ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

UFAFANUZI JUU YA UKHALIFA
UFAFANUZI JUU YA UKHALIFA NDANI YA QADHA'A NA QADAR Cha ajabu katika maudhui hii ni kwamba, Masunni pamoja na itikadi yao juu ya Qadhaa na Qadar na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu yeye ndiye anayewaendesha waja wake katika matendo yao na kwamba wao hawana hiyari kwa lolote lile, lakini Masunni haohao kuhusu jambo la Ukhalifa wanasema kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikufa na akaliwacha jambo hilo kuwa ni la mashauriano baina ya watu ili wao wenyewe wafanye uchaguzi. Nao' Mashia wako kinyume kabisa (na Masunni), kwani pamoja na itikadi yao kwamba watu ni wenye kuhiyarishwa katika matendo yao na kwamba waja wa Mwenyezi Mungu wanafanya wayatakayo (kulingana na kauli isemayo kuwa hapana kutenza nguvu wala uhuru usio mpaka, lakini kuna jambo moja baina ya mawili hayo) isipokuwa wao (Mashia) kuhusu Ukhalifa wanasema kwamba (wanaadamu) hawana haki ya kumchagua Khalifa! Na hapa inadhihiri kama kwamba kuna kupingana katika pande mbili hizo za Kisunni na Kishia toka hapo mwanzo, lakini ukweli hauko namna hiyo.


Masunni wanaposema kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye ambaye anayewaendesha waja wake katika matendo yao wanapingana na ukweli halisi, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu (kwao wao) ndiye mwenye utashi wa utendaji, lakini yeye Mwenyezi Mungu anawaachia waja utashi wa kufikiria tu, kwani aliyemchagua Abubakr siku ile ya Saqifah ni Umar, kisha baadhi ya Masahaba lakini wao hao ni wenye kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu ambaye amewafanya wao wawe ni njia tu si vinginevyo, haya ni kwa mujibu wa madai yao.

Amma Mashia pindi wanaposema kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa hiari (utashi) waja wake katika matendo yao, siyo kwamba wanapingana na kauli yao, kwani suala la Ukhalifa liko katika utashi wa Mwenyezi Mungu peke yake,- Na Mola wako anaumba akitakacho na ndiye mwenye kuchagua, wao hawana hiyari (katika hilo), - hii ni kwa kuwa Ukhalifa ni kama Utume siyo katika matendo ya waja na wala halikuwakilishwa kwao. Basi kama ambavyo Mwenyezi Mungu anavyomchagua Mtume wake kutoka miongoni mwa watu na kumtuma kwao, basi ndivyo hivyo hivyo kumuhusu Khalifa wa Mtume, na watu wanaweza kutii amri ya Mwenyezi Mungu na wanaweza wakaiasi kama hali halisi ilivyotokea zama za uhai wa Mitume katika zama zote. Hapo waja wanakuwa huru kukubali utashi wa Mwenyezi Mungu, muumini mwema atakubali alichokichagua Mwenyezi Mungu, na mwenye kukufuru neema ya Mola wake atakipinga kilichochaguliwa na Mwenyezi Mungu na atakifanyia ufidhuli.

Mwenyezi Mungu amesema:
"Basi yeyote atakayefuata muongozo wangu hatapotea wala hataaibika, na atakayepuuza mawaidha yangu, basi bila shaka atakuwa na maisha ya dhiki na siku ya Kiyama tutamfufua hali yakuwa ni kipofu, aseme ewe Mola wangu mbona umenifufua kipofu na hali nilikuwa nikiona? Mwenyezi Mungu atasema hivyo ndivyo, zilikujia aya zetu ukazipuuza kadhalika leo unapuuzwa. (Qur'an 20:123-126). Kisha hebu itazame nadharia ya Masunni juu ya jambo hili huenda usimtwishe lawama mtu yeyote kwani kila kilichotokea na kinachotokea kwa sababu ya Ukhalifa na damu zote zilizomwagika na kuvunjwa heshima (za vitu vitakatifu) yote hayo yanatokana na Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba baadhi ya Masunni wanaodai kuwa na elimu waliambatisha (matukio hayo) na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Lau Mola wako angetaka basi wasingeyafanya." (Qur'an, 6:112). Ama nadharia ya Mashia yenyewe inambebesha jukumu kila aliyesababisha upotofu na kila aliyeasi amri ya Mwenyezi Mungu, na kila mmoja kwa kadiri ya kosa lake na kosa la waliofuata uzushi wake mpaka siku ya kiyama: "Kila mmoja wenu ni mchunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu uchunga wake".

Mwenyezi Mungu amesema: "Wasimamisheni, bila shaka wao ni wenye kuulizwa" (Qur'an, 37:24).

