ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

TAQIYYAH
Kama tulivyotangulia kusema kuhusu kauli ya "Al-Bada'u, basi Taqiyyah nayo vile vile ni miongoni mwa mambo yanayopingwa kwa Masunni, na wao huwakejeli ndugu zao Mashia kwa hilo na kuwaona kuwa ni wanafiki, kwani hukidhihirisha ambacho sicho walichokificha...!! Na ni mara nyingi nimezungumza na baadhi yao na nikajaribu kuwakinaisha kwamba Taqiyyah siyo unafiki, lakini hawakukinaika, bali wakati mwingine utamkuta anayesikiliza jambo hili anachukia na wakati mwingine anashangaa, na hali yakuwa anadhani kuwa itikadi hii imezushwa katika Uislamu na kama kwamba ni miongoni mwa yaliyofanywa na Shia na uzushi wao. Lakini pindi mwenye kufuatilia atapofanya uchambuzi na akawa muadilifu, atakuta kwamba itikadi hii yote ni katika uti wa mgongo wa Uislamu na imetokana na Qur'an Tukufu na Sunna Tukufu ya Mtume (s.a.w.), bali mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu na hii sheria madhubuti havisimami ila kwa Taqiyyah.


Na jambo la kushangaza kwa Masunni ni kwamba, wao wanazipinga itikadi ambazo wanazitaja (ndani ya vitabu vyao) na vitabu vyao na sihahi zao na Musnad zao zimejaa mambo hayo na zinashuhudia dhidi yao. Hebu tuyasome kwa pamoja yale wayasemayo Masunni kuhusu Taqiyyah: Ibn Jarir na ibn Abi Hatim wamethibitisha kwa njia ya Al-Au'fi kutoka kwa ibn Abbas katika kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Isipokuwa kwa ajili ya kujilinda kutokana na shari zao" (Qur'an, 3:28) Amesema ibn Abbas "Taqiyyah (kujilinda) ni kwa ulimi, yeyote atakayelazimishwa jambo fulani aliseme hali ya kuwa jambo hilo ni la kumuasi Mwenyezi Mungu, naye akalisema kwa kuwachelea watu, na moyo wake umetulizana kwa imani, basi hali hiyo haitamdhuru kwani Taqiyyah ni kwa ulimi"

Taz: Ad-Durrul-Manthoor Fi Tafsir Bil- Maathur cha Jalalud-Din Suyuti. Na Al-hakim ameandika hadithi na kuisahihisha, na Al-Baihaqi ndani ya Sunan yake kwa njia ya A'taa1 kutoka kwa ibn Abbas amesema kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:"Isipokuwa kwa ajili ya kujilinda kutokana na shari zao" Kwamba: "At-Tuqah" yaani Taqiyyah ni kusema kwa ulimi na hali yakuwa moyo umetulizana (umethibiti) kwa imani: Taz: Sunanul-Baihaqi na Mustad-Rak Al-Hakim. Na amethibitisha Abdu bin Hamid kutoka kwa Al-Hasan amesema:"Taqiyyah inajuzu hadi siku ya Kiyama." Taz: Ad-Durrul-Manthoor cha Jalalud-Dinis-Suyuti Juz. 2 uk. 176.

Naye Abdur-Razzaq, ibn Saad, ibn Jabir, ibn Abi-hatim na ibn Mar-dawaih wamethibitisha na Al-Hakim amesahihisha ndani ya Mustadrak yake na Al-Baihaqi ndani ya Ad-Dalail amesema: "Washirikina walimuadhibu Ammar bin Yaasir hawakumwachia mpaka alipomtukana Mtume (s.a.w.) na akawataja Miungu yao kwa wema ndipo walipomuachia, alipofika kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) Mtume akasema, kuna nini huko? Ammar akasema shari tupu, kwani sikuachiwa mpaka nilipokutukana na nikawataja miungu wao kwa wema, Mtume akasema, wauonaje moyo wako, Ammar akasema, umetulizana (umethibiti) kwa imani, Mtume akasema, basi wakirudia tena nawe rudia tena, basi hapo ikashuka (aya isemayo) "Isipokuwa yule aliyelazimishwa na hali moyo wake umetulizana kwa imani" (Qur'an, 16:106) Na amethibitisha ibn Saa'd kutoka kwa Muhammad bin Siriin kwamba Mtume (s.a.w.) alimkuta Ammar hali yakuwa analia, basi Mtume akawa anampangusa macho yake huku akisema "Wamekuadhibu makafiri wakakuzamisha ndani ya maji nawe ukasema kadha wakadha, basi iwapo watarudia tena waambie hivyo hivyo (ulivyowaambia kwanza). Taz: Atabaqatul-Kubra cha ibn Saad.


