DALILI ZA KIAMA

 
Utafiti wa anaga na uvumbuzi

Sura ya 54 ya Qur'an inaitwa "Surat al- Qamar." Kwa kiswahili qamar tafsiri yake ni mwezi. Katika aya kadhaa sura hii inatutajia maangamizi yaliyowafika watu wa Nuhu, Ad, Thamud, Lut na Firaun kwasababu walikadhibisha mawaidha ya mitume. Wakati huo huo katika aya ya kwanza ya sura hii kuna ujumbe muhimu sana unaohusiana na siku ya mwisho:
Saa (ya kufika kiama) imekaribia; na Mwezi umepasuka (54:1). "Neno kupasuka" lililotumika katika aya hii ni tafsiri ya neno Shaqqa, ambalo katika kiarabu lina maana mbali mbali. Miongoni mwa maana hizo ni kukatua, kulima au kuchimbua ardhi. Kutoa mfano wa hili tunaweza kurejea aya ya 26 ya suratil Al-Abasa: Hakika tumemimina maji kwa nguvu (kutoka mawinguni). Kisha tukaipasua pasua ardhi. Kisha tukaotesha humo (vyakula vilivyo) chembe chembe. Na mizabibu na mboga. Na Mizaituni na Mitende. (80:25-29).

Kwahiyo maana ya neno "Shaqqa" hapa ni kukatua, kuchimbua ardhi ili kuotesha mimea mbali mbali. Kama tutarejesha kumbukumbu zetu mwaka 1969, tutaona moja ya maajabu makubwa ya Qur'an. Majaribio yaliyofanywa mwezini mnamo Julai 20,1969 yaweza kuwa kielezeo cha kutimia kwa maneno yaliyosemwa miaka 1400 iliyopita katika Suratil Qamar.

Katika tarehe hiyo, wanaanga wa Marekani walikanyaga mwezini. Wakachimba udongo wa mwezini na kufanya uchunguzi wa Kisayansi walichukuwa sampuli ya mawe na udongo. Kwa kweli hili ni jambo lenye mvuto mkubwa kwani kitendo hiki kinawafikiana kabisa na maelezo yaliyotolewa katika aya hiyo ya 26. Kusisitiza hili ni kwamba wakati wa Mtume hakuna mtu aliyejua kama mwezini kuna udongo mithili ya ardhi. Kwahiyo kutumika kwa neno shaqqa lenye maana ya kuchimba, kuchimbua au kukatua kama lilivyotumika katika aya hiyo ya 26 kunathibitishwa na huo uchunguzi wa mwaka 1969 ambapo wanaanga waliokwenda mwezini walichimba udongo wa mwezini ndio kusema wameitimiza kwa vitendo aya hiyo ya Qur'an. Ndio maana tunasema hii ni moja ya maajabu ya Qur'an.

Wakati wanaanga hawa walipochimba udongo wa mwezini, walikusanya kilo 15.4 za sampuli ya mawe na udongo. Sampuli hizi zikaja kuvuta hisia za wengi. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la anga la Marekani, NASA hamasa iliyoonyeshwa na watu juu ya sampuli hizi ilivunja rekodi ya hamasa zote zilizooneshwa katika safari zao zote za angani za karne ya 20. Safari ya mwezini inaelezewa kwa kauli mbiu hii "hatua moja ndogo ya mtu mmoja ni mwendo mkubwa wa kuruka kwa wanadamu wote". Huu ulikuwa ni wakati wa kihistoria wa utafiti wa anga. Ni tukio lililochukuliwa na Kamera, na kila mtu kutoka wakati huo hadi leo amelishuhudia.

Kama ilivyoelezwa katika aya ya kwanza ya Suratil al- Qamar, tukio hili kubwa lenyewe pia laweza kuwa ishara ya siku ya mwisho. Yaweza kuwa ishara kuwa ulimwengu upo katika siku za mwisho kabla ya hukumu. (Allahu A'alam). Mwisho hatuna budi kuzingatia kuwa kuna onyo kubwa kufuatana na aya hizi. Kuna ukumbusho kuwa ishara hizi zinatoa fursa muhimu kwa watu kuacha mwendo mbaya na kwamba wale wasiozingatia onyo hili basi watapata fadhaa kubwa pale watakapofufuliwa siku ya hukumu ambayo katika Qur'an inaelezewa kama siku yenye huzuni isiyoelezeka:

