DALILI ZA KIAMA

 
Kuangamia kwa Miji mikuu:

Vita na majanga
Miongoni mwa mambo aliyoyasema Mtume kuhusana na zama za mwisho ni hili:
Miji mikuu itaangamia na itakuwa kana kwamba haikupata kuwepo hapo kabla (Al-Muttaq Al-Hindi Al Burhan fi Alamat Al Mahadi Akhir al Zaman)
Kuangamia kwa miji mikuu iliyozungumzwa katika hadithi hii kunatukumbusha maangamizi ambayo yanatokea hivi leo kutokana na vita na majanga mbali mbali ya asili. Silaha za kisasa za Nyuklia, Madege ya Kivita, Mabomu, Makombora na Zana nyingine za kisasa zimesababisha maangamizi yasiyosemeka.

Zana hizi za hatari zimeleta kiwango kikubwa cha maangamizi ambacho dunia haijapa kukiona hapo kabla. Kwahakika miji mikuu ndio imekuwa malengo makuu ya mashambulizi na imekuwa ikiathirika zaidi kutokana na maangamizi haya. Maangamizi yasiyo na mfano ya vita ya pili ya dunia ni kielezeo cha haya. Kwa kutumika bomu la Atomic katika vita kuu ya dunia, miji ya Hiroshima na Nagasaka iliangamizwa kabisa.

Kutokana na Mabomu mazito, miji mikuu ya Ulaya na miji mingine mikubwa imepata kiwango kikubwa cha hasara. Buku la marejeleo (Encylopedia Britannica) linaelezea hasara iliyosababishwa na vita kuu ya pili ya dunia katika miji ya Ulaya: Maangamizi yaliyotokea yameigeuza sehemu kubwa ya Ulaya kuwa kama taka taka na ilimalizwa na mabomu ya moto, bara bara zilijaa mashimo matupu, sura ya nchi ilikuwa giza tupu njia za reli zikaharibiwa na kutofanya kazi, madaraja yalibomolewa na bandari zilijaa Meli. Berin, anasema Jenerali Lusias D. Clay, Naibu Gavana wa Jeshi katika ukanda wa Post war German, lilikuwa kama jiji la wafu.

Kwa kifupi maangamizi ambayo yalisababishwa na vita ya pili ya dunia yanashabihiana kabisa na hadithi ya Mtume (s.a.w) . Sababu nyingine ya maangamizi ya miji mikuu ni majanga ya asili. Ni ukweli wa kitakwimu kuwa zama tunazoishi hivi leo zimeshuhudia kuongezeka kwa idadi na madhara ya majanga ya asili. Katika miaka kumi iliyopita, majanga ya asili yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yalikuwa ni mambo ambayo hayakuwahi kutokea.

Maangamizi, Umasikini, mauaji, machafu kuongezeka
Sababu nyingine ya maangamizi katika miji ni majanga ya asili. Kulingana na takwimu, zama zetu zimeshuhudia ongezeko la idadi na ukubwa wa majanga ya asili. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kulikuwa na majanga yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Haya yalikuwa ni majanga ya aina yake.

Hatari kubwa ya uchafuzi wa hali ya hewa unaosababishwa na viwanda ni tishio kwa dunia nzima. Viwanda vinavuruga urari wa angahewa ya dunia na kuongeza mabadiliko ya hali ya hewa. Mwaka 1998 ulikuwa ni mwaka wa joto kali sana duniani tangu rekodi za hali ya hewa zianze kuwekwa. Kwa mujibu wa maelezo ya kituo cha taarifa za hali ya hewa cha Marekani, idadi kubwa ya majanga yaliyotokana na hali ya hewa ilikuwa mwaka huo wa 1998.

