MAHOJIANO BAINA YA MLAHIDI NA IMAMU JA'FAR SADIQ (A.S.)
|
|||||
|
MLAHIDI:
Sasa nijulishe kuhusu watu wanaoamini kuwa roho ya mtu huingia katika mwili mwingine mtu afapo. Juu ya msingi gani wanaithibitisha imani yao?
IMAMU:
Wale wanaoamini kuingia kwa roho ya mtu katika mwili mwingine, wameipuuza misingi yote ya dini, na wamejivika dhana zisizokuwa za kweli. Wanafikiri kuwa mbingu i tupu, na hakimo kitu cho chote ndani yake ambacho chaweza kuelezwa maana yake; na kwamba Mola wa dunia hii yu kama kiumbe. Wanasema kuwa chanzo cha hoja yao inatokana na dai la watu wasemao kwamba Mwenyezi Mungu amemwumba Adamu kwa mfano wa "mwili" wake. Wao hawaamini kuwepo kwa Pepo, Moto, Kiyama n.k. Kufuatana na itikadi yao, "Kiyama" maana yake ni kuingia kwa roho ya mtu aliyekufa katika mwili mwingine. Ikiwa mtu alifanya vitendo vizuri katika mwili wake zamani, basi roho yake itaingia katika mwili mzuri zaidi, na atapata hadhi kubwa katika maisha. Ikiwa amefanya vitendo viovu katika mwili wake wa zamani, au hakujua cho chote, basi roho yake itaingia katika miili ya wanyama, na atabaki katika hali mbaya. Hawaamini kufunga, kusali n.k. Wanapenda kujua yale tu yaliyo muhimu kwao. Kujitosheleza na tamaa zao za kidunia kunaruhusiwa kwao. Katika jambo hili, hawataona dhara lo lote ikiwa watazini na mwanamke ye yote wanayempenda hata akiwa ni dada, mabinti, mashangazi na wanawake walioolewa. Vile vile, inaruhusiwa kwao kula (au kunywa) mizoga, ulevi, damu n.k. Vitu hivi vinakatazwa na watu wote. Watuw enye dini wanawalaani. Na wanapotakiwa wathibitishe msingi wa msimamo wao wanafadhaika na kubabaika. Torati inakana madai yao, na Qurani inawalaani. Mbali na mambo haya, vile vile wanadhani kuwa Mwenyezi Mungu hutoka katika mwili mmoja na kuingia mwili mwingine, na kwamba roho zote ni za azali (hazina mwanzo wala mwisho). Wanasema kuwa roho hiyo hiyo ya Adamu bado inatoka mwili mmoja na kuingia mwili mwingine. Kwa hivyo, ikiwa Mwumba ni kama kiumbe chake, basi vipi inawezekana kusemwa kuwa mmoja wao ni mwumba wa wingine? Vile vile, wanasema kuwa malaika ni wazao wa Adamu (a.s.), na yule mwenye kujipatia hadhi kubwa katika dini yake baada ya kuzipita daraja za mitihani, huwa malaika. Kwa baadhi ya mambo wanaelekeana na Wakristo, na kwa mambo mengine wanaelekeana na wenye kumkana Mungu. wanasema kuwa vitu havina uhakika. Hivyo, hawali cho chote chenye nyama. Kwa kufuatana na imani yao, wanyama ni wazao wa Adamu, lakini wameyabadili maumbo yao. Kwa hivyo, hawali nyama zinazohusiana ambazo zimeharamishwa kwao. MLAHIDI:
Kuna kikundi cha watu wasemao kuwa Mwenyezi Mungu ni wa azali, na kitu kinachochakaa pia kilikuwa pamoja Naye tangu azali. Mwenyezi Mungu hana uwezo wa kujiondolea kitu kichakaacho. Kwa sababu hiyo, wanasema kuwa Mwenyezi mungu mwenyewe amejiambatanisha nacho na anaingia kwacho. Mwenyezi Mungu ameumba ulimwengu mzima kutokana na kitu hicho.