Na wamethibitisha ibn Jarir, ibn Mundhir, ibn Abi-Hatim na Al-Baihaqi ndani ya sunan yake kwa njia ya Ali kutoka kwa ibn Abbas kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu ..." Amesema: "Mwenyezi Mungu ameeleza kwamba, yeyote mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu baada ya kuwa amemuamini, basi mtu huyo ghadhabu toka kwa Mwenyezi Mungu zimshukie na atapata adhabu kali, ama yule mwenye kushurutishwa akasema kwa ulimi wake na moyo wake uko kinyume (cha hivyo) kwa kuwa na imani, (lakini akakufuru) kwa kujiokoa tokana na maadui zake, basi huyo hana makosa, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu huwaadhibu waja kwa yale waliyoamini mioyoni mwao". Taz: Sunan Al-Bayhaqi.


Na wamethibitisha mabwana ibn Abi Shaibah, ibn Jabir, Ibn Mundhir na ibn Abi Hatim kutoka kwa Mujahid amesema: "Aya hii ilishuka kwa watu wa Maka walioamini, basi baadhi ya Masahaba kutoka Madina wakawaandikia (wakasema), Hameni, hakika sisi hatuoni kwamba ninyi ni miongoni mwetu mpaka muhame mje kwetu, basi wakatoka kuelekea Madina, ghafla Maqurayshi wakawakamata njiani wakawatesa, wakakufuru hali ya kulazimishwa kufanya hivyo, basi kwa ajili yao ilishuka aya hii, "Isipokuwa yule aliyelazimishwa na hali moyo wake umethibiti kwa imani", Taz: Ad-Durrul-Manthoor cha Jalakud-Dinis-Suyuti Juz. 2uk 178. Naye Bukhar amethibitisha ndani ya sahih yake katika Babul-Mudaarati Maan-Nas, na ameeleza kutoka kwa Abud-Dar-dai amesema: "Hakika sisi tunaonyesha meno mbele ya nyuso za watu na hali yakuwa nyoyo zetu zinawalaani". Taz: Sahih Bukhar Juz. 7 uk. 102.


Naye Al-Halabi amethibitisha ndani ya Sira yake amesema: "Pindi Mtume wa Mwenyezi Mungu alipoushinda mji wa Khaybar, Hajjaj bin Ala-t alimwambia Mtume, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi ninazo mali huko Maka na ninao jamaa huko, nami nataka kuwatembelea, basi je, ninayo ruhusa ikiwa nitakutukana na nikasema jambo fulani? Mtume wa Mwenyezi Mungu alimruhusu aseme alitakalo". Taz: As-Si'ratul-Halabiyyah Juz. 3 uk. 61. Na imekuja ndani ya Kitabu kiitwacho Ihyau-Ulum cha Imam Ghazali amesema: "Hakika kuhifadhika damu ya Muislamu ni jambo la wajibu basi wakati wowote itakapokuwa makusudio ya kumwaga damu ya Muislamu yamefichikana ndani ya dhalimu, kumwambia uongo ni wajibu." Taz: Ihyau Ulumid-Din cha Hujjatul-Islam Abu Hamid Al-Ghazali.


Na amethibitisha Jalalud-Din As-Suyuti ndani ya kitabu kiitwacho Al-Ash-Ba'hu Wan-Nadhair amesema: "Inaruhusiwa kula mzoga wakati wa njaa (hakuna chakula kingine) na kunywa funda la pombe na kutamka neno la kufru (wakati wa matatizo) na lau haramu itaenea katika sehemu fulani kiasi kwamba haipatikani halali katika sehemu isipokuwa kwa nadra, basi inaruhusiwa kutumia (haramu) kwa kiasi cha Haja". Na amethibitisha Abubakr Ar-Razi ndani ya kitabu chake Ahkamul-Qur-an katika kufasiri kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Illa Antat-Taqu Minhum Tuqatan" Yaani (isipokuwa kwa ajili ya kujilinda kutokana na shari zao) amesema ina maana kuwa mtakapochelea kuzidhuru nafsi au baadhi ya viungo basi mtajilinda kutokana nao kwa kudhihirisha kuwafuata bila ya kuyaamini hayo yao, na hii ndiyo bayana inayokubaliana na tamko hilo na ndiyo msimamo wa kongamano la wanachuoni, kama ilivyokuja kutoka kwa Qatada juu ya kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
"Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wandani wao (watawala) kinyume cha Mwenyezi Mungu". Amesema (Qatadah) haifai kwa Muumini kumfanya kafiri kuwa mtawala katika dini yake, na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo, "Isipokuwa kwa kujilinda na shari zao inapelekea ruhusa ya kudhihirisha kufru wakati wa Taqiyyah Taz: Ahkamul-Qur'an cha Ar-Razi Juz. 2 uk. 10,


