MUANDAMO WA MWEZI

 

MUANDAMO WA MWEZI


MAZUNGUMZO BAADA YA KHABARI KUHUSU MUANDAMO WA MWEZI-SAYARI
Mazungumzo na wanafunzi wa Sheikh Nassor Bachoo juu ya suala la mwezi muandamo.
Muandishi:
Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui, Al-Zenjibari.
UTANGULI


, .


Baada ya hayo, sina budi kutoa shukurani na pongezi zangu za dhati kwa juhudi kubwa iliofanywa na ndugu zetu wa "Ansaru Sunna" Zanzibar kwa kutunga kitabu chao kujibu kitabu changu kuhusu miandamo ya mwezi. Mnamo mwezi Rajab, nilitumiwa meseji na mmoja wa ndugu zetu wa Zanzibar akiniambia "Je unajua kuwa kitabu chako cha mwezi kimejibiwa?" Nikamwambia sijui kwani sijaletewa kopi. Mara juzi tarehe 2/8/2009, nikajuilishwa na mmoja wa ndugu hapa Oman kuwa kitabu kimetumwa as soft copy katika E-Mail box yake. Kwa hivyo, nikafanya bidii ya kukipata ili nipate faida ya kile nisichokijua. Kwa bahati nilipokisoma sikuona kitu chochote cha kielimu, wala sikuona kwamba wameweza kuthibitisha dai lao kwamba muandamo mmoja ni hoja kwa walimwengu wote. Bali kilichokuwemo ni "Juma kafanya hivi; Juma kasema hivi". Kwa kweli, kwa habari nilioletewa kotoka Zanzibar ni kuwa waliowengi wanasema kuwa hawakuweza kujibu hoja za kitabu chetu UshahdiUuliowekwa Wazi. Lakini nami nasema kwamba wamejitahidi kadiri ya uwezo wao: kila ndege huruka kwa ubawawe.

Kasoro nyengine kubwa zilizomo katika kitabu chao ukiwacha kukosekana kwa mada ya kielimu ni:
1) Tadlis Kughushi. Mara nyingi wamekuwa wakitumia njia mbali mbali kuyaghushi maneno yangu na maneno ya wanavyuoni kama mutavyoona humu. Katika kufanya hivyo, kwa mfano:
a) Huchukua sehemu ndogo ya maneno yangu ambayo haileti maana kamili halafu ndio wakajibu bila ya msomaji kuweza kujua hoja gani hasa nilitoa.
b) Wakati mwengine hunukuu sehemu ya maneno yangu na kuondosha sehemu nyengine; maana ikafisidika. c) Kuhusu maneno ya Maulamaa pia wamefanya hivyo hivyo.
Jambo hili linanipa masikitiko na kuona kwamba labda watu hawa hawakukusudia kutafuta haki bali wamekusudia kuitetea rai fulani wanayoiamini. Hata hivyo, napenda kuwashukuru kwamba 90% ya kitabu chao kimeandikwa kwa lugha nzuri, sehemu moja moja wameteleza. Tunawapa udhuru, kwani ni vigumu mtu kuweza kuwacha hamasa 100%.


2) Kasoro ya pili ya kitabu chao: ni kutokujua wakisemacho. Hili lina picha tatu:
a) Wamenukuu maneno ya wanavyuoni, kisha wakayakoroga katika kuyafasiri kwa Kiswahili: hata maana yake kwa Kiswahili imewashinda. Sasa watu kama hawa vipi wanathubutu kujadili mambo ya elimu.
b) Wananukuu kanuni za Kiusuli kisha hawajui pa-kuziweka. Mara nyengine hunukuu kanuni iliodhidi yao; wao wanaitolea hoja hawajui kwamba maana ya kanuni hio inawapinga wao.
c) Wanaweza kukulaumu kwa kitu kisha kitu kisha na wao wakakifanya kile kile.
3) Tatu: ni kuwa sehemu kubwa ya kitabu changu hawakuweza kuijadili hata kwa hayo majibu yao dhaifu. Kwa hivyo, kimsingi kitabu kimewashinda.
4) Nne: ni kuwa hawajui Qias kinafanywa vipi na wakati gani, kwa hivyo utaona wanahoji kwa hoja ambazo hata wanavyoni hawazitaji kamwe.


5) Tano: ni kukariri kitu hicho kwa hicho mara baada ya ntyengine. Jambo hili likifanya kitabu kikose utunzi wa kitaalamu. Kwa hivyo, na mwenye kujibu hulazimika kukariri jawabu.
6) Sita: ni kuwa unapowapa hoja ya kielimu iliojengeka katika misingi ya fani za elimu na wakawa hawana jawabu ya kuijibu husema: "Lazima yatolewe madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni wenye kutegemewa". Na utaponukuu maneno ya wanavyuoni kuunga mkono hoja yako husema: "Kutegemea maneno, matupu ya mwanachuoni kama ni Khaas () bila ya kuonyesha dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa ni udhaifu".

