ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

KHITILAFU INAYOHUSU VIZTIO VIWILI
Hapo kabla kwa kupitia uchambuzi uliotangulia tumefahamu mtazamo wa Mashia na Masunni kuhusu Ukhalifa na namna Mtume alivyoufanyia umma kwa mujibu wa kauli za makundi hayo mawili. Basi je, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliuachia ummati wake kitu ambacho utakitegemea na kukirejea endapo itatokea hitilafu ambayo ni lazima itokee nayo ni ile aliyoisajili Mwenyezi Mungu ndani ya kitabu chake aliposema: "Enyi mulioamini mtiini Mwenyezi Mungu na mumtii Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu, basi na kama mtahitilafiana kuhusu jambo fulani, lirejesheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume ikiwa ninyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kufanya hivyo ni bora na matokeo yaliyo mema." (Qur'an, 4:59)


Naam, hapana budi kwa Mtume (s.a.w.) auachie ummah kanuni utakayoitegemea, kwani yeye Mtume ametumwa kuwa ni Rehma kwa viumbe, naye ni mwenye hima juu ya ummati wake uwe ni umma bora kuliko nyumati zingine na usije ukahitilafiana baada yake na kwa ajili hii basi wamepokea Mashaba wake na wana hadithi kutoka kwake kwamba yeye amesema: "Nimekuachieni vizito viwili ambavyo mkishikamana navyo kamwe hamtapotea baada yangu (navyo ni) Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu, na havitaachana viwili hivi mpaka vinifikie kwenye haudh, basi angalieni ni vipi mtakavyonifuata ndani ya viwili hivyo."

Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 148.
Na hadithi hii ni Sahih imethibiti na wameithibitisha wana hadithi kutoka pande zote mbili za Masunni na Shia, na wameisimulia ndani ya Musnad zao na katika sihahi zao kwa njia zaidi ya Masahaba thelathini. Na kwa kuwa mimi kama kawaida yangu sitoi hoja kupitia vitabu vya Mashia wala kauli za wanachuoni wao, basi imenilazimu niwataje wanachuoni wa Kisunni tu ambao wameithibitisha hadithi ya vizito viwili tena hali ya kuwa wanakiri juu ya usahihi wake ili uchambuzi huu siku zote uwe ni maudhui inayosifika kwa uadilifu (pamoja na kwamba uadilifu unapelekea pia kutaja kauli za Shia). Na hii ni orodha fupi ya wapokezi wa hadithi hii miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni:


1) Sahih Muslim, Kitabu Fadhail Ali bin Abi Talib Juz. 7 uk.122.
2) Sahih Tirmidhi Juz. 5 uk. 328.
3) Al-Imamun-Nasai ndani ya Khasais yoke uk.21.
4) Imam Ahmad bin Hanbal Juz. 3 uk. 17.
5) Mustadrak Al-Hakim Juz. 3uk.l09.
6) Kanzul-Ummal Juz. 1 uk. 154.
7) At-Tabaqaatil-kubra cha ibn Saad Juz. 2 uk.194.
8) Jamiul-Usul cha Ibn Al-Athir Juz. 1 uk. 187.
9) Al-Jamius-Saghir cha Suyuti Juz.l uk.353.
10) Maj-Mauz-Zawaid cha Al-Haithami Juz.9 uk.163.
11) Al-Fat-Hul-Kabir cha Nabahani Juz. 1 uk.451.
12) Usudul-Ghabah Fi Maarifatis-Sahabah cha ibn Athir juz,. 2 uk. 12.
13) Tarikh ibn AsakirJuz. 5 uk.436.
14) Tafsiri ibn KathirJuz. 4 uk.113.
15) At-Tajul-Jami'u Lil-Usul, Juz.3 uk.308.


Zaidi ya hawa yuko ibn Hajar ambaye ameitaja ndani ya Kitabu chake kiitwacho As-Sawaiqul-Muhriqah (ameitaja) hali yakuwa anakiri kusihi kwake na A-Dhahabi ameitaja ndani ya Tal-Khis yake hali ya kuwa amekiri kusihi kwake kwa sharti ya masheikh wawili (Bukhar na Muslim). Na Al-Khawar Zami Al-Hanafi, ibn Maghazili As-Shafii na Tabrani ndani ya Muujam yake, vile vile mwenye Siratun-Nabawiyyah katika Hamish ya Siratul-Halabiyyah na mwenye Yanabiul-Mawaddah na wengineo... Basi Je, hivi inafaa baada ya haya mtu yeyote akadai kwamba hadithi hii ya vizito viwili (Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi cha Mtume) Masunni hawaifahamu na eti kuwa ni katika uzushi wa Kishia? Mwenyezi Mungu aiangamize chuki, mtindo wa fikra na upinzani wa kijinga. Kwa hiyo basi, hadithi ya vizito viwili ambayo ndani yake Mtume (s.a.w.) ameusia kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi chake kitukufu, ni hadithi mutawatir, na ni sanad itokayo kwa Maimamu watukufu (wa nyumba ya Mtume s.a.w.).


Basi ni kwa nini baadhi ya watu wanaitilia mashaka hadithi hii na wanajaribu kwa juhudi zao kuibadilisha iwe ni "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna zangu" pamoja na kuwa huyo mwenye kitabu cha "Miftahu Kunuzis-Sunnah" ameithibitisha katika ukurasa wa 478 kwa anuani isemayo, "Usia wake Mtume juu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake," akiwa amenakili kwa Bukhari, Muslim, Tirmidhi na ibn Majah, lakini iwapo utafanya utafiti katika vitabu hivi vinne vilivyotajwa huenda usipate ishara ya karibu au ya mbali inayoashiria hadithi hii. Naam huenda ukapata ndani ya Bukhari anuani isemayo; "Mlango wa kushikamana na kitabu (cha Mwenyezi Mungu) na Sunnah" lakini hutaikuta hadithi hii. Sana sana kinachopatikana ndani ya Sahih Bukhar na katika vitabu vilivyotajwa ni hadithi isemayo:"Ametusimulia Tal-Hah bin Musarrif amesema:Nilimuuliza Abdallah bin Abi Afii r.a. (nikasema) hivi Mtume (s.a.w.) alikuwa ameusia? akasema, hapana nikasema, Vipi kumefaradhishwa kuusia kwa watu au wameamrishwa kuusia? akasema: Aliusia (kushikamana na) kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Taz: Sahihi Bukhari Juz. 3 uk. 186 oSahihi Tirmidhi Kitabul-Wasaya Sahihi Muslim Kitabul-Wasaya Sahihi ibn Majah Kitabul-Wasaya. Na wala hakuna hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ambayo ndani ya hadithi hiyo Mtume anasema:"Nimekuachieni vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu." Hata kwa makadirio ya kuwepo kwa hadithi hii ndani ya baadhi ya vitabu ni jambo lisilo na maana yeyote ile kwani Ijmai (makubaliano yaliyopo) yako kinyume cha hadithi hiyo kama ilivyotangulia hapa kabla. Kisha lau tutafanya uchambuzi kuhusu hii hadithi ya "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna yangu" tutaikuta haikubaliani na ukweli ulivyo siyo kwa maandiko wala kiakili nasi katika kuipinga hadithi hiyo tunayo baadhi ya mitazamo.

