DALILI ZA KIAMA

 
Kurudi kwa Nabii Isa duniani.

Isa au Yesu (a.s) ni Mtume aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu. Ni mmoja kati ya Mitume wanaozungumziwa sana katika historia ya dunia. Al-hamdulillahi kipo chanzo ambacho kwacho twaweza kupembua kipi sahihi na kipi si sahihi katika yale yaliyozungumzwa juu yake. Chanzo hicho ni Qur'an, kitabu pekee cha ufunuo ambacho hakija badilishwa wala kuhujumiwa.

Katika Qur'an tunasoma ukweli huu kuhusu Nabii Issa:
Masihi Issa bin Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni tamko lake (4:171) Kumbukeni waliposema Malaika: Ewe Maryam! Mwenyezi Mungu anakupa habari njema za neno litokalo kwake (la kukwambia 'zaa' utazaa). Jina lake ni masihi, Issa, mwana wa Maryam, mwenye heshima katika dunia na akhera, na ni miongoni mwa waliopelekwa mbele na Mwenyezi Mungu. (3:45)

Na (mtaje yule mwanamke) aliyejilinda, (aliyejihifadhi) nafsi yake, na tukampulizia Roho yetu na tukamfanya yeye na mwanaye kuwa miujiza kwa walimwengu (21:91). Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utu uzima wake na atakuwa katika watu wema (kabisa) (3:46). Issa (Yesu) alifanya miujiza kadhaa. Muujiza mwingine atakaofanya ni kuwa atarudi tena duniani katika siku za mwisho na atazungumza na watu.

Kisha tukawafuatisha nyuma Mitume wetu na tukamfuatisha Issa bin Maryam na tukampa Injili (57:27). Bila shaka wamekufuru wale waliosema, Mwenyezi Mungu ni Masihi (Issa) bin Maryam (5:72). Na makafiri (Mayahudi) walifanya (hila dhidi yake ili kumuua) na Mwenyezi Mungu akazipindua hila zao na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupindua hila (3:54).

Mwenyezi Mungu hakuacha Makafiri wamuue Issa/Yesu (a.s.), bali alimtowesha na akatoa habari njema kwa walimwengu kuwa siku moja atarudi tena duniani. Qur'an inatoa maelezo ya kurejea kwa Issa kwa ishara zifuatazo:
Na kwa ajili ya kusema kwao: Sisi tumemuua Masihi Issa Mwana wa Maryam Mtume wa Mungu hali hawakumuua wala hawakumsulubu bali walibabaishiwa (mtu mwingine). Na kwa hakika wale waliohitilafiana katika suala hilo wamo katika shaka. Hawana yakini kabisa juu ya jambo hili ispokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua (4:157)

Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mwenye hekma (4:158). Katika aya ya 55 ya suratil Al- Imran, tunasoma kuwa Mwenyezi Mungu atawaweka juu ya makafiri wale watu wanaomfuata Issa hadi siku ya kufufuliwa. Ni ukweli wa kihistoria kuwa, miaka 2000 iliyopita wafuasi wa Issa hawakuwa na nguvu za kisiasa. Wakristo ambao wameishi enzi hizo na ambao wanaishi zama hizi wameamini itikadi nyingi potofu. Kubwa kuliko zote ni Itikadi ya Utatu.

Hivyo ni wazi kuwa hawataweza kuitwa wafuasi wa Issa kwani kama inavyoelezwa katika Qur'an, wale wanaoamini Utatu wametumbukia katika upotofu. Kwa hali hiyo katika kipindi hicho cha kuelekea kiama, wafuasi halisi wa Issa watawashinda wapotevu na wao ndio watakaotimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyotolewa katika Suratil-Al Imran. Bila shaka kundi hili tukufu litajulikana pale Issa atakaporudi tena duniani. Isitoshe Qur'an inasema kuwa watu wa kitabu wote watamuamini Issa kabla hajafa:Na hakuna yeyote katika watu waliopewa kitabu ila humuamini Issa kabla ya kifo chake. Naye siku ya kiama atakuwa shahidi juu yao (4:159). Tunasoma wazi wazi katika aya hizi bado kuna ahadi tatu zinazomuhusu Issa ambazo bado hazijatimia. Kwanza kama walivyo binadamu wengine, Issa (a.s) atakufa. Pili Watu wote wa kitabu watamuona katika umbile lake la mwili na watamtii wakati akiwa hai. Hapana shaka kuwa biashara hizi mbili zitatimizwa pale Issa atakaporudi tena kabla ya siku ya mwisho. Bishara ya tatu juu ya Issa (a.s) kuwa shahidi juu ya watu wa kitabu, hiyo itatimizwa siku ya mwisho.

