ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

KUKUSANYA BAINA YA SALA MBILI
Miongoni mwa mambo ambayo Mashia wanaumbuliwa, ni kuchanganya Sala ya Adhuhuri na Alasiri na baina ya Sala ya Magharibi na I'sha. Masunni wakati wanapowaumbuwa Mashia, wenyewe huwa wanasisitiza kwamba wao ndiyo wanaoilinda Sala kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: "Bila shaka Sala kwa Waumini imekuwa ni faradhi yenye wakati maalum". Na kabla ya kuwaunga mkono au kuwa dhidi yao tunawajibika kufanya uchambuzi juu ya maudhui hii kwa kila upande na tuzione kauli za pande mbili (Shia na Sunni).

Ama Masunni wanaafikiana kuwa inafaa kukusanya baina ya (Sala ya) Adhuhuri na Alasiri na inaitwa "Jam'u1 Taqdi'm" Na kuchanganya huko Muz-Dalifah wakati wa I'sha baina ya hiyo sala ya I'sha na faradhi ya Magharibi na inaitwa: "Jam'u't-Taakhir". Na hili wanalikubali Waislamu wote Mashia na Masunni, bali vikundi vyote vya Kiislamu bila kubagua. Na tofauti iliyopo baina ya Mashia na Masunni ni ruhusa ya kukusanya baina ya faradhi mbili yaani Adhuhuri na Alasiri na Magharibi na I'sha katika siku zote tena bila ya udhuru wa safari. Ama Madhehebu ya Hanafi wao wanasema kuwa hairuhusiwi hata katika safari. Pamoja na kuwa kuna maandiko yaliyo wazi yanayoruhusu, na hasa katika safari, na kwa kusema kwao hivyo wamekwenda kinyume na makubaliano ya umma wa Kisunni na Kishia.


Ama Maliki na Shafii na Hanbal wao wanasema kuwa inaruhusiwa kukusanya baina ya faradhi hizo mbili wakati wa safari na wanahitilafiana baina yao juu ya ruhusa hiyo kwa udhuru wa khofu, maradhi, mvua, na tope. Ama Shia wao wanakubaliana bila kipingamizi juu ya ruhusa ya kukusanya wakati ambao siyo wa safari wala maradhi wala khofu yoyote. Na hiyo ni kwa kufuata maelezo waliyoyapokea kutoka kwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) katika kizazi kitukufu. Na hapa tunalazimika tusimame msimamo wa tuhuma na mashaka dhidi yao, kwani kila mara Masunni wanapotoa hoja dhidi ya Mashia, wao hujibu kwamba Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) ndiyo waliowafundisha na wakawabainishia kila lenye kuwatatiza na hujifakharisha kwamba wao wanawafuata Maimamu Maasum ambao wanaifahamu vyema Qur'an na Sunna. Nami binafsi naikumbuka sala yangu ya mwanzo niliyokusanya ilikuwa baina ya adhuhuri na alasiri, na iliongozwa na shahidi Muhammad Baqir As-Sadr (r.a.) wakati nilipokuwa Najaf, na hapo kabla nikitenganisha baina ya sala ya adhuhuri na Alasiri,* mpaka ilipofika siku hiyo njema ambayo nilitoka pamoja na Sayyid Muhammad Baqir As-Sadr nyumbani kwake kwenda kwenye Msikiti ambao alikuwa akiwaongoza wafuasi wake.Watu hao waliniheshimu na wakaniachia nafasi nyuma yake.


Sala ya Adhuhuri ilipomalizika iliqimiwa sala ya alasiri, nafsi yangu ilinishauri nijitoe kwenye safu lakini nilibaki kwa sababu mbili: Ya kwanza, heshima ya Sayyid As-Sadr na unyenyekevu wake katika sala kiasi kwamba nilitamani sala iendelee, na ya pili ni kuwepo kwangu katika nafasi ile nami nikiwa karibu mno kwake miongoni mwa wenye kusali na nilihisi nguvu yenye shinikizo inanifunga kwake.

