ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

ISMAH
Mashia wanasema:"Tunaitakidi kwamba Imam ni kama Nabii, ni wajibu awe Maasum (mwenye kuhifadhika) kutokana na machafu yote na maovu yenye kudhihiri na yenye kufichikana tangu miaka ya utotoni mpaka kufa (asiyafanye hayo) kwa kukusudia au kusahau. Kama ambavyo ni wajibu Imam awe amehifadhiwa kutokana na kusahau, kukosea na kughafilika, kwa sababu Maimamu ndiyo walinzi wa sheria na ndiyo wenye kuisimamia, hivyo hali yao katika jambo hilo ndiyo hali ya Mtume. Dalili ambayo imetupelekea tuitakidi Ismah ya Manabii ndiyo hiyo hiyo iliyotupelekea tuitakidi Ismah ya Mamimau bila tofauti yoyote. Taz: Aqaidul-Imamiyah uk. 67. Naam hivi ndivyo tunavyoona, haya ni maoni ya Mashia kuhusu maudhui ya Ismah basi je, ndani ya itikadi hii kuna kitu kinachopinga Qur'an na Sunna? Au kuna ambacho akili inakipinga? Au kuna ambacho kinauharibu Uislamu na kuuvuruga, au kipo kinachoshusha heshima ya Mtume au Imam?


Hapana, kamwe hatukukuta ndani ya kauli hii isipokuwa ni kukiunga mkono kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake, na mambo ambayo yanakubaliana na akili iliyo salimika na wala hakuna kinachoipinga, na yamo mambo ambayo yananyanyua heshima ya Mtume na Imam na kumtukuza. Basi hebu na tuanze utafiti wetu kwa kuisoma Qur'an Tukufo. Mwenyezi Mungu amesema: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu na kukutakaseni sana enyi watu wa nyumba (ya Mtume)". Qur'an, 33:33 Iwapo kuondoshewa uchafu ambako kunakusanya mambo mabaya, na kutakaswa kutokana na kila dhambi hakufidishi Ismah, basi ni nini maana yake? Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika wale wanaomuogopa (Mwenyezi Mungu) zinapowagusa pepeso za shetani hukumbuka, basi mara huwa wamekwishaiona njia". (Qur'an, 7:201) Ikiwa Muumini mcha Mungu, Mwenyezi Mungu humuhifadhi kutokana na vitimbi vya Shetani pindi anapojaribu kumwita na kumpotosha, Muumini hukumbuka na kuiona haki kisha huifuata, hivyo basi unafikirije kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu amemteua na akamuondoshea uchafu na kumtakasa sana sana?

Na anasema Mwenyezi Mungu: "Kisha tumewarithisha (tumewapa) kitabu wale tuliowachagua miongoni mwa waja wetu". (Qur'an, 35:32) Na yeyote achaguliwaye na Mwenyezi Mungu Mtukufu bila shaka anakuwa ni Maasum (aliyehifadhiwa) kutokana na makosa. Aya hii ndiyo aliyoitolea hoja Imam Ridhaa ambaye yeye ni miongoni mwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) dhidi ya wanachuoni aliowakusanya Khalifa wa Kibani Abbas aitwaye Maamum bin Harun Rashid. Imam aliwathibitishia kwamba wao Maimamu wa nyumba ya Mtume ndiyo waliokusudiwa kwenye aya hii, na kwamba Mwenyezi Mungu amewachagua na kuwarithisha wao elimu au Kitabu (Qur'an), na hao wanachuoni walimkubalia juu ya jambo hilo. Taz: Al-I'Qdul-Farid cha ibn Abdirabbih Juz. 3 uk. 42.

Hii ni baadhi ya mifano iliyokuja ndani ya Qur'an Tukufu, na ziko aya nyingine zinazofidisha juu ya Ismah ya Maimamu, kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo: "Maimamu wanaoongoza kwa amri yetu." Na nyinginezo, lakini tunatosheka kwa kiasi hiki kwa nia ya kufupisha maelezo. Na baada ya Qur'an Tukufu hebu angalia maelezo yaliyokuja ndani ya sunna ya Mtume. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Enyi watu hakika mimi ninaacha kwenu vitu ambavyo mkivichukua hamtapotea, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu": Taz: 1). Sahih Tirmidhi Juz. 5 uk. 328. 2). Al-Hakim ndani ya Mustadrak Juz. 3 uk. 148. 3). Al-Imam Ahmad bin Hambal ndani ya Musnad yake Juz. 5 uk. 189. Kama unavyoona bayana kwamba Maimamu kutoka nyumba ya Mtume (s.a.w.) wamehifadhiwa. Kwanza: Ni kwa kuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu kimehifadhiwa, hakifikwi na upotofu kabla au baadaye ni maneno ya Mwenyezi Mungu, na mwenye kukitilia shaka basi amekufuru. Pili: Ni kwamba mwenye kushikamana navyo "Kitabu na kizazi cha Mtume" atasalimika kutokana na upotofu. Hivyo basi hadithi hii imejulisha kwamba kitabu na kizazi cha Mtume haiwezekani kuwa vinamakosa. Na amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): "Bila shaka mfano wa watu wa nyumba yangu ni kama Safina ya Nuhu, atakayeipanda ataokoka na mwenye kuiacha ataangamia".


Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 2 uk. 343, Kanzul-Ummal Juz. 5 uk. 95, As-sawaiqul-Muhriqah cha ibn Hajar uk. 184. Kama uonavyo ubainifu kuwahusu Maimamu kutoka nyumba ya Mtume (s.a.w.) kwamba wao ni Maasum (wamehifadhiwa) kutokana na makosa, na kwa ajili hiyo husalimika kila apandaye Safina yao na kila atayeacha kupanda Safina hiyo ataangamia katika upotofu. Na amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): "Yeyote atakayependa kuishi maisha niliyoishi mimi na afe kifo nilichokufa mimi na aingie ndani ya pepo ambayo Mola wangu ameniahidi nayo ni pepo ya milele, basi na amtawalishe Ali na watoto wake baada yake, bila shaka wao hawatakutoweni nje ya mlango wa uongofu na hawatakuingizeni ndani ya mlango wa upotofu". Taz:

1) Kanzul-Ummal Juz. 6 uk. 155.
2). Maj-Mauz-Zawaid cha Al-Haithami Juz. 9 uk. 108.
3). Al-isabah cha Ibn Hajar Ai-As-Qalani.
4). At-Tabrani ndani ya Al-Jamiul-Kabir.
5). Tarikh Ibn AsakirJuz. 2 uk. 99.
6). Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 128
7). Hilyatul-Auliyai Juz. 4 uk. 349. 8). Ihqaqul-Haqi Juz. 5 uk. 108.
Kama uonavyo ya kwamba Maimamu kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) ambao ni Ali na wanawe,
wamehifadhiwa kutokana na makosa kwani wao kamwe hawatawaingiza watu waliowafuata katika mlango wa upotofu. Na hapana upinzani kwamba mtu anayekosea haiwezekani kwake kuwaongoa watu.
Na amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.):
"Mimi ni muonyaji na Ali ni muongozaji, na kwako ewe Ali wataongoka wenye kuongoka baada yangu:
Taz: 1). Tafsir At-Tabari Juz. 13 uk. 108.
2). Tafsir Ar-Razi Juz. 5 uk. 271.
3). Tafsir ibn Kathir Juz. 2 uk. 502.
4). Tafsir Ash-Shaukani Juz. 3 uk. 70.
5) Ad-Durrul-Manthoor cha Suyuti Juz. 4 uk. 45.
6). Nurul-Ab-Sar uk. 71.
7). Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 129.
8). Tafsir ibn JauziJuz. 4 uk. 307.
9). Shawahidut-TanzilJuz. 1 uk. 293.
10). A 1-Fusulul-Muhimmah Na yanabiul-Mawaddah.

Hii ni hadithi nyingine iliyo bayana kabisa kuhusu Ismah ya Imam kama ambavyo haifichikani kwenye akili. Imam Ali kwa nafsi yake mwenyewe ameithibitisha Ismah kwake mwenyewe na kwa Maimamu miongoni mwa wanawe pale aliposema: "Mnakwenda wapi na ni vipi mnadanganywa hali ya kuwa muongozo upo na aya ziko wazi na minara imesimikwa, basi vipi mnapotoshwa bali ni jinsi gani mnapotea hali yakuwa miongoni mwenu kimo kizazi cha Nabii wenu ambao ni walinzi wa haki, na ndiyo muongozo wa dini na ndimi za ukweli, basi waheshimuni kwa heshima nzuri ya Qur'an na muwafuate kama ngamia mwenye kiu kali afuatavyo (maji). Enyi watu kichukuweni kutoka kwa Mtume wa mwisho (s.a.w.), hakika hufariki mwenye kufariki miongoni mwetu (sisi watu wa nyumba ya Mtume) lakini anakuwa hajafariki, na huchakaa mwenye kuchakaa miongoni mwetu lakini siyo kwamba amechakaa, basi msiseme msiyoyajua, kwani haki imo ndani ya vile mnavyovikanusha. Na toshekeni kwa mtu ambaye ninyi hamna hoja yoyote dhidi yake, nami ndiye huyo mtu, basi je, sikukitumia ndani yenu kizito kikubwa na ninakuachieni kizito kidogo nami nimesimika kwenu bendera ya Imani..."[92]


Taz: Nahjul-Balaghah ya Imam Ali Juz. 1 uk. 155. Na baada ya ubainifu huu kutoka ndani ya Qur'an Tukufu na sunna tukufu ya Mtume na kauli za Imam Ali ambazo zote zinajulisha juu ya Ismah yao (a.s.) basi hivi kweli akili itapinga Ismah ya wale aliowachagua Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya uongofu? Jawabu ni kwamba, kamwe haiwezi kupinga, kinyume chake ni kwamba akili inasema kuwa, kuna ulazima wa kuwepo hiyo Ismah kwani yeyote ambaye amewakilishwa wajibu muhimu wa uongozi na kuongoa watu haiwezekani awe ni mtu wa kawaida anayezukiwa na makosa, kusahau na kisha kushehenezwa madhambi na makosa halafu aaibishwe na akosolewe na watu. Bali akili inaona ni lazima awe mjuzi mno kuliko wengine katika zama zake na muadilifu, mchamungu, na shujaa kuliko wote, sifa ambazo zinapandisha cheo cha kiongozi na kumtukuza mbele za watu na kumletea heshima kwa wote na utukufu na hatimaye wakamtii bila ya woga.


