu na Ubepari usio na mipaka unazuia mgawanyo wa kipato ulimwenguni kote na unakwaza maendeleo ya nchi changa na nchi zinazoendelea. Wakati ambapo kuna watu wachache wanaofurahia kipato kinachozidi mahitaji yao, kuna idadi kubwa ya watu wanaohangaika na matatizo ya umasikini na ufukara. Katika Ulimwengu wa leo umasikini umefikia hatua mbaya au kiwango kibaya sana.

Ripoti ya mwisho ya UNICEF ilieleza kuwa mmoja kati ya kila watu wanne duniani anaishi katika tabu na shida isiyoelezeka. Watu bilioni 1.3 duniani wanaishi kwa wastani wa chini ya dola moja kwa siku. Watu bilioni 3 duniani wanaishi kwa dola mbili kwa siku. Takribani watu bilioni 1.3 hawapati maji safi. Watu bilioni 2.6 hawapati maji salama.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la chakula duniani, (FAO), Mwaka 2000, watu milioni 826 duniani kote hawapati chakula cha kutosha. Kwa maneno mengine mmoja katika kila watu sita ana njaa. Katika miaka kumi iliyopita dhulma katika mgawanyo wa kipato imeongezeka kwa kiwango kisichosemeka.

Ripoti za umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, katika mwaka 1960 asilimia 20 (20%) ya watu wanaoishi katika nchi tajiri kabisa duniani walikuwa na pato lilozidi mara thelathini pato la nchi 20 masikini kabisa. Hadi kufikia mwaka 1995 iliongezeka mara 82. Kikiwa ni kielezeo cha kutoweka kwa haki ulimwenguni, mali za matajiri 225 wakubwa kabisa ulimwenguni ni sawa na pato la mwaka la asilimia 47 (47%) ya nchi masikini ulimwenguni.

Takwimu za sasa zinaonyesha yale ambayo Mtume (s.a.w) aliyasema juu ya kuongezeka kwa umasikini. Katika hadithi inabainishwa kuwa umasikini na njaa ni miongoni mwa dalili za kipindi cha kwanza cha zama za mwisho:

Masikini wataongezeka (Amal Al Diin Al Qazwin, Mufid Al Ulum wa Mubid Al humum) Kipato kitagawanywa kwa matajiri tu, hakuna mafao kwa masikini. (Tirmidhi). Ni dhahiri kuwa kipindi hicho kilichobashiriwa na Mtume (s.a.w) kinawiana na hali ya wakati wetu wa leo. Tukiangalia karne zilizopita tunaona kuwa shida na tabu zilizoletwa na ukame, vita na majanga mengine zilikuwa za muda mfupi na ziliishia katika eneo moja moja. Lakini umasikini na shida za leo ni za kudumu na sugu. Kwa hakika Mola wetu ni Mwingi wa Rehma, yeye hadhulumu watu lakini kwa sababu ya ukosefu wa shukurani wa wanadamu na maovu wanayoyafanya, umasikini na tabu vimeongezeka. Kwa hakika hali ya mambo ya kusikitisha inaonesha wazi kuwa dunia imetanzwa na uchoyo na ubinafsi.

Kuporomoka kwa maadili, kushamiri kwa ushoga na ukahaba
Katika zama zetu za leo kuna janga kubwa linalohatarisha uhai wa jamii ulimwenguni. Mithili ya virusi vinavyoua mwili, janga hili linasababisha msiba mkubwa wa kijamii. Janga hilo ni mmomonyoko wa maadili ambayo husaidia kustawisha jamii. Ushoga, Ukahaba, uhusiano haramu wa kijinsia kabla ya ndoa na nje ya ndoa, Filamu za ngono, Picha za ngono, unyanyasaji wa kijinsia na ongezeko la maradhi ya zinaa, mashindano ya kukaa uchi maarufu ulimbwende, uuzaji na utumiaji wa vileo na dawa za kulevya miongoni mwa vijana ni miongoni mwa ishara kubwa za kuporomoka kwa maadili.

Mambo haya ndiyo yamekuwa yakizishughulisha jamii. Idadi kubwa ya watu haijali hatari hii inayozidi kuwa kubwa na wanaiona kama jambo la kawaida tu. Lakini takwimu zinaonesha kuwa kila siku ipitayo kiwango cha hatari kinazidi kuongezeka. Ongezeko la maradhi ya zinaa ni kigezo kikuu cha kusaidia kuonesha ukubwa wa matatizo yanayomkabili mwanadamu. Kwa mujibu wa rekodi za Shirika la Afya ulimwenguni magonjwa yanayotokana na zinaa yanachukuwa sehemu kubwa ya maradhi. Ripoti zinaonesha kuwa kati ya kesi mpya za magonjwa ya zinaa zinazokadiriwa kufikia milioni 333 kila mwaka ulimwenguni kote, Ukimwi ndio tatizo kubwa zaidi.