Mtazamo wa Kwanza:
Wanahistoria na wanahadithi wameafikiana kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alizuia kuandika hadithi zake, na hapana yeyote aliyedai kwamba yeye alikuwa akiandika sunna ya Mtume katika zama zake, kwa hiyo kauli ya Mtume (s.a.w.) isemayo kuwa nimekuachieni "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna yangu " haikubaliki. Ama kuhusu Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kiliandikwa na kuhifadhiwa katika vifua (nyoyo) vya watu na iliwezekana kwa sahaba yeyote kurejea kwenye msahafu hata kama hakuwa miongoni mwa waliohifadhi.


Na ama kuhusu sunna ya Mtume hakuna kilichokuwa kimeandikwa au kukusanywa katika zama zake Mtume (s.a.w.), kwani sunna ya Mtume kama inavyoeleweka na kukubalika ni kila alichokisema Mtume au kukitenda au kukiri, na inavyofahamika pia ni kwamba Mtume alikuwa hawakusanyi Masahaba wake ili kuwafundisha sunna yake, bali alikuwa akizungumza katika kila tukio fulani na huenda wakahudhuria baadhi yao na huenda asiwe na mtu miongoni mwa Masahaba wake isipokuwa mmoja, basi itawezekana vipi kwa Mtume katika hali kama hii aseme kuwa nimekuachieni sunna yangu?

Mtazamo wa Pili:
Pindi Mtume alipozidiwa na maumivu hali ambayo ilitokea siku tatu kabla ya kufariki kwake, aliwataka Masahaba wamletee karatasi na wino ili awaandikie maandiko ambayo kamwe hawatapotea baada yake, Umar bin Al-Khatab akasema, "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu anaweweseka, kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu." Taz: Sahih Bukhar, Babu Maradhin-Nabii Wawafatih Juz. 5 uk 138. Bila shaka lau Mtume wa Mwenyezi Mungu hapo kabla angekuwa amewaambia kwamba nimekuachieni "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna zangu," ni kwa nini Umar alisema kuwa, Kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu? Na kwa kufanya hivyo yeye na Masahaba waliokubali usemi wake huo watakuwa wanampinga Mtume wa Mwenyezi Mungu? Nami sidhani kama Masunni wanaliridhia jambo hili.!!


Kwa hiyo basi tumefahamu yakuwa hadithi hii ilizushwa na baadhi ya watu waliokuja baadaye ambao wanawachukia watu wa nyumba ya Mtume na hasa baada ya kuwaweka mbali na Ukhalifa, na inakuwa kama kwamba huyu aliyeizusha hadithi hii ya "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu" alishangazwa kuwaona watu wameshikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na wamekiacha kizazi cha Mtume na kuwafuata watu wengine, basi akadhania kuwa kwa kuzusha hadithi hii atausahihisha mwenendo wao na kuepusha kukosolewa Masahaba ambao walikwenda kinyurne na usia wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).

Mtazamo wa Tatu:
Ni jambo maarufu kwamba tukio la kwanza lililomkabili Abubakar mwanzoni mwa Ukhalifa wake ni kule kuthibitisha kwake kuwapiga vita wanaozuwia kutoa zaka, licha ya upinzani wa Umar bin Al-Khatab dhidi yake na kutoa kwake ushahidi wa hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliposema: "Yeyote atakayesema Lailaha Illa llahu Muhammadun Rasulullah basi mali yake na damu yake vimehifadhika tokana nami isipokuwa kwa haki yake na hesabu yake iko kwa Mwenyezi Mungu". Basi lau kama sunna ya Mtume (s.a.w.) ingekuwa inajulikana, Abubakr asingekosa kuifahamu wakati yeye anastahiki mno kuijua sunna ya Mtume.


Pamoja na hayo hatimaye Umar bin Al-Khatab alikinaishwa na tendo la Abubakr kuibadilisha hadithi aliyoisimulia Umar na (pia akakinaishwa na) kauli ya Abubakr kwamba zaka ni haki iliyomo katika mali, lakini wao hao waliisahau au walijisahaulisha Sunna ya Mtume ya vitendo ambayo haikubali kubadilishwa, nayo ni ile inayohusu kisa cha Thalabah ambaye alikataa kutoa zaka kwa Mtume (s.a.w.), na Qur'an ikashuka kumuhusu huyo Thalabah. Pamoja na yote hayo Mtume wa Mwenyezi Mungu hakumuuwa Thalabah (kwa kukataa kwake kutoa zaka) wala hakumlazimisha kuitoa. Basi ni vipi hali ya Abubakr na Umar (je, hawakifahamu) kisa cha Usamah bin Zaid ambaye Mtume (s.a.w.) alimtuma kwenye jeshi fulani, na alipowavamia watu hao na kuwashambulia, alimkuta mtu fulani, alipomkamata yule mtu akasema, Lailah Illaha illa llah!! Lakini Usamah akamuuwa mtu yule, na khabari hizo zilipomfikia Mtume (s.a.w.) akasema, "Ewe Usamah umemuuwa baada ya kuwa amesema Lailaha Illa llah"? Usamah akasema:"Huyo alikuwa anajikinga tu" Basi Mtume (s.a.w.) hakuacha kukariri jambo hilo mpaka nikatamani lau nisingekuwa nimesilimu kabla ya siku hiyo. Taz: 1) Sahih Bukhar Juz. 8 uk. 36.