Aya nyingine katika Suratil Maryamu inaelezea kifo cha Issa (a.s): Na amani ipo juu yangu siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa (19:33). Tunapoilinganisha aya hii na aya ya 55 ya suratil Al-Imran tunaweza kubaini ukweli muhimu sana. Aya ya suratil Al-Imran inazungumzia kunyanyuliwa kwa Issa. Katika aya hii hakuna taarifa inayotolewa kuwa Issa alikufa au la. Lakini katika aya ya 33 ya Suratil-Maryam, kifo cha Issa kinazungumziwa. Kifo hiki kitatokea pale Issa atakaporudi tena duniani na kuishi kwa muda fulani na kisha kufa (Allah ndiye ajuaye).

Aya nyingine inayoelezea kurejea kwa Nabii Issa (a.s) Duniani inasema:
Na (Mwenyezi Mungu) atamfunza (Isa) kitabu na kujua elimu na kujua Taurati na Injili. (3:48). Ili kuelewa maana ya kitabu ambayo imetajwa katika lugha ya Kiarabu katika Aya hii, lazima tuziangalie aya nyingine za Qur'an ambazo zinahusiana na suala hili. Iwapo kitabu kinatajwa pamoja na Taurati na Injili katika aya moja, basi hiyo lazima iwe na maana kuwa kitabu hicho ni Qur'an. Aya ya tatu ya Suratil Al-Imrani yaweza kuwa mfano wa jambo hilo:
Mwenyezi Mungu, hakuna aabudiwaye kwa haki isipokuwa Yeye - Mwenye uhai wa milele, na mwendeshaji wa mambo yote. Amekuteremshia kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili zamani - ziwe uongozi kwa watu. Na akateremsha vitabu vingine vya kupambanua baina ya haki na Batil. (3:2-4).

Kwa hali hiyo kitabu kilichozungumziwa katika aya ya 48 ambacho Nabii Issa (a.s) anatakiwa kujifunza ni Qur'an tu. Tunajuwa kuwa Nabii Issa aliijuwa Taurati na Injili katika kipindi alichokuwa duniani ambacho ni takribani miaka 2000 iliyopita. Ni dhahiri kabisa kuwa ni Qur'an atakayoisoma pale atakaporudi tena duniani. Maelezo yanayotolewa na aya ya 59 ya Suratil Al-Imrani yanaonesha usawa baina ya Issa na Adam (a.s):

Bila shaka hali ya Issa kwa Mwenyezi Mungu ni kama hali ya Adam, alimuumba kwa udongo kisha akamwambia kuwa basi akawa. Katika aya hii twaweza kuona kuwa lazima viwepo vigezo vingi vya usawa baina Manabii hawa wawili. Kama tujuavyo, Adam na Issa (a.s.) wote wawili hawakuwa na Baba. Pia twaweza kupata usawa mwingine zaidi kutokana na aya ya hapo juu ambao ni kushuka kwa Nabii Adam ardhini akitokea peponi na kushuka kwa Nabii Issa kutoka alikohifadhiwa na Mwenyezi Mungu katika zama za mwisho. Qur'an inasema hivi kuhusu Issa:

Na kwa kweli (Issa) ni alama ya kiama, msikifanyie shaka na nifuateni. Hii ndio njia iliyonyooka. (43:61). Tunajuwa kuwa Nabii Issa aliishi karne sita kabla ya Qur'an kushushwa. Kwa hiyo aya hii haizungumzii kipindi cha kwanza cha maisha yake bali inazungumzia kuja kwake tena duniani katika zama za mwisho mwisho. Ulimwengu wa Kiislamu na wa Kikristo kwa pamoja unamsubiri kwa hamu Nabii Issa. Ujio mtukufu wa mgeni huyu utakuwa ishara muhimu ya siku ya mwisho.

Aidha ushahidi mwingine zaidi wa kurudi kwa Nabii Issa unabainishwa na neno la kiarabu, Wakahlan katika aya ya 110 ya Suratil Maida na aya 46 ya Suratil Al-Imran. Katika aya hizi tunabainishiwa haya:

Mwenyezi Mungu atakaposema: Ewe Issa Mwana wa Maryam! Kumbuka Neema yangu juu yako na juu ya Mama yako, nilipokusaidia kwa roho takatifu (Jibril), ukazungumza na watu katika Utoto wako na katika utu uzima wako (Wakahlan) (5:110). Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utu uzima wake na (atakuwa) katika watu wema (kabisa) (3:46).