KHUMS (1/5)
Khums vile vile ni miongoni mwa maudhui ambazo Mashia na Masuni wamehitilafiana ndani yake. Na kabla ya kuhukumu dhidi yao au kuwapasisha, hapana budi tufanye uchambuzi kwa kifupi juu ya maudhui ya Khums. Basi na tuanze na Qur'an tukufu: Mwenyezi Mungu anasema: "Na jueni ya kwamba chochote mnachokipata, basi sehemu yake ya tano (Khums) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume na Qaraba wa Mtume na Mayatima na Masikini na Wasafiri". (Qur'an, 8:41)


Naye Mtume (s.a.w.) amesema: "Nakuamuruni mambo manne:"Kumuamini Mwenyezi Mungu, na kusali Sala, na kutoa zaka na kufunga Ramadhan na mtoe (Khums) sehemu ya tano ya kile mnachokipata kwa ajili ya Mwenyezi Mungu". Taz: Sahih Bukhar Juz. 4 uk. 44. Basi Mashia kwa kufaata amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) huwa wanatoa sehemu ya tano (Khums) ya kile walichokipata kwa muda wa mwaka, na wanafasiri maana ya "Ghanimah" kuwa ni kila anachokipata mtu katika faida kwa ujumla. Ama Masunni wao wameafikiana kuhusisha Khums kwenye ngawira za vita peke yake na wakaifasiri kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Na jueni kwamba chochote mlichokiteka (mlichokipata) wakakusudia kuwa "Mlicho kipata katika vita ". Huu ni ufupi tu wa kauli za pande mbili- kuhusu Khums, na bila shaka wanachuoni wa pande mbili hizi wameandika makala nyingi tu kuhusu mas-ala haya.

Nami binafsi sijuwi ni vipi nitaikinaisha nafsi yangu na au mtu mwingine juu ya maoni ya Masunni ambayo nadhani yametegemea kauli za watawala wa kibanu Umayyah wakiongozwa na Muawiyah bin Abi Sufiyan ambaye alijinyakulia kila aina ya mali za Waislamu na kuzifanya kuwa ni zake yeye na jamaa zake. Basi kwa Masunni siyo ajabu kubadilisha aya ya Khums na kuifanya ihusike na uwanja wa vita tu, kwani mfumo wa aya tukufu umekuja ndani ya aya zinazohusu vita na-mapigano, na Masunni wanazo aya nyingi walizozibadilisha kwa kutegemea aya zilizokuja kabla yake au baada yake. Wao wanabadilisha, kwa mfano aya ya kuondolewa uchafu na kutakaswa mno watu wa nyumba ya Mtume, kwamba aya hiyo inahusika kwa wakeze Mtume kwa kuwa kilicho kabla yake na kilicho baada yake kinazungumzia wakeze Mtume (s.a.w.). Kama ambavyo wanaibadilisha kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: (Na ambao wanalimbikiza dhahahbu na fedha na hawazitoi katika njia ya Mwenyezi Mungu wabashirie adhabu kali) kwamba aya hii ni makhsusi kwa Ahl-kitabi (watu wa Kitabu, Wayahudi na Wakristo).


Na kisa cha Abu Dhar Al-Ghifa'ri (r.a.) yeye pamoja na Muawiyah na Uthman bin A'ffan na (jinsi Uthman) alivyomfukuza Abu Dhar toka Madina na kumpeleka Rub-Dhah kwa ajili ya jambo hilo (la kulimbikza dhahabu na fedha), ni kisa mashuhuri, kwani Abu dhar aliwakosoa kulimbikiza kwao dhahabu na fedha na alikuwa akitolea hoja kwa aya hii, lakini Uthman alimtaka ushauri Kaab Al-Ahbar kuhusu aya hiyo, naye akamwambia kuwa aya hiyo ilishuka maalum kwa Ahlul-Kitab. Abu-Dharr alimshutumu na kumwambia huyo Kaab "Umeangamia ewe mwana wa Kiyahudi, Je, wewe unatufundisha dini yetu?" Kwa ajili hiyo Uthman alikasirika kisha alimfukuza Abu-Dhar toka Madina akampeleka Rub-Dhah baada ya makemeo makubwa ya Abu-Dhar dhidi ya Uthman, Abu-Dharr alikufa huko akiwa peke yake na binti yake, hakupata hata mtu wa kumkosha na kumkafini. Masunni wanayo fani maarufu ya kubadili aya za Qur'an na hadithi za Mtume na wanayo elimu mashuhuri (kuhusu hilo) nayo ni kule kufuata (kwao) yale waliyoyabadilisha Makhalifa wa mwanzo na Masahaba Mashuhiri kuhusu maandiko yaliyowazi katika Kitabu na Sunna.[91]


Na lau tungetaka kulieleza hilo kwa undani basi ingebidi kuandika kitabu maalum, inatosha kwa mchunguzi arejee kitabu kiitwacho An-Nasu Wal-Ij-Tihad ili apate kufahamu ni vipi wabadilishaji walivyozichezea hukmu za Mwenyezi Mungu Mtukufu.. Nami kama mtafiti siwezi kuzibadili aya za Qur'an na hadithi za Mtume vile nipendavyo au kama yanavyonikalifisha Madhehebu yangu ninayoyafuata. Lakini sina njia iwapo Masunni wenyewe ndiyo ambao wamethibitisha ndani ya vitabu vyao sahihi kuwa Khums ni faradhi (kutolewa) mahala pasipo na vita, kwa ajili hiyo wakaitengua taawili yao na madhehebu yao (wakayatengua). Imekuja ndani ya Sahihi Bukhari katika mlango wa (Rikazut-Khums), Na amesema Malik na ibn Idris kwamba "Rikaz ni mali iliyo katika zama za Jahiliya, ikiwa kidogo au nyingi itolewe Khums na madini siyo Rikaz, na Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema, Ndani ya madini hapana kitu na katika rikaz itolewe Khums.