Ikiwa hali ya mambo iko namna hiyo, basi yanini kebehi yote hii na vitisho dhidi ya wanao itakidi hivyo? Bila shaka imasikia na kusoma Masunni wanavyoikosoa maudhui ya Ismah kwa kusema kwamba, Mashia ndiyo wanaomvisha nishani ya Ismah yule wampendaye, au yeyote azungumzaye kuhusu kuthibiti kwa Ismah (kwao wao) huwa amesema jambo bay a na la kufru, basi si hili wala lile, bali Ismah kwa Mashia ni kuwa huyo Maasum awe amezungukwa na uangalizi na uhifadhi wa Mola ili shetani asiweze kumpoteza, na wala nafsi inayoamrisha maovu isiweze kuishinda akili yake ikampeleka kwenye maasi. Jambo hili Mwenyezi Mungu hakuliharamisha kwa waja wake wamchao kama ilivyotangulia katika ay a isemayo: "Wale ambao wamchao Mwenyezi Mungu unapowapata upepeso wa Shetani hukumbuka, basi mara huiona haki". Na hii Ismah iliyokadiriwa kwa waja wa Mwenyezi Mungu huenda ikaondoka kwa kukosekana sababu zake ambazo ni ucha Mungu kwa hiyo mja atakapokuwa mbali na ucha Mungu Mwenyezi Mungu hawezi kumuhifadhi. Ama Imamu ambaye Mwenyezi Mungu amemchagua, huyo hapotoki wala kulegalega kwenye ucha Mungu na kumuogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu.


- Bila shaka imekuja ndani ya Qur'an simulizi juu ya Bwana wetu Yusuf (a.s.): "Kwa'hakika mwanamke huyo alimkusudia (Yusuf) na (Yusuf) naye angemkusudia mwanamke yule, lau kama asingeona dalili toka kwa Mola wake, tumefanya hivyo ili tumwepushie kila jambo la ubaya na la uovu. Hakika yeye (Yusuf) ni miongoni mwa waja wetu waliotakaswa". (Qur'an, 12:24) Na kwa sababu Bwana wetu Yusuf hakukusudia kufanya zinaa kama walivyofasiri baadhi ya wafasiri, kwani haiwezekani kabisa kwa Manabii wa Mwenyezi Mungu kufanya tendo hili baya.

IDADI YA MAIMAMU (NI KUMI NA WAWILI)
Mashia wanasema kwamba idadi ya Maimamu Ma'asum baada ya Mtume (s.a.w.) hi kumi na wawili, hawazidi wala kupungua, na Mtume wa Mwenyezi Mungu amewataja kwa majina yao na idadi yao. Taz: Yanabiul-Mawaddah cha Al-Qanduzi Al-Hanafi uk. 99 Juz. 3. Nao ni hawa wafuatao:

1) Imam Ali bin Abi Talib
2) Imam Hasan bin Ali
3) Imam Husein bin Ali
4) Imam Ali bin Husein (Zainul-Abidin)
5) Imam Muhammad bin Ali (Al-Baqir)
6) Imam Ja'afar bin Muhammad (As-Sadiq)
7) Imam Musa bin Ja'afar (Al-Kadhim)
8) Imam Ali bin Musa (Ar-Ridha)
9) Imam Muhammad bin Ali (Al-Jawad)
10) Imam Ali bin Muhammad (Al-Hadi)
11) Imam Al-Hasan bin Ali (Al-Askari)
12) Imam Muhammad bin Al-Hasan (Al-Mahdi)

Basi hawa ndiyo Maimamu kumi na wawili ambao Mashia wanazungumza kuhusu Ismah yao ili baadhi ya Waislamu wasijegubikwa na vitimbi. Hivyo basi Mashia hawaitambui hapo zamani wala sasa hivi Ismah nyingine isiyokuwa ya Maimamu hawa ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwataja kabla hata hawajazaliwa, na baadhi ya wanachuoni wa Kisunni wameyathibitisha majina yao (hao Maimamu) kama ilivyotangulia (kuelezwa). Nao Bukhar na Muslim wamethibitisha ndani ya Sahih zao hadithi inayohusu Maimamu kwa idadi yao ambayo ni kumi na wawili na wote ni kutokana na Qur'aish. Taz: 1). Sahih Bukhar Juz. 8 uk. 127. 2). Sahih Muslim Juz. 6 uk. 3. Na hadithi hizi hazisimami wala hazisihi isipokuwa tutakapozifasiri kuwahusu Maimamu wa nyumba ya Mtume ambao Mashia Imamiyah ndiyo wanaowazungumzia, na Masunni wao ndio wanaotakiwa kutatua utata huu, kwani idadi ya Maimamu kumi na wawili ambayo wameithibitisha ndani ya vitabu vyao mpaka sasa kwao imebakia kuwa ni fumbo ambalo hawalipatii jawabu!