IMAMU:
Mwenyezi Mungu atukuzwe! Vipi Mwenyezi Mungu ambaye ni Mwenye Uwezo asiwe na uwezo wa kujiondolea kitu? Ikiwa kitu kilikuwa kihai na cha azali, ina maana kuwa palikuwepo vitu viwili vya azali, ambavyo viliungana na vikaupanga ulimwengu. Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa, basi kifo kimetoka wapi? Ikiwa kitu hakina uhai, basi kwa huko kutokuwa nao, hakuwezi kuwa pamoja na mwenye kuwa wa azali. Uhai hauwezi kutoka pasipokuwa na uhai. Hii ni imani ya wale makafiri wabaya kabisa. Wao wanaendelea kufuata maandiko ya mababu zao na kuyakariri kwa ujinga na bila ya kufikiri. Hawawezi kuthibitisha yale wanayoyadai. Yote haya yameazimiwa kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuwakana. Wapo watu wasemao kuwa miili ni giza na roho ni nuru; baya halitoki kwenye nuru, na giza haliwezi kufanya zuri lo lote. Hivyo, si barabara kumlaumu mtu ye yote kwa ajili ya dhambi yake. Giza lenyewe halina kosa, kwa sababu ni kitendo chake; wala Mwenyezi Mungu asinyenyekewe, kwa sababu Nuru ni Mola, na Mola hajinyenyekei wala hamtaki mtu amtii. Hakuna mtu ye yote katika kikundi hicho mwenye haki ya kumwambia mwenziwe kwamba fulani amefanya zuri au baya, kwa sababu ubaya ni sifa ya giza. Kadhalika, uzuri ni sifa ya nuru, na nuru haiwezi kusema kuwa ni mtenda zuri na imefanya kitendo kizuri na kwamba hakuna mtendewa. Vile vile, kufuatana na imani yao, giza ni huru katika vitendo vyake, na imara katika mpango wake, na yenye nguvu zaidi kuliko nuru, ilivyokuwa miili ni mizima na madhubuti.
Hivyo, yule aliyeumba juu ya msingi, ingawa katika umbo tofauti, lazima awe Mwenyezi Mungu. Kila kitu ambacho chaweza kuonekana kama miti, matunda, ndege, wanyama n.k., lazima kiwe Mungu, kw sababu kimehusika na nuru. Ni maneno matupu wanapodai kwamba nuru itamiliki mwishowe. Wanasema kuwa nuru haiwezi kufanya kitendo cho chote, imejifunga, haina nguvu na haitaharuki. Kama nuru ingekuwa na nguvu sawa na giza, ingeweza kujifunga. Ingekuwa huru na yenye nguvu. Hivyo, kama haina uhuru na nguvu ila tu imefungika katika giza, basi mazuri na mema yanachanganyika pamoja na mabaya na maovu katika dunia hii. Kwa hivyo, ina maana kuwa giza linazaa mazuri pia, kama linavyozaa mabaya. Kwa maneno mengine, giza ni mwumba wa mazuri na mabaya. Ikiwa wanasema kuwa haimkiniki, basi haithibitiki giza wala nuru. Hivyo, madai yao hayafai. Kwa hivyo, mwisho wake ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja tu, wala kitu chochote kingine ghaira Yake hakina uhakika. Maani kafiri mkubwa, pamoja na wafuasi wake waliokuwa na fikira hizo. Wanaposema kwamba zaidi ya nuru na giza, kuna nguvu ya tatu yenye kuamua; basi hapana shaka kuwa nguvu ya tatu ni kubwa kuliko hizo mbili, kwa sababu wenye kudhiliwa, wajinga na wanaoonewa huomba msaada wa mwenye kutawala. Haya ni yale wanayoamini wafuasi wa Maani, na hadithi yao ni ndefu. MLAHID:
Nini habari ya Maani?
IMAMU:
Maani alifuata mafundisho ya Majusi, na katika baadhi ya mambo alikubaliana na Wakristo; hivyo, yalikuwa ni mchanganyiko wa makosa, naye hakuweza kufahamu hata dini moja. Aliamini kuwa ulimwengu umeumbwa na miungu miwili - nuru na giza; na kwamba nuru ipo katika kifungo cha giza. Wakristo wanakana itikadi hii, na Mamajusi wanaikubali
MLAHID: Ni nani Mamajusi? Nini dini yao? Je, Mwenyezi Mungu amewatumia Mtume ye yote kwao? Nimeona kwao vitabu vizuri, mawaidha na mafafanuzi ya kitaalam. Wanayo sherria ya dini iliyo kamili, ambayo kwayo wanafanyia vitendo vyao.
IMAMU:
Hakuna umati ambao miongoni mwao hakukuwepo mwonyaji. Bila shaka, Mtume pamoja na Kitabu amepelekwa na Mwenyezi Mungu kuwaongoza. Lakini watu walimkataa mtume huyo pamoja na Kitabu chake.