2) Sahih Muslim Juz. 1 uk. 67. Kwa hiyo basi, hatuwezi kuisadiki hadithi isemayo, "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu" Kwani wao Masahaba ndiyo wa mwanzo kutoijua sunna ya Mtume, basi itakuwaje kwa wale waliokuja baada yao na itakuwaje kwa mtu ambaye maskani yake yako mbali na Madina? (Hatoifahamu kabisa Sunna ya Mtume).

Mtazamo wa Nne:
Ni jambo maarufu pia kwamba mengi katika matendo ya Masahaba baada ya Mtume (s.a.w.) yalikuwa kinyume cha Sunna yake,kwa hiyo imma Masahaba hawa walikuwa wanaifahamu Sunna ya Mtume (s.a.w.) na waliikhalifu kwa makusudi kutokana na ijtihadi zao dhidi ya Nassi (matamko, matendo na iqrari) za Mtume (s.a.w.), na kwa ajili hiyo Masahaba hawa inawakumba kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pale aliposema:"Haiwi kwa Muumini wa kiume wala Muumini wa kike Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapoamua jambo wao wawe na hiyari katika jambo lao, na yeyote mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotevu ulio wazi." (Qur'an, 33:36) Na labda (tuseme) walikuwa hawaijui Sunna ya Mtume (s.a.w.), kwani haistahiki kabisa kwa Mtume (s.a.w.) katika hali kama hii kuwaambia Masahaba wake nimekuachieni Sunna yangu hali yakuwa yeye Mtume anajua kwamba Masahaba wake ambao ni watu wa karibu mno kwake hawaifahamu Sunna yake, basi hali itakuwaje kwa watakaokuja baada yao wakati hata Mtume hawakumfahamu na wala hawakumuona?


Mtazamo wa Tano:
Inafahamika pia kwamba Sunna ya Mtume haikuandikwa isipokuwa katika zama za dola ya Bani Abbas, na kwamba kitabu cha mwanzo kilichoandikwa kuhusu hadithi ni "Muwataa" cha Imam Malik, na hiyo ni baada ya fitna kubwa (kupita) baada ya tukio la Karbala na kushambuliwa mji wa Madina, kisha kuuawa kwa Masahaba hapo mjini Madina. Basi ni vipi baada ya matukio hayo mtu atakosa kuwatilia mashaka wasimulizi wa hadithi (za Mtume) ambao walijipendekeza kwa watawala ili waipate dunia? Kwa ajili hiyo hadithi za (Mtume) zimevurugika na kupingana zenyewe kwa zenyewe, nao umma wa Kiislamu umegawanyika kwenye Madhehebu mengi (kiasi kwamba) jambo ambalo limethibiti kwenye madhehebu haya, kwenye madhehebu mengine halikuthibiti, na kitu ambacho kwa hawa wanakiona ni sahihi, wale wanakipinga. Ni vipi tutaamini kamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema kuwa "Nimekuachieni kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu, na hali ya kuwa yeye anafahamu kwamba wanafiki na wapinzani watakuja mzulia? Hapana shaka Mtume (s.a.w.) alipata kusema,"Wako wengi wenye kunizulia, basi yeyote mwenye kunizulia na ajiandalie makazi yake motoni". Hivyo basi iwapo wazushi walikuwa wengi katika zama za uhai wake, ni vipi Mtume aulazimishe umma wake kufuata Sunna yake na hali hawaifahamu Sunna iliyo sahihi kutokana na ile isiyo sahihi na dhaifu kutokana na ile yenye nguvu?


Mtazamo wa Sita:
Masunni wanasimulia ndani ya vitabu vyao sahihi kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ameacha vizito viwili au Makhalifa wawili au vitu viwili, na wakati mwingine wanasimulia kuwa (Mtume ameacha) kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume wake na wakati mwingine wanasimulia kuwa (Mtume amesema) shikamaneni na sunna zangu na sunna za Makhalifa waongofu baada yangu. Jambo la muhimu (inataka lifahamike) ni kuwa, hadithi hii ya mwisho inaongeza kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake (inaongeza) sunna za Makhalifa, hivyo misingi ya sheria inakuwa ni mitatu badala ya miwili. Na yote hii inapingana na hadithi ya vizito viwili ambayo ni sahihi kwa kuwa wameafikiana kwenye hadithi hiyo Masunni na Mashia nayo ni ile isemayo; "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu", hadithi ambayo tumekwisha taja zaidi ya rejea ishirini (inamopatikana) miongoni mwa rejea za Kisunni zinazotegemewa ukiachilia mbali rejea za Kishia ambazo hatukuzitaja.


Mtazamo wa Saba:
Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu anafahamu vilivyo kwamba Masahaba wake ambao Qur'an ilishuka kwa lugha yao na Lahaja (Matamshi) yao (kama wasemavyo)-hawakuyafahamu mambo mengi miongoni mwa tafsiri ya (Qur'an) wala taawili yake, basi vipi itakuwa kwa watu watakaokuja baada yao, na ni vipi itakuwa kwa walioukubali Uislamu miongoni mwa Warumi na Wafursi na Wahabeshi na wote wasiokuwa Waarabu ambao hawakukifahamu Kiarabu wala kukizungumza? Na imethibiti katika athari ya kwamba Abubakr aliulizwa kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo: "Wafakihatan-Waabba" yaani, "Na matunda na malisho," basi Abubakr akasema:Ni mbingu gani itakayonifunika na ardhi gani itaniacha niketi humo endapo nitasema kuhusu kitabu cha Mwenyezi Mungu nisilolijua"? Taz: Al-Qastalani ndani ya Ir-shaad As-Sari Juz. 10 uk. 298 na ibn Hajar ndani ya Fat-h Al-Bari Juz. 13 uk. 230. Kama ambavyo Umar bin Al-Khatab pia hakuifahamu maana hii.

Imepokewa toka kwa Anas bin Malik amesema, "Hakika Umar bin Al-Khatab alisoma akiwa juu ya Minbar (Faanbat-naa Fiha Habban Wainaban Waqadh-ban Wazaitunan Wanakhlan Wahadaiqa Ghul-ban Wafakihatan Waabba) Yaani, "Kisha tukaotesha humo (vyakula vilivyo) chembe chembe, na mizabibu na mboga, na mizeituni na mitende, na mabustani yenye miti iliyosongamana na matunda na malisho". ( Qur 'an 80: 27- 31) Umar akasema: "Yote haya tunayajua, sasa hii Abban ni kitu gani? Kisha akasema: "Namuapa Mwenyezi Mungu hii ni takilifu (taabu) hulazimiki kufahamu nini Abban, fuateni yaliyobainishwa kwenu ndani ya kitabu, basi na muyatumie na yale msiyoyajua yategemezeeni kwa Mola wake". Taz: Tafsiri ibn Jarir Juz. 3 uk. 38 na Kanzul-Ummal Juz. 1 uk. 287, Al-hakim ndani ya Mustadrak Juz. 2 uk: 14 na Ad-Dhabi ndani ya Tal-Khis yake na Al-Khatib ndani ya Tarikh yake Juz. 11 uk. 468.