ELIMU YA MAIMAMU
Na miongoni mwa mambo ambayo Masunni huwakebehi Mashia ni kauli ya Mashia isemayo kwamba: "Maimamu kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.), Mwenyezi Mungu amewahusisha na elimu ambayo hakuwashirikisha pamoja na yeyote miongoni mwa watu, na kwa kuwa Imamu ni mjuzi mno kuliko watu wote wa zama zake, basi haiwezekani kwa yeyote kumuuliza Imam kisha akashindwa kutoa jawabu!! Basi je, madai haya yanayo dalili? Na tuanze na Qur'an kama ilivyo kawaida yetu katika kila uchambuzi tunaoufanya.. Mwenyezi Mungu anasema: "Kisha tumewarithisha (tumewapa elimu ya) kitabu wale ambao tumewateua miongoni mwa waja wetu". (Qur'an, 35:32) Aya hii inajulisha dalili iliyo wazi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameteua waja miongoni mwa watu na akawarithisha elimu ya Kitabu.


Basi je, tunaweza kuwafahamu waja hawa walioteuliwa? Hapo kabla tumeeleza kuwa Imamu wa nane miongoni mwa wale Maimamu wanaotoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) ambaye ni Ali bin Musa Ar-Ridhaa alitoa ushahidi ya kuwa aya hii ilishuka kuwahusu wao, na hali hii (aliisema) pindi Maamuni (Khalifa wa Banu Abbas) alipomkusanyia Imam (huyu) Maqadhi arobaini miongoni mwa Maqadhi mashuhuri, na kila mmoja wa Maqadhi hawa aliandaa mas-ala arobaini ili kumuuliza Imam Ali Ar-Ridhaa. Basi Imam (a.s.) aliwanyamazisha (alipowajibu wote bila kubabaika) na wao wakakiri kuwa yeye Imam ni mjuzi mno. ; Taz: Al-Iqdul-Farid cha ibn Abd Rabbih Juz. 3 uk. 42. Hivyo basi, ikiwa Imam huyu wa nane ambaye alikuwa hata hajafikia umri wa miaka kumi na minne wakati wa majadiliano kati yake na wanachuoni hao ambao walikiri juu ya elimu yake, basi vipi ishangaze (na kuwa ngeni) kauli ya Mashia isemayo kuwa Maimamu ni wajuzi mno, maadamu wanachuoni wa Kisunni wanakiri kuhusu hali hiyo kwa Maimamu. Ama tukitaka kufasiri Qur'an kwa Qur'an, basi tutapata aya nyingi zinazoelekeza maana moja, na zinabainisha kwamba Mwenyezi Mungu kwa hekima yake amewahusisha Maimamu kutoka ndani ya nyumba ya Mtume (s.a.w.) kwa elimu itokayo kwake, amewapa ili wawe ni Maimamu wa uongofu na taa za kuondosha kiza.


Mwenyezi Mungu anasema: "Humpa hekima amtakaye, na yeyote aliyepewa hekima, basi bila shaka amepewa kheri nyingi, na hawakumbuki ila wenye akili". (Qur'an, 2:269) Na amesema vile vile: "Basi ninaapa kwa maangukio ya nyota, na bila shaka hicho ni kiapo kikubwa lau kama mngejuwa, hakika hii ni Qur'an Tukufu, iliyowekwa ndani ya Kitabu kilichohifadhiwa (madhubuti) hapana atayekigusa (kukifahamu vyema) isipokuwa wale waliotakaswa". (Qur'an, 56:75-79) Mwenyezi Mungu ameapa katika aya hii kwa kiapo kikubwa ya kwamba Qur'an Tukufu inazo siri na maana za ndani zilizodhibitiwa, hawawezi kutambua maana zake na uhakika wake isipokuwa wale waliotakaswa, na hao waliotakaswa ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa sana sana.

Pia aya imejulisha kwamba, Qur'an ina undani ambao Mwenyezi Mungu amewahusisha kwa undani huo Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) na wala haiwezekani kwa asiyekuwa wao kuufahamu undani huo isipokuwa kupitia kwao. Hivyo basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ameelekeza juu ya ukweli huu akasema: "Msiwatangulie (Maimamu) mutaangamia, na wala msiwapuuze mtaangamia, na wala msiwafunze kwani wao ni wajuzi mno kuliko ninyi". Taz:
1). As-sawa'iqul-Muhriqah cha ibn HajarAsh-Shqfti uk. 148.
2). Ad-Durrul-Manthoor cha Suyuti Juz. 2 uk. 60.
3). Kanzul-UmmalJuz. 1 uk. 168.
4). Usudul-Ghabah Fii Maa'rifatis Sahabah Juz. 3 uk. 137.
Na kama alivyosema Imam Ali mwenyewe:
"Wako wapi wale waliodai kuwa wao wamebobea katika elimu kuliko sisi, huo ni uongo na ni dhulma dhidi yetu, Mwenyezi Mungu ametunyanyua sisi na wao akawatweza, na ametupa sisi wao akawanyima, na ametuingiza sisi wao akawatoa, kwetu sisi ndiko kunakoombwa uongofu na upotofu huondoka... Hakika Maimamu wanatokana na Quraish wamepandikizwa ndani ya tumbo hili toka kwa Hashim, haukubaliki Uimamu kwa asiyekuwa wao wala utawala haukubaliki toka kwa asiyekuwa wao." Taz: Nahjul-Balaghah Juz. 2 uk. 143, Muhammad Abdoh, Khutba namba 143. Na amesema Mwenyezi Mungu: "Waulizeni wenye kumbukumbu iwapo ninyi hamujui" (Qur'an, 16:43 na 21:7). Aya hii vile vile imeshuka kuwahusu Ahlul-Bait (a.s.).