Taz: Sahihi Bukhari Juz. 2 uk. 237 mlango wa Rikaz na Khums: Na imekuja ndani ya mlango wa vinavyotolewa baharini: Ibn Abbas (r.a.) amesema:"Nyangumi siyo katika rikaz, 'ni kitu ambacho bahari imekitoa", na amesema Hasan kuhusu Nyangumi na lulu, kuwa (hutolewa) Khums, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ameweka khums katika rikaz na si katika kitu ambacho hupatikana ndani ya maji. Taz: Sahihi Bukhari Juz: 2 uk. 136, "Babu Maa-yustakhraju minal-bahr. Na mchunguzi yeyote atafahamu kwa kupitia hadithi hizi kwamba machumo ya Ghanimah ambayo Mwenyezi Mungu amewajibisha khumsi ndani yake hayahusiki na mali ya uwanja wa vita pekee yake kwani rikaz ambayo ni hazina inayochimbuliwa ardhini ni miliki ya aliyeichimbua, lakini ni wajibu kutoa khums katika hazina hiyo kwa kuwa ni kipato.


Kama ambavyo mwenye kumvua nyangumi na lulu kutoka baharini inawajibikia kutoa khums kwani ni kipato. Na kutokana na hadithi alizozithibitisha Bukhar ndani ya sahihi inatubainikia kwamba khums haihusu kipato cha vita peke yake. Basi maoni ya Mashia siku zote yanabakia kuwa ni uthibitisho wa ukweli ambao haupingani ndani yake wala hauhitilafiani, na hiyo ni kwa kuwa wao katika hukmu zao na itikadi zao huwarejea Maimamu waongofu ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa mno, nao ndiyo wenza wa Qur'an, hapotei mwenye kushikamana nao na hupata amani mwenye kuwategemea. Hiyo ni kwa sababu hatuwezi kutegemea vita ili kuisimamisha dola ya Kiislamu na jambo hilo linakwenda kinyume na moyo safi wa Uislamu na wito wake wa amani, kwani Uislamu siyo dola ya kikoloni inayosimama (kuimarika) kwa kuyakalia mataifa na kuyapora uchumi wake jambo ambalo tawala za kimagharibi zinajaribu kutuhusisha nalo pale wanapomzungumzia Mtume wa Uislamu kwa kila aina ya dharau na wanasema kwamba, yeye Mtume alieneza Uislamu kwa nguvu na shinikizo la upanga ili kuyakalia mataifa mengine.


Na ilivyokuwa mali ni nguzo ya maisha na hasa ikiwa nadharia ya uchumi wa Kiislamu iriasisitiza juu ya kuanzisha kile ambacho leo hii kinaitwa kuwa ni Bima ya kijamii ili kuwadhamini maisha yao wale wenye dhiki na wasiojiweza kwa heshima, basi haiwezekani kwa dola ya Kiislamu kutegemea kile wanachokitoa Masunni katika zaka, kiasi ambacho katika hali nzuri kinalingana na asilimia mbili na nusu na hicho ni kiwango kidogo mno hakiwezi kusimamia mahitaji ya dola katika kuandaa nguvu na kujenga mashule, hospitali na kurahisisha mawasiliano, licha ya kumdhamini mtu mmoja mmoja kwa kipato cha kutosheleza mahitaji yake na kuyadhamini maisha yake, kama ambavyo haiwezekani kwa dola ya Kiislamu kutegemea vita zinazomwaga damu na muaji ya watu ili tu idhamini kuwepo kwake na kuendeleza taasisi zake kwa hesabu za waliouawa ambao hawakuutaka Uislamu.


Kwa hiyo Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) wao walikuwa ni watambuzi mno wa makusudio ya Qur'an, basi ni kwa nini isiwe hivyo wakati wao ndiyo wafafanuzi wa hiyo Qur'an, na walikuwa wakiiwekea mipango dola ya Kiislamu kuhusu mafundisho ya uchumi na jamii lau kama wangekuwa wanakubalika. Lakini kwa masikitiko makubwa ni kuwa utawala na uongozi ulikuwa mikononi mwa watu wengine, watu ambao waliupora Ukhalifa kwa nguvu na shinikizo, kwa kuwauwa watu wema miongoni mwa Masahaba na kuwateka kama alivyofanya Muawiyah, na walizibadilisha hukmu za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maslahi yao ya kisiasa na kidunia, basi wao wenyewe wakapotea na kuwapoteza wengine na kuuacha umma huu ukiwa chini ya unyonge ambao haukuweza kujikwamua mpaka leo hii. Hivyo basi mafunzo ya Maimamu wa Ahlul-Bayt yamebakia kuwa ni fikra na nadharia inayoaminiwa na Mashia, nao hawakupata hata hiyo nafasi ya kuziambatanisha kimatendo, kwani Mashia hao walikuwa wakifukuzwa mashariki na magharibi ya ulimwengu (kutokana na kuadhibiwa), si hivyo tu bali watawala hao wa Kibanu Umayah na Bani Abbas waliwafuatilia Mashia katika zama zote.