MLAHID: Mtume gani alikuwa huyo? Inasemekana kwamba alikuwa Khalif bin Sinaan.
IMAMU:
Khalid bin Sinaan alikuwa Mwarabu wa Kibedui. Hakuwa Mtume. Ni mawazo ya watu tu.
MLAHID: Je, alikuwa Zarasushtra?
IMAMU:
Zarasushtra alileta zaburi (wimbo) na akadai utume. Baadhi ya watu walimwamini, na baadhi yao walimkataa. Baadaye akafukuzwa mjini.
MLAHID:
Hebu nipe habari kuhusu Mamajusi. Je, walikuwa wema zaidi katika dini yao kuliko Waarabu?
IMAMU:
Waarabu katika zama za ujahili (ujinga) walikuwa karibu zaidi na dini ya haki kuliko Mamajusi; kwa sababu Mamajusi hawakumkubali Mtume ye yote. Walikana vitabu vyao na dalili zao. Hawakufuata desturi zao. Katika siku za mwanzo za Mamajusi, mfalme Kai Khusro aliwaua mitume mia tatu. Mamajusi walikuwa hawafanyi 'ghusl' (Mwogo wa Kidini) baada ya kutokwa na manii. Lakini Waarabu katika zama za Ujahili walikuwa wakifanya 'ghusl', na 'ghusl' (kuoga kwa utaratibu maalum baada ya kuwa na janaba n.k.) ni moja katika jambo la lazima katika dini yetu. Mamajusi walikuwa hawatahiri. Kutahiri ni jambo lenye kupendelewa sana ('sunnah') na Mitume. Nabii Ibrahim (a.s.) alianzisha jambo hili. Mamajusi walikuwa hawaoshi maiti zao wla hawakafini. Nabii Ibrahimu (a.s.) alianzisha jambo hili. Waarabu walikuwa wakifanya haya yote. Mamajusi walikuwa wakiwaacha maiti zao katika majangwa na milima. Lakini Waarabu walikuwa wakizizika makaburini, na hii ni desturi ya Mitume. Mamajusi walikuwa wakiwazini mama zao, na wakiwaoa binti zao na dada zao, lakini Waarabu walikuwa wakiona kuwa mambo hayo ni haramu. Mamajusi walikuwa hawalikubali Nyumba ya Mungu (Kaaba) na wakiliita Nyumba ya Shetani. Waarabu walikuwa wakihiji na kuiheshimu Kaaba, na waliiita Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Waarabu waliamini Torati na Injili, na walikuwa wakiwauliza maswali wafuasi wa vitabu hivyo na wakiyafuata maamrisho yake. Kwa hivyo, katika mambo haya yote, Waarabu walikuwa karibu zaidi na dini yetu kuliko Mamajusi.MLAHID:
Kuhusu kuwaoa dada, Mamajusi walitoa hoja kuwa desturi hiyo ilikuwa kawaida tangu zama za Adamu (a.s.)
IMAMU:
Kuhusu kuwaoa dada na mama, hakufuatani na hoja barabara, kwa sababu Adamu, Nuhu, Ibrahimu, Musa Isa na Manabii wote (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao), wamesema kuwa ni haramu. Katika Vitabu vya Mwenyezi Mungu, imetajwa kuwa ni haramu.MLAHID: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameharamisha ulevi, ingawa hakuna kitu kitamu kama hicho?
IMAMU: Mwenyezi Mungu ameharamisha ulevi kwa sababu ni chanzo cha maovu yote. Ulevi unamwathiri mwenye kunywa kwa jinsi ya kumpotezea fahamu zake zote, kumfanya amsahau Mwenyezi Mungu. hakuna dhambi asiyoifanya mlevi. Hujiingiza katika kila kitendo cha aibu. Huharibika sana hata akapoteza mema yote. Mlevi ana hatamu moja tu, ambayo ipo mikononi mwa Shetani. Ikiwa Shetani atamwamuru ayasujudie masanamu, basi atafanya. Huenda po pote ambapo Shetani humwongoza.MLAHID: Kwa nini Mweyezi Mungu ameharamisha kunywa damu?
IMAMU:
Kwa sababu humfanya mtu kuwa katili na humwondolea huruma, huupa mwili harufu mbaya na huibadili rangi yake. Wale wanywao damu, aghalabu huugua ukoma.