Taz: 1). Tafsirut-Tabari Juz. 14 uk. 134. 2). Tafsir ibn Kathir Juz. 2 uk. 570. 3). Tafsirul-Qur-tubi Juz. 11 uk: 272. ;,. 4). Shawahidut-Tanzil cha Al-Haskani Juz.luk. 334. 5). Yanabiul-Mawaddah. 6). Ih-Qa-Qul-Haqq cha At-Tustari Juz. 3 uk. 482. Na inafidisha kwamba umma (wa Kiislamu) baada ya kuondoka kwa Mtume wake hauna budi kuwarejea Maimamu wanaotoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) ili kuufahamu ukweli, na bila shaka Masahaba (r.a.) walimrejea Imam Ali bin Abi Talib ili awabainishie yaliyokuwa yakiwatatiza, kama ambavyo watu walivyowarejea Maimamu wa nyumba ya Mtume kwa miaka mingi ili wapate kufahamu halali na haramu na wapate (kunywa) elimu yao na mwenendo wao. Na iwapo Abu Hanifah anasema: "Lau si miaka miwili, basi Nuu'man angeangamia" akikusudia miaka miwili aliyoitumia kusoma kwa Imam Jaa'far Sadiq (a.s.) Na Imam Malik naye anasema: "Jicho halijaona wala sikio halijasikia, wala halijapita wazo katika moyo wa mtu yeyote (kuwa kuna) mbora kuliko Jaafar As-Sadiq kwa utukufu, elimu, ibada, na ucha Mungu" Taz: Kitabu Manaqib Ali bin Abi Talib kuhusu mazingira ya Imam Jaafar As-Sadiq. Kama mambo yako namna hii, Maimamu wa Kisunni wanakiri, basi ni za nini kebehi zote hizi na upinzani huu ni wa nini baada ya kuwepo dalili zote hizi na (hasa) baada ya historia ya Waislamu wote (kukubali) kwamba Maimamu toka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) walikuwa ni wajuzi mno kuliko watu wote wa zama zao? Basi ajabu iko wapi kwa Mwenyezi Mungu kuwahusisha mawalii wake aliowachagua (akawahusisha) kwa hekima na elimu, akawafanya kuwa ni kigezo cha waumini na kuwa viongozi wa Waislamu?

Lau Waislamu wangelifuatilia dalili za wao kwa wao, bila shaka wangetosheka na kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wangekuwa umma mmoja unaopeana nguvu na pasingekuwa na tofauti wala madhehebu mengi. Lakini hapana budi yatokee yote hayo ili Mwenyezi Mungu apate kupitisha jambo ambalo lilikuwa lazima litendeke:"Kusudi aangamiae, aangamie kwa dalili iliyo wazi na anayezindukana azindukane kwa dalili iliyo wazi na Mwenyezi Mungu ni msikivu mjuzi" (Qur'an 8:42)

AL-BADA'U
Al-Bada'u: Ni kumdhihirikia kitu katika jambo fulani alilotaka kulifanya kisha rai yake kubadilika kuhusu jambo hilo na akafanya kitu ambacho hakuwa ameazimia kukifanya hapo kabla. Ama kauli ya Mashia kuhusu Al-Bada'u na kuinasibisha kwa Mwenyezi Mungu, na kebehi dhidi yao kwamba (Al-Bada'u) inawajibisha kutokujuwa na upungufu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kama watakavyo Masunni kuichukulia kwa maana hii, basi tafsiri hii ni potofu na wala Mashia hawasemi hivyo kamwe, na yeyote mwenye kuwanasibishia hilo bila shaka amewazulia. Zifuatazo ndizo kauli zao zinazowashuhudia tangu hapo zamani mpaka sasa. Amesema Sheikh Muhammad Ridha Al-Mudhaffar ndani ya kitabu chake kiitwacho "Aqaidul-Ima 'miyyah': "Al-Bada'u kwa maana hii ni muhali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwani (itakuwa) ni kutokujua na ni upungufu, na hili haliwezekani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu (kutokujuwa na kuwa mpungufu wa sifa) na wala Mashia hawasemi hivyo". Imam Jaa'far As-Sadiq amesema: "Mwenye kudai kwamba Mwenyezi Mungu amedhihirikiwa na kitu mdhihiriko wa majuto, basi mtu huyo kwetu sisi (atakuwa) amemkufuru Mwenyezi Mungu Mtukufu" Na amesema pia kwamba: "Mwenye kudai kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amedhihirikiwa na kitu ambacho jana alikuwa hakukifahamu basi mimi niko mbali naye".