Tulipomaliza kuswali faradhi ya alasiri watu wakasongamana kwake wakimuuliza, basi nilibakia nyuma yake nikisikiliza maswali na majibu yake isipokuwa yale ambayo sikuyasikia vizuri (pindi yaulizwapo au pindi yajibiwapo). Hatimaye Sayyid alinichukua twende pamoja naye nyumbani kwake kwa ajili ya chakula cha mchana, na huko nilijikuta kuwa ni mgeni mheshimiwa, na hapo ndipo nilipoitumia fursa ya kikao hicho kumuuliza juu ya kukusanya baina ya Sala mbili nikasema: "Ewe Bwana wangu hivi inawezekana kwa Muislamu kukusanya baina ya faradhi mbili kama anayo dharura"? Akasema: "Inawezekana kukusanya baina ya faradhi mbili katika hali zote na bila ya dharura yoyote." Nikasema: "Ni ipi hoja yenu"? Akasema: "Ni kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikusanya baina ya faradhi mbili akiwa Madina na siyo katika safari wala khofu wala mvua wala dharura yoyote. Na hiyo ni kwa sababu tu ya kutuondoshea uzito, na jambo hili Al-Hamdulillah limethibiti kwetu sisi kupitia kwa Maimamu watakatifu na vile vile kwenu umethibiti".


Nilishangaa sana, ni vipi kwetu sisi limethibiti na sijalisikia kabla ya leo na wala sijamuona yeyote miongoni mwa Masunni akilitumia bali kinyume chake Masunni wanasema kuwa sala hubatilika ikiwa itasaliwa japo dakika moja kabla ya adhana, basi itakuwaje kwa anayeisali kabla ya masaa chungu nzima tena akaifuatisha baada ya Adhuhuri, au akasali sala ya I'sha wakai wa Magharibi, basi kwetu sisi inaonekana ni jambo baya na batili.

Sayyid Muhammad Baqir As-Sadr alifahamu wasi wasi wangu na kushangazwa kwangu, na hapo akamnong'oneza mmoja wa waliokuwepo hapo, yule akasimama haraka na akarudi na vitabu viwili, nikavifahamu kuwa ni Sahih Bukhar na Sahih Muslim. Sayyid As-Sadr akamkalifisha mwanafunzi yule anioneshe hadithi zinazohusu kukusanya baina ya faradhi mbili: Nikasoma mwenyewe ndani ya Sahih Bukhari namna Mtume alivyokusanya baina ya faradhi ya adhuhuri na alasiri, na vile vile faradhi ya magharibi na i'sha, kama ambavyo ndani ya Sahihi Muslim nilisoma mlango mzima unaohusu kukusanya baina ya sala mbili nyumbani bila ya khofu wala mvua wala safari.

Sikuficha kustaajabu na kushangaa kwangu japokuwa mashaka yaliniingia kwamba Bukhari na Muslim walizonazo wao huenda zikawa zimepotoshwa na nikanyamazia moyoni tu kwamba nitavirejea (kuvisoma) vitabu hivi (nyumbani) Tunisia. Sayyid Muhammad Baqir aliniuliza maoni yangu baada ya dalili hii. Nikasema: "Ninyi mko kwenye ukweli nanyi wakweli katika hayo myasemayo na napenda kukuulizeni swali jingine" Akasema: "Tafadhali (uliza)". Nikasema: "Je, inafaa kukusanya baina ya sala nne kama wafanyavyo watu wengi huko kwetu pindi warudipo usiku wanasali Qadhaa adhuhuri, alasiri na magharibi na i'sha"? Akasema: "Haifai".