Wakati dola mbili hizo zilipovunjika na Mashia wakaanzisha jamii (yao), hapo ndipo walipoutenda utekelezaji wa Khums ambayo walikuwa wakiitoa kwa Maimam (a.s.) kwa siri, na leo hii wanaitoa (hiyo Khums) kwa Mar-jaa wanayemqalid (kufuata Fat-wa zake) kwa niyaba ya Imam Mahdi (a.s.). Hawa Mar-jaa huisimamia hiyo khums kwa kuigawa katika sehemu zinazohusika kisheria, miongoni mwake ikiwa ni taasisi na vyuo vya elimu na sehemu zingine na kheri na maktaba za Jumuiya, na majumba ya mayatima na mahala pengine katika sehemu za mambo matukufu kama vile kulipa posho ya mwezi kwa wanafunzi wa elimu ya dini na maarifa mengine na pia mambo mengine (ya kheri) yasiyokuwa hayo.

Na inatutosha kutokana na maelezo haya kupata natija kuwa wanachuoni wa Kishia hawaitegemei serikali, kwani khums inatosheleza mahitaji yao na wao husimamia kumpa haki kila mwenye haki yake. Ama wanachuoni wa Kisunni wao wanategemea watawala na maofisa wa serikali katika nchi, na hapo ndipo mtawala anapopata nafasi ya kumkurubisha amtakaye miongoni mwao na au kumtenga (amtakaye) kufuatana na ushirikiano wao hao wanachuoni wa Kisunni na ofisa huyo ikiwemo kutoa kwa Fat-wa kwa maslahi yake. Kutokana na hali hiyo mwanachuoni (wa Kisunni) anakuwa yu karibu mno na mtawala kiasi cha kuwa mwanachuoni tu (haangalii maslahi ya dini) na hizo ndizo baadhi ya athari zenye madhara ambayo yameifanya faradhi ya khums isitumike kwa ile maana yake ambayo watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) walivyo ifahamu.


TAQ-LIID
Mashia wanasema: "Ama Furuud-Din ambazo ni hukmu za kisheria zinazohusika na matendo ya kiibada, kama vile Sala, Saumu, Zaka na Hijja, ni wajibu katika hukmu za mambo hayo lipatikane moja kati ya mambo matatu:
1) Mtu ajitahidi na achunguze dalili za hukmu kama anao ustahiki wa kufanya hivyo (uwezo wa elimu).
2) Au awe ni mwenye Ih-Tiyat katika matendo yake ikiwa anaweza kufanya Ih-Tiyat.
3) Au amfuate, Muj-Tahid ambaye amezimiliki sharti (za Ij-Tihad) na awe hai huyo anayemfuata, mwenye akili, muadilifu, mwenye elimu, mwenye kuihifadhi nafsi yake, mwenye kuheshimu dini yake, mwenye kuyapinga matamanio yake na mwenye kutii amriza Mola wake.
Na hii Ij-Tihad katika hukmu za furui ni wajibu wa kutosheleza (Wajibul-Kifayah) kwa Wasialmu wote, basi atapojitokeza mtu ambaye zimetimia kwake sharti, wajibu huo huondoka kwao Waislamu wengine, na hufaa kwao kumfuata huyo na kumrejea katika Furui za dini yao, kwani daraja ya Ij-tihad siyo katika mambo mepesi wala haipatikani kwa kila mtu bali inahitaji muda mwingi na elimu kubwa, maarifa na uchunguzi, na haya hayatengeneki isipokuwa kwa mtu mwenye bidii na juhudi na akautumia umri wake katika utafiti na kujifunza na hawapati Ij-tihad isipokuwa wale wenye hadhi tukufu.


Mtume (s.a.w.) amesema: "Yeyote ambaye Mwenyezi Mungu amemtakia kheri, humtaalamisha katika dini". Na kauli hii ya Mashia haitofautiani na kauli ya Masunni., isipokuwa katika sharti la kuwa hai yule Muj-Tahid. Tofauti iliyo bayana baina ya Mashia na Masunni ni katika kuitenda hiyo Taqlid, wakati ambapo Mashia wanaitakidi kuwa Muj-Tahid ambaye ametimiza sharti zilizotajwa ni naibu wa Imam (a.s.) katika hali ya kuwa kwake katika ghaibah (haonekani), basi Muj-Tahid ndiye mtawala na kiongozi kwa kila kitu, anayo haki aliyo nayo Imam katika kuamua mambo na kuhukumu baina ya watu. Hivyo basi Muj-Tahid aliyetimiza sharti kwa Mashia siyo mwenye kurejewa tu katika Fat-wa, bali anao utawala wote juu ya wafuasi wake, watamrejea katika hukmu na maamuzi baina yao katika yale waliyotofautiana miongoni mwa maamuzi, na watampa zaka na khums ya mali zao, azitumie kama inavyomuwajibishia sheria kwa niyaba ya Imam wa zama (a.s.) Ama kwa Masunni, Muj-Tahid hana daraja hii, lakini wao humrejea katika mas-ala ya Kifiqh mmoja wa Maimamu wa Madhehebu manne, ambao ni Abu Hanifa , Malik, Shafii na Ah-mad bin Hanbal, na hawa Masunni wa leo huenda wakakosa kulazimika kumfuata Imam mmoja maalum miongoni mwa hawa, kwani hupata wakachukua baadhi ya mas-ala toka kwa mmoja wao, na mas-ala mengine wakachukua kwa mwingine kufuatana na yanavyopelekea mahitaji yao, kama alivyofanya Sayyid Sabiq ambaye ametunga Fiqh iliyochukukuliwa toka kwa Maimamu hao wanne.