Kwa hiyo basi "Al-bada'u" waisemayo Mashia haivuki mipaka ya Qur'an kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema: "Mwenyezi Mungu hufuta ayatakayo na huyathibitisha (ayatakayo) na kwake ndiko kwenye msingi wa Kitabu" (Qur'an, 13:39). Na kauli hii Masunni wanaisema kama waisemavyo Mashia, basi ni kwa nini wanaumbuliwa Mashia na wala Masunni hawaumbuliwi ambapo wao (Masunni) wanasema Mwenyezi Mungu anabadilisha hukumu na kugeuza muda na riziki? Ibn Mar-Dawaih na ibn Asakir wamethibitisha (mapokezi) toka kwa Ali (a.s.) kwamba yeye alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuhusu aya hii isemayo: "Mwenyezi Mungu hufuta ayatakayo na huyathibitisha (ayatakayo) na kwake ndiko kwenye msingi wa kitabu." Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwambia: "Nitakutuliza kwa tafsiri ya aya hii, na nitawatuliza umma wangu baada yangu kwa tafsiri yake, (Mtume akasema) Kutoa sadaka kwa namna inayostahiki na kuwatendea wema wazazi wawili, na kutenda mema (ni mambo) yanayobadilisha maovu kuwa mema, na yanaongeza umri (wa kuishi) na yanakinga misukosuko ya maovu"

Naye ibn Al-Mindhir na ibn Abi1 Hatim na Al-Baihaqi ndani ya Ash-Shuabi toka kwa Qais bin Ubba'd (r.a.) amesema: "Kuna jambo Mwenyezi Mungu hulitenda katika kila usiku wa kumi wa miezi mitukufu, ama katika usiku wa kumi wa mwezi wa Rajab, ndani yake Mwenyezi Mungu huyafuta ayatakayo na huyathibitisha ayatakayo. Na amethibitisha Abd bin Hamid, ibn Jarir na ibn Mundhir toka kwa Umar bin Al-Khatab (r.a.) kwamba yeye Umar alisema hali yakuwa anatufu Al-Qaaba: "Ewe Mwenyezi Mungu ikiwa umeniandikia uovu au dhambi basi ifute, hakika wewe unafuta ukitakacho na unakithibitisha ukitakacho, na kwako ndiko kwenye msingi wa kitabu hivyo basi fanya iwe ni wema na ni msamaha".


Taz: Ad-Durrul-Manthoor Juz. 4 uk. 661. Naye Bukhar ndani ya sahihi yake juzuu ya nne ukurasa sabini na nane (Kitabu Bad'il-Khalqi Babu Dhikri L-Malaikah) amethibitisha kisa cha ajabu kinachosimulia miiraji ya Mtume (s.a.w.) na kukutana na Mola wake; miongoni mwa aliyoyasema Mtume (s.a.w.) ni kama ifuatavyo: "Kisha nikafaradhishiwa sala khamsini, nikaondoka mpaka nikafika kwa Musa akasema: Je, kuna nini ulichofanya? Nikasema nimefaradhishiwa sala khamsini, akasema: Mimi nawajua mno watu kuliko wewe nimeshughulika na wana wa Israel sana, hakika ummati wako hautaweza, basi rudi kwa Mola wako umuombe (akupunguzie), nikarudi nikamuomba na akazifanya kuwa arobaini. Nikarudi tena kwa Musa akaniambia kama alivyoniambia kwanza nikarudi kwa Mola naye akanipunguzia zikawa thelathini, Ishirini, Kumi, kisha tano, nikaja kwa Musa akasema umefanya nini? Nikasema amezifanya kuwa sala tano, akasema kama kwanza. Nikamwambia, Nimesalimu amri. Pakanadiwa Hakika mimi nimepitisha faradhi zangu na nimewapunguzia waja wangu na nitakuwa nalipa kwa kila tendo jema moja thawabu kumi." Na ndani ya riwaya nyingine vile vile Bukhari ameinakili riwaya hiyo ameandika, Na baada ya Muhammad (s.a.w.) kurudi kwa Mola wake mara nyingi baada ya kufaradhishiwa sala tano, Musa (a.s.) alimtaka Muhammad (s.a.w.) arudi kwa Mola wake ili ampunguzie, kwani ummati wake hawawezi (kutekeleza) japo sala tano, lakini Muhammad (s.a.w.) alimjibu Musa; "Namuonea haya Mola wangu".