Nikasema:"Uliniambia hapo kabla kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alitenganisha (Sala) na alikusanya na kwa ajili- hiyo tumefahamu nyakati za sala ambazo Mwenyezi Mungu ameziridhia." Akasema: "Hakika faradhi ya adhuhuri na alasiri zina wakati unaoshirikiana na unaanzia tangu kupinduka jua mpaka kuzama, na faradhi ya magharibi na i'sha pia zina wakati unaoshirikiana na unaanzia tangu kuzama jua hadi nusu ya usiku, na faradhi ya asubuhi ina wakati mmoja, unaanzia tangu kuchomoza al-fajiri hadi kuchomoza jua, basi yeyote atayekwenda kinyume cha nyakati hizi atakuwa amekwenda kinyume cha aya tukufu isemayo: "Bila shaka sala kwa waumini imekuwa ni faradhi yenye wakati maalum". Haiwezekani kwetu sisi kwa mfano kusali sala ya asubuhi kabla ya al-fajiri wala baada ya kuchomoza jua, kama ambavyo haiwezekani kwetu sisi kuswali faradhi mbili za adhuhuri na alasiri kabla ya kupinduka jua au baada ya kuzama jua kama ambavyo haifai kwetu sisi kuswali faradhi ya magharibi na i'sha kabla ya kuzama jua na baada ya nusu ya usiku.

Nilimshukuru Sayyid Muhammad Baqir As-Sadr, japokuwa nilikuwa nimekinaika kwa kauli zake zote lakini sikukusanya baina ya faradhi mbili baada ya kuachana naye isipokuwa niliporudi Tunisia na nikazama katika uchunguzi na nikauona ukweli. Hiki ndicho kisa changu na Shahid As-Sadr Mwenyezi Mungu amrehemu kuhusu kukusanya baina ya faradhi mbili, nakisimulia ili iwabainikie ndugu zangu miongoni mwa Masunni: Kwanza:Waone ni namna gani zinavyokuwa tabia za wanachuoni ambao ni wanyenyekevu mpaka kwa kweli wamekuwa ni warithi wa Mitume katika elimu na tabia. Pili:Ni namna gani hatuyajuwi mambo yaliyomo ndani ya sihah zetu na tunawaumbuwa wengine kwa mambo ambayo sisi wenyewe tunayaamini kusihi kwake na yamo ndani ya sihah zetu.


Imam Ahmad bin Hanbal amethibitisha ndani ya Musnad yake[97] kutoka kwa ibn Abbas amesema:"Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alisali (rakaa) saba na (rakaa) nane akiwa mjini Madina na hakuwa safarini". Na amethibitisha Imam Malik ndani ya kitabu kiitwacho Muwatta[98] kutoka kwa ibn Abbas amesema "Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alisali adhuhuri na alasiri zote (kwa pamoja) na magharibi na i'sha zote kwa pamoja pasi na khofu wala safari". Naye Imam Muslim amethibitisha ndani ya Sahih yake katika mlango wa kukusanya baina ya-sala mbili nyumbani (bila kuwa safarini) amesema:
"Imepokewa toka kwa ibn Abbas amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alisali adhuhuri na alasiri zote kwa pamoja, na magharibi na i'sha zote kwa pamoja bila khofu wala safari".[99] Kama ambavyo amethibitisha kutoka kwa ibn Abbas tena amesema:"Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya baina ya sala ya adhuhuri na alasiri na magharibi na i'sha akiwa Madina bila ya khofu wala mvua amesema nikamwambia ibn Abbas: "Kwa nini alifanya hivyo"? Akasema: "Ili asiwape uzito ummati wake."[100]

Na miongoni mwa mambo yatakayokujulisha ewe ndugu msomaji kwamba sunna hii ilikuwa mashuhuri kwa Masahaba na wakiitumia, ni yale aliyoyaeleza Muslim, ndani ya sahihi yake katika mlango huu huu amesema: "Ibn Abbas alituhutubia siku moja baada ya sala ya alasiri mpaka jua likazama na nyota zikadhihiri, watu wakaanza kusema, "Sala sala", amesema:Akamjia ibn Abbas mtu mmoja miongoni mwa Bani Tamim hapunguzi wala hakomi(kusema) sala sala. Basi ibn Abbas akasema, Je, unanifundisha sunna, ole wako, kisha akasema:Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amekusanya baina ya sala ya adhuhuri na alasiri na magharibi na i'sha, na katika mapokezi mengine, ibn Abbas alimwambia mtu yule "Ole wake unatufundisha sala nasi tulikuwa tukikusanya baina ya sala mbili zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Taz: Sahih Muslim Juz. 2 uk. 153 (Babul-jam'i bainas-salatain fil-hadhr).