Naye Bukhari amethibitisha ndani ya sahih yake kutoka kwa Qutaibah bin Said, kutoka kwa Sufiyan, kutoka kwa Al-Mukandar, amemsimulia toka Ur-Wah bin Zubair kwamba bibi Aisha alimueleza yakuwa, "Kuna mtu alibisha hodi nyumbani kwa Mtume (s.a.w.), Mtume akasema mkaribisheni, Oh! Mwana wa Al-Ashira ni muovu, au alisema ni muovu ndugu wa Al-Ashira. Alipoingia Mtume alizungumza naye kwa maneno laini, basi mimi nikasema (Yaani Aisha) Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu umesema uliyoyasema kisha umemfanyia upole katika mazungumzo? Mtume (s.a.w.) akasema: Ewe Aisha hakika watu wenye daraja ya shari kwa Mwenyezi Mungu ni mtu yule waliyemuacha watu au kumtelekeza ili kujilinda na uovu wake." Taz: Sahih Bukhari Juz. 7uk.81.

Na hii inatutosha kuwa ni dalili baada ya kuwa tumeonesha ndani ya maelezo yaliyotangulia ya kwamba masunni wanaamini kuwepo ruhusa ya Taqiyah mpaka kwenye mipaka yake ya mbali kwamba Taqiyah inaruhusiwa hadi siku ya qiyama kama maelezo yaliyopita hapo kabla, na kuwa ni wajibu kusema uongo kama alivyosema Ghazali, na kudhihirisha kufru nayo ni mwenendo na makubaliano ya wanachuoni, kama alivyolikubali jambo hilo Arrazi, na pia kujuzisha Tabasamu kwa dhahiri na kulaani kwa ndani, kama alivyokiri Bukhar. Na ruhusa ya mtu kusema atakavyo na kumtia dosari Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kuchelea mali yake kama alivyobainisha jambo hilo mwenye Sira tul-Halabiyyah, na mtu kusema mambo ambayo ndani yake ni maasi kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwachelea watu kama alivyokiri jambo hili Suyuti.


Basi hapana litalo halalisha kebehi ya Masunni na upinzani wao dhidi ya Mashia kwa ajili ya itikadi ambayo wao wenyewe wanaisema na kuisimulia ndani ya Sihahi zao na Musnad zao. (Vitabu vyao) ya kwamba itikadi hiyo (ya Taqiyyah) inaruhusiwa bali ni wajibu. Na Mashia hakuna chochote walichoongeza juu ya vile wasemavyo Masunni isipokuwa wao (Mashia) wametambulikana mno kuliko wengine katika matumizi ya Taqiyyah, kutokana na mateso, dhulma, na maudhi waliyoyapata toka kwa watawala wa Kibanu Ummayyah na Banu Abbas, kwani katika zama hizo ilikuwa inatosha kabisa kwa mtu kusema kwamba: "Huyu ni mfuasi wa Ahlul-Bayt" ili apambane na kifo chake na kuuliwa kwa mauaji mabaya akiwa mikononi mwa maadui wa watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.). Hivyo basi ilikuwa hapana budi kwa Mashia kuitumia Taqiyyah kwa kufuata maelekezo ya Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.). Imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar As-Sadiq (a.s.) amesema:"Taqiyyah ni dini yangu na ni dini ya wazazi wangu" na amesema: "Asiyekuwa na Taqiyyah basi huyo hana dini".


Na bila shaka Taqiyyah ilikuwa ni kielelezo cha Maimamu wa Nyumba ya Mtume kwa kujikinga na madhara wao wenyewe na wafuasi wao na wawapendao pia kuhifadhi damu yao na kusuluhisha hali ya Waislamu waliofitiniwa katika dini yao kama alivyofitiniwa Ammar bin Yasir (r.a.) na wengine. Ama Masunni, wao walikuwa mbali na balaa hilo, kwani wao kwa kipindi kirefo walikuwa wakikubaliana na watawala, hivyo basi hawakusumbuliwa si kwa kuuawa wala kuporwa mali (zao) na dhulma (yoyote dhidi yao haikuwepo) basi moja kwa moja hali hiyo ikawafanya wawe wapinzani mno wa Taqiyyah na kuwakejeli wanaoitumia. Kwa hakika watawala wa Kibanu Umayyah na Kibanu Abbas walitoa mchango mkubwa kuwafanya Mashia watambulikane mno kuitumia Taqiyyah.


Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameteremsha Qur'an (ikazungumzia) Taqiyyah, (Qur'an ambayo) inasomwa na hukmu zinatekelezwa, na kwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) yeye mwenyewe aliitumia Taqiyah kama ilivyokudhihirikia ndani ya Sahih Bukhar. Kadhalika Mtume alimruhusu Ammar bin Yasir amtukane na akufuru iwapo makafiri watarudia tena kumuadhibu. Si hivyo tu bali wanachuoni wa Kiislamu wameruhusu jambo hilo kwa kufuata kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, sasa basi ni kejeli gani na ni upinzani gani baada ya yote haya utakaokubalika kuelekezwa kwa Mashia? Bila shaka Masahaba watukufu walitumia Taqiyyah katika zama za watawala waovu mfano wa Muawiyah ambaye alikuwa akimuuwa kila aliyekataa kumlaani Ali bin Abi Talib, na kisa cha Hujri bin Adiyyi Al-Kindi na jamaa zake ni mashuhuri. Na mfano (watawala waovu) ni kama vile kina Yazid, ibn Ziyad na Abdul-Malik bin Marwan na wengine kama hao. Na lau ningetaka kukusanya ushahidi wa matendo ya Masahaba kuhusu Taqiyah, basi ingelazimu kitabu kamili, lakini ushahidi niliouleta miongoni mwa dalili za Masunni unatosha, shukrani zote ni zake Mwenyezi Mungu. Na sitaiacha fursa hii ipite ila niwasimulie kisa kizuri kilichonitokea mimi binafsi (nikiwa) pamoja na mwanachuoni mmoja miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni ambaye tulikutana naye ndani ya ndege. Tulikuwa tumealikwa kuhudhuria mkutano wa Kiislamu huko Uingereza, na tukawa tunazungumza juu ya Ushia na Usunni kwa kipindi cha masaa mawili. Huyu mwanachuoni alikuwa miongoni mwa watu wanaolingania umoja (miongoni mwa Waislamu) na nilipendezwa naye, isipokuwa sikupendezwa na kauli yake aliposema kwamba: "Inabidi Mashia waziache baadhi ya itikadi ambazo zinasababisha Waislamu wahitilafiane na kukebehiana wao kwa wao."


Mimi nilimuuliza: "Kama itikadi gani"? Kwa haraka sana akajibu: "Kama vile Mut'a na Taqiyyah." Mimi nilijaribu kumkinaisha kwa uwezo wangu ya kwamba Mut'a ni ndoa ya kisheria na Taqiyyah ni ruhusa toka kwa Mwenyezi Mungu, lakini aliendelea na mtazamo wake na haikumkinaisha kauli yangu wala hoja zangu, akidai kwamba yote niliyoyaleta ni sahihi lakini inabidi kuyaacha kwa ajili ya Maslahi muhimu ambayo ni umoja wa Waislamu. Nilishangazwa sana na hekima hii inayoamuru kuacha hukumu za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya umoja wa Waislamu na nikamwambia kwa kumfurahisha tu ya kwamba: "Lau umoja wa Waislamu utasimama juu ya jambo hili basi nitakuwa wa mwanzo kuitikia".

Tulishuka uwanja wa ndege wa London, nami nilikuwa nikitembea nyuma yake, na pindi tulipowafikia askari wa uwanja wa ndege yeye aliulizwa sababu za yeye kuja Uingereza na akawajibu kwamba amekuja kwa ajili ya matibabu, nami nilidai kwamba nimekuja kuwatembelea jamaa zangu fulani. Basi tukapita kwa salama bila ya kucheleweshwa mpaka tukafika mahala pa kukaguliwa mizigo na hapo ndipo nilipomnong'oneza nikamwambia, "Waonaje, Taqiyyah ni jambo linalofaa katika nyakati zote"? Akasema, "Kwa vipi"? Nikamwambia "Hapana shaka sisi tumewadanganya askari hawa, mimi kwa mujibu wa kauli yangu nimesema kuwa nimekuja kuwatembelea jamaa zangu, nawe kwa mujibu wa kauli yako umesema kuwa umekuja kwa ajili ya matibabu, wakati ambapo sisi tumekuja kwa ajili ya mkutano".