MLAHID: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameharamisha kula sehemu za mwili wa wanyama na ndege zambazo ni kama vifuko mnamofanyiwa maji yenye dawa yaingiayo damuni na kufanya kazi nyinginezo mwilini? Kama vile korodani).
IMAMU: Kwa sababu zinasababisha ukoma.
MLAHIDI: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameharamisha kula nyama ya mnyama aliyekufa (mzoga)?
IMAMU: Imeharamishwa ili kuweka mbali na (mnyama) yule aliyechinjwa kwa jina la Mwenyezi Mungu. isitoshe, mnyama anapokufa, damu yake huganda ndani ya nyama. Hivyo, nyama huwa nzito na mbaya inapochanganyika na damu.MLAHIDI: Lakini samaki vile vile ni mnyama aliyekufa!
IMAMU: Kutoka kwake nje ya maji kuna maana kuwa ni kujitolea kwake. Anapotolewa nje ya maji, huachwa juu mpaka afe mwenyewe. Ni hivyo, kwa sababu hana damu. Vivyo hivyo kwa nzige.
MLAHIDI: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameharamisha kuzini?
IMAMU: Kwa sababu huleta machafuko. Vizazi havitambulikani. Nasaba haziimariki. Mwanamke hajui yu nani baba wa mtoto wake. Mtoto hajui ni mwana wa nani. Huondoa ujamaa na ukabila.
MLAHIDI: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameharamisha kulawiti?
IMAMU: Kwa sababu kama kulawiti wanaume kungelihalalishwa, basi watu wasingewakaribia wanawake maana wasingefaa. Kwa sababu hiyo, vizazi visingeendelea. Isitoshe kuhalalishwa kwake kungesababisha mizozano mikubwa na misukosuko ya wenyewe kwa wenyewe.
MLAHIDI: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameharamisha kuwajamii wanyama?
IMAMU: Kulionekana kuwa hakufai kuwa mtu apoteze bure manii yake ili kwamba ikiwa mtoto atazaliwa asiwe na namna nyingine. Kama ingelikuwa halali, wanaume wangewajamii wanyama majike na kutosheleza tama zao za kimwili. Hayo yangesababisha machafuko makubwa. Hivyo, Mwenyezi Mungu ameturuhusu kuwapanda juu ya migongo yao wala si juu ya uke zao. Mwenyezi Mungu amewaumba wanawake kwa ajili ya wanaume ili kwamba wanaume wawapende na wajitosheleze nao tama zao za kimwili, na wanawake wawe vikimbilio vya tama za kiume na mama wa watoto wao.
MLAHIDI: Kwa nini tufanye 'ghusl' baada ya kuwa na janaba, wakati kitendo chetu ni cha halali; na katika kitendo cha halali hakuna unajisi?
IMAMU: Janaba ni kama hedhi, kwa sababu manii ni damu pia, ingawa haipo katika umbo hilo. Hutoka kwa kujamii, kujichua (uke au uume) au kwa kuzidi tamaa ya mwili. Mtu anapojamii, huvuta pumzi sana na huhisi harufu mbaya inatoka mwilini mwake. Kwa hivyo 'ghusl' ni lazima. Mbali ya mambo haya yote, 'ghusl' ya janaba ni jukumu ambalo Mwenyezi Mungu amemwamulia kiumbe chake ili amjaribie kwayo.
MLAHIDI:
Ewe Mwenye hekima! Unasema nini kuhusu wale watu wanaosema kuwa dunia nzima ipo chini ya usimamizi wa Nyota Saba?
IMAMU: Hawana uthibitisho wa kuthibitisha dai hilo. Hii ni dunia kubwa. Dunia yenye sayari ni kama dunia ndogo. Sayari zinazunguka kama dunia (galaxy). Zinafuata sheria za Mwenyezi Mungu na haziwezi kuacha njia zake. Miendo yao imeimarishwa. Hazisimami kabisa. Nyota zote hizi na sayari zimeamriwa kufanya kazi zao kama watumwa. Kama zilikuwepo tangu azali, zisingebadilika.MLAHIDI:
Nijulishe kuhusu wale wanaoamini kuwa Maumbile (Nature) yanasimamia kila kitu.
IMAMU:
Hao ni wanamaumbile. Hawana uwezo juu ya maisha yao au balaa, ambayo inawabadilisha usiku na mchana kutoka hali hii na ile. Watu hawa hawawezi kuepukana na uzee, wala hawawezi kujikinga na mauti.