Naye Imam Bukhar amethibitisha ndani ya sahih yake katika mlango wa wakati wa Magharib amesema, "Ametusimulia Adam, amesema. Ametusimulia Shuubah, ametusimulia Amr bin Dinar, amesema nilimsikia Jabir bin Zaid, kutoka kwa ibn Abbas amesema: Mtume (s.a.w.) aliswali (rakaa) saba zote kwa pamoja na (rakaa) nane zote kwa pamoja. Taz: Sahih Bukhar Juz. 1 uk.140 (Babu waqtil-maghrib). Kama ambavyo Bukhar amethibitisha ndani ya Sahih yake katika mlango wa wakati wa alasiri amesema: "Nilimsikia Abu Amamah akisema, tulisali na Umar bin Abdil-A'ziz sala ya adhuhuri kisha tukatoka mpaka tukaingia kwa Anas bin Malik tukamkuta anasali sala ya alasiri mimi nikasema: ewe Ammi ni sala gani hii uliyosali? Akasema:"Alasiri, na hii ni sala ya Mtume wa Mwenyezi Mungu tulikuwa tukiisali pamoja naye". Taz: Sahih BukharJuz. 1 uk. 138. (Babu waqtil-asr).


Pamoja na uwazi wa hadithi hizi, utakuta bado kuna watu wanaowakebehi Mashia kwa jambo hilo, na kuna wakati fulani hali hiyo ilitokea huko Tunis, pale Imam mmoja aliposimama mbele yetu katika mji wa Qafsah ili atutukane na kutuadhiri mbele ya wanaosali akasema: "Je, mumeiona hii dini waliokuja nayo, hakika wao baada ya sala ya adhuhuri husimama wakasali alasiri, bila shaka hii ni dini mpya siyo dini ya Muhammad ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, watu hawa wanakwenda kinyume cha Qur'an ambayo inasema: "Bila shaka sala kwa waumini imekuwa faradhi yenye wakati maalum." Na hakuacha kitu illa alishutumu wote waliouona ukweli.

Kuna mmoja wao alikwisha kuuona ukweli huu alinijia na alikuwa ni kijana mwenye kiwango kikubwa cha maarifa, akanisimulia kwa uchungu yale aliyoyasema Imam yule, basi mimi nilimpa Sahih Bukhar na Sahih Muslim, na nikamtaka amuoneshe juu ya kusihi kwa suala la kukusanya na ni sunna ya Mtume (s.a.w.) (nilifanya hivyo) kwa kuwa mimi sitaki kujadiliana naye kwani hapo kabla nilijadiliana naye kwa njia nzuri yeye akanikabili kwa shutuma na matusi na tuhuma mbaya. Hivyo la muhimu ni kwamba rafiki yangu (huyu) hakuacha kusali nyuma yake na baada ya kuisha sala yule Imam alikaa kama kawaida yake kwa ajili ya kusomesha, basi yule rafiki yangu alimuuliza juu ya kukusanya baina ya faradhi mbili. Yule Imam akasema:"Huo ni uzushi wa Mashia". Rafiki yangu akamwambia, "Lakini jambo hilo limethibiti ndani ya Sahih Bukhar na Sahih Muslim". Akampa, akausoma mlango wa kukusanya baina ya sala mbili. Basi ukweli ulipomgonga tena mbele ya watu wanaosali humo na kusikiliza darasa zake, alikifunga na akanirejeshea huku akisema: "Jambo hili lilikuwa ni maalum kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu nawe mpaka utapokuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu basi unaweza kusali (hivyo).