Hiyo ni kwa kuwa Masunni wanaitakidi kwamba kuna rehma ndani ya kuhitilafiana (wao kwa wao), kwa mfaho anayefuata Madhehebu ya Malik anaweza kufuata maoni ya Abu Hanifa pindi atakapokuta ufumbuzi wa tatizo lake ambalo huenda asiukute ufumbuzi wake kwa Malik. Nitapiga mfano juu ya jambo hilo ili imbainikie msomaji apate kufahamu makusudio hayo: Katika kikao cha Mahakama moja huko kwetu Tunisia kulikuwa na msichana aliyempenda mtu fulani na akataka aolewe na mtu huyo, lakini baba ya msichana huyo alikataa kumuoza binti huyo kwa kijana huyo kwa sababu ambazo Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye, basi yule binti akatoroka nyumbani kwa baba yake na akaolewa na kijana yule bila idhini ya baba yake, hapo ndipo baba yake alipopeleka mashitaka mahakamani dhidi ya ndoa hii.

Binti yule na mumewe walipofika mbele ya Qadhi na hakimu akamuuliza yule binti sababu ya kutoroka nyumbani na kuolewa bila idhini ya walii wake alisema: "Ewe Bwana wangu, umri wangu ni miaka ishirini na tano na nilipenda kuolewa na mume huyu kwa mujibu wa muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kwa kuwa baba yangu anataka kunioza mtu nisiyemtaka, basi nimejiozesha kwa mujibu wa maoni ya Abu Hanifah ambayo yananipa haki ya kuolewa na mtu nimtakaye kwani mimi tayari nimekwisha vunja ungo.


Basi yule Qadhi (Mwenyezi Mungu amrehemu ambaye yeye binafsi alinisimulia kisa hiki) anasema: "Basi tukayafuatilia mas-ala haya na tukamkuta yule msichana anayo haki, nami ninaamini kuwa kuna mwanachuoni fulani ambaye ni mtafiti ndiye aliyemuelekeza ni jambo gani atalolisema msichana huyo". Qadhi huyo anasema:"Nikayatupilia mbali madai ya yule baba na nikaipitisha ndoa ile, na yule baba alitoka hali ya kuwa amekasirika akipiga viganja vya mikono yake huku anasema: "Hanafatil-Kalbah" Yaani binti yake ameacha Madhehebu ya Malik na kumfuata Abu Hanifah, na hili neno "Al-Kalbah" ni la kumtweza binti yake ambaye hatimaye baba huyu alitamka kuwa amejitenga na binti yake (hayuko pamoja naye). Mas-ala yaliyopo hapa ni tofauti ya Ij-tihadi ya Madhehebu, wakati ambapo Malik anaona kuwa binti aliyebikra hafai kuolewa isipokuwa kwa idhini ya walii na hata kama atakuwa mkubwa, basi walii wake atakuwa mshiriki katika ndoa yake kumuozesha, hawezi kujiozesha na ni lazima huyo walii amkubalie. Abu Hanifah yeye anaona kwamba, Mwanamke bikra aliyevunja ungo, au akawa ni mkubwa anao uhuru wa kuchagua mume na kujiozesha mwenyewe.


Basi mas-ala haya ya kifiqh yaliwatenganisha baba na binti yake mpaka baba akamsusa binti, na ni mara nyingi wazazi wamekuwa wakiwasusa mabinti zao kwa sababu mbali mbali, miongoni mwake ikiwa ni kutoroka nyumbani na mwanaume fulani anayempenda amuowe, na kususa huku kuna matokeo mabaya, kwani ni mara nyingi (kwa kumsusa binti) humpelekea kumzulia binti kupata mirathi yake, na hatimaye binti anabakia kuwa ni adui wa nduguze ambao nao humsusa dada yao ambaye amewaaibisha. Kwa hiyo mambo hayako kama wasemavyo Masunni kuwa, ndani ya kutofautiana kwao kuna rehma au kwa uchache ni kuwa hakuna rehema katika kila Mas-ala yenye Ikhtilafu. Baada ya maelezo haya inabakia tofauti nyingine baina ya Masunni na Mashia, ambayo ni suala la kumfuata (katika Fat-wa) mtu aliyekwisha kufa.


Masunni wao wanawafuata Maimamu waliokwisha kufa tangu karne nyingi zilizopita, na kuwa mlango wa Ij-tihad umefungwa kwa hao tu tangu zama hizo, na wote waliokuja baada yao miongoni mwa wanachuoni wamefungika katika kufanya sherehe na tunzi za mashairi ya Fiqhi ndani ya Madhehebu manne. Na kwa hakika ziko sauti na makelele ya baadhi ya wanachuoni wa zama hizi kutaka mlango huo ufunguliwe na kuirejea Ij-tihad, kutokana na maslahi ya zama yanavyolazimisha na kutokana na upya wa mambo ambayo yalikuwa hayajulikani zama za Maimamu hao wanne.