MLAHIDI:
Unasema nini kuhusu wale wanaoamini kuwa dunia ilikuwepo na itaendelea kuwepo katika hali hii hii zama baada ya zama. Watu wataendelea kuzaliwa na kufa. Nyakati zitakuja na kuondoka. Ugonjwa na maradhi yatawapata watu. Balaa zitaleta uharibifu. Kila kitu cha mwisho kinaonyesha mwanzo wake. Ukoo mmoja unatuambia kuhusu koo zao zilizowatangulia. Zama ya sasa inadhihirisha zama za kale. Wameona dunia katika hali hii hii kama miti na mimea. Katika kila zama, baadhi ya watu huzaliwa miongoni mwa wanadamu ambao hutambua kilicho kizuri na kibaya kwa watu. Huandika vitabu juu ya fikira zao. Hekima na akili zao ni pazia baina yao na mtu wa kawaida. Ni akili yao na hekima yao ambazo huwaongoza katika njia iliyo sawa na kuwashawishi kuifuata. Inawahifadhi kutokana na vitendo vyote viovu na vibaya. Hawauani.IMAMU: Ole kwake! Umesema nini? Aliyezaliwa jana atakufa kesho. Hajui lililotukia kabla yake wala litakalotukia baada yake. Lazima pawepo mambo matatu: Ama mtu amejiumba mwenyewe, au ameumbwa na mtu mwingine, au yeye ni kiumbe wa azali; yaani amekuwepo daima. Yule asiyekuwepo kabla, hawezi kujiumba mwenyewe, vivyo hivyo, yule asiyekuwepo kabla na amekuwepo sasa, hawezi kujua asili yake. Na kama mtu alikuwepo tangu azali, hangeweza kubadilika, kwa sabab kilicho cha azali hakiwezi kubalika kwa sababu ya wakati, wala hakiwezi kutoweka au kuangamia. Juu ya haya, hatuoni msingi wowote usiowekwa na mtu. Kila sanaa tunayoona lazima ina msanifu. Ikiwa mtu anasema kuwa mtu ameumbwa na baba yake, basi swali huja, ni ani alimwumba baba yake; na ikiwa baba yake alimwumba yeye, basi lazima alimfanya kwa matakwa yake, na uso wake na sura yake lazima ziwe nzuri sana, pia lazima awe na uwezo juu ya maisha yake, tena aweze kumweka katika hali nzuri kama anavyotaka. Lakini ukweli ni kuwa, mtu akiwa mgonjwa, baba yake hawezi kumpa afya, na akifa hawezi kumhuisha. Kwa hakika, ikiwa mtu ana uwezo wa kumwumba mtu mwingine na kuweza kumpa roho ili aweze kwenda na kuwa na hisia, basi vile vile lazima awe na uwezo wa kumwepusha na mabaya yote. MLAHIDI:
Nini maoni yako kuhusu utabiri?
IMAMU:
Utabiri (unajimu) ni sayansi, na faida yake ni kidogo kuliko madhara yake. Hauwezi kubadili kilichojaliwa. Watabiri hawana uwezo wa kuwahifadhi wale wanaowaogopa. Ikiwa mtabiri anatabiri baadhi ya balaa zitakazotukia, basi hataweza kujiepusha nazo. Ikiwa anatabiri jambo zuri kwa mtu fulani, basi hawezi kufanya litokee mapema zaidi kuliko wakati uliojaliwa. Ikiwa anatabiri jambo baya, basi hawezi kuliepuka. Mtabiri anataka kushindana na Mwenyezi Mungu, na anafikiri kuwa anaweza kubadilisha majaliwa yake.
MLAHIDI:
Yupi bora zaidi - Mtume wa Mwenyezi Mungu au malaika?
IMAMU:
Mtume wa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi.
MLAHIDI:
Nini haja ya kuwachagua malaika, ambao wameaminiwa kazi ya kuandika mema na maovu ya watu, ingawa Mwenyezi Mungu Mwenyewe anajua mambo yote yaliyo siri na dhahiri.
IMAMU:
Mwenyezi Mungu amewachagua kwa kazi hii. Wao wanashuhudia yale yanayofanywa na viumbe Wake, ili kwamba viumbe wa Mwenyezi Mungu wazidi kumtii na kujikinga na maovu, wanapojua kuwa vitendo vyao vinarekodiwa. Kuna watu wanaokusudia kufanya dhambi, lakini mara wanakumbuka kwamba malaika wapo pamoja nao. Hivyo basi, hujikinga na dhambi wakifikiri kuwa Mwenyezi Mungu anawaona na malaika Wake wanashuhudia vitendo vyao. Ni kwa sbabu ya rehema na upole wa Mwenyezi Mungu kwamba amewachagua malaika ili kwamba mashetani wajiweke mbali na viumbe Vyake. Wao (malaika) wanawakinga wabaya na balaa. Malaika watabaki kuwa hawaonekani mpaka amri ya Mwenyezi Mungu itakapowafika katika namna ya mauti.