Rafiki yangu huyu anasema: "(Baada ya jibu hili) nikafahamu kwamba Imam yule ni mjinga tena mwenye chuki, nami nikaapa kuwa kuanzia siku ile sintasali nyuma yake"[101] Baada ya hayo nilimtaka rafiki yangu amrudie yule Imam amuonyeshe kwamba ibn Abbas alikuwa akiswali sala hiyo, na vile vile Anas bin Malik na Masahaba wengi. Basi ni kwanini yeye anataka kuihusisha kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Je, haikuwa kwetu sisi Mtume ni kiigizo chema? Lakini rafiki yangu alitoa udhuru akasema: "Hapana haja ya jambo hili huyo hawezi kukubali hata kama Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) atakuja.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu anastahiki shukrani, kwani baada ya vijana wengi kufahamu ukweli huu ambao ni kuchanganya baina ya sala mbili Tangu hapo wengi wao wameirudia sala baada ya kuwa waliiacha kwa sababu walikuwa wakipata taabu ya kupitwa na sala kwa nyakati zake na huzikusanya nyakati nne usiku na nyoyo zao zinachoka. Si hivyo tu, bali wameifahamu hekima ya kukusanya sala katika nyakati zake hali ya kuwa wametulizana, na wamefahamu hekima ya kauli ya Mtume (s.a.w.) isemayo: "Nisije kuwapa taabu umma wangu".


KUSUJUDU JUU YA UDONGO
Wanachuoni wa Kishia wamekubaliana juu ya kauli inayohusu ubora wa kusujudu juu ya ardhi kutokana na mapokezi wanayoyapokea kutoka kwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.), mapokezi hayo ni kauli ya babu yao ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu aliposema: "Bora ya Sijda ni (kusujudu) juu ya ardhi". Na katika mapokezi mengine (amesema), "Sijida haijuzu isipokuwa juu ya ardhi au kile kilichooteshwa ardhini kisicholiwa wala kuvaliwa".

Na mwenye Kitabu kiitwacho Wasailus-Shia' amesimulia toka kwa Muhammad bin Ali bin Husain kwa isnadi yake, toka kwa Hisham bin Al-Hakam toka kwa Abu Abdillah (a.s.) amesema: "Kusujudu juu ya ardhi ni bora kwani kunazidisha unyenyekevu, na unyenyekevu (ufanywe) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu". Na ndani ya mapokezi mengine kutoka kwa Muhammad bin Al-Hasan kwa isnad yake toka kwa Is'haq bin Al-Faali kwamba yeye alimuuliza Abu Abdillah (a.s.) kuhusu kusujudu juu ya mkeka na jamvi lililofumwa kwa matete, akasema, "Hapana ubaya, na kusujudu juu ya ardhi kwangu mimi ni bora zaidi, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa akipenda hivyo (yaani) kuweka bapa lake la uso ardhini, basi nami nakupendelea wewe kile alichokuwa akikipenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.)" Ama wanachuoni wa Kisunni wao hawaoni vibaya kusujudu juu ya mabusati na mazulia japokuwa ilivyo bora kwao ni kusujudu juu ya jamvi.


Na kuna baadhi ya riwaya ambazo amezithibitisha Bukhar na Muslim ndani ya sahihi zao (riwaya) ambazo zinasisitiza kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa na mswala uliotengenezwa kwa makuti akisujudu juu yake. Muslim amethibitisha ndani ya sahihi yake katika Kitabul-Haidh kutoka kwa Yahya bin Yahya na Abubakr bin Abi Shaibah, kutoka kwa Abu Muawiyah kutoka kwa Al-Aa'mash, naye toka kwa Thabiti bin Ubaid kutoka kwa Qasim bin Muhammad, naye toka kwa Aisha amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliniambia, nimchukulie jamvi langu humo msikitini, Aisha akasema, nikamwambia mimi ninahedhi, Mtume akasema:Bila shaka hedhi yako haiko mkononi mwako". Taz: Sahihi Muslim Juz. 1 uk. 168. Babu-Jawaz Ghaslil-Haidh Ra'asa Zaujiha), Sunan Abi Dawud Juz. 1 uk. 68 (Babul-Haidh Tanawul Minal-Masjid).