Na yasemwayo hapo kuhusu tafsiri ya kitabu cha Mwenyezi Mungu ndiyo yasemwayo kuhusu sunna tukufu ya Mtume, kwani ni hadithi ngapi za Mtume zimebakia kuwa ni mahali pa ikhitilafu baina ya Masahaba na baina ya Madhehebu na kati ya Masunni na Mashia, sawa sawa ikhtilafu hiyo iwe imekuja kutokana na usahihi wa hadithi au udhaifu wake, au tafsiri yake na kuifahamu hadithi hiyo, na kwa ufafanuzi ninamletea msomaji Mtukufu baadhi ya mifano kuhusu jambo hilo. 1. Khitilafu baina ya Masahaba juu ya kusihi kwa Hadithi au kuipinga Hadithi hiyo. Jambo hili lilimtokea Abubakr mwanzoni mwa siku zake za Ukhalifa pale bibi Fatmah binti ya Mtume (s.a.w.) alipomjia (Abubakr) akimtaka ampe shamba la Fadak ambalo Abubakr alilichukua kutoka kwa bibi Fatmah baada ya Mtume (s.a.w.) kufariki. Abubakr aliyakanusha madai ya bibi Fatmah yasemayo kwamba, baba yake bibi Fatmah ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu alimzawadia shamba hilo zama za uhai wake, pia bibi Fatmah alimtaka Abubakr ampe mirathi ya baba yake. Basi Abubakr akawambia bibi Fatmah kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema:"Sisi Mitume haturithiwi, chochote tulichokiacha ni sadaka."


Bibi Fatmah naye alimpinga Abubakr kuhusu hadithi hiyo (inayodaiwa) kuwa ni ya baba yake na alimpinga kwa mujibu wa kitabu cha Mwenyezi Mungu, na hapo ugomvi na khitilafu ukapamba moto kiasi kwamba bibi Fatmah alifariki akiwa kamkasirikia Abubakr wala hakumsemesha tena. Haya ni kama yalivyo ndani ya sahihi mbili, yaani Bukhar na Muslim. Kadhalika kuna khitilafu baina ya Aisha Ummul-muuminina na Abu Hurairah kuhusu Mtume, ambaye eti huamka asubuhi akiwa na janaba ndani ya mwezi wa Ramadhani. Kwa upande wa bibi Aisha anaona jambo hilo kuwa ni sahihi, wakati ambapo Abu Hurairah anaona kwamba mwenye kuamka asubuhi hali yakuwa ana janaba hana saumu.

Basi hebu kiangalie kisa hiki kwa ufafanuzi:
Imam Malik amethibitisha ndani ya Muwat-Taa, naye Bukhar ndani ya Sahihi yoke, imepokewa toka kwa bibi Aisha na Ummu Salamah wakeze Mtume (s.a.w.) kwamba wao wamesema, "Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa akiamka asubuhi akiwa na janaba inayotokana na jimai na siyo kujiotea katika mwezi wa Ramadhani kisha hufunga saumu" Na imepokewa toka kwa Abubakr bin Abdur-Rahman amesema:"Tulikuwa mimi na baba yangu tuko kwa Mar-wan bin Al-Hakam ambaye alikuwa ndiyo Amir wa Madina, akaelezwa kwamba Abu Hurairah anasema kuwa, mwenye kuamka asubuhi na janaba (katika mwezi wa Ramadhani) saumu ya siku hiyo ni batili." basi Mar-wan akasema:"Nakuapia ewe Abdur-Rahmah huna budi kwenda kwa mama wa waumini Aisha na Ummu Salamah ili uwaulize juu ya hilo" Abdur-Rahman alikwenda nami nikaenda naye mpaka tukaingia kwa Aisha akamsalimia kisha akasema, "Ewe Ummul-Muuminina, sisi tulikuwa kwa Mar-wan bin Al-Hakam akaambiwa kuwa Abu Hurairah anasema, mwenye kuamka asubuhi hali ya kuwa ana janaba, basi siku hiyo hana saumu, Aisha akasema, Sivyo alivyosema Abu Hurairah ewe Abdu Rahman je, hupendi kufanya vile alivyokuwa akifanya Mtume wa Mwenyezi Mungu"?


Abdur-Rahman akasema, "Hapana Wallahi", Aisha akasema, "Namshuhudia Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye alikuwa akiamka hali yakuwa anayo janaba iliyotokana na jimai na siyo ya kujiotea kisha hufunga siku hiyo." Amesema, Kisha tulitoka mpaka kukaingia kwa Ummu Salamah na akamuuliza juu ya hilo, naye akasema kama alivyosema Aisha, amesema, "Nakuapia ewe Abdur-Rahman hakika utapanda mnyama wangu yuko hapo mlangoni, na uende kwa Abu Hurairah kwani yeye yuko kwake huko basi umueleze jambo hilo. Kisha Abdur-Rahman akapanda nami nikapanda pamoja naye mpaka tukafika kwa Abu Hurairah. Abdur-Rahman akazungumza naye kiasi cha muda kisha akamueleza jambo hilo, basi Abu-Hurairah akasema: "Mimi sina ujuzi wa jambo hilo kwani kuna mtu fulani tu alinieleza." Taz: Sahihi Bukhar Juz. 2 uk. 232.