MLAHIDI:
Je, Mwenyezi Mungu amewaumba viumbe wake kwa ajili ya rehema au adhabu?
IMAMU:
Amewaumba kwa ajili ya rehema. Kabla ya kuwaumba, ilikuwa katika Elimu yake kuwa miongoni mwao wataadhibiwa kwa sababu ya vitendo vyao viovu na kukataa kwao Haki.
MLAHIDI:
Mshirikina anastahili adhabu kwa sababu amekataa kuamini dini. Lakini kwa nini yule anayeamini Umoja wa Mwenyezi Mungu na anamtambua Yeye aadhibishwe pia?
IMAMU:
Mshirikina atapata adhabu ya milele, na yule anayemuamini kuwa ni Mmoja, ataadhibiwa kwa kutojali wajibu wake. Kisha atatolewa kwenye adhabu. Mwenyezi Mungu hamdhulumu mtu ye yote.
MLAHIDI:
Je, kuna tabaka la baina ya Ukafiri na Uislamu?
IMAMU: Hakuna.
MLAHIDI:
Imani ni nini na kufuru ni nini?
IMAMU:
Imani maana yake: Mtu ausadiki Utukufu wa Mwenyezi Mungu ambao ni mbali na kuona Kwake, kama anavyousadiki utukufu anaouona. Kufuru ni kutousadiki Utukufu Wake.
MLAHIDI:
Ushirikina ni nini na shaka ni nini?
IMAMU:
Ushirikina maana yake: Kumshirikisha mtu ye yote pamoja na Mwenyezi Mungu. Shaka ni kuwa na wasiwasi juu ya unayoyaamini.
MLAHIDI:
Je, mwanachuoni anaweza kuwa mjinga?
IMAMU:
Mwanachuoni ni mwenye kujua yale yaliyopo katika elimu yake. Mjinga anaitwa mjinga kwa sababu ya kutokujua kwake.
MLAHIDI:
Baraka ni nini na balaa ni nini?
IMAMU:
Baraka ni chanzo cha mema ambayo mwenye kubarikiwa hushikilia, nayo humpeleka kwenye wokovu. Balaa ni chanzo cha visirani ambavyo mwenye kuzibiwa hushikilia, nayo humpeleka kwenye maangamizo. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mambo yote.
MLAHIDI:
Mwangaza wa taa huenda wapi, inapozimika taa?
IMAMU:
Unakwenda mahali ambao haurudi tena.
MLAHIDI:
Ndivyo ilivyo kwa binadamu pia. Roho huacha mwili unapokufa. Haimrudii tena, kama ambavyo mwangaza wa taa hauirudii taa baada ya kuzimika.
IMAMU:
Umekosea katika dhana yako. Moto unafunikika ndani ya kitu na kuhifadhika. Vitu huwaka moto kwa sababu ya vijisehemu vya moto kuweko ndani yao. Kwa mfano mawe na chuma, ukivigonganisha pamoja, cheche za moto zitatoka. Wewe unayaeleza hayo kwa mfano wa taa. Kuna tofauti baina yao. Moto hukaa katika mawe na chuma, wakati mwangaza wa taa hutoweka. Roho ni laini sana na nyembamba. Huvaa nguo chafu kwa kuingia ndani ya mwili wa mtu. Si kama taa, ambayo wewe umeizungumzia. Mwenyezi Mungu amewaumba viumbe ndani ya mifuko ya uzazi ya wanawake kwa maji safi, atawafufua baada ya mauti na atawahuisha baada ya kuangamia. Kuna kila aina ya vitu pamoja nayo, kama mishipa, vena, meno, nywele na mifupa n.k.
MLAHIDI:
Roho hukaa wapi (baada ya kutoka mwilini)?
IMAMU:
Hubaki chini ya ardhi, ambapo maiti hubakia mpaka siku ya ufufuo.
MLAHIDI:
Roho ya mtu aliyetiwa tanzi (aliyenyongwa) hukaa wapi?