Kwa mfano, Kimbunga kimeelezewa na wachunguzi wengi kuwa ndio janga baya mno la kimaumbile lililoikumba Amerika ya kati. Katika miaka michahe iliyopita vimbunga, dhoruba, tufani na majanga mengine yameleta maangamizi katika bara la Amerika na katika sehemu nyingine kadha wa kadha za dunia. Mbali na hayo mafuriko nayo yameleta maangamizi katika maeneo kadhaa ya watu. Aidha mitetemeko ya ardhi, Volkeno nayo pia yamesababisha maangamizi makubwa. Hivyo basi maangamizi yote haya yaliyotokea katika miji ni ishara muhimu.

Mitetemeko ya ardhi
Hapana shaka kuwa katika historia, hakuna majanga ya asili ambayo yamewaathiri watu kwa kiasi kikubwa kama mitetemeko ya ardhi. Mitetemeko ya ardhi hutokea mahali popote na wakati wowote. Kwa karne zote mitetemeko ya ardhi imesababisha maafa na hasara kubwa ya mali. Kwa sababu hii tetemeko la ardhi ni janga linalohofiwa mno. Hata teknolojia ya karne ya Ishirini na Ishirini na moja imeweza kwa kiasi kidogo sana kuzuia uharibifu wa tetemeko la ardhi.

Tetemeko la ardhi la mwaka 1995 kule Kobe laweza kuwa somo kwa wale wanaodhani kuwa teknolojia itaweza kudhibiti maumbile. Itakumbukwa kuwa tetemeko hili la ardhi lilitokea bila kutarajiwa kwenye eneo kubwa la viwanda na usafirishaji. Licha ya ukweli kwamba lilidumu kwa sekunde ishirini tu, kama lilivyoripoti gazeti la Time, bado lilisababisha hasara ya dola bilioni 100. Kadhalika tetemeko la ardhi ndani ya bahari lililofahamika kama Tsunami fukweni mwa nchi za Indonesia, Thailand na ukanda mzima wa Pwani ya Asia, lilikuwa la aina yake kupata kutokea katika historia ya mwanaadamu.


Katika miaka michache iliyopita mitetemeko mikubwa ya ardhi imetokea mara kwa mara na ndio matishio makubwa ya maisha ya watu duniani kote. Tukiangalia takwimu zilizokusanywa na kituo cha taarifa za matetemeko ya ardhi cha Amerika mwaka 1999 tunaona kuwa mitetemeko ipatayo 20, 832 ilitokea sehemu mbali mbali duniani. Matokeo yake watu wanaokadiriwa kufikia 500,000 walikufa. Matukio yote haya yanakumbushia maneno ambayo Mtume (s.a.w) aliyasema miaka 1400 iliyopita: Kiama hakitasimama mpaka pale mitetemeko ya ardhi itakapotokea mara kwa mara. (Bukhari).

Katika Qur'an kuna aya kadhaa zinazobainisha uhusiano kati ya mitetemeko ya ardhi na zama za mwisho. Sura ya 99 inaitwa suratil Zil Zaala ambayo maana yake ni mtikisiko au tetemeko la ardhi. Sura hii yenye aya nane inaelezea mtetemeko mkubwa wa ardhi na inasema kuwa kufuatia mtetemeko huo siku ya hukumu itakuwa imefika. Watu watafufuliwa makaburini na kutoa hesabu ya amali zao kwa Mwenyezi Mungu na kupata malipo yao hata kwa jambo dogo sana walilolifanya:

Itakapotetemeshwa ardhi kwa mtetemesho wake mkubwa. Na itakapotoa ardhi mizigo yake, na binadamu akasema (wakati huo) (oh!) ina nini leo ardhi? Siku hiyo itatoa habari zake zote kwa kuwa Mola wake ameifunulia (ameiamrisha kufanya hayo). Siku hiyowatu watatoka (makaburini) vikundi vikundi ili waonyeshwe vitendo vyao. Basi anayefanya wema hata kwa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jazaa yake na anayefanya uovu hata kwa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jazaa yake. (99:1-8).