Babus-Saim Yasbahu Junuban, Muwat-Taa ya Malik. Tan-Wirul-Hawalik Juz. 1 uk. 272. Muangalie ewe ndugu msomaji sahaba kama Abu-Hurairah ambaye kwa Masunni ni msimulizi (mashuhuri wa hadithi) katika Uislamu ni vipi anatoa fat-wa kwenye hukmu za dini yake kwa njia ya kudhani na kuinasibisha fat-wa hiyo kwa Mtume (s.a.w.) na hali yakuwa hamjui hata aliyemueleza hadithi hiyo! Kisa kingine cha Abu Hurairah ambacho ndani yake anajipinga mwenyewe. Amepokea Abdallah bin Muhammad, ametusimulia Hisham bin Yusuf, ametueleza Maamar naye kutoka kwa Az-Zuhri ambaye kapokea toka kwa Abu Maslamah naye toka kwa Abu Hurairah (r.a.) amesema "Amesema Mtume (s.a.w.), hapana kuambukiza wala ugonjwa wa manjano wala mkosi."

Bedui mmoja akasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu itakuwaje kwa ngamia ambaye huwa mchangani kama paa kisha akachanganyika na ngamia mwenye upele akamuambukiza, Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema, basi ni nani aliyemuambukiza yule wa kwanza"? Na imepokewa toka kwa Abu Salamah kwamba amemsikia Abu Hurairah akisema, "Mtume (s.a.w.) amesema, Mgonjwa asimkurubie asiyeumwa,"Kwa hiyo Abu Huraira akawa ameikanusha ile hadithi yake ya mwanzo sisi tukasema, "Siyo wewe uliyesimulia kwamba; hakuna kuambukiza? Basi akazungumza kihabeshi.(hatukumuelewa) Abu Salamah akasema basi sikumuona tena kusahau hadithi isipokuwa hiyo..."

Taz: Sahih Bukhar Juz. 7 uk. 31. Sahih Muslim Juz. 7 uk. 32. (Babu La 'Ad-wa- Walatirah). Ewe msomaji mwenye utambuzi hii ndiyo sunna ya Mtume, au ukipenda sema, "Haya ndiyo yanayonasibishwa kwa Mtume, mara Abu Hurairah aseme kwamba hana ujuzi wa hadithi yake ya mwanzo na kuwa eti kuna mtu fulani alimwambia, na mara nyingine wanapomkabili kutokana na kupingana (kwa hadithi zake) anashindwa kujibu lolote, bali anazungumza Kihabeshi ili asijefahamu yeyote yule."

Khitilafu kati ya bibi Aisha na ibn Umar.
Ibn Juraij amesimulia akasema, "Nilimsikia'Ataa' akieleza akasema, Ur-wa bin Zubair amenieleza akasema, Nilikuwa mimi na Umar tumeegemea kwenye chumba cha Aisha na hali yakuwa tunamsikia anavyopiga mswaki , mimi nikasema, Ewe baba Abdur-Rahman Mtume alifanya Umrah katika mwezi wa Rajab, akasema, ndiyo, basi mimi nikamwambia Aisha, Ewe mama yangu unasikia ayasemayo baba Abdur-Rahman, akasema kwani anasemaje? Nikasema anasema kuwa Mtume alifanya Umra katika mwezi wa Rajab, basi bibi Aisha akasema "Mwenyezi Mungu amsamehe baba Abdur-Rahman naapa Mtume hakufanya Umrah katika Mwezi wa Rajab na hakuna Umrah aliyoifanya isipokuwa mimi nilikuwa pamoja naye. Amesema mpokezi, yote hayo Ibn Umar anayasikia na hakusema hapana wala ndiyo alinyamaza". Taz: Sahih Muslim Juz. 3 uk. 61. Sahih Bukhar Juz. 5 uk. 86.


2. Khitilafu za Madhehebu kuhusu Sunna ya Mtume. Ikiwa Umar na Abubakr wanahitilafiana kuhusu sunna ya Mtume (s.a.w.)[83] na iwapo Abubakr anatofautiana na bibi Fatmah juu ya sunna ya Mtume,[84] na kama wakeze Mtume (s.a.w.) wanahitilafiana kuhusu sunna ya Mtume (s.a.w.)[85] pia Abu Hurayrah anajipinga na kuhitilafiana na mwana Aisha juu ya sunna ya Mtume.[86] Si hivyo tu, bali ibn Umar anahitilafiana na bibi Aisha katika sunna ya Mtume[87] naye Abdallah ibn Abbas na ibn Zubair nao wanahitilafiana juu ya sunna ya Mtume.[88] Kama ambavyo Ali bin Abi Talib na Uthman wanahitilafiana kuhusu sunna ya Mtume[89] kadhalika Masahaba wanahitilafiana baina yao kuhusu sunna ya Mtume kiasi cha kuwafanya waliofuata baada yao kuwa na madhehebu zaidi ya sabini, basi ibn Masoud akawa na madhehebu yake, pia ibn Umar, ibn Abbas, ibn Zubair, ibn Uyaynah, ibn Juraij na Al-Hasan Al-Basri na Sufiyan Athauri, Malik, Abu Hanifah, Shafii, Ahmad bin Hanbal na wengineo wengi, lakini mabadiliko ya kisiasa yaliyauwa madhehebu mengine yote na hapakubakia isipokuwa madhehebu manne maarufu kwa Masunni.

Pamoja na kupungua idadi ya madhehebu lakini wanatofautiana katika mas-ala mengi ya Kifiqhi, na hiyo imekuja kutokana na kutofautiana kwao katika sunna ya Mtume, kwani mmoja wao huenda akajengea hukmu yake katika mas-ala fulani kufuatana na hadithi aliyoiona kuwa ni sahihi miongoni mwa hadithi za Mtume (s.a.w.) wakati ambapo mwingine atajitahidi kwa maoni yake atafanya makisio (Qiyas) katika mas-ala mengine kutokana na kukosekana "Nassi" - Qur'an au hadithi.
3. Ikhtilafu ya Sunni na Shia kuhusu Sunna ya Mtume. Amma ikhtilafu ya Sunni na Shia katika mas-ala haya huenda ni kwa ajili ya sababu mbili za msingi. Mojawapo ni kule kukosa kusihi kwa hadithi upande wa Shia, itakapokuwa mmoja wa wapokezi ni mwenye kutuhumiwa katika uadilifu wake japokuwa ni sahaba, kwani Mashia hawasemi kuwa Masahaba wote ni waadilifu kama hali ilivyo kwa Masunni. Zaidi ya hapo Mashia wanaipinga hadithi inayopingana na riwaya (mapokezi) ya Maimamu wa nyumba ya Mtume, ina maana kwamba wao hutanguliza riwaya ya Maimamu hawa kuliko riwaya ya wengine hata kama wana daraja gani. Na kwa kufanya hivyo wanazo dalili kutoka ndani ya Qur'an na Sunna iliyothibiti (kwao wao) hata kwa makhasimu wao, na hapo kabla baadhi yake zimeashiriwa.