IMAMU:
Hubaki pamoja na malaika aliyejitoa maisha yake, mpaka atakapofufuliwa. Malaika huiweka kama anavyoiweka ya maiti wa kaburini.
MLAHIDI:
Niambie, nini kinachokuwa pamoja na roho je, ni damu?
IMAMU:
Naam, kitu muhimu kinachokuwa pamoja na roho ni damu. Kutokana na damu, hupatikana unyevu wa mwili. Damu inasafisha, inalainisha sauti na hulidhihirisha tendo la kucheka. Roho hutoka mwilini wakati damu inapoganda.
MLAHIDI:
Nini asili ya hewa?
IMAMU:
Hewa ni upepo unaopepea. Unapokuwa haupepei, unaitwa hewa. Maisha ya dunia hutegemea hewa. Ukisimama, machafuko yataanza katika mambo yote ya dunia. Hewa ni kama kipepeo. Hutoa uchafu wote katika vitu na kuvisafisha. Ni kama roho. Inapopulizwa kutoka mwilini, huchakaa na kubadilika umbo lake. Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Muumba bora kabisa.
MLAHIDI:
Je, roho hupotea angani baada ya kutoka mwilini au huendelea kuwapo?
IMAMU:
Roho huendelea kuwepo mpaka litakapopigwa Baragumu. Vitu vyote vitatanguka na kuangamia. Hakutabaki kitu kihisicho wala anayehisi. Baada ya hayo, vitu vyote vitakuwepo tena katika umbo la kwanza, katika hali ile ile aliyowaumba. Kutakuwepo kipindi kati ya kupigwa Baragumu na Marejeo. Kisha Baragumu la pili litapigwa.
MLAHIDI:
Vipi mwili uliofufuliwa wa mwanaume utakuwa mwanaume. Miili haitakuwepo kwa sababu ya kuoza. Viungo vitatanguka. Sehemu nyingine zitakuweko mahali ambako zitaliwa na wanyama. Viungo vingine vitageuka kuwa mchanga na vitachanganyika na mchanga. Kutokana na mchanga huo, utajengwa ukuta. Sehemu zingine zitaliwa na wadudu.
IMAMU:
Mwenyezi Mungu ambaye aliwaumba, akawapa umbo na sura, ana uwezo wa kuwaumba upya. Hakuwa na kalibu alipowaumbia kwanza?
Roho inashikilia vema pahali pake pa watu wema katika anga ya mwangaza na uwanda; na waovu katika pahali pa giza na pembamba. Miili itageuka kuwa mchanga (udongo) kama ilichoumbiwa kwanza. Wanyama na wadudu wataitapika miili waliyoila. Kila kitu kinahifadhiwa duniani. Hakufichiki cho chote Kwake. Hata kijichembe cha kitu katika giza totoro hakifichiki Kwake. Anajua idadi na uzani wa vitu. Mchanga wa watu watakatifu ni kama dhahabu katika mchanga. Wakati wa ufufuo, dunia itatikisika kama maziwa yanayosukasukwa.Mchanga wa mtu utakuwa safi kama dhahabu inayokuwa wakati inapooshwa kwa maji utakapopondwa kama mapovu ya maziwa, huo mchanganyiko utamiminwa katika kalibu. Hizo kalibu zitapelekwa mahali penye roho. Kwa amri ya (mwenyezi Mungu) Msanii wa Azali, hizo kalibu zitakuwa na maumbo ya mwanzo. Roho zitaingia ndani mwake. Kisha mtu atakuwa na umbo lake la asili, na hataona cho chote kigeni kwake. MLAHIDI:
Je, watu watafufuliwa miili mitupu?
IMAMU:
Watafufuliwa pamoja na sanda zao.
MLAHIDI:
Sanda zao zitatoka wapi? Zitakuwa zimeshaoza.
IMAMU:
Mwumba atakayefufua miili, vile vile atazifanya sanda mpya.
MLAHIDI:
Je, yule aliyekufa bila ya kuwa na sanda?
IMAMU:
Mwenyezi Mungu atazifunika sehemu zake ambazo zitatakikana kufunikwa.
MLAHIDI:
Je, watakusanywa kwa mistari?
IMAMU:
Itakuweko mistari elfu ishirini, urefu wke ni kama upana wa dunia.
MLAHIDI:
Je, vitendo vitapimwa kwa mizani?
IMAMU:
La! Vitendo si vitu, bali ni sifa. Ikiwa mtu hajui idadi ya vitu au uzito wake (kama ni chepesi au kizito) basi huvihesabu au huvipima. Lakini kwa Mwenyezi Mungu hakufichiki cho chote.