Takwimu za Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) zinaonesha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi tokea pale ulipoanza imefikia watu milioni 18.8. Ripoti za shirika hilo kwa mwaka 2000 zinaielezea hivi hali ya mambo: "Ukimwi una nafasi ya kipekee katika kuleta athari mbaya za kijamii, kiuchumi na katika mipango ya sensa ya maendeleo".

Miongoni mwa mambo mabaya kabisa yanayozidi kushamiri ni ushoga. Katika baadhi ya nchi jambo hili limehalalishwa kama ndoa, linapewa heshima zote za ndoa na limeundiwa vyama na jumuiya. Duniani kote uovu huu unapingwa. Kushamiri kwa ushoga hivi leo kunatukumbusha hatima ya watu wa Lut waliokithiri katika uovu huu. Kama isemavyo Qur'an walipoukataa wito wa Lut kuiendea njia sahihi, Mwenyezi Mungu aliuangamiza mji na watu wake kwa maangamizi makubwa.


Ni dhahiri kuwa zile hadithi zinazoelezea zama za mwisho na mporomoko wa maadili zinathibitika hivi leo. Hadithi moja inasema kuwa kutoweka kwa aibu katika dhambi ya ukahaba ni dalili ya kiama:

Kutashitadi maingiliano haramu ya kijinsia wazi wazi (Bukhari). Saa hiyo itafika wakati uzinzi utakapokuwa umeenea sana (Al-Haythami, kitab al fitan) Kufifia kwa maadili na hisia ya aibu kunaelezwa kwa maneno haya:

Saa ya mwisho haitasimama hadi pale watu watakapofanya uzinzi njiani (njia wanazopita watu) ( Ibn Iban na Bazzar). Yafaa kukumbuka kuwa hivi sasa matukio ya ukahaba yanayochukuliwa na kamera za siri yamekuwa yakioneshwa katika Internate, vituo vya Televisheni na katika magazeti yanayoitwa ya ngono na udaku. Makahaba wanaingiliana na wateja wao wazi wazi katikati ya mitaa. Hali kadhalika kuna Filamu na picha nyingi zinazosambazwa ulimwenguni kote ambazo zinaonesha uzinzi unavyofanyika wazi wazi. Takriban katika miji mingi duniani makahaba wamekuwa wakisimama na wateja wao na kufanya mambo ya ajabu barabarani hasa nyakati za usiku.

Hii ni dalili nyingine ya kiama iliyobainishwa katika hadithi. Mamilioni ya watu wanaishuhudia wenyewe dalili hii duniani kote. Hadithi zifuatazo zinaonyesha kuwa kuibuka kwa ushoga kuwa jambo la kawaida la maisha ni ishara kuu ya zama zinazokaribia siku ya mwisho:

Wanaume watawaiga wanawake na Wanawake watawaiga wanaume. (Allama Jalaluddin Swiyuti, Durre- Mansuri). Watu watazama katika ushoga na usagaji (Al Mutaqi al Hindi, Muntakhab, Kanzul Ummaal).

Vitendo vya wanaume kuwaiga wanawake na wanawake kuwaiga Wanaume vimekuwa vingi hivi leo. Tunashuhudia Wanaume wanaosuka nywele zao na pia tunashuhudia Wanaume wanaowasuka nywele wanawake kwenye Masaluni na majumbani. Imekuwa ni aina ya ajira kwa wanaume hawa hasa Wamasai kupita mitaani kusuka nywele akina Mama.

Pia tunashuhudia Wanaume wakivaa hereni masikioni na vidani shingoni. Tunashuhudia teknolojia ikitumika vibaya kubadilisha maumbile ambako kumeleta kiroja cha mwanaume kubeba uzazi na kujifungua! Kwa upande mwingine tunashuhudia Wanawake wakivaa mavazi ya Wanaume, wakijaribu kuiga usemaji wa kiume. Wakioa wanawake wenziwao na wakifanya kazi za mitulinga. Tunashuhudia wanawake wakivaa mavazi yenye kuonesha vivazi vyao vya ndani na maungo mateke ili kushawishi uzinzi.