DALILI ZA KIAMA

 
Vita na machafuko

Katika Hadithi moja Mtume (s.a.w) alizielezea zama za mwisho hivi: Mtume wa Allaha alisema: Harji (itazidi kuongezeka), Watu wakauliza harji ndio nini? Akajibu, ni mauaji, ni mauaji. (Bukhari). Maana ya harji iliyotajwa katika hadithi ya hapo juu ya Mtume (s.a.w) ni "machafuko makubwa" na "vurugu" ambavyo havitaishia mahala pamoja bali vitaenea duniani kote.

Pia kuhusiana na swala hili maneno mengine ya Mtume yanasema: Ile saa itafika wakati vurugu, umwagaji damu na machafuko yatakapokuwa mambo ya kawaida. (Al-Muttaqi Al-Hindi, Muntakhab Kanzul Ummaal) Ulimwengu hautakoma mpaka zije enzi ambapo kutakuwa na mauaji makubwa na umwagaji mkubwa wa damu (Muslim).

Tukizitafakari Hadithi hizo, tunafikishwa katika hitimisho muhimu. Mtume (s.a.w) alielezea mitafaruku, fujo, mauaji na vita vitavyoikumba dunia nzima na kuenea kwa hali ya khofu na akabainisha kuwa matukio haya ni ishara ya Kiama. Tukiangalia katika karne 14 zilizopita, twaona kuwa vita vilikuwa vya Kinchi kabla ya karne 20. Hata hivyo vita ambavyo vimemuathiri kila mtu duniani, vilivyoathiri mifumo ya siasa, na mifumo ya uchumi na jamii, vimerindima zaidi katika nyakati za karibuni hususan katika vita kuu mbili za dunia.

Katika vita kuu ya kwanza ya dunia zaidi ya watu Milioni 20 walikufa, na katika vita kuu ya pili ya dunia, zaidi ya watu Milioni 50 waliuawa. Vita kuu ya pili ya dunia ndiyo inayotambuliwa kuwa ni vita iliyomwaga damu nyingi mno, iliyokuwa kubwa mno na iliyoleta maangamizi makubwa katika historia.

Teknolojia ya sasa ya Kijeshi ikiwa ni pamoja na Silaha za Kibaolojia, Kikemia na Nyuklia ndio iliyozidisha madhara ya vita katika kiwango ambacho hakijapata kutokea katika historia. Kutokana na silaha za maangamizi ambazo zimezidi kuboreshwa, inakubaliwa na wengi kuwa Ulimwengu hautaingia katika vita ya tatu ya dunia.

Migogoro ambayo imetokea baada ya vita kuu ya pili ya dunia, vita baridi, vita vya Korea, vita ya Vietnam, mgogoro wa Warabu na Waisrael vita vya Ghuba na Iraq ni miongoni mwa matukio mabaya sana ya wakati wetu. Hali kadhalika vita vya kieneo, migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe vimesababisha maangamizi makubwa katika sehemu nyingi za dunia. Katika nchi kama Bosnia, Palestina, Chechnya, Iraq, Afghanistan, Kashmiri na sehemu nyingine nyingi, matatizo haya bado yanaendelea kumkumba mwanadamu.

Mfano mwingine wa machafuko yanayomuathiri mwanadamu mithili ya vita ni Ugaidi unaoratibiwa kimataifa kama wanavyokubali viongozi wengi kuwa vitendo hivi vya Ugaidi vimeongezeka mno katika nusu ya pili ya karne ya 20. Kwa kweli yawezekana kusema kuwa Ugaidi ni jambo makhususi la karne ya 20.

Jamii zilizobobea katika ubaguzi, Ukomunist na Itikadi nyingine kama hizo au zenye malengo ya Utaifa zimeshiriki katika vitendo vya kinyama kwa msaada wa teknolojia ya leo. Katika historia ya karibuni tu, vitendo vya Ugaidi mara kwa mara vimeleta maangamizi. Damu nyingi imemwagika na watu wasio na hatia ama wamejeruhiwa au wameuawa lakini bado wanadamu hawajapata fundisho kutokana na matukio haya ya balaa. Katika nchi nyingi za dunia Ugaidi unaendelea kuwa msingi wa tawala na sera.

Kuna aya nyingi katika Qur'an zinazohusiana na jambo hili. Katika Surati Arum inaelezwa kuwa machafuko yameikumba dunia kwasababu ya yale ambayo watu wameyafanya kwa mikono yao:

Uharibifu umedhihiri barani na baharini kwasababu ya yale iliyoyafanya mikono ya watu ili awaonjeshe adhabu ya baadhi ya mambo waliyoyafanya, huenda wakarudi (wakatubia kwa Mwenyezi Mungu) (30:41). Hatuna budi kusema kuwa aya hii inatukumbusha ukweli muhimu sana. Machungu na Masahibu yanayotokana na makosa ya wanadamu yanatupa fursa ya kutanabahi na kuepuka kuyarudia.