MLAHIDI:
Basi nini maana ya Mizani?
IMAMU:
Mizani maana yake ni uadilifu.
MLAHIDI:
NINI MAANA YA Mizani katika aya 2:9 "….. na ye yote mizani yake ikiwa nzito…?"
IMAMU:
Ina maana, "…. Na yeyote vitendo vyake vikiwa vizito…"
MLAHIDI:
Je, moto hautoshi hata mtu aadhibishwe pamoja na ng'e na nyoka?
MLAHIDI:
Je, moto hautoshi hata mtu aadhibishwe pamoja na ng'e na nyoka?
IMAMU:
Watu watakaoadhibiwa pamoja na hao ni wale tu ambao wanaamini kuwa mshirika wa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeviumba viumbe hivi; na kwamba hivi viumbe si vya Mwenyezi Mungu. kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu ataviwekea viumbe hivyo ili waadhibike kwa sababu ya matokeo mabaya ya itikadi yao ya batili.
MLAHIDI:
Vipi watu wanasema kuwa watu wa Peponi watakula matunda kutoka mitini. Kisha matunda hayo yatarudi katika hali yake ya kwanza. Tunda lililoliwa, litarudi pahali pake pale pale kwenye mti.
IMAMU:
Ndiyo, itakuwa vivyo hivyo. Mtu huwasha kibatari kutoka kingine, na mwangaza wa kwanza haupungui wakati dunia inaangaza.
MLAHIDI:
Huko, watu watakula na kunywa. Je, hawatakuwa na haja ya kunya na kukojoa?
IMAMU:
Chakula chao kitakuwa chepechepe sana na kitamu. Mavi hayatafanyika, badala yake yatatoka majasho.
MLAHIDI:
Vipi hurulaini (wanamwali wa Peponi) watabaki kuwa bikira baada ya kujamiiwa na waume zao?
IMAMU:
Hurulaini wameumbwa kutokana na kitu kilichotakasika na safi. Cho chote hakiwezi kuwabadilisha, wala dhara lolote kuwadhuru. Cho chote hakitoki kwenye sehemu zao za stara, wla hawapati hedhi. Matumbo yao ya uzazi hayatatungika mamba. Hakutakuwa na nafasi zaidi ya kuingia cho chote katika sehemu zao za stara isipokuwa uume.
MLAHIDI:
Ingawa hurulaini huvaa nguo, lakini musuli ya miguu yao itaonekana kwa waume zao. Vipi?
IMAMU:
Ni kama tunavyoona sarafu inayong'ara chini ya mto wenye maji safi.
MLAHDI:
Vipi watu wa Peponi watastarehe neema za Peponi wakati watoto, baba, mama na marafiki zao hawatakuwa pamoja nao. Ikiwa hawatakuwepo huko, lazima watakuwepo Motoni. Vipi watakuwa na furaha juu ya kuwa wapenzi wao wanaadhibiwa Motoni?
IMAMU: Watawasahau. Au watawaona baada ya kutolewa katika A'araf (mahali ambapo watu huwekwa kwa kungoja kutolewa uamuzi juu yao).TAMATI
27/12/2006KWA MKURUGENZI MWENDESHAJI NURRAIFO WAZO DISPENSARY TEGETA YAH: MALIPO YA MCHANGO WA UENDESHAJI OFISI KUU NA DR. MSIMAMIZI YA KILA MWEZI Mada ya hapo juu yahusika, tunaomba urejee barua yetu ya tarehe 25/7/2006 inayozungumzia mada hiyo hiyo iliopo hapo juu. Kulingana na hali ngumu ya mapato katika masiku ya hapo awali Ofisi Kuu ilikubali kupokea shilingi 30,000= kwa mwezi badala ya 60,000= kwa mwezi kwa maelezo kwamba ifikapo Januari 2007 tutaanza kuchukua shilingi 60,000= kama kawaida, hivyo tunakuomba na kukusisitizia ukumbuke jambo hilo kwani lipo wazi na halina utata wowote. Jambo lingine ni kwamba itakuwa makosa makubwa kumkabidhi mtu mwingine kuendesha Kituo bila ya kumkabidhi mtu huyo kwetu kwa maandishi na sisi kuonana nae ana kwa ana na wewe ukiwepo. Wako Katika Ujenzi wa Taifa A.M. MTULIA KATIBU MKUU |
|||||