Neno hili (Wakahlan) linajitokeza katika aya hizi mbili tu na linamzungumzia Issa peke yake. Neno hili limetumika kuelezea umri mkubwa zaidi wa Issa. Neno hili linazungumzia makamo baina ya miaka 30 na 50 ambacho ni kipindi cha mwisho cha ujana na mwanzo wa utu uzima. Wanazuoni wa Kiislamu wameafikiana juu ya tafsiri ya neno hili ambayo ni kipindi kinachovuka umri wa miaka 35.

Wanazuoni hawa wanaegemea hadithi iliyosimuliwa na Ibni Abasi inayosema kuwa Issa (a.s) alinyanyuliwa kwa Allah wakati alipokuwa kijana yaani mwanzoni mwa miaka ya 30 na atakaporudi tena duniani atakuwa na miaka mingine 40 ya kuishi. Issa(a.s) ataendelea kuishi hadi uzeeni baada ya kurudi duniani, hivyo basi aya hii yaweza kuchukuliwa kama ushahidi wa kurejea tena kwa Issa (a.s) duniani.

Kama ilivyokwishaelezwa, tunapoiangalia Qur'an kwa makini, tunaona kuwa neno hili Wakahlan limetumika kumuelezea Issa tu. Manabii wote wamezungumza na watu na kuwalingania kufuata dini moja sahihi. Wote kati yao walileta ujumbe wakiwa na umri mkubwa. Lakini Qur'an haisemi chochote kuhusiana na jambo hilo juu ya Mtume mwingine yeyote. Neno hili limetumika kwa Issa (a.s) tu na huu ni muujiza.

Misemo hii miwili, "katika utoto wake" na katika "utu uzima" inagusia miujiza miwili mikubwa. Muujiza wa kwanza ni kuwa Issa alizungumza wakati akiwa mtoto mchanga. Hili ni jambo ambalo halikuwahi kutokea hapo kabla na Qur'an inalielezea tukio hili la kimiujiza mara kadha wa kadha. Mara baada ya maneno haya kuzungumza na watu utotoni yanafuata maneno kuzungumza na watu katika utu uzima. Maneno haya pia yanaelezea muujiza. Kama maneno katika utu uzima yangezungumzia maisha yake ya awali kabla hajatoweshwa na Allah, kusema kwa Issa kusingelikuwa muujiza.

Na kwa vile usingekuwa muujiza basi usemi huu usingelitumika baada ya ule usemi wa kuzungumza katika utoto au kwa namna ya kuelezea muujiza. Kwa hali hiyo ule usemi wa "katika utoto" hadi katika "utu uzima" ungetumika na ungeelezea umri wa Issa tokea pale alipoanza kusema utotoni hadi pale aliponyanyuliwa kwa Mwenyezi Mungu.

Lakini aya inatutaka tuzingatie matukio mawili makubwa ya kimiujiza. La kwanza ni lile la kuzungumza katika utoto na lingine ni lile la Issa kuzungumza katika umri wa utu uziama. Hivyo basi usemi huu wa utu uzima una maana kuwa wakati ambao utakuwa ni muujiza. Nao ni ule wakati ambapo Issa atazungumza na watu katika umri wa utu uzima baada ya kuwa amerudi tena duniani. (Allahu A'alam).

Katika hadithi za Mtume (s.a.w) kuna habari ya kurudi tena kwa Issa (a.s). Katika hadithi chache habari hii inazungumzwa na habari juu ya kile ambacho Issa (a.s) atakifanya pale atakapokuwa duniani. Yafaa kumkumbusha msomaji juu ya jambo moja muhimu sana. Kwamba Mwenyezi Mungu alimtuma Mtume Muhammad (s.a.w) kwa Walimwengu wote akiwa kama Mtume wa mwisho. Mwenyezi Mungu alimfunulia Qur'an Mtume Muhammad (s.a.w) na kuwataka watu wote wafuate mafundisho ya Qur'an hadi siku ya hukumu.