Sasa Muslim anasema, Al-Khumrah ni kifaa kidogo cha kusujudia kwa kiasi cha kutosha kusujudu juu yake. Na miongoni mwa mambo ambayo yanatujulisha kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa akipenda kusujudu juu ya ardhi ni mapokezi aliyoyathibitisha Bukhar ndani ya sahih yake kutoka kwa Abu-Said Al-Khudri (r.a.) kwamba, "Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa akikaa itikafu katika kumi la kati ndani ya mwezi wa Ramadhani. Basi kuna mwaka fulani alikaa itikafu mpaka ilipofika usiku wa tarehe ishirini na moja nao ni usiku ambao asubuhi yake anatoka katika itikafu yake, akasema, yeyote aliyekuwa akikaa itikafu pamoja nami, basi na akae itikafu kumi la mwisho kwa hakika usiku huu nilioteshwa kisha nikasahaulishwa na uliniona vile nikisujudu katika maji na tope,basi utafuteni katika kumi la mwisho na muutafute katika (tarehe za witri). Mvua ilinyesha usiku huo na msikiti ulikuwa wa hema basi msikiti ukavuja, na macho yangu yalimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) juu ya uso wake kuna alama ya maji na tope asubuhi ya tarehe ishirini na moja". Taz: Sahih Bukhar Juz. 2 uk. 256 (Babul-itikaf -Fil-A 'shril-Awa'khiri).

Pia miongoni mwa mambo yanayotujulisha ni kwamba, Masahaba walikuwa wakiboresha kusujudu juu ya ardhi, na wakifanya hivyo mbele ya Mtume (s.a.w.) kama alivyothibitisha Imam An-Nasai ndani ya sunan yake katika mlango wa "Tabridul-haswa Lis-Sujud Alaiha"akasema: "Ametueleza Qataybah amesema, ametusimulia Ubba'd kutoka kwa Muhammad bin Amr kutoka kwa Said bin Al-Harith naye toka kwa Jabir bin Abdillah amesema:"Tulikuwa tukisali pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) sala ya adhuhuri, basi nikachukua gao la changarawe katika kiganja changu kulipoza kisha huligeuzia kwenye kiganja kingine ninaposujudu huliweka gao hilo kwa ajili ya paji langu la uso".


Taz: Sunan Al-Imam An-Nasai Juz. 2 uk. 204 (Babu Tabridul-Haswa Lis-Sujud A 'laih. Zaidi ya yote hayo, ni kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Ardhi imefanywa kwa ajili yangu kuwa ni mahala pa kusujudia na tahara". Taz: Sahih Bukhar Juz. 1 uk. 86 (Kitabut- Tayammum). Na vile vile amesema:
"Ardhi yote tumefanyiwa kuwa ni mahala pa kusujudia na udongo wake ni tahara." Taz: Sahih Muslim Juz, 2 uk. 64, (Kitabul-Masajid Wamawa-dhiu's-Salah). Basi ni vipi Masuni wanakuwa na chuki dhidi ya Mashia kwa kuwa tu wanasujudu juu ya ardhi badala ya kusujudu kwenye mabusati. Na ni vipi mambo yanafikia kiasi cha kuwakufurisha na kuwakejeli na kuwazulia kwamba wao (Mashia) ni waabudu sanamu? Na vipi wanawapiga (Mashia) huko Saudi Arabia kwa kuwa tu kumepatikana Turba (Udongo) ndani ya mifuko yao au mabegi yao? Je, huu ndiyo Uislamu unaotuamuru kuheshimiana sisi kwa sisi na kutokumdharau Muislamu anayempwekesha Mwenyezi Mungu, (Muislamu) ambaye anashuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, anasali, anatoa zaka na kufunga Ramadhan na kuhiji Maka.


Je, inaingia akilini kwamba Mashia wanavumilia taabu hizo na kupata hasara na kuja kuhiji kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu na kuzuru kaburi la Mtume (s.a.w.) na hali ya kuwa wanaabudu jiwe kama wanavyopenda baadhi ya watu kufikiria hivyo? Basi je, Masunni hawatosheki na kauli ya Shahidi Muhammad Baqir As-Sadr ambayo nimeinakili ndani ya kitabu changu cha mwanzo kiitwacho, "Thummah-Tadaytu" wakati nilipomuuliza juu ya Turbah akasema: Na kama isingalikuwa juu yenu fadhila ya Mwenyezi Mungu na Rehma yake katika dunia na akhera, bila shaka ingalikupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyoyashughulikia. Pindi mnapotangaza kwa ndimi zenu na mnasema kwa vinywa vyenu msilolijua na mnadhani ni jambo jepesi kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni jambo kubwa kabisa (Qur'an, 24:14)