Ama sababu ya pili kuhusu hitilafu iliyoko baina yao ni ile inayotokana na kufahamika kwa hadithi yenyewe, kwani huenda Masunni wakaifasiri vile ambavyo wasivyoifasiri Mashia, kama ile hadithi ambayo tumeionesha hapo kabla nayo ile kauli ya Mtume (s.a.w.) aliposema: "Ikhitilafu katika umma wangu ni rehma". Masunni huifasiri kwamba inahusu ikhtilafu ndani ya madhehebu manne katika mambo ya Kifiqhi kuwa hiyo ni rehma kwa Waislamu. Wakati ambapo Mashia huifasiri kuwa ni safari ya baadhi yao kwenda kwa wengine na kutilia mkazo suala la elimu (katika safari hizo) na mengineyo miongoni mwa mambo yenye faida. Au huenda tofauti baina ya Shia na Masunni ikawa siyo katika maf-humu ya hadithi ya Mtume, bali ikahusu mtu au watu waliokusudiwa na hadithi hiyo, na hilo ni kama ilivyo kauli ya Mtume (s.a.w.) aliposema: "Shikamaneni na sunna yangu na sunna ya Makhalifa waongofu baada yangu". Masunni huwa wanamaanisha kuwa waliokusudiwa hapo ni Makhalifa wanne, ama Mashia wao humaanisha kuwa ni Maimamu kumi na wawili kwa kuanza na Ali bin Abi Talib na kumalizia kwa Mahdi Muhammad bin Al-Hasan Al-Askari (a.s.).


Au kama vile kauli yake Mtume (s.a.w.) aliposema: "Makhalifa baada yangu ni kumi na wawili na wote ni Maquraish". Mashia humaanisha kuwa ni Maimamu kumi na wawili kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) wakati ambapo Masunni hawapati tafsiri ya kutosheleza kwenye hadithi hii, na kwa hakika wamehitilafiana (Mashia na Masunni) hata katika matukio ya kihistoria ambayo yanahusiana na Mtume (s.a.w.) kama ilivyo kuhusu siku aliyozaliwa Mtume, kwani Masunni husherehekea kuzaliwa kwa Mtume tarehe kumi na mbili mfunguo sita wakati Mashia husherehekea tarehe kumi na saba mwezi huo huo. Basi naapa, hakika hitilafu hii kuhusu sunna ya Mtume ni jambo la kawaida halikwepeki kama kutakuwa hakuna rejea watayoirejea wote na hukumu yake ipite na rai yake ikubalike kwa wote kama alivyokuwa Mtume (s.a.w.), kwani alikuwa akikata chanzo (chochote) cha hitilafu na akivunja ugomvi (vurugu) na kuhukumu kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu amemuonyesha hivyo (wafuasi wake) husalim amri japokuwa ndani ya nyoyo zao kuna dhiki (uzito), kwa hiyo kupatikana kwa mtu kama huyu ni jambo la lazima katika maisha ya umma (wa Kiislamu) kwa muda wote!!


Hivi ndivyo inavyohukumu akili na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) hawezi kughafilika kwa hilo na hali ya kuwa anafahamu kwamba umati wake utayabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu baada yake, basi ikawa ni lazima kwake kuuwekea umma wake mwalimu mwenye uwezo wa kuuongoza kwenye njia ya sawa pindi utakapotaka kupinda kutoka kwenye njia iliyonyooka. Na bila shaka Mtume aliuandalia kwa vitendo umma wake kiongozi Mtukufu ambaye yeye Mtume alitoa kila juhudi zake kumlea na kumfunza (kiongozi huyo) tangu alipozaliwa mpaka akafikia ukamilifu na kwa Mtume akawa na daraja ya Harun kwa Musa kisha akamkabidhi jukumu hili tukufu kwa kusema:
"Mimi nitapigana nao katika kushuka Qur'an nawe utapigana nao katika kuiawili" Taz: Al-Khawar-Zami ndani ya Manaqib uk. 44, Yan-Abiul-Mawaddah uk. 233. Al-Isabah cha ibn Hajar Al-Asqalani Juz.l uk. 25, Kifayatut-Talib uk. 334, Muntakhab Kanzil-Uinmal Juz. 5 uk. 36. Ih-Qaqul-Haqqi Juz. 6 uk. 36.

Na kauli yake Mtume isemayo: "Wewe ewe Ali utaubainishia umma wangu yale watayotofautiana ndani yake baada yangu". Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 122, Tarikh Dimishq ya ibn Asakir Juz. 2uk. 488, Al-Manaqib cha Al-Khawarzami uk. 236, Kanzul-Haqaiq cha Al-Manawi uk. 203, Muntakhab Kanzil-Ummal Juz. 5 uk.33, Yanabiul-Mawaddah uk. 128. Basi ikiwa kama Qur'an ambayo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu inahitajia mtu atakayeipigania katika njia ya kuifasiri na kuiweka bayana, kwa kuwa chenyewe ni kitabu ambacho hakisemi na kimebeba namna nyingi mbalimbali, na ndani yake kuna mambo ya dhahiri na yaliyojificha (yahitaji ufafanuzi) basi itakuwaje kuhusu hadithi za Mtume? Na kama mambo yako namna hii kuhusu kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna, basi haiwezekani kwa Mtume (s.a.w.) kuuachia umma wake vizito viwili vilivyo kimya visivyozungumza, kwani wenye nyoyo potovu hawataacha kuvibadilisha kwa lengo lao na wafuate zenye kushabihiana kwa kutaka fitna na kutaka dunia na itakuwa ni sababu ya kupotea wale wataokuja baada yao, kwani wao wamewadhania dhana nzuri na wakaitakidi juu ya uadilifu wao, na siku ya kiyama watajuta ndipo itakapothibitika kwao kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo:


"Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa (kuunguzwa) motoni watasema, laiti tungemtii Mwenyezi Mungu na tungemtii Mtume, na watasema, Mola wetu hakika tuliwatii mabwana wetu na wakubwa wetu basi wametupoteza njia, Mola wetu wape hawa adhabu maradufu na uwalaani laana kubwa" (Qur'an, 33:66-68) "Kila utakapoingia umma utawalaani wenzao mpaka watakapokusanyika wote humo wa nyuma yao watasema kwa wale wa mwanzo wao, Mola wetu hawa ndiyo waliotupoteza basi wape adhabu ya moto maradufu, atasema itakuwa kwenu nyote (adhabu) maradufu lakini ninyi hamjui" .(Qur'an, 7:38)