7) Saba: ni kuwa wanapotaka kukipinga kitu ambacho hawakitaki nao hawana hoja, husema hili hukulinukuu kutoka kwa "Wanavyuoni wenye kutegemewa"; wakitaka kuthibitisha wao jambo lao hunukuu mpaka maneno ya watu ambao hawakufika hata daraja ya uwanafunzi katika istilahi za kielimu.
8) Nane: ni kuwa jambo wasillolijua husema hakuna mwanachuoni aliyesema hivyo, ilhali wanavyuoni wamejaa waliosema hivyo. Yote haya yanaonesha kwamba wamekiingia kitu wasichokijua.
9) Tisa: ni kuwa kitabu chao chote hawakujadili mambo yenye maana, bali huchagua vile vipengele visivyo na umuhimu ndio wakajadili. Hizi ni baadhi ya kasoro kubwa za jawabu yao hio. Mimi nilitarajia kwamba katika kitabu chao watajadili mas-ala yenye maana. Lakini hatimae nakuta mambo kama kwanini nimesema "Vuta-nikuvute" na mfano wa hayo. Ilhali wale wakuu wetu wote hutumia lugha hizo katika vitabu vyao. Husomi kitabu cha fiq-hi au tafsiri au lugha ila utakuta maneno kama Maulamaa wamevutana, au wamesukumana, na mfano wa hayo. Na zote ni ibara zenye kumaanisha kuwepo kwa ikhtilafu kubwa tu: si kwamba waligombana au kupigana.


Hadi sasa ninapoandika jawabu hii, sijapata hard copy. Kwa hivyo, nitapowanukuu ndugu zangu sitoweza kuweka nambari ya ukurasa. Jawabu hii ni mukhtasari wa jawabu pana tutayoitayarisha katika mfumo wa kitabu baada ya kupata hard copy ya kitabu cha ndugu zetu. Kwa hivyo, kwa sasa ikiwa wana jawabu juu ya haya nitayosema humu, basi wasifanye haraka kuichapisha kwa vile nitatoa kitabu ambacho natarajia kwamba kitakuwa na ziada baada ya kupata kitabu chao na mimi kunafasika zaidi na ambacho yako mengi yaliojikariri humu katika kitabu nitayaondoa.


Kwa ajili ya faida ya ziada, jawabu hii nimekigawa sura mbili:
1) Sura ya kwanza nitanukuu makala ya Sheikh wa Mombasa juu ya suala hili la muandamo wa mwezi na jawabu yangu kwake.
2) Sura ya pili ndio tutazama mazungumzo yetu mimi na ndugu zangu wa Ansari wa Zanzibar. Natumia lugha "Mazungumzo" kwa vile sehemu kubwa ya kitabu chao haina hoja za kielimu: ni mazungumzo ya kawaida tu. Na mimi nilikuwa nasita: je nijibu hiki kitabu au nikiwache na kuwaacha watu wasome kitabu changu Ushahidi Uliowekwa Wazi na Kitabu chao pamoja na cha Sheikh Bachoo halafu watu walinganishe hoja tu? Nilitaraddad baina ya rai hii na hile kwa vile hoja za msingi ni zile zile hata tukiandika vitabu mia. Yanayozidi huwa ni mambo ya kushutumiana na kuongezea hoja ndogo ndogo. Hatimae nikaamua kuwajibu si kwa lengo la kufikisha risala kwa wasomi na watu wenye fahamu sahihi; bali kwa ajili kwamba wako watu wenye fahamu kama zao ni lazima twende kwa mujibu wa fahamu zao.


Na kwa sababu hio, naendelea kushindwa kuipa jawabu hii jina jina lenye kuonesha kuwa ni kitabu cha kielimu? Kukipa jina la kielimu kitabu chenye kujadili hoja za mitaani kinawafanya watu wakuone huna maana. Kwa hivyo, jina nililohisi linafaa jawabu hii ni kuiita :
MAZUNGUMZO BAADA YA KHABARI: KUHUSU MUANDAMO WA MWEZI-SAYARI.
Kwa kweli kama ndugu zetu walitafakari na kuijua nafasi yao ya elimu, basi wasingelipoteza wakati wao. Hawaoni hawa kwamba hata Saudia ilikuwa zamani na msimamo kama huo wao. Lakini baada ya kukutana kwa wanachuoni wao wakubwa akiwemo Sheikh Bin Baz na Sheikh Ibn Uthaimin na bodi ya wanachuoni wakuu wa huko, waligundua kwamba msimamo huo ni makosa na sahihi ni kuwa kila watu wafate muandamo wao. Jambo hili lilitaka liwape ndugu zetu mazingatio kwani:
1) Wale wa Saudia ni Maulamaa; wakati hawa hakuna hata aiyefikia daraja ya talib 'ilmi (mwanafunzi) kwa mujibu wa istilahi za kielimu.
2) Wanachuoni wa Saudia walitoa uamuzi huo baada ya kukutana wanachuoni hao wakazungumza kwa pamoja: haikuwa fikra ya mwanachuoni mmoja. Na hili linaifanya kauli iwe na nguvu. Nataka kusema kwamba suala zima la kufata muandamo wa mwezi, hoja yake ya msingi ni kuzielewa Hadithi mbili tu; nazo ni Hadithi isemayo: "Fungeni kwa kuuona mwezi" na Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas. Basi hizi ndio dalili mama za kujadiliwa: yaliobaki ni maelezo, sherehe na shubuhati. Kwa hivyo, mwisho wa kitabu hiki, nitajaribu nifanye mukhtasari juu ya vipi tunaweza kuzifahamu hadithi hizi, na natarajia kwamba kwa anayetaka kufahamu atafahamu.


Pia utaona kwamba mimi katika jawabu hii, sikuacha hata kipengele chao kimoja ila nimekijibu, wakati ndugu zetu hawakuweza kukijibu asilimia kubwa ya kitabu changu. Na hili linaonesha kwamba wanajilazimisha tu fikra fulani japokuwa ni fikra dhaifu kielimu. Katika jawabu hii, nitatumia neno "Munasema" kumaanisha nakala ya maneno yao; na neno "Jawabu" kumaanisha jawabu yangu kwao. Ahsantum Ndugu yenu katika dini Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui, Al-Zenjibari.