Ama Mashia hawaruhusu kumfuata mtu aliyekwisha kufa, na wao humrejea katika kila hukmu zao Muj-Tahid aliyehai ambaye ametimiza masharti tuliyoyataja hapo kabla, na hali hii ni tangu baada ya Ghaibah ya Imam aliye Maasum ambaye aliwalazimisha kuwarejea wanachuoni waadilifu katika zama za kuwa kwake katika Ghaibah mpaka atakapodhihiri. Sunni wa madhehebu ya Malik kwa mfano anaweza kusema jambo hili ni halali na hili ni haramu kwa mujibu wa Imam Maliki, hali ya kuwa Malik amekwisha kufa zaidi ya karne kumi na mbili zilizopita, hivyo hivyo msunni wa Hanafi na Shafii na Hambal, kwani wote hawa waliishi katika kipindi kimoja na baadhi yao wakasoma kwa wenzao. Kama ambavyo Masunni hawaamini juu ya Ismah ya Maimamu hawa ambao wao binafsi hawakudai kuwa na Ismah (kuhifadhika na dhambi) bali walikubali kukosea na wakati mwingine kutokosa, na wanasema kwamba wao wanalipwa katika kila Ij-tihad zao ajira mbili iwapo watapatia, na watalipwa ujira mmoja iwapo watakosea. Na Shia Imamiyyah kwa mfano, wanazo Mar-hala mbili katika Taqlid.

Mar-hala ya Kwanza:
Ni zile zama za Maimamu kumi na wawili, na zama hizo ziliendelea kwa muda wa kiasi cha karne tatu na nusu, na ndani ya zama hizo Shia alikuwa akimfuata Imam aliye Maasum (aliyehifadhiwa kutokana na makosa) ambaye hasemi jambo kwa maoni yake na jitihada yake, bali kwa elimu na riwaya alizozirithi toka kwa Babu yake ambaye ndiye mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Imam huyo husema kuhusu mas-ala (aliyoulizwa)." Baba yangu kapokea toka kwa Babu yangu ( na Babu yangu kapokea) toka kwa Jibril (na Jibril kapokea) toka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu."

Mar-hala ya Pili:
Ni zama za Ghaibah (ya Imam a.s.) zama ambazo zimeendelea mpaka leo, basi Shia husema kwa mfano: hili ni halali na hili ni haramu kwa maoni ya Sayyid Al-Khui au Sayyid Khumain na kila mmoja wao akiwa hai (sasa hivi wote wamefariki) na maoni yao Maimamu hawa hayavuki Ij-tihad katika kutoa hukmu ndani ya Qur'an na Sunna kwa mujibu wa riwaya za Maimamu wa nyumba ya Mtume kwanza, kisha Masahaba waadilifu. Nao wakati wanapozitafiti riwaya za Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) huziweka kwenye daraja la mwanzo, kwani Maimamu hawa wanapinga kutumia maoni binafsi ndani ya sheria na wanasema: "Hapana jambo lolote isipokuwa Mwenyezi Mungu anayohukmu yake, na iwapo hatukuiona hukmu fulani hiyo haimaanishi kwamba Mwenyezi Mungu amelipuuza hukmu hiyo, lakini kutokujuwa kwetu na kushindwa kwetu ndiyo mambo ambayo hayakutufikisha kwenye kuifahamu hukmu hiyo. Hivyo kutokukifahamu kitu siyo dalili ya kutokuwepo kwake Na dalili ya hilo ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Na hapana chochote tulichokiacha Kitabuni humu" (Qur'an, 6:38)


ITIKADIAMBAZO MASUNNI HUWAKEBEHI MASHIA
Miongoni mwa itikadi ambazo Masunni huwakebehi Mashia, jambo ambalo ni wazi kabisa kuwa hivyo ni vitimbi na matatizo yaliyoanzishwa na Banu Umayyah na Banu Abbas mwanzoni mwa Uislamu kutokana na chuki yao dhidi ya Imam Ali (a.s.) ambaye walimkera mpaka wakawa wanamlaani juu ya mimbari kwa miaka arobaini. Kwa ajili hiyo siyo ajabu kwao kumshutumu kila aliyemfuata Ali (a.s.) na kumtupia kila aina ya fedheha na aibu mpaka mambo yakafikia kwa Banu Umayyah na Banu Abbas aambiwe mmoja wao kuwa: "Uyahudi ni bora mno kwake kuliko kuambiwa kuwa yeye ni Shia ".


Na wafuasi wao waliliendeleza hilo kila wakati na kila mahala, na Shia akawa ni mwenye kutukanwa kwa Masunni kwa kuwa anawapinga katika itikadi zao na ametoka katika jamii yao, basi wao Masunni humuaibisha wapendavyo na kumtupia kila aina ya tuhuma na kumpachika majina mbali mbali, na kumkhalifu katika kila kauli zake na matendo yake. Je, huoni kwamba baadhi ya wanachuoni mashuhuri wa Kisunni wanasema kwamba, "Kuvaa pete mkono wa kulia ni sunna ya Mtume lakini ni wajibu kuiacha sunna hiyo kwa kuwa Mashia wamelifanya jambo hilo kuwa ni alama yao". Taz: Musanniful-Hidayyah. Kama alivyothibitisha Az-Zamakh-Shari ndani ya kitabu chake Rabiul-Abrar ya kwamba: "Mtu wa kwanza aliyevaa pete mkono wa kushoto kinyume cha Sunna ya Mtume ni Muawiyah bin Abi Sufiyan. Naye Hujjatul-Islam Abu Hamid Al-Ghazali anasema: "Bila shaka kusawazisha makaburi ndivyo ilivyosheria katika dini, lakini Marafidh (Mashia) walipolifanya jambo hilo kuwa ni kitambulisho chao tumewacha kusawazisha makaburi na tukawa tunayainulia mgongo."