Taz: Sahih BukharJuz. 4 uk. 250 Babul-Miiraj, Sahih Muslim Juz. 1 uk. 101 mlango wa Israi ya Mtume na kufaradhishwa swala. Naam (msomaji) soma na uone maajabu ya itikadi hizi zisemwazo na wasimuliaji wa Kisunni, lakini pamoja na hayo Masunni wanawatukana Mashia ambao ni wafuasi wa Maimamu kutoka katika nyumba ya Mtume kuhusu kauli ya Al-Bada'u. Na hawa Masunni ndani ya kisa hiki wanaitakidi kwamba Mwenyezi Mungu alimfaradhishia Muhammad (s.a.w.) sala khamsini kisha baada ya Muhammad kumrudia Mwenyezi Mungu (mara nyingi) ikamdhihirikia azifanye kuwa arobaini kisha ikamdhihirikia baada ya Muhammad kumrejea mara ya pili akazifanya kuwa thelathini, kisha ikamdhihirikia baada ya kurejea mara ya tatu akazifanya zikawa ishirini kisha baada ya kumrejea mara ya nne akazifanya kuwa kumi, kisha ikamdhihirikia baada ya kumrejea mara ya tano Mwenyezi Mungu akazifanya zikawa sala tano.


Na tukifumbia macho suala la kukubali riwaya hii au kutoikubali, ni kweli kabisa kwamba kauli ya "Al-Bada'u" ni Aqida madhubuti inayokubaliana na mafunzo ya dini ya Kiislamu na msingi wa Qur'an. "Bila shaka Mwenyezi Mungu habadilishi mambo ya watu mpaka wabadilishe yaliyoko katika nafsi zao". Na lau siyo itikadi yetu - Masunni na Mashia - kwamba Mwenyezi Mungu anabadilisha na kugeuza, basi sala zetu na dua zetu zisingekuwa na faida wala sababu wala maana, kama ambavyo sote tunaamini kwamba Mwenyezi Mungu hubadilisha hukmu na kufuta sheria kutoka kwa Nabii mmoja hadi mwingine, na hata katika sheria ya Mtume wetu (s.a.w.) kuna nasikh na mansukh (aya inayofuta na inayofutwa), hivyo basi kauli kuhusu "Al-Bada'u" siyo kufuru wala siyo kutoka katika dini na haiwafalii Masunni kuwaumbuwa Mashia kwa ajili ya itikadi hii, kama ambavyo haiwafalii Mashia vile vile kuwaumbuwa Masunni. Na ukweli ulivyo mimi naiona hii riwaya ya miraji kuwa inawajibisha kumnasibishia ujinga Mwenyezi Mungu Mtukufu na inaitia dosari heshima ya mtu Mtukufu aliyetambulikana katika historia ya wanaadamu naye ni Mtume wetu Muhammad (s.a.w.), pale inaposema kwamba Musa alimwambia Muhammad "Mimi nawajua mno watu kuliko wewe", na pia riwaya hii inamfanya Musa kuwa ni mbora ambapo lau si yeye, basi Mwenyezi Mungu asingeupunguzia ummati Muhammad.


Nami nashindwa kufahamu ni vipi Musa alifahamu kwamba ummati Muhammad hawawezi hata sala tano wakati ambapo Mwenyezi Mungu hakulijua hilo na anawakalifisha waja wake jambo wasiloliweza akawafaradhishia sala khamsini? Na hebu Ewe ndugu msomaji, wewe na mimi kwa pamoja tupime ni vipi zitafaradhishwa sala khamsini kwa siku moja, basi hapatakuwa na shughuli yoyote wala kazi yoyote wala hakuna kusoma hata kutafuta riziki wala harakati yoyote au jukumu lolote, (na kama ni hivyo) basi mtu atakuwa kama Malaika aliyekalifishwa kwa sala na ibada tu. Na hebu fanya mahesabu mepesi ili none uongo wa riwaya hii. Ukizidisha dakika kumi ambazo ni muda unaokubalika kiakili kutekeleza faradhi moja ya sala ya jamaa (uzidishe) mara khamsini utakuja muda uliofaradhishwa (kwa ajili ya sala) ni masaa kumi, hivyo basi ni juu yako uvumilie au uikatae dini hii inayowakalifisha wafuasi wake mambo zaidi ya uwezo wanaoweza kuumudu na kuwafaradhishia wasiyoyaweza.


Basi ikiwa Masunni wanawakebehi Mashia kwa kusema kwao juu "Al-Bada'u", na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hubadilisha na kugeuza vile apendavyo, hivyo ni kwa nini wao wenyewe hawajikosoi kuhusu kauli yao kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amegeuza na kubadilisha hukumu mara tano katika faradhi moja ndani ya usiku mmoja ambao ni usiku wa miraji? Mwenyezi Mungu ailaani chuki ya upofu na upinzani mbaya ambao unafunika ukweli na kuugeuza chini juu. Basi mtu mwenye chuki anamshinikiza anayemkhalifu katika maoni na kumpinga kwa mambo yaliyo wazi, kumkebehi, kueneza uzushi dhidi yake na vitisho kutokana na mambo ya kawaida ambayo yeye anayo makubwa kuliko hayo. Hali hii inanikumbusha yale aliyoyasema Bwana wetu Isa (a.s.) kuwaambia Wayahudi aliposema: "Ninyi mnatazama kapi kwenye macho ya watu, na wala hamtazami boriti lililoko machoni kwenu". Au kwa mfano wa msemaji aliposema: "Alinitupia maradhi yake na akatokomea"