Basi alitabasamu na akagundua kwamba amesema uongo mbele yangu hali ya kuwa ninamsikia, hivyo akasema: "Kwani katika mkutano wa Kiislamu si kuna matibabu ya nafsi zetu"? Mimi nilicheka huku nikisema: "Je, ndani ya mkutano huo si kuna kuwatembelea ndugu zetu"? Sasa ninarejea kwenye maudhui na ninasema kwamba, "Taqiyyah ilivyo, siyo kama wanavyodai Masunni kwamba eti ni namna fulani ya unafiki, bali kinyume chake ndiyo sahihi. Kwani unafiki ni kudhihirisha imani na kuficha ukafiri, wakati ambapo Taqiyyah ni kudhihirisha kufru na kuficha imani, na misimamo hii miwili iko mbali mbali kabisa. Msimamo huu yaani wa unafiki ni ule ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu ameusema (kama ifuatavyo):
"Na wanapokutana na wale walioamini husema tumeamini, na wanapokuwa faragha kwa mashetani wao husema sisi tuko pamoja nanyi, hakika sisi tunawacheza shere." Basi hii ndiyo imani kwa nje na ni kufru kwa ndani "Unafiki." Ama namna ya pili ya Taqiyyah ambayo Mwenyezi Mungu ameieleza (kama ifuatavyo): "Na akasema mtu mmoja muumini kutoka katika watu wa Firaun anayeficha imani yake." Hii ina maana ya kufru kwa nje na ni imani kwa ndani "Taqiyyah." Basi bila shaka muumini wa watu wa Firaun alikuwa akificha imani yake kwa ndani na hakuna aliyejua isipokuwa Mwenyezi Mungu na alikuwa akijidhihirisha kwa Firauni na watu wote kwamba yeye yuko kwenye msimamo wa dini ya Firaun. (Mwenyezi Mungu amemtaja ndani ya Kitabu choke kwa kuitukuza heshima yake). Ewe msomaji Mtukufu hebu twende pamoja ili upate kufahamu kauli ya Mashia juu ya Taqiyyah usije ukadanganyika na maneno ya uzushi na uongo yasemwayo juu ya Mashia.


Amesema Sheikh Muhammad Ridhaa Al-Mudhaffar ndani ya kitabu chake kiitwacho, "Aqaidul-Imamiyyah ". Ufuatao ndio usemi wake: "Taqiyyah inazo hukumu zake katika hali ya kuwa ni wajibu na kutokuwa wajibu kufuatana na tofauti ya mahala penye khofu ya madhara, (hukumu hizo) zimetajwa katika milango yake ndani ya vitabu vya wanachuoni wa Fiqh. Na Taqiyyah siyo wajibu katika kila hali, bali huenda ikajuzu au ikawajibika kinyume chake katika baadhi ya nyakati, kama vile itakapokuwa wakati wa kuidhihirisha haki na kuionesha kwa ajili ya kutetea dini na kuutumikia Uislamu na kuupigania katika njia yake, basi wakati huo mali hupuuzwa haipewi kima na wala nafsi hazipewi heshima (yaani haitoruhusiwa Taqiyyah ili kuokoa mali au kuokoa nafsi na dini iangamie). Na huenda Taqiyyah ikawa haramu katika matendo ambayo yanalazimisha kuua nafsi zinazo heshimika au (watu) kuzama katika batili au uovu ndani ya dini au madhara makubwa kwa Waislamu kwa kuwapotosha na kueneza dhulma na ujeuri miongoni mwao. Kwa vyovyote vile maana ya Taqiyyah kwa Shia siyo kuifanya Taqiyyah miongoni mwao kuwa ni Jumuiya ya siri kwa lengo la kuvunja na kuharibu - kama wanavyoidhania baadhi ya maadui zao wasio na upeo wa kufahamu mambo kwa mwelekeo wake na wala hawajilazimishi nafsi zao kufahamu mtazamo uliosahihi.


Kama ambavyo maana ya Taqiyyah siyo kuifanya dini na hukmu zake viwe ni mambo ya siri miongoni mwa siri ambazo haifai kuzitangaza kwa asiyefuata dini hiyo. Sasa basi inakuwaje (kudhaniwa vibaya) wakati Mashia wameandika ndani ya tunzi zao mambo yanayohusu Fiqhi, hukumu na uchambuzi wa maneno na itikadi zimejaa mashariki na magharibi na zimevuka mipaka inayotarajiwa na umma wowote unaofuata dini yake. Nawe msomaji bila shaka unaona ya kwamba, hakuna unafiki wala udanganyifu au uongo wala hadaa kama wanavyodai maadui wa Mashia.