Bila shaka upotevu haukuwa isipokuwa kwa mambo kama hayo, kwani hakuna umma ambao Mwenyezi Mungu aliutumia Mtume akawabainishia njia na kuwamulikia mahala pa kupita lakini wao (hao wenye kubainishiwa) baada ya Mtume wao walikuwa wakigeuza na kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu, basi je, mwenye akili anadhani kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu Isa (a.s.) aliwaambia Wakristo kwamba yeye ni Mungu? Kamwe hakuwaambia hivyo; "Sikuwaambia isipokuwa yale uliyoniamuru" Lakini matamanio na matakwa (yao) na kuipenda dunia ndiyo yaliyowavuta Wakristo kufanya hilo, je hakuwabashiria Nabii Isa kuja kwa Muhammad? Na kabla yake Musa aliwabashiria pia, lakini wakabadilisha jina la Muhammad na Ahmad kuwa "Mwokozi" nao mpaka leo bado wanamngojea!


Na je, Umati wa Mtume Muhammad ulikuwa umegawanyika kwenye madhehebu na vikundi vingi kufikia sabini na tatu na vyote vitaingia motoni isipokuwa kundi moja (hayakutokea haya) isipokuwa kwa sababu ya kubadilisha (ukweli ulivyo), na leo hii sisi tunaishi katikati ya vikundi hivi, je, kipo kikundi ambacho chenyewe kinajisema kuwa kimepotea, au kwa maelezo mengine? Je, kipo kikundi kimoja ambacho kinadai kwamba kimekwenda kinyume na kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake? Kinyume chake ni kwamba kila kikundi kinasema kuwa chenyewe ndicho kilichoshikamana na Kitabu (Qur'an) na Sunna, basi ufumbuzi uko wapi?

(Tuseme) ufumbuzi wa hili ulikuwa umefichika kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) au zaidi ya hapo (tuseme ufumbuzi wake ulifichika) hata kwa Mwenyezi Mungu? Namuomba Mwenyezi Mungu anisamehe, bila shaka yeye ni mpole kwa waja wake na anawapendelea mema, basi hapana budi awawekee ufumbuzi ili aangamie mwenye kuangamia hali yakuwa panaubainifu. (Nijuu yake kuchagua uongofu au upotofu). Siyo katika utaratibu wa Mwenyezi Mungu kuwapuuza viumbe wake na kuwaacha bila ya uongofu, vinginevyo basi labda kama tutaitakidi kwamba yeye ndiye aliyewatakia khitilafu hizo na vikundi hivyo na upotevu ili tu awatupe ndani ya moto wake, na hiyo ni itikadi batili na mbaya.

Namuomba Mwenyezi Mungu anisamehe na ninatubia kwake kutokana na kauli hii ambayo hailingani kabisa na utukufu wa Mwenyezi Mungu na hekima yake na uadilifu wake. Basi ile kauli ya Mtume (s.a.w.) kwamba yeye ameacha kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake siyo ufumbuzi unaoingia akilini kuhusu qadhiya yetu, bali inatuongezea utata na taawili ambayo haikati mzizi wa wenye fitna na wenye kupotoka, kwani huwaoni pale walipotoka dhidi 'ya Imam wao walinyanyua kitambulisho kisemacho: "Hapana hukmu yako ewe Ali bali hukmu ni ya Mwenyezi Mungu!! Hakika kwa nje ni kitambulisho kizuri, kinaichukua akili ya msikilizaji akadhani kuwa msemaji anahamu ya kutekeleza hukmu za Mwenyezi Mungu, na anapinga hukmu isiyokuwa hiyo miongoni mwa hukmu za watu, lakini ukweli halisi hauko hivyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Na wako miongoni mwa watu ambao kauli zao hapa duniani zinakufurahisha na humshuhudisha Mwenyezi Mungu yaliyomo nyoyoni mwao na hali wao ni wagomvi wakubwa kabisa". (Qur'an, 2:204) Naam ni mara ngapi tunahadaika kwa vitambulisho ambavyo dhahiri ni vizuri na wala hatujui ni kitu gani kilichojificha nyuma yake, lakini Imam Ali analifahamu hilo kwani yeye ni mlango wa mji wa elimu yeye aliwajibu "Hakika hayo ni maneno ya kweli yamekusudiwa (kutekeleza) uovu ".


Naam, ni maneno yaliyo ya kweli lakini yanakusudiwa (kutekeleza) maovu ilikuwaje hali hiyo? Ni wakati Makhawarij wanamwambia Imam kuwa, "Hukmu ni ya Mwenyezi Mungu na siyo yako ewe Ali". Je, hivi Mwenyezi Mungu atajidhihirisha hapa ardhini na awapambanulie yale waliyohitilafiana? Au wao wanafahamu kuwa hukmu ya Mwenyezi Mungu imo ndani ya Qur'an, lakini Ali ameibadilisha kwa maoni yake? Ikoje, basi hoja yao na ya yule asemaye kuwa wao ndiyo waliyoibadilisha hukmu ya Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa Ali ndiye mjuzi mno kuliko wao na ndiye aliyetangulia kusilimu?

Kwa hiyo hicho ni kitambulisho kizuri ili kuwadanganya watu wenye mawazo ya kawaida wapate kuwaunga mkono na kuwasaidia kumpiga vita Imam Ali na ili wapate maslahi yao kwa vita hivyo, kama inavyotokea leo hii kwani nyakati ni nyakati, na watu ni watu tu, vituko na vitimbi haviishi bali vinazidi kukua kwani wenye vitimbi wa zama hizi wanafaulu kutokana na uzoefu wa wale wa mwanzo, ni mara ngapi maneno ya kweli yanakusudiwa uovu katika siku zetu hizi? Ni anuani nzuri kama ile ambayo wanaitangaza Mawahabi mbele ya Waislamu nayo ni "Tauhidi, kutofanya shirki", basi ni nani miongoni mwa Waislamu atakayekosa kukubali?