Na huyu Ibn Taimiyyah anayesifiwa kuwa ni mwenye kuleta usuluhishi na wengine wanasema kuwa yeye muhuyishaji na muimarishaji (wa Sunna) anasema:"Na kutokana na hayo wameamua miongoni mwa wanazuoni kuacha baadhi ya sunna zitakapoonekana kuwa ni kitambulisho chao (Mashia), japokuwa kuacha siyo jambo la wajibu, lakini kulidhihirisha tendo hilo (la sunna) ni kujifananisha nao, na hapo anakuwa hatambulikani Sunni kutokana na Shia, na faida ya kujibagua kutokana nao kwa ajili ya kuwatenga na kwenda kinyume nao ni kubwa kuliko faida ya Sunna hii". Taz: Min-Hajus-Sunnah Juz. 2 uk. 143.


Na Al-Hafidh Al-Ira'qi alipokuwa akijadili juu ya kuteremsha kiremba amesema:"Sikuona kinachojulisha juu ya kuhusisha upande wa kulia isipokuwa ndani ya hadithi dhaifu kutoka kwa Tabrani na hata kwa kukadiria kuhusisha kwake huenda alikuwa akikiteremshia upande wa kulia na kisha hukirejesha upande wa kushoto kama wafanyavyo baadhi yao, isipokuwa jambo hilo limekuwa ni kitambulisho cha Mashia basi inapasa kuliepuka ili kuacha kujifananisha nao. Taz: Shar-Hul-Mawahibi cha Az-Zir-Qani Juz. 5 uk. 13. Sub-hanallah Walahaula wala Quwwata Ilia Billah!! Angalia Ewe ndugu yangu msomaji chuki hii yenye upotofu, ni vipi wanachuoni hawa wanaruhusu kwenda kinyume na Sunna ya Mtume (s.a.w.) kwa sababu tu Mashia wameshikamana na Sunna hizo mbili mpaka zikawa ni kitambulisho chao, kisha wanachuoni hao hawaoni vibaya kukiri wazi wazi juu ya jambo hilo, nami nasema: "Namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameidhihirisha haki kwa wenye macho, na kwa kila mwenye utakaso wa moyo anayetafuta ukweli.


Shukrani zinamstahikia Mwenyezi Mungu ambaye ametuonyesha kuwa Mashia ndiyo ambao wanaofuata sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na hilo ni kwa ushuhuda wenu ninyi Masunni kama ambavyo mumeshuhudia wenyewe kwamba ninyi mumeiwacha sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa makusudi ili tu muwapinge Maimamu wa nyumba ya Mtume na wafuasi wao wenye utakaso wa moyo, na mumefuata sunna ya Muawiyah bin Abi Sufiyan kama alivyoshuhudia hilo Imam Zamakhshari pale alipothibitisha kwamba, mtu wa kwanza kuvaa pete mkono wa kushoto kinyume cha sunna ya Mtume ni Muawiya bin Abi Sufiyan. Taz: Kitabu Rabii ul-Abrar cha Zamakh-shari.


Pia mmefuata sunna ya Umar katika bid'a yake ya tarawehe kinyume na sunna ya Mtume ambayo Waislamu wameamriwa waswali sunna majumbani mwao mmoja mmoja na siyo jamaa, kama alivyothibitisha jambo hilo Bukhar. Taz: Sahih yake Juz. 7 uk. 99 (Babu Maa-yajuzu Minal-Ghasbi Wash-Shiddat Liamri llah). Na kama ambavyo Umar mwenyewe amekiri kwamba Tarawehe ni Bid'a aliyoizusha pamoja na kuwa yeye hakuiswali kwani hakuiamini. Taz: Sahih Bukhar Juz. 2 uk. 252. Kitab Sala'tit-Tarawih. Imekuja riwaya ndani ya Sahih Bukhar iliyopokewa toka kwa Abdur-Rahman bin Abdil-Qari kwamba yeye amesema:"Nilitoka mimi na Umar bin Al-Khatab (r.a.) katika usiku mmoja wa mwezi wa Ramadhan kwenda msikitini tukawakuta watu wametawanyika, kuna anayesali peke yake na mwingine anasali na kigurupu, Umar akasema, hakika mimi naona lau nitawakusanya hawa (wakaswali) nyuma ya msomaji mmoja litakuwa ni jambo jema, kisha aliazimia akawakusanya nyuma ya Ubayi bin Kaa'b, halafu nilitoka pamoja naye usiku mwingine (tukawakuta) watu wanasali kufuata sala ya msomaji wao, Umar akasema "Bid'a nzuri ni hii". Taz: Sahih Bukhar Juz. 2 uk. 252 Kitabut-Tarawih.


Jambo la kushangaza ni kuwa yeye Umar aliiona kuwa ni Bid'a nzuri baada ya Mtume kuikataza? Na aliikataza pale Masahaba walipopiga makelele na kuugonga mlango wake (Mtume) ili aje awasalishe sunna ya mwezi wa Ramadhan, Mtume akawatokea hali ya kuwa amekasirika akawaambia: "Mmeng'ang'ania tendo lenu (hili) mpaka nikadhania kwamba mtafaradhishiwa, basi salini (sunna) majumbani mwenu kwani sala iliyo bora kwa mtu ni ile asaliyo nyumbani kwake isipokuwa sala ya faradhi". Taz: Sahih Bukhar Juz. 5 uk. 99, (Babu Ma'Yajuzu Minal-Ghadhab Wash-Shiddat Liamrillah). Kama ambavyo ninyi (Masunni) mlivyoifuata sunna ya 'Uthman bin 'Affan ambayo ni kutimiza sala ya safari kinyume na sunna ya Mtume (s.a.w.) ambapo alisali kwa kupunguza.