Saa (ya kufika Kiama) imekaribia na Mwezi umepasuka. Na wakiona muujiza hugeukia upande mwingine na kusema uchawi tu unazidi kuendelea! Ndio wamekadhibisha hivi na wamefuata matamanio ya nafsi zao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti. Na kwa yakini zimewajia habari zenye makatazo makubwa. Zenye hikma kamili lakini maonyo kwao hayafai kitu. Basi jiepushe nao. Na wakumbushe siku atakapoita mwiitaji huyo kuliendea jambo zito (la kiama). Macho yao yatainama chini, wanatoka katika makaburi kama kwamba ni Nzige waliotawanyika, wanamkimbilia muhitaji huyo na huku wanasema hao makafiri: Hii ni siku ngumu kabisa. (54:1-8).

Miaka 1400 iliyopita Mtume Muhammad (s.a.w) alitoa bishara nyingi kuhusiana na siku za mwisho na akaelezea maono yake juu ya wakati huo kwa maswahaba wake. Maneno haya muhimu yamerithishwa kwa vizazi na vizazi hadi kufikia leo hii. Yamo katika vitabu vya hadithi na katika maandiko ya wanazuoni wa Kiislamu.

Hadithi ambazo tutazinukuu katika kitabu hiki zina bishara hizo zilizotolewa na Mtume (s.a.w). Labda yaweza kuzuka shaka kwa msomaji kuhusiana na ukweli na usahihi wa hadithi hizi zinazozungumzia mwisho wa dunia. Ni ukweli unaofahamika kuwa, huko nyuma kulikuwa na hadithi nyingi za kughushi ambazo zilidaiwa kuwa za Mtume (s.a.w) lakini hadithi zinazoelezea mada yetu hii zitatambuliwa kirahisi kuwa zilitoka kwa Mtume (s.a.w).

Kuna utaratibu wa kutofautisha hadithi sahihi na hadithi zisizo sahihi. Kama tujuavyo hadithi zinazozungumzia zama za mwisho zinahusiana na matukio yatakayotokea baadaye. Kwasababu hii pale hadithi inapothibiti kulingana na wakati, shaka zote juu ya chanzo chake huondoka.

Wanazuoni kadhaa wa Kiislamu waliofanya utafiti juu ya mada ya zama za mwisho na juu ya dalili za kiama wametumia kigezo hiki. Mwana taaluma wa fani hii, Ulamaa Bediuzzaman Said Nursi amesema kuwa ule ukweli kwamba hadithi zinazohusu zama za mwisho zimeshabihiana na matukio na mambo yaonekanayo katika zama zetu unabainisha ukweli wa hadithi hizo. Baadhi ya dalili zilizotajwa katika hadithi ziliweza kuonekana katika baadhi ya maeneo ya dunia katika wakati wowote ule wa historia ya miaka 1400 ya Uislamu.

Lakini hilo pekee lisingeliweza kuthibitisha kuwa kipindi hicho kilikuwa zama za mwisho. Ili kipindi kiitwe cha zama za mwisho basi zile dalili zote za siku ya mwisho lazima zionekane na zitokee katika kipindi hicho hicho. Hii inaelezwa katika hadithi: Dalili zinafuatana moja baada ya nyingine kama vile shanga za mkufu zinavyoanguka moja baada ya nyingine pale kamba yake inapokatika (Tirmidhi).

Tunapoziangalia zama za mwisho kwa kuzingatia maelezo yaliyotolewa hapo juu, tunaibuka na hitimisho la kuajabisha. Dalili ambazo Mtume (s.a.w) alizielezea kwa kina zinatokea, hivi leo moja baada ya nyingine katika kila pembe ya dunia kama vile vile zilivyoelezwa. Kwahiyo hadithi moja kwa moja zinatoa picha kamili ya wakati wetu. Huu kwa hakika ni muujiza unaohitaji mazingatio makubwa sana. Kila dalili inayotokea inawakumbusha watu kuwa zama za mwisho zimekaribia, ile siku ambayo watu watatoa wenyewe hesabu ya amali zao mbele ya Mwenyezi Mungu. Hivyo basi watu wanapaswa kurejea upesi upesi katika maadili ya Qur'an.