Na huenda mtu fulani anaweza akapinga (akasema) kwamba tamko la "Al-Bada'u" halikutoka kwa Masunni, na kwamba kisa hiki (baina ya Mtume Muhammad na Mtume Musa) pamoja na kuwa maana yake kinajulisha juu ya kuweko mabadiliko katika hukmu, lakini haiwezekani kukata shauri kuwa lilimdhihirikia Mwenyezi Mungu. Nami ninasema hivi, kwa kuwa ni mara nyingi nilikuwa nikikieleza kisa cha Miiraji ili kutolea ushahidi wa kauli ya "Al-Bada'u" kwa Masunni, basi baadhi yao walinipinga juu ya rai hii, lakini baadaye waliikubali na niliwasimamisha kwenye riwaya nyingine kutoka ndani ya Sahih Bukhari inayoitaja "Al-Bada'u" kwa tamko lililo wazi bila ya utatanishi. Bukhari ameeleza maelezo yaliyotoka kwa Abu Hurairah kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Hakika kulikuwa na watu watatu miongoni mwa Bani Israeli mwenye mbaranga, kipofu na mwenye upara, Mwenyezi Mungu akaona awape mtihani, akawatumia Malaika, Malaika akamuendea mwenye mbaranga akamwambia, ni kitu gani ukipendacho mno, akasema, (napenda) rangi nzuri na ngozi nzuri (ya mwili) watu wamenichukia (kwa ubaya wa ngozi yangu) basi Malaika akampangusa na ugonjwa ule ukamuondokea, akampa rangi nzuri na ngozi nzuri, kisha akamwambia ni mali ipi uipendayo, akasema, ngamia, basi akapewa ngamia mwenye mimba. Kisha Malaika yule akamwendea mwenye kipara akamwambia, ni kitu gani ukipendacho mno, akasema, nywele nzuri na hiki kipara kiniondokee, watu wamenichukia (kwa ajili hii) basi Malaika akampangusa na kipara kikaondoka na akapewa nywele nzuri, kisha Malaika akamwambia, ni mali gani uipendayo, akasema ngombe, basi akampa ngombe mwenye mimba. Halafu Malaika akamwendea kipofu akamwambia, ni kitu gani ukipendacho mno, akasema, Mwenyezi Mungu ayarudishe macho yangu, basi akampangusa na Mwenyezi Mungu akamrudishia macho yake akamwambia ni mali gani uipendayo, akasema, mbuzi, basi akampa mbuzi mwenye kuzaa...


Ulipita muda fulani, yule Malaika alirudi baada ya ngamia, ng'ombe na mbuzi walipokuwa wengi kwa watu hawa kiasi kila mmoja wao akawa anamiliki kikundi (cha wanyama hao) basi akawaendea mwenye mbaranga na mwenye kipara na yule kipofu na kila mmoja wao akiwa katika hali yake, na akamtaka kila mmoja wao ampe alicho nacho, basi yule mwenye kipara na mwenye mbaranga wakamkatalia, na Mwenyezi Mungu akawarudisha katika hali yao waliyokuwa nayo hapo zamani, (ama) yule kipofu yeye akampa (Malaika alichokitaka) Mwenyezi Mungu akamzidishia na akambakishia macho yake. Taz: Sahih Bukhar Juz. 2uk. 259.

Na kwa sababu hii basi mimi nawaambia ndugu zangu (Masunni) ile kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Enyi mlioamini (watu fulani) wanaume wasiwakebehi wanaume (wengine) huenda wakawa bora kuliko wao, wala wanawake fulani wasiwakebehi wanawake (wengine) huenda wakawa bora kuliko wao, wala msijiaibishe wenyewe na wala msiitane majina mabaya, jina baya la ufasiki ni lile (aitwalo mtu) baada ya imani, na wasiotubu hao ndio madhalimu." (Qur'an, 49:11) Ni kama ambavyo natamani kwa moyo wangu wote kwamba Waislamu wangerejea kwenye muongozo wao, na waipuuze chuki (iliyojengeka baina yao) na waache ushabiki ili akili ipate kutulia mahala pake katika kila uchambuzi (unaofanywa) hata kama (uchambuzi huo) utafanywa na mpinzani wao, na wajifunze kutoka ndani ya Qur'ani Tukufu taratibu za uchambuzi na majadiliano kwa njia iliyo bora zaidi.


Bila shaka Mwenyezi Mungu alimpelekea ufunuo Mtume wake (s.a.w.) awaambie wapinzani, "Bila shaka ni sisi au ninyi, (kuna ambaye) yuko juu ya uongofu au katika upotofu uliodhahiri" (Qur'an, 34:24). Basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anaipandisha daraja ya washirikina hawa, naye anajiteremsha na kuwapa sehemu fulani itakayowafanya walete dalili zao na hoja zao ikiwa wanasema kweli. "Basi sisi tuko wapi kutokana na hii tabia tukufu (ya Mtume (s.a.w.)?