Na kama vile kundi fulani la Waislamu kujiita wenyewe kuwa ndiyo "Ahlis-Sunnah wal-Jamaa" Basi ni nani miongoni mwa Waislamu ambaye hatakubali kuwa pamoja na jamaa ambayo inafuata sunna za Mtume? Na kama kitambulisho cha Mabaathi (chama cha siasa Iraq na Syria) ambacho kina anuani isemayo, "Ummah mmoja wa Kiarabu wenye ujumbe wa kudumu" basi nani miongoni mwa Waislamu ambaye hatahadaika na kitambulisho hiki? Kabla hajafahamu undani wa chama cha Baath ambacho muasisi wake ni Mkristo aitwaye Mit-chel Aflaq? Ewe Ali bin Abi Talib, hapana shaka hekima yako imebakia na itaendelea kubakia, ni yenye kuvuma katika masikio ya zama zote, kwani ni maneno mangapi ya kweli lakini yamekusudiwa batili?


Kuna mwanachuoni fulani alipanda kwenye kiriri cha kutolea khutba na akatangaza kwa sauti kubwa akasema:"Yeyote mwenye kusema kwamba mimi ni Shia sisi tunasema wewe ni kafiri, na yeyote atakayesema mimi ni Sunni tunamwambia wewe ni kafiri, sisi hatutaki Shia wala Sunni bali tunataka Uislamu tu." Hakika ni maneno ya kweli lakini yamekusudiwa uovu, kwani ni Uislamu gani autakao mwanachuoni huyu? Na katika ulimwengu wetu leo kuna Uislamu wa aina nyingi, bali hata katika karne ya mwanzo Uislamu ulikuwa wa aina nyingi. Kuna Uislamu wa Ali na Uislamu wa Muawiyah na kila mmoja wao anao wafuasi wanaomuunga mkono mpaka mambo yakafikia kupigana. Pia upo Uislamu wa Husein na Uislamu wa Yazid aliyewaua watu wa nyumba ya Mtume eti kwa niaba ya kutetea Uislamu, na Husein (alionekana) katoka nje na Uislamu kwa ajili ya kumpinga Yazid. Upo pia Uislamu wa Maimamu wa nyumba ya Mtume na wafuasi wao, na kuna Uislamu wa watawala na raia zao na kila siku zinavyopita tunakuta tofauti baina ya Waislamu. Si hivyo tu, bali upo Uislamu wa kuwaachia watu watende wapendavyo (ilimradi wao ni Waislamu) kama wanavyouita watu wa Magharibi kwani wafuasi wa Uislamu huu wanawapendelea Mayahudi na Wakristo na wanawanyenyekea wenye nguvu kubwa (Marekani na Urusi wakati huo). Kadhalika upo Uislamu wa siasa kali kama unavyoitwa na watu wa magharibi kuwa ni Uislamu usiopenda mageuzi au hata kuwaita wendawazimu?


Na baada ya yote haya hakuna nafasi inayobakia ya kuisadiki hadithi ya "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna yangu" Kutokana na sababu zilizotajwa. Ukweli unabakia kuwa wazi katika ile hadithi ya pili ambayo Waislamu wameafikiana kwayo, nayo ni ile isemayo "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu," kwani hadithi hii inatatua matatizo yote na hakuna ikhtilafu inayobakia katika kuiawili aya yoyote ndani ya Qur'an, na au kuisahihisha na kuifasiri hadithi yoyote ile ya Mtume pindi tutakapowarejea watu wa nyumba ya Mtume ambao tumeamriwa kuwarejea hasa pale tutakapofahamu kwamba hawa ndiyo ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwabainisha kuwa ndiyo wanaostahiki kwa hilo. Hakuna Mwislamu yeyote mwenye mashaka juu ya elimu yao nyingi, uchamungu wao na kuipa kwao nyongo dunia, na bila shaka Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu, akawatakasa na kuwarithisha elimu ya kitabu (Qur'an), basi hawakhitilafiani kuhusu kitabu hicho wala hawatatengana nacho mpaka siku ya Qiyama. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema:

"Hakika ninaacha kwenu makhalifa wawili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kamba iliyonyooshwa kutoka mbinguni hadi ardhini, na kizazi changu watu wa nyumba yangu, bila shaka viwili hivyo havitatengana mpaka vinifikie kwenye Haudhi". Taz: 1) Musnad Ahmad bin Hanbal, Juz. 5 uk. 122.


2) Ad-Durrul-Manthoor Juz. 2 uk. 60.
3) Kanzul-UmmalJuz. 1 uk. 154.
4) Maj-Mauz-Zawaid Juz. 9 uk. 162.
5) Yanabiul-Mawaddah uk. 38 na 183.
6) Abaqatul-An-war Juz. 1 uk. 16.
7) Mustdrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 148.

"Na ili niwe pamoja na wakweli Assadiqina, inanipasa kusema haki na isinizuwie kufanya hivyo lawama ya yeyote mwenye kulaumu, na lengo langu ni kupata radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuiridhisha dhamiri yangu kabla ya watu kuniridhia". Na ukweli uliyomo ndani ya uchunguzi huu uko upande wa Mashia ambao wamefuata wasia wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kuhusu kizazi chake na wamewatanguliza juu ya nafsi zao, na wakawafanya kuwa ni Maimamu wao ambao kwao hujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwapenda na kuwafuata. Hakika wanastahiki pongezi kwa kufuzu hapa duniani na huko akhera pale atakapofufuliwa mtu pamoja na yule aliyempenda, basi ana hali gani siku hiyo aliyewapenda (watu wa nyumba ya Mtume) na akafuata uongofu wao?


AmesemaAz-Zamakhshari kuhusu makusudio haya: "Yamekuwa mengi mashaka na ikhtilafu, na kila mmoja anadai kuwa yeye ndiyo njia ya sawa. Mimi nimeshikamana na Lailaha Illa llah, na mapenzi yangu yako kwa Ahmad na Ali. Hakika mbwa alifaulu kwa kuwapenda watu wa pangoni (As-habul-Kahfi), basi vipi mimi niwe muovu kwa kukipenda kizazi cha Mtume? Ewe Mwenyezi Mungu tujaalie tuwe miongoni mwa wanaoshikamana na kamba ya kuwatawalisha wao (kizazi cha Mtume), na utujaalie miongoni mwa wapitao njia zao na wale wapandao ndani ya Merikebu yao na wale wanaoueleza Uimamu wao na wenye kufufuliwa katika kundi lao, bila shaka wewe unamuongoa umtakaye kwenye njia iliyonyooka.