Taz: Sahih Bukhari Juz. 2 uk. 35. Pia bibi Aisha alibadilisha na akasali rakaa nne. Taz: uk. 36 Sahih Bukhari Juz. 2 Na lau ningetaka kuyakusanya yote mambo ambayo ndani yake mmeikhalifu sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) basi jambo hilo lingelazimu kuandika kitabu maalum, lakini ushahidi wenu unatosha katika yale mliyoyakiri ninyi wenyewe na ushahidi wenu pia unatosha kwa kukiri kwenu kuwa Mashia ndiyo ambao wameifanya sunna ya Mtume kuwa ni kitambulisho chao. Hivi baada ya haya inabakia dalili yoyote kuhusu kauli ya watu wajinga ambao wanadai kuwa Mashia wamemfuata Ali bin Abi Talib na Masunni wao ndiyo wamemfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu? Je, watu hawa wanataka kuthibitisha kwamba Ali alikwenda kinyume cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) .... na akazusha dini mpya? Hakika ni maneno machafu kabisa yatokayo vinywani mwao, kwani Ali mwenyewe ndiyo sunna halisi ya Mtume naye ndiye mfasiri wa sunna hiyo na ndiye mwenye kuisimamia na Mtume alikwishasema kumuhusu Ali: "Ali kwangu mimi anayo daraja niliyonayo mimi kwa Mola wangu".


Taz: As-Sawaiqul-Muhriqah. As-Sawaiqul-Muhriqah cha ibn Hajar uk. 106, Dhakhairul-Uqba uk. 64, Riyadhun-Nadhrah Juz. 2 uk. 215, Ihqaqul-Haq Juz. 7uh217. Maana ya hadithi hiyo ni kwamba: Kama ambavyo Mtume Muhammad ndiye pekee anayefikisha ujumbe toka kwa Mola wake, basi Ali ndiye pekee atayefikisha ujumbe toka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Lakini dhambi ya Ali ni kule kutokuukubali Ukhalifa wa aliyekuwa kabla yake, na dhambi ya Mashia wake ni kwamba wao wamemfuata katika hilo wakapinga kuwa chini ya Ukhalifa wa Abubakar, Umar na Uthman na kwa ajili hiyo wakaitwa kuwa ni "Marafidh " yaani wapinzani.


Kwa hiyo basi, pindi Masunni wanapopinga itikadi za Kishia na kauli zao hilo ni kwa sababu mbili tu: Ya Kwanza:Ni uadui ambao moto wake uliwashwa na watawala wa Kibanu Umayyah kwa kutumia uongo na madai (ya uzushi) na kutengeneza riwaya za uongo. Ya Pili:Ni kwamba itikadi za Mashia zinapingana na mwenendo wa Masunni wa kuwaunga mkono Makhalifa (ambao hawakustahiki Ukhalifa) na pia kuyaona makosa yao na Ij-Tihadi zao dhidi ya maandiko (Qur'an na Sunna) kuwa ni sawa na ni sahihi, khususan watawala wa Kibanu Umayyah wakiongozwa na Muawiyah bin Abi Sufiyan. Na mpaka hapa mwenye kutafiti na kufuatilia atakuta kwamba tofauti baina ya Shia na Sunni ilianza siku ya Saqifah na ikaendelea ikawa kubwa na kila tofauti iliyokuja baada yake imezaliwa na kutokana ana hapo, Dalili kubwa ya hilo ni kwamba itikadi zile ambazo Masunni huwakebehi ndugu zao Mashia, zinao uhusiano thabiti na maudhui ya Ukhalifa na zinatokana na maudhui hiyo; kama vile tofauti ya idadi ya Maimamu, Tamko la Uimamu, Ismah, Elimu ya Maimamu, Badau, Taqiyyah, Mahdi anayengojewa na mengineyo.


Nasi tunapochunguza ndani ya kauli za pande mbili hizi (Shia na Sunni) hali ya kuwa ni wenye kujiepusha na upendeleo basi huenda tusikute tofauti kubwa baina ya itikadi zao, na wala hatutakuta uhalali wa kuikuza (tofauti iliyopo) na kebehi hii, kwani wewe wakati unasoma vitabu vya Sunni anayewashutumu Mashia, utadhania kabisa kwamba Mashia wamebomoa Uislamu na kwenda kinyume cha misingi yake na sheria zake na wamezusha dini nyingine. Wakati ambapo mtafiti muadilifu atakuta katika kila itikadi ya Kishia iko asili iliyothibiti ndani ya Qur'an na Sunna hata katika vitabu vya hao wanaowapinga Mashia na kuwatukana kutokana na msimamo wao ndani ya itikadi hizo. Vile vile hakuna ndani ya itikadi hizo jambo linalopingana na akili nukuu au mwenendo mwema. Na ili ukubainikie usahihi wa haya ninayoyadai ewe msomaji mwenye utambuzi, nitakuonesha itikadi hizo.