Issa (a.s) atarudi tena kimiujiza duniani katika zama za mwisho lakini, kama alivyosema Mtume (s.a.w), hatoleta mafundisho mapya. Dini sahihi ambayo Mitume wote wamefundisha ni Uislamu ambayo Isa atapaswa kuifuata pale atakaporudi duniani. Katika Qur'an na katika Hadithi hakuna utata kuwa Issa (A.S) atarudi tena duniani katika zama za mwisho. Baada ya Waislamu kusema kuwa yumkini Isa (A.S) atarudi tena Duniani, na Mumammad (S.A.W) ni mtume wa mwisho, hakuna mpingano kati ya mambo haya mawili; Muhammad kuwa Mtume wa mwisho na Issa kurudi tena Duniyani.

Pale Issa atakaporejea kwa mara ya pili, hatoleta Dini mpya, bali atafuata yaleyale aliyofundisha Mtume Muhammad (S.A.W), Qur'an na Sunnah. Al-A'llama Imam Rabbani anasema ; "Issa (A.S) atashuka toka mbinguni , lakini atafuata njia ya Muhammad". [Imam Rabbani, Vol.11, Letter 67].

Imam Nawawi kasema Isa (A.S) atarejea na kufuata njia ya Muhammad (S.A.W). [Al-Qawl al-mukhtasar fi a'llamat al-Mahd al-Muntanzar]. Qadi Lyad nae kasema; Isa atatawala kwa sheria aizopewa Muhammad na atahuisha mambo ambayo watu wake waliyatelekeza. [Ibin Majah].

Mwanazuoni mkubwa wa karne iliyopita Bediuzzaman Said Nursi ametoa ufafanuzi muhimu juu ya suala hili katika kitabu chake Risalel Nnuur Collection. Kwa mujibu wa ufafanuzi wake, Isa (A.S) atarudi tena Duniani katika zama za mwisho, na atazihamisha itikadi zinazopingana na Uislamu. Chini ya uongozi wake, Wakristo watasilimu, Nguvu kubwa ya wapinzani wa Dini ya Haki itaondoshwa kabisa, imani za kipuuzi zitaondoshwa, na ulimwengu utafuata Qur'an. Labda swali muhimu linalotarajiwa kuulizwa ni je, Isa atatambuliwa namna gani? Au ni sifa gani zitakazowawezesha watu kumtambua Issa?

Jibu ni kuwa, atakuwa na dalili zote za Utume zilizotajwa katika Qur'an. Mbali na hivyo, atakuja na ishara zinazomthibitisha kuwa yeye ndiye Masihi Isa Bin Maryamu. Wakati atakapokuja hapatakuwa na hata mtu mmoja ambaye alipata kumuona hapo kabla. Ndio kusema hakutakuwa na mtu hata mmoja atakayemtambua. Hakuna atakayeweza kumtambua kwa haiba wala sauti yake. Hakuna atakayeweza kusema kuwa yeye alimjua hapo kabla kwa kiwiliwili chake au alimwona mahali fulani na hakutakuwa na hata mmoja aliyeiona familia au nduguze ili kuweza kumfananisha.

Wale wote waliomjua walikwishakufa miaka 2000 iliyopita. Maryamu(a.s), Zakariya(as), Wanafunzi(wafuasi) wake walioishi naye kwa miaka miwili ya ujumbe wake pamoja na wale wote waliokuwepo wakati wake walikwishakufa. Kama tulivyofafanua katika kurasa za mbele, kwa amri ya kun fayakun ya Mwenyezi Mungu, Isa aliweza kuja duniani bila baba. Mwenyezi Mungu anamfananisha Isa na Adamu katika aya hii:
Bila shaka hali ya Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama hali ya Adamu; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia "kuwa", basi akawa(3:59).

Ayah hii inabainisha kuwa Mwenyezi Mungu alisema "kuwa" Adamu akawa na Isa pia akawa kwa nyakati tofauti. Adamu hakuwa na mama wala baba wakati ambapo Isa hakuwa na baba lakini alikuwa na mama. Lakini akirudi tena duniani mama yake hatokuwa hai. Hivyo basi, ule ubabaishaji utakaokuwa umefanywa na Masihi wa uongo zama hata zama hautakuwa na hautaleta utatanishi. Hakutakuwa na shaka Isa kama ni yeye au la. Hakuna atakayepata kisingizo kusema huyo sio Isa(a.s). Kwa kumalizia hapa ni kwamba maelezo yote yaliyotolewa yatupelekee kutanabahi kuwa muda au miadi kuhusu kurudi tena kwa Yesu duniani na mambo atakayoyafanya, hauko mbali. Ahadi ya kurejea kwa Isa iwe changamoto kwetu ya kujiandaa kukutana naye.